T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 04:55:01

ODM yazua dhoruba kwa kung'ang'ania kiti cha Kindiki mkutanoni Naivasha

MVUTANO kuhusu nani atakuwa Naibu Rais iwapo Rais William Ruto atashinda muhula wa pili uliibuka katika kikao cha faragha cha viongozi wa Kenya Kwanza na ODM mjini Naivasha Jumatatu. ODM ilisisitiza kuwa inataka nafasi hiyo katika makubaliano ya kisiasa yanayosukwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kwa mujibu wa duru kadhaa zilizohudhuria kikao hicho, Naibu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Kisii, Simba Arati, ndiye aliyeibua suala hilo. Bw Arati alitaka serikali igawanye nafasi za serikali nusu kwa nusu, akisema nafasi ya Naibu Rais inapaswa kwenda kwa ODM kwa kuwa Rais Ruto, ambaye atakuwa mgombeaji urais wa muungano huo, anatoka UDA. Kauli hiyo iliwakera baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya, ambao walihisi kuwa madai hayo hayakuwa na heshima kwa Naibu Rais Kithure Kindiki, aliyekuwa ameketi karibu na Rais Ruto. Hata hivyo, Mbunge wa Khwisero, Bw Christopher Aseka, alimtetea Bw Arati, akisema ODM inapaswa kuchukuliwa kama mshirika sawa na Kenya Kwanza na kupewa nafasi ya kumpendekeza mgombea mwenza. "Hakuna mtu aliyetoka kwenye mkutano. Kulikuwa na manung'uniko na kutoridhika kutoka upande mwingine, jambo ambalo ni la kawaida kwa sababu suala hili limewahi kusababisha kutokubaliana," alisema Bw Aseka. Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed, alithibitisha kuwa Bw Arati ndiye aliyeibua suala hilo, lakini akakanusha kuwa kulikuwa na mvutano. "Ni kweli Arati aliliibua, lakini hakukuwa na ugomvi. Kwanza tulikubaliana kuunda muungano, kisha suala la nafasi litajadiliwa baadaye," alisema Bw Mohamed. Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, alisema suala la Naibu Rais halikujadiliwa kwa kina katika mkutano huo. "Hatukufikia kiwango hicho. Nafasi ya Naibu Rais itajadiliwa sambamba na kuundwa kwa muungano. Mazungumzo kama hayo hayawezi kufanywa katika chumba chenye viongozi zaidi ya 300," alisema. Kwa mujibu wa Bw Nassir, mkutano ulijikita zaidi katika mafanikio ya serikali katika kilimo, afya, uchumi na sekta nyingine ambazo viongozi waliambiwa wanapaswa kuelezea zaidi kuelekea uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, huku mvutano kuhusu nafasi hiyo ukiendelea, Prof Kindiki alikaa kwa utulivu kabla Rais Ruto kumwita kutoa muhtasari wa yaliyojadiliwa. "Tunahitaji kufunga mjadala kuhusu tuliyojadili leo, na hakuna mtu bora anayeweza kuunganisha masuala ya uchumi, jamii, elimu, ugatuzi na diplomasia kuliko naibu wangu," Rais Ruto alisema. Kauli hiyo ilipokelewa kwa shangwe na wabunge wanaomuunga mkono Rais na ilitafsiriwa kama ishara ya imani ya Rais kwa Prof Kindiki. Kwa dakika arobaini na tano, Prof Kindiki alielezea mafanikio ya serikali katika elimu, miundombinu, diplomasia na afya, bila kuingia katika mjadala kuhusu nafasi yake. ODM imekuwa ikiongeza presha kutaka nafasi hiyo, huku Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, akiwa mmoja wa viongozi wanaopendekezwa na chama hicho. Bw Oparanya pia anapendekezwa na baadhi ya viongozi wa Magharibi mwa Kenya kama njia ya kukabiliana na umaarufu unaoongezeka wa Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Hata hivyo, kura za maoni zinaonyesha Prof Kindiki bado anaongoza katika orodha ya wanaopendwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto. Kura ya maoni iliyotolewa Julai 13 ilimweka Prof Kindiki mbele kwa asilimia 34, akifuatiwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga kwa asilimia 11, Kiongozi wa ODM Dr Oburu Oginga kwa asilimia tano na Waziri wa Madini Hassan Joho kwa asilimia nne. Bw Oparanya, Spika wa Bunge Moses Wetang'ula na Waziri Mkuu Musalia Mudavadi pia wametajwa kama wanaoweza kuchukua nafasi hiyo. Wakati huo huo, kamati ya watu 10 iliyoteuliwa kuandaa mpango wa pamoja wa uchaguzi wa 2027 imepewa mwezi mmoja kukamilisha kazi yake. Kamati hiyo inatarajiwa kuandaa manifesto ya pamoja na makubaliano ya muungano kabla ya kuyawasilisha kwa Wakenya. Duru zilizohudhuria mkutano huo zilisema ingawa pande hizo mbili zimekubaliana Rais Ruto ndiye atakuwa mgombea wa urais, suala linalobaki kuwa gumu ni nani atakuwa mwaniaji mwenza. Kwa mujibu wa duru hiyo, uamuzi wa mwisho kuhusu mgombea mwenza utaachiwa Rais Ruto, ambaye atazingatia uwezo wa mgombea huyo kuleta kura kwa muungano. "Huu ni mchezo wa nambari na kwa sasa mtu yeyote kutoka katika muungano anaweza kuchaguliwa. Iwe ni kutoka ODM au Kenya Kwanza, mgombeaji atachaguliwa kulingana na kura anazoweza kuleta," duru iliongeza. Hali hiyo inaashiria kuwa vita vya kumrithi Prof Kindiki kama Naibu Rais au kumdumisha vitakuwa miongoni mwa masuala makuu yatakayoamua muungano wa kisiasa kuelekea 2027. TAARIFA YA CECIL ODONGO, SAMWEL OWINO, VITALIS KIMUTAI NA JOSEPH OPENDA

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 03:55:16

Ruto kuzindua rasmi safari ya Kenya kuwa kama Singapore: Gumzo la 'Vision 2060' ni leo

RAIS William Ruto leo, Jumatano Agosti 12, 2026, anaanzisha mchakato wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu mustakabali wa Kenya, huku akiwahusisha wataalamu na wananchi katika kuandaa mpango wa maendeleo wa muda mrefu. Mchakato huo unaanza wakati ambapo nchi tayari inaanza kuangazia mambo zaidi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 na mjadala kuhusu mwelekeo wa uchumi wa Kenya ukizidi kushika kasi. Lengo ni kuandaa mpango utakaodumu hata serikali zikibadilika na kuepuka hali ya kila serikali kuja na vipaumbele vyake vipya. Rais Ruto anataka kuandaa mpango utakaopeleka Kenya zaidi ya Ruwaza ya 2030 na kuiweka katika njia ya kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha juu. Miongoni mwa wataalamu wanaoshiriki mjadala huo ni Profesa Hiroyuki Hino, mwanauchumi kutoka Japan, ambaye anaamini Kenya inaweza kujifunza kutokana na mafanikio ya kiuchumi ya nchi kama Singapore, Korea Kusini na Vietnam. Profesa Hino amefanya kazi na Kenya tangu miaka ya 1990 alipokuwa mjumbe mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF). Anasema Kenya haipaswi kuangazia pekee ujenzi wa barabara, reli na miradi mikubwa ya miundombinu. Badala yake, anasema nguvu kubwa ya Kenya iko kwa wananchi wake. "Hoja yangu kuu ni nguvu ya Wakenya binafsi. Kama ilivyokuwa Mashariki mwa Asia, mafanikio ya kiuchumi yalichangiwa sana na nguvu ya watu," alisema. Profesa Hino anasema nchi zilizofanikiwa kiuchumi hazikujenga miundombinu pekee. Ziliweka pia mifumo inayowasaidia watu kufanya kazi kwa ufanisi na kunufaika kutokana na juhudi zao. Anasema Ruwaza ya 2030 ilifanikisha baadhi ya mambo, hasa katika miundombinu na ukuaji wa uchumi wa kati ya asilimia tano na sita. Hata hivyo, anasema matunda ya ukuaji huo hayakuwafikia Wakenya wengi wa kawaida. "Faida za ukuaji wa uchumi hazikuwafikia watu wa kawaida," alisema. Anasema mpango mpya unapaswa kupima mafanikio kwa kuangalia huduma kama maji safi na salama, nishati safi ya kupikia, huduma za afya na mapato ya wananchi. Profesa Hino anaamini safari hiyo itakuwa ngumu sana, lakini inawezekana. Anasema Kenya pia inapaswa kufikiria upya namna ya kufadhili maendeleo badala ya kutegemea serikali pekee. Anashauri kuimarisha biashara ndogo, kuongeza uzalishaji na kutumia mbinu mpya za kupata fedha. Pia anasisitiza ushiriki wa wananchi. Anasema mpango huo utadumu zaidi iwapo Wakenya watahusika katika kuandaliwa kwake. "Watu wote wakihusika katika mchakato, wataumiliki mchakato huo na hatimaye kuumiliki mpango wenyewe," alisema. Kwa mtazamo wake, umiliki huo unaweza kusaidia mpango mpya kuendelea hata serikali zikibadilika. Anasema Wakenya hawapaswi kusubiri serikali pekee kutatua matatizo yao. Badala yake, wanapaswa kushiriki katika kutoa mawazo na mapendekezo ya jinsi changamoto za nchi zinavyoweza kutatuliwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 12 Aug 2026 02:55:34

Gachagua auma serikali, akosoa vikali sera za Ruto

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua jana alikosoa vikali utawala wa Rais William Ruto akiwasilisha tathmini yake kuhusu sekta mbalimbali. Katika hotuba yake kwa taifa, Bw Gachagua alisema tathmini hiyo inalenga kupima "ahadi dhidi ya utendaji, nia dhidi ya utekelezaji na matarajio dhidi ya matokeo". Alipitia kurasa 39, akitaja alichodai kuwa ni kushindwa kwa serikali katika uchumi na huduma kwa umma, ufisadi, zigo la kodi, magenge ya wahuni, utekaji nyara, ahadi za uongo na kubadilishwa kwa sera. Bw Gachagua alikuwa sehemu ya timu iliyomsaidia Dkt Ruto kushinda uchaguzi wa 2022 na akahudumu kama Naibu Rais hadi uhusiano wao wa kisiasa ulipovurugika na akang'atuliwa ofisini mnamo Oktoba 17, 2024. Kiongozi huyo wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) alisema Wakenya walichagua serikali ya Kenya Kwanza mnamo 2022 kwa kuamini Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Kuanzia Mashinani na ahadi za kuboresha maisha yao. Miaka minne baadaye, alisema serikali imeshindwa kutimiza ahadi hizo. "Mpango huo umeshindwa. Ni batili na wa kupotosha!" alisema Bw Gachagua. Alidai serikali sasa imeelekeza nguvu zake katika mchakato wa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo, Ajenda ya Vipengele 10 na mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa ruwaza ya baada ya 2030, badala ya kutimiza ahadi za awali. Gachagua alielekeza sehemu kubwa ya shutuma zake kwa uchumi na gharama ya maisha. Alisema ahadi ya Kenya Kwanza ya kuweka fedha zaidi mifukoni mwa Wakenya imegeuka kuwa mzigo wa kodi, makato ya kisheria na bei za bidhaa kupanda. Alitaja bei ya mafuta ya Petroli ambayo imeongezeka kutoka Sh159.12 kwa lita Agosti 2022 hadi Sh214.03. Dizeli imepanda kutoka Sh140 hadi Sh222.86. Alisema ongezeko hilo limechangia kupanda kwa gharama ya usafiri na chakula huku likipunguza uwezo wa familia kutumia fedha kwa mahitaji mengine. Pia, alikosoa sera za kodi akisema familia sasa zinatumia fedha nyingi zaidi kununua chakula, mafuta, umeme na bidhaa nyingine muhimu. Takwimu za Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) zinaonyesha mfumuko wa bei ulifikia asilimia 6.5 Julai, kiwango cha pili cha juu zaidi katika kipindi cha miezi 30. Gachagua pia alikosoa deni la taifa, akisema limeongezeka kutoka Sh8.66 trilioni Agosti 2022 hadi Sh13.02 trilioni. Alisema zaidi ya Sh4 trilioni zimekopwa katika miaka minne ya utawala wa Rais Ruto, bila maendeleo yanayolingana na kiwango hicho cha madeni. Katika afya, Gachagua alishutumu serikali kwa kutotekeleza ahadi ya Afya kwa Wote na kubadilisha NHIF na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Alikosoa kusitishwa kwa mipango ya Linda Mama na Edu Afya, akisema hatua hiyo imeongeza mzigo kwa familia. Katika usalama na haki za binadamu, Gachagua alishutumu serikali kwa kile alichokiita "kuvunjika kabisa kwa sheria na utulivu". Alidai magenge ya wahuni yameruhusiwa kufanya kazi pamoja na polisi na serikali imeshindwa kuwajibisha waliohusika na mauaji na utekaji nyara.

read more