T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 04 Oct 2026 14:08:18

Hauhitaji pesa nyingi kujipatia mwonekano mpya, vidokezo hivi vitakufaa sana

NI rahisi sana kuzoea 'mavazi sare' yenye rangi tulivu zinazofanana au zinazokaribiana sana na miundo ileile inayofanya uonekane kama mtu anayerudia mavazi yaleyale kila uchao. Wengi wana mazoea ya kuvalia ama sare ya kazi, chuo, jeans, sweatpants, fulana na koti, mavazi ambayo ni rahisi kuambatanisha na yenye mwonekano unaotabirika kila wakati. Hakuna kosa kubwa unalofanya kwa kuchagua mtindo rahisi ikizingatiwa shughuli tele na muda usiotosha wa kujikwatua na kuwahi pilka' pilka zinazokusubiri kila uchao. Hata hivyo, mtindo huu unaporudiwa kila mara huanza kuchusha na kukupa mwonekano wa mtu aliyechoka asiye mchangamfu wala kujali nafsi yake, jambo ambalo halifai kamwe hasa kwa binti anayeelewa mitindo ibuka ya fashoni na kuendana na majira. Kujikwatua kwa mavazi, kujipodoa na mapambo hakufai kuwa jambo la kuchusha. Kunapaswa kuwa jambo la kukuchangamsha linaloibua msisimko kila unapoamka na kujiandaa kutoka nyumbani kwako asubuhi. Mavazi ya kuchangamsha hayamaanishi kujilazimushia rangi zote au mavazi yote ya kisasa.bila.kutilia maanani iwapo yanawndana na umbo la mwili wako au rangi ya ngozi. Katika ukumbi huu wa fashoni, leo hii tutajifahamisha kuhusu baadhi ya mavazi na mitindo unayohitaji kubadilisha ili kuboresha mwonekano wako na kukufanya uwe mtanashati, mstaarabu n mwenye mvuto wa kipekee kila wakati. Jeans na blazer badala ya suti kamili Kuambatisha jeans na koti (blazer) yenye mishono na muundo uliochongeka vyema na inayokutoshea vizuri pasipo kubana au kupwaya mtindo rahisi na wa kuvutia mno. Unaweza pia kutia nakshi mseto huu wa mavazi kwa kujumuisha kaptula ndefu ya kitambaa na mishono thabiti bila kusumbuka sana. Polo shirt Badala ya kuvaa fulana na sweta kila mara, anza kujikwatua kwa shati aina ya polo zilizoshonwa kwa kitambaa cha sufi au pamba. Mtindo huu hasa.shati zenye mistari zitavutia upya katika safu yako ya mavazi bila kulazimika kubadilisha yote. Unaweza kupata shati za rangi anuai kwa bei nafuu na kuziambatisha upendavyo. Siri ni kuacha wazi sehemu ya shingoni (collar) na kuweka ndani ya mshipi (tuck) sehemu ndogo ya shati upande wa mbele. Rangi nyekundu Mbinu rahisi zaidi ya 'kuchangamsha' mavazi yenye rangi tulivu ya kuchusha ni kutia nakshi kwa kutumia rangi nyekundu. Iwe ni kiatu maridadi chekundu, kitambaa laini cha hariri unachojifunga shingoni mwako au fulana jekundu ya kushonwa unayowekelea mabegani mwako kwa ustaarabu. Nakshi ya rangi nyekundu hunogesha mwonekano na kufanya mavazi ambayo kwa kawaida yanachudha, kuonekana yenye kuchangamsha, kuvutia na ya kisasa. Hauhitaji kujikoleza kwa rangi nyekundu. Hata kitambaa chekundu unachojifunga mkononi kinatosha kubadilisha mwonekano wako na kuonyesha unaelewa na kuendana na majira ya fashoni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 04 Oct 2026 14:19:17

Maandamano nje ya kanisa jijini kuhusu mwanamke aliyedhulumiwa

HALI ya wasiwasi ilizuka nje ya Kanisa la Redeemed Gospel, Buruburu jijini Nairobi, Jumapili baada ya mamia ya vijana kuandamana wakitaka haki itendeke kwa mwanamke aliyenaswa kwenye video akidhulumiwa na wenzake. Katika video ambayo imesambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, mwanamke huyo anaonekana akishambuliwa na kuzuiwa kutoka kwenye chumba na wasichana wanne. Tukio hilo liliwakasirisha Wakenya wengi, huku baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakidai mmoja wa wasichana wanaodaiwa kumshambulia mwanamke huyo ni mshirika wa kawaida wa kanisa la Burubuviru. Hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Felix Kavoli, alipuuzilia mbali madai kwamba yeye ni baba wa mmoja wa wasichana hao. "Waambieni watu wa mitandao ya kijamii kwamba wamekosea, wameelewa vibaya na wanakuja mahali pasipofaa. Sina binti anayesoma katika Chuo Kikuu cha Riara. Binti zangu ni watu wazima na wanafanya kazi, na majina yao yanajulikana. Sina mtoto anayesoma katika Chuo Kikuu cha Riara," akasema Mchungaji Kavoli. Mchungaji huyo pia aliwaambia waandamanaji wa Gen-Z kwamba tukio hilo la madai ya unyanyasaji halikutokea kanisani na hivyo hawakupaswa kusababisha vurugu huko. "Halimhusu Mchungaji Kavoli na lilifanyika huko nje. Kwa nini shetani analipinga kanisa?" akauliza. Polisi walizunguka kanisa hilo baada ya maandamano, huku maafisa wa kukabiliana na ghasia wakitumwa eneo hilo wakati waandamanaji wakitaka haki kwa mwathiriwa. "Tuko hapa kudai haki kwa Jahenda (anayedaiwa kuwa mwathiriwa). Kwa nini kanisa linaunga mkono hili?" akasema mmoja. Wengine waliitaka kanisa lichukue hatua dhidi ya wasichana wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo. "Haki kwa Jahenda. Haki daima. Amani, amani, amani," kijana mwengine alisema. Jumamosi, Chuo Kikuu cha Riara kilithibitisha kuwa baadhi ya watu wanaoonekana kwenye video hiyo ni wanafunzi wake na kulaani tukio hilo, kikisema hatua zitachukuliwa. "Tumeona video ambayo imesambazwa mtandaoni ikionyesha wasichana kadhaa wakimtishia na kumshambulia mwanamke mwengine katika eneo linaloonekana kuwa choo cha umma. Chuo Kikuu cha Riara kinalaani vikali vitendo vya unyanyasaji, vitisho, maonevu, au utovu wa nidhamu," akasema Makamu Mkuu wa Chuo hicho katika taarifa. Chuo hicho kiliongeza kuwa ingawa tukio hilo linalodaiwa lilitokea nje ya chuo, tabia hiyo ilikiuka moja kwa moja maadili ya taasisi hiyo na kanuni za maadili ya wanafunzi. "Uongozi wa chuo umeanza uchunguzi wa ndani kuhusu suala hilo kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Wanafunzi na sera za taasisi, na tumejitolea kushirikiana na kitengo cha uchunguzi, "Chuo Kikuu cha Riara kinaendelea kujitolea kudumisha elimu iliyo salama, yenye heshima na inayowajibika, kama ambavyo tumekuwa tukifanya," ikasema taarifa hiyo.

read more