T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 18 Sep 2026 05:55:21

Ruto amponda tena Uhuru akimlaumu kuvunja makubaliano ya 'Yangu kumi na Yako kumi'

RAIS William Ruto amemshambulia tena mtangulizi wake, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akimlaumu kwa kusaliti makubaliano ya kisiasa waliyofikia walipokuwa washirika na sasa kufadhili siasa za upinzani dhidi ya serikali yake. Dkt Ruto alisema yeye na Bw Kenyatta walikubaliana kuwa Rais huyo wa zamani angeongoza kwa miaka 10 kabla ya kumkabidhi yeye uongozi wa nchi kwa miaka mingine 10. Hata hivyo, alidai Bw Kenyatta alipuuza makubaliano hayo ulipofika wakati wake wa kugombea urais na badala yake akamuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022. "Hukutimiza. Badala yake, ulifanya kazi dhidi yangu," Rais alisema alipokuwa akizungumza Sindo. Dkt Ruto alisema alimuunga mkono Bw Kenyatta katika chaguzi nne na kusimama naye alipohitaji msaada wa kisiasa. "Nilikuunga mkono katika chaguzi nne na nikakulinda. Ulipofika wakati wako wa kunisaidia, hukufanya hivyo hata kwa siku moja. Lakini baadaye Mungu alinisaidia kuwa Rais wa watu wa Kenya," alisema. Hata hivyo, Rais alisema hamlaumu Bw Kenyatta kwa kutomuunga mkono, akisema ilikuwa haki yake ya kidemokrasia kumuunga mkono mgombea aliyemtaka. Lakini alimshutumu kwa kuhujumu serikali ya Kenya Kwanza na kufadhili siasa za upinzani. "Unashusha hadhi ya afisi ya Rais mstaafu. Unashusha hadhi yako mwenyewe kama mtu," alisema. Kauli hizo zilitolewa muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kuunga mkono sheria inayowazuia marais wastaafu kushikilia nyadhifa za uongozi katika vyama vya kisiasa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka madarakani. Hata hivyo, mahakama haikuwazuia kuwa wanachama wa vyama au kushiriki shughuli za kisiasa. Bw Kenyatta ametangaza ataacha uongozi wa Jubilee kufuatia uamuzi huo. Dkt Ruto pia alikosoa rekodi ya kiuchumi ya serikali iliyotangulia, akidai serikali yake ilirithi uchumi uliokuwa katika hali mbaya. "Tumelipa sehemu kubwa ya madeni na kupunguza mfumuko wa bei. Pia tumeongeza mara mbili akiba yetu ya fedha za kigeni," alisema. Alidai pia serikali yake imeajiri walimu 100,000, kujenga madarasa 23,000 na kufanya mabadiliko katika sekta ya afya. Kauli za Rais zilijiri akimaliza ziara ya siku tano Nyanza, ambapo alitembelea Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori, akizindua miradi na kutangaza mipango mingine ya thamani ya mabilioni ya pesa.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Wachezaji wa Harambee Stars wagoma kufanya mazoezi kulalamikia kutolipwa posho

Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, wamesusia mazoezi kuelekea mechi yao ya kwanza ya Kundi D ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 dhidi ya Eritrea, iliyopangwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Nyayo. Taarifa zinaonyesha kuwa kikosi hicho kiliripoti kambini jijini Nairobi Jumanne, lakini wachezaji walikataa kufanya mazoezi wakidai kulipwa marupurupu yao pamoja na kuboreshwa kwa maslahi wakichezea timu ya taifa. Mkuu wa Miradi na Timu za Taifa katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Athanus Obango, alisema Jumatano kuwa wachezaji wanadai posho za mechi za Senegal na Lesotho ambazo bado hawajalipwa. "Suala ni kwamba posho za mechi ya Senegal zimechelewa sana kulipwa, na pia wanataka posho za mechi ya Lesotho. Kila mchezaji anadaiwa takriban Sh80,000," alisema Obango. Aliongeza kuwa jukumu la kulipa posho za wachezaji ni la serikali na si FKF, huku akielezea matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi haraka. "Baadhi ya wanaogoma kwa sasa hawakuwa hata kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Lesotho na Senegal. Wanasema wanaonyesha mshikamano na wenzao," alisema. Mchezaji mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina alisema ni wachache tu katika kikosi cha sasa walioshiriki mechi hizo mbili na wana haki ya kulipwa posho zao. "Hata hivyo, ninavyojua, baadhi yao wanachochewa na watu wa nje wanaotaka kudhoofisha timu ya taifa katika vita vyao dhidi ya uongozi wa FKF. Mimi si sehemu ya mgomo huo," alisema mchezaji huyo. Kenya ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Lesotho Juni 4 na Juni 27 mwaka huu katika Uwanja wa Lukas Moripe mjini Johannesburg, Afrika Kusini, ikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza kabla ya kupokea kichapo cha 4-1 katika pambano la pili. Mnamo Novemba 8, 2025, Harambee Stars pia ilipokea kichapo cha mabao 8-0 kutoka kwa Senegal katika mechi nyingine ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mardan Sports Complex mjini Antalya, Uturuki. Kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy wa Afrika Kusini, anatarajiwa kuzungumza na wanahabari baadaye Jumatano kuhusu mgomo huo wa wachezaji. Wiki iliyopita McCarthy alitangaza kikosi cha wachezaji 24, wengi wao wakicheza soka ya kulipwa nje ya nchi, kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Eritrea. Baada ya mechi ya Eritrea, Kenya itasafiri kucheza dhidi ya Guinea mjini Conakry Oktoba 1. Timu nyingine katika kundi hilo ni Afrika Kusini. Wakati huo huo, Eritrea iliwasili nchini Jumanne na imekuwa ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Police Sacco. Kenya, ambayo ni mwenyeji mwenza wa Afcon 2027, tayari imejihakikishia nafasi ya kushiriki fainali hizo na inashiriki mchujo huo ili kudumisha kiwango cha ushindani na utimamu wa wachezaji wake. Si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Harambee Stars kugoma kutokana na malipo ya posho. Tukio maarufu lilitokea mwaka 2005 wakati timu hiyo iligoma kusafiri kwenda Kigali, Rwanda, kwa michuano ya Kombe la Cecafa Senior Challenge kutokana na kutolipwa marupurupu yao. Ingawa suala hilo lilitatuliwa baadaye, timu iliondolewa katika mashindano hayo baada ya kuchelewa kuwasili.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Wawili wafariki, sita wajeruhiwa basi likigonga lori Kwale

Watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Mghalani kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Tarafa Ndogo ya Samburu, Lydia Mambo, basi la Dreamline lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Mombasa liligonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara kati ya Mackinnon na Taru, Kaunti ya Kwale. Bi Mambo alithibitisha kuwa mmoja wa waliofariki alikuwa abiria aliyekwama ndani ya basi hilo. "Lori hilo lilikuwa limeharibika barabarani na dereva wake hakuwa ameweka alama zozote za tahadhari, jambo ambalo huenda lilichangia ajali hiyo kulingana na matokeo yetu ya awali ya uchunguzi," alisema. Maafisa wa polisi walifika haraka eneo la tukio na kuwaokoa abiria, huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Kwa mujibu wa Bi Mambo, eneo la tukio tayari limeshughulikiwa na magari hayo mawili kuvutwa hadi Kituo cha Polisi cha Taru huku uchunguzi ukianza. Afisa wa Utekelezaji wa Sheria za Trafiki katika Ukanda wa Pwani, Asha Wario, amewatahadharisha madereva wanaotumia barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Mombasa-Nairobi kuwa waangalifu na kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za trafiki. "Ningependa kuwasihi madereva wawe waangalifu kwa sababu nyingi ya ajali hizi hutokea asubuhi. Hii ina maana kuwa hutokea kutokana na mwonekano hafifu unaosababishwa na manyunyu ya mvua za asubuhi," alisema Bi Wario. Alisisitiza kuwa madereva watakaopatikana wakikiuka sheria za trafiki watafikishwa mahakamani, akiongeza kuwa juhudi pia zinaendelea za kuelimisha madereva wa mabasi na malori kuhusu usalama barabarani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Hesabu za Gachagua zinavyozidi kuwa ngumu mlimani

Hesabu za kisiasa za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 zinazidi kuwa ngumu kutokana na swali moja muhimu - iwapo ataruhusiwa kugombea au atalazimika kusalia nje ya debe na kujadiliana kisiasa kutoka pembeni. Hatima yake kisiasa inahusishwa moja kwa moja na mapambano yake ya kisheria kufuatia kutimuliwa kwake afisini  Oktoba 2024. Ingawa Mahakama Kuu ilikataa kufutilia mbali uamuzi wa Seneti wa kuidhinisha kuondolewa kwake madarakani, iliamua kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa. Gachagua amekata rufaa. Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, suala hilo si kuhusu uwezo wake wa kugombea tu, bali pia kuhusu ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya, ambako amekuwa akijijenga kama kinara mkuu wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto. Iwapo mahakama haitafungua njia yake ya kugombea, Gachagua atakabiliwa na uamuzi mgumu. Mchambuzi wa siasa Steve Ngari anasema kumuunga mkono mgombea wa upinzani ambaye hana mizizi ya Mlima Kenya kunaweza kupunguza uwezo wake wa kushawishi eneo hilo kuunga mkono muungano huo na pia kudhoofisha nafasi yake ya kujadiliana ndani ya muungano unaoongozwa na viongozi kutoka maeneo mengine. Kwa upande mwingine, akimuunga mkono mwanasiasa mwingine kutoka Mlima Kenya kuwania urais, huenda akasaidia kuibua mpinzani mpya ambaye baadaye atachukua nafasi yake ya ushawishi katika eneo hilo. Mambo yanazidi kuwa magumu kutokana na uwezekano mkubwa wa Naibu Rais Kithure Kindiki kubaki katika tiketi ya Kenya Kwanza kama mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027. Wafuasi wa serikali mlimani wamekuwa wakitumia uwepo wa Profesa Kindiki kama hoja kwamba eneo hilo bado  linawakilishwa katika kazi ya juu serikalini na hivyo halijatengwa kisiasa. Kindiki mwenyewe ameonya kuwa eneo hilo linaweza kushushwa hadhi katika upinzani. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa, amesema kuwa baada ya Ruto, nafasi inayofuata ya uongozi wa taifa inaweza kwenda kwa Mlima Kenya, ilhali katika upinzani eneo hilo linaweza kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata nafasi kama hiyo. Rais Ruto pia ameonyesha hadharani kumuunga mkono naibu wake, hali inayowapa wapinzani changamoto ya kueleza kwa nini Mlima Kenya unapaswa kujitenga na tiketi ya Ruto-Kindiki. Mchambuzi wa siasa Geoffrey Mboya anasema vita vya kisiasa vinavyoibuka si kuhusu nani atakuwa mgombea wa upinzani pekee, bali nani atawakilisha na kujadiliana kwa niaba ya maslahi ya Mlima Kenya. Swali hilo limezidi kuwa tata kutokana na kuibuka kwa wanasiasa kadhaa kutoka eneo hilo wanaotajwa kuwa na uwezo wa kuathiri hesabu za kisiasa za Gachagua. Miongoni mwao ni Seneta wa Nyandarua John Methu, ambaye ni mmoja wa washirika wake wa karibu na Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP). Tangu Gachagua aanze safari yake za kisiasa nje ya nchi, Methu ameonekana kuchukua jukumu kubwa katika shughuli za chama hicho. Kuna minong'ono kwamba Gachagua anaweza kumteua Methu kama sura ya Mlima Kenya katika tiketi ya upinzani iwapo yeye mwenyewe hataidhinishwa kugombea. Hata hivyo, wakili Chris Omore anaonya kuwa kumpandisha hadhi mwanasiasa mwingine kunaweza kuunda kituo kipya cha nguvu za kisiasa ambacho baadaye kinaweza kumpokonya Gachagua ushawishi wake. Mjadala huo pia unaeleza umuhimu wa kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi, ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania urais na amekutana mara kadhaa na Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro. Kwa mujibu wa wakili Nelson Osiemo, Wanjigi ni tofauti na Methu kwa sababu tayari anajitokeza kama mgombea wa urais mwenye mtandao wake wa kisiasa wa kitaifa. Ikiwa upinzani hatimaye utachagua mgombea kutoka nje ya Mlima Kenya, Wanjigi anaweza kuwa mgombeaji kutoka eneo hilo. Hilo linaibua swali iwapo Gachagua atamuunga mkono, atashirikiana naye kisiasa au ataendelea kusukuma DCP kama chombo kikuu cha upinzani  Mlima Kenya. Gachagua mwenyewe amesema yuko tayari kumuunga mkono yeyote atakayeshinda mchakato wa uteuzi wa mgombeaji wa upinzani. Lakini si rahis hata. Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameanzisha chama cha People's Party of Kenya (PPK) na ameanza kampeni ya kitaifa ya kujenga chama hicho. Hatua hiyo imeibua kituo kingine cha ushawishi katika Mlima Kenya. Aidha, juhudi za Gachagua kutaka vyama vya kisiasa vya eneo hilo viungane chini ya DCP zimepata upinzani kutoka kwa viongozi kama Peter Munya, Justin Muturi na Lenny Kivuti, ambao wanasisitiza kuwa vyama vinaweza kushirikiana bila kuvunjwa. Kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua naye anaendelea kuwa moja ya sauti muhimu za kisiasa kutoka Mlima Kenya, huku mgombea wa Jubilee Fred Matiang'i akionekana kuongeza ushindani ndani ya upinzani. Huku viongozi kama Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakitajwa katika tiketi ya  upinzani, swali kuu linasalia jinsi muungano huo utakavyovutia kura za Mlima Kenya bila kumpa mmoja wa viongozi wa eneo hilo nafasi ya juu kwenye tiketi. Kwa Gachagua, huo ndio mtihani mkubwa. Akiidhinishwa kugombea, atawaomba wapigakura wa Mlima Kenya wamuunge mkono moja kwa moja. Lakini akizuiwa, atalazimika kuamua ni nani atakayebeba matarajio ya kisiasa ya eneo hilo. Wachambuzi wanasema ikiwa ataweza kuunganisha maslahi ya Methu, Wanjigi, Nyoro, Karua, Munya na Muturi chini ya mradi mmoja wa upinzani, bado atabaki na ushawishi mkubwa hata bila kuwapo kwenye karatasi ya kura.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 8 hours ago

Jinsi wakulima wamejipanga kuepuka hasara ya mvua kubwa ijayo ya El Nino

JANET Omollo, mkulima katika eneo la Nyatike, Kaunti ya Migori, ameshuhudia mengi katika shughuli zake za kilimo. Miongoni mwa changamoto alizokumbana nazo, ni kutovuna mazao ya kutosha licha ya kutumia muda wake mwingi shambani, kupanda mbegu bora na hata kuweka mbolea akilenga kuboresha mazao yake ya mpunga, mahindi, maharagwe na nyanya. Akiwa mkulima wa kutegemea mvua, anasema kuwa wakati mwingi, mvua huchelewa au hata kunyesha kwa wingi zaidi na kuharibu mazao hayo shambani. "Kama sasa nimepanda maharagwe kwenye ekari mbili za shamba. Tayari, nimepanga kuwa mazao nitakayovuna, nitauza na kutumia pesa hizo kumlipia mwanangu karo shuleni," anasema. Lakini kwa sasa matumaini yake ni kuwa, kufikia wakati ambapo mvua ya El Nino itaanza, atakuwa amevuna maharagwe yake. Hii ni kwasababu maharagwe huathiriwa na mvua nyingi, na yeye tofauti na wenzake, alipanda mapema. "Kutokana na mabadiliko ya hali ya anga, niligundua kuwa ni vyema kwetu wakulima kupanda pindi tu mvua ya kwanza inaponyesha baada ya mavuno yaliyotangulia kinyume na hapo awali ambapo nilikuwa nikisubiri mvua ya muda mrefu. Hii imenisaidia sana kwani ukija nyumbani kwangu, hutakosa chakula kama mahindi, maharagwe na njugu kwenye ghala langu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani," anaeleza Janet. Kaunti ya Migori ni miongoni mwa sehemu kadhaa nchini ambazo zitapokea kiasi kikubwa cha mvua wakati wa El Nino. Mkulima huyu anasema kuwa kutolewa kwa taarifa hiyo mapema kumemsaidia kujiandaa ili kuepuka hasara. "Tulianza kupokea taarifa kuhusu El Nino wiki kadhaa kabla ya kuvuna mazao yetu ya msimu uliotangulia. Kwa vile huwa nakodisha shamba ninalofanyia kilimo, msimu huu nimekodisha shamba kwenye sehemu ambazo hazina historia ya kupata mafuriko hapa Migori. Hii ni mojawapo ya juhudi zangu za kujiandaa ili kuzuia hatari za mvua ya El Nino shambani," mkulima huyo anasema. Wakati uo huo, anasema kuwa msimu huu, amesusia kupanda mpunga kwa sababu kilimo chake hutegemea unyunyiziaji wa maji badala ya mvua. Hivyo kupanda mpunga wakati wa El Nino kungempa hasara kubwa. Yeye huuza zao hilo Uganda. "Mwaka wa 2023 wakati kulikuwa na mvua nyingi ndipo pia nilikuwa natarajia kuvuna mpunga lakini mvua ilikuwa ikinyesha usiku na mchana. Hivyo nilipata hasara ya asilimia kumi kutoka kwenye kilimo cha mpunga kwa sababu mashini ya kuvuna haingeingia shambani kutokana na matope mengi ambayo yalikuwa yakisababisha mashine hiyo kuharibika. Ilibidi tucheleweshe kuvuna hadi mvua ilipopungua," anaeleza Janet. Katika eneo la Bonde la Ufa, ambapo maporomoko na mvua ya mawe hushuhudiwa wakati wa mvua nyingi kama ya El Nino, mkulima Norah Khamuye ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Gotabet nurseries, anasema kuwa mvua hiyo itakayoshuhudiwa kati ya mwezi wa Oktoba na Desemba mwaka huu, itashuhudiwa wakati ambapo miche anayopanda ya parachichi na makadamia itakuwa kwenye hatua muhimu ya kutoa maua. "Wakati wa mvua kubwa miaka miwili iliyopita, tuliathirika sana kwa sababu hatukuwa na vyandarua na neti za kukinga miche yetu kwenye mvua. Hivyo basi, mvua kubwa iliharibu miche yetu yote iliyokuwa kwenye bustani ya miche ya miti," anasimulia Norah. Huku mvua ya El Nino ikitarajiwa wiki chache zijazo, Norah sasa anasema kuwa pamoja na wenzake, wameweka vyandarua na neti kama juhudi zao za kuzuia hasara kama waliyopata mwaka huu. Aidha ana imani kuwa hatua hiyo pia itakinga miche dhidi ya wadudu na hali mbaya ya hewa wakati wa mvua hiyo inayokisiwa kuwa itakuwa nyingi sana sehemu hiyo ya Bonde la Ufa. "Tunatarajia kuvuna miche yetu kati ya mwezi wa Februari na Machi mwakani. Hiyo ina maana kuwa bila hatua hiyo ya kuhakikisha kuwa tumekinga bustani ya miche ya miti, basi El Nino hii inayo uwezo wa kutuletea hasara kubwa sana. Hiyo ndiyo sababu tumechukua hatua madhubuti mapema," anaeleza mkulima huyo. Hata hivyo, wakulima tofauti wakiweka juhudi za kudhibiti hasara, kuna hofu pia ya upungufu wa chakula wakulima wakiepuka kukuza mazao fulani kutokana na El Nino. Pia sehemu kadhaa nchini zilipata hasara kubwa sana kwenye msimu uliopita kutokana na kiangazi kilichoshuhudiwa kati ya mwezi wa Aprili na Mei. Haya ni kwa mujibu wa Geoffrey Wanjala kutoka shirika wakuzaji nafaka la Cereal Growers Association. "Kwa bahati mbaya, tunaelekea hatari nyingine ya njaa kwa sababu wakulima waliopanda kuchelewa watavuna wakati wa mvua. Kwanza, watavuna kidogo kwa sababu ya kiangazi na pia hicho kidogo kitaharibika kutokana na ukosefu wa jua la kutosha kuyakausha mahindi yao ambayo yataoza na kuathiri viwango na ubora wa mazao yao. Watakapopeleka mazao hayo kwenye soko, wanunuzi watakataa kuyanunua," anaeleza mtaalamu huyo. Wakati uo huo, Wanjala anawashauri wakulima watakaovuna mazao yao wakati wa mvua kutumia mashini za kukausha mazao na kisha kuhifadhi mahindi hayo kwenye mifuko maalum inayosaidia kuhifadhi nafaka vizuri. "Pia tunaona nafasi nzuri sana kwa wakulima kutokana na El Nino kwani wakulima wanaweza kutumia mvua hiyo kubwa kupanda mazao ambayo yanakuwa haraka kama vile soya, alizeti na aina fulani ya mbegu za mahindi yanayokuwa chini ya miezi mitatu ili kulipia hasara ambayo wakulima wameshuhudia kutokana na kiangazi msimu uliopita," anashauri Wanjala. Kulingana na ripoti ya idara ya utabiri wa hali ya anga nchini, kuna uwezo wa zaidi ya asilimia 99 ya taifa kushuhudia mvua ya El Nino na asilimia 56 za nchi kushuhudia El Nino kali katika miezi yote ya Oktoba, Novemba na Disemba. Kaunti za Migori, Bungoma, Trans Nzoia, Nairobi, Wajir, West Pokot, Samburu na Marsabit ni miongoni mwa sehemu ambazo idara hiyo imetaja kushuhudia mvua zaidi ya kadri wakati wa El Nino.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Wakazi wa Lamu walia kutoshirikishwa kikamilifu ujenzi wa kituo cha Dangote ukianza

MAANDALIZI ya kuanza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha kampuni ya Dangote katika Kaunti ya Lamu yameshika kasi, huku wakazi wakizidisha wito wa kutaka kushirikishwa kikamilifu na kutatuliwa masuala ya fidia za miradi mikubwa ya zamani. Jumatatu, wajumbe wa Kenya wakiongozwa na Rais William Ruto, walikutana na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Dangote Industries, pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Amerika. Rais Ruto alisema Kenya iko tayari kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda hicho cha ukanda wa Afrika Mashariki. "Tumejitolea kuhakikisha mradi huu wa kihistoria unatekelezwa huku tukihakikisha unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi," alisema Dkt Ruto. Jumanne, Naibu Rais Kithure Kindiki alithibitisha kuwa hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi huo imepangwa kufanyika Septemba 30. Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Prof Kindiki alisema maandalizi ya hafla hiyo yanaelekea kukamilishwa ili kuhakikisha inaendeshwa kwa hadhi inayostahili. Naibu Rais alisema viongozi wa nchi za ukanda huu wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo pamoja na jamii za Lamu. "Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu utatusaidia kuunda nafasi za ajira 50,000 katika eneo hili. Pia tunafurahia kwa sababu mradi huu utawezesha jamii za Lamu na eneo la Pwani kupitia uundaji wa ajira na fursa nyingine," aliongeza. Wiki iliyopita, Rais Ruto alisema shughuli za ujenzi wa kiwanda hicho na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi Lamu huenda zikaendelea kwa wakati mmoja. Kauli hiyo ilizua malalamiko miongoni mwa wakazi wa Lamu wanaodai kuwa, bado kuna masuala ya fidia ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya mradi wa bomba hilo, huku wakitaka uwazi kuhusu mipango ya kiwanda hicho. Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari katika Ikulu ya Kisumu, Rais Ruto alisema serikali inashauriana na Dangote Group kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Turkana. Wakazi kupitia Chama cha Wakulima wa Kililana, kundi la kijamii linalowawakilisha wamiliki wa ardhi na wakazi wanaoishi hasa katika maeneo yanayopakana na sehemu za mradi wa Uchukuzi kati ya Bandari ya Lamu-South Sudan-Ethiopia (LAPSSET), wamehoji kwa nini mipango inaonekana kuendelea kwa kasi huku masuala muhimu yanayoathiri jamii yakiwa bado hayajatatuliwa. Katibu wao, Bw Mohamed Rajab, alitoa wito wa ushirikishwaji wa umma ili kutatua masuala ya fidia kabla ya hatua nyingine za mradi huo kuendelea. Bw Rajab alihoji kwa nini hadi sasa serikali imeendelea kuwa kimya kuhusu eneo ambako kiwanda cha mafuta cha Dangote kitajengwa Lamu. "Kwa nini serikali inawaacha wenyeji gizani kuhusu eneo halisi ambako kiwanda hiki kinachokusudiwa kitajengwa? Kwa nini ratiba inaendeshwa kwa haraka? Hakuna mtu ambaye amekuja kutueleza eneo hilo liko wapi," alisema Bw Rajab. Aliongeza kuwa bado kuna masuala ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba katika miaka iliyopita. "Ardhi yetu ilichukuliwa na hatukufidiwa. Tutatafuta haki mahakamani kuhusu masuala haya yote," alisema. Bw Mbwana Shee, Mwenyekiti wa Shungwaya Welfare Association, shirika la kijamii linalotetea haki za ardhi za jamii ya asili ya Bajuni huko Lamu, alielezea masikitiko kwamba kila mara serikali inapopanga kuwekeza katika mradi mkubwa kaunti hiyo, wenyeji huachwa nje ya maamuzi yanayogusa moja kwa moja maisha na riziki zao. Bi Raya Famau, mwanaharakati wa mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa Lamu Women Alliance, aliitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na mashauriano ya uwazi na jamii zote zilizoathirika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Trump ashambulia mahakama ya ICC, ataka nchi wanachama kujiondoa

Rais wa Amerika Donald Trump, Jumanne alitumia hotuba yake katika Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kushambulia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akitaka nchi wanachama wake kujiondoa mara moja katika taasisi hiyo aliyodai"haifuati sheria." Wakati huo huo, alitoa kauli kali dhidi ya Iran, akitishia kuiangamiza iwapo haitabadilisha mienendo yake. Katika hotuba yake iliyodumu takriban dakika 25 Jumanne, Trump alisema Amerika haitambui mamlaka yoyote ya ICC juu yake wala raia wake. Alisema Amerika haitaruhusu wanajeshi wake au raia wake kushtakiwa au kufanyiwa kesi na mahakama ambayo, kwa mujibu wake, haina mamlaka juu ya taifa hilo. Trump aliwaambia wajumbe kutoka mataifa 125 wanachama wa ICC waliokuwapo ukumbini kwamba wanapaswa kujiondoa rasmi kutoka mahakama hiyo. "Nahimiza nchi zote wanachama wa ICC kujiondoa mara moja katika taasisi hii ambayo imepoteza mwelekeo," alisema. Kauli hiyo ina uzito mkubwa kwa Kenya kutokana na historia yake na ICC. Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais William Ruto walishtakiwa mwaka 2012 kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-2008. Hata hivyo, mashtaka dhidi yao yalifutwa mwaka 2014 na 2015 baada ya changamoto za ushahidi na madai ya kuingiliwa kwa mashahidi. Kutokana na historia hiyo, mjadala kuhusu nafasi ya ICC nchini Kenya umeendelea kuwa mgumu kisiasa. Wachambuzi wanaona kuwa wito wa Trump wa nchi kujiondoa ICC unajiri wakati Rais Ruto amekuwa akiunga mkono kuimarishwa kwa taasisi za kimataifa badala ya kuzidhoofisha. Katika hotuba yake katika UNGA 81, Ruto alisisitiza kuwa changamoto kuu ya Afrika si ukosefu wa fedha, bali mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao unaweka vizuizi dhidi ya maendeleo ya bara hilo. Pia alirejelea wito wa muda mrefu wa Afrika kutaka uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Tofauti na Trump ambaye ameonyesha kutoamini taasisi za kimataifa, Ruto amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuzifanyia mageuzi ili ziwe na usawa zaidi kwa mataifa yanayoendelea. Wakati huo huo, Trump alielekeza mashambulizi yake kwa Iran kwa kuuliza ikiwa taifa hilo litachagua makubaliano yatakayoliwezesha kujijenga upya na kuwa moja ya mataifa makubwa duniani au likabiliwa na hatua kali kutoka Amerika. Alihoji ikiwa angekubali makubaliano ambayo yangeruhusu Iran kuimarika au kuiangamiza haraka ili isipewe nafasi ya kusababisha madhara kwa mataifa mengine. Trump alisema Amerika inaweza kusukuma Iran katika hali mbaya sana isiyokuwa na nafasi ya kupona wala kujenga mustakabali wake. Alipokuwa akitoa hotuba hiyo, baadhi ya wajumbe wa Iran waliondoka ukumbini alipokuwa akielezea operesheni za kijeshi  dhidi ya taifa hilo katika miezi sita iliyopita. Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pamoja na Waziri wa Masuala  ya Kigeni Abbas Araghchi, ambao walikuwa New York kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa, hawakuhudhuria kikao hicho wakati Trump akizungumza. Trump pia alitoa wito kwa mataifa yote duniani kushirikiana katika kuitenga Iran kiuchumi hadi ikome kushambulia usafirishaji wa kimataifa baharini, kusitisha mpango wake wa nyuklia na kuacha kuunga mkono ugaidi. Alidai kuwa uongozi wa Iran unaonyesha udhaifu na si nguvu, akisema taifa hilo ambalo awali lilikuwa na ushawishi mkubwa Mashariki ya Kati limepoteza nguvu zake. Aidha, alishutumu serikali ya Tehran kwa ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wake na kuonya kuhusu hatari ambayo ingekumba dunia iwapo Iran ingepata silaha za nyuklia. Trump alisema utawala wake ulijaribu kwanza njia ya mazungumzo kwa kupatia Iran nafasi ya ushirikiano kamili wa kiuchumi kwa sharti la kuacha mpango wake wa nyuklia na msaada kwa makundi ya kigaidi, lakini Tehran ilikataa pendekezo hilo. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Trump aligusia vita vya Ukraine akisema anaamini vita hivyo vinaweza kumalizika mapema kuliko wengi wanavyotarajia. Alisema Amerika inaendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Urusi na Ukraine na akaonyesha matumaini kuwa makubaliano ya kusitisha vita yatafikiwa ndani ya muda mfupi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 10 hours ago

Barua mbili zaibuka kuhusu usajili wa jina 'Ukombozi' linalogonganisha Sifuna na Kalonzo

BARUA mbili zinazokinzana zinazodaiwa kuhifadhi jina la 'Ukombozi' kwa makundi mawili tofauti zimeweka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) katikati ya mzozo mpya unaowahusu kiongozi wa Wiper Patriotic Movement Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Washirika wa Bw Sifuna jana walidai kulikuwa na njama baada ya Bw Musyoka kuzindua The Ukombozi Alliance (TUA), baada ya kufanikiwa kuhifadhi jina hilo katika ORPP. Bw Musyoka na viongozi wenzake wa upinzani wamebadilisha jina la Azimio La Umoja One Coalition kuwa TUA wanapojiandaa kwa uchaguzi wa urais wa 2027. Barua ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou ya Septemba 8, 2026 ilikataa ombi la kundi la Bw Sifuna la kubadilisha jina la United Democratic Party (UDP) kuwa 'Ukombozi People's Party (UPP),' ikisema linafanana na 'The Ukombozi Alliance (TUA). Bw Lorionokou alisema TUA lilihifadhiwa Julai 20, 2026. Hata hivyo, vuguvugu la Linda Mwananchi baadaye liliweka wazi barua nyingine ya ORPP ambayo inadaiwa kuidhinisha kuhifadhiwa kwa jina hilo na Bw Allan Akivaga. "Maombi yenu yamezingatiwa kwa mujibu wa sheria na jina Ukombozi People's Party (UPP) limeidhinishwa. Uhifadhi wa jina hilo utakuwa kwa kipindi kisichozidi siku 90 kuanzia tarehe ya barua hii," ORPP ilisema katika barua ya Machi 13, 2025. Katika mahojiano ya hivi majuzi na Taifa Leo, Bw Lorionokou alithibitisha kuwa UPP lilikuwa limehifadhiwa na Bw Akivaga. "UPP ni chama ambacho nadhani kiliomba mwezi Machi 2025 kuwa chama cha kisiasa na kimekuwa katika mchakato. Katika rekodi zangu, UPP ni jina lililohifadhiwa kwa chama cha kisiasa ambacho kiko katika mchakato wa kusajiliwa," Bw Lorionokou alisema. Mbunge wa Funyula Oundo Midenyo alisema "mbinu za kuwapotosha watu zinazotumiwa na serikali" hazitazuia azma ya Bw Sifuna na akasema kundi hilo litakuwa na chama ifikapo Jumatatu ijayo. "Tumepoteza Ukombozi Party lakini hata mtoto wako akifa unaendelea kuishi na hilo ndilo tutakalofanya. Kuna vyama vingi sana kwa hivyo hatuna wasiwasi. Nataka kuwahakikishia wafuasi wetu kwamba chama kipya bado kitakuwa na nembo ya Linda Mwananchi na pia rangi zake. Hatujakata tamaa hata kidogo," Bw Oundo alisema. Hata hivyo, msemaji wa Wiper Ndegwa Njiru alimtetea Bw Musyoka dhidi ya madai kwamba anapanga njama dhidi ya Bw Sifuna. Alisema Bw Musyoka amekuwa akitumia kauli 'Komboa Kenya' tangu 2025. "Rekodi zinaonyesha kwamba mapema Aprili 2025, wakati Sifuna bado alikuwa Katibu Mkuu wa ODM, Musyoka alikuwa tayari ametumia na kutangaza kauli hiyo. Neno Ukomboa ndilo limezaa Ukombozi," Bw Njiru alisema. Kiongozi wa Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa pia aliambia Nation kwamba Azimio lilihifadhi jina hilo kabla ya Bw Natembeya kuanza mchakato wa kubadilisha jina la UDP. "Jina hilo tayari limeidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa. Tuliomba kuhifadhi The Ukombozi Alliance zamani kabla ya mpango wa kubadilisha jina la chama cha Jirongo kuwa Ukombozi People's Party," Bw Wamalwa alisema. Kuwepo kwa Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Suba South Caroli Omondi wakati wa uzinduzi wa muungano huo mpya pia kumekuwa kukichunguzwa kwa karibu na baadhi ya washirika wa Bw Sifuna. Gavana Orengo na Bw Omondi ni wanachama wa Linda Mwananchi. Hata hivyo, Bw Caroli pia ni Katibu Mkuu wa muungano wa Azimio, ambao sasa umepewa jina TUA. Taifa Leo imefahamu kuhusu mipango ya kumteua Bw Orengo kuchukua nafasi ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti wa muungano huo. Bw Kenyatta Jumanne alijiuzulu rasmi kama kiongozi wa Jubilee Party. Pia anatarajiwa kujiuzulu kama mwenyekiti wa muungano huo ili kutoa nafasi kwa mabadiliko zaidi. "Linda Mwananchi haitawahi kuwa sehemu ya Azimio na Edwin Sifuna bado ndiye mgombea wetu wa urais. Hakutakuwa na mchujo wa Orengo kwa sababu tumeamua mgombea wetu ni Sifuna," Bw Oundo alisema. "Orengo anaweza kuchukua nafasi yoyote katika Azimio lakini katika Linda Mwananchi tunajadili mambo kwanza kabla ya kuyaweka hadharani. Kwa hivyo Caroli na Orengo walipohudhuria mkutano wa Azimio, yaliyotokea huko si sehemu ya Linda Mwananchi na sisi si sehemu ya Azimio," mbunge huyo alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Kindiki afanya zaidi ya ziara 30 Mlimani kusaka ushawishi

KWA miezi 10 iliyopita, Naibu Rais Kithure Kindiki amefanya zaidi ya ziara 30 katika eneo lake la nyumbani Mlima Kenya, kukagua miradi ya maendeleo au kufuta ushawishi wa wapinzani katika eneo hilo. Akiandamwa na mashambulizi kutoka kwa viongozi kadhaa wa upinzani katika eneo la Mlima Kenya, Prof Kindiki, ambaye kwa kiasi kikubwa anapambana peke yake, amejikita katika kuonyesha na kuharakisha miradi ya serikali. Miongoni mwa vigogo wa kisiasa wa Mlima Kenya wanaompigana vita kisiasa ni Rigathi Gachagua, John Methu, Ndindi Nyoro, Martha Karua, Justin Muturi, Gitonga Mukunji, Peter Munya, Mithika Linturi na Kawira Mwangaza. Hata hivyo, kwa mujibu wa Prof Kindiki, nguvu yake kuu ni kwamba "ana kazi nyingi za kuonyesha katika Mlima Kenya akiwa naibu rais, ilhali Bw Gachagua hana rekodi ya maendeleo wakati alikuwa ofisini." Katika hafla mbalimbali, Prof Kindiki amekuwa akisisitiza kuwa wapigakura wanapaswa kuwahukumu viongozi kwa kuzingatia rekodi yao ya maendeleo. "Imesemwa kuwa taji huwa na thamani mradi tu linavaliwa. Likiondolewa, linakuwa kipande cha chuma kisicho na thamani. Msidanganywe na watu ambao hawakuwahi kuja kwenu wala kuwafanyia lolote walipokuwa mamlakani," Prof Kindiki amekuwa akisema. Kati ya ziara nyingi alizofanya katika eneo la Mlima Kenya, amezuru Meru zaidi ya mara 15, Tharaka Nithi takriban mara saba na Embu karibu mara saba, huku akizuru Kirinyaga mara nne. Katika upande wa magharibi wa Mlima Kenya, Prof Kindiki amefanya ziara mara tisa, sita kati ya hizo akiwa ameandamana na Rais William Ruto. Katika eneo la Mashariki mwa Mlima Kenya, Naibu Rais amekuwa akikagua miradi, kukutana na viongozi wa mashinani, kufanya mikutano na maafisa wa United Democratic Alliance (UDA) au kupokea uungwaji mkono kutoka kwa wazee. Pia amekuwa akihudhuria ibada za kanisa na kuandaa mikutano ya kuwawezesha wananchi, ambapo amekuwa akieleza rekodi ya maendeleo ya utawala wa sasa. Prof Kindiki amekuwa akiorodhesha miradi ya mabilioni ya fedha, ikiwemo masoko, barabara, usambazaji wa umeme mashambani na nyumba za gharama nafuu, kama ushahidi wa kazi anazofanya Rais. Katika Kaunti ya Meru, Prof Kindiki anasema serikali inajenga zaidi ya kilomita 500 za barabara kwa gharama ya zaidi ya Sh42 bilioni, inaboresha hospitali mbili kwa zaidi ya Sh1.1 bilioni na kujenga masoko 21 ya kisasa. Alisema Kituo cha Kukusanya na Kuchakata Mazao ya Kilimo cha Kaunti ya Meru kimekaribia kukamilika, huku viwanja viwili vya michezo vya Maua na Urru vikiboreshwa kwa zaidi ya Sh350 milioni. "Washindani wetu wanajua tu kutukana na kubuni kauli mbiu. Lakini Wakenya wanataka barabara, masoko ya kisasa, maji na hospitali bora na hili ndilo tunalolenga," Naibu Rais alisema Meru wiki iliyopita. Katika Kaunti ya Embu, Naibu Rais Kindiki alisema serikali inajenga masoko 12, inatekeleza miradi 10 ya barabara na kuboresha uwanja wa Embu. Alisema serikali pia inaendelea na mradi wa maji wa Kiambere pamoja na kuboresha Hospitali ya Embu Level Five. "Wanaotuambia tuondoke serikalini wanapaswa kuelewa kwamba miradi hii yote ya maendeleo, hasa barabara, isingeweza kutekelezwa bila nguvu tuliyo nayo tukiwa ndani ya serikali," Prof Kindiki aliwaambia maafisa wa UDA. Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Naibu Rais anasema takriban miradi 13 ya barabara inaendelea, huku serikali ikiwa imejitolea kuunda upya daraja la Nithi kwa gharama ya Sh7 bilioni. "Kwa karibu miaka 40, daraja la Nithi limekuwa likigharimu maisha ya watu. Ni Rais Ruto aliyejitolea kukomesha vifo hivyo. Mkandarasi wa daraja la Nithi tayari yuko katika eneo la ujenzi akisubiri fidia ya ardhi," Naibu Rais alisema. Prof Kindiki sasa anategemea miradi hiyo kuhamasisha watu wa eneo lake kumuunga mkono huku akikabiliana na ushindani wa ndani kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Je, safari ya Sifuna kuingia ikulu imeanza kuyumba?

SIASA za upinzani nchini Kenya zimefika mahali ambapo umaarufu wake hauwezi tena kuficha madhaifu katika ngazi ya uongozi wake. Linda Mwananchi ilipoibuka, ilionyesha kusudi la kujenga kizazi kipya cha upinzani na kumweka Edwin Sifuna katika nafasi ya kuwania urais. Swali linabakia iwapo vuguvugu hili linajenga mashine ya uchaguzi au linazalisha vyama vya kuyeyusha nguvu zake? Mvutano kuhusu ni chama kipi cha kutumia katika uchaguzi wa 2027 unajenga ufa ulio wazi. Babu Owino anaegemea Mwananchi Party, huku George Natembeya akiunga mkono Ukombozi People's Party kama chombo cha Sifuna. Ripoti kinzani zinaonyesha Sifuna anatarajiwa kuzindua chama chake mwanzoni mwa Oktoba, naye Babu akielekeza nguvu zaidi katika Mwananchi Party na azima yake ya ugavana Nairobi. Lakini pia imetokea kwamba Kalonzo Musyoka amebadilisha muungano wa Azimio kuwa The Ukombozi Alliance. Hili ndilo donda la kisiasa linafyonza Linda Mwananchi. Uaminifu uko wapi? Muungano wa kisiasa hauhitaji makubaliano katika kila jambo ila lazima kuwe na msingi kuhusu nani anaongoza, chombo gani kinatumika na kila mmoja yuko tayari kutoa nini kwa ajili ya mradi wa pamoja. Ikiwa kila kiongozi anajenga chama chake, bila shaka kila chama kitakuwa na maslahi, wagombea, mtandao na mamlaka yake ya kibinafsi na kuhatarisha muungano huo. Urais haujengwi kwa umaarufu wa mikutano pekee. Unahitaji muundo wa kitaifa, wagombea katika maeneo mbalimbali, mawakala, rasilimali, ujumbe mmoja na makubaliano ya kisiasa yanayoweza kustahimili joto la uchaguzi. Historia ya Kenya imejaa mafunzo mazito kisiasa. Katika mwaka wa 1992, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, wapinzani waligawanyika kila mmoja kwa tamaa yake huku Daniel arap Moi akipata ushindi wa rahisi dhidi ya wapinzani Kenneth Matiba, Mwai Kibaki na Jaramogi Oginga Odinga na wengine. Tatizo lilikuwa kugawanyika kwa nguvu hiyo ya upinzani miongoni mwa wagombea kadhaa. Huenda picha hiyo ya mwaka 1992 isijirudie 2027 kwani mazingira ya kisiasa ni tofauti lakini kanuni za kisiasa hazina tofauti: kura zilizogawanyika haziwezi kuhesabiwa kama kura moja wakati wa kuamua urais. Mgogoro unaokumba Linda Mwananchi si suala dogo la chama. Ni mjadala kuhusu mamlaka, urais na udhibiti wa mamlaka ya kisiasa. Babu anadai kumuunga mkono Sifuna, huku msimamo wake kuhusu Mwananchi Party ukiashiria picha kinzani. Sifuna ana kibarua cha pekee kuviunganisha vyama vyote vinavyochipuka ndani ya Linda mwananchi kwa makubaliano madhubuti ili kuepuka mgawanyiko unaoshuhudiwa sasa. Ni sharti ahakikishe majadiliano ya kina kuelekea kuimarisha muungano mpana wa Linda Mwananchi. Ikiwa kila mmoja ataendelea kujenga himaya yake, Sifuna atajikuta akiwa na jina, umaarufu na jukwaa bila asasi thabiti za kushindana kwenye uchaguzi. Hapo huenda ikawa ndipo mwanzo wa urais wake kubaki tu kuwa wazo lenye mvuto na msisimko maridadi kisiasa ambalo bado halijageuzwa kuwa mradi wa uchaguzi uliokamilika. Suala muhimu kwa sasa si kushabikia kuwa Linda Mwananchi ina watu wanaoishabikia bali kutathmini iwapo uongozi wake una uaminifu, nidhamu na umoja wa kutosha kuwageuza watu hao kuwa nguvu moja ya kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Korti yakataa kuzuia IEBC kuweka kituo cha kuthibitisha matokeo ya kura za urais

MAHAKAMA Kuu imeunga mkono uhalali wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais katika ngazi ya kitaifa. Jaji Gregory Mutai alikataa ombi la viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua na Fred Matiang'i pamoja na mwanaharakati Okiya Omtatah Okoiti, waliopinga jukumu la IEBC katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura. Walalamishi walidai kuwa matokeo ya urais yaliyotangazwa na kuthibitishwa na maafisa wa uchaguzi katika maeneo bunge ni ya mwisho na hayapaswi kuhesabiwa au kuthibitishwa tena katika ngazi ya kitaifa. Hata hivyo, Jaji Mutai alisema Katiba inataka IEBC kujumlisha na kuthibitisha matokeo hayo katika ngazi ya kitaifa ili kubaini iwapo mgombea ametimiza kiwango kinachohitajika kuchaguliwa kuwa Rais. "Jukumu la kujumlisha na kuthibitisha si kuingilia kinyume cha Katiba uamuzi wa mwisho wa maeneo bunge," Jaji alisema. Uamuzi huo umehifadhi Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura, lakini ukaweka mipaka ya mamlaka ya IEBC. Tume inaweza kujumlisha na kuthibitisha takwimu zilizotangazwa katika maeneo bunge, lakini haina mamlaka ya kuzibadilisha, kuzifuta au kuzirekebisha isipokuwa kwa amri ya mahakama. Mahakama pia ilisema jukumu hilo ni la IEBC kwa pamoja na si la mwenyekiti pekee. Jaji Mutai alisema matokeo yaliyothibitishwa katika maeneo bunge, yakiwemo yaliyo katika Fomu 34A na 34B au fomu zitakazochukua nafasi ya hizo, ndiyo yatakayokuwa msingi katika ngazi ya kitaifa. Alisema hakuna takwimu za kielektroniki au hifadhidata inayoweza kuchukuliwa kuwa bora kuliko rekodi hizo. Mahakama pia ilikataa mapendekezo ya kuweka muda maalum wa kuchapisha sajili ya wapigakura, kutangaza vituo vya kupigia kura na kuanzisha mfumo wa kura, ikisema masuala hayo yako ndani ya mamlaka ya IEBC na Bunge. Kuhusu madai ya ubaguzi, Jaji alisema matokeo ya urais yanashughulikiwa tofauti kwa sababu Rais anahitaji kutimiza kiwango maalum cha kitaifa. Uamuzi huo unatarajiwa kuzingatiwa katika mchakato wa kurekebisha sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Sibanduki Jubilee, asema Uhuru akimpokeza Matiang'i uongozi wa chama

RAIS (mstaafu) Uhuru Kenyatta jana alikabidhi rasmi uongozi wa Chama cha Jubilee kwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i, lakini akaeleza kuwa hataondoka katika chama hicho bali atasalia kama mshauri mkuu huku maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027 yakishika kasi. Akizungumza mbele ya wanachama wa Jubilee baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kuidhinisha mabadiliko hayo, Bw Kenyatta alisema ataendelea kuhudhuria mikutano ya chama na kutoa ushauri kwa viongozi na wanachama. "Siwezi kuondoka Jubilee, niende wapi? Nitachukua nafasi ya mshauri mkuu. Nitaendelea kuhudhuria mikutano ya Jubilee na kutoa ushauri kama mwanachama mkuu wa chama," alisema. Uhuru alisema hatua hiyo inalenga kutii sheria na kuandaa chama kwa uchaguzi ujao badala ya kujiondoa katika siasa. "Tunaposubiri Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC), Matiang'i ambaye alikuwa naibu wangu atachukua nafasi ya uongozi. Siachi siasa, tunajiandaa kwa uchaguzi ujao," alisema. Hatua hiyo imejiri baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa rais mstaafu hawezi kuendelea kushikilia nafasi rasmi ya uongozi katika chama cha kisiasa kwa muda unaozidi unaoruhusiwa kisheria. Hata hivyo, mahakama ilisema hukumu hiyo haimzuii rais mstaafu kubaki mwanachama wa chama au kushiriki shughuli za kisiasa. Kupitia uamuzi wa NEC, Dkt Matiang'i ameidhinishwa kuwa mrithi wa Bw Kenyatta, hatua ambayo inasubiri kuthibitishwa rasmi na wajumbe wa chama kupitia NDC. "Ninakubali jukumu la kuongoza Chama cha Jubilee," alisema Dkt Matiang'i baada ya kutangazwa kuwa mrithi wa Uhuru. Aidha, Dkt Matiang'i, ambaye tayari amepewa tiketi ya Jubilee kuwania urais mwaka ujao, aliwataka wanachama kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuimarisha nafasi ya muungano huo katika uchaguzi ujao. "Huu utakuwa mwaka wa ushirikishaji na wa kufafanua upya uongozi wa nchi yetu," alisema. Hata hivyo, suala la mrithi wa Uhuru halijakosa utata. Naibu kiongozi wa chama Jeremiah Kioni amewahi kuonyesha nia ya kutaka wadhifa huo na kusisitiza kuwa kiongozi achaguliwe kupitia mifumo ya chama. Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu pia ametaka suala hilo liamuliwe na wajumbe wa chama katika NDC. Mbali na masuala ya uongozi wa Jubilee, Bw Kenyatta alirejelea uchaguzi wa urais wa 2022 na kutetea uamuzi wake wa kumuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga. Alipinga madai kwamba, alishindwa kisiasa na Rais William Ruto katika uchaguzi huo. "Wanaposema walinishinda, ni mimi nilikuwa kwenye kura au Raila Odinga? Walinishandaje ilhali nilikuwa tu nikimuunga mkono Raila?" alihoji. Uhuru aliendelea kudai kuwa Raila ndiye aliyeshinda uchaguzi huo licha ya matokeo rasmi yaliyomtangaza Dkt Ruto mshindi. Tume ya IEBC ilimtangaza Dkt Ruto mshindi kwa kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,942,930 za Bw Odinga, matokeo yaliyothibitishwa na Mahakama ya Juu. Kauli hizo zilipingwa na viongozi wa UDA. Katibu Mkuu wa chama hicho Hassan Omar alisema matamshi ya Uhuru yanaonyesha bado hajakubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2022. Wakati huo huo, Bw Kenyatta alipuuzilia mbali madai kwamba analenga kurejea kuwania urais, akisema Katiba inaruhusu mihula miwili pekee na kwamba tayari alihudumu kwa vipindi hivyo viwili. Badala yake, alisema Jubilee inapaswa kujipanga kuandaa wagombea wa nyadhifa mbalimbali kuanzia uwakilishi wa wadi, ubunge, ugavana hadi Seneti, huku ikitafuta mshirika atakayeongoza muungano wa upinzani kwenye kinyang'anyiro cha urais mnamo 2027. Katika mpangilio huo mpya, Uhuru anabaki kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Jubilee akiwa mshauri mkuu, huku Dkt Matiang'i akipewa jukumu la kuendesha shughuli za kila siku za chama na kuongoza kampeni zake za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 22 Sep 2026 16:19:22

Mwanablogu kulipwa Sh5 milioni kwa kuvamiwa na polisi

MAHAKAMA Kuu imempa mwanablogu na mtumiaji wa mitandao ya kijamii, Ndiang'ui Kinyagia, fidia ya Sh5 milioni baada ya kubaini kwamba maafisa wa polisi walikiuka haki zake walipovamia nyumba yake, kuipekua, kutwaa mali yake na kumzuia kusafiri kwa uhuru. Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Patricia Nyaundi wa Kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu jijini Nairobi, mahakama ilisema polisi waliingia nyumbani kwa Kinyagia mnamo Juni 21, 2025, bila kibali cha mahakama na bila kuthibitisha kuwa walitimiza masharti ya kufanya upekuzi bila kibali hicho. Jaji Nyaundi alisema maafisa hao walishindwa kuwasilisha sababu zilizoonyesha kwamba kupata kibali cha mahakama kungeathiri au kuchelewesha uchunguzi wao. "Sehemu ya 60 ya Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi si tu tamko la kawaida. Ni kinga ya kikatiba iliyowekwa kisheria ili kulinda haki za wananchi," alisema jaji huyo. Kinyagia, ambaye ni mjasiriamali wa teknolojia na mchangiaji wa masuala ya umma mtandaoni, alipata umaarufu mnamo Juni 2025 baada ya kujificha alipogundua kwamba maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walikuwa wakimtafuta kufuatia chapisho la mtandaoni lililohusishwa na maandamano yaliyokuwa yakipangwa dhidi ya serikali. Polisi walikuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu ujumbe uliowekwa katika mtandao wa X waliodai ulikuwa wa uchochezi na wenye maudhui ya uasi. Baada ya kufuatilia akaunti hiyo hadi kwa Kinyagia na kupata usaidizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Kenya, maafisa walielekea nyumbani kwake. Mahakama ilielezwa kwamba polisi walipiga kambi katika makazi hayo kwa muda mrefu kabla ya kuvunja mlango na kuingia ndani waliposhindwa kumpata. Walipekua nyumba hiyo na kuondoka na vifaa mbalimbali huku wakiacha orodha ya vitu vilivyochukuliwa kwa msimamizi wa eneo hilo. Jaji Nyaundi aliamua kuwa hatua hiyo ilikiuka haki za Kinyagia za faragha, mali, utu, usalama wa kibinafsi na uhuru wa kutembea. Mahakama pia ilizuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) pamoja na polisi kuendelea kumshtaki Kinyagia kuhusiana na uchunguzi huo, ikisema mchakato mzima ulianza kwa vitendo visivyozingatia Katiba.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 22 Sep 2026 13:09:55

Vyombo vya habari Amerika vyamgomea Trump

WASHINGTON, Amerika: TELEVISHENI Amerika Jumatatu zilisitisha kwa pamoja kurusha matangazo ya shughuli za Rais Donald Trump kutoka Ikulu ya White House, baada ya CNN, Politico na MS NOW kuzuiwa kuingia katika jengo hilo. Trump alitangaza marufuku hiyo Ijumaa, akishutumu mashirika hayo kwa 'kuandika habari za kutunga na uongo' kuhusu utawala wake. Vyombo hivyo vilisema waandishi wao walizuiwa kuingia White House mnamo Jumamosi. CNN, Politico na MS NOW baadaye zilitangaza kuwa zitawasilisha kesi dhidi ya utawala wa Trump ili kutetea kanuni kwamba serikali haiwezi kuamua kile ambacho vyombo vya habari vinaripoti. Kufuatia hatua hiyo, White House ilianzisha kituo chake cha matangazo mtandaoni, Trump TV, kinachorusha sehemu za video ya rais saa 24 kwa siku. Vyombo vingine vya habari pia vilisema havitashiriki katika mfumo wa pamoja wa kuripoti shughuli za rais. New York Times na Washington Post, kwa mfano, zilisema hazitachapisha picha za matukio ya Trump. Hatua hiyo ilisababisha kukosekana kwa picha za televisheni za Trump akipanda ndege ya Air Force One au akiwasili New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Trump pia alishiriki katika hafla ya kuzindua uwanja mpya wa helikopta ya Marine One katika bustani ya White House. Hafla hiyo ilikuwa mbashara kwenye tovuti ya White House, ingawa sauti ya hotuba yake haikusikika. Baadaye rais alionekana kwenye televisheni baada ya kukutana na Meya wa New York Zohran Mamdani. Mamdani alimweleza kuwa waandishi wote wa habari watakaribishwa katika mkutano na wanahabari. Trump alisema hakushtushwa na hatua hiyo, akisema vyombo vya habari vilivyodai vitamsusia havijawahi kufanya hivyo. Mfumo wa ushirikiano wa vyombo vya habari huyawezesha mashirika ya habari kushirikiana ili kupunguza gharama na matumizi ya nafasi wakati wa kuripoti shughuli za rais. Bryan Boughton, mkuu wa afisi ya Fox News Washington, alisema katika barua pepe kuwa mfumo huo hautaendelea kuripoti shughuli za Trump zinazowashirikisha vyombo vyote vya habari. Alisema hatua hiyo ilifuatia White House kuzuia CNN kutekeleza jukumu lake katika ziara ya Trump New York. Siku hiyo hiyo, CNN, Politico na MS NOW ziliwasilisha kesi Mahakamani jijini Washington, zikisema White House ilifuta vibali vya waandishi wao bila kuwapa taarifa wala nafasi ya kujitetea. Vyombo hivyo vilisema hatua hiyo inatishia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya umma kupata habari huru bila kuingiliwa na serikali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 22 Sep 2026 10:55:31

Wakazi wajenga ua kuzunguka  ardhi ya chuo baada ya agizo la Ruto

Wanajamii wa eneo la Oloitikosh katika Kaunti ya Kajiado wameanza kuweka ua kuzunguka ekari 60 za ardhi inayomilikiwa na Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Kajiado East (TVET), wiki mbili baada ya Rais William Ruto kuagiza ardhi hiyo ilindwe kwa ajili ya upanuzi wa taasisi hiyo. Shughuli ya kuweka ua Jumatatu iliongozwa na Naibu Chifu wa Oloitikosh, Moses Karaine, kwa ushirikiano na wakazi wa eneo hilo. Hatua hiyo imefuatia madai kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya awali ya chuo hicho yenye ukubwa wa ekari 76 ilinyakuliwa na kugawanywa na watu binafsi kwa ushirikiano wa mabroka na baadhi ya wanasiasa. Inadaiwa kuwa chuo kilibaki na ekari saba pekee ambako majengo yake yamejengwa. Wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo hilo wiki mbili zilizopita, Rais Ruto aliamuru ekari 60 zilizokuwa zikizozaniwa ziwekwe ua mara moja ili kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye ya chuo hicho. "Ardhi hii lazima ilindwe na kuwekwa ua. Nitarudi mwenyewe kukagua maendeleo. Baadaye TVET hii inaweza kukua na kuwa chuo kikuu," alisema Rais wakati wa uzinduzi wa mabweni ya wanafunzi chini ya mpango wa Boma Yangu. Chuo hicho, ambacho kina umri wa miaka 10, kwa sasa kina takriban wanafunzi 800 wanaosomea kozi mbalimbali za kiufundi. Pia ndicho taasisi pekee ya serikali katika Kaunti ya Kajiado iliyo na kituo cha kidijitali cha Jitume Digital Hub. Mkuu wa chuo hicho, Watiri Kiragu, alisifu hatua ya rais akisema kurejeshwa kwa ardhi hiyo kutatoa nafasi muhimu kwa upanuzi wa taasisi hiyo siku zijazo. "Msingi wa upanuzi wa taasisi yoyote ni upatikanaji wa ardhi. Uamuzi huu ni wa manufaa makubwa kwa maendeleo ya chuo," alisema. Mzee Daniel Lepatei, ambaye alipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa ua huo, alisema jamii imejitolea kulinda ardhi hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Kwa mujibu wake, mabroka wa ardhi walianza kugawa sehemu ya ardhi hiyo miaka mitano iliyopita na kupata barua za ugavi kwa njia isiyo halali. "Amri ya rais imeokoa mustakabali wa vijana wetu. Fedha za kujenga ua zimepatikana na taratibu za kurejesha ardhi zimekamilika," alisema. Nao viongozi wa jamii walidai kuwa baadhi ya maafisa wa utawala, wanasiasa na maafisa wa ardhi walihusishwa na unyakuzi wa ardhi hiyo. Hata hivyo, Waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Kajiado, Hamilton Parseina, alisema barua zote za ugavi zilizokuwa zimetolewa kwa watu binafsi tayari zimefutwa. "Ardhi hii ni mali ya chuo cha TVET. Barua zilizokuwa zimetolewa hapo awali zimebatilishwa ili kuruhusu upanuzi wa taasisi hiyo," alisema. Hatua ya kuzungusha ua ardhi hiyo imepokelewa kwa furaha na wakazi, ambao wanasema italinda rasilimali ya umma wakati ambapo maeneo mengi ya Kitengela yanaendelea kukabiliwa na ongezeko la visa vya unyakuzi wa ardhi ya taasisi za umma.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 22 Sep 2026 11:28:41

Murkomen sasa atangaza vita dhidi ya pombe Baringo

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewaamuru maafisa wa usalama katika Kaunti ya Baringo kuimarisha msako dhidi ya pombe haramu na kuwawajibisha wanaohusika na biashara hiyo. Bw Murkomen alisema amepokea ripoti kwamba utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu, ikiwemo ile inayodaiwa kuwa na kemikali ya ethanol, umeongezeka Kabarnet na maeneo ya jirani. Akizungumza wikendi wakati wa ibada ya madhehebu mbalimbali katika Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Kabarnet, Bw Murkomen aliwataka maafisa wa usalama kumtafuta mwanamke anayejulikana kwa jina la Targok, ambaye anadaiwa kujihusisha na biashara hiyo. "Nimeambiwa wakuu wa maeneo wamejaribu kukomesha pombe haramu, lakini kuna baadhi ambayo ni mbaya sana, kama yenye kemikali ya ethanol. Nimesikia kuna mwanamke anayeitwa Targok, ambaye ni mtengenezaji na muuzaji wa pombe haramu na mara nyingi hukamatwa na kuachiliwa mahakamani," akasema. Bw Murkomen alimtaka Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Baringo Macharia Wanjau kuhakikisha Targok anakamatwa na kufikishwa mahakamani. Alimweleza Kamishina wa Kaunti ya Baringo Wesley Koech kuwa nafasi yake itakuwa hatarini iwapo maafisa wa usalama watashindwa kukabiliana na biashara hiyo. "Ni jukumu lako kuchagua kati ya Targok maarufu na kazi yako. Chagua kumwokoa yeye au kazi yako," akasema. Wiki moja iliyopita, polisi walivamia boma moja katika kijiji cha Kaprogonya, nje kidogo ya Kabarnet, wakipata kile walichokieleza kuwa chumba cha siri kilichojengwa chini ya sakafu ya bafu. Polisi walikuwa wakimtafuta Targok baada ya kupata taarifa za kijasusi kwamba pombe haramu na kemikali zilikuwa zimefichwa katika boma hilo. Hata hivyo, alikuwa tayari ametoroka walipofika. Baada ya kupekua eneo hilo kwa karibu saa mbili, maafisa waligundua shimo chini ya vigae vya bafu. Ngazi iliwaongoza hadi kwenye chumba cha chini kilichojengwa kama tangi la majitaka. Ndani walipata zaidi ya mitungi 40, kila mmoja ukiwa na kemikali iliyoshukiwa ya ethanol kwa jumla ikiwa zaidi ya lita 1,000. Naibu Kamishina wa Kaunti ya Baringo ya Kati Joseph Ng'eny alisema boma hilo lilionekana kutengenezwa kwa njia maalumu ili kuficha biashara hiyo. "Kwa mtazamo wa kwanza unaweza kudhani hii ni nyumba ya kawaida, lakini tulipoingia tuligundua ilikuwa kiwanda cha kutengeneza pombe haramu," akasema. Mbali na pombe haramu, Bw Murkomen aliwataka machifu na wazee wa vijiji kuacha kushughulikia kesi za ubakaji na kulawiti watoto, akisema washukiwa wanapaswa kukamatwa na kufikishwa kortini. Alisema baadhi ya wahalifu wa unyanyasaji wa kimapenzi ni watu wanaoaminika na familia, wakiwemo jamaa, walimu, wachungaji na watu wengine wenye mamlaka.

read more