T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 23:55:41

Mfungwa wa zamani amtafuta hakimu aliyemhukumu ili kumshukuru

MFUNGWA wa zamani ameshangaza wengi baada ya kumtafuta hakimu aliyemhukumu kifungo cha miaka minne gerezani ili kumshukuru. Kila siku ya kazi saa tatu kamili asubuhi, Hakimu Mkazi Eugene Pascal Nabwana huketi katika Mahakama Nambari Moja ya Wamunyu, Kaunti ya Machakos, kusikiliza kesi mbalimbali, lakini asubuhi ya Julai 2 ilikuwa tofauti. Karibu dakika 10 pekee kabla ya aanze shughuli zake za kila siku, msimamizi wa mahakama pamoja na msaidizi wa mahakama walimfuata na kumwomba akutane kwa muda mfupi na mtu aliyekuwa akimsubiri nje. Mwanzoni hakimu huyo alisita, lakini baada ya kushawishiwa alikubali. Alipotoka nje alimkuta mwanaume aliyeonekana mwenye wasiwasi. Muda mfupi baadaye, mgeni huyo alimshukuru kwa kifungo cha miaka minne alichotumikia gerezani, akisema ndicho kilichogeuza maisha yake na kumtia hamasa ya kutafuta elimu. Miaka minne iliyopita, akiwa Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, takribani kilomita 620 kutoka Wamunyu anapohudumu sasa, Bw Nabwana alikuwa amemhukumu Mwendwa Kilatya Nthenge, 35, kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mifugo. Baadaye, Bw Nabwana alihamishwa na kuwa Mkuu wa Kituo katika Mahakama ya Wamunyu, nafasi anayoshikilia hadi sasa. Bw Kilatya alitumikia kifungo chake katika Gereza la Hindi GK, Kaunti ya Lamu, kati ya mwaka 2023 na 2026. Aliposimama tena mbele ya hakimu huyo, mfungwa huyo wa zamani alieleza kuwa alipokuwa gerezani alijiunga na Mpango wa Elimu Magerezani na kujiandikisha kufanya mtihani wa KCSE na kupata wastani wa alama ya D (Plain). "Nina furaha kukutana nawe tena, mheshimiwa. Ulinifunga miaka minne gerezani. Sijaja kulipiza kisasi bali kukushukuru sana. Baada ya kunihukumu, ulifika Gereza la Hindi na kutuhimiza wafungwa, akiwemo mimi, kwamba bado tunaweza kusoma tukiwa gerezani. Nilichukua ushauri wako kwa uzito," alisema Bw Kilatya. Baada ya kutoka gerezani, Bw Kilatya alisema amekuwa akifanya vibarua mbalimbali ili kujikimu na kuweka akiba kidogo, lakini hana uwezo wa kifedha wa kujiunga na chuo kikuu. Kwa sababu hiyo, alimwomba hakimu huyo amshauri, amwelekeze au amsaidie kupata ufadhili ama watu wanaoweza kumwezesha kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo. "Ndoto yangu ni kujiunga na chuo kikuu nianze kwa kusomea cheti cha Usimamizi na Utawala wa Biashara. Kutoka hapo nitaendelea kupanda ngazi za elimu hatua kwa hatua. Changamoto ni kwamba sina Sh240,000 zinazohitajika kukamilisha kozi hiyo. Natamani kujiunga na Chuo Kikuu cha Africa Nazarene ambako kozi hiyo inatolewa. Naomba msaada," alisema Bw Kilatya. Bw Nabwana aliahidi kuwashirikisha wadau mbalimbali na wasamaria wema ili kumsaidia kufanikisha ndoto yake. Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nabwana alisema kukutana tena na Bw Kilatya kulikuwa ushahidi kwamba wakati mwingine adhabu ya mahakama inaweza kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa ya maisha ya mtu. "Sikuwahi kufikiria jambo kama hilo lingeweza kutokea," alisema Bw Nabwana. Hakimu huyo alisema kilichomgusa zaidi ni kwamba Bw Kilatya hakumwomba fedha za chakula wala msaada wa kutafutiwa kazi. "Nimeanza kuwatafuta watu mbalimbali ili tuone kama tunaweza kumpatia fedha hizo. Nilimpongeza kwa kupata alama ya D akiwa gerezani, huku akifundishwa na walimu watatu wa kujitolea. Hilo pekee ni mafanikio makubwa. Kinachonifurahisha zaidi ni kwamba bado ana hamu kubwa ya kuendelea na masomo yake," alisema Bw Nabwana. Alisema simulizi ya Bw Kilatya ni mfano mmoja tu wa mabadiliko mengi yanayotokea ndani ya mfumo wa mahakama lakini mara nyingi hayapati nafasi ya kusimuliwa. Kwa mujibu wa Bw Nabwana, maafisa wa mahakama hushuhudia watu wengi wakibadilika na kuwa bora zaidi baada ya kupitia mkondo wa sheria.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 23:25:58

Kindiki awazidi Wanga na Oburu kwa mbio za mgombea-mwenza wa Ruto

NAIBU wa Rais Prof Kithure Kindiki yuko pazuri kudumisha nafasi yake kama mgombea-mwenza wa Rais William Ruto, kulingana na matokeo ya utafiti. Kwa mujibu wa matokeo ya Infotrak, Prof Kindiki amewazidi kwa mbali wanasiasa wengine ndani ya Serikali Jumuishi. Hapo jana, utafiti huo ulionyesha kuwa Prof Kindiki anaongoza kwa asilimia 34 kati ya wale wanaotajwa kuwa wagombea-wenza wa Rais Ruto na ni pekee aliyepata zaidi ya asilimia 20. Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga anafuata kwa asilimia 11, huku Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga na Waziri wa Madini Hassan Joho wakiwa na asilimia tano na nne mtawalia. Bi Wanga ashatangaza kuwa analenga kutetea kiti chake Homa Bay naye Dkt Oginga analenga Useneta wa Siaya kwa mara nyingine. Bw Joho amekuwa akisukumwa na baadhi ya wanasiasa kutoka ukanda wa Pwani ambako ana ushawishi mkubwa wa kisiasa. Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi wamekuwa wakitajwa na baadhi ya wanasiasa kutoka Magharibi mwa nchi kama wanaotea nafasi ya Profesa Kindiki lakini hawakuorodheshwa popote. Wiki jana, Bw Mudavadi hata hivyo akiwa Kaunti ya Trans Nzoia, aliweka wazi kuwa hataki kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto bali analenga kuwahi urais mnamo 2032. Kinaya ni kuwa eneo la Magharibi na Nyanza, Prof Kindiki anapigiwa upatu kwa asilimia 36 and asilimia 28. Kiwango cha Nyanza kinazidi hata asilimia 21 ya Bi Wanga eneo hilo. Vivyo hivyo Pwani mwa nchi, Bw Joho ana asilimia 11 huku Profesa Kindiki akiwa na asilimia 23. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amekuwa akiongoza viongozi wa Mlima Kenya Mashariki kusisitiza kuwa Prof Kindiki asalie naibu rais huku akisema wako tayari kuagana na wenzao wa Mlima Kenya Magharibi debeni kama hawataungwa mkono. Katika eneo la Mlima Kenya, Profesa Kindiki alijizolea asilimia 22 kati ya wale ambao wanataka awe mgombeaji mwenza wa Rais. Katika matokeo ya utafiti wa TIFA yaliyotolewa mnamo Mei 14, Profesa Kindiki alikuwa na asilimia 59 huku Bi Wanga aliyemfuata akiwa na asilimia 12. Dkt Oginga alipata asilimia tatu huku Bw Joho akitoka na asilimia moja. Iwapo matokeo haya ni ya kuzingatiwa, basi huenda mjadala wa nani anastahili kuwa mgombeaji mwenza wa Rais 2027 ukatatuliwa mapema na kumwezesha kujipanga. Kama mwishowe Rais atamteua Profesa Kindiki kama mgombeaji mwenza ana nafasi ya kuwahi zaidi ya kura 1.3 za Mlima Kenya Mashariki ambazo ni kaunti za Embu, Meru na Tharaka-Nithi

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 22:55:30

Kampeni zakamilika Ol Kalou wakazi wakibaki na maswali matatu ya kutafakari

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou zilipokamilika rasmi Jumatatu, wapigakura walibaki wakitafakari masuala matatu tofauti yaliyotawala kampeni kabla ya uchaguzi wa Alhamisi. Swali kuu lililozua mjadala ni iwapo uchaguzi huo unafaa kuwa kura ya maoni kuhusu utawala wa Rais William Ruto, kama kinavyosisitiza chama cha Democracy for Citizens Party (DCP). Suala jingine ni iwapo wakazi wanapaswa kukiunga mkono chama tawala UDA ili kuendeleza miradi ya maendeleo na kuonyesha kuwa Nyandarua inaweza kuamua hatima yake ya kisiasa bila kushawishiwa na kaunti jirani za Mlima Kenya. Hoja ya tatu ni kwamba wapigakura wapuuze siasa za kitaifa na wamchague mgombeaji wanayeamini ndiye anayefaa zaidi kuwakilisha Ol Kalou. Tofauti na chaguzi zilizopita, mikutano ya kampeni haikutoa taswira halisi ya uungwaji mkono wa kisiasa. Mikutano ya UDA na DCP ilihudhuriwa na makundi yaliyokuwa yakizunguka kutoka mkutano mmoja hadi mwingine bila kujali chama kilichoandaa. Wadadisi wa kisiasa wanakadiria kuwa zaidi ya nusu ya waliohudhuria mikutano mikubwa walikuwa sehemu ya makundi hayo. Isitoshe, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo wafuasi walivaa mavazi ya vyama vyao kipindi chote cha kampeni, wengi walikuwa wakivua kofia na fulana mara tu mikutano ilipomalizika. Haikuwa jambo la kushangaza kuona mtu mmoja akiwa na kofia za UDA na DCP na kuzivaa kulingana na mkutano aliokuwa akihudhuria. Katika kampeni zote, viongozi wa DCP walieleza kuwa uchaguzi huo ni nafasi ya kumwaadhibu Rais Ruto na serikali yake kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kile walichodai ni usaliti dhidi ya eneo la Mlima Kenya. Wakiongozwa na Seneta wa Nyandarua John Methu, viongozi hao walidai kuwa miradi mingi ya maendeleo iliyozinduliwa wakati wa kampeni ilikuwa mbinu ya kuwahonga wapigakura. Ujumbe huo ulitawala pia mkutano wa mwisho wa DCP uliofanyika katika Bustani ya Ol Kalou Jumatatu. "Ni lazima tukatae mgombeaji wa UDA kwa sababu Rais Ruto alitusaliti baada ya kumpa uungwaji mkono mkubwa katika uchaguzi mkuu wa 2022. Kumkataa yeye na mgombeaji wake kutarejesha heshima ya kisiasa ya jamii yetu. Kenya nzima inaangalia Nyandarua kwa sababu uchaguzi huu utaweka msingi wa kumwondoa mamlakani 2027," akasema Seneta Methu. Mgombeaji wa DCP Kamau Ngotho aliwataka wapigakura kutumia uchaguzi huo kuonyesha kutoridhishwa kwao na serikali ya Kenya Kwanza. "Kura ya DCP ni ujumbe mzito kwa Kenya na dunia dhidi ya mauaji ya waandamanaji wa Gen Z, gharama ya juu ya maisha na mfumo wa afya unaodorora," akasema. Kwa upande wake, UDA iliwataka wapigakura kutenganisha siasa za kitaifa na maendeleo ya eneo lao. Chama hicho kilisema Nyandarua imekuwa ikitengwa kwa miaka mingi na kwamba kuunga mkono serikali kutahakikisha miradi inayoendelea inakamilika. Mratibu wa kampeni za UDA na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nyandarua Faith Gitau aliwashutumu viongozi wa DCP kwa kutumia malalamishi ya eneo hilo kisiasa ilhali walipokuwa serikalini hawakutekeleza maendeleo. "Wanaozungumzia usaliti walikuwa katika nyadhifa za juu serikalini lakini hawakufanyia Nyandarua maendeleo. Aliyekuwa Naibu Rais atuambie ni mradi gani mkubwa aliouletea kaunti hii. Miradi mingi mnayoiona sasa ilianzishwa baada ya kuondoka kwake," akasema katika mkutano wa mwisho wa UDA katika uwanja wa JM Kariuki KMTC.

read more