T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 07:55:28

Wakili anavyobadili maisha ya wafugaji maeneo kame

KATIKA maeneo kame ya Laikipia, Samburu na Isiolo ambako kwa miaka mingi wafugaji wamekuwa wakitegemea madalali kuuza mifugo yao kwa bei ya hasara, mambo yanaanza kubadilika. Leo hii wengi wanapata wanunuzi, kufuatilia bei za soko, kupata huduma za mifugo na hata kuomba mikopo yote hayo kupitia simu za mkononi bila kulazimika kusafiri mamia ya kilomita. Maria Mbeneka Mutua ndiye mstari wa mbele kuleta mabadiliko hayo. Mbeneka ni wakili kitaaluma ila pia ameingilia sekta ya ufugaji kwa kuzindua mfumo unaowapa wafugaji, hasa wanawake, nafasi ya kunufaika zaidi kupitia jasho lao. Kupitia jukwaa la kidijitali la Flockr lililoundwa na kampuni yake Ranch Experts Limited, Mbeneka amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya zaidi ya wafugaji 4,500 maeneo ya Laikipia, Samburu na Isiolo. "Karibu asilimia 70 ya wanaonufaika ni wanawake na vijana ambao wamepata mafunzo ya ufugaji wa kisasa, biashara na matumizi ya teknolojia," aliambia Akili Mali wakati wa mahojiano. Zaidi ya miaka 20 iliyopita Mbeneka alikuwa akijishughulisha na biashara ya uchinjaji nyama eneo la Rumuruti, Laikipia. Akiwa mfanyabiashara wa nyama alibaini kuwa ubora wa bidhaa hiyo ulitegemea moja kwa moja namna mifugo walifugwa. Ufahamu huo ulimfanya abadili mbinu. Badala ya kusubiri mifugo wafike kichinjioni alianza kutangamana na wafugaji ili kuboresha uzalishaji, afya ya mifugo na miundomsingi ya masoko. Ndipo uasisi wa Ranch Experts ulichipukia. [caption id="attachment_189866" align="alignnone" width="2560"] Maria Mbeneka akionyesha tuzo ya Tri-Nations aliyoshinda mwezi jana. Picha|Maktaba[/caption] Mbeneka asema kadri alivyozidi kufanya kazi na jamii za wafugaji, aligundua wanawake walikuwa nguzo muhimu katika utunzaji wa mifugo lakini mara nyingi walitengwa katika maamuzi ya kibiashara. Mwaka 2020 akaanzisha mpango wa goat-for-delivery Laikipia. Kupitia mpango huo wakunga wa jadi walipewa mbuzi kwa kila mama waliyemshawishi kujifungua hospitalini. Karibu mbuzi 450 walisambazwa, na wengi wao walizaana wakawa kitega uchumi cha familia nyingi. "Tuligundua wanawake hao hawakuwa wahudumu wa afya pekee, bali pia walinzi muhimu wa mifugo katika jamii zao," anasema. Kutokana na matukio aliyoshuhudia Mbeneka aliunda mitandao ya wanawake wanaokusanya mifugo kwa ajili ya biashara na baadaye akaanzisha Flockr, jukwaa la kidijitali linalowaunganisha wafugaji na wanunuzi ili kutoa huduma za mifugo, taarifa za bei ya soko, usafirishaji, bima na mikopo. "Kupitia Flockr wafugaji hupata taarifa hizo zote na huduma moja kwa moja," aeleza. Jukwaa hilo limesaidia wafugaji kufanya maamuzi bora kuhusu uzalishaji na mauzo, huku ikipunguza utegemezi wa madalali. Sekta ya ufugaji Kenya ina thamani ya karibu Sh1 trilioni, lakini bado haijatumia kikamilifu fursa zilizopo kutokana na ukosefu wa mifumo bora ya taarifa na masoko. Mbeneka anataja gharama kubwa za usafirishaji wa mifugo, ushuru wa kaunti – ada inayotozwa kusafirisha mizigo na bidhaa kutoka kaunti moja hadi nyingine - ucheleweshaji wa vibali na athari za mabadiliko ya tabianchi kuwa miongoni mwa changamoto zinazozuia sekta hiyo kunawiri. Hata hivyo, anaamini suluhisho lipo katika kujenga mifumo inayothamini mfugaji. "Licha ya changamoto hizo ninaamini mifumo bora, matumizi ya teknolojia na kupiga jeki wanawake ndiyo njia ya kufanya sekta ya mifugo kuwa kichochea kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi nchini," anahoji. Jitihada zake zilimfanya kutambuliwa katika Maonyesho ya Mifugo ya Tri-Nations 2026 yaliyofanyika nchini Tanzania, ambapo alitunukiwa Tuzo ya Mwanamke Bora mwaka huu. "Nilipotangazwa mshindi mwanzoni sikuamini. Lakini baadaye nikatambua kuwa kazi tuliyofanya na wafugaji imepiga hatua za mmbali kuliko nilivyodhania," asema kwa tabasamu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 06:55:34

Ukuzaji wa mimea-tiba ulivyoibuka kimbilio kwa wenye uhaba wa ardhi Kiambu

KAUNTI ya Kiambu inaendelea kupoteza ardhi ya kuendesha kilimo kutokana na ukaribu wake kwa jiji kuu la Nairobi, ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa majengo ya makazi na biashara. Kwa sababu hiyo wakulima wamegeukia mimea yenye thamani ya juu isiyohitaji shamba kubwa kukuzwa, miongoni mwao mimea tiba, ili kuunda hela nzuri. Kati ya wakulima hao ni George Wang'ang'a na William Gitau, vijana barobaro kutoka kata ya Kagaa katika wadi ya Kamburu. Kati ya mimea tiba ambayo wanakuza ni pamoja na orange thyme, lemon thyme, garden sage, mint, white oregano, African blue basil, lemon grass, verbena, lemon balm, lavender, marjoram, stevia na blue vervain. Wang'ang'a asema ingawa Kiambu inafahamika kwa kilimo cha kuzalisha mimea ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, ndizi na maparachichi waliamua kuzamia kilimo cha mimea tiba kutokana na uhaba wa mashamba katika sehemu kubwa ya kaunti hiyo ambayo pia inafahamika kwa kukuza majani chai kwa wingi. Aidha, alihoji kuwa umiliki wa mashamba mengi eneo hilo ni wa wakongwe au kifamilia hivyo huwa vigumu vijana kutengewa kipande kwa ajili ya kilimo. Katika kipande cha robo ekari wawili hao wanakuza zaidi ya mimea tiba 30. Walivutiwa na kilimo hiki kutokana na mapenzi yao ya kutunza mazingira. Pia lengo lao ni kutoa suluhu la kudumu kwa watu ambao wanaugua maradhi mbalimbali kupitia mimea hiyo asilia. Msukumo huo ulichochewa na hamasisho kutoka kwa shirika la Healthy Living Tech-Agri Campaign, ambalo huwaleta pamoja wakulima wa mimea tiba na mashirika husika ya kijamii. Wang'ang'a anatoa mfano wa thyme ambao husaidia kurahisisha shughuli ya kumeng'enya chakula tumboni. Aidha, lemon grass na rosemary hutumika kama kiungo cha kuandaa chai. "Mimea tiba inapendwa na watu wanaoishi mijini maana hawapati vyakula asilia kwa wingi. Vile vile, inatumika sana na watu wanaougua maradhi yasiyoambukiza kama vile saratani au shinikizo la damu," aliambia Akili Mali wakati wa mahojiano hivi majuzi. Isitoshe, mimea tiba hutumika katika viwanda kutengeneza tembe za dawa mbalimbali hususan vijalizo [supplements kwa Kimombo] na pia vipodozi asilia. Wang'ang'a alidokeza kuwa sababu nyingine kuu ya kuzamia kilimo hiki ni kwamba wakulima wengi nchini wanakuza mimea yenye thamani ya chini kama vile mahindi. "Kwa mfano, katika robo ekari unaweza kuvuna miti tiba ambayo thamani yake ni sawa na mahindi yaliyopandwa katika ekari tano ya shamba," anaeleza. Kwa upande wake Gitau asema kilimo cha mimea tiba ni cha manufaa sana kwa sababu mavuno yake ni mengi kutokana na kipande kidogo tu cha ardhi. Pili, anasisitizia hitaji lake kubwa na soko tayari lenye uhakika si tu humu nchini bali pia kimataifa. Tatu, anahoji kwamba wakulima hutumia gharama ndogo sana kwa sababu mimea tiba haihitaji pembejeo nyingi kama vile mbolea au dawa za kemikali kuua wadudu kwani inakuzwa katika mazingira yake asilia. "Mimea hii hutumika kuimarisha virutubisho mchangani. Pia kwa nyuki ni malighafi ya kuzalisha nta inayotumika katika kuunda asali," asema. Gitau aeleza kwamba alipata ujuzi wa kukuza aina mbalimbali ya mimea tiba baada ya kutangamana na mashirika kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula na Kilimo (FAO). Pia amekuwa akishirikiana na Wizara ya Kilimo ya Kaunti ya Kiambu miongoni mwa mashirika mengine kuhamasisha wakulima wadogo kuhusu manufaa ya kukuza mimea yenye thamani. Aidha makundi ya akina mama na vijana kutoka Kiambu yameanza kuona umuhimu wa mimea tiba kama kitega uchumi. Kwa sababu ni kilimo kinachohitaji mtaji mdogo, faida yake ni kubwa ikizingatiwa kuwa baadhi ya mavuno huuzwa hadi Sh6,000 kwa kilo. Lakini pia kuna changamoto kama vile uhaba wa mvua. Vile vile, si wawekezaji wengi wamejitosa kufadhili kilimo hicho cha mimea tiba.

read more