taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Sifuna awatikisa Mudavadi, Atwoli; waanza ziara Magharibi kumtetea Ruto kwa wananchi
WIMBI la kisiasa la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi limewafanya baadhi ya viongozi wakuu wa serikali kutoka eneo la Magharibi kuanza kampeni kali kwa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027. Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye amekuwa akijiepusha na shughuli za kisiasa, ameanza ziara za mashinani kuimarisha uungwaji mkono wa chama tawala cha UDA. Mwishoni mwa wiki, Bw Mudavadi alikutana na waliowania tiketi za UDA kutoka Magharibi, huku Katibu Mkuu wa Cotu-K Francis Atwoli akiwa miongoni mwa waliohusika na mikakati ya kupanga mkutano huo. Mnamo Jumatatu, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya pia alikutana na wabunge 25 kutoka Magharibi jijini Kisumu kujadili jinsi ya kumfanyia Rais Ruto kampeni. "Tulikutana kujadili masuala yanayohusu uchaguzi ujao na jinsi tunavyoweza kujiweka vyema kama jamii," akasema Bw Oparanya. Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula nao wamebuni kikosi cha kampeni kinacholenga Magharibi na Nyanza, kwa lengo la kuimarisha uungwaji mkono kwa Rais Ruto. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema shughuli hizo zinaonekana kulenga kukabili kuongezeka kwa ushawishi wa mrengo wa Linda Mwananchi. Azma ya Bw Sifuna kuwania urais imeibua msisimko katika eneo hilo, huku kukiwa na hofu kwamba vuguvugu hilo linaweza kutokomeza umaarufu wa ODM na pia UDA. Bw Mudavadi alisema uchaguzi wa 2027 utahitaji maandalizi mazuri, akiwataka wagombea wa UDA kuimarisha miundo ya chama mashinani na kuhakikisha usajili wa wapigakura unaongezwa. Alikadiria kuwa kuna wapiga kura milioni 1.5 wenye vitambulisho ambao bado hawajajisajili kutoka eneo la Magharibi. "Njia ya kuelekea 2027 haitashindwa kwa kelele, bali kwa mpangilio, uaminifu na kura," akasema. Bw Atwoli aliwataka wagombea kumuunga mkono Bw Mudavadi kama kinara wa kisiasa wa eneo hilo, akisema Bw Sifuna bado hajatosha mboga. "Yeye atakuwepo baada yetu, lakini wakati wake si sasa," akasema Bw Atwoli. Hata hivyo, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi anayeegemea mrengo wa Linda Mwananchi alipuuzilia mbali mkutano huo, akisema hauwatikisi. Alisema UDA imepoteza umaarufu Magharibi na ndio maana mkutano huo ulifanyika Kisumu badala ya mji wa Magharibi. "Wameingiwa na hofu na unaweza kuona kukata tamaa katika shughuli zao. Eneo hili lina maeneobunge 33, lakini uliuona idadi ya wagombea waliohudhuria mkutano huo," akasema. Bw Osotsi alidai kuwa baadhi ya viongozi na wagombea kutoka eneo hilo wanasubiri tu chama kipya cha Linda Mwananchi kuanzishwa rasmi ili waondoke UDA na ODM. Hata hivyo, Bw Wandayi na Bw Savula wamesisitiza kuwa wataendelea kuwarai wenyeji wa Magharibi na Nyanza kumuunga mkono Rais Ruto, wakisema uongozi wake ndio utahakikisha maendeleo zaidi katika maeneo hayo.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 2 hours ago
Serikali yawataka wakulima wavune mazao yao kabla ya El Nino kuanza
WAKULIMA wameshauriwa kutumia wiki tatu zijazo kukamilisha uvunaji, ukaushaji mazao yao na kuandaa mashamba yao kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua ya El Nino. Ushauri huo umetolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga (KMD) inayoshikilia kuwa hali ya ukame itaendelea kushuhudiwa maeneo mengi ya nchi katika mwezi huu wa Septemba. "Wakati huu ambapo hali ya anga ni kavu, wakulima wanafaa kuvuna mazao yao yaliyokomaa, kuyakausha na kuyahifadhi ili yasiharibike," akaeleza Naibu Mkurugenzi wa idara hiyo, Paul Oloo. "Aidha, mwezi huu wa Septemba ni mwafaka kwa wakulima kutayarisha mashamba yao, kurekebisha miundo msingi ya kuvuna maji, kuzibua mitaro ya kupitisha maji, kununua mbegu na pembejeo zingine kwa ajili ya upanzi wakati wa msimu wa mvua wa Oktoba-Novemba-Desemba," akaongeza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 28 minutes ago
Wakazi wa Magadi wahofia kukosa huduma za hospitali baada ya kampuni kufurushwa
HUDUMA za matibabu katika Hospitali ya Magadi zinaendelea bila kukatizwa licha ya mzozo unaoendelea kati ya Serikali na kampuni ya Tata Chemicals. Hata hivyo, hofu imetanda miongoni mwa wakazi baada ya Rais William Ruto kuelekeza Serikali ya Kaunti ya Kajiado kuchukua usimamizi wa hospitali hiyo. Hospitali hiyo ya kiwango cha nne inahudumia wakazi kutoka Shompole, Olkiramatian na Olkeri Oldonyonyokie, wakiwemo wajawazito na wagonjwa wanaohitaji upasuaji, huduma za nje na kulazwa. Rais Ruto alitoa agizo hilo Jumamosi alipokuwa katika ziara ya maendeleo Kajiado, siku moja kabla ya kuagiza Tata Chemicals kuondoka nchini. "Hospitali ni ya wananchi. Serikali ya kaunti ichukue usimamizi wa hospitali ili kuwawezesha wakazi kuendelea kupata huduma za matibabu," alisema Rais Ruto. Hata hivyo, wakazi wana hofu kuwa mabadiliko ya ghafla ya usimamizi yanaweza kuvuruga huduma. Ziara ya Taifa Leo hospitalini humo Jumatatu ilionyesha idadi kubwa ya wagonjwa, hasa katika kitengo cha uzazi. Hii ni tofauti na hali ya wiki mbili zilizopita, ambapo idadi ya wagonjwa ilikuwa imepungua baada ya kampuni kufungwa na kusababisha mzunguko wa fedha katika eneo hilo kudorora. Hospitali hiyo iliyo na vitanda 54 ilijengwa na kuwekewa vifaa na Tata Chemicals, ambayo pia imekuwa ikiendesha shughuli zake. Inatoa huduma kwa wakazi kwa gharama nafuu, huku madaktari, wauguzi, wahudumu wa afya na wafamasia wakiajiriwa na kampuni hiyo. Bi Purity Naisiae alisema alifikishwa hospitalini usiku baada ya kuanza kupata maumivu ya kujifungua nyumbani. Alijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya upasuaji. "Hospitali hii ni tegemeo letu. Imeendelea kudumisha viwango vyake kwa miaka mingi," alisema. Mama yake, Bi Esther Nganoni, alisema hospitali hiyo imechangia kupunguza vifo vya watoto katika maeneo ya mashambani. "Tunapita maeneo yenye wanyama hatari usiku tukiwa na matumaini ya kupata matibabu hapa," alisema, akiomba kaunti isibadilishe usimamizi kwa haraka. Wakazi walisema hospitali hiyo ndiyo tegemeo lao kuu kwa huduma maalumu, hasa uzazi, upasuaji na kulazwa. Hofu yao imeongezwa na mgomo wa wahudumu wa afya katika hospitali za umma, ambao tayari umeathiri huduma katika kaunti kadhaa. Hospitali ya Rufaa ya Kajiado, ambayo ndiyo mbadala karibu, iko zaidi ya kilomita 100 kutoka Magadi. Msimamizi wa Hospitali ya Magadi, Dkt Raymond Birya, alisema hospitali hiyo hupokea angalau wanawake 21 wanaojifungua kila mwezi. Alisema hospitali ina dawa za kutosha kwa takriban miezi mitatu na inaendelea kutoa huduma saa 24. "Milango yetu bado iko wazi kwa wagonjwa," alisema Dkt Birya. Mzozo huo ulianza baada ya Wizara ya Madini kuagiza Tata Chemicals kusitisha shughuli zake Julai 29 kwa madai ya kutofuata masharti.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Waboni wataka fidia kwa 'kuharibiwa maisha' na operesheni ya KDF
JAMII ya Waboni katika Kaunti ya Lamu inaishinikiza serikali ya kitaifa kuwalipa fidia kwa kutatiza hali yao ya kawaida ya kimaisha kwa miaka 11 ambayo oparesheni ya kupambana na ugaidi imekuwa ikiendelezwa eneo hilo. Kulingana nao, oparesheni ya kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab katika Msitu wa Boni iliyoanza mwaka wa 2015, imewazuia kuishi walivyozoea kwa kuwinda wanyamapori, kuchuma matunda ya mwituni na kuvuna asali asili msituni. Wakiongozwa na Diwani wa Zamani wa Basuba, Bw Mohamed Delo, waliitaka serikali ya kitaifa kuwalipa fidia ili wagharamie shughuli nyingine za kimaisha zisizowahitaji kuingia msituni. "Ingekuwa haki kama walivyolipa wavuvi walioathiriwa na Bandari ya Lamu Sh1.76 bilioni basi pia na sisi tufidiwe sawia," akasema Bw Delo, akisisitiza kuwa ombi lao halimaanishi wanapiga vita serikali. Bw Omar Bwana Barissa, mzee wa kijiji cha Basuba, alisema jamii hiyo pia ina madhabahu ya kitamaduni ndani ya msitu wa Boni. "Tangu operesheni ianzishwe hata kufika huko ndani ya msitu angalau kuomba haiwezekani," akasema Bw Barissa. Bi Halima Musa, mkazi wa kijiji cha Mararani, alisema wamejaribu kubadili maisha kwa kuingilia kilimo, lakini wanakumbwa na changamoto ya uvamizi wa wanyamapori wanaoharibu mashamba yao kila mara. Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Stephen Sangolo alisema bado hajapokea malalamishi rasmi kutoka kwa jamii hiyo kuhusu fidia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Ekari 30,000 za msitu wa Mlima Kenya zateketea kwa moto
KARIBU ekari 30,000 za maeneo ya nyanda za juu katika Msitu wa Mlima Kenya zimeteketea kutokana na moto mkali uliozuka Septemba 1. Afisa wa kuhifadhi Misitu Kaunti ya Meru Wellington Ndaka, alisema moto huo umeathiri sehemu nne za misitu ya Ruthumbi, Mucheene, Marania na Meru, huku ukitishia kusambaa hadi sehemu nyingine yenye miti ya kiasili. Bw Ndaka alisema moto huo ulikuwa ukienea kwa kasi kutokana na upepo mkali, ukavu na vichaka vya nyanda za juu ambavyo hushika moto kwa urahisi. Zaidi ya watu 800, wakiwemo wakazi, maafisa wa Shirika la Misitu Kenya (KFS), walinzi wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) na wanajeshi, walishiriki juhudi za kuuzima moto huo. Mashirika ya uhifadhi msitu kama Mount Kenya Trust, Lewa Wildlife Conservancy, Rhino Ark, Borana Conservancy, Kisima Farm na Tropic Air, pia yalishiriki juhudi za kuzima moto. "Juhudi za kuuzima moto huo zinatatizwa ardhi kavu na hali ya hewa iliyopo. Tunatumia mashine za KDF na KFS kutengeneza njia za kuzuia moto ili usisambae hadi kwenye miti ya kiasili," akasema Bw Ndaka. Moto huo ulisambaa kutoka Kibaranyaki kuelekea Rutundu, Ziwa Alice na Ziwa Ellis, huku upepo mkali ukichochea kuenea kwake baada ya baadhi ya maeneo kuzimwa. Wazima moto walilazimika kusafirishwa kwa helikopta hadi maeneo ya chini ya mlima ili kudhibiti moto uliokuwa ukielekea Korongo la Kathita na Ziwa Rutundu. Hata walilazimika kujiondoa kutokana na upepo mkali. Bw Ndaka aliwaomba wafadhili na mashirika kusaidia kwa chakula, vifaa vya kuzimia moto na mafuta, huku wanachama wa mashirika ya kijamii wakihimizwa kujitolea katika shughuli za uokoaji. Moto huo ulizuka wakati maafisa wengine walikuwa wakidhibiti moto katika misitu ya Aberdare, ambako zaidi ya ekari 200 ziliteketea. Akikagua shughuli za kuzima moto Mlima Kenya, Katibu Mkuu wa Misitu Gitonga Mugambi alisema ujenzi wa uwanja wa ndege ni muhimu ili kusaidia kukabiliana na dharura kama hizo. "Kama tungekuwa na uwanja wa ndege katika msitu, ingekuwa rahisi kudhibiti moto unaosambaa kwa kasi katika Mlima Kenya," akasema. KFS imesema zaidi ya ekari 96,000 za misitu zimeharibiwa na moto katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Wapwani walalamikia ongezeko la vijana kutekwa na kupatikana Nairobi
VIONGOZI na wakazi wa Mombasa wameelezea wasiwasi kuhusu visa vya vijana kupotea, huku baadhi yao baadaye wakipatikana Nairobi na katika viunga vya jiji hilo. Tukio la hivi majuzi lilihusisha wasichana wawili wenye umri wa miaka 16 na 17 ambao waliokolewa wikendi baada ya kudaiwa kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki moja. Wapelelezi kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) sasa wanategemea ushahidi wa kieletroniki katika kesi ambapo mwanaharakati Caleb Ngwena anachunguzwa kwa madai ya ubakaji na ulanguzi wa watoto kuhusu kisa hicho. Wasichana hao wawili waliokolewa katika eneo la Kasarani, Nairobi baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja. Ngwena alifikishwa katika Mahakama ya Shanzu, iliyowaruhusu wapelelezi kumzuilia kwa wiki mbili ili kukamilisha uchunguzi wao. Mahakama iliagiza azuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Mjambere, baada ya kukubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kwamba waathiriwa hao ni watu walio katika mazingira hatari na kwamba kumwachilia Ngwena kwa sasa kunaweza kuhatarisha ushahidi na kuingilia kati uchunguzi. "Mahakama imeridhika kwamba polisi wamewasilisha sababu nzito na za msingi za kumzuia Ngwena ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi wao. Ombi hilo limekubaliwa na atazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mjambere kwa muda wa siku 14," mahakama iliamua. Wasichana hao ni wanafunzi wa Kidato cha Tatu na majirani katika mtaa wa Red Estate, Kiembeni. Walitoweka usiku wa Agosti 25 na kusababisha mama zao kupiga ripoti katika Kituo cha Polisi cha Kiembeni siku iliyofuata. Ngwena alikamatwa nyumbani kwake Kiembeni Septemba 2 na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Mjambere. Polisi walisema alisafiri hadi Nairobi akiwa ameandamana na maafisa wa DCI Kisauni mnamo Septemba 3 katika juhudi za kuwatafuta wasichana hao. Wasichana hao waliokolewa siku iliyofuata katika eneo la Kasarani, huku wachunguzi wakisema Ngwena alisaidia katika kuwapatia mahali walikokuwa. Wasichana hao waliwaeleza wachunguzi kwamba walichukuliwa kwa nguvu na Ngwena pamoja na mwanamume mwingine usiku walipotoweka. Walisema walilazimishwa kuingia katika gari ambalo hawakulitambua na kusafirishwa kutoka Kiembeni hadi Nairobi, kabla ya kupelekwa Kaunti ya Kiambu. Inadaiwa walifungiwa katika chumba kimoja na kubakwa. Wachunguzi sasa wanafuatilia mawasiliano na ushahidi wa kifedha uliofanyika kabla na baada ya wasichana hao kutoweka. Polisi walisema kulikuwa na mawasiliano mengi pamoja na fedha zilizotumwa kwenda kwenye simu za wasichana hao. Laini za simu walizotumia zilisajiliwa kwa majina ya mama zao. Polisi wanataka kupata taarifa kutoka Safaricom kuhusu akaunti tano za M-Pesa kwa kipindi cha Julai 20 hadi Septemba 6. Taarifa hizo zinajumuisha stakabadhi zilizotumika kufungua akaunti, taarifa za M-Pesa na rekodi za matumizi ya simu. Pia, wanachunguza taarifa za akaunti tatu za Airtel Money pamoja na rekodi zinazohusiana na matumizi ya simu kwa kipindi hicho. Mahakama iliwaruhusu wapelelezi kuchunguza simu nne zilizopatikana, ambazo ni Oppo A9 2020, Samsung Galaxy A04e, Calus W999 na simu ya Nokia. Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) kimeruhusiwa kufikia simu hizo, kuchunguza yaliyomo na kutoa faili pamoja na programu zilizohifadhiwa kwenye vifaa hivyo. Mpelelezi wa kesi hiyo John Andama, alisema muda wa ziada wa kumzuilia Ngwena ulihitajika ili kupata ripoti za kitabibu za wasichana hao, kuchanganua rekodi za simu na rekodi za fedha, kutoa taarifa kutoka kwenye simu hizo na kurekodi taarifa za mashahidi wengine. Polisi pia walisema Ngwena anawasaidia katika juhudi za kuwakamata washukiwa wengine wanaohusishwa na kisa hicho.Kupitia wakili wake, Ngwena alipinga kuzuiliwa kwake na kuomba aachiliwe kwa dhamana. Upande wa utetezi ulipinga ombi la polisi, ukilitaja kuwa na kasoro za kisheria, huku ukipinga maelezo ya polisi kuhusu safari zake na kukana madai kwamba ndiye aliyewaongoza maafisa hadi Nairobi. "Ni polisi waliompeleka mshtakiwa Nairobi; si kwamba yeye ndiye aliyewaongoza hadi huko," wakili huyo aliambia mahakama. Hakimu alisema polisi wana wajibu wa kutoa sababu za msingi za kuendelea kumzuilia mshukiwa baada ya muda uliowekwa na Katiba. Hata hivyo, mahakama ilisema polisi wamewasilisha sababu za msingi za kuendelea kumzuilia Ngwena, ikizingatia mazingira ya waathiriwa na umuhimu wa kulinda ushahidi. Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Mombasa, Bi Zamzam Mohamed, alisema karibu visa 13 vya matineja kupotea vimeripotiwa tangu Agosti. Aliwataka wazazi kuwa waangalifu na kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuzuia visa kama hivyo. "Mambo si mazuri huku nje. Vijana wengi wanapotea, kwa hivyo ninawahimiza wazazi kuwachunga watoto wao kwa makini. Kaeni pamoja na watoto wenu, zungumzeni nao, eleweni changamoto zao," alisema mwishoni mwa wiki iliyopita. Waathiriwa wote wamepelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na ushauri nasaha, huku taarifa zikiwa zimechukuliwa kutoka kwa familia zao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Moto kambi ya Ruto wandani wakivurugana wakisaka ubabe
UBABE wa kisiasa kati ya mawaziri au watumishi wa umma na wanasiasa wanaoumuunga mkono Rais William Ruto unaendelea kutokota, hali inayoweza kuathiri kuchaguliwa kwake tena mnamo 2027. Mivutano hiyo imejitokeza katika maeneo ambayo Rais anatarajiwa kupata kura nyingi huku ikiwa wazi Mlima Kenya iliyokuwa ngome yake ya kisiasa inaendelea kumponyoka. Katika Kaunti ya Kakamega, mvutano kati ya Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Gavana Fernandes Barasa umetokota na kufikia kilele. Bw Barasa amemtaka Rais Ruto amtimue Bw Oparanya, akidai waziri huyo amekuwa akifanya mikutano ya usiku kupanga njama za kumng'oa 2027. "Namwambia Rais Ruto kwamba tunamheshimu, lakini hapa Kakamega umetuletea mzozo kupitia Waziri Oparanya, ambaye hajui kazi yake wala haelewi majukumu yake. Kazi yake hapa ni kufanya mikutano ya usiku ya kuniondoa madarakani na kunipangia mabaya. Kazi uliyompa haitusaidii. Tafadhali mpe mtu mwingine," akasema Bw Barasa. Gavana huyo pia anadai Bw Oparanya anamuunga mkono Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda kuwania ugavana. Bw Oparanya, aliyekuwa gavana wa Kakamega kati ya 2013 na 2022, amekanusha madai hayo akisema hana mgombea anayemuunga mkono. Alimtaka Bw Barasa kujikita katika kutetea kiti chake. "Anaonekana kupigana vita na nafsi yake kwa sababu yeye si mtu wa hadhi yangu kisiasa. Kwa nini nimfadhili mtu ampinge? Uchaguzi ni wa ushindani na ikiwa anaogopa ushindani basi aachane na siasa," akasema Bw Oparanya kwenye mahojiano na Taifa Leo. Mbunge wa Khwisero Christopher Aseka pia alimkosoa Bw Barasa, akisema rekodi yake ya maendeleo si ya kuridhisha. "Amewahi kufanya nini kuhusiana na masuala ya maendeleo? Amekuwa akiorodheshwa vibaya katika maendeleo na miradi mingi iliyoanzishwa na Oparanya haijakamilika. Rekodi ya Barasa katika maendeleo ni duni na hatutamruhusu kuendeleza siasa za chuki hadi kumtaka Rais amtimue Oparanya," akasema Bw Aseka. Kajiado pia imekuwa uwanja wa mzozo kati ya Msimamzi wa Wafanyakazi Ikulu Katoo ole Metito na Gavana Joseph Ole Lenku, ambao wote waligombea ugavana 2022. Bw Lenku, anayelenga sasa kiti cha useneta, amepinga mpango wa kisiasa wa UDA na ODM unaomuunga mkono Bw Metito kugombea ugavana na Judy Pareno kuwania useneta. Pia ametishia kuondoka ODM na kujiunga na Linda Mwananchi. "Kuna mtu anatudharau mbele yako, lakini hatutavuruga mkutano wako wala kulipiza kisasi. Katoo anadai kuwa msemaji wa Wamaasai ilhali yeye ni msemaji wako. Walisema pia Amboseli haitarejeshwa kwa jamii, lakini neno lako ndilo la mwisho," akasema Bw Lenku wakati wa mkutano wa Rais katika kaunti yake wikendi. Katika Bonde la Ufa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen anakabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaodai anawadhamini wagombeaji ili kuwa na ushawishi eneo hilo baada ya Rais Ruto. Mbunge wa Keiyo Kusini Gideon Kimaiyo mnamo Agosti 5 alikerwa na Bw Murkomen na akasema Kaunti ya Elgeyo-Marakwet si himaya yake kisiasa. "Elgeyo-Marakwet haitakuwa ufalme wa mtu yeyote, wala hatafanikiwa na mipango yake Keiyo Kusini. Ikiwa unataka kuwa kinara, pigana na wanaowania nafasi hiyo pamoja nawe, si Keiyo Kusini," akasema Bw Kimaiyo. Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alimtaka Bw Murkomen kuweka kando ndoto zake za 2032 na kumsaidia Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Aweke kando kwa sasa ndoto zake za 2032 na za kuwa kinara, na amsaidie Rais. Hawezi kupigania kuwa msemaji wa jamii wakati tuna Rais Ruto," akasema. Busia nako hali si tofauti, Katibu Mkuu wa Biashara Ndogo Ndogo Susan Mangéni naye akimshambulia aliyekuwa Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, akidai anapinga kuchaguliwa kwa Rais Ruto kichinichini. "Ababu Namwamba, unapinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto kwa sababu umeumia. Watu wa Budalang'i hawataendelea kuishi katika umaskini wa kudumu kwa sababu ya ubinafsi wako. Wewe si Budalang'i na Budalang'i si wewe," akasema Bi Mangéni. Wawili hao wamekuwa na uhasama mkali kuhusiana na siasa za UDA.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Wageni waingiwa na taharuki tele kutokana na agizo la Rais Ruto
MAMIA ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini jana waligubikwa na taharuki na wasiwasi baada ya Rais William Ruto kuamuru msako dhidi yao hasa wale wanaofanya biashara ndogondogo. Amri hiyo iliyotolewa wiki jana Septemba 2 wakati wa mkutano na wafanyabiashara wadogo (MSME) ilisababisha pilkapilka za kukimbilia stakabadhi za kusafiri, baadhi ya biashara kufungwa na ripoti za vitisho na kuhangaishwa katika sehemu mbalimbali nchini. Mtanziko huo ulitokana na kile wanachosema raia wa kigeni walielewa kama amri ya kuondoka na ufafanuzi uliofuata kutoka kwa serikali kwamba msako huo unalenga wale wanaoendesha shughuli kinyume cha masharti ya uhamiaji, kibali cha kazi na sheria nyinginezo. Jijini Nairobi, raia wa Burundi waliojawa wasiwasi walipanga foleni nje ya ubalozi wao jana, baadhi wakisaka stakabadhi za dharura kusafiri kurejea makwao huku wengine wakitafuta msaada wa kuhalalisha biashara zao na kuendelea kuwepo nchini. Matukio hayo yaliashiria suitafahamu iliyofuatia matamshi ya Rais huku raia wa kigeni wanaofanya biashara wakichanganyikiwa kuhusu iwapo waliagizwa kuondoka nchini au wanahitajika kuhalalisha biashara na hadhi yao ya uhamiaji. Nchini kote, wasiwasi uligeuka hofu ikiripotiwa kuwa raia wa kigeni walichelea kufungua biashara zao, kuacha makao yao na katika baadhi ya maeneo madai ya kuhangaishwa na wizi. Serikali, hata hivyo, inasisitiza msako huo si amri ya kuwafurusha raia wa kigeni nchini. Maafisa wanasema wanaolengwa ni wale wanaoendesha biashara zao bila vibali vya kazi, leseni au hadhi ya uhamiaji inayohitajika, huku raia wa kigeni wafanyabiashara waliosajiliwa wakilindwa. Jijini Nairobi, mamia ya raia wa Burundi walijitokeza katika ubalozi wao wakisaka stakabadhi za usafiri na msaada, huku baadhi wakisema wanajiandaa kurejea makwao kwa sababu hawahisi kuwa salama tena kenya. Foleni ndefu zilipangwa nje ya balozi huku wafanyabiashara waliozongwa na wasiwasi wakiitisha ufafanuzi kuhusu hatima yao. Katika Ubalozi wa Burundi, baadhi ya raia waliozungumza na vyombo vya habari walisema waliondoka nchi yao kusaka nafasi za kitega uchumi na waligeuza Kenya kuwa makao yao ya pili. "Nchi yetu ni ndogo, tunakabiliwa na ukosefu wa ajira na hatuna shughuli nyingi zinazofanyika ndiposa tuling'ang'ana kuja Kenya kuyainua maisha yetu. Tumewajua Wakenya kama watu wa amani na taifa bora Afrika lakini sijakula kwa siku mbili nilipojua tunatimuliwa," akasema Erick Bizimana, aliyekuja Kenya 2022. Mjini Murang'a, Jean Niyonzima, 28, ambaye amechuuza kahawa na mandazi kwa miaka mitano alisema alisimamishwa na maafisa wawili wa polisi Septemba 6 akidai alilazimishwa kusalimisha Sh3,000. Mfanyabiashara mwengine Esperance Ndayishimiye, 24, anayeuza mavazi ya wanawake Murang'a, alisema hali imevurugika. Homa Bay, raia kadhaa wa kigeni waliripoti biashara zao kuvunjwa na mali ikiwemo vifaa vya simu, viatu na nguo kuibiwa. Mfanyabiashara raia wa Rwanda Zarubbabel Rusesabagina alisema alipoteza sehemu kubwa ya mali yake ikiwemo pasipoti, kadi ya ATM, vitambulisho na Sh16,000 pesa taslimu. Mjini Kisii, wafanyabiashara wengi raia wa Uganda, Burundi na Rwanda hawakufungua biashara zao jana wakihofia kukamatwa na mali yao kuporwa. Miji ya Narok, Kericho, na Bomet, raia wa kigeni wachuuzi pia walijiepusha kwenda barabarani huku baadhi wakiripotiwa kusafiri Nairobi kuwasilisha malalamishi kwa serikali. Jijini Mombasa, raia wengi wa kigeni ambao kwa kawaida huchuuza bidhaa au kufanya kazi katika vinyozi, hoteli na vituo vya kuoshea magari hawakuwepo pia. Lakini mjini Nyahururu, baadhi ya wanafanyabiashara waliapa kuwalinda raia wa kigeni ambao wameishi nao kwa miaka mingi. "Tumeishi nao kwa miongo mingi, watoto wetu wanasoma pamoja shuleni. Wengi wao walizaliwa na kulelewa hapa, ni nyumbani ya pekee wanayojua, amri ya rais haina uhalisia," akasema mfanyabiashara Philip Kahome. Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui alisema baadhi ya raia wa kigeni wanatumia vibaya hati za kusafiria na mipango ya kuingia nchini kwa kushiriki biashara wakiwa kwenye hadhi ya mwekezaji au mtalii bila vibali vya kazi vinavyohitajika. Bw Kinyanjui alisema raia wa kigeni watakaopatikana wakikiuka masharti ya uhamiaji watapokonywa hati zao kulingana na sheria. Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Abraham Korir Sing'oei vilevile aliwahakikishia raia wa kigeni kwamba matamshi ya Rais hayapaswi kufasiriwa kama amri ya jumla dhidi ya raia wote wa kigeni wafanyabiashara. Alisema wafanyabiashara wadogo na wakubwa na waajiriwa wa mataifa yote walio na stakabadhi zinazohitajika, ikiwemo vibali vya kazi wamelindwa kisheria kuendesha shughuli zao Kenya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 17 hours ago
MAONI: Tusikosoe Rais na Serikali ili kutafuta sifa tu, tukosoe kwa heshima na ushahidi
RAIS ni mtumishi wa wananchi na anapaswa kuwajibishwa kuhusu maamuzi ya serikali yake. Hata hivyo, kukosoa uongozi hakupaswi kugeuzwa kuwa mashindano ya kutafuta makofi kutoka kwa wananchi. Ni jambo la kawaida kwa wanasiasa kukosoa serikali ili kujijengea umaarufu. Lakini ukosoaji usio na hoja unaweza kupotosha umma na kuleta mgawanyiko. Tunahitaji viongozi wanaoweza kusema ukweli hata kama ukweli huo hauwafurahishi mashabiki wao. Wananchi na viongozi wana haki ya kumuuliza rais maswali magumu. Serikali inaposhindwa kutoa huduma bora, kupambana na ufisadi, kuunda nafasi za ajira au kupunguza gharama ya maisha, ni wajibu wa viongozi kuzungumzia matatizo hayo. Lakini kukosoa hakumaanishi kutumia matusi, dhihaka au lugha ya uchochezi. Matusi hayabadilishi sera mbaya kuwa nzuri wala hayatatui tatizo la mwananchi. Badala yake, yanaweza kugawanya wananchi na kuwafanya viongozi kushindwa kujadili masuala muhimu kwa utulivu. Viongozi wa upinzani wanapaswa kukumbuka kwamba wananchi wanawatazama. Wanapozungumza kwa hasira na kutumia lugha chafu, vijana na watoto wanaojifunza kutoka kwao wanaweza kuona kwamba tofauti za kisiasa zinahalalisha ukosefu wa heshima. Vivyo hivyo, wafuasi wa serikali hawapaswi kumtetea Rais kwa kila jambo hata pale ambapo kuna makosa yanayohitaji kurekebishwa. Uzalendo si kuficha makosa ya serikali. Uzalendo ni kuonyesha kasoro na kupendekeza njia bora za kuzitatua. Tunapaswa kujenga utamaduni wa kisiasa ambapo hoja inajibiwa kwa hoja, si kwa matusi. Rais akifanya vizuri, tumpongeze. Akikosea, tumkosoe kwa heshima na ushahidi. Lengo la ukosoaji linapaswa kuwa kuboresha uongozi na maisha ya wananchi, si kumdhalilisha Rais au kufurahisha umma. Kwa hivyo, tusimkosoe Rais kwa kutafuta makofi. Tumkosoe kwa ukweli, uwajibikaji na nia ya kuijenga Kenya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 20 hours ago
MAONI: Watanzania wasiogope 'vita' vya kuitafuta katiba mpya
HUKU Kenya ikitathmini hatua ilizokwisha kupiga katika utekelezaji wa Katiba yake'mpya' tangu ilipoidhinishwa 2010, Tanzania nayo inashuhudia mwamko mpya wa kuisaka katiba mpya. Kenya na Tanzania zilipata uhuru kwa ukaribu mno kiwakati. Huku Tanzania ikitupilia mbali nira ya ukoloni mkongwe wa Wajerumani na Waingereza, Desemba 9,1961 na kuwa Jamuhuri mnamo Aprili 26, 1964 (kufuatia muungano wa Tanganyika na Zanzibar), Kenya ilijikomboa kutoka kwa Waingereza Desemba 12, 1963, na kuwa Jamuhuri 1964. Wakenya na Watanzania ni 'watu wamoja' waliotenganishwa na mipaka ya wakoloni. Inatia moyo kwamba, baada ya miaka 16 tangu Kenya ijipatie Katiba 'mpya', tumeanza kuona vuguvugu nchini Tanzania kuisaka katiba mpya. Tangu uhuru nchini Tanzania, kuna mabadiliko mengi yaliyojiri kijamii, kiuchumi na kisiasa - kiasi kwamba, upo uwezekano mkubwa kuwa, Katiba ya Uhuru haiwezi tena kukidhi matakwa na matamanio ya Watanzania. Tanzania ima mengi ya kujifunza kutokana na safari na mchakato na mapambano yaliyojiri Kenya katika kuitafuta Katiba mpya. Kwanza, safari hiyo ya takriban miongo miwili haikuwa rahisi. Ilikumbwa na vikwazo na upinzani mkubwa wa kisiasa na hata kusababisha maafa. Lakini Wakenya hawakukata tamaa. Misukumo iliyochochea utashi wa katiba mpya nchini Kenya katika miaka ya 1990 ilisababishwa na mabadiliko mengi kwenye katiba ya uhuru yaliyomlimbikizia mamlaka rais na kumfanya awe mtawala wa kiimla. Dalili hizo zinaonekana Tanzania. Kwa sababu hiyo, wanaharakati na asasi za kidini zilijifungata masombo kuicheza ngoma ya mabadiliko ya katiba. Harakati hizo zilizaa matunda pale Kifungu cha 2A cha Katiba kiliporekebishwa kuirejesha Kenya kwenye mkondo wa demokrasia ya siasa za vyama vingi. Jambo hilo haikubadilisha hali ya rais mwenye mamlaka au nguvu nyingi. Mapambano hayo yalikwama baina ya 2000 -2005. Mnamo 2000, mwanasheria, Prof Yash Pal Ghai wa Tume ya Marekebisho ya Katiba (CKRC) alianza kukusanya maoni kutoka kwa umma, na kuandaa Mswada wa Bomas (Bomas Draft). Wasomi teule wa Kisiasa waliubadilisha mswada huo kuwa Wako Draft - ambao Wakenya waliuangusha katika kura ya maoni ya mwaka 2005. Mkosi wa ghasia za baada ya uchaguzi mnamo 2007/2008 ulitia chachu kwa wanasiasa na wasomi teule kutambua kwamba, ilikuwa ni hatari kwa usalama wa nchi yenye asasi zilizopendelea upande mmoja. Machafuko hayo nusura yaisambaratishe Kenya. Kamati ya Wataalamu ilipitia miswada tangulizi ya katiba. Mnamo Agosti 2010 asilimia 67 ya Wakenya waliipitisha Katiba hiyo kwenye kura ya maoni, na kuzindua serikali za ugatuzi. Bitugi Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 20 hours ago
Ruto sasa atumia maafisa wa umma 'kubembeleza' Mlima
RAIS William Ruto sasa anawategemea makatibu wa Baraza la Mawaziri na maafisa wengine wa serikali kupeleka ujumbe wa serikali mashinani katika juhudi za kurejesha uungwaji mkono wa Mlima Kenya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Mikakati hiyo inalenga kueleza wakazi mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza na kupunguza malalamishi kwamba eneo hilo limetengwa tangu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuondolewa mamlakani Oktoba 2024. Rais Ruto amekiri kuwa serikali imekuwa na tatizo la kuwasilisha mafanikio yake kwa wananchi, hali ambayo amedai imeacha nafasi kwa taarifa potovu na kuchochea kutoridhika. Maafisa wa serikali sasa wanafanya mikutano ya hadhara katika eneo la Mlima Kenya kueleza mipango ya serikali na kushughulikia malalamishi ya wananchi. Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alifanya baraza la wananchi Nyeri kupitia mpango wa Jamii Imara Mashinani, ambako alijibu maswali kuhusu afya, kilimo na miundombinu. Bi Muthoni alisema serikali imegundua pengo la mawasiliano kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), akieleza kuwa wananchi wengi hawajui wanaweza kulipa michango yao kwa awamu kupitia mpango wa Lipa SHA Polepole. Maafisa wengine waliohusika katika mikutano hiyo ni Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na Katibu Mkuu wa Kawi Alex Wachira. Katika upande wa miundombinu, Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KeNHA), Winfrida Ngumi, alisema miradi ya barabara yenye thamani ya zaidi ya Sh46 bilioni imekamilika au inaendelea Nyeri. Alisema pia barabara za Mau Mau, ambazo zilikuwa zimesimama, zimeanza tena baada ya wakandarasi kulipwa zaidi ya Sh5.5 bilioni.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 07:37:33
Mwenye nyumba ya "Bikira Maria" Kisii aibomoa, adai kuchoshwa na mamia ya 'mahujaji'
MWANAMUME mwenye nyumba huko Kisii ambapo picha ya "Bikira Maria" inasemekana kuonekana ameibomoa kwa hasira kutokana na idadi kubwa ya watu wanaowasili kwake kushuhudia tukio hilo la kushangaza. Charles Onsombi wa kijiji cha Getare, kata ndogo ya Emenwa, eneobunge la Bobasi, sasa anafurusha mtu yeyote anayetaka kuingia kwake akimtishia kumdhuru kwa upanga mkali ambao anatembea nao. Onsombi ni mume wa Bi Maria Onsombi, ambaye aliripoti kwa majirani kwamba ameona picha hiyo kwenye ukuta wa jiko lake. Mume huyo kulingana na majirani, amekuwa akiishi sehemu za Mombasa huku mkewe akisalia Kisii. Pindi aliposikia habari kuwa kwake kumekuwa eneo la "muujiza" alifunga safari moja kwa moja na kuwasili kijijini Jumamosi asubuhi. Alipofika nyumbani, alikuta maskani yake madogo yamejaa mahujaji, waendesha boda boda na wahubiri ambao walikuwa wamegeuza njia yake ya miguu kuwa barabara yenye shughuli nyingi. Akiwa amekasirika, alichukua jembe Jumapili usiku na kubomoa jiko la udongo lililokuwa limegeuka "madhabahu." "Amekuwa mkali sana. Anawafukuza watu akiwa na upanga pamoja na jamaa mwingine. Anasema hakuna Bikira Maria kwake, ni moshi tu ulioonwa," alisema kijana mmoja aliyekatazwa kuingia langoni. Nyumba hiyo maarufu, iliyokuwa na ukuta wenye umbo la rangi nyeupe-kijivu lililofanana na mwanamke aliyefunikwa, ilikuwa imebomolewa na kubaki rundo la matope. Jiko la mawe matatu lililokuwa likionyesha mahali ambapo Bi Onsombi alipiga magoti kupika, lilikuwa limetawanyika. Kwa mujibu wa mke huyo, alikuwa ametoka tu kuwasha jiko lake ili kuandalia familia yake chakula cha jioni alipoona kitu kama kivuli kwenye ukuta wa upande wa kaskazini, takribani futi tatu kutoka sakafuni, mahali pale pale ambapo huinama kuwasha moto. Kilichoanza kama taarifa ya jirani mmoja kwa mwingine kilienea kwa kasi. Kufikia Jumatatu, njia ya kuelekea nyumbani kwa Mzee Onsombi ilikuwa imefanywa barabara kubwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu. Waendesha boda boda walikuwa wakitoza Sh100 kwa safari kutoka kituo cha Emenwa hadi Getare, wanafunzi waliovalia sare walikuwa wakitoroka masomo ili kwenda kuliona tukio hilo, na wahubiri kutoka maeneo ya mbali kama Ogembo na Nyamache walikuwa wakimiminika hapo, lakini walifukuzwa kwa nguvu na Bw Onsombi, ambaye hata aliwatishia kuwadhuru. "Siwataki hapa. Ikiwa mnataka udongo huu uliobomolewa, niambieni ili niwawekee kwenye mifuko ya kubebea," Bw Onsombi alisikika akisema. Jikoni mwao hapakuwa na kitu cha kipekee. Jiko hilo lilijengwa kwa kuta za udongo zilizochakaa kutokana na moshi wa kuni uliokusanyika kwa miaka mingi, huku sufuria chache zikining'inia kwenye misumari. Lakini kwenye ukuta huo kulikuwa na umbo lenye urefu wa takribani inchi 18, ambalo kwa muumini lilifanana na mwanamke aliyefunikwa kwa vazi refu, mikono yake ikiwa imekunjwa kana kwamba anaomba. Baadhi ya mahujaji walifika na kuugusa ukuta huo. Wengine walipiga magoti na kusali. Wengine walipiga picha kwa ajili ya TikTok. Kanisa Katoliki limekanusha madai kwamba picha hiyo iliyokuwa kwenye ukuta wa jiko la mwanamke huyo ilikuwa ya "Bikira Maria", mama wa Yesu Kristo kama inavyosema Biblia. Padri Edward Nyakundi wa Parokia ya Nyamagwa alitembelea nyumba hiyo Jumapili, wakati umati wa watu uliendelea kuongezeka, na akakanusha madai kwamba umbo hilo lilikuwa la Bikira Maria. "Hebu niwaulize. Katika ile miaka ya nyuma ambayo Biblia inazungumzia kuhusu Bikira Maria, ni nani aliyekuwepo kumpiga picha na kujua sura yake ilivyokuwa?" Padri Nyakundi aliwauliza wakazi alipofika nyumbani hapo Jumapili asubuhi, na kuwaacha watu waliokuwa wamekusanyika katika ukimya wa mshangao. Padri huyo aliwakumbusha waumini kwamba Kanisa Katoliki lina utaratibu mkali na mrefu wa kuthibitisha madai ya maono au miujiza ya kuonekana kwa watu watakatifu. Mchakato huo unaweza kuchukua miaka na huhusisha uchunguzi wa kitheolojia, kisaikolojia na kisayansi unaofanywa na dayosisi na hatimaye makao makuu ya kanisa huko Vatican. "Kanisa huwa makini sana. Tumekuwa na taarifa nyingi kama hizi. Nyingi huishia kuwa matukio ya kawaida ya ndoto. Lakini hatuwezi kupuuza imani ya watu," alisema katekista mmoja wa eneo hilo ambaye aliomba kutotajwa jina. Bi Maria Onsombi, ambaye alikuwa amepata umaarufu wa ghafla na ambaye simulizi yake iliwaunganisha waumini wa madhehebu tofauti katika jiko moja lililojaa moshi, sasa amenyamaza na hakuonekana Taifa Leo ilipozuru eneo hilo. Majirani wanasema amekwenda kukaa kwa jamaa yake aliye karibu, akihofia hasira za mume wake. Polisi kutoka kituo cha Igare wamewekwa kwenye tahadhari ili kuzuia makabiliano yoyote kati ya mmiliki huyo aliyekasirika na mahujaji ambao bado wanaendelea kufika bila kujua kwamba madhabahu waliyokuja kuiona sasa yamegeuka kuwa rundo la matope.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 05:32:37
Tanzania yaomboleza kifo cha mume wa Rais Samia, Hafidh Ameir Hassan
DAR ES SALAAM, Tanzania TANZANIA inaendelea kuomboleza mauti ya Mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Hafidh Ameir Hassan. Hassan alifariki Jumatatu asubuhi alipokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua maradhi ya moyo. Tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania Deogratius Ndejembi, aliyesema Hassan alifariki mwendo wa saa mbili asubuhi katika hospitali moja Zanzibar. "Wananchi wenzangu, ni kwa masikitiko makubwa ninawafahamisha kuhusu kifo cha Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan," akasema Ndejembi. "Alifariki Septemba 7, 2026, mwendo wa saa mbili asubuhi katika Hospitali ya Emilio Mzena Memorial, Zanzibar, alipokuwa akipokea matibabu ya ugonjwa wa moyo," akaongeza. Makamu wa Rais alitoa pole kwa Rais Samia, familia, ndugu na marafiki wa marehemu pamoja na Watanzania wote, akisema maandalizi ya mazishi yalikuwa yashaanza katika eneo la Kizimkazi, Zanzibar. Hafidh Ameir na Samia Suluhu walifunga ndoa 1978 na walijaliwa watoto wanne, akiwemo Wanu Hafidh Ameir, ambaye ni mwanasiasa na mbunge Tanzania. Hassan alikuwa msomi na mtaalamu wa kilimo, lakini alijulikana zaidi kwa kutopenda kujihusisha na shughuli za hadhara au za umma. Katika kipindi chake kama Mume wa Rais, aliishi maisha ya faragha na hakujihusisha sana na mitandao ya kijamii, kiasi kwamba umma ulijua machache kumhusu. Baada ya kifo chake, viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Kenya William Ruto, walituma rambirambi kwa Rais Samia. Rais Ruto alimsifu Hassan kuwa baba mpendwa na mwana mashuhuri wa Tanzania, akitoa pole kwa niaba yake binafsi na Wakenya wote. "Nimepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Hafidh Ameir Hassan, mume wa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," akasema Rais Ruto. "Kenya iko pamoja na ndugu na dada zetu wa Tanzania katika kipindi hiki cha maombolezo. Mwenyezi Mungu amfariji Rais Samia na familia yake, awape nguvu katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho ya Hafidh Ameir Hassan mahali pema peponi," akaongeza Rais Ruto. Bado viongozi wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania walikuwa wakiendelea kutuma rambirambi kwa familia ya Rais Samia.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 02:55:30
Mackenzie na wenzake kujua hatima yao mwezi huu
MSHUKIWA wa mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie, na washtakiwa wenzake wanatarajiwa kujua hatima yao mwezi huu katika kesi inayohusu vifo vya watoto 191. Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa mwaka mmoja baada ya kesi hiyo kuanza Septemba mwaka uliopita. Mackenzie anakabiliwa na mashtaka hayo pamoja na washtakiwa wengine 30, ambao upande wa mashtaka umedai walihusika sana katika vifo vya watoto hao. Kesi hiyo ilikuwa ya aina yake, huku Biblia, Quran na Katiba zikitajwa kwa kina na upande wa mashtaka pamoja na washtakiwa katika juhudi zao za kutetea misimamo yao. Washtakiwa walitumia aya za Biblia kuhalalisha kukaa kwao msituni na vifo vilivyofuata, huku upande wa mashtaka ukirejelea Biblia kuonyesha kwamba hata wakati wa Yesu Kristo, aina fulani za dawa zilikuwepo za kukabiliana na magonjwa na dharura, na kwamba watu hawakutegemea maombi pekee kwa ajili ya uponyaji. Wakati mmoja, kesi ya mauaji ya Shakahola iligeuka kuwa kama darasa la thiolojia, huku maswali yakiibuliwa kuhusu iwapo wale wanaodaiwa kufunga hadi kufa kwa imani kwamba wangeenda mbinguni na kukutana na Yesu, kwa hakika wako mbinguni. Hata hivyo, hakukuwa na jibu la moja kwa moja, kwani hakuna aliyeweza kusema kwa uhakika ni hatima gani iliyowakuta wale waliokufa njaa. Wakati mwingine, Mackenzie alitaka upande wa mashtaka kuthibitisha kwamba wale anaodaiwa kuwaua kupitia kufunga hawako mbinguni. Upande wa mashtaka ulipuuza maswali hayo na kuyataja kuwa ni masuala ya kithiolojia, ukisisitiza kwamba lengo lake halikuwa kuamua masuala ya imani, bali kuthibitisha vipengele vya uhalifu katika hatia ziliosababisha maafa hayo. Upande wa mashtaka umeomba Mahakama Kuu kuamua Mackenzie ana hatia ya mauaji, ukisema umethibitisha kikamilifu kwamba vifo vilitokea, chanzo chake, jukumu la Mackenzie katika kuvisababisha, pamoja na hali yake ya akili wakati huo. Kulingana na upande wa mashtaka, ushahidi wa kisayansi wa uchunguzi wa miili na vipimo vya baada ya kifo ulithibitisha kuwa njaa ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya vifo miongoni mwa waathiriwa wengi. "Ingawa sababu ya kifo cha baadhi ya miili haikuweza kubainishwa kimatibabu kwa sababu ilikuwa imeoza sana au kubaki mifupa pekee, mahakama inaweza kuhitimisha kwamba nao walikufa kwa njaa kutokana na mazingira yaliyozunguka vifo hivyo," alisema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina. Ushahidi uliowasilishwa na Serikali ulionyesha kuwa asilimia 48.9 ya miili yote iliyochunguzwa, wakiwemo watu wazima na watoto, walikufa kutokana na njaa, huku sababu ya kifo kwa asilimia 45.9 ikiwa haikubainika. Hata hivyo, washtakiwa wamejitetea kwamba ingawa kesi hiyo kuwa imezungukwa na msiba, imejaa majonzi na hisia nzito, mahakama si jukwaa la maombolezo, bali ni kitengo vha haki, kinachohitaji ushahidi. Kupitia kwa wakili wao Lawrence Obonyo, washtakiwa walisema kutokea kwa kifo pekee, hata kama ni cha kusikitisha kiasi gani, hakumaanishi moja kwa moja kwamba washtakiwa wana hatia. Bw Obonyo aliitaka mahakama isiruhusu uzito wa janga la Shakahola kufunika kile alichokitaja kuwa udhaifu na mapengo katika ushahidi wa upande wa mashtaka. Upande wa mashtaka uliita mashahidi 120 kuthibitisha kesi yake, huku washtakiwa wakiita mashahidi zaidi ya 21 kujitetea.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 01:55:03
Ofisi 3 zinazohusishwa na Rais Ruto zafyonza Sh100 bilioni-ripoti
OFISI tatu zinazohusishwa na Rais William Ruto zilitumia Sh33 bilioni katika mwaka uliokamilika Juni 2026, kiwango cha juu zaidi kuwahi kutumiwa na ofisi za maafisa wakuu wa Serikali, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Wizara ya Fedha. Matumizi hayo ya ofisi za Rais William Ruto, Naibu Rais Kithure Kindiki na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi yanafanya jumla ya fedha zilizotumiwa na ofisi hizo tangu Kenya Kwanza iingie madarakani mwaka 2022 kufikia Sh100.23 bilioni. Kwa miaka minne, matumizi ya urais yamezidi Sh89.9 bilioni zilizotumiwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, katika miaka 10 ya uongozi. Ripoti ya Wizara ya Fedha kuhusu hali ya uchumi na bajeti ya mwaka wa kifedha 2025/26 inaonyesha Ikulu ilitumia Sh18.4 bilioni. Katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka huo, Aprili hadi Juni 2026, Ikulu ilitumia Sh6.8 bilioni. Hii ni sawa na wastani wa Sh570 milioni kwa wiki au Sh81.3 milioni kila siku. Katika kipindi hicho, Rais Ruto aliandaa shughuli mbalimbali katika Ikulu, huku maelfu ya watu wakifika katika hafla kadhaa. Miongoni mwa waliomtembelea Ikulu ni wanachama wa Maendeleo ya Wanawake mnamo Aprili 1, 2026, pamoja na viongozi wa mashinani kutoka kaunti mbalimbali. Mnamo Mei 11, Ikulu pia iliandaa karamu ya kitaifa kwa wajumbe wa Mkutano wa Africa Forward. Ikulu imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha tangu Rais Ruto aingie madarakani. Kati ya Julai 2022 na Juni 2026, ilitumia jumla ya Sh43 bilioni, sawa na asilimia 43 ya zaidi ya Sh100 bilioni zilizotumiwa na ofisi zilizo chini ya Urais. Katika robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha 2025/26, Ikulu ilitumia Sh4.56 bilioni. Kiasi hicho kilishuka hadi Sh3.17 bilioni katika robo ya pili, kabla ya kupanda hadi Sh3.85 bilioni katika robo iliyomalizika Machi 2026. Katika robo ya mwisho, matumizi yalipanda kwa karibu theluthi mbili hadi Sh6.83 bilioni. Kati ya Sh18.4 bilioni zilizotumiwa na Ikulu katika mwaka huo, Sh17.12 bilioni zilitumika katika shughuli za kawaida. Fedha hizo ziligharamia mishahara ya wafanyakazi, mafuta ya magari ya viongozi, marupurupu na tiketi za ndege za maafisa wanaosafiri ndani na nje ya nchi, pamoja na chakula cha wageni. Kwa mwaka huu wa kifedha, Ikulu imetengewa takriban Sh13.5 bilioni, ingawa kiasi hicho kinaweza kubadilika wakati wa marekebisho ya bajeti. Ofisi ya Rais ilifuata Ikulu kwa matumizi ya Sh8 bilioni. Kati ya kiasi hicho, Sh6.68 bilioni zilitumika katika shughuli za kawaida. Hii ni wastani wa Sh667.75 milioni kila mwezi au karibu Sh22 milioni kila siku. Ofisi ya Naibu Rais Kindiki ilitumia Sh5.2 bilioni, huku Sh100 milioni pekee zikitumika kwa shughuli za maendeleo. Kwa upande wake, Ofisi ya Mudavadi ilitumia Sh602 milioni, zote zikiwa za shughuli za kawaida. Idara ya Serikali ya Masuala ya Bunge ilitumia Sh433 milioni, huku Idara ya Serikali ya Masuala ya Baraza la Mawaziri ikitumia Sh226 milioni. Kwa jumla, matumizi ya ikulu, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Naibu Rais na Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri yalifikia asilimia 98 ya Sh32.9 bilioni zilizotumiwa na Urais. Mwaka wa kifedha 2024/25, Urais ulitumia Sh21 bilioni, chini ya Sh22.8 bilioni zilizotumiwa mwaka uliotangulia na Sh23.3 bilioni zilizotumika katika mwaka wa kwanza wa serikali ya Rais Ruto, 2022/23. Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema matumizi yote yaliidhinishwa na wabunge. Alisema ofisi zilizo chini ya urais hazitekelezi miradi moja kwa moja, bali zinahusika zaidi na sera, uratibu na kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Rais na Naibu Rais.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 07 Sep 2026 00:55:52
'Picha ya Bikira Maria' kwenye ukuta jikoni yaibua gumzo Kisii
KATIKA vilima vya eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, nyumba ndogo ya udongo ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitumika kama jikoni sasa imegeuka kuwa kivutio cha mamia ya waumini na wadadisi. Ni katika kijiji cha Getare, Emenwa, ambako mkulima Mary Onsombi, ambaye ni Mkatoliki mcha Mungu, anasema aligundua picha inayofanana na Bikira Maria kwenye ukuta wa jikoni lake uliojaa weusi kutokana na moshi. Kilichoanza kama kivuli hafifu Ijumaa kilikuwa kimevutia maelfu ya wanakijiji kufikia Jumapili. Watu walifika kutoka maeneo mbalimbali, wakiwemo wahudumu wa bodaboda, wanafunzi na wahubiri wa madhehebu tofauti, wote wakitaka kujionea kile wanachokirejelea kama "Bikira Maria". Jirani yake, Gladys Nyandika, alisema Bi Onsombi aliona picha hiyo alipokuwa ameketi karibu na jiko lake. "Alifikiri ni moshi. Alichukua kipande cha kitambaa na kujaribu kuifuta. Kadri alivyoifuta, ndivyo ilivyozidi kudhihirika. Alisema picha hiyo ilifanana kabisa na sanamu ya 'Bikira Maria' aliye kanisani kwao," alisema. Jikoni humo hakuna jambo la kipekee. Kuna kuta za udongo zilizotiwa weusi na moshi wa kuni, jiko la mawe matatu na sufuria chache zilizoning'inizwa kwenye misumari. Lakini kwenye ukuta wa kaskazini, karibu futi tatu kutoka chini na eneo ambalo Bi Onsombi hupiga magoti anapopika, kuna umbo la kijivu-nyeupe lenye urefu wa takriban inchi 18. Kwa waumini, umbo hilo linafanana na mwanamke aliyevaa vazi refu na kufunika kichwa, huku mikono ikiwa kama yule anayeomba. Kwa wenye mashaka, huenda ni muundo uliotokana na moshi wa miaka mingi, maji kupenya ukutani na udongo kuchubuka. Jikoni hiyo sasa imegeuka kuwa mahali pa sala, huku watawa na waumini Wakatoliki wakisongamana ndani wakiwa na rozari mikononi. "Mungu akiamua kujionyesha, lazima uje uone, iwe wewe ni Mkatoliki au la," alisema mfuasi wa SDA aliyesafiri kutoka Nyamakoroto, Nyamira. Diwani wa Masige Mashariki, Michael Motume, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kutembelea boma hilo. Alisema aliona picha isiyo ya kawaida iliyofanana na sanamu maarufu ya Bikira Maria ya Kanisa Katoliki, lakini akasema hana mamlaka ya kuthibitisha iwapo ni muujiza. Kufikia Jumapili asubuhi, njia ya kuelekea kwa Onsombi ilikuwa imejaa watu. Baadhi walipiga magoti na kusali, huku wengine wakipiga picha na video kwa TikTok. Wahudumu wa bodaboda nao walipata biashara nzuri, wakitoza Sh100 kwa safari kutoka Emenwa Centre hadi Getare. Watawa waliofika eneo hilo hawakutoa maelezo mengi, lakini walionekana kuchukua picha na kuandika kumbukumbu, huenda kwa ajili ya kuwajulisha viongozi wa Kanisa Katoliki katika Dayosisi ya Kisii. Kanisa Katoliki bado halijatoa taarifa kuhusu madai hayo ya muujiza. Vyanzo vya kanisa vilisema halikimbilii kuthibitisha madai kama hayo. Mtaalamu mmoja wa kanisa alisema ripoti kama hizo zimewahi kutokea nchini, zikiwemo picha zinazoonekana kwenye miti na miamba, na nyingi baadaye kubainika kuwa matukio ya kawaida ya kimaumbile.
read moreRight Column Content