T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 07:55:20

Uchaguzi wa 2027 utakuwa ghali zaidi katika historia ya Kenya

UCHAGUZI Mkuu wa 2027 unatarajiwa kuwa ghali zaidi katika historia ya Kenya, huku makadirio yakionyesha kuwa serikali, vyama vya kisiasa na wagombea watatumia zaidi ya Sh272 bilioni katika mchakato mzima wa uchaguzi. Kiasi hicho kinajumuisha bajeti ya Sh74.8 bilioni ambayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imekadiria kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo pamoja na takriban Sh197.35 bilioni ambazo wagombea wanaweza kutumia katika kampeni zao iwapo watazingatia viwango vya matumizi vilivyowekwa na tume hiyo. Kwa miaka mingi, uchaguzi nchini Kenya umejulikana kwa nyimbo, kauli mbiu na kampeni za kuvutia. Hata hivyo, matumizi makubwa ya fedha yameibua maswali kuhusu vipaumbele vya taifa wakati sekta muhimu kama afya, elimu na kilimo zinaendelea kukabiliwa na changamoto za ufadhili. Kiasi cha Sh272 bilioni ni zaidi ya nusu ya fedha zilizotumiwa kuendesha kaunti zote 47 nchini katika mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2025, ambazo zilikuwa Sh470.7 bilioni. Pia fedha hizo zinaweza kulipa kikamilifu madeni ambayo serikali za kaunti zinadaiwa ya zaidi ya Sh156 bilioni. Kwa mtazamo mwingine, kiasi hicho ni kikubwa kuliko bajeti za baadhi ya sekta muhimu katika uchumi. Kwa mfano, sekta ya afya ilitengewa Sh177.2 bilioni, elimu ya juu Sh163.9 bilioni na elimu ya msingi Sh136.6 bilioni katika bajeti ya hivi karibuni ya serikali. IEBC inasema gharama kubwa ya uchaguzi inatokana na teknolojia ya uchaguzi, vifaa vya kutambua wapigakura, mifumo ya kutuma matokeo, karatasi za kura zenye vipengele vya usalama pamoja na ongezeko la idadi ya wapigakura. Tume hiyo inalenga kusajili wapigakura milioni 28.5 kufikia mwaka 2027, ikilinganishwa na milioni 22.1 waliopiga kura mwaka 2022. Ongezeko hilo litahitaji vituo vya kupigia kura 55,393 kutoka vituo 46,229 vilivyotumika mwaka 2022. Kwa upande wa wagombeaji, viwango vipya vya matumizi ya kampeni vinaonyesha kuwa kinyang'anyiro cha kisiasa kitahitaji fedha nyingi zaidi. Mgombea urais ataruhusiwa kutumia hadi Sh6.1 bilioni, kutoka Sh4.7 bilioni mwaka 2022. Wagombeaji wa ugavana, useneta, ubunge na uwakilishi wa wanawake pia watatumia mabilioni ya fedha katika kampeni zao. Mbunge wa Likuyani, Innocent Mugabe, anasema kiwango cha matumizi kilichowekwa na IEBC ni cha chini ikilinganisha na hali halisi ya kampeni. "Nilitumia takriban Sh50 milioni mwaka 2022. Ukiwa na nia ya kushinda, lazima utumie fedha zaidi," alisema. Kwa mujibu wa IEBC, mipaka ya matumizi ya kampeni inalenga kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, uwazi na uwajibikaji, na kwamba matokeo ya uchaguzi yanaamuliwa na wapigakura badala ya nguvu ya fedha. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wamehoji jinsi sheria hizo zitakavyotekelezwa, wakisema bado Kenya ina mfumo mkubwa wa matumizi ya fedha taslimu ambao ni vigumu kufuatilia. Iwapo makadirio ya sasa yatatimia, uchaguzi wa 2027 utaweka rekodi mpya kama uchaguzi wa gharama kubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 30 Aug 2026 06:55:37

Azma ya Raila Jnr Kibra yachemsha Orero, Imran

KUJITOSA kwa Raila Junior katika kinyang'anyiro cha ubunge wa Kibra, Nairobi, kumeanza kuzua pingamizi miongoni mwa baadhi ya wawaniaji wa ODM, huku mwana huyo wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga akisaka kiti hicho 2027. Kibra kwa miongo imekuwa ngome ya kisiasa ya familia ya Odinga. Marehemu Raila aliwakilisha eneo hilo bungeni kuanzia 1992 hadi 2013, wakati Kibra ilikuwa sehemu ya Lang'ata. Kila mara nchi ilipokabiliwa na maamuzi magumu ya kisiasa, Raila alirejea Kibra kutoa mwelekeo ambao baadaye ulikumbatiwa na maeneo mengine nchini. Mnamo Novemba 30, 2009 wakati wa mvutano kuhusu uamuzi wa kufurusha watu kutoka msitu wa Mau, Raila alitangaza hadharani kwamba alikuwa tayari kurejea Kibra akapike mandazi iwapo suala hilo lingemgharimu kisiasa. Kuingia kwa Raila Junior katika kivumbi hicho kumezua ushindani mkali wa kisiasa kati yake, mbunge wa sasa wa Kibra Peter Orero na aliyekuwa mbunge wa hapo Imran Okoth. Junior amekuwa akishiriki miradi ya kijamii na kukutana na makundi mbalimbali huku akiweka misingi ya kampeni zake kuelekea 2027. "Kibra ilikuwa ngome ya kisiasa ya babangu, na kama familia tumekuwa na safari ndefu pamoja na watu wa eneo hili. Nikichaguliwa nitamakinikia sana elimu kwa kuhakikisha basari zinapatikana ili pasiwe na mtoto anayekosa fursa ya kupata elimu," mwana huyo mdogo wa Raila alisema katika mahojiano na Jamvi.  "Najua baadhi ya sekta kama afya na maji zimekabidhiwa serikali za kaunti, lakini nitafanya kila niwezalo kuhakikisha huduma hizo zinafikia watu wa Kibra. Tutazingatia sana kuboresha maisha ya wakazi kwa kila njia iwezekanavyo," akaongeza. Junior pia alifichua kuwa kwa miaka mingi alikuwa miongoni mwa wandani waliompangia babake mikakati ya kisiasa huko Kibra. Wiki hii mama yake, Ida Odinga, alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, alitangaza kwamba amempa Raila Junior baraka za kutimiza ndoto zake za kisiasa, ikiwemo azma yake ya kuwania ubunge wa Kibra. "Nyinyi watu wa Kibra mmeamua na sina chaguo jingine. Namkabidhi mwanangu mikononi mwenu. Viongozi mlio hapa mtunze, mfundishe na mpe mwongozo. Wengi wenu mlianza siasa pamoja na Baba. Mwonyesheni njia," akasema Mama Ida. Alisisitiza kuwa siasa za Junior zinapaswa kuwa safi na zisizo na matusi wala vurugu, akisema Kibra ilikuwa msingi wa safari ya kisiasa ya familia ya Odinga. "Washawishi watu kwa maneno yako na uwaambie kile unachoweza kuwafanyia," akasema. Hata hivyo, mbunge wa sasa Orero anadai Junior anasukumwa na baadhi ya wawakilishi wadi (MCAs) maalum ambao hawana ushawishi wa kisiasa Kibra. Alisisitiza yuko tayari kukutana na Junior kwenye debe. "Baadhi ya wawakilishi wadi maalum wanaomsukuma wamepoteza uchaguzi mara nne, na wanalenga maslahi yao binafsi. Hata hivyo, kazi yangu Kibra iko wazi kwa kila mtu kuona. Sina mpinzani. Aje tushindane, nami nitamshinda," akahoji Orero. Alishangaa kwa nini Junior amejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho ilhali dada yake, Winnie Odinga, aliwahi kukinyemelea kabla kujiondoa na kuelekeza nguvu zake katika kivumbi cha useneta Nairobi. Orero alisema licha ya kuwa karibu na familia ya Odinga hajazungumza na Mama Ida kuhusu azma ya Junior. "Kuna nini cha kuzungumza? Junior ana haki yake ya kidemokrasia na sitaki kuwadharau au kuonekana niko kwenye vita nao. Waache watu waamue," akasema mbunge huyo. Kwa upande wake aliyekuwa mbunge Imran Okoth ametishia kuondoka ODM na kuwania kiti hicho kama mgombea huru iwapo chama hakitaendesha uteuzi wa haki na huru. "Junior yuko huru kuja kuwania lakini ajue sisi ni wanachama wa ODM na tunasisitiza kusiwe na mapendeleo yoyote. Orero, Junior na mimi tushindane kwa haki, na atakayeshinda apewe tiketi ya ODM," akahoji.

read more