T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 22 Jul 2026 03:55:39

Serikali yakubali ukosoaji wa ufadhili elimu ya juu; yaweka mpango wa 'kufaidi wote'

WANAFUNZI wote watakaofuzu kujiunga na vyuo vikuu nchini watapata ufadhili kamili wa masomo kutoka kwa serikali iwapo pendekezo jipya la ufadhili wa elimu ya juu litapitishwa na Bunge. Rais William Ruto alitangaza hatua hiyo Jumanne katika Ikulu, akisema serikali imewasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria yatakayowezesha kila mwanafunzi anayefaulu mtihani wa kitaifa na kupata nafasi katika chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu kufadhiliwa kikamilifu bila kujali hali ya kifedha ya wazazi wake. "Kwa sasa tuna pendekezo bungeni litakalowezesha elimu ya juu kuwa ya wote. Haitajali mtoto anatoka katika familia gani, bali uwezo wake kitaaluma. Mwanafunzi yeyote anayefaulu na kupata nafasi chuoni atapata ufadhili kamili," alisema Rais Ruto. Aliwahimiza wabunge kuharakisha kupitisha marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) ili wanafunzi watakaoanza masomo Septemba mwaka huu wanufaike kwa mfumo huo mpya. Tangazo hilo linaashiria kuwa serikali inaweza kuachana na mfumo wa sasa wa ufadhili wa elimu ya juu ulioanzishwa mwaka wa 2023 ambao umekoselewa na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu. Rais alisema mfumo wa awali haukufaulu kwani ulisababisha vyuo vikuu vingi kukumbwa na matatizo ya kifedha baada ya serikali kushindwa kutoa kiwango cha fedha ilichoahidi. "Baadaye tukaanzisha mfumo wa usawa ambapo wazazi walichangia sehemu ya karo, serikali ikatoa sehemu kupitia ufadhili na sehemu nyingine kupitia mkopo. Tulidhani ungeleta usawa lakini umeonekana kutotosha," alisema. Aliongeza kuwa chini ya mfumo mpya, wazazi watakuwa na hiari ya kuchangia karo za watoto wao, lakini iwapo hawataweza kufanya hivyo, serikali itagharimia masomo yote. "Hatutaki mwanafunzi yeyote ashindwe kuendelea na masomo kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Rais. Hata hivyo, maelezo ya kina kuhusu mfumo huo bado hayajatolewa. Katibu wa Elimu ya Juu, Dkt Beatrice Inyangala, alisema pendekezo hilo bado linashughulikiwa kabla ya kuwasilishwa rasmi kwa wadau na Bunge. "Bado tunalifafanua na kulikamilisha. Ni mchakato unaohitaji muda," alisema. Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma, Prof Daniel Mugendi, pia alisema bado hajapokea maelezo kamili ya mfumo huo. "Hatujapata maelezo ya kina. Yakikamilika tutashirikishwa kwa majadiliano zaidi," alisema. Changamoto ya ufadhili wa elimu ya juu imekuwa ikisumbua serikali kwa miaka kadhaa. Madeni ya vyuo vikuu vya umma yameongezeka kutoka takriban Sh60 bilioni mwaka wa 2022 hadi zaidi ya Sh85 bilioni sasa. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa HELB Geoffrey Monari amependekeza taasisi hiyo ipate fedha kupitia masoko ya kifedha kwa kutoa dhamana ya kijamii ya thamani ya Sh500 milioni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata ufadhili kwa wakati. Kwa sasa, takriban 450,000 wanaonufaika na mikopo ya HELB wanaendelea kulipa mikopo yao, hali inayowezesha bodi hiyo kukusanya karibu Sh700 milioni kila mwezi. Mbali na mikopo, HELB hutenga Sh237 milioni kila mwaka kama ufadhili kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo Sh137 milioni huenda kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Sh100 milioni kwa wanafunzi wa vyuo vya TVET.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Mabadiliko katika uume yanayohitaji ushauri wa daktari haraka upesi

MABADILIKO katika uume yanaweza kuwa ishara ya matatizo makubwa ya kiafya, yakiwemo kisukari, magonjwa ya figo na saratani, hii ni kulingana na utafiti ulioangazia dalili ambazo wanaume wengi hupuuza. Mtaalamu wa Masuala ya Matibabu, Shafi Wardak, wa kliniki ya The Forbury, Uingereza, kwenye utafiti huo, anaonya kuwa wanaume hawapaswi kumakinik   ia uwezo wa uume kupata ashiki pekee, bali pia mabadiliko mengine yasiyo ya kawaida katika kiungo hicho. Kati ya dalili ambazo zinaonyesha huenda mambo si kawaida, ni mabadiliko ya kukojoa. Kukojoa mara nyingi kunaweza kuashiria kisukari, maambukizi kwenye njia ya mkojo au kuongezeka kwa tezi dume. Mkojo dhaifu unaweza kuashiria kuziba kwa njia ya mkojo au saratani ya tezi dume. Kukojoa kidogo na mkojo mweusi kunaweza kuashiria upungufu wa maji mwilini au matatizo ya figo. Pia kuna vipele na vidonda kwenye uume ambavyo vinaweza kusababishwa na magonjwa ya zinaa au saratani ya uume. Vidonda visivyouma vinaweza kuwa ishara ya maradhi kama kaswende. Mabadiliko ya ngozi pia ni ya kuangaliwa kwa kuwa kubadilika rangi, kuchubuka kunaweza kuashiria magonjwa ya ngozi au maambukizi yanayohitaji uchunguzi wa kina wa daktari. Uume kupinda wakati wa ashiki na kusababisha maumivu kunaweza kuashiria ugonjwa wa 'Peyronie', unaosababishwa na kovu kujijenga ndani ya misuli za uume. Pia harufu na mabadiliko ya shahawa ni jambo la kutathminiwa. Harufu isiyo ya kawaida inaweza kuashiria uvimbe wa kichwa cha uume nako kupungua kwa shahawa au nguvu ya kumwaga kunaweza kuhusishwa na kisukari, upungufu wa homoni za kiume au kuzibwa kwa mirija. Wardak anashauri wanaume kuosha sehemu za siri kwa maji na sabuni isiyo kali na kuvaa chupi safi zinazopitisha hewa. "Hata mabadiliko madogo katika, rangi au mwonekano wa ngozi, kama vile vipele, uvimbe au madoadoa, yanapaswa kuzingatiwa. Ingawa baadhi ya mabadiliko yanaweza kusababishwa na mwasho mdogo, mengine yanaweza kuashiria maambukizi au magonjwa yanayoandama sehemu za siri," akasema Wardak. Wataalamu wanasisitiza kuwa dalili hizi hazithibitishi moja kwa moja ugonjwa fulani, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu badala ya kujitibu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Ushindi wa Democrats wamweka Netanyahu matatani

JERUSALEM, Israel: WAPINZANI wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wametumia ushindi wa chama cha Democrats katika uchaguzi wa katikati ya muhula Amerika kumshutumu kwa kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa Israel na vyama vikuu vya kisiasa Amerika. Democrats walipata viti vingi katika Seneti na Bunge la Congres katika uchaguzi wa Jumanne, Novemba 3, matokeo ambayo ni pigo kwa Rais Donald Trump, huku hasira za wapigakura kuhusu vita vya Amerika na Israel dhidi ya Iran zikichangia matokeo hayo. Ushindi huo unajiri wiki moja baada ya muungano wa mrengo wa Netanyahu kupoteza wingi wa viti katika uchaguzi wa Israel. Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democrats nchini Israel, Yair Golan, alisema matokeo hayo yanaonyesha jinsi Netanyahu alivyopoteza uungwaji mkono Amerika. "Matokeo yanaonyesha jinsi Netanyahu alivyo sumu kisiasa miongoni mwa Democrats na Republican," akasema. Kiongozi mwengine wa upinzani, Yair Lapid, alisema Israel haiwezi kumudu kuendelea kuwa na Netanyahu mamlakani. "Anahatarisha usalama wetu, anadhoofisha demokrasia yetu na ataharibu hadhi yetu katika kiwango cha kimataifa," akasema. Amerika imekuwa mshirika mkuu wa Israel kwa miongo kadhaa, ikitoa mabilioni ya dola kama msaada wa kijeshi tangu miaka ya 1970. Hata hivyo, uungwaji mkono huo umepungua kutokana na vita Gaza na mashambulizi dhidi ya Iran. Trump, ambaye alikuwa amemuunga mkono Netanyahu, aliahidi kusitisha msaada wa kila mwaka wa dola bilioni nne kwa Israel. Profesa Udi Sommer wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv alisema Bunge jipya linalotawaliwa na Democrats linaweza kuiwekea Israel shinikizo kupitia uchunguzi na maamuzi ya bajeti. "Ushindi mkubwa wa Democrats na kushindwa kwa Republican vinaashiria sura mpya ya uhusiano kati ya Amerika na Israel," akasema. Rais Isaac Herzog anatarajiwa kuanza mashauriano kuhusu kuunda serikali mpya wiki hii.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Iran wapiga sherehe kumcheka Trump kwa poteza uchaguzi wa nusu muhula

TEHRAN, Iran: SERIKALI ya Iran imekaribisha kushindwa kwa chama cha Republican cha Rais Donald Trump katika uchaguzi wa katikati ya muhula Amerika, ikisema wapigakura wameonyesha bayana kuwa wanapinga vita vilivyoanzishwa na Washington dhidi ya Tehran. Democrats walinyakua viti vingi katika Seneti na Bunge la Congress katika uchaguzi wa Jumanne, ushindi ambao umehusishwa na hasira za raia kuhusu gharama ya maisha na uamuzi wa Trump kuanzisha vita vilivyosababisha kupanda kwa bei ya mafuta. Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ambaye pia anaongoza mazungumzo ya upatanishi, alisema, kwa kupiga kura namna hivyo, raia wa Amerika wametuma ujumbe wa wazi kuwa hawataki vita hivyo. "Kwa sababu ya kupanda kwa gharama ya maisha, raia wa Amerika wamesema hawataki vita nasi tunaunga mkono ujumbe huo," aliandika kwenye mtandao wa X. Pia alionya Amerika dhidi ya kuishambulia tena Iran na kupuuza maoni ya wananchi wake. Kiongozi wa Kidini Iran, Mojtaba Khamenei, alisema uhasama wa Amerika dhidi ya nchi yake utaendelea bila kujali chama kitakachokuwa madarakani. Alionya dhidi ya kuonyesha dalili zozote za kujisalimisha kwa Amerika. "Amerika inaona mwisho wa utawala wake wa kimataifa kuwa bado uko mbali, lakini sisi tunaona umekaribia," akasema. Hata hivyo, maafisa wawili wakuu wa Iran walisema kuwa licha ya kufurahia ushindi wa Democrats, Tehran ina wasiwasi kuwa Trump anaweza kuanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi ili kufidia kushindwa kwa chama chake. Kwa hivyo, Iran bado iko katika hali ya tahadhari ya juu. Vita vilianza Februari 28 baada ya Amerika na Israel kuishambulia Iran, ambayo ilijibu kwa kushambulia Israel na mataifa ya Ghuba yenye vituo vya kijeshi vya Amerika. Mapigano hayo yameathiri usafirishaji wa mafuta na gesi duniani, huku shughuli za usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz zikitatizika. Katika taarifa yake, Khamenei alilaumu sera za Washington kwa kuongeza gharama kwa wananchi wake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Kindiki, Mudavadi washtakiwa kugawa mamilioni kwenye mikutano

NAIBU wa Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na viongozi wengine wa serikali wamefikishwa kortini kuhusiana na mamilioni ya pesa wanayotoa katika hafla tofauti nchini. Katika kesi yake, mlalamishi Kelvin Kipchirchir anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ichunguze chanzo cha fedha na mali wanayogawa kwa wananchi. Bw Kipchirchir anadai viongozi hao wamekuwa wakigawa pesa, magari, pikipiki na bidhaa nyingine katika hafla za uwezeshaji bila kuwa sehemu ya mipango rasmi ya serikali. Anataka Mahakama Kuu kuagiza EACC ichunguze chanzo cha utajiri huo na kubaini iwapo viongozi hao walikiuka sheria za maadili na matumizi ya rasilimali za umma. Kesi hiyo iliyowasilishwa Julai 31, 2025, ilitajwa Jumatano mbele ya Jaji Roselyne Aburili, lakini haikuendelea baada ya Kipchirchir kukosa kufika mahakamani. Mawakili wa serikali na wa Bunge waliomba kesi hiyo itupiliwe mbali. Jaji Aburili alisema mahakama haitatupilia mbali kesi ambayo wahusika tayari wamewasilisha hoja zao kwa maandishi. Kipchirchir anadai Kindiki amegawa zaidi ya Sh1 bilioni, huku Mbunge Oscar Sudi akidaiwa kutoa Sh145 milioni kupitia pesa taslamu na bidhaa. Viongozi wengine waliotajwa ni Spika wa Bunge Moses Wetang'ula, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah, msaidizi wa Rais Farouk Kibet, wabunge Didmus Barasa na Silvanus Osoro, pamoja na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot. Mlalamishi anasema fedha hizo hazikutengewa bajeti wala kutangazwa kama miradi rasmi ya serikali. Anadai baadhi ya hafla hizo zilitumia majukwaa na rasilimali za umma na huenda zikawa njia ya kuwashawishi wapiga kura. Anataka mahakama izuie viongozi hao kugawa mali nje ya mipango iliyoidhinishwa na kuagiza EACC ichunguze chanzo cha fedha hizo. Kesi itatajwa Januari 19, 2027, kuweka tarehe ya uamuzi kutolewa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Wandani wa Sifuna wajipata kwenye mng'ang'anio wa tiketi Bungoma

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na kibarua Kaunti ya Bungoma, ambako washirika wake watatu wanang'ang'ania tiketi ya chama cha Linda Mwananchi kuwania ugavana katika uchaguzi wa 2027. Bw Sifuna ametangaza nia ya kuwania urais 2027 kupitia chama hicho. Washirika wake Gavana wa zamani Wycliffe Wangamati, Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi na mfanyabiashara Zacharia Barasa nao wanataka ugavana. Hali ni tofauti na kaunti jirani ya Trans Nzoia, ambako Gavana George Natembeya anaonekana kuwa mgombea mkuu wa Linda Mwananchi. Bw Wangamati alihudumu kama gavana kati ya 2017 na 2022, kabla ya kushindwa na gavana wa sasa Ken Lusaka. Bw Wangamati aliunga mkono Azimio, huku Lusaka akiwa katika kambi ya Rais William Ruto. Bw Wangamati anaamini atapata tiketi ya Linda Mwananchi na kwamba yupo tayari kushiriki mchujo dhidi ya wapinzani wake. "Nimekuwa nikifanya kampeni na nilichokiona ni kwamba wakazi wa Bungoma wanataka nirudi kuwa gavana kwa sababu ya kazi niliyofanya. Niko tayari kwa mchujo wa Linda Mwananchi," akasema. "Gavana ajaye wa Bungoma atatoka Linda Mwananchi. Rekodi yangu ya maendeleo iliweka kiwango cha juu na nataka kurejea nimalize kazi yangu," akaongeza. Bw Wangamati alitaja barabara kuu yenye njia mbili Bungoma, Uwanja wa Kanduyi na Hospitali mpya ya kaunti yenye zaidi ya vitanda 300 aliyotekeleza akiwa gavana. Pia ameahidi kurejesha ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wanafunzi 300 aliowasaidia kusoma Amerika. Bw Sifuna alimkaribisha rasmi Bw Wanyonyi katika chama hicho wakati wa kuwatambulisha viongozi wake jijini Nairobi Ijumaa iliyopita. Bw Wanyonyi, nduguye Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula, anakabiliwa na kibarua cha kujenga upya siasa zake Bungoma baada ya kujikita Nairobi, ambako amekuwa mbunge tangu 2013. "Bungoma si ufalme wa kuichagua familia ya Wetang'ula kila uchaguzi. Uongozi wao haujasaidia kaunti hii katika maendeleo. Watu hawako tayari kwa uongozi wa familia ya Wetang'ula lakini sisi sasa tumemkubali Sifuna," akasema. Bw Wanyonyi alisema aliondoka ODM na kurejea nyumbani kwa wito wa kuhudumia nyumbani. "Mimi na Sifuna tulikatishwa tamaa ODM, na mliona walivyonitendea Nairobi mnamo 2017. Nilikuwa kipenzi cha wengi na ningekuwa gavana Nairobi, lakini nilikubali kurejea kwenye kiti changu cha ubunge. Sauti ya Mungu imeniambia nirudi nyumbani kuwania Bungoma," akasema. "Tunahitaji kuboresha miundombinu katika shule zetu. Nisaidieni kuibadilisha Bungoma, mabadiliko yataonekana katika maisha ya watu wetu," akasema. Bw Wanyonyi amekuwa akiwakilisha eneobunge la Westlands tangu 2013, huku siasa zake zikijikita zaidi jijini Nairobi. Kurejea Bungoma kunamaanisha atahitaji kuwashawishi wapigakura kwamba ana uhusiano na masuala ya kaunti. Kwa upande wake, Bw Barasa anasema juhudi zake za kutetea mali na maslahi ya umma zinampa msingi wa kuomba uungwaji mkono wa wakazi wengi. Bw Barasa, mfanyabiashara kutoka Bumula, alieleza kuwa alipigania kurejeshwa kwa ardhi ya uwanja wa ndege kwa umma mahakamani na pia Kiwanda cha sukari cha Nzoia. "Mimi ni mtu ambaye nimekuwa nikipigania kaunti hii. Nilienda mahakamani na kupigania uwanja wa ndege urejeshwe. Sifuna akipanda ngazi ya uongozi wa kitaifa na mimi kuwa gavana, kaunti hii itaongozwa vyema," akasema. Bw Barasa anaamini atapata tiketi ya Linda Mwananchi akisema ameitumikia kaunti kabla ya kuwania wadhifa. Amesema kuwa Mabw Wangamati na Wanyonyi walimpata katika siasa za Bungoma na ana uwezo wa kuwashinda.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Wizara sasa yabadilisha kalenda ya elimu kuanzia mwaka wa 2027 kukabili migomo

WIZARA ya elimu imepanga upya kalenda ya shule ya mwaka wa 2027 huku ikirefusha likizo za katikati ya muhula na kubadilisha vipindi vya likizo katika mabadiliko yaliyofuatia ghasia zilizoshuhudiwa shuleni katika muhula wa pili 2026. Kalenda mpya inapunguza muhula wa pili kutoka wiki 14 hadi wiki 13 katika viwango vyote vya shule na kuongeza muhula wa tatu kutoka wiki tisa hadi 10. Wanafunzi pia watakuwa na likizo ndefu zaidi za katikati ya muhula huku likizo ya Februari ikiongezeka kutoka siku tano hadi tisa kwa shule za chekechea, msingi na sekondari ya msingi, na siku 10 kwa sekondari ya juu na shule za upili. Likizo ya katikati ya muhula mnamo Juni itaongezeka vilevile kutoka siku tano hadi siku 11 kwa shule za msingi na sekondari msingi, na siku 12 kwa sekondari ya juu na sekondari. Mabadiliko hayo yamefuatia tangazo alilotoa Waziri wa Elimu Julius Ogamba Juni kwamba Wizara itaainisha kalenda ya shule kuhakikisha usawazishaji wa muda wa kusoma, baada ya ghasia zilizoathiri shule 204. Wizara ilihusisha baadhi ya machafuko na uchovu kwa wanafunzi, ikiwemo masuala mengine kama vile shinikizo la mtihani, changamoto za uongozi, hali duni za bweni, shinikizo la wanarika na matumizi ya dawa za kulevya. Oktoba, Ogamba aliteua timu ya wanachama 52 kutoka taasisi mbalimbali iliyoongozwa na Profesa Peter Mulwa Mbithi, kuchunguza kiini cha ghasia na kupendekeza mageuzi ya kuboresha maslahi, usalama na nidhamu kwa wanafunzi. Chini ya kalenda mpya, kalenda ya masomo 2027 itaanza Januari 4 ambapo shule za chekechea, msingi na sekondari ya msingi zitafunga kwa muhula wa pili Aprili 9, baada ya wiki 14.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Waziri Joho arejea shuleni, aendea digrii ya uzamili na kupuuzilia mbali kejeli za D-

WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Bahari na Masuala ya Ubaharia, Bw Hassan Joho, ametoa changamoto kwa vijana wajitahidi maishani, huku ikifichuka kwamba anaendeleza masomo ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM). Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa Laila Abubakar, alithibitisha Bw Joho ni mwanafunzi katika chuo hicho licha ya majukumu yake mazito katika Baraza la Mawaziri. Duru katika chuo hicho zilisema anasomea shahada ya uzamili katika Masomo ya Maendeleo, akiwa anakamilisha mwaka wake wa kwanza huku mitihani ikiendelea. Kozi hiyo huchukua miaka miwili. Kwa miaka mingi, Bw Joho amekuwa akikejeliwa kwa kupata alama ya D- kwenye mtihani wake wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE). Hata hivyo, amekuwa akieleza safari yake kama ushahidi wa uvumilivu, akitaja umaskini na changamoto za kifedha alizokabiliana nazo akiwa kijana kuwa sababu kuu zilizochelewesha masomo yake. Akizungumza chuoni humo Jumanne, Bw Joho alitafakari kuhusu gharama ya kupoteza muda na vikwazo vya kimuundo vinavyowakabili vijana kutoka familia zisizojiweza. "Muda unaweza kuwa na gharama kubwa kwa baadhi ya watu, kiasi cha kubadilisha maisha yao kabisa. Niulizeni mimi, mtu ambaye alipata fursa ya kuendelea na elimu ya juu akiwa mtu mzima," alisema Bw Joho. Alieleza jinsi umaskini unavyowalazimu vijana wengi kufanya kazi kabla ya kuendelea na masomo, akisimulia masaibu yake mwenyewe alipokuwa shule ya upili ambapo alilazimika kusawazisha kazi na masomo. "Nilifanya kazi nilipokuwa shule ya upili. Kwa kweli, siku nitakapoandika kitabu changu, nitaeleza kisa hicho kwa undani. Nilikuwa na makubaliano mazuri na mkuu wa shule. Nilimwambia 'bwana, usijisumbue kunihusu, usinifukuze' kwa sababu bado nilikuwa nikiondoka shuleni mapema tofauti na wanafunzi wengine. Kwa nini? Kwa sababu nilihitaji kufanya kazi kujiongezea kipato," alifichua. Aliwahimiza vijana kushiriki katika siasa bora ili kusaidia kuunda sera zitakazowalinda vizazi vijavyo dhidi ya changamoto kama hizo. Wakati wa kuhojiwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uteuzi mwaka 2024 kuhusu uteuzi wake katika Baraza la Mawaziri, Bw Joho alizungumzia kwa uwazi historia yake ya elimu mbele ya jopo lililoongozwa na Spika wa Bunge Moses Wetang'ula. Aliwaambia wabunge kuwa alipata alama ya D- (minus) katika KCSE mwaka wa 1993 katika Shule ya Upili ya Serani, akieleza kuwa changamoto za kijamii na kiuchumi zilimwathiri kielimu. Baada ya mitihani yake ya KCSE mwaka 1993, changamoto za kifedha zilimlazimu Bw Joho kuchelewesha kujiunga na masomo ya baada ya sekondari. Baadaye alifuata mkondo rasmi wa elimu, akihitimu kozi ya cheti katika usimamizi wa biashara mwaka 2008 na diploma ya usimamizi wa rasilimali watu mwaka 2007. Baadaye alipata Shahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kampala mwaka wa 2013 na shahada ya pili kutoka Gretsa University mjini Thika. Kabla ya kujiunga na TUM, Bw Joho pia alisomea uongozi wa umma katika Harvard Kennedy School of Government. Akizungumzia maswali ya mara kwa mara kuhusu vyeti vyake vya elimu wakati wa kuhudumu kama Mbunge wa Kisauni (2007–2013) na Gavana wa Mombasa (2013–2022), Bw Joho alisema viongozi hushukiwa bila haki, akisisitiza kuwa njia zisizo za kawaida za kupata elimu zinaweza pia kutoa viongozi waliohitimu kikamilifu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Wimbi la kuhama vyama lashika kasi kuelekea 2027

VIONGOZI wa kisiasa wameanza kuhama vyama kwa wingi huku uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027 ukikaribia, kila mmoja akitafuta tiketi ya chama anachoamini kitampa nafasi nzuri ya kushinda. Katika siku za hivi majuzi, makao makuu ya vyama mbalimbali yamekuwa na shughuli nyingi, huku viongozi na wanasiasa wanaotaka kuwania nyadhifa tofauti wakipokelewa kutoka vyama pinzani. ODM ni miongoni mwa vyama vinavyopokea wageni wengi, kikilenga kuimarisha ushawishi wake kote nchini licha ya kuwa kitashiriki uchaguzi wa kwanza bila mwanzilishi wake, marehemu Raila Odinga. Naibu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Gavana wa Kisii Simba Arati amesema chama hicho hakitaisha kufuatia kifo cha Raila, kama baadhi ya wapinzani wake wanavyodai. Arati alisema ODM bado kina nguvu na milango yake iko wazi kwa wanasiasa wanaotaka kujiunga nacho. "ODM kiko imara sana na tunawaambia wasubiri waone. Tuko tayari kupokea wanachama zaidi. Wiki ijayo tutapokea wabunge saba ambao wameonyesha nia ya kujiunga nasi kutoka vyama vingine," alisema. Miongoni mwa viongozi waliojiunga na ODM ni aliyekuwa Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, aliyeondoka Kanu ya Gideon Moi akiwa ameandamana na madiwani saba walio mamlakani pamoja na wagombeaji wengine. Poghisio alisema analenga kuwania ugavana wa Pokot Magharibi kwa tiketi ya ODM katika uchaguzi ujao. Alisema chama hicho kina historia nzuri katika eneo hilo na kina nafasi ya kushinda viti vingi vya kisiasa. "ODM imekuwa chama chenye nguvu Pokot Magharibi. Si mara yangu ya kwanza kuvaa rangi ya chungwa. Nilikuwa mmoja wenu miaka iliyopita kabla ya ODM kugawanyika na nilikuwa mwenyekiti wa kitaifa wa ODM-Kenya. Sasa tunataka kuwezesha ODM kupata ugavana, madiwani 20 na wabunge wanne," alisema. Hata hivyo, Poghisio alisisitiza kuwa eneo hilo litaunga mkono azma ya Rais William Ruto kutetea kiti chake mwaka 2027. Kuhamia kwa Poghisio na wenzake ODM kulifuatia kupokelewa kwa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, aliyehama UDA ya Rais Ruto. Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda, aliyechaguliwa kwa tiketi ya Kanu, pia ameonyesha nia ya kujiunga na ODM. Silas Jakakimba naye alipokelewa rasmi ODM baada ya kuondoka UDA. Anatarajia kuwania ubunge Suba Kaskazini mwaka 2027, kiti kinachoshikiliwa na Millie Odhiambo. Huku ODM ikipokea wanachama wapya, chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) kinachoongozwa na Mbunge wa Gem David Ochieng pia kimekuwa kikivutia wanasiasa. Mnamo Jumanne kilipokea wabunge Oku Kaunya wa Teso Kaskazini na Joseph Oyula wa Butula, ambao walichaguliwa kupitia ODM. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pia kinatarajiwa kupokea wagombeaji kutoka vyama vingine. Gachagua amedai kuwa wabunge kadhaa waliochaguliwa kwa tiketi ya UDA wanasubiri muda mwafaka wa kuhamia upande wake. Katika kaunti ya Nairobi, wabunge wote watatu wa Jubilee waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita wametangaza kuwa watatetea viti vyao kupitia DCP. Hao ni Yusuf Hassan wa Kamukunji, Mark Mwenje wa Embakasi ya Kati na Amos Mwago wa Starehe. Mbunge wa Kariobangi Kaskazini James Gakuya, aliyechaguliwa kupitia UDA, pia ameonyesha nia ya kutafuta tiketi ya DCP kuwania ugavana wa Nairobi. Wakati huohuo, vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna linatarajiwa kuvutia wagombeaji wapya. Winnie Odinga, binti wa Raila na mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ameashiria uwezekano wa kuwania useneta Nairobi mwaka 2027 kupitia ODM au Linda Mwananchi. Hata hivyo, bado hajafanya uamuzi kuhusu chama atakachotumia, huku akiwaomba wafuasi wake na wanaomfuatilia mitandaoni kumsaidia kuchagua chama kinachofaa. Mabadiliko haya yanaashiria kuwa safari ya kuwania tiketi za vyama imeanza mapema, huku wanasiasa wakipima nguvu za vyama na nafasi zao za kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Kalonzo aingia baridi baada ya Gachagua kumkaribisha Ngilu nyumbani Wamunyoro

USHIRIKIANO unaochipuka kati ya kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda ukazua ushindani mpya wa kisiasa katika ngome ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, baada ya aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu kuingia kwenye hesabu za upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027. Mkutano wa Gachagua na Ngilu nyumbani kwake Wamunyoro Jumanne umeibua maswali kuhusu mikakati ya kuunganisha Mlima Kenya, Magharibi na maeneo ya Kusini Mashariki ili kuunda muungano wenye nguvu za kumkabili Rais William Ruto. Gachagua alilinganisha mazungumzo hayo na muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) uliofanikisha kuondoa KANU madarakani mwaka 2002 baada ya kutawala kwa miaka 40. Alikumbuka jinsi aliyekuwa rais marehemu Mwai Kibaki alivyoshirikiana na marehemu Michael Kijana Wamalwa wa Magharibi, huku Ngilu akiwa miongoni mwa viongozi walioungana kumng'oa KANU. Washirika wa Gachagua na Sifuna wanasema wanataka kufufua mkakati huo kupitia kile wanachokiita "Muungano wa Milima", unaolenga kuunganisha Mlima Kenya na eneo la Mlima Elgon, ambako Sifuna ana ngome yake ya kisiasa. Aidha, wanataka kupanua ushawishi wao katika Kusini Mashariki, eneo ambalo Kalonzo amekuwa na ushawishi mkubwa kupitia chama cha Wiper. Mmoja wa maafisa wa kambi hiyo aliambia Taifa Leo kuwa wanatambua uwezo wa kura za Mlima Kenya na Magharibi na wanataka maeneo hayo yawe nguzo za muungano wao. Alidokeza kuwa Ngilu anaweza kusaidia kuvutia wafuasi wa Kusini Mashariki iwapo Kalonzo hatakubaliana na mpango wao. Hata hivyo, hatua ya Ngilu kukutana na Gachagua imezua hasira katika kambi ya Kalonzo. Seneta wa Kitui Enoch Wambua alimshutumu Ngilu kwa kutaka kudhoofisha azma ya Kalonzo kuwania urais. Alimtaja kama mwanasiasa anayebadilisha misimamo kwa manufaa binafsi na kudai mkutano wa Wamunyoro ulilenga kuunda kituo kingine cha nguvu za kisiasa kushindana na Wiper eneo hilo. Wambua pia alidai Ngilu aliwahi kushirikiana na wapinzani wa Kalonzo katika uchaguzi uliopita ili kushinikiza uwezo wake wa kuwa naibu wa marehemu Raila Odinga upimwe kupitia kinachofahamika kama mahojiano. Lakini Seneta wa Makueni Dan Maanzo alimtetea Ngilu, akisema bado ni sehemu ya mashauriano ya upinzani na hakuna njama iliyofichwa katika mkutano huo. Maanzo alionya kuwa hakuna jamii moja au mbili zinazoweza kushinda uchaguzi wa urais pekee, akisema upinzani haupaswi kupoteza chama, mgombeaji au hata kura moja. Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala amekuwa akitetea muungano wa Mlima Kenya na jamii ya Mulembe, akisema lengo ni kuunganisha wapinzani ili kumbwaga Ruto. Hata hivyo, Gachagua amejitenga na matamshi ya Malala, akisema hayawakilishi msimamo rasmi wa chama. Mvutano mwingine unahusu nani anafaa kuongoza upinzani katika uchaguzi wa 2027. Wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya Linda Mwananchi, Kalonzo alionya dhidi ya kutangaza mgombeaji mapema kabla ya mashauriano na taratibu rasmi za vyama kukamilika. Alisema Sifuna anafaa kusubiri uamuzi wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Linda Mwananchi Movement (LMM) lililopangwa Novemba 13. Kwa upande wake, viongozi wa Wiper katika Pwani wamesisitiza kuwa Kalonzo anapaswa kuwania urais mwenyewe iwapo hatapewa tiketi ya pamoja ya upinzani, wakipinga uwezekano wa kuwa mgombeaji mwenza wa kiongozi mwingine. Mkutano wa Ngilu na Gachagua kwa hivyo umeongeza mwelekeo mpya katika mazungumzo ya upinzani. Hata hivyo, bado hakuna makubaliano rasmi kuhusu mgombeaji mmoja, ugavi wa nafasi za uongozi au muundo wa muungano. Wachambuzi wanasema changamoto kubwa kwa wapinzani ni kugeuza mikutano na kauli za kisiasa kuwa makubaliano yatakayoruhusu viongozi wenye matarajio tofauti kufanya kazi pamoja bila kudhoofisha ngome zao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Utafiti wabaini kaunti ambazo biashara hunawiri kwa urahisi, na hurekodi pato nzuri

WANAOENDESHA biashara katika kaunti za Tana River, Pokot Magharibi, Kajiado na Mandera wana nafasi kubwa ya kupata mapato ya zaidi ya Sh50,000 kwa mwezi kuliko wenzao katika maeneo mengine nchini. Utafiti mpya wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) unaonyesha kuwa kaunti hizo zinaongoza kwa idadi ya biashara za familia zilizo na mapato yanayozidi kiwango hicho kila mwezi. Katika utafiti wa Kenya Mini Demographic and Health Survey wa 2025-2026, Tana River inaongoza kwa asilimia 32.3 ya biashara za familia zinazoingiza zaidi ya Sh50,000 kila mwezi. Hii ina maana kuwa karibu biashara moja kati ya tatu katika kaunti hiyo huingiza kiasi hicho, sawa na angalau Sh600,000 kwa mwaka. Pokot Magharibi inashika nafasi ya pili kwa asilimia 25.4, ikifuatiwa na Kajiado kwa asilimia 22.3 na Mandera kwa asilimia 20.3. Hizi ndizo kaunti nne pekee nchini ambako zaidi ya biashara moja kati ya tano zinazoendeshwa na familia huingiza mapato yanayozidi Sh50,000 kwa mwezi. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa biashara za familia katika maeneo hayo zina uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato ikilinganishwa na sehemu nyingine za nchi. KNBS inasema biashara zinazopata wastani wa Sh50,000 au zaidi kwa mwezi zinapatikana katika asilimia 15 ya familia za mijini, ikilinganishwa na asilimia sita ya familia za mashambani. Utafiti huo ulifanywa kati ya Novemba mwaka jana na Februari 2026, ukihusisha familia 26,380 kote nchini. Ulijikita katika masuala mbalimbali yakiwemo afya, hali ya maisha na shughuli za kiuchumi za familia. Kaunti nyingine zilizo na biashara nyingi zenye mapato ya zaidi ya Sh50,000 ni Kericho, Nyandarua, Nairobi, Kiambu, Machakos na Marsabit. Katika Kericho, biashara 13 kati ya 74 zilizoshiriki utafiti zilikuwa zikipata kiasi hicho. Nyandarua ilikuwa na biashara sita kati ya 33, huku Nairobi ikiwa na biashara 226 kati ya 1,338. Kiambu ilirekodi biashara 58 kati ya 383, Machakos 27 kati ya 179, huku Marsabit ikiwa na asilimia 13.7 ya biashara zilizofanyiwa utafiti. Licha ya baadhi ya kaunti kuwa na biashara zinazopata mapato makubwa, utafiti unaonyesha kuwa biashara nyingi za familia nchini bado zinapata kiasi kidogo. KNBS ilisema asilimia 34 ya biashara za familia nchini ziliripoti mapato ya wastani ya Sh5,000 au chini kwa mwezi. Biashara zilizokuwa zikijizolea kati ya Sh10,000 na Sh19,999 zilichangia asilimia 22, huku zile zilizopata kati ya Sh20,000 na Sh49,999 zikiwa asilimia 21. Kwale inaongoza kwa kuwa na biashara nyingi zaidi zinazopata chini ya Sh5,000 kwa mwezi, huku asilimia 64.6 ya biashara zilizoshirikishwa katika utafiti katika kaunti hiyo zikiangukia kundi hilo. Turkana inafuatia kwa asilimia 61.3, Busia ikiwa na asilimia 60.4, Kilifi asilimia 56.2 na Tharaka Nithi asilimia 56. Kaunti nyingine zenye idadi kubwa ya biashara zinazopata mapato hayo madogo ni Wajir kwa asilimia 54.1, Siaya (53), Bungoma (52.2), Samburu (51.4) na Kakamega (50.2). Hii ina maana kuwa biashara hizo hupata chini ya Sh170 kwa siku, au chini ya Sh60,000 kwa mwaka. Utafiti huo pia unaonyesha kuwa familia moja kati ya tano nchini inaendesha biashara, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa lengo la kupata mapato. Ingawa biashara nyingi za familia ziko maeneo ya mashambani, biashara kubwa kubwa zaidi ziko mijini, ambako robo ya familia zina angalau mwanachama mmoja anayeshughulika na biashara. Turkana inaongoza kwa asilimia 42.7 ya familia zinazoendesha biashara, ikifuatiwa na Kisumu kwa asilimia 33, Homa Bay (32.1) na Migori (31.8). KNBS ilibaini pia kuwa uwezekano wa familia kuendesha biashara huongezeka kadiri hali yake ya kiuchumi inavyokuwa bora. Katika familia zilizo katika kundi la chini zaidi la utajiri, ni asilimia 10 pekee zinazoendesha biashara, ikilinganishwa na asilimia 27 katika kundi la familia tajiri zaidi. Matokeo haya yanaonyesha tofauti kubwa katika uwezo wa biashara za familia kuzalisha mapato, huku baadhi ya maeneo yakirekodi mafanikio makubwa na mengine yakikabiliwa na mapato duni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 04 Nov 2026 17:02:48

T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 04 Nov 2026 14:34:29

Man United yazinduka usingizini na kung'ata mtu hatimaye

BAYERN Munich na Paris Saint-Germain (PSG) zimeimarisha matumaini yao ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kupata ushindi mnono dhidi ya Atletico Madrid na Villarreal mtawalia Jumanne usiku. Manchester United ilionyesha juhudi za kupambana kwa kurejea kutoka nyuma kwa mabao mawili na kuichapa AS Roma 3-2 katika mechi ya kusisimua kwenye Uwanja wa Old Trafford. Bayern ilipata ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Atletico Madrid, ambayo iliwasumbua kwa muda mrefu. Lennart Karl aliifungulia Bayern ukurasa wa mabao dakika ya 54 kabla ya Konrad Laimer kuongeza la pili dakika ya 74, akitumia pasi ya Harry Kane. PSG nayo iliweka rekodi kwa kufunga mabao manne ndani ya dakika 17 za mwanzo katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Villarreal. João Neves, Désiré Doué na Senny Mayulu walifunga mabao matatu ndani ya kipindi cha dakika tano kabla ya Fabián Ruiz kuongeza la nne. Ruiz alifunga tena kipindi cha pili kabla ya David Boly, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza katika mashindano hayo, kukamilisha karamu ya mabao. Katika Uwanja wa Old Trafford, Manchester United ilijipata nyuma kwa mabao mawili baada ya Matías Soulé na Donyell Malen kuifungia Roma. Malen alifunga kupitia penalti. Hata hivyo, Bruno Fernandes aliipatia United bao la kwanza kupitia penalti iliyopigwa upya kabla ya Matheus Cunha kufunga mabao mawili ndani ya dakika nne na kuipa timu hiyo ushindi wa 3-2. Barcelona nayo iliilaza Aston Villa 3-0. Lamine Yamal alifungua ukurasa wa mabao dakika ya saba kabla ya Raphinha kufunga mawili kipindi cha pili, akitumia nafasi iliyotokana na shuti iliyopanguliwa na baadaye pasi ya João Cancelo. Inter Milan iliicharaza Feyenoord 3-0. Yann Bisseck alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti ya mbali kabla ya Pio Esposito kuongeza la pili kwa kichwa kutokana na krosi ya Djed Spence. Piotr Zielinski alikamilisha ushindi huo kwa shuti kali ya mbali kipindi cha pili. Katika mechi nyingine, Galatasaray iliilaza Stuttgart 2-0 kupitia mabao mawili ya Aleksei Batrakov. Sporting CP iliishinda Shakhtar Donetsk 1-0 kupitia Issa Doumbia. LASK nayo iliichapa Slovan Bratislava 4-0 ambapo Kasper Jørgensen alifunga mawili, Robert Ljubičić akaongeza la tatu na Samuel Adeniran akafunga la nne. Bodø/Glimt na Lille zilitoka sare ya 0-0. PSG inaongoza msimamo kwa alama 12, huku Barcelona na Aston Villa zikiwa miongoni mwa timu sita zilizo na pointi tisa. Kabla ya mechi hizo, viwanja mbalimbali barani Ulaya vilikaa kimya kwa dakika moja kuomboleza kifo cha mchezaji wa Tenerife, Jesus de Miguel, aliyefariki dunia Jumanne. Ratiba ya Europa League: Milan v Ferencavaros (20.45pm) Palace v Hoffenheim (20.45pm) Sparta Braha v Bournemouth (20.45pm) NEC v Omonio (20.45pm) Anderlecht v RB Salzburg (20.45pm) Real Sociedad v OL (20.45pm) Levski Sofia v Jagiellonia (20.45pm) Torreen v Ararat-Armenia (23.00pm) Celtic v Besikitas (23.00pm) Sturm Graz v Celjie (23.00pm) H-Beersh-Sheva v OFI (23.00pm) AZ v Juventus (23.00pm) Leverkusen v Marsaille (23.00pm) Benfica v Lech Poznari (23.00pm)

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 04 Nov 2026 14:54:48

Wapigakura wampa Trump kipigo kikali kwa kupuuza uchumi, kuzua vita Iran na bei ghali ya bidhaa

WASHINGTON DC, AMERIKA: CHAMA cha Democrats kimefanikiwa kunyakua udhibiti wa mabunge yote mawili ya Marekani, baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Jumanne, Novemba 3, 2026, katika matokeo yanayochukuliwa kuwa pigo kubwa la kisiasa kwa Rais Donald Trump na chama chake cha Republican. Ushindi huo unamaanisha kuwa Wanademocrats watakuwa na udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa pili wa utawala wa Trump, unaotarajiwa kukamilika Januari 2029. [caption id="attachment_193611" align="alignnone" width="2560"] Abdul El-Sayed, aliyechaguliwa kuwa Mwislamu wa kwanza kuingia Seneti Amerika baada ya uchaguzi uliofanyika Jumanne. Picha|Reuters[/caption] Matokeo hayo yanaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Marekani, ambapo wapigakura wameonyesha kutoridhishwa na namna serikali ya Trump inavyoshughulikia masuala muhimu yanayowahusu raia, ikiwemo kupanda kwa gharama ya maisha, vita vya Iran, ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na madai ya ufisadi serikalini. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya Marekani, chama cha Democratic kilipata viti kadhaa vya Seneti kutoka kwa Republican katika majimbo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa ngome za chama hicho tawala. Miongoni mwa majimbo hayo ni Texas, Iowa, Kansas, Ohio, Maine, North Carolina na South Carolina. Katika jimbo la Texas, Wanademocrats walipata ushindi muhimu katika kinyang'anyiro cha Seneti, huku James Talarico akimshinda mgombea wa Republican Ken Paxton. Ushindi huo ni muhimu kwa chama hicho kwa sababu Texas imekuwa ikiegemea Republican katika uchaguzi wa kitaifa kwa muda mrefu. Vilevile, katika jimbo la Maine, mgombea wa Democratic Troy Jackson alimshinda Seneta Susan Collins wa Republican, aliyekuwa akitetea kiti chake baada ya kuhudumu kwa mihula mitano. Huko Kansas, Wanademocrats walipata ushindi wa kihistoria kwa kuchaguliwa kwa seneta wao wa kwanza katika kipindi cha karibu karne moja. Katika Bunge la Wawakilishi, Wanademocrats pia walipata mafanikio makubwa kwa kunyakua zaidi ya viti 24 kutoka kwa Republican. Ushindi huo uliwasaidia kurejesha udhibiti wa asasi hiyo ya kutunga sheria, ambayo ina jukumu muhimu katika kupitisha miswada ya matumizi ya serikali, bajeti na sheria nyingine za kitaifa. Matokeo ya uchaguzi huo pia yalionyesha mabadiliko katika uongozi wa majimbo. Wagombea wa Democratic walishinda nyadhifa za ugavana katika majimbo kadhaa yaliyokuwa yakiongozwa na Republican, yakiwemo Georgia, Ohio, Iowa na Texas. Kwa jumla, chama hicho kinatarajiwa kudhibiti nyadhifa nyingi zaidi za magavana kuliko wapinzani wake, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010. Ushindi wa Wanademokrasia umehusishwa kwa kiasi kikubwa na kutoridhika kwa wapigakura kuhusu hali ya uchumi. Gharama za bidhaa na huduma zimekuwa mojawapo ya masuala makuu katika kampeni, huku wapinzani wa Trump wakilaumu sera za serikali yake kwa kushindwa kupunguza mzigo wa maisha kwa Wamarekani. Vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran pia vilichangia mjadala wa uchaguzi. Baadhi ya wapigakura walionyesha wasiwasi kuhusu gharama za vita hivyo na athari zake kwa usalama wa taifa na uchumi. Suala la ushuru wa bidhaa kutoka nje na madai ya ufisadi katika utawala wa Trump pia lilitajwa miongoni mwa mambo yaliyoathiri maamuzi ya wapigakura. Kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanywa na Associated Press, wapigakura wengi walitaka Bunge litumie mamlaka yake kuhakikisha kuwa rais hawajibiki kwa maamuzi yake bila kukaguliwa. Takribani asilimia 70 ya waliohojiwa walisema Bunge halikuwa likifanya vya kutosha kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka ya urais. Hata hivyo, Trump amepunguza uzito wa kushindwa kwa chama chake, akisema kuwa yeye mwenyewe hakuwa mgombea katika uchaguzi huo. Pia alilaumu baadhi ya wagombea wa Republican kwa kutofanya kampeni nzuri na kutetea sera zake. Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa utawala wa Trump katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake. Kwa kuwa chama cha Democratic kitakuwa na udhibiti wa mabunge yote mawili, kitapata uwezo mkubwa wa kuzuia miswada inayoungwa mkono na rais, kukataa baadhi ya wateule wake katika nyadhifa za serikali na kuanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za utawala wake. Hata hivyo, ushindi huo hauondoi mamlaka ya rais kutekeleza baadhi ya sera zake kupitia mamlaka ya kiutendaji. Trump pia ana uwezo wa kupinga miswada inayopitishwa na Bunge kwa kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu (veto), hivyo huenda kukazuka mvutano mkubwa kati ya Ikulu ya White House na Bunge. Uchaguzi wa katikati ya muhula hufanyika kila baada ya miaka miwili, katikati ya kipindi cha miaka minne cha rais. Kwa kawaida, uchaguzi huo hutumiwa na wapigakura kutathmini utendaji wa rais na chama chake, huku viti vyote vya Baraza la Wawakilishi na takribani theluthi moja ya Seneti vikiwania. Kwa ushindi huu, Wanademokrasia sasa wana nafasi ya kuimarisha usimamizi wa serikali ya Trump na kuathiri mwelekeo wa sera za Marekani hadi uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2028.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 04 Nov 2026 13:43:11

Mchango wa siasa katika kueneza Kiswahili kupitia kauli mbiu 'Skiza Wakenya,' 'Usawa ni Sawa,' na 'Linda Mwananchi'

MATUMIZI mbalimbali ya lugha yamethibitisha kwamba katika siasa za Kenya, mbali na mawasiliano, lugha ni nyenzo muhimu ya ushawishi na uhamasishaji. Wanasiasa huitumia kueleza sera zao, kujenga taswira zao na kuwavutia wapigakura. Kiswahili kimekuwa chombo muhimu katika kuendeleza mambo hayo. Kwa mfano, kinatumiwa katika kauli mbiu za vyama vingi, hata pale ambapo majina ya vyama hivyo ni ya Kiingereza. Kwa mfano chama cha The National Alliance (TNA) kilitumia kauli mbiu "Kazi Iendelee", Democratic Citizens Party (DCP) kinatumia "Skiza Wakenya", The Clean Alliance Party of Kenya (CAP-K) nacho kinatumia "Maisha Mapya, Uongozi Mpya", The Equitable Party kina kauli mbiu "Tusawazishe", People's Party of Kenya hutumia "Sauti ya Wakenya", huku Mwongozo Party of Kenya kinatumia "Sote Pamoja". Kauli hizi zinaonyesha jinsi vyama vinatumia Kiswahili kuwasilisha ujumbe kwa wananchi. Aidha, zinadhihirisha kuwa lugha ni sehemu ya mkakati wa kisiasa unaolenga kujenga uhusiano kati ya chama na wapigakura. Uamuzi wa kutumia Kiswahili badala ya Kiingereza au lugha za jamii unaeleweka tunapozingatia nafasi yake nchini. Ni lugha ya taifa na mojawapo ya lugha rasmi inayowaunganisha wananchi wa makabila, maeneo na matabaka mbalimbali. Hivyo basi, mwanasiasa anayekitumia ana nafasi ya kufikisha ujumbe wake kwa hadhira pana zaidi. Hili ni muhimu hasa wakati wa kampeni, ambapo viongozi huwasiliana na watu wenye tofauti za kiisimu na kitamaduni. Faida ya Kiswahili katika siasa haiishii kwenye kura, kwani wanasiasa wanakieneza kila wanapokitumia. Wanakuwa pia mabalozi wa lugha hii wanapoizungumza katika mikutano ya hadhara, mijadala ya kisiasa, mahojiano ya vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali. Wanapozunguka nchini kuuza sera zao, wanakieneza Kiswahili na kukifanya sehemu ya mawasiliano ya kila siku. Kwa njia hii, siasa huipa lugha hii nafasi ya kusikika na kutumiwa na watu wengi katika mazingira tofauti. Uwezo Zaidi ya hayo, Kiswahili kina uwezo wa kisanaa unaowawezesha wanasiasa kubeba mawazo mapana kwa maneno machache. "Kazi Iendelee", "Sote Pamoja" "Mbele Pamoja" na "Maisha Mapya, Uongozi Mpya" ni kauli fupi, rahisi kukumbuka na rahisi kurudiwa zinazosheheni taarifa muhimu kwa umma. Kauli za hivi karibuni kama "Usawa ni Sawa," "Linda Mwananchi" na "Linda Ground" nazo zinaonyesha jinsi maneno ya Kiswahili yanavyoweza kubeba ujumbe wa kijamii na kisiasa kutegemea muktadha. Maneno kama usawa, haki na mwananchi yanagusa hisia na kuibua mijadala kuhusu masuala yanayowahusu raia. Matumizi haya yanakipa Kiswahili nafasi katika mijadala ya kitaifa na kuifanya iwe hai na ambayo inatumika kueleza masuala ya uongozi, uchumi na maendeleo. Pia, yanaondoa lugha hii katika mtazamo ambao unahusu mazungumzo ya kawaida pekee, na kuisawiri kuwa inaweza kubeba hoja nzito za kisiasa na kijamii. Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha matumizi ya lugha na utekelezaji wa sera. Kauli mbiu inaweza kuvutia wananchi, lakini haithibitishi kikamilifu kuwa ahadi zitatekelezwa. Wananchi wanapaswa kuchunguza sera, mipango na matokeo ya viongozi. Kwa hakika, wanasiasa wana nafasi muhimu katika kueneza Kiswahili nchini. Wanapokitumia kuwasilisha sera na kuwasiliana na wananchi, wanakuwa sehemu ya juhudi za kukikuza na kukipa nafasi katika ramani ya kitaifa na kimataifa. Kila jukwaa la kisiasa linalotumia Kiswahili ni fursa ya kukitangaza na kukieneza. Wanasiasa wanabeba bendera ya Kiswahili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 04 Nov 2026 11:28:11

Korti yampa Mbunge wa Mosop Abraham Kirwa siku 5 kueleza kwa nini kiti chake kisitangazwe kuwa wazi

MBUNGE wa Mosop Abraham Kirwa amepewa siku tano kueleza sababu za kutohudhuria vikao vya Bunge kwa zaidi ya miaka miwili, katika kesi inayolenga kiti chake kitangazwe kuwa wazi. Jaji Roselyne Aburili wa Mahakama Kuu aliruhusu Kirwa na Spika wa Bunge la Kitaifa kujibu madai ya mpigakura Timothy Tororey kwamba wakazi wa Mosop wameachwa bila uwakilishi wa kutosha. Jaji aliagiza mbunge huyo na Spika kuwasilisha majibu na hoja zao za maandishi ndani ya siku tano kuanzia Novemba 2, 2026. Tororey naye amepewa siku tano baada ya kupokea majibu hayo kuwasilisha stakabadhi na hoja za ziada. Tororey, mkazi na mpigakura wa Mosop, anadai Kirwa amekuwa nje ya nchi kwa muda mrefu na kukosa vikao na shughuli rasmi za Bunge. Anasema hali hiyo imewanyima wakazi nafasi ya kuwakilishwa katika mijadala, kupiga kura na maamuzi kuhusu matumizi ya rasilimali za taifa. Pia anamlaumu Spika kwa kushindwa kuchukua hatua, akisema sheria inaruhusu kiti cha mbunge kutangazwa wazi iwapo atakosa vikao vinane mfululizo bila ruhusa. Hata hivyo, Spika kupitia Karani wa Bunge Samuel Njoroge alisema Kirwa alipata ruhusa ya kutohudhuria vikao kwa sababu za kiafya ili kupata matibabu nje ya nchi. Kirwa pia alisema alikuwa akisafiri kutafuta matibabu na alikuwa amepata idhini ya Spika. Alidai hakuwahi kupewa rasmi stakabadhi za kesi hiyo, bali aliifahamu kupitia Bunge. Akikubali ombi lao Jaji Aburili alisema suala hilo linaweza kuathiri hatima ya mbunge aliyechaguliwa na wananchi, hivyo ni muhimu asikilizwe kabla ya uamuzi wa mwisho. "Maamuzi yanayoombwa yanaweza kuathiri muda wa kuhudumu kwa mbunge aliyechaguliwa na, kwa upana zaidi, wapigakura anaowawakilisha," alisema.

read more