T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 29 Sep 2026 12:17:18

Vyuo vikuu vya umma mbioni kuzuia mgomo wa wahadhiri unaojongea

VYUO VIKUU vya umma vinaendelea na juhudi za dharura kutafuta suluhu ya mzozo wa Mkataba wa Pamoja wa Kazi (CBA) kabla ya wahadhiri kutekeleza tishio lao la kugoma ndani ya siku chache zijazo. Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) kimesisitiza kuwa notisi yake ya mgomo bado ipo na kwamba wahadhiri watasusia kazi Oktoba 2, 2026 ikiwa mazungumzo kuhusu CBA mpya ya kipindi cha 2025 hadi 2029 hayatapiga hatua za kuridhisha. Katika Chuo Kikuu cha Nairobi, wasimamizi wameanza tena mashauriano na viongozi wa vyama vya wafanyakazi pamoja na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) ili kutatua masuala yaliyosalia kuhusu mikataba ya awali ya wafanyakazi. Chuo hicho kinasema kilikamilisha mazungumzo ya CBA ya miaka 2017 hadi 2021 na vyama vitatu vinavyotambuliwa rasmi, ambavyo ni UASU, KUSU na KUDHEIHA, mwezi Aprili mwaka huu. Baada ya mazungumzo hayo, mikataba hiyo iliwasilishwa kwa SRC kwa ushauri kabla ya kusajiliwa rasmi. Hata hivyo, SRC ilieleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya marupurupu yaliyopendekezwa, yakiwemo ya nyumba, likizo, vitabu, maprofesa, matibabu ya meno na macho, pamoja na marupurupu ya wafanyakazi wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali. Kutokana na hali hiyo, SRC ilitaka chuo hicho kurekebisha baadhi ya vipengele au kuwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa marupurupu hayo yanaweza kugharamiwa kwa njia endelevu. Wakati huo huo, vyuo vikuu vya umma vimeeleza kuwa havina uwezo wa kifedha wa kufadhili CBA mpya bila msaada wa ziada kutoka Wizara ya Fedha. Viongozi wa vyuo hivyo wanasema taasisi hizo tayari zinakabiliwa na upungufu wa zaidi ya Sh100 bilioni kutokana na fedha ambazo serikali haijatoa kikamilifu chini ya mfumo mpya wa ufadhili wa wanafunzi. Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu wa Vyuo Vikuu vya Umma, Profesa Daniel Mugendi, amesema ukosefu wa fedha umeweka vyuo katika hali ngumu ya kutekeleza majukumu ya kawaida ya masomo, wafanyakazi na shughuli za uendeshaji. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UASU, Dkt Constantine Wasonga, amesema vyuo haviwezi kutegemea karo ya wanafunzi kufadhili mishahara ya wahadhiri. Amesisitiza kuwa serikali ndiyo inapaswa kutoa fedha maalum za kutekeleza CBA mpya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 29 Sep 2026 11:52:45

Matumizi ya fedha: Wawasilisha kesi kaunti zisikiuke Katiba

WATETEZI wa haki za kiraia wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka taasisi za usimamizi wa fedha za umma zizuiwe kuidhinisha matumizi ya serikali za kaunti yanayozidi kiwango cha asilimia 35 ya mapato kinachoruhusiwa kutumiwa kwa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi. Walalamishi hao, akiwemo Laban Omusundi pamoja na mashirika ya Ignite Kenya na Sheila Kendi, wanadai kuwa Mdhibiti wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), Seneti na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameshindwa kutekeleza sheria licha ya ripoti za ukaguzi kuonyesha ukiukaji huo kwa miaka kadhaa.Katika kesi hiyo, wanataka mahakama itangaze kuwa matumizi yoyote ya fedha za kaunti yanayozidi kiwango cha asilimia 35 ni kinyume cha Katiba na sheria za usimamizi wa fedha za umma. Pia wanataka taasisi hizo ziagizwe kuchukua hatua za kuhakikisha hitaji hili linatekelezwa kikamilifu.Jaji Julius Nang'ea aliidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuagiza walalamishi kuwasilisha stakabadhi za kesi kwa washtakiwa mara moja. Hata hivyo, hakutoa maagizo ya muda waliyokuwa wameomba.Mzozo huo unahusu Kanuni ya 25(1)(b) ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Serikali za Kaunti ya mwaka 2015, ambayo inaelekeza kuwa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa kaunti hayafai kuzidi asilimia 35 ya jumla ya mapato ya kaunti. Walalamishi wanasema kiwango hicho kiliwekwa kulinda uthabiti wa kifedha na kuhakikisha angalau asilimia 65 ya mapato ya umma yanatumiwa katika maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, serikali za kaunti zilitumia Sh207.99 bilioni kwa mishahara na marupurupu katika mwaka wa kifedha wa 2023/24, sawa na asilimia 45 ya mapato yao yote. Ripoti hiyo ilionyesha kuwa ni kaunti chache sana zilizofanikiwa kuzingatia kiwango kilichowekwa kisheria.Taarifa za hivi majuzi pia zinaonyesha kuwa kaunti 42 zilitumia kati ya asilimia 37 na 63 ya mapato yao kwa mishahara na marupurupu katika miezi tisa hadi Juni 2026. Kwa kipindi hicho, kaunti hizo zilitumia Sh171.36 bilioni kwa mishahara dhidi ya mapato ya Sh386.59 bilioni. Walalamishi wanaonya kuwa ongezeko la matumizi ya mishahara limeathiri utoaji wa huduma muhimu kama afya, maji, usafi wa mazingira, kilimo na ujenzi wa barabara. Wanasema hali hiyo imechangia kukwama kwa miradi ya maendeleo, uhaba wa dawa hospitalini, kucheleweshwa kwa malipo ya wasambazaji na kuongezeka kwa madeni ya kaunti.Kesi hiyo, ambayo imetaja kaunti zote 47 kama wahusika wenye maslahi, itatajwa tena mahakamani Oktoba 12 kwa maelekezo zaidi

read more