T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 10:32:28

Benki ya KCB yadai kuna njama ya kuilaghai Sh146 bilioni

BENKI ya KCB imepiga ripoti kwa DCI ikitaka ichunguze kampuni ya Foxcapital inayodai ilituma Sh146 bilioni kwenye akaunti yake kutoka ng'ambo kuhusiana na uwekezaji wa dhamana za serikali. Benki hiyo inadai kwamba stakabadhi zilizowasilishwa na kampuni hiyo kortini kudai fedha hizo ni ghushi na inataka DCI kubaini ni nani aliziandaa, kusambaza na kuziwasilisha kortini. Mzozo unahusisha €978,675,835 (Sh146.3 billion), ambazo Foxcapital inasema ilituma kwa akaunti yao ya KCB Oktoba mwaka jana kama malipo kwa kampuni ya Uingereza, Bay Bionics Ltd, iliyotambuliwa zamani kama BB Biotech AG Limited. Foxcapital iliwasilisha kesi mapema mwezi huu ikidai kwamba KCB ilipokea fedha hizo za kigeni lakini ikakosa kuziweka kwenye akaunti yake, na kufanya Mahakama Kuu kubana hela hizo ikisubiri iamuliwe iwapo benki hiyo kweli ilipokea pesa hizo na kukataa kuzipeana kwa kampuni husika. Katika kilio chake kwa DCI kitengo cha Ulaghai wa Benki, KCB Group, kupitia Afisa Mkuu Mtendaji Paul Russo anatilia shaka stakabadhi zilizotumiwa na Foxcapital kudai pesa hizo. Stakabadhi zinajumuisha arafa za SWIFT, ripoti ya tukio ya Aprili 17, barua ya Mei 18 ya kuangazia kosa la kiuchumi na utathmini wa kiufundi wa Julai 1. KCB inasema stakabadhi zinazodaiwa kutoka UBS Switzerland AG na maafisa wa KCB sio halisi. Kulingana na malalamishi hayo, KCB iliandikia UBS Agosti 13, 2026 ikitaka thibitisho la stakabadhi na malipo. KCB inasema UBS ilijibu ikisema stakabadhi na maagizo ya malipo "hayajatoka kwa UBS Switzerland AG na kwa hivyo sio halali." KCB inasema inatilia shaka stakabadhi hizo baada ya kupata kwamba hakuna mtiririko wa malipo kama hayo kutoka kwenye mitambo yao. "Ikichukuliwa kwa pamoja, kukosekama kwa malipo hayo kwenye mitambo yetu, UBS Switzerland AG kukana stakabadhi na kiapo cha Ushahidi kutoka kwa maafisa wa KCB pamoja na stakabadhi za kutiliwa shaka kunaipa KCB kuamini kwamba kuna njama ya kuilaghai Sh146 bilioni inayoendeshwa na Foxcapital," KCB inasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 10:01:06

Home Boys ndio mabingwa ligi ya 'Weka Panga chini'

KLABU ya Home Boys FC kutoka mtaa wa Gadeni ndiyo iliyotawazwa bingwa wa michuano ya ligi ya 'Weka Panga Chini' kisiwani Lamu. Hii ni baada ya kuilaza timu ya Real Madrid kutoka mtaa wa Wiyoni magoli 2-1 kwenye fainali kali iliyochezewa katika uwanja wa Twaifu mjini Lamu Jumapili. Ligi hiyo maalum ya mpira wa miguu ilishirikisha klabu 16 za Lamu za vijana wa chini ya miaka 18. Ilizinduliwa mapema Agosti, dhamira kuu ikiwa ni kukabiliana na uhalifu wa mapanga na dawa za kulevya miongoni mwa vijana eneo hilo. Wafadhili wakuu ni Idara ya Usalama kupitia kitengo cha Polisi wa Watalii (TPU), Bodi ya Utalii ya Lamu (LTA), Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) na serikali ya kaunti ya Lamu. Fainali ilishuhudia idadi kubwa ya mashabiki waliofika kushangilia timu zao. Mshindi wa kwanza (Home Boys FC) alituzwa Sh30,000 pesa taslimu, kikombe na jezi ilhali wa pili (Real Madrid FC) ikituzwa Sh20,000 na jezi. Nambari tatu iliendea klabu ya Lamu Boys FC kutoka mtaa wa Langoni kisiwani Lamu, hivyo kupokea kitita cha Sh10,000 na jezi. Mechi ya fainali ilihudhuriwa na kamanda wa polisi wa watalii (TPU) ukanda wa Pwani, Bw David Kabiru, aliyekariri wito wa vijana wa Lamu, Pwani na Kenya kwa jumla kuhubiri amani, kujiepusha na makundi ya uhalifu na dawa za kulevya. "Nimefurahia kushuhudia soka tamu hapa kisiwani Lamu. Mfahamu kwamba mshindi si klabu ya Home Boys pekee eti kwa sababu imeshinda fainali. Wote walioshiriki ligi hii ni washindi. Ninaambiwa karibu vijana 270 wameshirikishwa kwenye michuano hii. Nyote mjue ni washindi na tuendelee kushirikiana kudumisha Amani," akasema Bw Kabiru. Mwenyekiti wa LTA, Bi Fridah Njeri aliahidi ushirikiano wake na wadau wengine ili kuona kwamba ligi nyingine sawia inaanzishwa kufikia Disemba mwaka huu. "Tutahakikisha kila msimu wa likizo tunazindua ligi maalum ya soka ili tuwashughulishe vijana wetu na kuwaepusha na majanga, hasa mihadarati," akasema Bi Njeri. Naibu wa LTA, Bw Jamil Mbarak ambaye pia alihudhuria fainali ya ligi hiyo uwanjani Twaifu aliwashauri vijana kujiepusha na mizozo na hasira. "Hasira hazijawahi kusuluhisha mambo. Tujifunze kudhibiti hasira zetu. Tujiepusha na mizozo na badala yake tupendane na kuhubiri amani ili Lamu iendelee kuwa kivutio bora cha watalii," akasema Bw Mbarak. Katibu wa kamati andalizi, ambaye pia ni Mwakilishi wa Vijana katika FKF, Lamu, Bw Athman Farid, maarufu Pirezi, aliwapongeza wanasoka wote walioshiriki ligi hiyo kwa kudumisha nidhamu kipindi chote cha wiki tatu ambapo ligi imekuwa ikiendelea. Kwenye ligi hiyo, kiungo Mohamed Ali kutoka klabu ya Lamu Boys FC ndiye aliyetawazwa mfungaji bora akiwa na magoli 7 ilhali kipa bora akawa ni Mohamed Farid kutoka Real Madrid FC. Mchezaji aliyeibuka bora na mwenye nidhamu zaidi ni Abdallah Abdulmalik kutoka Real Madrid FC ilhali mchezaji aliyetawazwa kuwa mwenye kipaji cha kutegemewa ni Daniel Chome kutoka timu ya Dragon Junior FC. Wote walituzwa pesa taslimu na vyeti vya kutambua juhudi zao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 26 Aug 2026 08:55:08

Sababu zilizomfanya aache mahindi, ahamie kilimo cha 'managu'

ALIPOMTEMBELEA rafiki yake katika shamba la Matuiku, kilomita chache kutoka mji wa Elburgon mnamo 2020, Benson Muchai hakujua kwamba mazungumzo kati yao yangebadilisha kilimo chake cha mahindi alichokifanya kwa muda mrefu na kuanza kilimo cha mazao ya muda mfupi ambacho kingempa mauzo mazuri bila kutumia pesa nyingi mwishoni mwa msimu. Muchai, 38, anasema mkulima huyo alikuwa akipanda mboga aina ya mnavu (managu) katika shamba lake la nusu ekari. Rafikiye Muchai alimwambia kuwa kwa kila miezi mitatu hadi minne, alipokea takriban Sh1.5 milioni kutoka kwa mauzo, akiongeza kuwa kilimo hicho kilikuwa rahisi kwani hakina kazi nyingi na bei yake kwenye soko ilikuwa nzuri. Alipomuuliza rafiki yake siri ya mafanikio hayo yalikuwa nini, alimjibu kuwa kwa kupata maji ya kutosha, mkulima yeyote anaweza kuwekeza na kustawi katika kilimo cha managu hata kwenye eneo dogo. Baada ya kushauriana na mkewe, walikubaliana kubadilisha shamba lao la mahindi na kuanza kilimo cha managu kwenye nusu ekari ya shamba walilokodisha katika maeneo ya Elburgon, Kaunti ya Nakuru. Wakati wa mahojiano hivi majuzi, Muchai alisema kuwa kwa mtaji wa Sh20,000, alikodisha shamba la nusu ekari kwa Sh7,500. Alinunua gramu 100 za mbegu na mifuko mitano ya samadi ya mifugo ambayo aliisambaza shambani kabla ya kulima. Alichanganya mbegu hizo na mfuko wa vumbi ya mbao na kupanda kwenye mitaro huku akizipa nafasi ya 15cm na baadaye kunyunyizia maji ya kutosha. Mbegu hizo ziliota kati ya wiki mbili hadi tatu, kulingana na usambazaji wa maji. Katika wiki ya tatu, mkulima alinyunyizia shamba lake dawa za kumaliza magugu na kusambaza samadi zaidi shambani baada ya mwezi mmoja. "Mboga za managu huwa tayari kuvunwa baada ya siku thelathini na wiki moja. Katika mavuno yangu ya kwanza, nilivuna kilo 800 na kuuza katika soko la ndani kwa Sh70 kwa kila kilo," anasema Muchai, akiongeza kuwa mauzo aliyopata hayangelinganishwa na alichopata kila mwaka kutokana na mauzo ya gunia la mahindi la kilo 90 alilouza kwa Sh2,400 na Sh1,800 mtawalia kulingana na msimu. Anaongeza kuwa wakati wa msimu mzuri, alikuwa akivuna kati ya magunia 25 na 30 ya mahindi kutoka kwa eneo hilo la nusu ekari kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita tofauti na kilimo cha managu ambapo wakulima wanaweza kuvuna zaidi ya kilo 1,500 kila wiki kwenye eneo sawia. Muchai anasifia soko la mboga hizo ikilinganishwa na kilimo cha mahindi kwa sababu anauzia wateja moja kwa moja Kilimo hicho kimemwezesha kununua shamba lake mwenyewe ambapo analima managu zaidi na mazao mengine, hulipa karo ya shule kwa watoto wake na kukidhi mahitaji mengine nyumbani. Anaeleza kuwa kwa sasa huvuna zaidi ya kilo 2,500 wakati wa msimu mzuri au wa mvua huku kilo moja kwa sasa ikiuzwa kwa Sh50. Baada ya kuvuna mboga kwa miezi minne mfululizo, Muchai hufanya mzunguko wa mazao kwa kupanda karoti, brokoli, maharagwe na viazi baadhi ya mazao mengine ya muda mfupi, lakini huhakikisha kuwa anaendelea kukuza managu katika eneo tofauti ili kuwadumisha wateja wake. "Nimeongeza shamba langu la managu hadi ekari mbili na nusu kabla ya kufikia maono yangu ya kupanda hadi zaidi ya ekari tano katika miaka miwili ijayo mradi tu niwe na maji ya kutosha," anasema. Mboga hizo hutoa mbegu ambazo huvunwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kupanda kwa msimu ujao. Anasema kuwa hii humfaidi kwa kuzalisha mbegu za kutosha bila kununua kutoka kwa maduka ya pembejeo. Tangu alipoanza kupanda managu kwa miaka sita iliyopita, Muchai anasema hajawahi kumbana na ugonjwa wowote unaoathiri mazao yake, mradi tu yanasimamiwa vizuri na kupewa virutubisho sahihi. Kulingana na Sarah Kimani ambaye hupanda zao hilo kwenye robo ya shamba lake, anapata zaidi ya Sh 150,000 kutokana na mauzo kila mwezi, hasa wakati mvua inanyesha kwa wingi. Aliongeza kuwa siku chache baada ya kutathmini hali ya shamba la Muchai, aliamua kuanza kilimo chake mwenyewe. "Kwa miaka miwili iliyopita tangu nilipopanda managu, sijutii kwa sababu nimeweza kupata faida bila kutumia pesa nyingi shambani tofauti na mazao mengine kama vile mahindi na viazi ambapo nilikuwa nikitumia pesa nyingi. Mpango wangu ni kupanua shamba langu na kupanda zaidi ili kukidhi mahitaji ya wateja ambao wamezidi kuongezeka," anaeleza Sarah.

read more