T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 05:55:39

Mzozo kuhusu ardhi ya Ruaraka wazidi kutokota Matiang'i akiwa bado kwenye 'mix'

KAMPUNI mbili zinazohusishwa na marehemu mfanyabiashara Francis Mburu, zimewasilisha kesi katika Mahakama Kuu zikitaka kuzuia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kurejesha Sh1.5 bilioni zilizolipwa kama fidia ya ardhi kulikojengwa shule mbili za umma eneo la Ruaraka, Nairobi. Afrison Export Import Limited na Huelands Limited, zinataka mahakama izuie EACC kuanzisha mchakato wa kurejesha fedha hizo hadi rufaa yao iliyo mbele ya Mahakama ya Juu itakapoamuliwa. EACC inadai karibu Sh2.5 bilioni kutoka kwa watu binafsi na kampuni, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i, Katibu wa Idara ya Uhamiaji Belio Kipsang, pamoja na kampuni zinazohusishwa na familia ya Mburu. Tume hiyo inalenga kurejesha fedha zilizolipwa kampuni binafsi kama fidia ya ekari 13.77 za ardhi hiyo iliyoko Ruaraka, ambayo serikali inasema tayari ilikuwa mali ya umma. Kupitia barua za madai, EACC imewataka walengwa wote kurejesha Sh1.5 bilioni pamoja na riba ya asilimia 12 kwa mwaka tangu Januari 2018, fedha hizo zilipolipwa kampuni ya Whispering Palms Estate Limited. Miongoni mwa waliopokea notisi hizo ni aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Ardhi ya Taifa (NLC) Muhammad Swazuri, makamishna wa zamani Tom Konyimbih na Emma Muthoni Njogu, pamoja na wakurugenzi wa kampuni husika Mark Mungai Mburu na Justin Sam Mburu. Katika stakabadhi zilizowasilisha kortini, Afrison Export Import Limited na Huelands Limited, kupitia mkurugenzi mwenza Mark Mburu, zinasema EACC imechukua hatua mapema mno kurejeshwa kwa fedha hizo kabla ya Mahakama ya Juu kusikiliza na kuamua rufaa yao. Mburu alisema EACC, kupitia barua ya Julai 6, ilitaka fedha hizo zirudishwe na kuonya kuwa hatua za kisheria ingechukuliwa ikiwa kampuni hizo hazingetii agizo hilo. Kampuni hizo zinahoji kuwa kesi yao imepangwa kutajwa Agosti 14 katika Mahakama ya Juu na kwamba hatua ya EACC inaweza kuathiri haki yao ya kusikilizwa kwa usawa. "Uamuzi wa mshtakiwa ni wa haraka mno, hauna mantiki na unakiuka kanuni za utawala wa haki kwa sababu unataka kutekeleza matokeo ya hukumu ambayo bado iko katika mchakato wa rufaa," zilisema kampuni hizo. Rufaa yao inapinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba fidia hiyo ilitolewa kinyume cha sheria. Kampuni hizo zinadai majaji hawakuzingatia kikamilifu ushahidi wao kuhusu umiliki wa ardhi pamoja na historia ya mgogoro huo. Pia, zinasema Mahakama ya Rufaa ilishindwa kutofautisha kati ya masharti ya mipango ya maendeleo ya ardhi na utaratibu wa kikatiba wa kutwaa mali binafsi kwa manufaa ya umma. Kwa mujibu wa kampuni hizo, mahakama ilitafsiri visivyo idhini ya upangaji wa ardhi kana kwamba ingeweza kutumika kuhamisha mali ya kibinafsi kwa matumizi ya umma bila kufuata masharti ya Katiba kuhusu unyakuzi wa ardhi. Aidha, zinadai kuwa mahakama ilikiuka haki za kikatiba za kumiliki mali na usalama wa hati miliki za ardhi. Kampuni hizo zinasisitiza kuwa hakuna fedha za umma zilizopotea na zinaitaka NLC kulipa salio la Sh1.77 bilioni ambalo lilikuwa limeidhinishwa kama sehemu ya fidia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 13 Aug 2026 04:55:55

Jiandae kwa mwaka mgumu, Kalonzo amuonya Ruto

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Party, Kalonzo Musyoka, amemuonya Rais William Ruto kwamba mwaka wake wa mwisho mamlakani utakuwa mgumu, huku upinzani ukiahidi kuongeza ukosoaji wa serikali kuelekea uchaguzi wa 2027. Bw Musyoka alisema sauti ya upinzani itabadilika na kuwa kali zaidi katika siku 365 zijazo, huku akimshutumu Rais Ruto kwa kukiuka Katiba na kushindwa kutekeleza ahadi za manifesto ya Kenya Kwanza. "Tutaweka kila kitu wazi na kuwaeleza Wakenya jinsi Rais Ruto amekiuka Katiba na kufanya kinyume na manifesto yake," alisema. Kiongozi huyo wa Wiper alianza ziara ya siku tano Pwani Jumatano, akitarajiwa kuzuru Kwale, Kilifi, Mombasa na Taita-Taveta. Alianza ziara hiyo kwa kuhudhuria mkutano mkuu wa kila mwaka wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) huko Diani, Kwale, kabla ya mikutano ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya Pwani. Bw Musyoka pia alitumia ziara hiyo kushinikiza serikali kutatua mzozo wa kidiplomasia kati ya Kenya na Sudan uliosababisha kusimamishwa kwa uuzaji wa bidhaa za Kenya, ikiwemo chai. Sudan ilisimamisha uagizaji wa bidhaa kutoka Kenya Machi 2025 baada ya Nairobi kuandaa mkutano wa viongozi wa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), hatua ambayo Khartoum ilisema ilikuwa kuingilia masuala yake ya ndani. Kabla ya marufuku hiyo, Sudan ilikuwa ikiagiza takriban kilo milioni 35 za chai ya Kenya kila mwaka, zenye thamani ya dola milioni 69. Bw Musyoka alisema amekutana na Balozi wa Sudan nchini Kenya, Kamal Gubara, na kujadili namna ya kumshawishi Rais wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kuondoa marufuku hiyo. "Tulipatana kwamba atapeleka mazungumzo kwa viongozi wa juu ili kuomba Rais Burhan aondoe marufuku na kuwezesha biashara kati ya Kenya na Sudan," alisema. Bw Musyoka pia aliishutumu serikali kwa madai ya kuruhusu bandari ya Mombasa kutumiwa kuingiza silaha zinazolengwa Sudan, akisema hatua hiyo imechangia kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa East Africa Tea Trade Association George Omuga, alisema zaidi ya kilo milioni 3.44 za chai zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 10.3 bado zimekwama katika maghala ya Mombasa. Alisema chai hiyo ilikuwa imechanganywa na kufungashwa maalum kwa ajili ya soko la Sudan na hivyo ni vigumu kuipeleka katika masoko mengine. Bw Omuga alisema kufunguliwa kwa soko la Sudan kutawasaidia wakulima, wafanyabiashara na wauzaji wa chai nchini Kenya.

read more