T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 03:55:39

Linda Mwananchi ilivyopokonywa jina

VUGUVUGU la Linda Mwananchi limetishia kufanya maandamano ya kila siku nje ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) iwapo ombi lake la kusajiliwa kama chama cha kisiasa halitashughulikiwa. Hatua hiyo inazidisha mvutano kati ya vuguvugu hilo na ofisi ya Msajili wakati Linda Mwananchi ikijaribu kujibadilisha kuwa chama rasmi cha kisiasa kabla uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza wakati wa ziara ya Linda Mwananchi ya kukutana na wananchi katika Kaunti ya Busia siku ya Ijumaa, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alilaumu watu ambao hakuwataja kwa kujaribu kunyakua jina linalohusishwa na vuguvugu hilo. Osotsi alisema kundi hilo litampa Msajili hadi kesho kutatua suala hilo. Alionya kuwa iwapo suala hilo halitatatuliwa basi wafuasi wa Linda Mwananchi wataanza kufanya mikutano ya kila siku nje ya ofisi za ORPP. "Ruto ametuma wakora kule kwa ofisi ya msajili wa vyama eti wanajaribu kunyakua hii jina yetu. Mimi nataka kuambia William Ruto, Ibara ya 38 inaruhusu Mkenya yeyote kuunda chama," alisema Osotsi. Akaongeza: "Tunaambia huyo msajili kama hutapatiana hiyo jina Jumatatu, tutaandaa mikutano ya kila siku kwa hiyo ofisi." Mzozo huo umejikita katika maombi ya kusajili chama na namna Ofisi ya Msajili inashughulikia jina linalopendekezwa na Linda Mwananchi. Mvutano huo ulipata sura mpya baada ya ORPP kuripotiwa kusajili Liberty National Democratic Alliance, kinachojulikana kama LINDA Party. Hatua hiyo imeibua mvutano mpya na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pamoja na washirika wake katika Linda Mwananchi. Usajili wa chama kinachotumia jina LINDA umeleta changamoto mpya kwa juhudi zao. Kwa mujibu wa ripoti, chama hicho kipya kinahusishwa na kundi tofauti ambalo pia lilikuwa limejitahidi kupata utambulisho wa kisiasa kwa kutumia jina "Linda". Kundi hilo pinzani limepinga madai ya Linda Mwananchi kwamba ndilo lenye haki ya kutumia jina hilo. Madai hayo yameibua swali kuhusu kundi lenye haki ya kutumia jina na nembo zinazohusishwa na "Linda". Mzozo huo pia umewekea Ofisi ya Msajili shinikizo kutoka pande zote. Viongozi wa Linda Mwananchi wamekuwa wakisisitiza kuwa tayari wamejenga utambulisho wa kisiasa kupitia jina hilo, hivyo wanafaa kupewa nafasi ya kukitumia chama hicho. Hatua ya hivi majuzi inafuatia mikutano kati ya viongozi wa Linda Mwananchi na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou. Ripoti zinasema kuwa Msajili alikubali kupitia upya uamuzi wa awali wa kukataa jina la Linda Mwananchi baada ya mashauriano na wawakilishi wa vuguvugu hilo. Hatua hiyo ilikuwa imeibua matumaini miongoni mwa viongozi na wafuasi wa Linda Mwananchi kwamba mchakato wa usajili ungeendelea. Hata hivyo, usajili ulioripotiwa wa LINDA Party umeleta changamoto mpya na kugubika Linda Mwananchi na mzozo mwingine kuhusu jina inalotaka kutumia. Wadadisi wanasema haki inayotokana na Kifungu 38 cha Katiba - kinachowapa raia haki ya kuunda au kushiriki katika uundaji wa chama cha kisiasa - inaambatana na masharti ya kisheria yanayosimamia usajili wa vyama vya kisiasa nchini. Ofisi ya Msajili ina jukumu la kusajili na kudhibiti vyama pamoja na kusimamia taratibu za kisheria zinazohusu kuanzishwa kwa vyama. Linda Mwananchi sasa inataka ORPP itatue mzozo huo ili iweze kukamilisha miundo yake kabla ya uchaguzi ujao. Usajili wa chama ni hatua muhimu katika kubadilisha vuguvugu hilo kuwa chombo rasmi cha uchaguzi. Kwa sasa, viongozi wake wameweka Jumatatu kuwa siku ya mwisho kwaMsajili wa Vyama kushughulikia suala hilo kabla kuanza kwa mikutano ya kila siku nje ya ofisi hiyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 04:55:36

Tofauti zaibuka kuhusu tarehe ya kuandaa uchaguzi

INGAWA Katiba ya 2010 iliweka tarehe ya uchaguzi ili iwe wazi na ya kutabirika, suala hilo limefikishwa mahakamani angalau mara tano tangu 2015. Kesi hizo zimehusisha majaji 13 na kuzua tafsiri tofauti kuhusu maana ya kifungu kinachosema uchaguzi ufanyike "Jumanne ya pili ya Agosti katika kila mwaka wa tano". Mzozo huo umeibuka tena baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Malindi Mugure Thande kuamua kuwa uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Agosti 2026 badala ya 2027. Mwanasheria wa masuala ya Katiba Waikwa Wanyoike anasema mkanganyiko huo unatokana na dhana kwamba Katiba inamhakikishia kila kiongozi aliyechaguliwa kipindi cha miaka mitano. Vita vya kwanza vilianza kabla ya uchaguzi wa 2017 baada ya watu watatu kupinga tarehe iliyokuwa imewekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC). Walidai kuwa uchaguzi wa madiwani wa kaunti (MCAs) Agosti 8, 2017 ungekatiza kipindi chao cha miaka mitano kwa karibu miezi minane. Jaji Edward Muriithi aliamua Aprili 2017 kuwa kulikuwa na mkanganyiko kati ya vifungu viwili vya Katiba kuhusu muda wa madiwani na tarehe ya uchaguzi. Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ilibatilisha uamuzi huo Novemba 2017 na kusema tarehe ya uchaguzi iliyowekwa na Katiba haiwezi kubadilishwa. Kesi nyingine iliwasilishwa mwaka 2018 na mwanaharakati Okiya Omtatah na Nyakina Wycliffe Gisebe. Walidai uchaguzi ulipaswa kufanyika Agosti 2021 badala ya 2022. Jaji Weldon Korir alikataa kesi hiyo Novemba 2020, akisema uchaguzi wa viongozi wote unapaswa kufanyika siku moja baada ya kipindi cha miaka mitano. Mwaka 2022, aliyekuwa Seneta mteule Paul Njoroge alipinga tarehe ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9. Jaji Anthony Mrima alikataa hoja hiyo. Mzozo huo ulifika Mahakama ya Juu mwaka 2025 baada ya mwanasheria Dkt Owiso Owiso na wanaharakati Khelef Khalifa na Ashioya Biko kutaka mahakama hiyo ieleze kifungu cha 136(2)(a). Mahakama hiyo ya majaji saba haikugusia kiini cha kesi na ikaiondoa Agosti 15, 2025 kwa misingi ya mamlaka yake. Walalamishi hao walienda Mahakama Kuu ya Malindi, ambako Jaji Thande aliamua kuwa uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Jumanne, Agosti 11, 2026. Bw Wanyoike anaunga mkono tafsiri hiyo akisema Katiba haimhakikishii Rais, wabunge na maseneta kipindi kamili cha miaka mitano. Hata hivyo, mwanasheria Dudley Ochiel anapinga akisema historia ya kutunga Katiba inaonyesha wazi kuwa Kenya ilikusudia kuwa na mzunguko wa uchaguzi wa miaka mitano. "Historia ya Katiba haiungi mkono nia ya kuanzisha vipindi vya miaka minne kwa viongozi waliochaguliwa," alisema. Mwanasheria Ndung'u Wangenye anasema Mahakama ya Juu ndiyo itakayotoa jibu la mwisho kuhusu suala hilo. "Suluhisho la mwisho litakuwa uamuzi wa Mahakama ya Juu," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 05:55:57

Malumbano ya ubabe Mlimani kati ya Gachagua, Munya raha kwa Ruto

MALUMBANO yanayoendelea kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya huenda yakawa habari njema kwa Rais William Ruto anapojiandaa kutetea kiti chake katika uchaguzi wa 2027. Kinachoonekana kama mzozo wa kawaida kuhusu vyama kinaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa za upinzani, hasa katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapigakura. Mzozo huo ulizuka baada ya viongozi wa vyama kadhaa kupinga kauli zinazohusishwa na Gachagua, kwamba vyama vidogo vinafaa kuvunjwa ili vijiunge na Democracy for the Citizens Party (DCP). Miongoni mwa waliopinga wazo hilo ni kinara wa Democratic Party (DP) Justin Muturi, kinara wa Party of National Unity (PNU) Peter Munya na kinara wa Devolution Empowerment Party (DEP) Lenny Kivuti. Viongozi hao walisema umoja wa upinzani haupaswi kujengwa kwa masharti au shinikizo, bali kupitia mashauriano, kuheshimiana na ushirikiano wa hiari. Hata hivyo, malumbano hayo yanaibua swali kubwa kuhusu nani atakuwa na ushawishi mkubwa Mlima Kenya kuelekea 2027. Tangu kuondolewa kwake kama Naibu Rais, Gachagua amekuwa akijaribu kujijenga kama kiongozi mkuu wa kisiasa wa eneo hilo. DCP imekuwa chombo muhimu katika mkakati huo, huku washirika wake wakijaribu kuunganisha wanasiasa wa mlimani chini ya chama kimoja kabla ya mazungumzo ya muungano wa kitaifa. Lakini msimamo wa Muturi, Munya na Kivuti unaonyesha kuwa si viongozi wote wanaompinga Ruto wako tayari kufuata mkondo wa Gachagua. Hilo linaweza kuwa pigo kwa mpango wa Mlima Kenya kuzungumza kwa sauti moja kuelekea 2027. Eneo hilo huwa na nguvu kisiasa linapoungana. Katika chaguzi zilizopita, viongozi walioweza kuunganisha kura za eneo hilo walipata usemi mkubwa katika mazungumzo ya kisiasa kitaifa. Lakini sasa kuna dalili za vituo vingi vya nguvu vita vya ndani vikionekana kuchacha. Jambo linalojitokeza kwenye mzozo huo ni kwamba baadhi ya viongozi wanaompinga Ruto sasa wanatumia nguvu nyingi kumjibu Gachagua, kuliko kueleza namna watakavyompinga Rais katika uchaguzi ujao. Badala ya mjadala kuwa Ruto dhidi ya upinzani, unaanza kuwa Gachagua dhidi ya viongozi wengine wa upinzani na wachambuzi wa siasa wanasema hili linaweza kumfaa Ruto. "Kadiri viongozi hao wanavyobishana kuhusu nani anafaa kuongoza Mlima Kenya, ndivyo wanapoteza muda wa kujenga kampeni moja kubwa ya kitaifa dhidi ya serikali.Kila tofauti ya maoni inaongeza uwezekano wa upinzani kuingia 2027 ukiwa umegawanyika," asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Kiini cha mzozo huo ni: nani ana haki ya kuzungumza kwa niaba ya Mlima Kenya? Washirika wa Gachagua wamemtaja kama kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo kufuatia kuondolewa kwake mamlakani. Lakini wapinzani wake wanasema hakuna mtu aliyepewa mamlaka ya kuwa msemaji wa eneo lote. Muturi, Munya na Kivuti wanasisitiza kwamba hakuna mkutano uliowahi kufanyika kumpa Gachagua mamlaka hayo. Pia wanakumbusha kuwa hata marais wa zamani Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta hawakuwahi kudai vyama vingine vivunjwe ili kuonyesha uaminifu kwao. Wanasema Gachagua anaweza kuwa na ushawishi mkubwa, lakini sio eti hana mpinzani. Viongozi hao pia wanaonekana kuhofu kwamba DCP inaweza kuwa chama kikubwa kinachotawala vyama vingine vidogo. Kwao, kulazimisha vyama vidogo kuvunjwa hakutaimarisha demokrasia. Kwa Ruto mzozo huo unaweza kuwa faida kubwa. "Viongozi wanaompinga wanapogawanyika nafasi ya kujenga upinzani mmoja wenye nguvu hupungua. Aidha, mivutano ya hadharani inaweza kuwafanya wapigakura wa Mlima Kenya kutokuwa na uhakika kuhusu upande wa kuunga mkono," asema Dkt Lilian Kimani, mchanganuzi wa siasa. Anasema hii inaweza kumpa Ruto nafasi ya kujaribu kurejesha ushawishi wake katika eneo ambalo wapinzani wameanza kujishindia.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 06:55:18

Hofu kijijini watoto 10 wakijitia kitanzi

HOFU imetanda katika eneo la Ndabibi Central, Naivasha, baada ya watoto wasiopungua 10 kujitia kitanzi katika kipindi cha mwaka mmoja. Wakazi wanasema visa hivyo vimeacha familia zikijiuliza kinachowasukuma watoto wadogo kujiua. Miongoni mwa waliofariki ni Cynthia Muthoni, mwanafunzi wa Gredi ya Sita. Asubuhi ya Juni 6, alionekana kuwa sawa nyumbani kwao. Rachael Wahu Kariuki na binti yake walikuwa wameenda mtoni kufua nguo kabla ya kurejea nyumbani. Mchana, Wahu alimwacha Muthoni akiosha vyombo na kumuagiza apike chakula kabla ya yeye kurejea kazini. Karibu saa tisa alasiri, mama huyo alirudi nyumbani na kumpata binti yake akiwa katika hali nzuri. Aliondoka tena baada ya kuitwa shuleni. Muda mfupi baadaye, majirani wawili walifika kwa pikipiki na kumuomba awafuate. Walimpeleka kwa jirani, ambapo Wahu aliambiwa binti yake alikuwa amefariki baada ya kujitia kitanzi. Dada yake ndiye aliyegundua na kuwaarifu majirani. "Nilimwacha akiwa na furaha. Hakuwa amefanya kosa lolote na hatukuwa tumegombana. Sijui ni nini kilimfanya ajitie kitanzi," alisema Wahu kwa machozi. Mama huyo alisema Muthoni alikuwa amewahi kuugua ugonjwa wa figo. Dawa alizokuwa akitumia zilifanya mwili wake uvimbe na akaanza kuogopa kuchekwa na wanafunzi wenzake. Alikuwa pia amekataa kurejea shuleni na alitaka kujiunga na mafunzo ya ufundi. Kilomita chache kutoka hapo, familia ya Kiragu Mochogua ilikuwa ikiomboleza kifo cha binti yao wa miaka 16, Jane Wanjiru. Jane alikuwa ameenda kutafuta kuni lakini hakurudi nyumbani.Baba yake alimfuata msituni baada ya kuona nyayo zake.Huko ndiko alipompata binti yake akiwa amefariki. Mama yake, Phyllis Wambui, alisema Jane alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya afya na aliacha shule akiwa Darasa la Tano. Dada yake mdogo pia aliacha shule akiwa Darasa la Tatu ili kumhudumia. Familia ilikuwa imeanza kupanga kumrudisha Jane shuleni baada ya afya yake kuimarika. Lakini alifariki kabla ya mpango huo kutimia. Kifo cha Beth Nyaguthie Juma, mwanafunzi wa Gredi ya Sita, pia kimeongeza majonzi katika eneo hilo. Kaka yake, Peter Chege Juma, alisema alipokea simu ya dharura kutoka kwa majirani na kukimbia nyumbani. Alisema kifo cha dada yake kilimvunja moyo kiasi kwamba aliondoka nyumbani kwao na kukodisha nyumba. "Mama yetu alifariki 2024. Dada yangu alikuwa kitindamimba. Kifo chake kilituacha na maumivu makubwa," alisema. Chifu msaidizi wa Ndabibi Central, Aseth Kariuki, alisema visa hivyo vinazidi kuwa vya kutisha. Alisema watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 na 15 ndio walioathirika zaidi. "Mwaka huu pekee, tumewazika watoto watano waliofariki baada ya kujitia kitanzi Ndabibi. Tulipofuatilia visa hivyo, wazazi na walimu walisema hawakuona ishara zozote za hatari," alisema. Mercy Wangui Mburu, mwalimu na mhudumu wa kulinda watoto, alisema angalau watoto 10 wamefariki kwa kujitia kitanzi katika eneo hilo tangu Juni mwaka uliopita. Watoto wengine saba wamejaribu kujiua.Wengi wa walioathirika wana umri wa miaka 12 hadi 17. Wangui alisema wahudumu wa jamii wamelemewa na visa hivyo. "Tunahitaji washauri wa kitaalamu. Hata kama watakaa hapa kwa miezi miwili. Tunataka kuelewa watoto hawa wanapitia nini kwa sababu wanateseka kimya kimya," alisema. Alitaka serikali za kitaifa na kaunti kuingilia kati na kuimarisha huduma za afya ya akili katika shule, makanisa na familia. Mtaalamu wa ushauri nasaha Meshack Ondieki alisema wazazi wanapaswa kuwasikiliza watoto wao na kuzingatia mabadiliko katika tabia zao. Alisema ishara za kuangaliwa ni pamoja na kujitenga na familia, kushuka kwa matokeo shuleni, kupoteza hamu ya shughuli walizopenda na kubadilika kwa uhusiano wao na wenzao. Pia alisema kukosa hamu ya kula, uchovu wa mara kwa mara, kupuuza usafi wa kibinafsi na kukataa kushiriki shughuli za kawaida vinaweza kuwa ishara kwamba mtoto anapitia matatizo ya kihisia. Alisema mabadiliko hayo hayafai kupuuzwa kama tabia za kawaida za ujana, hasa yanapotokea kwa pamoja. Kulingana na takwimu za Kaunti ya Nakuru zilizotajwa na wataalamu wa afya ya akili, zaidi ya visa 400 vinavyohusiana na kujiua viliripotiwa kati ya Januari 2020 na Aprili 2025. Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa changamoto inayokabili watoto na vijana katika eneo hilo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 09 Aug 2026 02:55:04

ODM sasa yamkalia Ruto ngumu kuhusu 2027, yataja matakwa 8

CHAMA cha ODM kimeweka matakwa manane mbele ya Rais William Ruto kabla ya uchaguzi wa 2027, huku viongozi wa chama hicho wakitarajiwa kuyajadili katika mkutano wa siku tatu wa serikali jumuishi unaoanza Naivasha leo Jumapili. Mkutano huo unawakutanisha magavana, manaibu wao na wabunge wa ODM, UDA na vyama vingine vinavyounga mkono serikali jumuishi. Ingawa mkutano huo umeelezwa kuwa wa kuimarisha uhusiano na kujenga mwafaka, ODM inataka serikali itekeleze makubaliano yaliyofikiwa kabla ya chama hicho kuendelea kushirikiana na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027. ODM inataka utekelezaji wa ajenda ya vipengele 10 iliyokuwa msingi wa makubaliano ya kisiasa kati ya Rais Ruto na marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alisema viongozi watapitia hatua zlizopigwa katika kutekeleza makubaliano hayo. Ajenda hiyo inahusisha masuala yaliyokubaliwa na pande hizo mbili wakati wa mazungumzo yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa nchini. ODM pia inataka serikali kutoa mwelekeo kuhusu miswada iliyotokana na Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco). Baadhi ya mapendekezo ya Nadco yalihusu kuanzishwa kwa afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na Waziri Mkuu. Chama hicho kinataka kujua hatua ambayo serikali imechukua kutekeleza mapendekezo hayo. ODM inataka hatua zaidi kuchukuliwa kuhusu fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi. Bi Wanga alisema suala hilo litakuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo. Hii ni mojawapo ya masuala ambayo chama hicho kinataka serikali ishughulikie kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa. ODM pia inataka kuwe na uwazi kuhusu mustakabali wa ushirikiano wake na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027. Chama hicho kinataka kujua jinsi ushirikiano huo utakavyofanya kazi na nafasi ya kila chama katika maandalizi ya uchaguzi. Huku uchaguzi ukikaribia, viongozi wa vyama hivyo wameanza kushindana kuhusu maeneo ya kisiasa na nafasi mbalimbali. ODM inataka ngome zake za jadi za kisiasa zilindwe katika mpango wa ushirikiano wa uchaguzi. Suala la kutengewa maeneo limekuwa chanzo cha mvutano kati ya ODM na UDA. ODM imekuwa ikitaka ngome zake ziheshimiwe, huku UDA ikitaka kila chama kiruhusiwe kuwasilisha wagombea katika maeneo yote isipokuwa kiti cha urais. Gavana wa Mombasa na naibu kiongozi wa ODM Abdullswamad Nassir alisema suala hilo litashughulikiwa na kamati maalum ya vyama hivyo. Suala la nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto 2027 pia limekuwa nyeti. Baadhi ya viongozi wa ODM tayari wamemuunga mkono Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya kwa wadhifa huo. Hilo limezua ushindani na washirika wa Naibu Rais Kithure Kindiki. ODM inataka ushirikiano huo utoe nafasi ya chama kushiriki katika maamuzi muhimu kuhusu uchaguzi wa 2027. Chama hicho pia kinataka kuwe na mpango wa pamoja wa kuelekea uchaguzi wa 2027. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed alisema mkutano huo utatoa mwelekeo kuhusu uchaguzi ujao. "Kutakuwa na maamuzi mazito yatakayotoa mwelekeo wa kisiasa. Viongozi watatoa mwongozo wa kuelekea 2027," alisema. Mpango huo unatarajiwa kuangazia mikakati ya kampeni, ushirikiano wa vyama na ujumbe wa serikali kwa wapigakura. ODM pia inataka kushiriki katika mjadala kuhusu Ruwaza mpya ya Rais Ruto ya 2060. Rais anatarajiwa kuzindua mpango huo Agosti 12, siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa Naivasha. Mkutano huo pia unafanyika wakati ODM na UDA zinakabiliwa na ushindani wa kisiasa katika maeneo mbalimbali. Mabadiliko ya uaminifu wa kisiasa, hasa Mlima Kenya, yameongeza presha kwa Rais Ruto. UDA imepoteza baadhi ya washirika wake wakuu, wakiwemo magavana Irungu Kang'ata wa Murang'a na Kiarie Badilisha wa Nyandarua pamoja na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.  Wakati huo huo, vuguvugu la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna linaendelea kupanua mbawa zake.  ODM ina wasiwasi kuwa vuguvugu hilo linaweza kupunguza nguvu zake katika baadhi ya ngome zake za jadi kuelekea uchaguzi wa 2027.

read more