T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 04:55:27

Maraga ampa Ruto siku saba achapishe ripoti iliyopendekeza mageuzi ya polisi lau sivyo aitoe yeye

ALIYEKUWA Jaji Mkuu David Maraga amempa Rais William Ruto muda wa siku saba kuchapisha ripoti ya jopo la marekebisho ya polisi iliyowasilishwa kwake mnamo 2023, akionya kwamba asipofanya hivyo ataichapisha mwenyewe. Maraga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa jopo hilo, alisema mojawapo ya mapendekezo makuu katika ripoti hiyo ilikuwa kurejesha uhuru wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ili kuzuia kile alichokitaja kama kutekwa, kutumiwa vibaya na kuingiliwa kwa taasisi hiyo. "Kwa kuwa ripoti hii iliandaliwa kwa gharama ya umma na kwa mujibu wa Kifungu cha 35 cha Katiba, ninakutaka uichapishe mara moja na bila kuhaririwa ndani ya siku saba. Usipofanya hivyo, nitaitoa mimi mwenyewe," alisema Maraga. Alisisitiza kuwa NPS ni huduma huru ya usalama wa taifa ambayo haipaswi kupewa maagizo na mtu yeyote, ikiwemo Rais, katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Hata hivyo, Maraga alisema hivi majuzi nchi imeshuhudia kile alichokiita "ghasia za kisiasa zilizopangwa, matumizi ya magenge ya wahuni na upendeleo wa polisi" katika maeneo ya Homa Bay, Keumbu na Ol Kalou, pamoja na matukio ya vurugu katika makanisa ya Kisumu, Nairobi na Witima. Homa Bay ilikumbwa na vurugu Jumapili wakati mkutano wa kisiasa wa Linda Mwananchi ulipovurugwa, ambapo watu wawili, akiwemo afisa wa polisi, waliuawa huku wengine 46 wakijeruhiwa. Kulingana na Maraga, matukio hayo yaliyotokea chini ya utawala wa Rais Ruto yanaashiria kurejea kwa siasa za ghasia na matumizi ya idara za usalama kuzima sauti za wanaopinga serikali. "Hii ni njia ambayo nchi iliwahi kupitia hapo awali kwa gharama kubwa. Haipaswi kuirudia tena," alisema mgombea huyo wa urais wa chama cha United Green Movement (UGM), akihusisha hali hiyo na kile alichokiita "kutekwa kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi."

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 05:55:36

Linda Mwananchi waapa kuchukua hatua za kisheria na kiraia kukabili serikali kuhusu uhuni

VUGUVUGU la Linda Mwananchi limetangaza mkakati wa kukabiliana na kile inachodai ni ongezeko la ghasia za kisiasa nchini. Mkakati huo unahusisha hatua kali za kisheria mahakamani, kushinikiza idara za usalama, uasi wa kiraia na kuhamasisha zaidi mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari. Kundi hilo limesema hatua hizo zitachukuliwa kufuatia vurugu zilizovuruga ziara yake katika Kaunti ya Homa Bay Jumapili iliyopita, ambapo watu walifariki dunia, makumi kujeruhiwa na mali kuharibiwa. Badala ya kujiondoa kwenye shughuli za kisiasa, viongozi wa Linda Mwananchi wanasema tukio la Homa Bay limeimarisha azma yao ya kupinga kile wanachokiita ghasia na vitisho vinavyofadhiliwa na serikali. Kundi hilo linasema kwa sasa litafuata njia za kisheria, lakini limeonya kuwa huenda likalazimika kutumia hatua za kiraia ikiwa serikali haitawawajibisha waliohusika na vurugu hizo. Gavana wa Siaya, James Orengo, ambaye ni mmoja wa viongozi wa vuguvugu hilo, alisema Jumanne kuwa yuko tayari kukabiliana na kile alichokiita "ugaidi wa serikali" na akashutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kupanga mashambulizi dhidi ya wapinzani wa kisiasa. "Tuko tayari. Niko tayari kukabiliana na changamoto yoyote inayotokana na ghasia za serikali. Huu ni ugaidi wa serikali unaoendelezwa na Rais William Ruto na lazima awajibike," alisema Bw Orengo nje ya makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika Barabara ya Kiambu, Nairobi. Alikuwa amemsindikiza Bw Oliver Jaoko, maarufu kama Olivetti, ambaye polisi wanamtafuta kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa katika mkutano wa Linda Mwananchi mjini Homa Bay. Bw Orengo pia alishutumu serikali kwa kuandaa mazingira ya kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, ingawaje hakutoa ushahidi wowote kuhusiana na madai hayo. "Rais Ruto anajaribu kutuandaa kuahirisha uchaguzi. Hilo halitawezekana," alisema. Kundi hilo limetaja maeneo manne ya mkakati wake: mahakama, maandamano na uasi wa kiraia, kushinikiza polisi na vyombo vingine vya usalama, na kuhamasisha mashirika ya kiraia na wanahabari kufuatilia shughuli zake moja kwa moja. Njia ya kwanza ni kupitia mahakama. Katika taarifa yake ya Jumatatu, Linda Mwananchi lilisema litashinikiza uwajibikaji kupitia Katiba, mahakama na taasisi nyingine za kisheria. "Kila mhuni na afisa ambaye sura yake ilinaswa kwenye kamera akihusika katika vurugu hizi, alionekana na anatambulika," kundi hilo lilisema. "Tutatumia Katiba, mahakama na taasisi zote za kisheria kuhakikisha kuna uwajibikaji." Pia limetaka Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) zifanye uchunguzi kuhusu mwenendo wa maafisa wao wakati wa vurugu za Homa Bay. Linda Mwananchi linadai maafisa wa usalama walitazama tu huku wafuasi wake wakishambuliwa au walisaidia kuvuruga shughuli zake za kisiasa. Madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru na vyombo vya usalama bado havijayakubali hadharani. Kundi hilo linadai msafara wake ulikumbana na vizuizi vya barabarani tangu mpaka wa Kisumu na Homa Bay, na kuendelea kukabiliwa na vizuizi ndani ya kaunti hiyo. Linaongeza kuwa watu wenye silaha waliokuwa wamejipanga kando ya barabara walifyatulia risasi msafara huo. Moja ya madai makubwa zaidi yanahusu mtu aliyekamatwa na wafuasi wake Nyandiwa ambaye alidaiwa kujitambulisha kama afisa wa NIS. Kundi hilo linasema simu yake ilichukuliwa na baadaye watu waliojieleza kuwa maafisa wakuu wa polisi waliwasiliana wakitaka irejeshwe. Nguzo ya pili ya mkakati huo ni shinikizo la kisiasa kupitia maandamano na uwezekano wa uasi wa kiraia. Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi, alisema kundi hilo linaweza kuchukua hatua za kiraia iwapo Rais Ruto ataendelea kudumisha serikalini maafisa wanaotuhumiwa kupanga ghasia za kisiasa. "Tutarejea kwenye hatua za kiraia ikiwa Ruto ataendelea kuwaweka watu hawa serikalini," alisema Seneta Osotsi. Nguzo ya tatu ni kishinikiza polisi moja kwa moja. Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, walimsindikiza Jaoko kwenda kujisalimisha kufuatia maslahi ya polisi katika uchunguzi wa vurugu hizo. Bw Owino alishutumu polisi kwa kushindwa kuchukua hatua wakati timu ya Linda Mwananchi ilishambuliwa Homa Bay, akisema walipaswa kurejesha utulivu na kulinda wananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 06:55:23

Mwanasheria Mkuu akosa kujibu iwapo waliotimuliwa afisini wanaweza kuwania 2027

MZOZO wa kisheria kuhusu iwapo viongozi waliotimuliwa afisini kupitia bunge wanaweza kugombea nyadhifa za kisiasa kabla ya kesi zao kukamilika bado utaendelea kushuhudiwa nchini. Hii ni baada ya Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, kukosa kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu utata huo. Suala hilo lina umuhimu mkubwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, ambao wote waliondolewa mamlakani na Bunge na wanapinga kutimuliwa kwao kortini. Bi Oduor ameishauri Mahakama ya Juu kutosikiza ombi la kutoa ushauri wa kikatiba kuhusu iwapo viongozi walioondolewa mamlakani kupitia bunge wanaweza kugombea nyadhifa za kisiasa kesi zao zikiendelea mahakamani. Mawakili wa Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Ayub Bundi, hata hivyo, wamesema Mwanasheria Mkuu hakujibu maswali manane ambayo Mahakama ya Juu ilimtaka kuyashughulikia. Mawakili wa Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Ayub Bundi, hata hivyo, walisema Mwanasheria Mkuu hakujibu maswali manane ambayo Mahakama ya Juu ilimtaka kuyajibu. Mojawapo ya maswali hayo ni iwapo rufaa au kesi ya kupinga kuondolewa mamlakani inaweza kusimamisha amri ya kikatiba ya uamuzi huo na kumruhusu kiongozi huyo kugombea uchaguzi. "Baada ya kupitia ushauri huo, ni wazi kwamba haujajibu wala kushughulikia masuala hayo," wakasema mawakili hao. Walimtaka Mwanasheria Mkuu kufuata maagizo ya Mahakama ya Juu kwa kutoa ushauri wa kisheria unaojibu kila swali lililowasilishwa. Bw Gachagua aliondolewa mamlakani Oktoba 2024. Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi yake Juni 2026, lakini amekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Kiongozi huyo wa DCP ametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa 2027. Bi Mwangaza naye aliondolewa kama Gavana wa Meru Agosti 2024 baada ya Bunge la Kaunti kupitisha hoja ya kumtimua na Seneti kuithibitisha. Mahakama Kuu ilikataa kesi yake Machi 2025, lakini amekata rufaa kupinga uamuzi huo. Anaongoza chama cha Umoja na Maendeleo (UMP) na analenga kuwania kiti cha ugavana tena. Bw Bundi aliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Juu Aprili 2026, akitaka ufafanuzi kuhusu masharti ya Katiba yanayohusu masharti ya kugombea nyadhifa za kisiasa. Mahakama ilimwagiza kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu ndani ya siku 21. Bi Oduor alisema kesi hiyo haifai kuendelea kwa sababu inahusu maswali yenye msingi na huenda ikaathiri kesi za baadaye. "Afisi hii inaona kwamba kesi hii haikidhi masharti ya Katiba ya Mahakama ya Juu kutoa ushauri wa aina hii," akasema. Hata hivyo, mawakili wa Bw Bundi wanasisitiza kuwa Mwanasheria Mkuu hakutimiza maagizo ya mahakama kwa sababu hakujibu maswali muhimu. Kwa sasa, Mahakama ya Juu bado haijatoa uamuzi kuhusu suala hilo. Hii inaacha swali la iwapo Gachagua na Mwangaza wanaweza kugombea uchaguzi wa 2027 likiwa halijajibiwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 10:30:08

Serikali yatetea mageuzi katika sekta ya afya licha ya changamoto

SERIKALI imetetea mageuzi yake katika sekta ya afya, ikisema imetekeleza ahadi nyingi ilizotoa wakati wa kampeni licha ya changamoto mbalimbali. Rais William Ruto alisema maendeleo katika sekta ya afya hayapaswi kupimwa kwa idadi ya sheria zilizopitishwa au watu waliosajiliwa pekee, bali kwa uzoefu wa mgonjwa anayepata huduma. "Kipimo halisi cha mafanikio ni ikiwa mgonjwa anapata huduma za afya zinazotegemewa, nafuu na zenye kuheshimu utu wake," alisema Rais. Alizungumza wakati wa Kongamano la kwanza la Kitaifa la Afya nchini Kenya lililoandaliwa na Wizara ya Afya chini ya kaulimbiu "Mageuzi yamewasilishwa, Afya ni Haki", ambalo linalenga kujadili changamoto na mafanikio ya sekta hiyo. Rais alisema alipoingia mamlakani, mojawapo ya vipaumbele vyake vilikuwa kufufua mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), ambao alihisi ulikuwa umedorora. Hivyo, UHC ikawa moja ya nguzo tano za Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kutoka Chini kwenda Juu. Kwa mujibu wake, maradhi yanaweza kufilisi familia na kuwafanya wananchi kuingia katika umaskini, jambo lililomsukuma kutunga sheria nne mpya za afya mwaka 2023 zilizozaa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Kati ya Wakenya milioni 32.3 waliosajiliwa chini ya SHA, zaidi ya milioni nane wamepokea huduma za matibabu. Idadi hiyo inajumuisha akina mama milioni 1.2 waliosaidika kujifungua salama na zaidi ya 500, 000 kwa upasuaji tangu mpango huo uanzishwe. Rais alipuuziliaa mbali madai kwamba ameacha ajenda ya "hasla", akisema ana ushahidi kuwa wananchi wa kipato cha chini ndio wanufaika wakubwa wa SHA. "Haya si mageuzi ya siku moja. Ni safari endelevu ya kupunguza pengo kati ya ahadi tulizotoa na huduma anayopokea kila Mkenya," alisema. Hata hivyo, wadau wa afya walihoji kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana katika sera, changamoto kubwa bado ipo katika utekelezaji. Mkurugenzi Mkuu wa Reproductive Health Network Kenya, Bi Nelly Munyasia, alisema Kenya imepiga hatua katika sera za afya ya uzazi, lakini huduma hizo hazijafikishwa kikamilifu kwa wananchi. "Baadhi ya sera bora zaidi zinasalia kwenye makaratasi kwa sababu rasilimali hazijaelekezwa ipasavyo ili kuzitekeleza," alisema. Alisisitiza umuhimu wa ufadhili endelevu, miundombinu ya kutosha, wafanyakazi wenye ujuzi na mifumo bora ya rufaa za wagonjwa. Kwa upande wake, Patrick Oyaro wa mradi wa Liverpool VCT and Research Kenya (LVCT), alisema huduma za watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi zinapaswa kujumuishwa kikamilifu chini ya SHA. "Kwa muda mrefu huduma za Ukimwi zimefadhiliwa na wafadhili. Tunahitaji kubadili hali hiyo na kuhakikisha zinaingizwa kwenye SHA," alisema. Kongamano hilo linafanyika wakati ambapo nchi inashuhudia mgomo wa wahudumu wa afya wa UHC na wauguzi. Mwenyekiti wa Muungano wa Maafisa wa Utabibu Kenya, Peterson Wachira, alisema Kenya bado iko mbali na malengo ya Ruwaza ya 2030 ya kuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika. Aliongeza kuwa nchi pia haijafikia Azimio la Abuja linalotaka asilimia 15 ya bajeti ya taifa kutengewa sekta ya afya. "Mfumo wa usimamizi wa wahudumu katika afya umegawanyika mno. Upendeleo na ufisadi zimekithiri na wafanyakazi wengi wa afya wanateseka kutokana na uchovu na msongo wa mawazo," alisema. Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU), Dkt Dennis Miskella, alisema changamoto kubwa inayopuuzwa ni masuala ya wafanyakazi wa afya. "Kaunti zaidi ya 40 bado hazijalipa mishahara ya madaktari. Tunahitaji mjadala wa kina kuhusu uongozi na usimamizi wa sekta hii," alisema. Alipendekeza kuwa magavana washughulikie huduma za msingi za afya huku serikali kuu ikisimamia huduma za matibabu ya kiwango cha juu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 19 Aug 2026 12:34:06

Makosa ya kudondosha viambishi vya idadi ya nomino katika wingi

KATIKA Kiswahili, upatanisho wa kisarufi ni muhimu tunapotaja idadi. Mojawapo ya makosa yaliyozoeleka ni kuhesabu miezi bila kutumia kiambishi cha nomino ambacho ni mi-. Ni kawaida kukutana na sentensi kama vile: *Msimu huo mvua ilinyesha kwa mwezi tatu. Sentensi hii si sahihi. Nomino mwezi inamaanisha kipindi cha siku ishirini na nane hadi thelathini na moja. Kwa hivyo katika wingi itakuwa miezi. Vilevile, kivumishi cha idadi tatu kinafaa kichukue kiambishi mi-. Ili kuisahihisha tutasema: Msimu huo mvua ilinyesha kwa miezi mitatu. Makosa mengine yaliyozoeleka katika kuhesabu nomino ni kuvipa vivumishi tasa viambishi vya idadi: sita, saba, tisa na kumi. Kila mara utakumbana na sentensi kama vile: Nilipofika darasani niliwapata wanafunzi *wasita. Vikombe *visaba vimeoshwa na mpishi. Magari *matisa yameegeshwa. Miti *mikumi ilipandwa jana. Sentensi hizi si sahihi kwani zimetumia viambishi vya nomino mwanzoni mwa vivumishi sita, saba, tisa na kumi. Tunafaa kuzisahihisha kwa kusema: Nilipofika darasani niliwapata wanafunzi sita. Vikombe saba vimeoshwa na mpishi. Magari tisa yameegeshwa. Miti kumi ilipandwa jana. Kosa jingine la kawaida tunapohesabu nomino ni kukosa kutumia viambishi vya nomino tunapotaja vivumishi vya idadi vinavyobadilika katika wingi. Aghalabu utakumbana na sentensi kama: *Nilinunua vitabu kumi na moja. *Wageni tano wamewasili kwetu. Tunafaa kusema: Nilinunua vitabu kumi na kimoja. Wageni watano wamewasili kwetu. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kuhesabu nomino kwa usahihi, afanye mazoezi ya kuhesabu nomino ainati katika umoja na wingi.

read more