T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 11 Sep 2026 08:55:30

TAHARIRI: El Nino sasa imekaribia, tukae ange

KWA muda wa miezi kadhaa, wataalamu wa hali ya anga wamekuwa wakiutahadharisha ulimwengu kuhusu ujio wa mvua ya El Nino. Kulingana na ripoti za kitaalamu, kipindi cha kuanza kwa mvua hiyo inayotarajiwa kuzua madhara tele kimewadia. Huku mvua hiyo kubwa ikitarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya Kenya kuanzia Oktoba, Serikali imewaonya wananchi wanaoishi kando ya mito, katika maeneo ya mabonde na maeneo mengine yenye hatari kuhama mapema na kutafuta makao salama. Ushauri huu haupaswi kupuuzwa. Ni wito wa kuokoa maisha. Historia ya Kenya imejaa mifano ya madhara yanayosababishwa na mvua kubwa. Mafuriko huvamia makazi, mito huvunja kingo, hubomoa madaraja na kuvuruga barabara. Katika maeneo yenye miinamo, udongo uliolowa maji unaweza kusababisha maporomoko ya ardhi, huku nyumba zisizo imara zikiwa katika hatari ya kuporomoka. Wakazi wanaoishi kando ya mito na katika maeneo yaliyotambuliwa kuwa hatari wanapaswa kuzingatia maagizo ya kuhama. Familia katika maeneo kama vile Budalang'i na Nyando zinapaswa pia kuwa na mpango wa dharura unaoeleza mahali pa kwenda, njia salama za kufika huko na namna ya kuwasiliana iwapo wanafamilia watatenganishwa na mafuriko. Aidha, wananchi wanapaswa kusaidia mamlaka kusafisha mifereji na njia za kupitisha maji. Mifereji iliyozibwa na taka huzidisha mafuriko, hasa mijini. Serikali za kaunti nazo zinapaswa kuhakikisha mifereji inasafishwa, madaraja na barabara zinazohitaji matengenezo zinashughulikiwa na vituo vya kuhifadhi waathiriwa vinaandaliwa mapema. Madereva nao hawapaswi kujaribu kuvuka maji yanayotiririka kwa kasi. Maji yanayosonga yana nguvu kubwa na yanaweza kulisomba gari pamoja na abiria wake. Wazazi wanapaswa kuwaonya watoto dhidi ya kucheza au kuvuka mito na mifereji iliyojaa maji. Muhimu zaidi, wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na maonyo kutoka kwa mamlaka badala ya kutegemea uvumi mitandaoni. Serikali imesema imeanza kutumia viongozi wa mashinani, wakiwemo machifu na viongozi wa Nyumba Kumi, kufikisha tahadhari kwa wananchi. Madhara ya El Nino yanaweza kupunguzwa ikiwa tahadhari zitachukuliwa mapema. Serikali na wananchi wana jukumu la kuhakikisha kuwa tahadhari hizi kuhusu mvua hiyo zinazingatiwa kwa dhati. Wakati wa kuhama ni kabla ya mafuriko, nao wakati wa kujiandaa ni sasa. Tusisubiri maafa yatufundishe thamani ya tahadhari na maisha yetu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 11 Sep 2026 07:55:52

Kunywa chai moto sana huongeza hatari ya saratani ya umio – Utafiti

KUNYWA chai, kahawa au vinywaji vingine vikiwa moto sana kunaweza kuongeza hatari ya kupata saratani ya umio, kulingana na utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza. Utafiti huo, uliochapishwa katika Jarida la International Journal of Cancer, ulihusisha watu 977,282 wenye umri wa juu na umeelezwa kuwa mojawapo ya tafiti kubwa zaidi kuchunguza uhusiano kati ya joto la vinywaji na saratani ya umio. Watafiti waligundua kuwa watu waliokunywa vinywaji vilivyo na joto la nyuzi 65 au zaidi walikuwa na hatari karibu mara tatu zaidi ya kupata saratani hiyo ikilinganishwa na waliokunywa vinywaji vya vuguvugu. Kulingana na watafiti, mvuke wenye joto kali unaweza kuharibu chembe zinazofunika umio wakati unapopita kuelekea tumboni. "Kunywa vikombe sita au zaidi vya vinywaji vya moto kwa siku kunaweza kuongeza hatari hiyo. Kuongezwa kwa maziwa kunaweza kupunguza joto kidogo, lakini chai au kahawa yenye maziwa bado inaweza kuwa moto kupita kiasi," unasema utafiti huo. Chai inayotengenezwa mara tu baada ya maji kuchemka inaweza kuwa na joto la karibu nyuzijoto 100. Inapomiminwa kwenye kikombe, joto hilo hupungua hadi karibu nyuzi 90–95. Wataalamu wanashauri watu kusubiri kwa dakika chache kabla ya kunywa ili kinywaji kipoe hadi joto linalofaa. Mtaalamu wa Afya, Dk Keren Papier, alisema tafiti za awali Amerika Kusini, ambako watu wengi hunywa kinywaji cha mitishamba kikiwa moto sana, pia zilionyesha uhusiano wa kupata aina hiyo ya saratani. Hata hivyo, watafiti walisema hatari ya jumla ya kupata saratani ya umio bado ni ndogo hata kupitia unywaji wa vinywaji moto. Njia muhimu zaidi za kupunguza hatari ni kutovuta sigara na kupunguza unywaji wa pombe. Dalili za saratani ya umio zinaweza kujumuisha kiungulia, maumivu ya koo au kifua na kupungua uzani wa mwili.

read more