T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 04:55:42

Oburu angali Uingereza, asubiri madaktari wampe idhini kurejea

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, bado yuko nchini Uingereza akipokea matibabu huku familia yake ikisema hali yake imeimarika lakini bado hajaruhusiwa na madaktari kurejea nchini. Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, ambaye ni dadake mdogo, alisema mwanasiasa huyo mkongwe anaendelea kufuatiliwa na madaktari na familia haijafanya mipango yoyote ya haraka ya kumrejesha nyumbani. Kwa mujibu wa Bi Odinga, jambo la msingi kwa sasa ni kuruhusu madaktari kukamilisha kukagua afya yake kabla ya uamuzi wowote kufanywa kuhusu safari yake ya kurejea Kenya. "Ameimarika sana, lakini hatujapanga kurejea kwake Kenya kwa sasa," alisema Bi Odinga akiwa Uingereza. Aliongeza kuwa familia haina haraka ya kumrejesha nchini kwa kuwa bado ana miadi kadhaa ya matabibu ambayo lazima ahudhurie. Bi Odinga alifafanua kuwa Dkt Oginga hajalazwa hospitalini kwa sasa. Badala yake, anaishi karibu na hospitali anayohudumiwa ili iwe rahisi kuhudhuria ukaguzi na miadi ya madaktari. "Hajalazwa. Tunaishi karibu na hospitali, kwa hivyo ni rahisi kwake kuonana na madaktari wakati wowote anapohitajika," alisema. Familia hiyo imesisitiza kuwa afya ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 83 ni muhimu zaidi kuliko majukumu yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, hawataki kuharakisha kurejea kwake kabla madaktari kuthibitisha kuwa yuko katika hali nzuri. Habari hizo zinajiri huku Dkt Oginga akiendelea kushiriki shughuli mbalimbali kwa njia ya mtandao akiwa Uingereza. Wiki hii alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akieleza kuwa yeye na mkewe, Mama Judy, walimpokea Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Maurice Makoloo, katika makazi yao.  Alisema walijadili jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Uingereza, kusaidia Wakenya wanaoishi ughaibuni pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji na ujuzi wao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 03:55:09

Ziara ya Nyanza ilivyomkweza Raila Jnr katika siasa za taifa

NYOTA ya kisiasa inaonekana imeanza kumng'aria Raila Jnr, mwanawe marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga akionekana kujitosa kwenye siasa mzimamzima kwa kuungana na Rais William Ruto katika ziara ya siku tano eneo la Nyanza. Raila Jnr aliandamana na Rais Ruto alipoanza ziara yake Kaunti ya Kisumu, akaenda naye katika Kaunti ya Siaya kisha akafululiza na kiongozi wa nchi hadi Kaunti ya Migori. Ni mkutano wa Kaunti ya Homa Bay, siku ya mwisho ya ziara ya Rais mnamo Alhamisi ndiyo alikosa kwa sababu familia ilikuwa ikizindua kamati ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha 'Baba' Nairobi. Hadhi ya Raila Jnr ilionekana kuwa juu wakati wa mkutano wa viongozi waliochaguliwa katika eneo la Luo Nyanza mnamo Jumapili kwenye ikulu ya Kisumu. Baada ya wabunge na maseneta kutoka kaunti zote nne kutambulishwa, Kiongozi wa wachache Junet Mohamed alimwalika Raila Jnr ahutubu. Hii inaweza kufasiriwa kuwa huenda alipewa hadhi ya juu kwa kuwa baada ya kumaliza hotuba yake, Bw Mohamed aliwaalika magavana kisha Rais akapewa nafasi ya kuongea. "Mheshimiwa karibu sana Kisumu na mimi kama kijana wa baba nasema kuwa mlikuwa na ndoto sawa na Raila si kwa eneo la Nyanza pekee bali pia Kenya mzima," akasema Jnr huku akishangiliwa na umati ambao ulisikika ukisema 'wewe ndiye baba aliyebaki'. "Watu wetu kile ningependa kuwaambia ni kwamba Baba alituambia tukae pamoja na tufanye hivyo kwa kusalia ndani ya ODM," akaongeza akiwa ameandamana na shangazi yake Tabby Osewe. Mnamo Jumatatu, Jnr aliandamana na Rais Ruto katika kufungua miradi mbalimbali katika Kaunti ya Kisumu ikiwemo barabara ya Chiga-Rabuor na miradi mingine katika eneobunge la Muhoroni. Familia ya Baba yaunga Ruto Mnamo Jumanne, Junior aliandamana na Rais katika kutathmini na kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo daraja la Dho Goye, kukagua uwanja wa Jaramogi mjini Siaya miongoni mwa miradi mingine. "Mheshimiwa Rais nakukaribisha hapa Siaya na nina kuku ambaye Mama Ida amenipa nikupee. Hapa sisi tunakuunga mkono kupitia chama cha ODM na kama familia ya baba tuko nawe hadi 2027," akasema. "Huku ni nyumbani, mimi na ami yangu Dkt Oburu Oginga tunakuunga. Kama watu wa Siaya endelea kutuhudumia na miradi ijae huku kwa sababu tuko nawe hadi mwisho," akasema baada ya kualikwa na Rais. Ziara ya Migori nayo ilionekana kusisimua zaidi kwa sababu Jnr alishangiliwa huku akisema ana ndoto ya kisiasa ya babake ambayo lazima ayatimize. "Mimi pia ni Raila na baba aliacha chama kikubwa na si cha wazee pekee bali watu wote. Kwa sasa tuko ndani ya Serikali Jumuishi na hata eneo letu pia nalo lazima liendelee," akasema akiwa Migori. Kwenye mahojiano na Taifa Leo baada ya ziara hiyo ya Nyanza, Jnr alisema kuwa analenga kutia bidii katika siasa na kujitafutia umaarufu badala ya kutumia jina la familia. "Siwezi kuketi tu kwa sababu mimi ni mwana wa Raila, lazima pia nionyeshe juhudi na kujifunza kutoka kwa wanasiasa wazoefu ambao watanishika mkono. Mimi pia sasa ni mwanasiasa," akasema akisisitiza kuwa pia ataendeleza kampeni yake katika eneobunge la Kibra. Analenga kumbandua mbunge wa sasa Peter Orero ambaye alikuwa mwandani wa marehemu babake na anahudumu muhula wake wa kwanza. Aliyekuwa mbunge Imran Okoth pia anasaka kiti hicho Jnr, 46, akiingia bungeni mwaka ujao, atakuwa anafanya hivyo kwa umri sawa na alivyofanya babake mnamo 1992. Marehemu Raila alichaguliwa mbunge wa Langata kupitia Ford Kenya huku babake akiwahi nafasi kama hiyo kule Bondo. Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo, ni wazi Rais Ruto ameamua kumshika Jnr mkono na kumtambisha baada ya dadake Winnie kutoonekana kujihusisha sana na masuala ya uongozi. "Winnie ni mbunge wa EALA na hata mwanzoni alionekana kujihusisha sana kisiasa kuliko Jnr. Hata hivyo, Jnr ameonyesha wazi yuko tayari kushikwa mikono na kufanya kazi na Rais,'' akasema Bigambo "Baada ya kuidhinishwa na Mama Ida awanie kiti cha ubunge wa Kibra, inaonekana ameamua kujitosa mzimamzima katika siasa na kupigania nafasi yake. Yupo pazuri kuwa mrithi wa siasa za ufalme wa Jaramogi," akaongeza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 20 Sep 2026 02:55:27

Museveni asema ameshangazwa na ujanja wa Kenya

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amesema nchi yake ilisitisha ununuzi wa mafuta kupitia Kenya baada ya kugundua kile alichokitaja kuwa udanganyifu uliokuwa ukiigharimu mabilioni ya shilingi kupitia mabroka. Akizungumza nchini Uganda, Museveni alisema mpango uliokuwa ukitumika haukuwa wa serikali kwa serikali (G2G) kama ulivyowasilishwa, bali ulikuwa mpango wa "serikali kwa mabroka", ambapo Uganda ilinunua bidhaa za petroli kupitia mawakala waliokuwa wakinufaika kwa gharama ya walipa ushuru. Uganda, ambayo haina bandari ya bahari, kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea Bandari ya Mombasa na mtandao wa mabomba ya mafuta wa Kenya kuagiza mafuta yake. "Kulikuwa na mawakala nchini Kenya waliokuwa wakiuzia Uganda mafuta. Hii ilikuwa janga kubwa. Sikujua hadi nilipoelezwa na seneta mmoja kutoka Kenya," alisema Museveni. Kulingana na rais huyo, alipopewa taarifa hizo aliwaagiza maafisa wake wa nishati kuchunguza suala hilo lakini hatua za haraka hazikuchukuliwa. Hata hivyo, baada ya uchunguzi zaidi, Uganda ilibadili mfumo wake wa ununuzi wa mafuta. Kwa sasa Uganda inaagiza mafuta kupitia ushirikiano kati ya Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na kampuni ya Vitol, kufuatia mabadiliko ya sera yaliyofanywa mnamo 2023. Museveni alisema hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za mafuta. Kulingana na takwimu zilizotolewa na Katibu wa Wizara ya Nishati nchini Uganda, Irene Batebe, Uganda ilikuwa ikilipa wastani wa Sh15,340 kwa tani moja ya dizeli chini ya mfumo wa zamani, ikilinganishwa na Sh10,790 chini ya mfumo wa sasa. Kwa petroli, gharama ilishuka kutoka Sh12,675 kwa tani moja hadi Sh7,995, huku gharama ya mafuta ya ndege ikishuka kutoka Sh14,853 hadi Sh10,303 kwa tani moja. Aidha, serikali ya Rais William Ruto ilieleza kuwa mpango wa serikali kwa serikali (G2G) ulianzishwa mnamo 2023 ili kupunguza shinikizo la fedha za kigeni nchini. Serikali ilisema sekta ya mafuta ilikuwa ikihitaji karibu Sh64.7 bilioni kwa mwezi fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa mafuta, hali ambayo ilikuwa ikitishia akiba ya fedha za kigeni na usalama wa nishati nchini. "Sitasahau takwimu hizo. Zinathibitisha jinsi tulivyokuwa tukipunjwa kwa miaka mingi," alisema Museveni. Kauli yake imezua mjadala mkubwa nchini Kenya, hasa kutokana na jinsi serikali ya Rais William Ruto ilivyokuwa imewasilisha mpango wa G2G kama suluhu ya kupunguza shinikizo la fedha za kigeni na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini. Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Kenya Charles Owino alijibu kwa njia ya kidiplomasia akisema uhusiano kati ya Kenya na Uganda unaendelea kuwa mzuri. "Tuna uhusiano mzuri wa kikazi na Uganda. Tunaendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali ya miundombinu ya mafuta," alisema Owino. Wakati huo huo, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ameunga mkono madai ya Museveni akisisitiza kuwa mpango huo uliwanufaisha watu binafsi badala ya serikali ya Kenya. Akizungumza katika mkutano nchini Amerika, Gachagua alidai kuwa biashara ya mafuta ni ya thamani ya mabilioni ya pesa na kwamba wanaonufaika ni watu walio ndani ya utawala wa Kenya Kwanza. Kwa upande wake, mshauri wa rais wa masuala ya uchumi David Ndii alipinga madai hayo kupitia mtandao wa X, akisema kampuni zinazouzia Kenya mafuta zinamilikiwa na serikali husika, huku kampuni inayouzia Uganda ikiwa ya kibinafsi. Mjadala huo umeendelea kuibua maswali kuhusu uwazi katika biashara ya mafuta na iwapo mfumo wa G2G uliokuwa ukitumika uliwanufaisha wananchi au mawakala. Licha ya mvutano huo wa kisiasa, Kenya na Uganda zinaendelea kutegemeana kiuchumi, hasa katika sekta za biashara, usafirishaji na nishati, huku wadadisi wakisubiri kuona iwapo madai ya Museveni yatachochea uchunguzi zaidi kuhusu biashara ya mafuta katika eneo la Afrika Mashariki.

read more