T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 31 Jul 2026 06:55:10

Matumaini tele mbegu za kiume zikiundwa katika maabara

KWA miaka mingi, wanaume waliogunduliwa kuwa gumba kabisa wamekuwa wakikabiliwa na ukweli mchungu kwamba huenda wasiweze kupata watoto. Hata hivyo, utafiti mpya umeibua matumaini mapya baada ya wanasayansi kufanikiwa kutengeneza seli za awali za mbegu za uzazi za kiume katika maabara kwa kutumia seli zilizotokana na damu ya binadamu. Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Cell Stem Cell na watafiti wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania nchini Amerika, unaonyesha hatua kubwa katika juhudi za kutengeneza mbegu za uzazi nje ya mwili wa binadamu. Ingawa mbegu hizo hazikufikia ukomavu kamili wa kurutubisha yai, watafiti wanasema wamefikia hatua ambayo haijawahi kufikiwa katika tafiti za binadamu. Wataalamu walitumia seli zilizobadilishwa kutoka kwenye damu na kuzielekeza kuwa seli za mwanzo zinazoweza kukua na kuwa mbegu za uzazi. Baadaye waliziweka katika mazingira yanayofanana na korodani ndogo maabarani, ambako ziliendelea kukua na kuonyesha shughuli za vinasaba zinazofanana kwa asilimia 97 na ukuaji wa kawaida wa mbegu za uzazi kwa binadamu. Iwapo teknolojia hii itafanikiwa kukamilishwa, inaweza kuwapa matumaini wanaume wanaokabiliwa na ugumba usiotibika kupata watoto wao kuzaa kwa kutumia mbegu zilizotengenezwa maabarani. Ugumba wa wanaume ni tatizo kubwa duniani lakini mara nyingi huzungumziwa kwa kiwango kidogo. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mmoja kati ya sita hukumbwa na changamoto hili katika kipindi cha maisha yake ya uzazi. Takriban asilimia 20 hadi 30 ya visa hivyo husababishwa na matatizo ya mwanaume pekee, huku katika asilimia 30 hadi 40 matatizo ya mwanaume na mwanamke yakichangia kwa pamoja. Nchini Kenya, Chama cha Madaktari wataalamu wa Mfumo wa Mkojo kinasema kati ya asilimia 10 na 15 ya wanandoa hushindwa kupata watoto, na katika asilimia 60 ya visa hivyo tatizo huwa linahusu mwanaume kwa kiwango fulani au kikamilifu. Mojawapo ya hali ngumu zaidi ni ile ambapo mwanaume hukosa mbegu za uzazi. Kuna aina mbili za hali hiyo. Ya kwanza hutokana na kuziba kwa njia za kupitisha mbegu na mara nyingi inaweza kutibiwa kwa upasuaji na ya pili hutokea pale korodani zinaposhindwa kabisa kuzalisha mbegu za uzazi, jambo ambalo lina tiba chache na ndilo lililolengwa na watafiti katika utafiti huu. Kwa sasa, wanaume wengi wenye tatizo hilo hulazimika kufanyiwa upasuaji wa kutafuta mbegu za uzazi moja kwa moja kwenye korodani. Hata hivyo, katika baadhi ya wagonjwa nafasi ya kupata hata mbegu moja inayoweza kutumika ni karibu asilimia 40 pekee. Zaidi ya hayo, matibabu hayo pamoja hugharimu kati ya Sh150,000 na zaidi ya Sh500,000 kwa mzunguko mmoja nchini Kenya. Gharama hizi hazifadhiliwi na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Katika utafiti huo, seli hizo ziliendelea kukua hadi hatua ambayo ni seli za mwanzo kabisa zinazozalisha mbegu za uzazi. Hata hivyo, hazikufikia hatua ya mwisho ya kuwa mbegu kamili zinazoweza kurutubisha yai. Kiongozi wa utafiti huo, Dkt Kotaro Sasaki wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, alisema tofauti kati ya seli za binadamu na zile za panya zilizotumika kusaidia ukuaji huenda ndiyo iliyozuia kukamilika kwa mchakato huo. Hatua inayofuata ni kutumia seli zinazotokana na binadamu badala ya panya ili kuona kama mbegu kamili zinaweza kutengenezwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 31 Jul 2026 07:55:32

Yafichuka daktari aliyeuawa kwa risasi asubuhi jijini aliwahi kuripoti kupokea vitisho

MAUAJI ya mwanasaikolojia Dkt Victoria Nthunya Mutiso kwa kupigwa risasi katika Barabara ya Mbagathi Link, Nairobi, Jumatano asubuhi, yamezua maswali mapya baada ya kubainika alikuwa ameripoti matukio mawili ya kutishiwa maisha miezi michache kabla ya kuuawa. Sasa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanachunguza iwapo matukio hayo yanahusiana na mauaji yake. Kwa mujibu wa taarifa za awali za polisi, Dkt Mutiso alikuwa akisafiri kuelekea kazini ndani ya teksi, gari la rangi nyeusi lilipoziba njia katika eneo la Mbagathi. Mtu aliyekuwa na bunduki alikaribia gari lao na kumpiga risasi kabla ya kutoroka. Wapelelezi wanaamini huenda alifuatwa alipoondoka nyumbani kwake. Mkurugenzi wa Mawasiliano katika DCI, John Marete, alisema maafisa wa kitengo cha mauaji wanaendelea kukusanya ushahidi wa kisayansi na kurekodi taarifa za mashahidi. Alisema watu wawili wanaochunguzwa, mwanamume na mwanamke, wanazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. Mnamo Februari mwaka huu, Dkt Mutiso aliripoti katika Kituo cha Polisi cha Mlolongo kuwa kundi la watu, akiwemo aliowatambua kuwa maafisa wa polisi, walivamia nyumba yake, kuharibu mali na kujaribu kuwaondoa kwa nguvu waliokuwa ndani. Alidai operesheni hiyo iliongozwa na afisa mmoja mkuu wa polisi. Baadaye alilalamika kuwa hakupatiwa mara moja nambari ya kuripoti tukio hilo (OB), ingawa aliipokea baadaye mwezi Mei. Kisha Julai 7, aliripoti tukio jingine baada ya mtu aliyekuwa ameabiri pikipiki kushuka akiwa na kitu kilichoonekana kama bunduki na kuelekea kwenye gari lake akiwa amesimama kwenye msongamano wa magari jijini Nairobi. Aliondoka haraka na kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kilimani. Wiki tatu baadaye, alipigwa risasi na kuuawa. Wapelelezi pia wanachunguza iwapo mauaji hayo yanahusiana na mzozo wa muda mrefu kuhusu nyumba aliyokuwa akiishi, ambao ulihusisha kesi kuhusu umiliki na ndoa zilizodumu kwa zaidi ya miaka 20 na hatimaye kusababisha kufurushwa kwa wakazi. DCI imesema uchunguzi unaendelea kubaini iwapo mizozo hiyo au matukio ya awali yalichangia mauaji hayo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 31 Jul 2026 08:55:07

Njuguna Ndung'u aanika Ruto, asema hulazimu mawaziri kufanya anachokitaka kwa woga

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung'u, amemshutumu Rais William Ruto kwa kuingilia utendakazi wa taasisi huru, akisema mtindo huu umezorotesha uwezo wa kutekeleza majukumu ipasavyo. Akizungumza katika mkutano kuhusu misaada nchini Uswizi, Prof Ndung'u alisema taasisi nyingi zina uwezo wa kufanya maamuzi sahihi lakini zinalemazwa na kile alichokitaja kuwa tabia ya mtu mmoja kutaka kudhibiti kila kitu. "Hivi sasa Rais wa sasa anaingilia utendakazi wa taasisi zote. Nendeni mkaninukuu," alisema Prof Ndung'u, akiongeza kuwa maafisa wengi hulazimika kufuata maagizo kwa hofu. Alisema akiwa Waziri wa Fedha alikataa kushiriki mikataba au mipango ambayo haikuwa sahihi. Hii ni mara ya kwanza Prof Ndung'u kuzungumzia hadharani changamoto alizokumbana nazo akiwa serikalini kabla ya kuondolewa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofuatia maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024. Kauli zake zimeibua tena mjadala kuhusu mtindo wa uongozi wa Rais Ruto. Wakosoaji wanasema anapenda kusimamia karibu kila uamuzi wa serikali, huku wafuasi wake wakimtetea wakisema ni kiongozi anayefuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya serikali. Prof Ndung'u pia alikosoa sera ya kuongeza ushuru ili kuimarisha mapato ya serikali, akisema ushuru mkubwa mara nyingi hupunguza mapato badala ya kuyaongeza. Alisema tofauti za kisiasa ndani ya serikali pia zilichangia ugumu wa kusimamia uchumi alipokuwa Waziri wa Fedha.

read more