T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

ODM sasa yaelekeza shoka kwa Osotsi Seneti baada ya 'kummaliza' Sifuna

CHAMA cha ODM sasa kinapanga kumng'oa Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi katika wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Kaunti na Hazina Maalum ya Seneti (CPIC), wiki moja tu baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuondolewa kama Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti. Taarifa zinaonyesha kuwa maseneta walioteuliwa wanaohudumu katika kamati hiyo wanashinikizwa na viongozi wa ODM pamoja na chama tawala cha UDA kutia saini hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wa Bw Osotsi ili kuharakisha kuondolewa kwake. Vyanzo ndani ya ODM vimesema chama hicho kinapanga kumweka Seneta wa Taita Taveta Johnes Mwaruma katika nafasi yake. Kamati hiyo ilipanga kufanya kikao jana jioni kujadili mabadiliko hayo, lakini kikao hicho hakikuwa kimefanyika kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii. Kamati ya CPIC inaongozwa na Bw Osotsi huku Seneta wa Migori Eddy Oketch akiwa makamu mwenyekiti. Wanachama wengine ni Peris Tobiko, Raphael Chimera, George Mbugua, William Kisang, Agnes Muthama, Beth Syengo na Hamida Kibwana. Bw Osotsi alithibitisha kufahamu mpango huo lakini akasema ni "wa kisiasa" unaolenga viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi, unaompinga Rais William Ruto. "Huu ni hila ya kisiasa inayoratibiwa na Oburu Oginga pamoja na Rais Ruto. Kamati hii imefanya kazi kubwa kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu. Hakuna msingi wa kuniondoa kwa madai ya utendakazi duni," alisema. Alisema kamati hiyo imechangia kuboresha usimamizi wa fedha za kaunti na kampuni za maji nchini na kwamba mpango wa kumng'oa unafanana na ule uliomuondoa kama naibu mwenyekiti wa ODM. Bw Osotsi ni miongoni mwa viongozi wa mrengo wa Linda Mwananchi unaojumuisha Seneta Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, ambao wanapinga azma ya Rais Ruto kutafuta muhula wa pili mwaka wa 2027. Katika miezi ya hivi majuzi, mrengo wa Kiongozi wa ODM Oburu Oginga umekuwa ikiwashinikiza viongozi hao kuondolewa katika nyadhifa mbalimbali za chama na Bunge. Mnamo Machi 27, 2026, Bw Osotsi aliondolewa kama mmoja wa manaibu viongozi wa ODM wakati wa Mkutano Maalum wa Wajumbe wa Kitaifa.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Sonko afufua madai dhidi ya Mahakama ya Juu

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko ameanzisha tena mashambulizi dhidi ya Mahakama ya Juu, akihoji jinsi ilivyoshughulikia rufaa yake kuhusu kung'olewa madarakani na kudokeza kuwa anajiandaa kuwasilisha ombi jipya la mapitio ya uamuzi huo akitegemea kile alichokitaja kuwa ushahidi mpya na wa kushawishi. Katika taarifa ya kina aliyoitoa Alhamisi, Sonko alihoji kwa nini Mahakama ya Juu sasa inataka ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kuhusu iwapo afisa wa umma aliyeng'olewa madarakani anaweza kugombea uchaguzi wakati rufaa yake bado inaendelea, ilhali mahakama hiyo tayari ilitoa msimamo kuhusu suala hilo katika kesi yake. "Swali langu kwa Mahakama ya Juu, hasa kwa Jaji Mkuu, ni hili: Kwa nini iombe ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kuhusu iwapo maafisa wa umma waliotimuliwa wanaweza kugombea uchaguzi wakati kesi zao bado zinaendelea, ilhali Mahakama ya Juu tayari ilitoa uamuzi kuhusu kung'olewa kwangu? Zaidi ya hayo, kwa nini itafute ushauri huo ilhali Jaji Mkuu alikuwa tayari amesema hadharani, siku chache kabla ya hukumu ya rufaa yangu, kwamba gavana aking'olewa hubaki ameng'olewa?" alihoji Sonko. Sonko pia alirejelea matukio yaliyotangulia uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Julai 2022 uliothibitisha kuondolewa kwake madarakani. Alidai kuwa  Jaji Mkuu Martha Koome alisema hadharani, wakati rufaa yake bado ilikuwa ikiendelea, kwamba gavana aking'olewa hubaki ameng'olewa. Kwa mujibu wa Sonko, aliwasilisha ombi rasmi akimtaka Jaji Mkuu ajiondoe katika kesi hiyo kwa madai kuwa kauli hizo zilionyesha upendeleo, lakini ombi lake lilikataliwa. "Wakati rufaa yangu ilikuwa bado inasikilizwa Mahakama ya Juu, Jaji Mkuu alisema katika mahojiano na Spice FM kwamba gavana aking'olewa hubaki ameng'olewa. Kwa kuwa kesi ilikuwa bado haijaamuliwa, niliona kauli hizo zilitoa taswira kwamba uamuzi ulikuwa tayari umefikiwa. Niliandika nikitaka ajiondoe katika kesi hiyo lakini alikataa na akaendelea kushiriki katika kutoa hukumu. Hilo linanifanya niulize: Je, uamuzi kuhusu rufaa yangu ulikuwa tayari umeamuliwa?" alisema. Pia alihoji msururu wa matukio yaliyoishia na hukumu ya Mahakama ya Juu. Alisema kuwa mnamo Julai 13, 2022, Mahakama Kuu ya Mombasa iliamua kwamba kwa kuwa rufaa yake Mahakama ya Juu ilikuwa bado haijakamilika, alikuwa hajamaliza njia zote za kisheria na hivyo alikuwa na haki ya kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kugombea ugavana wa Mombasa. Hata hivyo, Sonko alisema Mahakama ya Juu ilimwagiza kuwasilisha hoja zake ndani ya saa chache akiwa bado katika Mahakama Kuu ya Mombasa, ikasikiliza kesi hiyo  Julai 14 na kutupilia mbali rufaa yake Julai 15. "Kinachonisumbua zaidi ni kilichotokea Julai 13. Nilipokuwa Mahakama Kuu ya Mombasa siku nzima, Mahakama ya Juu ilitoa maagizo kwamba niwasilishe hoja katika rufaa yangu ifikapo Julai 14. Mawakili wangu walieleza mahakama kwamba tulikuwa katika kesi nyingine na tukaomba muda unaotolewa kwa kawaida chini ya taratibu za mahakama. Ingawa mahakama ilikiri kulikuwa na hitilafu katika muda uliowekwa, bado iliendelea na kesi hiyo," alisema. Sonko alisisitiza kuwa kung'olewa kwake kulichochewa kisiasa. Alidai kuwa baadhi ya waliowasilisha na kuunga mkono hoja ya kumwondoa madarakani baadaye walijitenga nayo hadharani na kudai walifanya hivyo chini ya shinikizo. Kwa maoni yake, matukio hayo yanazua maswali mapya kuhusu uadilifu wa mchakato mzima wa kumng'oa madarakani. Pia alinukuu uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), akisema mahakama hiyo ilibaini mapungufu ya kiutaratibu katika jinsi kesi yake ilivyoshughulikiwa. Kwa mujibu wa Sonko, mahakama hiyo ya kikanda iliamua kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa zilikiuka haki yake ya kupata kesi ya haki chini ya Katiba ya Kenya na hazikuendana na misingi ya utawala bora, utawala wa sheria na uwajibikaji iliyoainishwa katika Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sonko alisema masuala anayoyaibua hayahusu kesi yake pekee, bali yanagusa uhuru wa mahakama, uwazi na imani ya wananchi kwa mfumo wa haki. "Maswali yangu kwa Mahakama ya Juu ni rahisi. Kwa nini kauli  zilitolew hadharani kuhusu kesi iliyokuwa bado mahakamani? Kwa nini ombi langu la Jaji Mkuu kujiondoa lilikataliwa? Kwa nini nilipewa saa chache tu kuwasilisha hoja badala ya muda wa kawaida? Kwa nini kulikuwa na haraka ya kumaliza rufaa yangu wakati suala la kustahili kwangu kugombea ugavana wa Mombasa lilikuwa bado linashughulikiwa na mahakama nyingine? Na sasa kwa nini Mwanasheria Mkuu anaombwa kutoa ushauri kuhusu jambo ambalo Mahakama ya Juu tayari iliamua katika kesi yangu?" alihoji. .

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Dalili za maambukizi ya matumbwitumbwi yaani 'mumps' miongoni mwa watoto

SIKU chache zilizopita, baadhi ya shule jijini Nairobi zilionya wazazi kuhusu visa vinavyoshukiwa kuwa vya matumbwitumbwi (mumps), ugonjwa unaoambukiza na kuenea kwa urahisi miongoni mwa watoto. Tahadhari hizo zimezua wasiwasi miongoni mwa wazazi huku shule zikiwataka kufuatilia watoto wao kwa dalili kama homa, uchovu na kuvimba kwa tezi za kutengeneza mate kwenye koo au chini na mbele ya masikio. Dkt Varsha Vekaria-Hirani, daktari bingwa wa watoto, anaeleza kuwa mazingira ya shule yanaweza kuchangia kuenea kwa ugonjwa huo kwa sababu ya msongamano wa wanafunzi, ukaribu wa watoto na tabia ya kushirikiana chakula na chupa za maji. Matumbwitumbwi ni maambukizi ya virusi yanayoathiri tezi za kutengeneza mate (parotid glands), almaarufu kama findofindo zinazopatikana kwenye koo na mbele ya masikio na ambazo hutoa mate wakati mtu anapotafuna chakula. "Matumbwitumbwi husababishwa na virusi ambavyo huenea sana hasa pale ambapo kuna msongamano. Kwa kawaida mlipuko wake huwa ya msimu," anaeleza Dkt Vekaria-Hirani. Anasema ugonjwa huo huenea kupitia matone ya hewa yanayotolewa na mtu aliyeambukizwa anapokohoa au kupiga chafya. Mtu aliyeambukizwa anaweza pia kueneza virusi hivyo kupitia mate. "Msongamano wa wanafunzi madarasani na watoto kushirikiana chakula au chupa za maji shuleni huenda zikachangia kuenea kwa matumbwitumbwi," alisema. Hata hivyo, hakuna data rasmi ya kitaifa inayoonyesha ongezeko la visa vya matumbwitumbwi nchini. Dkt Vekaria-Hirani anaeleza kuwa ingawa visa vimeripotiwa na baadhi ya shule, hasa Nairobi, na wahudumu wa afya wamekuwa wakiwaona watoto wenye ugonjwa huo mara kwa mara, takwimu rasmi za kitaifa hazipatikani.Mombasa pia imetajwa miongoni mwa maeneo ambako visa vimeripotiwa. "Kwa sasa hakuna data rasmi ya kitaifa, lakini baadhi ya shule zimeripoti ongezeko la visa na sisi kama wahudumu wa afya tumekuwa tukiwaona watoto wenye matumbwitumbwi mara kwa mara," alisema. Watoto walio chini ya miaka 15, hasa wanaokwenda shule, wanaonekana kuwa miongoni mwa walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Dalili za awali Dkt Vekaria-Hirani anaeleza kuwa matumbwitumbwi huanza kwa dalili zinazoweza kufanana na mafua au maambukizi mengine ya virusi. Katika siku tatu au nne za kwanza, mtoto anaweza kupata homa, udhaifu, maumivu ya misuli, uchovu na kukosa hamu ya kula. Baadaye, tezi ya kuunda mate inaweza kuanza kuvimba upande mmoja au pande zote mbili. Uvimbe huo kwa kawaida huambatana na maumivu ambayo huongezeka mtoto anapotafuna chakula. Vyakula vyenye uchachu vinaweza kufanya maumivu kuwa makali zaidi kwa sababu huchochea uzalishaji wa mate. "Wazazi wanapaswa kuangalia homa, uchovu, kukosa hamu ya kula na baadaye uvimbe wenye maumivu chini au mbele ya masikio," alisema. Hata hivyo, si kila uvimbe katika eneo hilo ni matumbwitumbwi. Maambukizi ya koo kama tonsils na pharyngitis yanaweza pia kusababisha kuvimba kwa tezi hizo. Kinachofanya matumbwitumbwi kuwa vigumu kudhibiti ni kwamba mtoto anaweza kuwaambukiza wengine kabla ya wazazi kutambua kuwa ana ugonjwa huo. Dkt Vekaria-Hirani anasema mtu aliyeambukizwa anaweza kuanza kueneza virusi siku moja au mbili kabla ya kuvimba kwa tezi za kutengeneza mate. Mtoto anaweza kuendelea kuwa mwenye uwezo wa kuambukiza wengine kwa takriban siku tano baada ya kuanza kwa uvimbe. Hii ina maana kuwa mtoto anaweza kwenda shuleni akiwa na homa kidogo, uchovu au kukosa hamu ya kula bila wazazi kujua kuwa tayari anaweza kuwaambukiza wengine. Kipindi cha mtu kuambukizwa hadi kuanza kuonyesha dalili kinaweza kuwa kati ya wiki mbili na tatu. Dkt Vekaria-Hirani anawashauri wazazi kuwaruhusu watoto wanaoshukiwa kuwa na matumbwitumbwi kukaa nyumbani na kuepuka kuwapeleka shuleni au kutangamana na watoto wengine. Anasema mtoto anapaswa kubaki nyumbani kwa siku tano baada ya kuanza kuonyesha dalili za kuwa na findofindo kooni. Wazazi pia wanapaswa kuijulisha shule ili hatua za kuzuia maambukizi zichukuliwe. "Mtoto anapaswa kubaki nyumbani kwa siku tano, shule ijulishwe na mtoto aonekane na daktari ili achunguzwe iwapo kuna matatizo mengine," alisema. Kwa matumbwitumbwi yasiyo na madhara mengine, matibabu hulenga kudhibiti dalili kama homa na maumivu. Dkt Vekaria-Hirani alisema antibiotiki hazitibu ugonjwa huo kwa sababu unasababishwa na virusi, wala si bakteria. Ingawa watoto wengi hupona bila kupata changamoto, matumbwitumbwi yanaweza kusababisha madhara mengine. Miongoni mwa matatizo hayo ni kuvimba kwa korodani kwa wavulana, hali inayojulikana kama orchitis, na uvimbe wa ovary kwa wasichana. Ugonjwa huo pia unaweza kusababisha maambukizi au uvimbe wa ubongo, ikiwemo meningitis na encephalitis. Baadhi ya wagonjwa wanaweza pia kupoteza uwezo wa kusikia au kupata uvimbe wa kongosho, unaojulikana kama pancreatitis. Dkt Vekaria-Hirani anawashauri wazazi kutafuta matibabu ya haraka mtoto anapopata maumivu ya korodani, maumivu makali ya tumbo, kuchanganyikiwa, maumivu makali ya kichwa au kutapika. Dkt Vekaria-Hirani alisema chanjo dhidi ya matumbwitumbwi kwa sasa haijajumuishwa katika ratiba ya kawaida ya chanjo za KEPI nchini Kenya. Hii inamaanisha kuwa watoto wengi hawana kinga maalumu dhidi ya ugonjwa huo. Familia pia zinashauriwa kunawa mikono mara kwa mara, kutoshirikiana chakula au chupa za maji na watu wengine na kusafisha sehemu zinazoguswa mara kwa mara. Watoto wafundishwe pia kufunika mdomo wanapokohoa au kupiga chafya. Dkt Vekaria-Hirani alisema baadhi ya wazazi wanaamini kimakosa kuwa matumbwitumbwi yanahitaji antibiotiki. Wengine huamini kuwa kila mvulana au msichana anayeugua ugonjwa huo atakuwa tasa. Kwa sasa, wazazi wanahimizwa kuwa macho kwa dalili za ugonjwa huo na kutafuta ushauri wa daktari mapema ili kupunguza hatari ya maambukizi kuenea shuleni na katika jamii.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Bei ya mahindi yaanza kupanda baada ya mavuno duni Bonde la Ufa

BEI ya mahindi imepanda kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Bonde la Ufa kutokana na mavuno duni yaliyosababishwa na mvua isiyotabirika. Hali hii inazua hofu ya ongezeko zaidi la bei ya unga na kulazimu serikali kuwazia kuagiza mahindi kutoka nje ili kuzuia upungufu wa chakula. Katika Kaunti ya Nakuru, gunia la mahindi la kilo 90 sasa linauzwa kati ya Sh4,500 na Sh4,600 kutoka takriban Sh3,700 miezi miwili iliyopita, ishara ya kupungua kwa akiba katika mojawapo ya maeneo makuu yanayozalisha mahindi nchini. Katika Kaunti ya Narok, ambapo uvunaji umeanza katika sehemu za Narok Kusini, Narok Kaskazini na Narok Magharibi, gunia hilo linauzwa kati ya Sh4,000 na Sh4,600. Ongezeko hilo linajiri huku wakulima wengi katika Bonde la Ufa wakiripoti mavuno duni kutokana na kiangazi cha muda mrefu, uhaba wa mvua na magonjwa yaliyoshambulia mazao wakati wa hatua muhimu ya ukuaji. Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO) limesema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri pakubwa uzalishaji wa mahindi katika maeneo mengi. "Maeneo mengi yalipata mvua chache. Magonjwa na wadudu pia wamezidisha hali hiyo, jambo litakaloathiri uzalishaji msimu huu," alisema Mkurugenzi Mkuu wa Kalro, Dkt Patrick Ketiema, mjini Naivasha. Wakulima wengi wamepata hasara baada ya mazao kuharibika hasa katika maeneo ya Njoro, Rongai, Mauche na Elburgon, Kaunti ya Nakuru. Wakulima wa Uasin Gishu, Trans Nzoia, Nandi, Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet pia wanasema mahindi yao yalidumaa baada ya mvua kukatika wakati wa kipindi muhimu cha ukuaji. Hasara kama hiyo pia imeripotiwa katika eneo la Trans Mara, hasa maeneobunge ya Emurua Dikirr na Kilgoris. Kutokana na mavuno duni, wakulima wengi sasa wanakadiria hasara. Baadhi yao wameamua kung'oa mahindi kabla ya kukomaa ili kuandaa mashamba kupanda tena mvua ya El Niño inayotarajiwa mwezi Septemba na Oktoba ikianza. Wengine wamekata mahindi yaliyokauka na kuyatumia kama lishe ya mifugo, huku wengine wakipanda maharagwe, ambayo hukomaa kwa muda mfupi, ili kurejesha sehemu ya fedha walizowekeza. Narok, wakulima wanasema uzalishaji umepungua karibu kwa nusu. "Kwa wastani, mkulima anavuna kati ya magunia 10 na 15 kwa ekari ilhali zamani tulikuwa tukivuna kati ya magunia 20 na 27," alisema mkulima Julius Rotich wa eneo la Katakala. Aliwashutumu mabroka kwa kutumia udhaifu wa wakulima kununua mahindi moja kwa moja mashambani kwa bei ya kati ya Sh3,500 na Sh3,700 kwa gunia, licha ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kutoa bei ya Sh4,000.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Mpiga mbizi hodari ambaye ameokoa maisha ya wengi baharini kwa miaka 32

BW Mohamed Salim Ahmed ni mpiga mbizi mashuhuri ambaye ametumia sehemu kubwa ya maisha yake kuitumikia jamii, taifa na mataifa ya nje. Hata hivyo, mchango wake kwa jamii haujatambuliwa rasmi. Bw Salim, 52, kutoka Majengo, eneobunge la Mvita, kaunti ya Mombasa, tangu akiwa kijana amekuwa akihatarisha maisha yake katika kuokoa maisha na hata kuopoa miili ya wale wanaokufa baharini. Alikuwa kwenye kikosi cha wapiga mbizi waliojitolea kuokoa maisha, kusaka na kuopoa miili ya mamia ya wasafiri waliozama baharini kwenye mkasa wa Feri ya MV Mtongwe mwaka wa 1994. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 272. Wakati huo Bw Salim alikuwa akifanya kazi na kampuni ya wapigambizi ya Divecon. "Mimi na wapiga mbizi wenzangu wapatao 14 tulifikishwa haraka kwenye eneo la mkasa. Nilikuwa mstari wa mbele kupiga mbizi tukisaka watu na kuwaokoa na pia kuiopoa miili ya wale ambao tayari walikuwa wameangamia," akasema Bw Salim. Shughuli hiyo ilichukuwa karibu siku saba mfululizo, usiku na mchana. [caption id="attachment_190448" align="alignnone" width="2560"] Salim Mohamed Ahmed, 52, ambaye alikuwa miongoni mwa walioshughulikia waathiriwa wa ajali ya MV Mtongwe mnamo 1994. PICHA|KEVIN ODIT[/caption] Mbali na Mtongwe, Bw Salim amewahi kuiwakilisha Kenya katika shughuli ya kutafuta manusura na kuopoa miili ya waliofariki kwenye majanga ya feri na meli nchi jirani za Tanzania, Zanzibar, Madagascar na kwingineko. Anakumbuka Mei 21, 1996, wakati huo akifanya kazi na jeshi la wanamaji la Kenya kama mpiga mbizi ambapo walitumwa eneo la Mwanza, Tanzania. Hii ni baada ya ajali ya Meli ya MV Bukoba kutokea katika Ziwa Victoria, hatua chache kabla ya kufika bandari ya Mwanza. Meli hiyo, iliyokuwa ikitokea Bukoba, ilizama na kusababisha vifo vya watu karibu 1000 katika moja ya majanga mabaya zaidi ya usafiri wa majini kuwahi kutokea nchini Tanzania na Bara zima la Afrika kwa jumla. Uzito wa janga hilo ulilemea nchi ya Tanzania, hali iliyomlazimu Rais Benjamin Mkapa kwa wakati huo kuitisha msaada wa wanamaji na wapiga mbizi kusaidia kwenye shughuli za uokoaji na utafutaji. Bw Salim pia alikuwa miongoni mwa wapiga mbizi wataalamu waliofika Mwanza, Tanzania kutoa msaada wa kiufundi. "Tulishirikiana na wenzetu kutoka Tanzania na Afrika Kusini kutafuta na kuopoa miili ya mamia ya abiria waliopoteza maisha," akasema Bw Salim. Anakiri kuwepo kwa mazingira magumu na changamoto tele zilizokumba shughuli hiyo. "Meli yenyewe ilikuwa imezama umbali wa mita kadhaa ndani ya ziwa. Meli yenyewe ilikuwa na daraja la kwanza, la pili na la tatu. Wengi wa waathiriwa walikuwa wamejifungia ndani kabisa ya vyumba vya daraja la tatu, hivyo ilitulazimu kukata vyuma,kuingia ndani na kuopoa miili," akaeleza Bw Salim. Bw Salim anasema kuwa licha ya kutekeleza majukumu hayo mazito na ya kishujaa, serikali bado haijamtambua kwa lolote. "Mara nyingi nimekaa kujiuliza kwani serikali inakosa shukrani? Najivunia kutekeleza majukumu ya kishujaa miaka yote ila hakuna utambuzi rasmi hadi sasa," akasema Bw Salim. Bw Salim kwa sasa anafanya kazi kama Afisa wa Divisheni wa Masuala ya Majanga chini ya serikali ya kaunti ya Mombasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Murkomen atetea polisi kuhusu uhuni: 'Kenya iko salama kuliko wakati mwingine wowote ule'

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametetea uongozi wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi huku maswali yakiendelea kuibuka kuhusu kuenea kwa ghasia katika uchaguzi mdogo eneo bunge la Ol Kalou wiki iliyopita. Kauli yake inajiri licha ya kuagiza uchunguzi baada ya uchaguzi huo uliogubikwa na vurugu, ambapo watu waliokuwa wamejifunika nyuso walidaiwa kuwashambulia wakazi na hata kuwafyatulia risasi maafisa wa polisi waliokuwa kazini. Akizungumza Alhamisi wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kisasa wa Kutambua Alama (MBIS) katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Bw Murkomen alisema ana imani kamili na uongozi wa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na kuwataka maafisa wa DCI kukabiliana vikali na magenge ya wahalifu. "Heshima yangu kwa Inspekta Jenerali ni kubwa. Nina imani kamili na uongozi wake. Aliteuliwa na Rais, akathibitishwa na Bunge na tangu ashike wadhifa huo ametekeleza majukumu yake kwa heshima na utaalamu," alisema. Hata hivyo, hakueleza kwa nini hadi sasa hakuna mshukiwa aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani, wiki moja baada ya watu wenye silaha kuzua hofu Ol Kalou, kuwaua watu wawili na kuvuruga uchaguzi huo. Tukio hilo lilirekodiwa kwa picha na video zilizokuwa zikisambazwa mitandaoni, huku nambari za usajili za baadhi ya magari yaliyodaiwa kutumiwa na washambuliaji pia zikichapishwa. Bw Murkomen alisisitiza kuwa hali ya usalama nchini imeimarika kwa kiasi kikubwa. "Kenya iko salama kuliko wakati mwingine wowote. Mashambulizi, ujambazi, ugaidi, wizi na uhalifu vimepungua. Takwimu zinajieleza zenyewe," alisema. Kauli hiyo imeibua mjadala huku serikali ikikosolewa kwa kujivuta kuhusu uchunguzi wa ghasia za Ol Kalou ambapo magenge yalishambulia wananchi, wanahabari na wafuasi wa wanasiasa hadharani. Ingawa mapema wiki hii Rais William Ruto aliagiza maafisa wa usalama kuwakamata wahalifu na kukomesha magenge ya wahuni, hakuna washukiwa wa ghasia hizo waliotangazwa kukamatwa rasmi. Badala yake, Bw Murkomen aliwahakikishia maafisa wa DCI kuwa serikali inaunga mkono juhudi zao za kupambana na wahalifu. "DCI, tunawaunga mkono. Shughulikieni wahalifu hawa bila kuyumba. Sasa mna teknolojia ya kisasa ya kuwatambua," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Gachagua kuwinda ngome ya Kindiki baada ya Ol Kalou kumweka roho juu

SIKU chache baada ya kupata ushindi katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou, aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua sasa ameelekeza juhudi zake Mlima Kenya Mashariki katika kile wachambuzi wa siasa wanasema ni mkakati wa kupanua ushawishi wake tayari kwa uchaguzi mkuu wa 2027. Baada ya mgombea wa chama chake cha DCP, Sammy Waweru, kushinda kwa kishindo uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Bw Gachagua anaamini tayari amejijengea msingi imara katika Mlima Kenya Magharibi. Sasa analenga kuzima ushawishi wa Prof Kindiki katika kaunti za Meru, Embu na Tharaka Nithi, ambazo zimeendelea kuwa ngome muhimu ya Kenya Kwanza. Katika juhudi hizo, Bw Gachagua ametangaza ziara ya siku sita katika kaunti za Meru na Embu, hatua inayotajwa kuwa kubwa zaidi ya kisiasa katika eneo linalohusishwa na Prof Kindiki. Hatua hiyo imejiri siku chache baada ya Bw Gachagua kumtetea hadharani Prof Kindiki dhidi ya viongozi wa Kenya Kwanza wanaotaka kugawa Mlima Kenya katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Aliwataka wafuasi wake wasimshambulie binafsi Naibu Rais, akisisitiza kuwa Mlima Kenya unapaswa kubaki na umoja wa kisiasa. Hata hivyo, wachambuzi wanasema msimamo huo si wa maridhiano bali ni mkakati wa kutuliza hali ya kisiasa kabla ya kuanza kampeni katika Mlima Kenya Mashariki. Mchambuzi wa siasa John Anditi alisema Bw Gachagua anataka kuwavutia wapigakura wa Mashariki kabla ya Prof Kindiki kuimarisha zaidi ushawishi wake. "Anajaribu kujionyesha kama mtetezi wa umoja wa Mlima Kenya huku akizuia eneo hilo kugeuka ngome ya UDA pekee," alisema. Matokeo ya chaguzi ndogo yameonyesha mgawanyiko wa kisiasa katika eneo hilo. Huku DCP ikishinda Ol Kalou, UDA ilitwaa kiti cha ubunge cha Mbeere Kaskazini na viti vya wadi za Evurore na Muminji mwaka jana, hali iliyofasiriwa kama ushahidi kuwa Prof Kindiki bado ana ushawishi mkubwa Mashariki. Kutokana na hali hiyo, Mlima Kenya sasa umegawanyika katika mirengo miwili ya kisiasa. Mlima Kenya Magharibi, unaojumuisha Nyeri, Nyandarua, Murang'a, Kiambu na sehemu za Nakuru, unaonekana kuegemea upande wa Bw Gachagua. Mashariki, inaohusisha Meru, Embu na Tharaka Nithi ndiko Prof Kindiki anaongoza uimarishaji wa ufuasi wa Kenya Kwanza. Kwa Rais Ruto, hali hiyo inaleta changamoto na fursa kwa wakati mmoja. Ingawa Prof Kindiki amezuia kuporomoka kwa uungwaji wa UDA katika Mlima Kenya Mashariki, ushawishi wa Bw Gachagua Magharibi unatishia muungano uliomuingiza Dkt Ruto mamlakani mwaka wa 2022. Wakili Nelson Osiemo alisema hatua ya Bw Gachagua inalenga kuunganisha Mlima Kenya na kujijenga kama msemaji mkuu wa eneo hilo. Alisema ndiyo sababu amekuwa na mikutano na mgombea urais wa chama cha Safina Jimi Wanjigi na kuzungumza vyema kuhusu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na Prof Kindiki. Wakati huo huo, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amependekeza Mlima Kenya Mashariki ujitafutie mwelekeo wake wa kisiasa iwapo viongozi wa Magharibi hawatamuunga Prof Kindiki. Kauli hiyo imepingwa na Waziri wa Ardhi Alice Wahome, aliyesema Mlima Kenya haupaswi kugawanywa kwa misingi ya kisiasa. Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua anaamini Bw Gachagua anajijenga kama kiongozi mkuu wa kisiasa wa Mlima Kenya. "Anataka kuonekana kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuwalinda viongozi wa Mlima Kenya na kuwaunganisha," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Hofu Cameroon Rais Biya akikosa kuonekana hadharani kwa siku 45

YOUNDE, Cameroon: CHAMA tawala nchini Cameroon, CPDM (Cameroon People's Democratic Movement), Jumatano kiliitisha mkutano usio wa kawaida wa viongozi wake wakuu huku shinikizo ikiongezeka kuhusu kutoonekana hadharani kwa Rais Paul Biya, 93. Biya amekuwa nje ya nchi kwa siku 45 na uvumi umetanda kotekote kuhusu hali yake ya afya. Biya, anashikilia rekodi ya kuwa kiongozi wa taifa mwenye umri mkubwa zaidi duniani. Rais huyo aliondoka Cameroon Juni 7 kwa kile kilichoelezwa na Ikulu kuwa ziara fupi ya kibinafsi barani Ulaya. Tangu wakati huo hajarejea nyumbani, huku serikali ikikosa kutoa taarifa kuhusu tarehe anayotarajiwa kurejea. Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPDM, Jean Nkuete, aliyeitisha mkutano huo, hakufichua ajenda yake. Katika taarifa, alisema tu kuwa kitakuwa "kikao muhimu cha kazi". Haikubainika mara moja iwapo mkutano huo unahusiana na kutokuwepo kwa Biya kwa muda mrefu. Biya amekuwa madarakani tangu 1982 na kwa miaka mingi amekuwa akiishi Uswizi na mataifa mengine ya Ulaya. Hata hivyo, kutokana na umri wake mkubwa, safari zake zimeendelea kuzua maswali kuhusu afya yake, mahali aliko na uwezo wake wa kuendelea kuongoza taifa hilo. Safari ya sasa ndiyo ya muda mrefu zaidi ambayo amewahi kufanya akiwa nje ya nchi. Baada ya kutoweka kwa muda mnamo 2024, serikali ilipiga marufuku mijadala kuhusu afya ya rais huyo. Hata hivyo, hatua hiyo haijawazuia viongozi wa upinzani kuhoji hali hiyo. Mnamo Julai 18, chama cha upinzani cha Cameroon Democratic Union kilitaka mamlaka "kuwapa wananchi maelezo ya kutosha kuhusu uongozi wa taifa". Mbunge wa upinzani Jean Michel Nintcheu naye aliandika katika ukurasa wake wa Facebook Julai 17 akitaka Mahakama ya Kikatiba kutangaza kuwa nafasi ya urais i wazi. Serikali imekuwa ikikanusha ripoti kwamba Biya anapatiwa matibabu nje ya nchi, ikisisitiza kuwa ana uwezo wa kuendelea kuongoza Cameroon akiwa ughaibuni. Mnamo Aprili, wabunge waliidhinisha kurejeshwa kwa wadhifa wa makamu wa rais ambaye angekuwa wa kwanza kumrithi Biya iwapo nafasi ya urais ingebaki wazi. Hata hivyo, nafasi hiyo bado haijajazwa. Licha ya kushinda uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba mwaka jana, Biya bado hajateua baraza jipya la mawaziri akifanya kazi na wale waliokuwepo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Buyu awinda kuweka historia katika pambano la ubingwa la UBO dhidi ya Ramadhani

BONDIA wa Kenya Javan Buyu atamenyana na Mtanzania Idd Ramadhani kuwania taji la Shirika la Universal Boxing Organization (UBO) la Inter-Continental uzani wa lightweigt, katika mashindano ya ndondi yatakayofanyika Jumamosi hii kwenye ukumbi wa Edge Convention Centre jijini Nairobi. Pambano hilo ni mojawapo ya mapambano 11 yaliyoandaliwa na promota Maurice Odera kupitia UFS BXNG (Ultra Fight Series Boxing), waandalizi wakuu wa ndondi za kulipwa nchini Kenya, kwa udhamini wa SportPesa. Buyu, ambaye ni bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki, ana nafasi ya kutwaa taji lake la tatu la kulipwa na kuwa miongoni mwa mabondia wachache wa Kenya kushinda mkanda wa ngazi ya mabara. Bondia huyo amesema yuko tayari kwa mtihani huo baada ya kufanya maandalizi ya miezi mitatu bila kuacha jambo lolote kwa bahati. "Nimekuwa nikifanya mazoezi na kumuomba Mungu kwa ajili ya taji hili. Mimi na timu yangu tumefanya kazi kubwa kujiandaa kwa Julai 25 na tuko tayari. Tumeimarisha kila eneo muhimu litakalotupa ushindi," alisema Buyu. Bingwa huyo wa Kenya na wa Pugilist Syndicate of Tanzania (PST) amesema ameboresha uwezo wake wa kutembea ulingoni, kupiga mashambulizi ya kushtukiza na ngumi za mwilini ili kumzidi ujanja mpinzani wake. "Taji hili lina maana kubwa kwangu kwa sababu litawapa motisha vijana wanaoanza mchezo wa ndondi na pia litafungua milango ya kupigana kwenye majukwaa makubwa duniani," alisema. Buyu alitwaa ubingwa wa Kenya Oktoba mwaka jana baada ya kumshinda Christopher Osicho kabla ya kuongeza mkanda wa PST kwa kumcharaza Mtanzania Nasoro Madimba kwa Technical Knockout katika raundi ya tatu mapema mwaka huu. Amesema tayari amemchunguza Ramadhani kupitia video zake. "Ni bondia mzuri, ningempa alama saba kati ya 10, lakini nina kila kitu kinachohitajika kumlazimisha akate tamaa. Namwahidi pambano zuri, lakini aandae moyo wa kukubali kushindwa," alisema. Hata hivyo, Buyu alikataa kutabiri jinsi pambano hilo litakavyomalizika. "Mashabiki waje wajionee jinsi nitakavyoshinda," alisema. Aidha, aliipongeza SportPesa pamoja na UFS BXNG kwa kuendeleza ndondi za kulipwa nchini kwa kuwapa mabondia nafasi ya kupigania mataji makubwa. "Naishukuru SportPesa kwa nafasi hii. Wanasaidia kukuza ndondi nchini Kenya na kuwapa wanamichezo nafasi ya kujionyesha. Najivunia kuiwakilisha Kenya na SportPesa," alisema Buyu, ambaye amesema pia anapigania kutimiza ndoto ya marehemu babake aliyewahi kushiriki ndondi za mashuleni katika Shule ya Upili ya Maranda. Pia alimpongeza promota Maurice Odera kwa mchango wake katika kukuza mchezo huo. Kwa upande wake, Ramadhani amesema amewasili nchini kwa lengo moja tu, kutwaa mkanda huo na kurejea nao Tanzania. "Nataka Buyu ajitayarishe kwa sababu Ramadhani Idd si bondia wa mchezo," alisema. Mtanzania huyo, aliyeshinda mapambano tisa kati ya 10 ya kulipwa, anaamini Buyu hajawahi kukutana na bondia wa kiwango chake. "Buyu alipata shida dhidi ya Martin Shekevuli, lakini mimi nilimwangusha kwa knockout. Hiyo inaonyesha tofauti yetu," alisema. Ramadhani alisema kipigo chake pekee kilitokana na uamuzi wa pointi dhidi ya Mrusi Levan Kasaia nchini Poland, uzoefu ambao amesema umemjengea uwezo wa kukabiliana na pambano hilo. "Nimekuwa kambini kwa karibu miezi mitatu na kila kitu kiko sawa. Nimetumwa kuleta mkanda nyumbani na naamini nitarudi nao Tanzania," alisema. Pia aliwataka waamuzi kuhakikisha haki inatendeka. "Buyu akishinda apewe mkanda. Mimi nikishinda nipewe mkanda. Hicho ndicho ninachoomba," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Obado apatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno, akiwa mjamzito

ALIYEKUWA Gavana wa Migori Okoth Obado, amepatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno, aliyekuwa mjamzito. Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori Caspal Obiero pia walipatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi huyo. Jaji Cecilia Githua wa Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi alisema upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kuwa watatu hao walishirikiana kupanga na kutekeleza mauaji ya Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ujauzito wa wiki 28 alipouawa mwezi Septemba 2018. Mahakama ilisema Sharon alitekwa nyara, akabakwa na baadaye kuuawa ili kuzuia uhusiano wake na Obado pamoja na ujauzito wake usijulikane kwa umma. "Nimeridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa unaonyesha msururu kamili wa matukio usioacha shaka kwamba washtakiwa walishirikiana na watu wengine ambao hawako mahakamani kutekeleza mauaji hayo. Ushahidi unaonyesha wazi kwamba walisababisha kifo cha Sharon," alisema Jaji Githua. Kwa mujibu wa mahakama, Obado ndiye aliyekuwa na sababu ya kutaka Sharon auawe, akitoa fedha na kuchochea mpango huo huku Oyamo akisaidia utekelezaji wake na Obiero akitoa usaidizi wa kimipango na kusaidia kuficha uhalifu huo. Mahakama ilisema majukumu ya kila mmoja yalionyesha maandalizi ya makusudi,  ushiriki wao na juhudi za kuficha mauaji hayo. "Hivyo basi, ninapata kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu bila shaka yoyote," alisema jaji. Hukumu hiyo inahitimisha kesi iliyodumu kwa karibu miaka saba. Kesi hiyo ilichelewesha  kutokana na maombi 16 ya kisheria, kuhamishwa kwa jaji aliyekuwa akiisikiliza baada ya mashahidi 25 kutoa ushahidi, pamoja na kusimamishwa kwa kesi kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya Jaji Mkuu kuagiza isikizwe tena. Kwa jumla, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 42 kuthibitisha kesi yake. Mahakama ilitupilia mbali utetezi wa Obado kwamba alikuwa amekubali ujauzito huo na kuendelea kumsaidia Sharon kifedha. Jaji Githua alisema ingawa Obado alikiri kujua kuhusu ujauzito huo mwezi Machi 2018, baadaye alianza kumuepuka Sharon, akasitisha msaada wa kifedha na kujaribu kuzuia uhusiano wao usijulikane hadharani. "Si jambo la bahati mbaya kwamba alianza kuwa na wasiwasi mara tu ilipoonekana kuwa habari hizo zingechapishwa. Ni wazi alitaka kuzuia suala hilo lisifikie umma," alisema jaji. Mahakama ilisema Sharon alikuwa akimtaka Obado akubali hadharani kuwa mimba ilikuwa yake, amnunulie nyumba na gari, pamoja na kumtafutia kazi. Alidai kuwa angeweka wazi uhusiano wao iwapo madai hayo yasingetimizwa. Jaji alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kwamba fedha ambazo Sharon alipokea kupitia Oyamo hazikuwa za kumsaidia, bali zilikuwa sehemu ya njama za kumshawishi aachane na mpango wa kufichua siri hiyo huku maandalizi ya kumuua yakiendelea. Ushahidi wa rafiki wa karibu wa Sharon ulionyesha kuwa Obado alimpa Sh30,000 ili atoe mimba na akamwelekeza awasiliane na Oyamo kuhusu masuala yote yaliyohusu ujauzito huo. Shahidi huyo pia alisema Sharon alikuwa amemchezea rekodi za sauti za mazungumzo yake na Obado, ambapo alikuwa akimsihi asichapishe picha zao kwenye mitandao ya kijamii na kumshawishi mara kwa mara kutoa mimba akisema muda ulikuwa ukiisha. Mahakama pia ilitegemea ushahidi wa rafiki wa familia kwa jina Lawrence aliyejaribu kupatanisha wawili hao baada ya Obado kukubali kuwa alijua kuhusu ujauzito huo. Kwa mujibu wa ushahidi huo, Obado alimwahidi Sharon kuwa angemnunulia shamba na kumjengea nyumba iwapo angeacha kufichua uhusiano wao. Hata hivyo, Jaji Githua alisema ahadi hizo hazikuwa za dhati bali zilikuwa mbinu ya kununua muda huku mpango wa kumuondoa Sharon ukiendelea kutekelezwa. Kwa hukumu hiyo, watatu hao sasa wanasubiri mahakama kutangaza adhabu watakayopatiwa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwanafunzi huyo, kesi ambayo ilivuta hisia za taifa kwa miaka kadhaa. Jana, Mahakama ilifuta dhamana ya watatu hao, wakazuiliwa rumande hadi Agosti 18 kusubiri ripoti ya kabla ya kuhukumiwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 23 Jul 2026 02:55:11

Hakimu asimamishwa kazi kwa dai la kupokea hongo ili kutoa hukumu nafuu

MAAFISA wawili wa Mahakama ya Kangema, Kaunti ya Murang'a, walikamatwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa madai ya kuomba na kupokea hongo kutoka kwa mfanyabiashara aliyepatikana na hatia ili kumsaidia kupata hukumu nafuu. Wawili hao walikamatwa Jumanne mjini Kangema katika operesheni ya EACC wakidaiwa kupokea Sh150,000 kutoka kwa mlalamishi. Na huku uchunguzi ukiendelea katika ofisi za EACC Kanda ya Kati mjini Nyeri, Jaji Mkuu Martha Koome alitangaza kuwa hakimu anayehusika amesimamishwa kazi kwa muda. Bi Koome alisema madai hayo ni mazito na yakithibitishwa yatakuwa ukiukaji mkubwa wa sheria pamoja na maadili ya maafisa wa mahakama. 'Mahakama haiwezi kuvumilia ufisadi au mwenendo wowote unaodhoofisha imani ya wananchi katika utoaji wa haki,' alisema katika taarifa. Aliongeza kuwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imeanza taratibu za kinidhamu dhidi ya afisa huyo huku uchunguzi wa jinai ukiendelea. Jaji Mkuu alisisitiza kuwa Mahakama ina sera ya kutovumilia ufisadi na kwamba maafisa wa mahakama hawawezi kutoa haki huku wakijihusisha na uhalifu. Kwa mujibu wa EACC, uchunguzi ulianza baada ya mfanyabiashara mmoja wa Murang'a kuwasilisha malalamishi. Mfanyabiashara huyo alikuwa amepatikana na hatia mnamo Julai 2, 2026 katika kesi ya kupata fedha kwa njia ya udanganyifu na alitarajiwa kuhukumiwa Julai 22. Mkurugenzi wa EACC Kanda ya Kati Japheth Baithalu alisema afisa wa huduma ya uangalizi wa wafungwa alidaiwa kumfuata mfanyabiashara huyo akisema alikuwa ametumwa na hakimu. Inadaiwa alimtaka Sh170,000 akiahidi fedha hizo zingemwezesha kupata ripoti nzuri ya uangalizi na hivyo kuepuka kifungo cha jela. Baada ya kupokea taarifa hiyo, EACC iliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa washukiwa hao katika mkahawa mmoja mjini Kangema walipokuwa wakidaiwa kupokea Sh150,000.

read more