T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 01 Oct 2026 04:55:30

Wagonjwa hatarini: Jinsi dawa zenye dosari hupenya Kenya

MGONJWA anapoingia hospitalini hupokea matibabu akiamini dawa alizopewa ni salama na zenye ubora unaostahili. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya dawa zenye kasoro huingia katika mfumo wa afya na kuwafikia wagonjwa kabla ya dosari zake kugunduliwa. Mwaka huu pekee, Bodi ya Dawa na Sumu Kenya (PPB) imetoa maagizo 16 ya kuondoa sokoni dawa na bidhaa za matibabu zinazoshukiwa kuwa na matatizo ya ubora. Dawa hizo zimehusisha za kugadisha, vifaa vya pumu, dawa za tumbo na bidhaa nyingine muhimu zinazotumiwa hospitalini kila siku. Mkurugenzi Mkuu wa PPB, Dkt Ahmed Mohamed, amesema ongezeko la visa vya kuondolewa kwa dawa sokoni linaonyesha kuwa mifumo ya ufuatiliaji imeimarika na sasa inafanikiwa kugundua matatizo ambayo hapo awali yangeweza kupita bila kugunduliwa. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, changamoto inaanzia katika hatua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa dawa. Baadhi ya dosari hutokana na utengenezaji katika viwanda vya nje ya nchi, huku nyingine zikisababishwa na hali mbaya ya uhifadhi au usafirishaji wa dawa kabla hazijamfikia mgonjwa. Dawa nyingi zilizoondolewa sokoni mwaka huu zilitengenezwa katika nchi za kigeni, hasa India. Kampuni kadhaa zilihusishwa na matatizo kama kubadilika kwa rangi ya dawa, kushindwa kufikia viwango vya kemikali vinavyohitajika au kuwepo kwa hitilafu zinazoweza kuhatarisha afya ya watumiaji. Mfamasia wa viwandani katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTTRH), Dkt Lonary Ngetich, anasema dawa zinazotengenezwa Kenya mara nyingi huondolewa sokoni kutokana na hitilafu zinazoonekana kwa macho kama uchafu. Kinyume chake, dawa nyingi za nje huonyesha matatizo ya kemikali yanayoweza kugunduliwa tu kupitia maabara. Anasema hata dawa inayotoka kiwandani ikiwa katika hali nzuri inaweza kuharibika kutokana na joto kali, unyevunyevu au uhifadhi usiofaa wakati wa usafirishaji na usambazaji. Madhara ya dawa hizo kwa wagonjwa yanaweza kuwa makubwa. Dawa zisizo na kiwango sahihi cha kemikali zinaweza kusababisha ugonjwa kuendelea kuenea,  viungo vya mwili kutofanya kazi au hata kifo. Aidha, matumizi ya dawa hafifu yanaweza kuongeza tatizo la dawa, ambapo bakteria na vimelea hujenga uwezo dhidi  ya dawa. Ingawa PPB ina mifumo ya kupokea ripoti kutoka kwa wahudumu wa afya na wananchi, wataalamu wanaonya kuwa mara nyingi dosari hugunduliwa baada ya wagonjwa tayari kutumia dawa hizo. Ili kudhibiti hali hiyo, serikali inatekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Dawa Hafifu na Bandia. Mpango huo unalenga kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ugavi, kuboresha ufuatiliaji wa soko na kuhakikisha ni dawa salama pekee zinawafikia Wakenya. Kulingana na takwimu za PPB, visa vya dawa zenye kasoro vilivyoripotiwa viliongezeka kutoka 42 mwaka 2021 hadi 85 mwaka 2023 kabla ya kupungua katika miaka iliyofuata. Aidha, bidhaa bandia zilianza kugunduliwa mwaka 2023. Hata hivyo, kiwango halisi cha wagonjwa walioathiriwa na dawa hizo bado hakijabainishwa rasmi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 01 Oct 2026 03:55:32

Orengo anaelekea wapi kisiasa? Mdahalo wachacha akikosa mikutano ya upinzani

KUKOSEKANA kwa Gavana wa Siaya James Orengo katika mikutano kadhaa muhimu ya viongozi wa upinzani katika siku za hivi majuzi kumezua mjadala mkubwa kuhusu hatua yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kwa mwanasiasa ambaye amekuwa nguzo muhimu katika siasa za upinzani kwa miongo kadhaa, kila hatua yake au hata kutokuwepo kwake katika hafla muhimu huibua maswali mengi. Hali hiyo imefanya wengi kujiuliza iwapo Orengo anajiandaa kujiunga na muungano mpya wa kisiasa au anapanga kuanzisha mkondo wake mwenyewe. Baada ya kuwa kimya kwa muda, Orengo alijitokeza Septemba 21 wakati wa uzinduzi wa muungano mpya wa The Ukombozi Alliance, uliobadilishwa jina kutoka Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party. Watazamaji wa kisiasa walitafsiri hatua hiyo kama ishara kwamba huenda alikuwa akijipanga kupata nafasi mpya katika upinzani. Hata hivyo, siku chache baadaye alikosekana katika kikao muhimu cha viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi ambapo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa muungano huo katika uchaguzi wa 2027. Kutokuwepo kwake kulionekana kuwa na uzito mkubwa kwa sababu hapo awali jina lake lilikuwa likitajwa miongoni mwa wale waliokuwa wakitazamwa kama viongozi wanaoweza kuwania nafasi ya juu katika muungano huo. Orengo pia hakuhudhuria mkutano wa kisiasa uliofanyika Narok licha ya jina lake kuwekwa kwenye mabango ya viongozi walioalikwa. Viongozi waliokuwepo ni pamoja na kiongozi wa muda wa Jubilee Fred Matiang'i na kiongozi wa People's Party of Kenya Ndindi Nyoro. Katika mahojiano maalum, Orengo aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu huku akisema bado anaunga mkono umoja wa upinzani katika mapambano ya kuleta mabadiliko nchini. "Ninaunga mkono mapambano ya mageuzi yanayohitaji umoja na hatua za kisiasa. Wafuasi wangu wawe watulivu. Nitafafanua hatua yangu inayofuata kwa wakati unaofaa," alisema. Ingawa hakufichua mipango yake, taarifa zinaonyesha kuwa Orengo anafikiria kufufua chama cha Liberal Democratic Party (LDP), ambacho zamani kilihusishwa na Raila Odinga na marehemu Dennis Kodhe. Kidokezo kubwa zaidi kilitolewa Jumatano alipoweka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema, "Maadhimisho ya Baba yanakaribia, jiandaeni," akiambatisha picha ya kofia yenye rangi rasmi za LDP, yaani kijani, bluu na nyeupe. Wadadisi wa siasa wanaamini kuwa hatua hiyo huenda ikawa njia ya Orengo kujijengea nafasi mpya ya kujadiliana na makundi mbalimbali ya upinzani, yakiwemo Ukombozi Alliance na Linda Mwananchi. Chanzo cha karibu naye kinasema Orengo anaamini eneo la Nyanza linafaa kuwa na sauti yenye uzito zaidi katika siasa za upinzani. Wafuasi wake wanahisi baadhi ya viongozi ndani ya Linda Mwananchi wanajaribu kupunguza ushawishi wake. Hata hivyo, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amepuuzilia mbali madai ya mzozo mkubwa ndani ya vuguvugu hilo. Amesema tofauti za maoni kati ya Orengo, Sifuna na mbunge Babu Owino ni jambo la kawaida katika mfumo wa vyama vingi. Kwa sasa, hatua anayopanga Orengo bado ni siri. Lakini uchaguzi wa 2027 unapokaribia, kila ishara inaonyesha kuwa gavana huyo wa Siaya anajitayarisha kufanya uamuzi muhimu ambao unaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za upinzani nchini.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 01 Oct 2026 02:55:24

Mbwembwe ujenzi wa kiwanda cha kipekee Afrika Mashariki ukianza Lamu

KENYA imezindua rasmi ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta na bidhaa za petroli cha Dangote East Africa Petroleum Refinery and Petrochemicals SEZ katika Kaunti ya Lamu, mradi unaotarajiwa kugharimu takriban Sh2 trilioni. Shughuli ya uwekaji jiwe la msingi iliongozwa na Rais William Ruto katika Bandari ya Lamu jana na kuhudhuriwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais wa Benin Romuald Wadagni na Rais wa Togo Jean-Lucien Savi de Tové. Mwekezaji mkuu wa mradi huo, bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, pia alikuwepo. Rais Ruto alisema mradi huo ni hatua muhimu katika juhudi za Afrika za kujitegemea kiuchumi kwa kusindika rasilimali zake badala ya kuziuza kama malighafi. "Mradi huu ni zaidi ya kiwanda cha kusafisha mafuta. Ni uwekezaji katika usalama wa kawi, ukuaji wa viwanda na ushirikiano wa kikanda. Ni thibitisho kuwa Afrika sasa inaweza kufadhili, kujenga na kuongeza thamani ya bidhaa zake hapa nyumbani," alisema Rais Ruto. Aliongeza kuwa kwa muda mrefu Afrika imekuwa ikitoa malighafi huku mataifa mengine yakinufaika kwa kuzisindika, kuzitengeneza na kupata ajira pamoja na mapato yanayotokana nazo. Kwa mujibu wa Rais, Kenya ilitumia zaidi ya Sh530 bilioni mwaka uliopita kuagiza bidhaa za mafuta kutoka nje, hali inayoonyesha umuhimu wa kuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo ndani ya eneo hili. "Lazima tuzalishe zaidi ya tunachotumia. Lazima tuongeze thamani ya bidhaa tunazozalisha na kupunguza kutegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje," alisema. Rais Museveni aliunga mkono maono hayo akisema viwanda vitasaidia kufungua fursa mpya za kiuchumi katika eneo la Afrika Mashariki. Alitumia mfano wa msimamo wa Uganda wa kutotuma madini ya chuma kusindikwa nje ya nchi ili kusisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali ndani ya nchi husika. Kiongozi huyo pia alitoa wito wa kuharakishwa kwa muungano wa Afrika Mashariki ili kurahisisha biashara, uwekezaji na uhamaji wa wafanyakazi katika ukanda huu. "Tunapaswa kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki ambapo wananchi wanaweza kuvuka mipaka kwa urahisi na kufanya kazi popote katika eneo hili," alisema. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema  hatua ya Afrika kutegema pakubwa masoko ya nje umefanya bara hili kukumbwa na misukosuko ya bei na changamoto za ugavi wa bidhaa muhimu. Alisema kiwanda cha Lamu kitasaidia kuleta huduma za usindikaji wa mafuta karibu na soko la Afrika Mashariki na kupunguza gharama ya kupata bidhaa za petroli. "Kadri viwanda na idadi ya watu vinavyoongezeka, mahitaji ya mafuta nayo yanaongezeka. Mradi huu utakuwa na mchango mkubwa katika sehemu hii ya bara," alisema. Bilionea Aliko Dangote alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 40 ijayo na utakuwa mfano wa kile ambacho Waafrika wanaweza kufanikisha wanaposhirikiana. Alisema Afrika imebarikiwa kwa rasilimali nyingi lakini inaendelea kupoteza mapato kwa kuuza malighafi na kuagiza bidhaa zilizotengenezwa. "Lazima Afrika ijitosheleze. Hatupaswi kutegemea nchi nyingine kwa bidhaa muhimu. Asilimia 94 ya dawa tunazotumia zinaagizwa kutoka nje. Tunahitaji kujenga viwanda vyetu na kuimarisha uzalishaji wa ndani," alisema. Dangote aliongeza kuwa kundi lake linapanga kuwekeza zaidi  katika sekta mbalimbali za Afrika ifikapo mwaka 2030, zikiwemo madini, viwanda, bandari na kawi. Mradi wa Lamu unatarajiwa kuwa msingi wa maendeleo ya mji mkubwa wa viwanda unaozunguka bandari hiyo. Pia utaongeza mahitaji ya huduma za usafirishaji, uhandisi, ujenzi, makazi na kawi huku ukifungua maelfu ya nafasi za kazi. Viongozi waliohudhuria hafla hiyo walisisitiza kuwa maendeleo ya Afrika yatapatikana kupitia ongezeko la viwanda, usindikaji wa rasilimali ndani ya bara na ushirikiano wa kikanda unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa mataifa ya Afrika.

read more