T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 14 Jul 2026 09:58:15

Utafiti waonyesha itakuwa vita vikali kuelekea fainali ya Kombe la Dunia

ARGENTINA, Uingereza, Ufaransa na Uhispania zimesalia hatua mbili pekee kutwaa taji la Kombe la Dunia huku mashindano yakiingia katika hatua yake ya kusisimua zaidi. Timu hizo nne zimeonyesha ubora wa hali ya juu katika mechi sita walizocheza hadi sasa, huku takwimu zikionyesha kuwa hakuna timu iliyo na nafasi rahisi kuelekea fainali. Ingawa mabingwa watetezi Argentina wamefunga mabao mengi zaidi kwa jumla, wakiwa na mabao 17, Ufaransa wameonekana kuwa timu hatari zaidi katika mashambulizi. Les Bleus wameongoza kwa wastani ya mabao, idadi ya mashuti na nafasi bora za kufunga kwa kila dakika 90, jambo linaloonyesha nguvu yao kubwa katika safu ya ushambuliaji. Kwa upande wa Uhispania, licha ya kufika hatua ya nusu fainali, wamekuwa na changamoto kufunga. Mabingwa hao wa Ulaya wamepiga mashuti 110 sawa na Ufaransa, lakini wamefunga mabao 11 pekee ikilinganishwa na 16 ya Les Bleus. Uingereza nao wamekuwa na nafasi chache zaidi za wazi ikilinganishwa na wapinzani wao wa nusu fainali, lakini wamekuwa wakitumia vizuri nafasi wanazopata kupitia uwezo wa Jude Bellingham na nahodha Harry Kane. Kwenye safu ya ulinzi, Uhispania wamekuwa timu bora zaidi baada ya kuweka lango salama katika mechi zao za mwanzo na kuruhusu bao lao la kwanza pekee katika ushindi wa robo fainali dhidi ya Ubelgiji. Ufaransa pia wameonyesha uimara mkubwa nyuma, wakiruhusu mabao mawili pekee katika mechi sita, hali inayofanya nusu fainali yao dhidi ya Uhispania kuwa pambano la kuvutia kati ya mashambulizi makali na ulinzi thabiti. Katika nusu fainali nyingine, Uingereza na Argentina zinatarajiwa kushambuliana zaidi kutokana na udhaifu wa pande zote katika safu ya ulinzi. Timu hizo mbili zimeruhusu mabao sita kila moja katika mashindano haya. Argentina wamekimbia umbali mrefu zaidi kwa jumla, kilomita 706.5, lakini hilo limetokana na kucheza muda wa ziada katika baadhi ya mechi zao. Baada ya kuzingatia muda wa kucheza, mabingwa hao wamekuwa na idadi ndogo zaidi ya mbio na presha dhidi ya wapinzani. Kinyume chake, Uhispania wamekuwa timu yenye nguvu zaidi kimwili, wakiongoza kwa kukimbia, kufanya mbio kali na kuwabana wapinzani. Mbali na hilo, La Roja wamekuwa wakitawala mchezo kwa kumiliki mpira kwa asilimia 66, idadi kubwa zaidi katika mashindano haya, huku wakiwa na usahihi mkubwa wa pasi pamoja na Argentina kwa asilimia 90.4. Uingereza wanaweza kupata matumaini kutokana na udhaifu wa Argentina katika mipira ya juu. Three Lions wamefunga mabao manne ya vichwa, idadi inayowapa nafasi ya kutumia nguvu yao kwenye mipira ya krosi na mipira iliyokufa. Hata hivyo, Argentina bado wana silaha yao kubwa katika nahodha Lionel Messi. Nyota huyo ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika ubunifu wa mashambulizi, akiwa amepiga pasi nyingi za kupenya kuliko mchezaji mwingine yeyote katika mashindano haya. Messi amekuwa tishio kwa uwezo wake wa kufungua nafasi na kuwatengenezea wenzake nafasi za kufunga, jambo ambalo Uingereza italazimika kulidhibiti katika nusu fainali yao. Kwa upande wa Uingereza, uwezo wao wa kutumia mipira ya pembeni unaweza kuwa changamoto kubwa kwa Argentina. Wamekuwa timu bora zaidi kwa krosi katika mchezo wa wazi, huku moja kati ya kila krosi nne ikimpata mchezaji mwenzao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 14 Jul 2026 08:00:50

Kifungo cha maisha gerezani kwa mwanajeshi aliyeua mke na wanawe wawili Laikipia

ALIYEKUWA Meja wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Peter Mugure Mwaura, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya Mahakama Kuu kumpata na hatia ya kumuua mkewe na watoto wao wawili. Jaji Martin Muya alisema mauaji hayo yalikuwa ya kinyama na yaliyopangwa kwa umakini. "Nimezingatia ripoti kuhusu athari za mauaji haya kwa familia ya waathiriwa. Mauaji ya watu hawa watatu yalikuwa ya kinyama," alisema Jaji Muya. Jaji pia alisema Mugure hakuonyesha hata chembe ya majuto kwa kitendo chake. "Kwa kuzingatia mazingira ya kesi hii, nakuhukumu kifungo cha maisha gerezani," akaamua. Hukumu hiyo ilitolewa siku chache baada ya mahakama kumpata na hatia ya kumuua mkewe Joyce Syombua Maua, mwenye umri wa miaka 31, binti yao Shanice Mugure Mwaura mwenye miaka 10 na mwanao Peter Mwaura Junior, almaarufu Prince Michael, mwenye miaka mitano. Waendesha mashtaka walitaka Mugure ahukumiwe kifo wakisema aliangamiza familia yake kwa mpango uliotekelezwa kwa umakini. Hata hivyo, mahakama iliamua kifungo cha maisha baada ya kuzingatia uzito wa uhalifu huo, athari zake kwa familia ya marehemu na muda ambao Mugure alikuwa amezuiliwa rumande. Baada ya hukumu kutolewa, Mugure alisema hakukubaliana nayo. "Kwa heshima kubwa kwa mahakama, sikubaliani na uamuzi huu," alisema akiwa kizimbani. Jaji Muya alimweleza kuwa ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Kesi hiyo ilianzia Oktoba 2019 baada ya Mugure kumwalika Joyce na watoto wao kwenda kumtembelea katika Kambi ya Jeshi la Anga la Kenya mjini Nanyuki. Joyce alisafiri kutoka Nairobi akiwa na watoto hao akiamini walikuwa wanaenda kuungana kama familia. Hawakurudi tena nyumbani. Ushahidi ulionyesha walikesha nyumbani kwa Mugure kabla ya kwenda kula chakula cha mchana katika Hoteli ya Kilimara Springs. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuonekana wakiwa hai. Mahakama ilibaini kuwa waliporejea kambini, Mugure aliwaua wote watatu. Kisha aliweka miili yao kwenye mifuko maalumu ya kuhifadhia maiti, akaipakia kwenye buti ya gari lake na kuipeleka Thigithu, Kaunti ya Laikipia, ambako aliizika katika kaburi la kina kifupi. "Ushahidi unaonyesha mshtakiwa alimuua mkewe na watoto wake wawili, akaweka miili yao kwenye mifuko ya maiti na kuificha kwenye buti ya gari kabla ya kuwazika Thigithu," alisema Jaji Muya.

read more