T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 06:57:03

Serikali kuzindua ujenzi wa kaburi la Raila leo

FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga leo itakabidhi serikali sehemu ya kujenga kaburi la heshima la mwanasiasa huyo mashuhuri wa upinzani. Hafla hiyo itafanyika Kang'o ka Jaramogi, Bondo, Kaunti ya Siaya. Wakati huo huo, mwanawe marehemu, Raila Odinga Junior ameanza kuweka msingi wa kuingia katika siasa za uchaguzi huku akilenga kuwania kiti cha ubunge cha Embakasi Kusini katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Jumapili, Raila Junior alikutana na kiongozi wa ODM ambaye pia ni ami yake , Dkt Oburu Oginga, ambapo walijadili maandalizi ya ujenzi wa kaburi hilo pamoja na siasa. Katika mahojiano na Taifa Leo, Raila Junior alisema mazungumzo yao yalihusu masuala mbalimbali ya kifamilia, huku sherehe ya kukabidhi eneo hilo kwa serikali ikiwa ajenda kuu. Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Ummi Bashir, Gavana wa Siaya James Orengo, wanafamilia, ukoo wa Kawuor pamoja na wakazi wa Bondo wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo katika Kang'o ka Jaramogi, ambako mwili wa Raila ulizikwa. Hafla hiyo itakuwa ya kwanza kwa Dkt Oginga na Gavana Orengo kushiriki jukwaa moja tangu kuzuka kwa mgawanyiko ndani ya ODM kuhusu uongozi wa chama. Gavana Orengo anahusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi na amekuwa akijitambulisha kama kiongozi halali wa ODM. Kaburi la heshima la Raila litajengwa karibu na lile la babake, aliyekuwa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga, aliyefariki Januari 20, 1994. Jaramogi alikuwa miongoni mwa vinara waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini na aligombea urais mnamo 1992, akimaliza katika nafasi ya nne. Raila Junior, ambaye aliteuliwa kuwa kiongozi wa familia ya Odinga baada ya kifo cha babake, alisema anaendelea kumheshimu Dkt Oburu kama mzee wa familia, mlezi na kiongozi wa kisiasa. Alisema humshauri mara kwa mara kuhusu masuala ya kifamilia na pia ya kisiasa. "Tulizungumza kuhusu masuala ya familia na hafla ya kukabidhi serikali eneo la kujenga kaburi la heshima la Baba. Bila shaka tulijadili pia siasa na maisha kwa ujumla, lakini kwa sasa tunazingatia suala lililo mbele yetu," alisema Raila Junior. Aidha, Raila Junior alimweleza Dkt Oburu kuhusu azma yake ya kuwania ubunge wa Embakasi South katika uchaguzi wa 2027. Wiki juzi akiwa Homa Bay, Bw Raila Jnr aliwaomba wakazi wa Nyanza kumuunga mkono kisiasa, akisema ana uwezo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi. Kama dada yake Winnie Odinga, ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Raila Junior pia analenga kuingia katika siasa za uchaguzi, ishara kwamba familia ya Odinga itaendelea kuwa sehemu ya siasa ambazo baba yao aliitawala kwa miongo kadhaa. Bi Winnie pia ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa kisiasa nchini na anatarajiwa kugombea ubunge katika Kaunti ya Nairobi. Hata hivyo, bado hajafanya uamuzi wa mwisho iwapo atawania kiti cha Kibra au Lang'ata, maeneo yanayotambuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya marehemu Raila.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 20 Jul 2026 06:57:38

Faith Odhiambo: Linda Mwananchi kuwa chama kabla ya mwaka kuisha

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK), Faith Odhiambo, amesema vuguvugu la Linda Mwananchi litageuzwa kuwa chama cha kisiasa kabla ya mwisho wa mwaka huu, huku likijiandaa kushiriki siasa za uchaguzi mkuu wa 2027. Odhiambo alisema maandalizi ya kukisajili chama hicho yanaendelea, ingawa huenda kisitambulike kwa jina la Linda Mwananchi. "Huenda chama kisitumie jina la Linda Mwananchi, lakini tutakizindua mwaka huu," alisema akizungumza katika mahojiano  na kituo kimoja cha televisheni Jumatatu, Odhiambo, ambaye hivi majuzi alijiunga na vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, alisema hatua hiyo inalenga kupatia kundi hilo jukwaa rasmi la kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kauli yake inajiri siku chache baada ya viongozi wa Linda Mwananchi kutangaza kuwa wameamua kujiondoa rasmi ndani ya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), wakisema ni wakati wa kuanzisha mkondo mpya wa kisiasa katika upinzani. Aliyekuwa Mwenyekiti wa LSK Faith Odhiambo . Picha|MaktabaTangazo hilo lilitolewa wakati wa ziara ya viongozi waa vuguvugu hilo katika Kaunti ya Taita Taveta mnamo Julai 18, ambapo walizungumza na wafuasi wao katika maeneo ya Mwatate, Wundanyi na Voi. Akihutubia wafuasi hao, Mbunge wa Suba Kusini na msemaji wa vuguvugu hilo, Caroli Omondi, alisema uhusiano kati ya Linda Mwananchi na ODM umefikia kikomo. "Sasa imefika wakati wa kuvunja uhusiano tuliokuwa nao na Orange Democratic Movement. Ni wakati wa kujiondoa ODM," alisema Omondi. Mbunge huyo pia alikosoa mwelekeo wa sasa wa ODM, akidai kuwa chama hicho kimetema misingi iliyokuwa ikikisimamia. "ODM imesaliti si Raila Odinga pekee, bali pia misingi na maadili aliyokuwa akiyapigania," alisema. Pia alimtaka Rais William Ruto kuruhusu mchakato wa usajili wa chama hicho kuendelea bila kuingiliwa. "Rais Ruto aache kuishinikiza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa usajili wa chama cha Linda Mwananchi," alisema. Wakati huo huo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ameendelea kuchochea mjadala wa kisiasa baada ya kudokeza kuwa huenda akawania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Akizungumza katika mkutano huo, Sifuna alisema amepata msukumo kutoka kwa vijana kuwania uongozi wa juu nchini. "Vijana wameniita, na sasa natoka kuwa Katibu Mkuu hadi Ikulu," alisema. Viongozi kadhaa kutoka eneo la Magharibi wanaomuunga mkono Sifuna wamepongeza hatua ya kuanzishwa kwa chama kipya, wakisema kitakuwa chombo muhimu cha kisiasa kitakachowaunganisha wafuasi wake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more