T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 03 Oct 2026 14:47:52

Mjamzito afa, adaiwa kusukumwa kutoka gari la polisi kwa kukosa hongo

HUZUNI na ghadhabu zimetanda katika kijiji cha Mugambaciura, Kaunti ya Kirinyaga, kufuatia kifo cha mwanamke mjamzito aliyedaiwa kusukumwa kutoka kwa gari la polisi lililokuwa likiendeshwa baada ya yeye na mumewe kushindwa kutoa hongo ya Sh1,000 iliyodaiwa na maafisa wa polisi. Bi Catherine Mwende, ambaye alikuwa mjamzito wa miezi ya mwisho, alifariki papo hapo pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni baada ya kuanguka barabarani. Mumewe, Anthony Muturi, alipata majeraha mikononi na miguuni lakini alinusurika. Kulingana na Bw Muturi, mkasa huo ulitokea Ijumaa walipokuwa wakielekea shambani kuvuna miraa. Akiwa pamoja na mkewe, alisema gari la polisi lilisimama na maafisa waliokuwa ndani wakawapa lifti hadi walikokuwa wakielekea. Hata hivyo, walipofika karibu na walikokusudia kushuka, mambo yalibadilika ghafla. Bw Muturi alisema walipowaomba maafisa hao wasimamishe gari ili washuke, walidai walipe Sh1,000 kama ishara ya shukrani kwa lifti waliyopewa. "Walipotusimamisha mwanzoni hawakutuambia kuwa tulihitajika kulipia safari hiyo. Tulishangaa walipoanza kutudai pesa tulipofika tunakokwenda," alisema Muturi. Kwa mujibu wake, yeye na mkewe waliwaeleza polisi kuwa hawakuwa na fedha hizo, jambo lililosababisha mabishano makali. Ndipo, kwa mujibu wa madai yake, maafisa hao waliwasukuma kutoka kwenye gari hilo lililokuwa bado likiendeshwa. Mwende alianguka kifudifudi barabarani na kufariki pamoja na mtoto wake ambaye alikuwa hajazaliwa. Muturi, ambaye alitibiwa hospitalini na kuruhusiwa kurejea nyumbani, sasa anataka serikali kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanywa na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria. "Nimepoteza mke wangu na mtoto wangu ambaye alikuwa hajazaliwa. Maafisa waliohusika wanapaswa kuwajibishwa," alisema kwa huzuni. Kisa hicho kimezua hasira miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, ambao wamewashutumu maafisa wa polisi kwa kuwadhulumu wananchi kwa kisingizio cha kuwapa lifti. Mchungaji Ephantus Mwangi alisema ikiwa madai hayo yatathibitishwa, basi hatua kali za kisheria zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya maafisa wote waliohusika. "Kama wakazi tunataka haki itendeke. Polisi wanaopatikana na hatia lazima wawajibishwe kwa mujibu wa sheria," alisema. Baada ya tukio hilo, wakazi wenye hasira walifunga barabara ya Piai-South Ngariama wakipinga kile walichokitaja kuwa ukatili wa polisi. Pia walifukuza maafisa wa usalama waliofika eneo hilo kuchukua mwili wa marehemu. Hali ya taharuki ilitawala huku waandamanaji wakitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya maafisa wanaohusishwa na kisa hicho. Baadhi ya wakazi walidai kuwa matukio ya maafisa wa polisi kudai fedha kutoka kwa watu wanaowapa lifti yamekuwa yakitokea mara kwa mara. "Majuzi tu tulipewa lifti na kisha tukaombwa tulipe Sh500," alisema mkazi mmoja, Alfred Muthomi. Lawrence Mugo, mwendesha bodaboda aliyefika eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo, alisema alishtushwa na hali aliyokuta. "Sikuamini nilichokiona. Mwanamke alikuwa ameaga dunia huku mwanamume akiwa amejeruhiwa vibaya kando ya barabara," alisema. Aliyekuwa Naibu Gavana wa Kirinyaga, Peter Ndambiri, amelaani tukio hilo na kuitaka Idara ya Polisi kufanya uchunguzi usioegemea upande wowote ili ukweli ujulikane. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Mwea Mashariki, Henry Gitonga, alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichotokea na kuwataka wakazi kuwa watulivu wakati mamlaka zikichunguza madai hayo. Tukio hilo limeibua maswali mazito kuhusu mienendo ya baadhi ya maafisa wa usalama na uhusiano wao na wananchi. 

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 03 Oct 2026 14:03:26

Ruto akamilisha ziara Pwani, awapa mabwanyenye onyo kali kuhusu ardhi

RAIS William Ruto jana alihitimisha ziara yake ya siku nane katika eneo la Pwani kwa ahadi mpya za kutatua tatizo sugu la ukosefu wa ardhi miongoni mwa wakazi huku akionya  mabwanyenye wanaomiliki ardhi bila kuitumia. Hata hivyo, idadi ndogo ya hati miliki zilizotolewa Kaunti ya Mombasa imeibua maswali kuhusu kasi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi katika eneo hilo. Mombasa ilipokea hati miliki 4,360 pekee, idadi ndogo ikilinganishwa na kaunti nyingine za Pwani. Kwale ilipokea hati 94,175, Kilifi ikapata 36,826 huku Taita Taveta ikipewa hati 31,318. Kaunti za Lamu na Tana River zilipokea jumla ya hati 22,770. Maeneo ya Mombasa kama Zum Zum, Katani, Kwa Bulo na Aldina yameendelea kukwama kutokana na kesi  mahakamani na kutopatikana kwa idhini kutoka kwa wamiliki wa ardhi walioko nje ya eneo hilo. Akizungumza katika uwanja wa Mama Ngina Waterfront, Mombasa, Rais alisema serikali haitaruhusu maelfu ya wakazi kufurushwa kutoka mashamba ambayo wameishi kwa miaka mingi. "Hatutakubali tamaa ya baadhi ya mabwanyenye wanaozuia juhudi za kutatua dhuluma za kihistoria za ardhi katika Pwani. Tuko tayari kufanya mazungumzo lakini hatutaruhusu wananchi kufurushwa," alisema. Rais alihitimisha ziara yake Lamu ambapo aligawa hati miliki 20,189 kwa wakazi wa maeneo mbalimbali. Hafla hiyo pia ilitumiwa kuhimiza wakazi kuunga mkono  mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote pamoja na eneo maalum la viwanda kwa gharama ya Sh2 trilioni. Rais alisema serikali imetenga Sh7.5 bilioni kujenga nyumba 3,000 kwa wafanyakazi watakaoajiriwa katika kiwanda hicho. "Tunataka wafanyakazi watakaokuja kufanya kazi hapa wapate makazi bora na mazingira mazuri ya kazi," alisema. Waziri wa Madini na Uchumi wa Bahari, Ali Hassan Joho, alisema mradi huo unaweza kubadilisha kabisa uchumi wa Pwani,  ukanda ambao umekuwa ukilalamikia kutengwa kwa miaka mingi. Naye Gavana wa Lamu, Issa Timamy, alisema wenye ardhi halali watakaoathiriwa na mradi huo watapata fidia. Waziri wa Ardhi, Alice Wahome, alisema utoaji wa hati miliki utawapa maelfu ya wakazi umiliki rasmi wa ardhi zao na kumaliza migogoro ya muda mrefu. Hata hivyo, huku wakazi wa Lamu wakisherehekea kupokea hati miliki, maelfu ya wakazi wa Mombasa bado wanasubiri migogoro ya ardhi kutatuliwa ili waweze kupata nyaraka zao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 03 Oct 2026 13:47:38

Mgomo wa wahadhiri wachacha, wakataa dili ya serikali

WAHADHIRI na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu vya umma wamekataa pendekezo jipya la serikali kuhusu Mkataba wa Makubaliano ya Kazi (CBA) wa miaka ya 2025 hadi 2029, wakisema halikidhi matakwa yao. Mzozo huo unahusisha tofauti kubwa kati ya madai yaliyowasilishwa na vyama vya wafanyakazi vya UASU, KUSU na KUDHEIHA na mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Umma (IPUCCF), linalowakilisha waajiri. Vyama hivyo vilipendekeza nyongeza kubwa ya mishahara na marupurupu mbalimbali. UASU, kwa mfano, ilitaka mishahara ya msingi iongezwe kwa kiwango cha kati ya asilimia 36 na 68 kulingana na daraja la kazi. Pia ilipendekeza nyongeza ya asilimia 57 ya marupurupu ya nyumba, ya usafiri ya hadi Sh60,000 kwa baadhi ya daraja na ya maprofesa ya Sh80,000. Aidha, chama hicho kilitaka marupurupu ya vitabu ya kati ya Sh65,000 na Sh90,000 kwa mwaka, ya likizo ya hadi Sh70,000 pamoja na bima ya matibabu, meno na macho. Hata hivyo, waajiri walipendekeza ongezeko la chini zaidi. Baada ya kupitia chaguo mbalimbali, IPUCCF ilipendekeza mishahara iongezwe kwa asilimia mbili kila mwaka katika kipindi cha miaka minne ya CBA. Hii inatafsiriwa kuwa nyongeza ya jumla ya asilimia 8.25 pekee kufikia mwaka 2029. Katibu Mkuu wa UASU, Dkt Constantine Wasonga, alisema vyama vya wafanyakazi havikushirikishwa kikamilifu katika kufikia uamuzi huo. "Hatuwezi kupewa kiwango cha mwisho halafu tuelezwe tukubali. Maafikiano ya pamoja yanahitaji mazungumzo ya kweli," alisema. Mwenyekiti wa KUSU, Dkt Charles Mukhwaya, alisema wafanyakazi wamechoshwa na mazungumzo yasiyozaa matunda. "Hatuwezi kuendelea kuzunguka katika jambo moja milele. Ikiwa haki zetu hazitazingatiwa, tuko tayari kwenda barabarani kudai tunachostahili," alisema. Kwa upande wake, KUDHEIHA imesema pendekezo la sasa halikidhi matarajio ya wafanyakazi na haiwapi nafasi ya kupanda madaraja kazini.

read more