taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 16 Sep 2026 03:55:36
Ruto amshambulia Orengo, amtaka aache kuwa 'kibaraka wa Uhuru', ajiunge na serikali
KATIKA siku yake ya tatu ya ziara ya Nyanza, Rais William Ruto alipeleka mapambano yake ya kisiasa dhidi ya vuguvugu la Linda Mwananchi hadi Siaya, ngome ya Gavana James Orengo, akiwataka wapigakura kukataa vyama vipya ambavyo alisema havijathibitisha uwezo wao wa kuongoza nchi. Rais Ruto aliwataka wakazi kuunga mkono vyama vilivyo katika serikali jumuishi, akipuuza vyama vipya ambavyo bado havijasajiliwa rasmi. Alisema vyama hivyo havina uzoefu, mtandao wa kitaifa wala mipango thabiti ya kuongoza Kenya. Ziara yake Siaya ilikuwa na umuhimu wa kisiasa, hasa kwa kuwa viongozi wa Linda Mwananchi wanatarajiwa kuzuru eneo hilo siku chache zijazo. Rais Ruto pia alimshambulia Gavana Orengo kwa kuhusishwa na vuguvugu hilo, akimtaka badala yake kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo Siaya. "Namwambia Orengo aache kundi hilo linaloitwa Linda Sponsors au Linda Sponyo na ajiunge nami katika safari hii ya maendeleo na kujenga hospitali. Je, ninyi watu mlimchagua ajiunge na Linda Sponsors? Kwa nini anaruhusu kuwa kibaraka wa kisiasa na kutumiwa na rais mstaafu?" Rais Ruto alisema. Pia alimshambulia Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akimlaumu kwa kuacha jukumu la kuwa kiongozi mstaafu na kuingia katika siasa za upinzani dhidi ya serikali yake. Rais Ruto alisema Bw Kenyatta alikuwa akiwafadhili wanasiasa wanaompinga baada ya kushindwa kutekeleza baadhi ya mipango aliyokuwa nayo katika sekta ya elimu na afya. Akizungumza alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Dhogoye, Siaya, Rais Ruto aliunganisha ujumbe wa maendeleo na siasa, akisema serikali jumuishi imefungua ukurasa mpya wa maendeleo katika Nyanza. "Serikali jumuishi ndiyo muungano pekee wenye uwezo wa kuunganisha taifa letu. Ndiyo yenye historia ya utekelezaji, maono ya kuaminika ya siku zijazo na mpango wa kushughulikia changamoto zinazokabili taifa," alisema. Alionya wapigakura dhidi ya kuunga mkono vyama vipya, akisema Kenya haiwezi "kujaribu" viongozi wasio na historia ya utekelezaji. "Taifa letu halitajaribu watu wanaofanya majaribio. Msicheze kamari na watu ambao hawana mpango au historia ya wazi ya kuwafanyia kazi wananchi," alisema. Rais Ruto pia alimwalika Mbunge wa Ugenya David Ochieng, ambaye anaongoza chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG), kujiunga na serikali jumuishi. Bw Ochieng alikubali ombi hilo, lakini akaomba Rais Ruto kumuunga mkono katika azma yake ya kumrithi Bw Orengo kama Gavana wa Siaya. Aliahidi kumpa Rais Ruto asilimia 99.9 ya kura za Ugenya katika uchaguzi wa 2027 iwapo atapata uungwaji mkono huo. "Nimefurahia kufanya kazi nawe, Mheshimiwa Rais, kwa sababu umekuwa rafiki mzuri. Umetusaidia kuendeleza Ugenya... ndiyo maana tutakupa asilimia 99.9 ya kura zetu," alisema Bw Ochieng. Viongozi walioandamana na Rais Ruto walitumia ziara hiyo kumshambulia Gavana Orengo, ambaye hakuwa kwenye ziara hiyo. Waziri wa Kawi na Petroli Opiyo Wandayi alisema viongozi wengi wa Siaya wameungana isipokuwa mmoja, akimtaja Bw Orengo. "Rais Ruto, tuachie Orengo sisi. Tutahakikisha anaenda nyumbani," alisema Bw Wandayi. Gavana wa Homa Bay na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga pia alimshambulia Bw Orengo, akimtaka aache kupotosha jamii ya Luo. Naibu Gavana wa Siaya William Oduol alijitangaza kuwa kaimu gavana kutokana na kutohudhuria kwa Bw Orengo. Rais Ruto alitaja miradi kadhaa ya maendeleo ambayo serikali imepanga kutekeleza Siaya. Alisema ujenzi wa barabara ya kilomita 500 inayozunguka Ziwa Victoria utaanza Novemba 2026, baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya miaka 15. Barabara hiyo itaunganisha Busia na Muhuru Bay kaunti ya Migori kupitia Siaya, Kisumu na Homa Bay. Aidha, Sh32 bilioni zitatumika kujenga kilomita 400 za barabara mpya Siaya. Rais Ruto pia alisema Sh10 bilioni zimetengwa kwa uchumi wa baharini, ikiwemo utafiti na teknolojia ya uzalishaji wa samaki wachanga, gati nne, huduma za feri na vituo vya uokoaji.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Kituo kipya cha huduma za uwekezaji Nyali kufaidi Pwani
Benki ya Standard Chartered imefungua kituo kipya cha huduma za kifedha cha Priority Centre katika eneo la Nyali, Mombasa, hatua inayolenga kuwahudumia wateja wenye uwezo mkubwa wa kifedha katika eneo la Pwani. Kituo hicho kitatoa huduma maalumu za ushauri kuhusu uwekezaji, upangaji wa mali, ufadhili, uhifadhi wa utajiri na mipango ya kurithisha mali vizazi vijavyo. Benki hiyo imesema hatua hiyo inalenga kuwaleta karibu wananchi wa Pwani na fursa za uwekezaji wa kimataifa kupitia mtandao wake mkubwa duniani. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,Birju Sanghrajka, Mkurugenzi Mkuu wa Standard Chartered Kenya, alisema Mombasa imeendelea kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi nchini kutokana na ukuaji wa biashara, utalii, usafirishaji na viwanda. Alibainisha kuwa uchumi wa kaunti hiyo una thamani ya zaidi ya Sh700 bilioni, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma za kifedha za hali ya juu. Kwa upande wake, Edith Chumba, Mkuu wa Huduma za Utajiri wa Standard Chartered Kenya na Afrika Mashariki, alisema wateja wengi wanahitaji ushauri unaovuka mipaka ya uwekezaji wa kawaida ili kuwasaidia kujenga, kuhifadhi na kuhamisha utajiri wao kwa vizazi vijavyo. Kauli hiyo pia ilionyesha kuwa Mombasa inaendelea kuimarika kama kitovu cha biashara na uwekezaji. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, Bandari ya Mombasa ilihudumia tani milioni 22.3 za mizigo, huku tani 566,400 zikisafirishwa kwa reli. Aidha, zaidi ya wageni wa kimataifa 96,700 waliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huo. Kituo kipya cha Nyali kinaongeza uwepo wa huduma za Priority Banking za Standard Chartered nchini Kenya, huku benki hiyo ikilenga kupanua huduma zake kwa wateja wenye utajiri mkubwa nje ya Nairobi na kuwapa fursa za kifedha kutoka shirika la kimataifa
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 5 hours ago
Sifuna ngangari licha ya misukosuko ya kupata chama
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na shinikizo la kupata chama atakachotumia kuwania urais katika uchaguzi wa 2027, huku pia akishughulikia tofauti za kisiasa ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi. Timu yake iko katika Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), ikipinga uamuzi wa kuhifadhi jina la "Linda" kwa mtu mwingine. Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa upinzani wanamtaka Bw Sifuna awe mgombea mwenza wa kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, katika uchaguzi huo. Hata hivyo, ndani ya Linda Mwananchi kuna viongozi wenye mipango tofauti ya kisiasa, hali inayotishia umoja wa vuguvugu hilo. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesajili The Mwananchi Party (TMP), huku Mbunge wa Saboti Caleb Amisi akiondoka na kuunda People's Renaissance Movement (PRM). Bw Sifuna pia ameingia kwenye mzozo na Bw Musyoka baada ya kiongozi huyo kuhifadhi jina la The Ukombozi Alliance (TUA) kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP). ORPP ilikataa ombi la upande wa Bw Sifuna kubadili jina la United Democratic Party (UDP) kuwa Ukombozi People's Party (UPP), ikisema jina hilo linafanana na TUA. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema suala la tarehe ya Oktoba 15 iliyowekwa na IEBC halimaanishi Bw Sifuna lazima awe tayari na chama kufikia siku hiyo. Alisema tarehe muhimu kisheria ni Februari 2027, wakati wagombea watapaswa kuwa wanachama wa chama kwa angalau miezi sita kabla ya uchaguzi. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alisema timu hiyo tayari imekubaliana kuhusu chama kitakachotumiwa na Bw Sifuna na kwamba kitazinduliwa Oktoba 3. Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka alisema maandalizi ya uzinduzi yanaendelea na akakanusha madai kwamba Bw Sifuna atakuwa mgombea mwenza wa Bw Musyoka. Alisema mazungumzo pia yanaendelea na chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu uwezekano wa ushirikiano. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema licha ya kushindwa kupata jina la Ukombozi, Linda Mwananchi itaendelea na mipango yake na Bw Sifuna atasalia kuwa mgombea wake wa urais. Alisema chama kipya kitazinduliwa kikiwa na nembo na rangi zinazohusishwa na Linda Mwananchi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Tunataka hivi: Wadau wa elimu wapendekeza mabadiliko makubwa katika Mswada wa elimu 2026
WADAU wa elimu wanataka mabadiliko makubwa katika Mswada wa Elimu ya Msingi wa 2026, ikiwemo kuimarishwa kwa ushiriki wa wazazi, mfumo wa elimu wa 2-6-3-3 kukitwa katika sheria na serikali kubeba kikamilifu gharama ya elimu ya msingi. Mswada huo unapendekeza kuchukua nafasi ya sheria iliyopo kuhusu elimu ya msingi na unahusu usimamizi wa shule, ufadhili, ustawi wa wanafunzi, walimu, ubora wa elimu na data za elimu. Katika mapendekezo yao kwa Bunge kuhusu miswada ya Elimu ya Msingi na Elimu ya Juu, Uteuzi na Ufadhili wa Wanafunzi ya 2026, wadau pia wanataka wazazi wapewe mamlaka zaidi kisheria na mfumo wa usimamizi wa vifaa vya kufunza ufanyiwe mabadiliko. Kundi la Elimu Bora Working Group (EBWG) limehoji sababu za kuwasilisha miswada hiyo kabla ya sera mpya ya kitaifa ya elimu kuidhinishwa. Kundi hilo linataka mfumo wa 2-6-3-3 — miaka miwili ya elimu ya chekechea, sita ya msingi, mitatu ya sekondari msingi na mitatu ya sekondari pevu — uwekwe wazi kwenye sheria. Linasema kuacha mfumo huo uamuliwe kupitia kanuni kunaweza kupatia serikali ijayo nafasi ya kubadilisha mfumo wa elimu bila kuhitaji sheria mpya. EBWG pia inataka vigezo vya kuwaweka wanafunzi katika mikondo ya shule ya upili viwekwe wazi, ikiwemo matokeo, maslahi, uwezo na hatua za kuwasaidia wanafunzi kutoka makundi yaliyotengwa. Kuhusu ufadhili, kundi hilo linataka serikali iwajibike kikamilifu kugharamia miundomsingi, vifaa vya kufunza, chakula, usafi na mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu. Linasema mianya inayoruhusu shule kutoza "ada za ziada" inaweza kutumiwa kurejesha ada kwa jina jingine. Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) nacho kinataka kitambuliwe kikamilifu kisheria na kupewa uwezo wa kumiliki mali, kuajiri wafanyakazi, kuendesha akaunti na kushtaki au kushtakiwa kwa jina lake. NPA pia kinataka miundo yake ya uwakilishi kuanzia shuleni hadi kitaifa ihifadhiwe na neno PTA libadilishwe kuwa Parents Associations. Shirika la Education Stakeholders Association of Kenya (ESAK) limependekeza pia lipewe nafasi ya kuteua mwakilishi katika kila Bodi kati ya 47 za Elimu za Kaunti. ESAK linasema wadau wengi wa elimu wameachwa nje ya bodi hizo licha ya kuwa na mchango muhimu katika usimamizi wa elimu ya msingi. Kuhusu elimu ya juu, EBWG inataka serikali iwafadhili kikamilifu wanafunzi na wanafunzi wa mafunzo ya ufundi, huku ufadhili huo ukijumuisha karo, malazi, chakula, vifaa, usafiri, afya na utafiti. Pia linataka mikopo, ruzuku, ufadhili wa masomo na basari zitofautishwe wazi na wanafunzi waendelee kupata ufadhili hadi watakapokamilisha masomo yao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Kindiki asihi mlima kumwamini aupeleke 'canaan'
NAIBU wa Rais Kithure Kindiki amewaomba wapiga kura wa Mlima Kenya wamwamini kuwaongoza katika mazungumzo ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Prof Kindiki alisema eneo hilo linahitaji umoja na ajenda ya maendeleo ili kupata manufaa zaidi kisiasa na kiuchumi. Akizungumza Maragua alipokagua ujenzi wa barabara ya Gwathamaki-Mbombo yenye urefu wa kilomita 16 kwa thamani ya Sh1 bilioni, Prof Kindiki alisema Mlima Kenya unapaswa kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umeungana. "Mlima ni mmoja. Ajenda ni maendeleo. Thamani ni mazungumzo ya pamoja yanayolenga mwananchi bila kupoteza mwelekeo wa miradi ya maendeleo. Niaminini niwafanyie mazungumzo. Nia yangu ni ustawi wa watu wetu na utulivu wa taifa," alisema. Alisema wakosoaji wa Rais William Ruto wanaodai kuwa aliahidi mengi hawatafanikiwa, akisisitiza kuwa serikali itaonyesha matokeo kupitia miradi ya maendeleo. Prof Kindiki alizungumza siku nne baada ya kundi la wazee wa Mlima Kenya kumteua kuwa msemaji mkuu wa eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027. Hata hivyo, uteuzi huo umezua mgawanyiko miongoni mwa wazee, hasa upande wa magharibi wa Mlima Kenya. Mlezi wa Kiama Kia Ma, Kung'u Muigai, na mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Kikuyu, Wachira Kiago, wamekataa kutambua mkutano wa Kirigiti Stadium, Kiambu, wakisema haukuwa na uhalali wala ushawishi unaodaiwa. Profesa Kindiki aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuepuka siasa za hisia na badala yake kuzingatia utawala na maendeleo. Alisema pia eneo hilo halipaswi kujitenga kisiasa, bali linapaswa kushirikiana na Wakenya wengine katika kutafuta mustakabali bora wa nchi. Naibu Rais alisema serikali imetenga Sh56 bilioni kujenga takriban kilomita 1,200 za barabara za lami katika Kaunti ya Murang'a. Alisema wakulima pia wananufaika kutokana na ongezeko la bei za mazao, akitaja kahawa ambayo bei yake imeongezeka kutoka Sh50 hadi Sh130 kwa kilo na maziwa kutoka Sh35 hadi Sh50 kwa lita. Alisema bei ya mbolea imeshuka kutoka Sh7,000 hadi Sh2,000 kwa gunia, huku mbegu ya mahindi iliyothibitishwa ikishuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo. Prof Kindiki pia alitaja miradi ya umeme, masoko ya mazao, nyumba za gharama nafuu, mabweni ya wanafunzi na vituo vya ICT miongoni mwa miradi inayoendelea Murang'a.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 8 hours ago
Mbunge afichua ODM ilivyozima nyota ya PAA ya Kingi
AFISA wa zamani wa ngazi ya juu katika chama cha Spika wa Seneti Amason Kingi, Pamoja African Alliance (PAA), amefichua matukio yaliyopelekea chama hicho kuamua hakitakuwa na wagombeaji katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Mbunge wa Ganze, Bw Kenneth Tungule, ambaye alikuwa katibu mkuu wa chama hicho, amelaumu siasa za ushirikiano wa ODM na UDA kwa kudhoofisha PAA. Kulingana naye, baadhi ya viongozi wa Pwani walimshinikiza Rais William Ruto kukivunja chama hicho baada ya kuhisi wangekumbwa na ushindani mkali kwa vile PAA ilikuwa imeanza kuvutia wanasiasa wenye ushawishi. Chama hicho kilitangaza uamuzi wake usio wa kawaida Machi, huku Bw Kingi akisisitiza kuwa chama hicho hakikuvunjwa, bali hakitawasilisha wagombea katika uchaguzi ujao. "Rais Ruto hakushinikiza kuvunjwa kwa PAA, kama watu wengi wanavyodai. Rais alikuwa akipokea shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hili, hasa viongozi waliohisi kuwa PAA ilikuwa ikiingia katika ngome yao. Unajua ni chama gani ninachomaanisha. Kwa sababu Pwani imekuwa ngome ya chama fulani kwa miongo kadhaa," alisema Bw Tungule katika mahojiano ya redio. Baadhi ya maafisa wake waliondoka na kuunda chama kingine kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Leba, Bw Kazungu Kambi. Wanasiasa kadha waliojiunga na chama hicho, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa, walilazimika kujipanga upya. Bi Jumwa, ambaye ana azma ya kuwania ugavana, alikuwa ameondoka UDA baada ya kubaini kuwa viongozi wa chama hicho Kilifi walikuwa wakimpigia debe Gavana Gideon Mung'aro wa ODM. Baadaye alirejea UDA kabla ya kuhama tena kutafuta chama kingine upande wa upinzani. Katika mwaka wa 2022, PAA ilishinda viti vitatu vya ubunge, kupitia kwa Bw Tungule, Bw Gonzi Rai wa Kinango na Anthony Kenga wa Rabai, pamoja na viti kadhaa vya udiwani. Pwani imekuwa ngome ya ODM kwa muda mrefu, ambapo aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, hayati Raila Odinga, alikuwa na ushawishi mkubwa. Chama hicho kinashinikiza ugawaji wa maeneo ya kisiasa kama sehemu ya makubaliano ya kabla ya uchaguzi na UDA, na uwepo wa vyama vidogo vya Kenya Kwanza vinavyowasilisha wagombea katika maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome zake ungeathiri nia hiyo. Mbunge wa Ganze alisema maafisa wa PAA walisafiri hadi Nairobi kukutana na Rais na kutoa hoja dhidi ya kuvunjwa kwa chama hicho. "Tulipokutana naye, tulimweleza jinsi tulivyohisi kuhusu kuvunjwa kwa chama. Tulimwambia kuwa hatua hiyo ingeenda kinyume na maslahi yake. Lakini msukumo kutoka upande mwingine ulikuwa mkubwa zaidi," alisema mbunge huyo wa muhula wa kwanza. Bw Tungule alisema aliendelea kupinga kuvunjwa kwa chama hicho akiwa katibu mkuu, lakini akatambua kuwa maafisa wengine wa chama walikuwa tayari wamekubali uamuzi huo. "Rais angepata kura nyingi zaidi kitaifa. Watu wengi wangetoka kuunga mkono wagombea wao, na mwishowe, tungekusanya kura nyingi zaidi kwa urais," alisema. Mbali na Bi Jumwa, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo pia alikuwa amejiunga na PAA. Bw Mbogo, ambaye anapanga kuwania ugavana wa Mombasa, sasa amejiunga na chama cha Jubilee kilicho upande wa upinzani. Awali, Bw Kingi aisema Rais Ruto alikuwa amehisi mgawanyiko wa vyama ndani ya Kenya Kwanza unaweza kuathiri uwezo wa kushinda viti vingi uchaguzini.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Jubilee hakukaliki Kioni na Matiang'i waking'ang'ania kiti cha Kenyatta
Mabadiliko ya uongozi katika Chama cha Jubilee yamezua vita vipya vya kuwania usukani wa chama hicho, huku uteuzi wa Dkt Fred Matiang'i kushika hatamu ukishindwa kuzima mjadala kuhusu nani anafaa kukiongoza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Sasa mchuano huo unaelekea Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC), ambapo aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, amesema wajumbe ndio wanaopaswa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo Dkt Matiang'i ataendelea kuwa kiongozi wa chama au nafasi hiyo ichukuliwe na Naibu Kiongozi wa Chama, Jeremiah Kioni. Bw Kioni Jumatano alikataa kueleza wazi msimamo wake kuhusu iwapo atampinga Dkt Matiang'i katika mkutano huo. "Tunahitaji mahojiano maalum," alisema Bw Kioni alipohojiwa kuhusu hatua yake ya kukosa kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Jubilee (NEC) kilichofanyika Jumanne na iwapo atachuana na Dkt Matiang'i kwenye NDC. Kimya chake kilijiri siku moja baada ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kukabidhi uongozi wa chama kwa Dkt Matiang'i, hatua ambayo bado inasubiri kuidhinishwa rasmi na wajumbe katika NDC. Kwa mujibu wa maafisa wa chama, ni Dkt Matiang'i na Beatrice Gambo pekee, ambaye ni Naibu Kiongozi wa Chama anayesimamia mikakati, waliohudhuria hafla hiyo kutoka makundi mawili ya manaibu viongozi wa chama. Kutokuwepo kwa Bw Kioni kulivutia hisia, hasa kwa kuzingatia kwamba amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa kiongozi wa Jubilee anafaa kuchaguliwa na wajumbe badala ya kuteuliwa kupitia makubaliano ya viongozi wa juu. Mrengo wake sasa unatarajiwa kuongeza juhudi za kushawishi wajumbe kabla ya NDC inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba. Hali hiyo imezua mapambano ya kipekee ya kisiasa ambapo Dkt Matiang'i ni mgombea wa urais wa Jubilee na wakati huohuo kiongozi wa muda wa chama, huku Bw Kioni akiendelea kuhudumu kama naibu kiongozi mwenye ushawishi ndani ya chama. Na Bw Wambugu ameweka wazi msimamo wake. "Matiang'i hakuwa chaguo langu la kwanza kuwa kiongozi wa chama, ingawa ndiye mgombea wangu ninayempendelea wa urais. Mimi nilimpendelea Kioni. Lakini ninaweza kukubali uamuzi huu hadi NDC ambayo Uhuru amesema itafanyika karibuni, halafu tuone wajumbe watasema nini," alisema. Msimamo huo unatenganisha nafasi mbili ambazo zimeonekana kufungamana ndani ya Jubilee: uongozi wa chama na uteuzi wa mgombea wa urais. Jubilee ilimuidhinisha Dkt Matiang'i kuwa mgombea wake wa urais mnamo Oktoba mwaka jana, wakati ambao Bw Kioni alikuwa Katibu Mkuu wa chama. Dkt Matiang'i pia aliteuliwa kuwa Naibu Kiongozi wa Chama. Hatua hiyo ilionekana kumweka Dkt Matiang'i katikati ya juhudi za kufufua chama hicho. Hata hivyo, azma ya Bw Kioni kutwaa uongozi wa chama imeibua kitovu kingine cha mamlaka. Katibu mkuu huyo wa zamani wa chama amekuwa akisisitiza kuwa kiongozi wa Jubilee anapaswa kuibuka kupitia mchakato wa NDC badala ya kukabidhiwa madaraka moja kwa moja. Kutokana na hali hiyo, Jubilee sasa inakabiliwa na swali gumu: Je, mgombea wa urais wa chama anapaswa kuwa kiongozi wa chama moja kwa moja, au wajumbe ndio wanafaa kuamua ni nani atakayeshikilia nafasi hiyo? Bw Wambugu, ambaye amehusika katika migogoro kadhaa ya ndani ya Jubilee, ameibuka kama mmoja wa watu wanaopinga vikali dhana kwamba Dkt Matiang'i anapaswa kurithi moja kwa moja nafasi ya Bw Kenyatta. Katika barua yake ya wazi kwa Dkt Matiang'i Jumanne, alimpongeza kwa kuaminiwa kushika usukani wa chama, lakini akasisitiza kuwa uamuzi huo bado unategemea idhini ya NDC. Aliwataka viongozi wapya wa chama kutoa ratiba wazi ya mkutano huo na hatua zitakazofuatwa kabla yake, ishara kwamba vita vya kuwania ushawishi ndani ya chama vinaweza kuwa vikali. "NDC inatoa fursa ya kutatua masuala yaliyosalia kuhusu uongozi, kurekebisha miundo ya chama panapohitajika, kufanya upya mamlaka ya viongozi wa kitaifa na kuwapa wanachama nafasi ya kuamua mwelekeo wa chama chao kupitia wajumbe wao," alisema. Aidha, alionya dhidi ya maamuzi yasiyofuata taratibu rasmi za chama, akisema masuala yanayowahusu wanachama na wanaotaka kugombea yanafaa kushughulikiwa kupitia vyombo vinavyotambulika kikatiba. Msimamo huo unaendana na hoja ya awali ya Bw Kioni kwamba Jubilee ni chama cha kitaifa na viongozi wake wanapaswa kuchaguliwa na wajumbe. NDC sasa imeibuka kuwa uwanja mkuu wa mapambano ya kisiasa ndani ya Jubilee wakati chama hicho kinajaribu kurekebisha miundo yake kufuatia miezi kadhaa ya migogoro ya ndani na kesi mahakamani. Jaribio kubwa la kwanza kwa Dkt Matiang'i linaweza kuwa mgogoro ambao haujatatuliwa kuhusu nafasi ya Katibu Mkuu wa chama. Hivi majuzi, Mahakama ya Migogoro ya Vyama vya Kisiasa ilibatilisha uteuzi wa Moitalel Ole Kenta kama Katibu Mkuu wa Jubilee, ikisema hakutimiza masharti ya uanachama wakati wa uteuzi wake. Ingawa Jubilee imepinga uamuzi huo na kuahidi kutumia njia za kisheria kuupinga, Bw Wambugu amesema chama kinafaa kurekebisha utaratibu uliotumika badala ya kuendeleza mzozo huo. "Suala lililo mbele yetu si Kenta kama mtu binafsi. Ni mchakato wa kujaza nafasi ya Katibu Mkuu," alisema. Kwa Dkt Matiang'i, mgogoro huo ni mtihani wa mapema wa uwezo wake wa kurejesha imani ya wanachama katika taasisi za chama akijiandaa kwa NDC na uchaguzi wa 2027. Katika hafla ya Jumanne, Bw Kenyatta na Dkt Matiang'i walisisitiza umuhimu wa umoja ndani ya chama na kuwataka wanachama kuacha kutegemea mahakama kutatua migogoro ya ndani. "Tusiendelee kurudisha chama nyuma kupitia kesi za mahakamani. Tuungane na vyama vyenye malengo sawa," alisema Bw Kenyatta. Dkt Matiang'i naye alitoa wito wa kutatua migogoro kupitia miundo ya chama. "Tafadhali tusikimbilie mahakamani. Tuna mifumo ya kutatua matatizo yetu ndani ya chama," alisema. Hata hivyo, vita vya Jubilee si kuhusu nyadhifa pekee. Chama hicho bado kina mtandao wa kitaifa wa kisiasa, chapa inayotambulika na ufadhili wa umma. Kwa mwaka wa kifedha wa 2026/27, Jubilee imetengewa Sh128.86 milioni kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa. Ingawa kiwango hicho kimeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ambayo Jubilee ilikuwa mojawapo ya vyama vikuu nchini, udhibiti wa chama bado una umuhimu mkubwa. Udhibiti huo huamua nani atasimamia miundo ya chama, wanachama, michakato ya uteuzi wa wagombea na nafasi ya chama katika mazungumzo ya miungano kuelekea uchaguzi wa 2027. Ndiyo maana ushindani kati ya Dkt Matiang'i na Bw Kioni unaweza kuwa muhimu zaidi kadri NDC inavyokaribia. Ingawa Bw Kenyatta ameachia rasmi uongozi wa chama, amesema ataendelea kuwa mwanachama na mshauri mwandamizi. Hata hivyo, uwepo wake una maana kwamba mabadiliko hayo hayawezi kuonekana tu kama kubadilishwa kwa viongozi. Bado ana ushawishi mkubwa ndani ya historia na mtandao wa kisiasa wa Jubilee.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Jiandaeni vya kutosha El Nino huja na magonjwa, kaunti zaonywa
Katika maeneo mbalimbali nchini, Wakenya wanaangalia anga kwa hofu na matumaini, kama walivyofanya wakati wa misimu mikubwa ya El Niño ya 1997, 2015 na 2023. Hata hivyo, mwaka huu tahadhari imeongezeka baada ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya (KMD) kutangaza kuwa kuna uwezekano wa asilimia 81 wa kutokea kwa El Niño kali, huku kukiwa na asilimia 97 ya mvua kuendelea hadi miezi ya kwanza ya mwaka 2027. Kwa Wizara ya Afya, utabiri huo si jambo la kupuuzwa. Katibu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, amewaandikia magavana wote wa kaunti akiwatahadharisha kujiandaa kukabiliana na magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo, malaria na homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever), ambayo huongezeka wakati wa mafuriko. Wizara hiyo ilikumbusha kuwa katika msimu wa El Niño wa 2023-2024, watu 175 walifariki dunia, 40 wakatoweka na 242 kujeruhiwa. Zaidi ya watu 384,000 walihamishwa makwao na kuwekwa katika kambi 170 za muda. Aidha, vituo 64 vya afya viliathiriwa na kushindwa kutoa huduma kutokana na mafuriko. Bi Muthoni alisema kaunti zote zinapaswa kuwa tayari kwa kiwango cha chini, huku zile zinazokabiliwa na hatari kubwa ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa na utapiamlo zikichukua hatua za haraka zaidi. Kaunti zilizotajwa kuwa na hatari kubwa ya mafuriko ni pamoja na Mandera, Wajir, Marsabit, Garissa, Kitui, Makueni, Machakos, Lamu, Kilifi, Kwale, Tana River, Taita Taveta na Mombasa. Maeneo mengine yaliyo katika hatari ni Budalang'i, Kano na Tana Delta. Ripoti hiyo pia imeonya kuhusu hatari ya homa ya Bonde la Ufa katika kaunti za Marsabit, Wajir, Isiolo, Mandera na Garissa, hasa maeneo yaliyo karibu na mito na mabwawa yanayofurika. Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa, David Koros, alisema mvua ya Oktoba hadi Desemba itachochewa na mchanganyiko wa El Niño na hali ya joto katika Bahari ya Hindi, jambo linalotarajiwa kuongeza kiwango cha mvua nchini. Wakati huohuo, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema linajiandaa kwa hali ambayo huenda ikawa mbaya zaidi kuliko misimu iliyoshuhudiwa katika miongo miwili iliyopita. Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Stephen Muleshe, alisema changamoto kubwa inayotarajiwa ni milipuko ya magonjwa yanayoenezwa kupitia maji machafu, majeraha yatokanayo na mafuriko na kuvurugika kwa huduma za lishe na afya. Msimu mbaya zaidi wa El Niño nchini Kenya unasalia ule wa 1997-1998, uliosababisha vifo vya takriban watu 2,000, kuathiri zaidi ya watu milioni 1.5 na kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na uharibifu wa barabara, madaraja, mifugo na miundombinu mingine. Wataalamu sasa wanaonya kwamba ikiwa maandalizi hayatatiwa maanani, mvua inayotarajiwa zinaweza kuathiri afya, usafiri, kilimo na uchumi kwa kiwango kikubwa katika miezi ijayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Amerika yamezea mate madini ya Kenya bila kuficha
Amerika imeongeza hamu yake katika madini muhimu ya Kenya wakati ambapo serikali ya Rais William Ruto inataka kuendeleza uwezo wa kuchakata madini ndani ya nchi badala ya kuyauza nje yakiwa ghafi. Suala hilo lilijitokeza kwa uzito wakati wa mkutano kati ya Rais Ruto na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika, Marco Rubio, Septemba 21, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, viongozi hao wawili walijadili diplomasia ya biashara pamoja na amani na usalama wa kikanda, huku madini muhimu yakitajwa kama eneo kuu la ushirikiano wa kiuchumi. Waziri huyo alitafutia kampuni za Amerika nafasi ya kushiriki katika sekta hiyo. "Walizungumza kuhusu jinsi fursa zilizopo katika madini muhimu nchini Kenya zinavyoweza kuweka nchi kama mhusika muhimu katika sekta hiyo huku zikifungua nafasi kwa kampuni za Amerika kuongeza thamani ya bidhaa hizo," alisema msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Tommy Pigott. Majadiliano hayo yamejiri chini ya wiki mbili baada ya afisa mkuu wa Amerika kusema kuwa Washington iko tayari kusaidia Kenya kuendeleza viwanda vinavyohusiana na migodi ya madini muhimu. Hatua hizi zinaashiria kuongezeka kwa maslahi ya kibiashara ya Amerika katika madini ya Kenya na Afrika kwa jumla huku ikitafuta kupunguza uwezo wa China. Mapema mwezi huu, Naibu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika anayeshughulikia masuala ya Afrika, Frank Garcia, alisema wanataka kampuni za Amerika kuwekeza katika uchakataji wa madini, mafunzo kwa wafanyakazi, uhamishaji wa teknolojia na viwanda vinavyoweza kuibuka kutokana na hazina za madini nchini Kenya. Bw Garcia alisema utawala wa Rais Donald Trump uko tayari kusaidia Kenya kujenga mitambo ya usindikaji wa madini na kusisitiza kuwa kampuni za Amerika zinataka kushiriki katika kuongeza thamani ya madini badala ya kuyachimba na kuyasafirisha nje moja kwa moja. Mwelekeo huo mpya umefanya madini ya Kenya kuwa na mvuto mkubwa kimataifa. Katika eneo la Pwani, madini adimu kama niobium yaliyopo katika Kilima cha Mrima, Kaunti ya Kwale, yamevutia kampuni kadhaa za kimataifa huku Kenya ikitafakari jinsi ya kuendeleza rasilimali hiyo. Madini mengine kama titanium, chromite, coltan na manganese pia yamegunduliwa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Pwani, ikiwemo kaunti za Tana River na Kilifi. Madini ya adimu hutumika katika utengenezaji wa bidhaa nyingi za teknolojia ya hali ya juu, huku niobium ikitumika kutengeneza vifaa vinavyotumika katika sekta za anga, silaha na matumizi mengine ya viwandani. Mbali na Amerika, kampuni za Australia pia zimeonyesha nia ya kufanya utafiti wa madini katika Kilima cha Mrima. Eneo hilo linakadiriwa kuwa na akiba ya madini adimu yenye thamani ya takriban Sh8 trilioni na niobium yenye thamani ya takriban Sh4.5 trilioni. Waziri wa Madini Hassan Joho, ambaye ni sehemu ya ujumbe wa Kenya mjini New York, alisisitiza msimamo wa serikali wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa Africa Minerals Strategy Group kuhusu maendeleo ya madini muhimu barani Afrika. "Msimamo wa Kenya uko wazi. Hatuwezi kukubali kuondolewa kwa madini yetu bila kuongeza thamani hapa nchini. Madini yetu, lithiamu, shaba na niobium lazima yasafishwe na kuchakatwa nchini kabla ya kusafirishwa nje ili manufaa yaongezeke, teknolojia ihamishwe na ajira za kitaalamu zibaki Afrika," alisema Joho. Aliongeza kuwa ongezeko la mahitaji ya madini muhimu limeweka Afrika katika nafasi ya kipekee ndani ya uchumi wa kimataifa wa madini na kupatia fursa ya kuwa mhusika mkuu katika mifumo ya usambazaji duniani. Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika ilisema mjadala kuhusu madini muhimu ni sehemu ya uhusiano mpana wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, ikitaja Kenya kama mshirika muhimu asiye mwanachama wa NATO na wa biashara anayekua kwa kasi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 11:22:17
Wachezaji wa Harambee Stars wagoma kufanya mazoezi kulalamikia kutolipwa posho
Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, wamesusia mazoezi kuelekea mechi yao ya kwanza ya Kundi D ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 dhidi ya Eritrea, iliyopangwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Nyayo. Taarifa zinaonyesha kuwa kikosi hicho kiliripoti kambini jijini Nairobi Jumanne, lakini wachezaji walikataa kufanya mazoezi wakidai kulipwa marupurupu yao pamoja na kuboreshwa kwa maslahi wakichezea timu ya taifa. Mkuu wa Miradi na Timu za Taifa katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Athanus Obango, alisema Jumatano kuwa wachezaji wanadai posho za mechi za Senegal na Lesotho ambazo bado hawajalipwa. "Suala ni kwamba posho za mechi ya Senegal zimechelewa sana kulipwa, na pia wanataka posho za mechi ya Lesotho. Kila mchezaji anadaiwa takriban Sh80,000," alisema Obango. Aliongeza kuwa jukumu la kulipa posho za wachezaji ni la serikali na si FKF, huku akielezea matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi haraka. "Baadhi ya wanaogoma kwa sasa hawakuwa hata kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Lesotho na Senegal. Wanasema wanaonyesha mshikamano na wenzao," alisema. Mchezaji mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina alisema ni wachache tu katika kikosi cha sasa walioshiriki mechi hizo mbili na wana haki ya kulipwa posho zao. "Hata hivyo, ninavyojua, baadhi yao wanachochewa na watu wa nje wanaotaka kudhoofisha timu ya taifa katika vita vyao dhidi ya uongozi wa FKF. Mimi si sehemu ya mgomo huo," alisema mchezaji huyo. Kenya ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Lesotho Juni 4 na Juni 27 mwaka huu katika Uwanja wa Lukas Moripe mjini Johannesburg, Afrika Kusini, ikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza kabla ya kupokea kichapo cha 4-1 katika pambano la pili. Mnamo Novemba 8, 2025, Harambee Stars pia ilipokea kichapo cha mabao 8-0 kutoka kwa Senegal katika mechi nyingine ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mardan Sports Complex mjini Antalya, Uturuki. Kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy wa Afrika Kusini, anatarajiwa kuzungumza na wanahabari baadaye Jumatano kuhusu mgomo huo wa wachezaji. Wiki iliyopita McCarthy alitangaza kikosi cha wachezaji 24, wengi wao wakicheza soka ya kulipwa nje ya nchi, kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Eritrea. Baada ya mechi ya Eritrea, Kenya itasafiri kucheza dhidi ya Guinea mjini Conakry Oktoba 1. Timu nyingine katika kundi hilo ni Afrika Kusini. Wakati huo huo, Eritrea iliwasili nchini Jumanne na imekuwa ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Police Sacco. Kenya, ambayo ni mwenyeji mwenza wa Afcon 2027, tayari imejihakikishia nafasi ya kushiriki fainali hizo na inashiriki mchujo huo ili kudumisha kiwango cha ushindani na utimamu wa wachezaji wake. Si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Harambee Stars kugoma kutokana na malipo ya posho. Tukio maarufu lilitokea mwaka 2005 wakati timu hiyo iligoma kusafiri kwenda Kigali, Rwanda, kwa michuano ya Kombe la Cecafa Senior Challenge kutokana na kutolipwa marupurupu yao. Ingawa suala hilo lilitatuliwa baadaye, timu iliondolewa katika mashindano hayo baada ya kuchelewa kuwasili.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 08:51:28
Wawili wafariki, sita wajeruhiwa basi likigonga lori Kwale
Watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Mghalani kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Tarafa Ndogo ya Samburu, Lydia Mambo, basi la Dreamline lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Mombasa liligonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara kati ya Mackinnon na Taru, Kaunti ya Kwale. Bi Mambo alithibitisha kuwa mmoja wa waliofariki alikuwa abiria aliyekwama ndani ya basi hilo. "Lori hilo lilikuwa limeharibika barabarani na dereva wake hakuwa ameweka alama zozote za tahadhari, jambo ambalo huenda lilichangia ajali hiyo kulingana na matokeo yetu ya awali ya uchunguzi," alisema. Maafisa wa polisi walifika haraka eneo la tukio na kuwaokoa abiria, huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Kwa mujibu wa Bi Mambo, eneo la tukio tayari limeshughulikiwa na magari hayo mawili kuvutwa hadi Kituo cha Polisi cha Taru huku uchunguzi ukianza. Afisa wa Utekelezaji wa Sheria za Trafiki katika Ukanda wa Pwani, Asha Wario, amewatahadharisha madereva wanaotumia barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Mombasa-Nairobi kuwa waangalifu na kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za trafiki. "Ningependa kuwasihi madereva wawe waangalifu kwa sababu nyingi ya ajali hizi hutokea asubuhi. Hii ina maana kuwa hutokea kutokana na mwonekano hafifu unaosababishwa na manyunyu ya mvua za asubuhi," alisema Bi Wario. Alisisitiza kuwa madereva watakaopatikana wakikiuka sheria za trafiki watafikishwa mahakamani, akiongeza kuwa juhudi pia zinaendelea za kuelimisha madereva wa mabasi na malori kuhusu usalama barabarani.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 09:00:46
Hesabu za Gachagua zinavyozidi kuwa ngumu mlimani
Hesabu za kisiasa za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 zinazidi kuwa ngumu kutokana na swali moja muhimu - iwapo ataruhusiwa kugombea au atalazimika kusalia nje ya debe na kujadiliana kisiasa kutoka pembeni. Hatima yake kisiasa inahusishwa moja kwa moja na mapambano yake ya kisheria kufuatia kutimuliwa kwake afisini Oktoba 2024. Ingawa Mahakama Kuu ilikataa kufutilia mbali uamuzi wa Seneti wa kuidhinisha kuondolewa kwake madarakani, iliamua kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa. Gachagua amekata rufaa. Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, suala hilo si kuhusu uwezo wake wa kugombea tu, bali pia kuhusu ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya, ambako amekuwa akijijenga kama kinara mkuu wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto. Iwapo mahakama haitafungua njia yake ya kugombea, Gachagua atakabiliwa na uamuzi mgumu. Mchambuzi wa siasa Steve Ngari anasema kumuunga mkono mgombea wa upinzani ambaye hana mizizi ya Mlima Kenya kunaweza kupunguza uwezo wake wa kushawishi eneo hilo kuunga mkono muungano huo na pia kudhoofisha nafasi yake ya kujadiliana ndani ya muungano unaoongozwa na viongozi kutoka maeneo mengine. Kwa upande mwingine, akimuunga mkono mwanasiasa mwingine kutoka Mlima Kenya kuwania urais, huenda akasaidia kuibua mpinzani mpya ambaye baadaye atachukua nafasi yake ya ushawishi katika eneo hilo. Mambo yanazidi kuwa magumu kutokana na uwezekano mkubwa wa Naibu Rais Kithure Kindiki kubaki katika tiketi ya Kenya Kwanza kama mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027. Wafuasi wa serikali mlimani wamekuwa wakitumia uwepo wa Profesa Kindiki kama hoja kwamba eneo hilo bado linawakilishwa katika kazi ya juu serikalini na hivyo halijatengwa kisiasa. Kindiki mwenyewe ameonya kuwa eneo hilo linaweza kushushwa hadhi katika upinzani. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa, amesema kuwa baada ya Ruto, nafasi inayofuata ya uongozi wa taifa inaweza kwenda kwa Mlima Kenya, ilhali katika upinzani eneo hilo linaweza kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata nafasi kama hiyo. Rais Ruto pia ameonyesha hadharani kumuunga mkono naibu wake, hali inayowapa wapinzani changamoto ya kueleza kwa nini Mlima Kenya unapaswa kujitenga na tiketi ya Ruto-Kindiki. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema vita vya kisiasa vinavyoibuka si kuhusu nani atakuwa mgombea wa upinzani pekee, bali nani atawakilisha na kujadiliana kwa niaba ya maslahi ya Mlima Kenya. Swali hilo limezidi kuwa tata kutokana na kuibuka kwa wanasiasa kadhaa kutoka eneo hilo wanaotajwa kuwa na uwezo wa kuathiri hesabu za kisiasa za Gachagua. Miongoni mwao ni Seneta wa Nyandarua John Methu, ambaye ni mmoja wa washirika wake wa karibu na Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP). Tangu Gachagua aanze safari yake za kisiasa nje ya nchi, Methu ameonekana kuchukua jukumu kubwa katika shughuli za chama hicho. Kuna minong'ono kwamba Gachagua anaweza kumteua Methu kama sura ya Mlima Kenya katika tiketi ya upinzani iwapo yeye mwenyewe hataidhinishwa kugombea. Hata hivyo, wakili Chris Omore anaonya kuwa kumpandisha hadhi mwanasiasa mwingine kunaweza kuunda kituo kipya cha nguvu za kisiasa ambacho baadaye kinaweza kumpokonya Gachagua ushawishi wake. Mjadala huo pia unaeleza umuhimu wa kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi, ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania urais na amekutana mara kadhaa na Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro. Kwa mujibu wa wakili Nelson Osiemo, Wanjigi ni tofauti na Methu kwa sababu tayari anajitokeza kama mgombea wa urais mwenye mtandao wake wa kisiasa wa kitaifa. Ikiwa upinzani hatimaye utachagua mgombea kutoka nje ya Mlima Kenya, Wanjigi anaweza kuwa mgombeaji kutoka eneo hilo. Hilo linaibua swali iwapo Gachagua atamuunga mkono, atashirikiana naye kisiasa au ataendelea kusukuma DCP kama chombo kikuu cha upinzani Mlima Kenya. Gachagua mwenyewe amesema yuko tayari kumuunga mkono yeyote atakayeshinda mchakato wa uteuzi wa mgombeaji wa upinzani. Lakini si rahis hata. Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameanzisha chama cha People's Party of Kenya (PPK) na ameanza kampeni ya kitaifa ya kujenga chama hicho. Hatua hiyo imeibua kituo kingine cha ushawishi katika Mlima Kenya. Aidha, juhudi za Gachagua kutaka vyama vya kisiasa vya eneo hilo viungane chini ya DCP zimepata upinzani kutoka kwa viongozi kama Peter Munya, Justin Muturi na Lenny Kivuti, ambao wanasisitiza kuwa vyama vinaweza kushirikiana bila kuvunjwa. Kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua naye anaendelea kuwa moja ya sauti muhimu za kisiasa kutoka Mlima Kenya, huku mgombea wa Jubilee Fred Matiang'i akionekana kuongeza ushindani ndani ya upinzani. Huku viongozi kama Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakitajwa katika tiketi ya upinzani, swali kuu linasalia jinsi muungano huo utakavyovutia kura za Mlima Kenya bila kumpa mmoja wa viongozi wa eneo hilo nafasi ya juu kwenye tiketi. Kwa Gachagua, huo ndio mtihani mkubwa. Akiidhinishwa kugombea, atawaomba wapigakura wa Mlima Kenya wamuunge mkono moja kwa moja. Lakini akizuiwa, atalazimika kuamua ni nani atakayebeba matarajio ya kisiasa ya eneo hilo. Wachambuzi wanasema ikiwa ataweza kuunganisha maslahi ya Methu, Wanjigi, Nyoro, Karua, Munya na Muturi chini ya mradi mmoja wa upinzani, bado atabaki na ushawishi mkubwa hata bila kuwapo kwenye karatasi ya kura.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 07:55:19
Jinsi wakulima wamejipanga kuepuka hasara ya mvua kubwa ijayo ya El Nino
JANET Omollo, mkulima katika eneo la Nyatike, Kaunti ya Migori, ameshuhudia mengi katika shughuli zake za kilimo. Miongoni mwa changamoto alizokumbana nazo, ni kutovuna mazao ya kutosha licha ya kutumia muda wake mwingi shambani, kupanda mbegu bora na hata kuweka mbolea akilenga kuboresha mazao yake ya mpunga, mahindi, maharagwe na nyanya. Akiwa mkulima wa kutegemea mvua, anasema kuwa wakati mwingi, mvua huchelewa au hata kunyesha kwa wingi zaidi na kuharibu mazao hayo shambani. "Kama sasa nimepanda maharagwe kwenye ekari mbili za shamba. Tayari, nimepanga kuwa mazao nitakayovuna, nitauza na kutumia pesa hizo kumlipia mwanangu karo shuleni," anasema. Lakini kwa sasa matumaini yake ni kuwa, kufikia wakati ambapo mvua ya El Nino itaanza, atakuwa amevuna maharagwe yake. Hii ni kwasababu maharagwe huathiriwa na mvua nyingi, na yeye tofauti na wenzake, alipanda mapema. "Kutokana na mabadiliko ya hali ya anga, niligundua kuwa ni vyema kwetu wakulima kupanda pindi tu mvua ya kwanza inaponyesha baada ya mavuno yaliyotangulia kinyume na hapo awali ambapo nilikuwa nikisubiri mvua ya muda mrefu. Hii imenisaidia sana kwani ukija nyumbani kwangu, hutakosa chakula kama mahindi, maharagwe na njugu kwenye ghala langu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani," anaeleza Janet. Kaunti ya Migori ni miongoni mwa sehemu kadhaa nchini ambazo zitapokea kiasi kikubwa cha mvua wakati wa El Nino. Mkulima huyu anasema kuwa kutolewa kwa taarifa hiyo mapema kumemsaidia kujiandaa ili kuepuka hasara. "Tulianza kupokea taarifa kuhusu El Nino wiki kadhaa kabla ya kuvuna mazao yetu ya msimu uliotangulia. Kwa vile huwa nakodisha shamba ninalofanyia kilimo, msimu huu nimekodisha shamba kwenye sehemu ambazo hazina historia ya kupata mafuriko hapa Migori. Hii ni mojawapo ya juhudi zangu za kujiandaa ili kuzuia hatari za mvua ya El Nino shambani," mkulima huyo anasema. Wakati uo huo, anasema kuwa msimu huu, amesusia kupanda mpunga kwa sababu kilimo chake hutegemea unyunyiziaji wa maji badala ya mvua. Hivyo kupanda mpunga wakati wa El Nino kungempa hasara kubwa. Yeye huuza zao hilo Uganda. "Mwaka wa 2023 wakati kulikuwa na mvua nyingi ndipo pia nilikuwa natarajia kuvuna mpunga lakini mvua ilikuwa ikinyesha usiku na mchana. Hivyo nilipata hasara ya asilimia kumi kutoka kwenye kilimo cha mpunga kwa sababu mashini ya kuvuna haingeingia shambani kutokana na matope mengi ambayo yalikuwa yakisababisha mashine hiyo kuharibika. Ilibidi tucheleweshe kuvuna hadi mvua ilipopungua," anaeleza Janet. Katika eneo la Bonde la Ufa, ambapo maporomoko na mvua ya mawe hushuhudiwa wakati wa mvua nyingi kama ya El Nino, mkulima Norah Khamuye ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Gotabet nurseries, anasema kuwa mvua hiyo itakayoshuhudiwa kati ya mwezi wa Oktoba na Desemba mwaka huu, itashuhudiwa wakati ambapo miche anayopanda ya parachichi na makadamia itakuwa kwenye hatua muhimu ya kutoa maua. "Wakati wa mvua kubwa miaka miwili iliyopita, tuliathirika sana kwa sababu hatukuwa na vyandarua na neti za kukinga miche yetu kwenye mvua. Hivyo basi, mvua kubwa iliharibu miche yetu yote iliyokuwa kwenye bustani ya miche ya miti," anasimulia Norah. Huku mvua ya El Nino ikitarajiwa wiki chache zijazo, Norah sasa anasema kuwa pamoja na wenzake, wameweka vyandarua na neti kama juhudi zao za kuzuia hasara kama waliyopata mwaka huu. Aidha ana imani kuwa hatua hiyo pia itakinga miche dhidi ya wadudu na hali mbaya ya hewa wakati wa mvua hiyo inayokisiwa kuwa itakuwa nyingi sana sehemu hiyo ya Bonde la Ufa. "Tunatarajia kuvuna miche yetu kati ya mwezi wa Februari na Machi mwakani. Hiyo ina maana kuwa bila hatua hiyo ya kuhakikisha kuwa tumekinga bustani ya miche ya miti, basi El Nino hii inayo uwezo wa kutuletea hasara kubwa sana. Hiyo ndiyo sababu tumechukua hatua madhubuti mapema," anaeleza mkulima huyo. Hata hivyo, wakulima tofauti wakiweka juhudi za kudhibiti hasara, kuna hofu pia ya upungufu wa chakula wakulima wakiepuka kukuza mazao fulani kutokana na El Nino. Pia sehemu kadhaa nchini zilipata hasara kubwa sana kwenye msimu uliopita kutokana na kiangazi kilichoshuhudiwa kati ya mwezi wa Aprili na Mei. Haya ni kwa mujibu wa Geoffrey Wanjala kutoka shirika wakuzaji nafaka la Cereal Growers Association. "Kwa bahati mbaya, tunaelekea hatari nyingine ya njaa kwa sababu wakulima waliopanda kuchelewa watavuna wakati wa mvua. Kwanza, watavuna kidogo kwa sababu ya kiangazi na pia hicho kidogo kitaharibika kutokana na ukosefu wa jua la kutosha kuyakausha mahindi yao ambayo yataoza na kuathiri viwango na ubora wa mazao yao. Watakapopeleka mazao hayo kwenye soko, wanunuzi watakataa kuyanunua," anaeleza mtaalamu huyo. Wakati uo huo, Wanjala anawashauri wakulima watakaovuna mazao yao wakati wa mvua kutumia mashini za kukausha mazao na kisha kuhifadhi mahindi hayo kwenye mifuko maalum inayosaidia kuhifadhi nafaka vizuri. "Pia tunaona nafasi nzuri sana kwa wakulima kutokana na El Nino kwani wakulima wanaweza kutumia mvua hiyo kubwa kupanda mazao ambayo yanakuwa haraka kama vile soya, alizeti na aina fulani ya mbegu za mahindi yanayokuwa chini ya miezi mitatu ili kulipia hasara ambayo wakulima wameshuhudia kutokana na kiangazi msimu uliopita," anashauri Wanjala. Kulingana na ripoti ya idara ya utabiri wa hali ya anga nchini, kuna uwezo wa zaidi ya asilimia 99 ya taifa kushuhudia mvua ya El Nino na asilimia 56 za nchi kushuhudia El Nino kali katika miezi yote ya Oktoba, Novemba na Disemba. Kaunti za Migori, Bungoma, Trans Nzoia, Nairobi, Wajir, West Pokot, Samburu na Marsabit ni miongoni mwa sehemu ambazo idara hiyo imetaja kushuhudia mvua zaidi ya kadri wakati wa El Nino.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 06:55:03
Wakazi wa Lamu walia kutoshirikishwa kikamilifu ujenzi wa kituo cha Dangote ukianza
MAANDALIZI ya kuanza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha kampuni ya Dangote katika Kaunti ya Lamu yameshika kasi, huku wakazi wakizidisha wito wa kutaka kushirikishwa kikamilifu na kutatuliwa masuala ya fidia za miradi mikubwa ya zamani. Jumatatu, wajumbe wa Kenya wakiongozwa na Rais William Ruto, walikutana na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Dangote Industries, pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Amerika. Rais Ruto alisema Kenya iko tayari kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda hicho cha ukanda wa Afrika Mashariki. "Tumejitolea kuhakikisha mradi huu wa kihistoria unatekelezwa huku tukihakikisha unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi," alisema Dkt Ruto. Jumanne, Naibu Rais Kithure Kindiki alithibitisha kuwa hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi huo imepangwa kufanyika Septemba 30. Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Prof Kindiki alisema maandalizi ya hafla hiyo yanaelekea kukamilishwa ili kuhakikisha inaendeshwa kwa hadhi inayostahili. Naibu Rais alisema viongozi wa nchi za ukanda huu wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo pamoja na jamii za Lamu. "Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu utatusaidia kuunda nafasi za ajira 50,000 katika eneo hili. Pia tunafurahia kwa sababu mradi huu utawezesha jamii za Lamu na eneo la Pwani kupitia uundaji wa ajira na fursa nyingine," aliongeza. Wiki iliyopita, Rais Ruto alisema shughuli za ujenzi wa kiwanda hicho na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi Lamu huenda zikaendelea kwa wakati mmoja. Kauli hiyo ilizua malalamiko miongoni mwa wakazi wa Lamu wanaodai kuwa, bado kuna masuala ya fidia ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya mradi wa bomba hilo, huku wakitaka uwazi kuhusu mipango ya kiwanda hicho. Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari katika Ikulu ya Kisumu, Rais Ruto alisema serikali inashauriana na Dangote Group kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Turkana. Wakazi kupitia Chama cha Wakulima wa Kililana, kundi la kijamii linalowawakilisha wamiliki wa ardhi na wakazi wanaoishi hasa katika maeneo yanayopakana na sehemu za mradi wa Uchukuzi kati ya Bandari ya Lamu-South Sudan-Ethiopia (LAPSSET), wamehoji kwa nini mipango inaonekana kuendelea kwa kasi huku masuala muhimu yanayoathiri jamii yakiwa bado hayajatatuliwa. Katibu wao, Bw Mohamed Rajab, alitoa wito wa ushirikishwaji wa umma ili kutatua masuala ya fidia kabla ya hatua nyingine za mradi huo kuendelea. Bw Rajab alihoji kwa nini hadi sasa serikali imeendelea kuwa kimya kuhusu eneo ambako kiwanda cha mafuta cha Dangote kitajengwa Lamu. "Kwa nini serikali inawaacha wenyeji gizani kuhusu eneo halisi ambako kiwanda hiki kinachokusudiwa kitajengwa? Kwa nini ratiba inaendeshwa kwa haraka? Hakuna mtu ambaye amekuja kutueleza eneo hilo liko wapi," alisema Bw Rajab. Aliongeza kuwa bado kuna masuala ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba katika miaka iliyopita. "Ardhi yetu ilichukuliwa na hatukufidiwa. Tutatafuta haki mahakamani kuhusu masuala haya yote," alisema. Bw Mbwana Shee, Mwenyekiti wa Shungwaya Welfare Association, shirika la kijamii linalotetea haki za ardhi za jamii ya asili ya Bajuni huko Lamu, alielezea masikitiko kwamba kila mara serikali inapopanga kuwekeza katika mradi mkubwa kaunti hiyo, wenyeji huachwa nje ya maamuzi yanayogusa moja kwa moja maisha na riziki zao. Bi Raya Famau, mwanaharakati wa mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa Lamu Women Alliance, aliitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na mashauriano ya uwazi na jamii zote zilizoathirika.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 06:17:21
Trump ashambulia mahakama ya ICC, ataka nchi wanachama kujiondoa
Rais wa Amerika Donald Trump, Jumanne alitumia hotuba yake katika Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kushambulia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akitaka nchi wanachama wake kujiondoa mara moja katika taasisi hiyo aliyodai"haifuati sheria." Wakati huo huo, alitoa kauli kali dhidi ya Iran, akitishia kuiangamiza iwapo haitabadilisha mienendo yake. Katika hotuba yake iliyodumu takriban dakika 25 Jumanne, Trump alisema Amerika haitambui mamlaka yoyote ya ICC juu yake wala raia wake. Alisema Amerika haitaruhusu wanajeshi wake au raia wake kushtakiwa au kufanyiwa kesi na mahakama ambayo, kwa mujibu wake, haina mamlaka juu ya taifa hilo. Trump aliwaambia wajumbe kutoka mataifa 125 wanachama wa ICC waliokuwapo ukumbini kwamba wanapaswa kujiondoa rasmi kutoka mahakama hiyo. "Nahimiza nchi zote wanachama wa ICC kujiondoa mara moja katika taasisi hii ambayo imepoteza mwelekeo," alisema. Kauli hiyo ina uzito mkubwa kwa Kenya kutokana na historia yake na ICC. Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais William Ruto walishtakiwa mwaka 2012 kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-2008. Hata hivyo, mashtaka dhidi yao yalifutwa mwaka 2014 na 2015 baada ya changamoto za ushahidi na madai ya kuingiliwa kwa mashahidi. Kutokana na historia hiyo, mjadala kuhusu nafasi ya ICC nchini Kenya umeendelea kuwa mgumu kisiasa. Wachambuzi wanaona kuwa wito wa Trump wa nchi kujiondoa ICC unajiri wakati Rais Ruto amekuwa akiunga mkono kuimarishwa kwa taasisi za kimataifa badala ya kuzidhoofisha. Katika hotuba yake katika UNGA 81, Ruto alisisitiza kuwa changamoto kuu ya Afrika si ukosefu wa fedha, bali mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao unaweka vizuizi dhidi ya maendeleo ya bara hilo. Pia alirejelea wito wa muda mrefu wa Afrika kutaka uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Tofauti na Trump ambaye ameonyesha kutoamini taasisi za kimataifa, Ruto amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuzifanyia mageuzi ili ziwe na usawa zaidi kwa mataifa yanayoendelea. Wakati huo huo, Trump alielekeza mashambulizi yake kwa Iran kwa kuuliza ikiwa taifa hilo litachagua makubaliano yatakayoliwezesha kujijenga upya na kuwa moja ya mataifa makubwa duniani au likabiliwa na hatua kali kutoka Amerika. Alihoji ikiwa angekubali makubaliano ambayo yangeruhusu Iran kuimarika au kuiangamiza haraka ili isipewe nafasi ya kusababisha madhara kwa mataifa mengine. Trump alisema Amerika inaweza kusukuma Iran katika hali mbaya sana isiyokuwa na nafasi ya kupona wala kujenga mustakabali wake. Alipokuwa akitoa hotuba hiyo, baadhi ya wajumbe wa Iran waliondoka ukumbini alipokuwa akielezea operesheni za kijeshi dhidi ya taifa hilo katika miezi sita iliyopita. Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pamoja na Waziri wa Masuala ya Kigeni Abbas Araghchi, ambao walikuwa New York kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa, hawakuhudhuria kikao hicho wakati Trump akizungumza. Trump pia alitoa wito kwa mataifa yote duniani kushirikiana katika kuitenga Iran kiuchumi hadi ikome kushambulia usafirishaji wa kimataifa baharini, kusitisha mpango wake wa nyuklia na kuacha kuunga mkono ugaidi. Alidai kuwa uongozi wa Iran unaonyesha udhaifu na si nguvu, akisema taifa hilo ambalo awali lilikuwa na ushawishi mkubwa Mashariki ya Kati limepoteza nguvu zake. Aidha, alishutumu serikali ya Tehran kwa ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wake na kuonya kuhusu hatari ambayo ingekumba dunia iwapo Iran ingepata silaha za nyuklia. Trump alisema utawala wake ulijaribu kwanza njia ya mazungumzo kwa kupatia Iran nafasi ya ushirikiano kamili wa kiuchumi kwa sharti la kuacha mpango wake wa nyuklia na msaada kwa makundi ya kigaidi, lakini Tehran ilikataa pendekezo hilo. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Trump aligusia vita vya Ukraine akisema anaamini vita hivyo vinaweza kumalizika mapema kuliko wengi wanavyotarajia. Alisema Amerika inaendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Urusi na Ukraine na akaonyesha matumaini kuwa makubaliano ya kusitisha vita yatafikiwa ndani ya muda mfupi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Wed, 23 Sep 2026 05:55:56
Barua mbili zaibuka kuhusu usajili wa jina 'Ukombozi' linalogonganisha Sifuna na Kalonzo
BARUA mbili zinazokinzana zinazodaiwa kuhifadhi jina la 'Ukombozi' kwa makundi mawili tofauti zimeweka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) katikati ya mzozo mpya unaowahusu kiongozi wa Wiper Patriotic Movement Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Washirika wa Bw Sifuna jana walidai kulikuwa na njama baada ya Bw Musyoka kuzindua The Ukombozi Alliance (TUA), baada ya kufanikiwa kuhifadhi jina hilo katika ORPP. Bw Musyoka na viongozi wenzake wa upinzani wamebadilisha jina la Azimio La Umoja One Coalition kuwa TUA wanapojiandaa kwa uchaguzi wa urais wa 2027. Barua ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou ya Septemba 8, 2026 ilikataa ombi la kundi la Bw Sifuna la kubadilisha jina la United Democratic Party (UDP) kuwa 'Ukombozi People's Party (UPP),' ikisema linafanana na 'The Ukombozi Alliance (TUA). Bw Lorionokou alisema TUA lilihifadhiwa Julai 20, 2026. Hata hivyo, vuguvugu la Linda Mwananchi baadaye liliweka wazi barua nyingine ya ORPP ambayo inadaiwa kuidhinisha kuhifadhiwa kwa jina hilo na Bw Allan Akivaga. "Maombi yenu yamezingatiwa kwa mujibu wa sheria na jina Ukombozi People's Party (UPP) limeidhinishwa. Uhifadhi wa jina hilo utakuwa kwa kipindi kisichozidi siku 90 kuanzia tarehe ya barua hii," ORPP ilisema katika barua ya Machi 13, 2025. Katika mahojiano ya hivi majuzi na Taifa Leo, Bw Lorionokou alithibitisha kuwa UPP lilikuwa limehifadhiwa na Bw Akivaga. "UPP ni chama ambacho nadhani kiliomba mwezi Machi 2025 kuwa chama cha kisiasa na kimekuwa katika mchakato. Katika rekodi zangu, UPP ni jina lililohifadhiwa kwa chama cha kisiasa ambacho kiko katika mchakato wa kusajiliwa," Bw Lorionokou alisema. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema "mbinu za kuwapotosha watu zinazotumiwa na serikali" hazitazuia azma ya Bw Sifuna na akasema kundi hilo litakuwa na chama ifikapo Jumatatu ijayo. "Tumepoteza Ukombozi Party lakini hata mtoto wako akifa unaendelea kuishi na hilo ndilo tutakalofanya. Kuna vyama vingi sana kwa hivyo hatuna wasiwasi. Nataka kuwahakikishia wafuasi wetu kwamba chama kipya bado kitakuwa na nembo ya Linda Mwananchi na pia rangi zake. Hatujakata tamaa hata kidogo," Bw Oundo alisema. Hata hivyo, msemaji wa Wiper Ndegwa Njiru alimtetea Bw Musyoka dhidi ya madai kwamba anapanga njama dhidi ya Bw Sifuna. Alisema Bw Musyoka amekuwa akitumia kauli 'Komboa Kenya' tangu 2025. "Rekodi zinaonyesha kwamba mapema Aprili 2025, wakati Sifuna bado alikuwa Katibu Mkuu wa ODM, Musyoka alikuwa tayari ametumia na kutangaza kauli hiyo. Neno Ukomboa ndilo limezaa Ukombozi," Bw Njiru alisema. Kiongozi wa Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa pia aliambia Nation kwamba Azimio lilihifadhi jina hilo kabla ya Bw Natembeya kuanza mchakato wa kubadilisha jina la UDP. "Jina hilo tayari limeidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa. Tuliomba kuhifadhi The Ukombozi Alliance zamani kabla ya mpango wa kubadilisha jina la chama cha Jirongo kuwa Ukombozi People's Party," Bw Wamalwa alisema. Kuwepo kwa Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Suba South Caroli Omondi wakati wa uzinduzi wa muungano huo mpya pia kumekuwa kukichunguzwa kwa karibu na baadhi ya washirika wa Bw Sifuna. Gavana Orengo na Bw Omondi ni wanachama wa Linda Mwananchi. Hata hivyo, Bw Caroli pia ni Katibu Mkuu wa muungano wa Azimio, ambao sasa umepewa jina TUA. Taifa Leo imefahamu kuhusu mipango ya kumteua Bw Orengo kuchukua nafasi ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti wa muungano huo. Bw Kenyatta Jumanne alijiuzulu rasmi kama kiongozi wa Jubilee Party. Pia anatarajiwa kujiuzulu kama mwenyekiti wa muungano huo ili kutoa nafasi kwa mabadiliko zaidi. "Linda Mwananchi haitawahi kuwa sehemu ya Azimio na Edwin Sifuna bado ndiye mgombea wetu wa urais. Hakutakuwa na mchujo wa Orengo kwa sababu tumeamua mgombea wetu ni Sifuna," Bw Oundo alisema. "Orengo anaweza kuchukua nafasi yoyote katika Azimio lakini katika Linda Mwananchi tunajadili mambo kwanza kabla ya kuyaweka hadharani. Kwa hivyo Caroli na Orengo walipohudhuria mkutano wa Azimio, yaliyotokea huko si sehemu ya Linda Mwananchi na sisi si sehemu ya Azimio," mbunge huyo alisema.
read moreRight Column Content