T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 08:55:45

EACC yafichua mtandao mpana wa maafisa wa kaunti kutumia wanafamilia kufyonza mamilioni

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imefichua mtandao mpana wa ufisadi katika serikali za kaunti ambapo maafisa wa umma wanadaiwa kutumia watoto, wake na jamaa zao wa karibu kupata zabuni za serikali. Kesi nyingi zilizochunguzwa na tume hiyo zinaonyesha kuwa baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakikwepa sheria zinazowazuia kufaidika na zabuni za taasisi wanazofanyia kazi kwa kusajili kampuni kwa majina ya ndugu zao. Katika Kaunti ya Kitui, EACC ilibaini kuwa kati ya mwaka 2018 na 2025, kampuni za Shanel Construction Company Ltd, ECO Stone Company Ltd, AZ Links Company Ltd, DTK Construction Company Ltd na 4 Walls Company Ltd zililipwa jumla ya Sh14.1 milioni na serikali ya kaunti. Kwa mujibu wa rekodi, kampuni hizo zinamilikiwa na Josephine Mwikalu Wambua, Makoma Wambua na Emmanuel Wambua. Hata hivyo, uchunguzi wa EACC ulibaini kuwa watu hao ni jamaa wa karibu wa Gladys Mami Kivoto, Afisa Mkuu katika Idara ya Kilimo, Uvuvi na Unyunyuzaji ya Kaunti ya Kitui. Wakati zabuni hizo zilipokuwa zikitolewa na malipo kufanywa, Bi Kivoto alikuwa ndiye afisa mwenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi katika idara hiyo. Tume hiyo inadai kuwa alitumia nafasi yake kuhakikisha jamaa zake wanapewa zabuni na kulipwa. Uchunguzi pia ulifuatilia mzunguko wa fedha kati ya kampuni hizo, wamiliki wake na Bi Kivoto. Watu hao wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ulaghai katika shughuli za ununuzi wa umma. Katika Kaunti ya Turkana, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imeanza mashtaka dhidi ya Peter Long'ole Apua, afisa mkuu wa fedha wa kaunti hiyo na mkurugenzi wa Apuco Holdings Group. Jamaa zake Christopher Imuron Apua na Moses Along'ole Apua pia ni wakurugenzi wa kampuni hiyo iliyolipwa Sh62 milioni na serikali ya kaunti. Kaunti hiyo pia inahusishwa na kesi ya Lilian Akiru Louruka, mwalimu wa chekechea, ambaye kampuni yake ya Natiltila Company Ltd ilipewa zabuni tano zenye thamani ya Sh30 milioni. EACC inadai kuwa yeye na mume wake ndio wakurugenzi wa kampuni hiyo. Katika Kaunti ya Nakuru, kampuni tatu za Denken Building and Construction Limited, Murinchamba Investments Limited na Windcom Solutions Limited zilipokea zaidi ya Sh120.6 milioni kutoka kwa serikali ya kaunti kati ya mwaka wa fedha wa 2020/21 na 2024/25. Uchunguzi ulionyesha kuwa kampuni hizo zinamilikiwa na mchumba wa mfanyakazi wa kaunti anayehudumu kama mwanauchumi. EACC ilibaini kuwa baadhi ya fedha zilitumwa kwa maafisa waliokuwa wakihusika katika mchakato wa zabuni, ukaguzi wa kazi na uthibitishaji wa malipo. Mojawapo ya kampuni hizo pia ilidaiwa kuwasilisha stakabadhi za kughushi wakati wa zabuni. Katika uchunguzi mwingine wa Nakuru, kampuni za Tirzah Logistics, Purim Logistics na Nemoca Enterprises zilipokea Sh45.64 milioni kutoka kwa serikali ya kaunti. Wakurugenzi wa kampuni hizo walibainika kuwa watoto wa afisa mkuu mmoja. Kaunti ya Migori pia imekumbwa na tuhuma sawa. EACC ilichunguza kampuni za Enigma Solutions na Enigma Solutions Limited na kubaini kuwa zilihusishwa na afisa mkuu wa afya ya umma, huku mume wake akiwa mkurugenzi pekee na mtia saini wa akaunti za benki za kampuni hizo. Kampuni hizo zilipata mikataba 19 ya thamani ya Sh27.2 milioni kati ya mwaka 2023 na 2024 kwa usambazaji wa chakula, vifaa vya ofisi, utengenezaji wa magari na huduma nyingine. Katika Wajir, maafisa wawili wa kaunti walidaiwa kuhamisha hisa za kampuni yao kwa mtu mwingine lakini wakaendelea kuwa watiao saini wa akaunti zake za benki. Kampuni hiyo ililipwa Sh3.99 milioni bila kufuata taratibu za ununuzi. Kaunti ya Marsabit nayo ilitajwa baada ya afisa wa afya kudaiwa kuwa mkurugenzi wa kampuni iliyolipwa Sh45.6 milioni kwa bidhaa na huduma ambazo baadhi yake hazikuwasilishwa. Uchunguzi wa EACC unaonyesha kuwa mtindo wa kutumia wanafamilia kupata zabuni umeenea hata nje ya serikali za kaunti. Katika Taasisi ya Rift Valley Institute of Science and Technology (RVIST), kampuni ya Afripath Care Kenya Limited ilipewa zabuni ya Sh57 milioni. Tume ilibaini kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo ni shemeji wa Mbunge wa Kitutu Chache North. Baada ya malipo kufanywa, karibu Sh40 milioni zilihamishwa kutoka kwa akaunti ya kampuni hiyo kwenda kwa mbunge huyo. EACC ilisema mbunge huyo alitumia Sh10 milioni kununua ardhi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 07:55:20

Kinachochangia matineja kuwa na hamu kubwa ya kula bila kunenepa

BAADHI ya maudhui katika mitandao ya kijamii hasa watoto wanapokaribia kufunga shule kwa likizo, huwa ni watu wakiulizana kuhusu bajeti zao za chakula. Mbali na kiwango cha chakula, kuna wale wanaozungumzia saa ambapo wana wao hutaka kula, wengine hata wakisaka chakula usiku wa manane. Hata hivyo, wataalamu wa lishe wanasema kuwa watoto hawa ambao pia wako katika umri ambao muda wao mwingi wanatumia katika masomo, asilimia ishirini ya kiwango cha chakula wanachokula kila mara hutumika na ubongo. Kulingana na Tom Wanjala, baba wa watoto watatu ambaye kifungua mimba wake ana umri wa miaka 16 na mchezaji wa mchezo wa raga, anasimulia jinsi alivyoshuhudia mabadiliko hayo kwa mwanawe. "Punde tu kifungua mimba wangu alipofikisha umri wa miaka 13, alianza kula chakula kingi zaidi. Hivi majuzi alipokuwa nyumbani kwenye likizo nilipokuwa nikimuangalia anavyokula sima maanake nilikuwa naye mezani, ndipo nilithibitisha kuwa katika umri wake na pia akiwa mtoto wa kiume anakula zaidi ya watu wengine katika familia," anasema mzazi huyo. Baba huyo pia anasema kuwa mwanawe alipokuwa wa umri mdogo, hamu yake ya kula ilikuwa chini sana. Kulingana naye, kumuona mwanawe kuwa na hamu ya juu ya kula kunamdhihirishia jinsi anavyozidi kukua. Hamu ya kula imezidi "Hata mwanangu ambaye ana umri wa miaka 10 pia nimegundua kuwa hamu yake ya kula imezidi kuongezeka kinyume na alivyokuwa akila hapo awali. Miaka ya hapo awali haswa walipokuwa chini ya umri wa miaka saba, nilikuwa nikiwalazimisha wote wawili kula lakini kwa sasa wanataka chakula wenyewe tena kwa wingi," anaongeza Tom. Mzazi huyo ambaye anaelewa sayansi ya matumizi ya lishe mwilini miongoni mwa watoto wanaobalehe, anasema kuwa kwa sasa jukumu lake ni kuhakikisha kuwa wanawe hawakosi chakula ilikuwasaidia kukua. "Huwa namruhusu mwanangu ale kwa sababu najua atafika katika umri ambapo hamu yake ya chakula itapunguka jinsi tu yangu ilivyopunguka. Nilipokuwa kwenye umri wa kubalehe nilikuwa nikila jinsi tu mwanangu anavyokula kwa sasa. Nafahamu kuwa anahitaji nguvu nyingi za kutembea, kucheza na pia kwenye shughuli tofauti maanake ni vigumu sana kumpata akiwa ameketi tu na kutulia sehemu moja akiwa nyumbani," anasimulia. Alfrique Otieno Mwana, pia anashuhudia hali sawia kwake. "Kifungua mimba wangu yuko katika Gredi 10. Wakati alipokuwa nyumbani kwenye likizo na kuketi kwenye meza alikuwa akipakua chakula kingi ambacho alikuwa akila chote. Mwenzake mdogo ambaye pia ni mvulana wa umri wa miaka 10 pia hula kiwango cha juu cha chakula kinyume na hapo awali," anasema mzazi huyo. Wakati uo huo, Alfrique anasema kuwa kifungua mimba wake ambaye yuko katika shule ya bweni huwa na hamu ya juu ya chakula kutokana na tamaa ya kukosa chakula cha nyumbani kwa muda. "Anapokuja nyumbani wakati wa likizo anataka sana kula chapati na akipewa moja au mbili hashibi. Unapata anakula tatu au nne ndiposa anashiba. Huwa namhimiza ale hadi ashibe kwa sababu hivyo ndivyo babangu alivyonifunza kula ilmradi siharibu chakula. Ninapomuona mwanangu anapokuwa na hamu ya juu ya kula chakula najua ni umri wake ambao ataupita siku za usoni," anasema. Ishara ya kukua Kama tu Tom, mzazi Alfrique pia anakumbuka jinsi wanawe walipokuwa wachanga hawakuwa na hamu ya kula chakula. Kuwaona hamu yao ikiongezeka ni ishara kwake kuwa wanakua. "Wakati wakiwa kwenye likizo wanakula mara tatu kwa siku na pia wanakula vitafunio katikati. Kitinda mimba wangu wa umri wa miaka miwili angali hana hamu ya kula hivyo mara nyingi anakula kiamsha kinywa kuchelewa kisha anakula chajio mapema kwa sababu huwa anaamka kuchelewa na pia analala mapema," anasema Alfrique. Kiwango cha lishe katika umri wa watoto wanaobalehe hutegemea na viwango vyao vya ukuaji. Haya ni kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe ya kitabibu katika hospitali ya, Aga Khan University Hospital, Valentine Young Kwadha. Wakati uo huo, anaeleza kuwa mabadiliko yanayoendelea katika mwili wa mtoto kuanzia umri wa miaka 10 huhitaji ale chakula kingi zaidi ya alivyokuwa akila hapo awali. Hali hii anasema huchangia mtoto anayebalehe kula angalau asilimia 25 ya chakula zaidi ya kiwango ambacho mtu mzima katika familia hula. "Haistahili kuwa jambo la kushtua kuona mtoto anayebalehe akila chakula kingi kwa sababu hicho ndicho kiwango wanachohitaji kulingana na shughuli za kimwili..Mahitaji ya nguvu mwilini mwa watoto hawa kwa ujumla huanzia 2,000 hadi 3,000 kilokalori kila siku. Hii ni sawa na kusema kuwa mtoto anakula mara sita kwa siku kwa sababu wanakula mara nyingi na kiwango cha chakula wanachokula pia kinaongezeka," anaeleza mtaalamu huyo. Kiwango cha mazoezi ya mwili Pia anasema kuwa kiwango cha chakula watoto hawa hula hutofautiana kulingana na urefu, jinsia na kiwango cha mazoezi miongoni mwao. Kwa mfano, mtoto wa umri wa miaka 13 aliye na urefu wa sentimita 120 atakula chakula zaidi ya mwenzake wa umri sawa lakini urefu wake ni sentimita 100. "Jinsi mwili unavyotumia nguvu na virutubisho kuanzia umri wa miaka 10 hadi 13 huwa juu miongoni mwa watoto wavulana ukilinganishwa na wasichana. Katika umri huu, miili ya wasichana huunda seli za mafuta zaidi huku miili ya wavulana ikiunda misuli. Misuli inahitaji nguvu na virutubisho zaidi," anasema Valentine. Anawashauri wazazi wa watoto walio katika umri wa kubalehe kuwa watoto hao wanastahili kula kila baada ya saa 3-4. Kiamsha kinywa, chakula cha mchana na chajio anasema zinastahili kuwa sehemu kuu ya mlo wao. Katikati ya milo hiyo, anasema kuwa watoto hao wanastahili kula vitafunio kama vile matunda, njugu na sehemu ya kile walichobakisha wakati wa kiamsha kinywa kwa kuzingatia lishe bora. "Sahani ya mtoto anayebalehe inastahili kuwa na wanga, vitamini na protini. Katika umri huu, watoto wanahitaji protini zaidi. Kwa mfano, ikiwa aina ya chakula cha protini unaowalisha ni mayai, basi watahitaji mayai mawili wakati wa kiamsha kinywa, mayai mawili wakati wa chakula cha mchana na mayai mawili kwa chajio. Mayai hayo yatawapa kiwango cha protini wanayohitaji siku hiyo," anaeleza Valentine. Vilevile, anawashauri wazazi kutowalisha watoto zaidi au kiwango cha chini cha chakula ili kuzuia watoto hao kukabiliwa na athari za utapiamlo. Hali hiyo huweza kubainishwa kupitia ushauri wa mtaalamu wa lishe kwa sababu kila mtoto huhitaji ushauri binafsi kulingana na kiwango cha lishe miili yao inahitaji. Kadhalika, anahimiza wazazi kuhakikisha kuwa watoto hawa wanapata usingizi wa kutosha wa kati ya saa nane hadi 10 mfululizo kila usiku, muda ambao pia hawastahili kuwa wanakula.

read more