T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 06:55:10

Zogo latokota majagina wa riadha wakitaka makaburi karibu na uga wa Keino yabomolewe

MVUTANO mkali unaohusu upanuzi wa uwanja wa mamilioni ya pesa wa Kipchoge Keino umechukua mkondo mpya baada ya kundi la wanariadha mashuhuri waliostaafu North Rift wakitaka ubomozi wa makaburi uendelee. Wanariadha hao wakiongozwa na mwanariadha mkongwe Abraham Chelang'a wanataka utawala wa kaunti ya Uasin Gishu kuendelea na mpango wa kubomoa makaburi ya kihistoria ya Wakristo ambayo yamekuwa kando ya uwanja huo kwa zaidi ya karne moja. Pendekezo la kubomoa makaburi kwa upanuzi wa kisasa ili kuwa na sehemu ya kufanyia mazoezi ya kujiandaa, limeibua mjadala mkali wa umma; huku familia za watu waliozikwa hapo na makundi ya kuhifadhi urithi wa eneo hilo yakipinga vikali pendekezo hilo. Hata hivyo, wanariadha wa zamani wanahoji kuwa mji wa Eldoret—ambao kwa muda mrefu umekuwa ukijulikana kama makao makuu ya riadha duniani—unahitaji sana miundombinu ya michezo ya viwango vya kimataifa, na kwamba hoja za kihisia hazipaswi kukwamisha maendeleo ya kisasa ya michezo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Eldoret siku ya Alhamisi, Bw Chelang'a alisisitiza msimamo wake wa kutaka makaburi husika yabomolewe, akisema kuwa thamani ya kiuchumi kutokana na michezo katika uwanja wa viwango vya kimataifa ni kubwa zaidi kuliko kuhifadhi eneo hilo la zamani la makaburi. "Hatuwezi kuruhusu historia kuzuia mustakabali wa vijana wetu. Thamani ya uwanja wa kisasa wa hadhi ya kimataifa kwa eneo hili ni kubwa zaidi kuliko kuhifadhi makaburi yenye umri wa zaidi ya karne moja. Makaburi haya yapo mahali ambapo uwanja unapaswa kupanuliwa kama eneo la kufanyia mazoezi ya kujianda kushiriki mashindano. Bila uwanja huo wa mazoezi, Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletics) halitaidhinisha uwanja huo kwa ajili ya mashindano ya kimatiafa," alisema Bw Chelang'a. Bw Chelang'a alitoa wito kwa serikali ya kaunti kusimama imara licha ya kuongezeka kwa shinikizo za kusitisha upanuzi lengwa. Alihimiza utawala wa kaunti, chini ya uongozi wa gavana Jonathan Bii, kupuuza vitisho kutoka kwa wale wanaopinga mradi huo na kuendelea na upanuzi. Ujenzi wa uwanja huo unapaswa kukamilika kabla ya mwezi Oktoba kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za kitaifa za mashujaa mnamo Oktoba 20.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 28 Aug 2026 05:55:10

Hofu Ziwa Bogoria likikaribia kuungana na Ziwa Baringo

KUNA uwezekano wa Ziwa Bogoria na Ziwa Baringo kuungana hivi karibuni huku umbali kati yao ukipungua hadi chini ya kilomita tatu kutoka kilomita 20. Hali hiyo imezua hofu ya janga la kimazingira kwa kuwa maziwa hayo mawili yana sifa tofauti. Ziwa Baringo lina maji yasiyo na chumvi, huku Bogoria likiwa na maji yenye chumvi. Kwa zaidi ya muongo mmoja, wakazi wa Loboi, Baringo Kusini, wamekuwa wakishuhudia Ziwa Bogoria likipanuka na kuelekea kwenye makazi, mashamba na biashara zao. Maji hayo tayari yamemeza nyumba, kituo cha afya, maeneo ya malisho na maelfu ya ekari za mashamba. Wataalamu wanaonya kuwa iwapo maziwa hayo yataungana, mfumo wa ikolojia wa Baringo unaweza kuathirika pakubwa. Samaki, viboko, mamba na jamii zinazotegemea maji ya Baringo zinaweza kuwa miongoni mwa waathiriwa. Serikali sasa inapanga kujenga bwawa na mitaro ya kuzuia maji ya Bogoria kuelekea Baringo. Mpango huo unajumuisha ujenzi wa tuta la kilomita tano huko Sandai, bwawa katika Mto Waseges na mtaro wa takriban kilomita 40. Mtaro huo utatumika kuondoa maji mengi kutoka Baringo kuelekea Chemolingot na hatimaye Bonde la Suguta. Timu ya mashirika mbalimbali, ikiwemo Idara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, imekuwa ikichunguza eneo hilo. Gavana wa Baringo, Benjamin Cheboi, alisema mafuriko hayo yamezidi uwezo wa serikali ya Kaunti. "Mafuriko haya ni makubwa sana na kama serikali ya kaunti hatuwezi kuyakabili peke yetu. Ndiyo maana tumeomba usaidizi kutoka kwa serikali ya kitaifa na washirika wengine," alisema. Wakazi wanasema Bogoria ilianza kupanuka kwa kasi mwaka 2010, hali iliyoongezeka mwaka 2013. Bw Bismark Kibet alisema zaidi ya vijiji sita, kikiwemo Chepng'erechi na Kaprong'uno, vimeathirika huku Bw Jonathan Tireito akisema wakazi walidhani maji yangepungua baada ya muda. "Tulidhani yangepungua lakini hayajapungua. Yamefunika nyumba, maeneo ya malisho, mashamba na hata zahanati yetu," alisema Bw Tireito. Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Bogoria James Kimaru, alisema eneo la ziwa limeongezeka kutoka takriban kilomita 34 za mraba mwaka 2013 hadi karibu kilomita 45 kwa sasa. Barabara na miundombinu mingine katika hifadhi hiyo imehamishwa, huku chemchemi za maji moto na maeneo yaliyokuwa yakivutia watalii kutazama flamingo yakizama. Profesa Simon Onywere, mtaalamu wa mipango ya mazingira na jiolojia, alisema umbali kati ya maziwa hayo ulipungua kutoka zaidi ya kilomita 20 hapo awali hadi kilomita saba mwaka 2020 na sasa ni chini ya kilomita tatu. "Kuungana kwa maziwa haya kumekaribia na ni suala la muda tu," alisema. Alisema maji mengi kutoka Mto Waseges yanaendelea kuingia Bogoria, hivyo kuongeza uwezekano wa maji yenye chumvi kuelekea Baringo. "Ikiendelea hivi, Ziwa Baringo linaweza kuwa na maji ya chumvi na kuhatarisha samaki, viboko, mamba na jamii zinazolitegemea," alisema. Serikali pia inapanga kutumia maji hayo kwa unyunyizaji, huku mpango mpana ukilenga angalau ekari 100,000 katika Baringo na Turkana. Wakati huo huo, Ziwa Baringo lenyewe limepanuka kutoka kilomita 178 za mraba hadi zaidi ya 260. Afisa Mkuu wa Hifadhi, Bw Jackson Komen, alisema nyumba, shule, biashara na hoteli zimeathirika.

read more