T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 19 Sep 2026 07:55:30

Hofu genge la 'panga boys' likirejea mitaa ya Mombasa

KWA Said Faiz Khamis, 29, safari ya kawaida ya bodaboda usiku iligeuka kuwa jinamizi baada ya kushambuliwa kwa mapanga na kujeruhiwa kwenye kichwa na vidole. Mkazi huyo wa Maweni alisema mnamo Septemba 15, saa tano usiku, abiria mmoja alimuomba ampeleke nyumbani kwake eneo la Barsheba, Kisauni. Bw Khamis alimweleza abiria huyo kuwa angemfikisha steji na hangeingia kwenye kitongoji. Hata hivyo alipomfikisha kwenye steji, abiria alimuomba amfikishe nyumbani kwake, mita chache kutoka steji. Hata hivyo, alipomfikisha genge la majambazi waliokuwa na silaha walijitokeza na kumvamia. "Niligundua kuwa abiria alikuwa amepanga watu waliokuwa wanasubiri kunishambulia kwa mapanga. Niliponea chupu chupu na kutoroka lakini nilikuwa nimekatwa katwa kichwani na kwenye vidole. Nilihepa na funguo za pikipiki yangu kwa kutumia vichochoro," alisema. Kupitia msaada wa waendesha bodaboda wenzake, alipata pikipiki hiyo katika kituo cha polisi cha Kiembeni mnamo Septemba 17. Hata hivyo, hii haikuwa mara yake ya kwanza kushambuliwa. Mapema mwaka huu, mwendo wa saa tisa usiku, Bw Khamis alisema alikuwa akimpeleka abiria katika Soko la Kongowea alipovamiwa na vijana waliokuwa kwenye pikipiki. "Walinipiga kichwani na kunikata kata na kuninyang'anya pikipiki yangu, simu na kila kitu nilichokuwa nacho kilienda. Walimuibia abiria wangu pesa zote ambazo alikuwa anaenda nazo Kongowea kununua bidhaa za biashara," alisema. Baada ya kutafuta fedha na kununua pikipiki nyingine, alirejea kazini. Hata hivyo, baada ya kujeruhiwa kwa mara ya pili amemua kuacha kazi hiyo. "Sasa nimeamua kuacha hii kazi. Kichwa changu kimekatwa vibaya mara mbili. Hii kazi ni hatari sana na nina bahati niko hai," alisema. Visa hivyo vimeibua hofu mpya kuhusu mashambulizi ya usiku katika maeneo ya Kisauni huku wakazi na wahudumu wa bodaboda wakidai magenge ya vijana wenye silaha butu yanaendelea kuwahangaisha wakazi. Mwenyekiti wa kamati ya usalama ya jamii ya Maweni na dereva wa bodaboda, Bw Samson Omondi, alidai kuwa magenge hayo wakati mwingine hutumia wanawake kama chambo. "Wanawake huwafuata waendesha bodaboda kwenye steji wakitaka huduma zetu. Wanapofikishwa waendako, abiria huchelewesha malipo kwa M-Pesa au kupiga simu, kumbe ni njama ya kuwapa muda washirika wao kujitokeza kutushambulia," alisema. Bw Omondi aliwataka maafisa wa polisi kuimarisha operesheni na kuwakamata wanaohusika, akisema baadhi yao wanajulikana na jamii. Vikundi vya kutetea haki za binadamu pia vimeitaka serikali kuchukua hatua ya kuimarisha usalama. Mratibu wa Vocal Africa Pwani, Wild Sketty, alisema shirika hilo limeorodhesha watu wanane waliodaiwa kushambuliwa kwa mapanga kati ya saa nne usiku na saa kumi na mbili asubuhi ndani ya wiki moja Kisauni. Hata hivyo, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Kisauni, Bw Jamleck Mbuba, aliwatuliza wakazi akisema polisi tayari wamewakamata baadhi ya washukiwa na wanaendelea kuwasaka wengine. "Tutawakamata wanaojificha. Tupeni muda, lakini mtusaidie kwa kutoa taarifa ili tuwatambue wahalifu walioko miongoni mwenu," alisema.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 29 minutes ago

Korti yakataa kuzuia IEBC kuweka kituo cha kuthibitisha matokeo ya kura za urais

MAHAKAMA Kuu imeunga mkono uhalali wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais katika ngazi ya kitaifa. Jaji Gregory Mutai alikataa ombi la viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua na Fred Matiang'i pamoja na mwanaharakati Okiya Omtatah Okoiti, waliopinga jukumu la IEBC katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura. Walalamishi walidai kuwa matokeo ya urais yaliyotangazwa na kuthibitishwa na maafisa wa uchaguzi katika maeneo bunge ni ya mwisho na hayapaswi kuhesabiwa au kuthibitishwa tena katika ngazi ya kitaifa. Hata hivyo, Jaji Mutai alisema Katiba inataka IEBC kujumlisha na kuthibitisha matokeo hayo katika ngazi ya kitaifa ili kubaini iwapo mgombea ametimiza kiwango kinachohitajika kuchaguliwa kuwa Rais. "Jukumu la kujumlisha na kuthibitisha si kuingilia kinyume cha Katiba uamuzi wa mwisho wa maeneo bunge," Jaji alisema. Uamuzi huo umehifadhi Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura, lakini ukaweka mipaka ya mamlaka ya IEBC. Tume inaweza kujumlisha na kuthibitisha takwimu zilizotangazwa katika maeneo bunge, lakini haina mamlaka ya kuzibadilisha, kuzifuta au kuzirekebisha isipokuwa kwa amri ya mahakama. Mahakama pia ilisema jukumu hilo ni la IEBC kwa pamoja na si la mwenyekiti pekee. Jaji Mutai alisema matokeo yaliyothibitishwa katika maeneo bunge, yakiwemo yaliyo katika Fomu 34A na 34B au fomu zitakazochukua nafasi ya hizo, ndiyo yatakayokuwa msingi katika ngazi ya kitaifa. Alisema hakuna takwimu za kielektroniki au hifadhidata inayoweza kuchukuliwa kuwa bora kuliko rekodi hizo. Mahakama pia ilikataa mapendekezo ya kuweka muda maalum wa kuchapisha sajili ya wapigakura, kutangaza vituo vya kupigia kura na kuanzisha mfumo wa kura, ikisema masuala hayo yako ndani ya mamlaka ya IEBC na Bunge. Kuhusu madai ya ubaguzi, Jaji alisema matokeo ya urais yanashughulikiwa tofauti kwa sababu Rais anahitaji kutimiza kiwango maalum cha kitaifa. Uamuzi huo unatarajiwa kuzingatiwa katika mchakato wa kurekebisha sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Sibanduki Jubilee, asema Uhuru akimpokeza Matiang'i uongozi wa chama

RAIS (mstaafu) Uhuru Kenyatta jana alikabidhi rasmi uongozi wa Chama cha Jubilee kwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i, lakini akaeleza kuwa hataondoka katika chama hicho bali atasalia kama mshauri mkuu huku maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027 yakishika kasi. Akizungumza mbele ya wanachama wa Jubilee baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kuidhinisha mabadiliko hayo, Bw Kenyatta alisema ataendelea kuhudhuria mikutano ya chama na kutoa ushauri kwa viongozi na wanachama. "Siwezi kuondoka Jubilee, niende wapi? Nitachukua nafasi ya mshauri mkuu. Nitaendelea kuhudhuria mikutano ya Jubilee na kutoa ushauri kama mwanachama mkuu wa chama," alisema. Uhuru alisema hatua hiyo inalenga kutii sheria na kuandaa chama kwa uchaguzi ujao badala ya kujiondoa katika siasa. "Tunaposubiri Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC), Matiang'i ambaye alikuwa naibu wangu atachukua nafasi ya uongozi. Siachi siasa, tunajiandaa kwa uchaguzi ujao," alisema. Hatua hiyo imejiri baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa rais mstaafu hawezi kuendelea kushikilia nafasi rasmi ya uongozi katika chama cha kisiasa kwa muda unaozidi unaoruhusiwa kisheria. Hata hivyo, mahakama ilisema hukumu hiyo haimzuii rais mstaafu kubaki mwanachama wa chama au kushiriki shughuli za kisiasa. Kupitia uamuzi wa NEC, Dkt Matiang'i ameidhinishwa kuwa mrithi wa Bw Kenyatta, hatua ambayo inasubiri kuthibitishwa rasmi na wajumbe wa chama kupitia NDC. "Ninakubali jukumu la kuongoza Chama cha Jubilee," alisema Dkt Matiang'i baada ya kutangazwa kuwa mrithi wa Uhuru. Aidha, Dkt Matiang'i, ambaye tayari amepewa tiketi ya Jubilee kuwania urais mwaka ujao, aliwataka wanachama kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuimarisha nafasi ya muungano huo katika uchaguzi ujao. "Huu utakuwa mwaka wa ushirikishaji na wa kufafanua upya uongozi wa nchi yetu," alisema. Hata hivyo, suala la mrithi wa Uhuru halijakosa utata. Naibu kiongozi wa chama Jeremiah Kioni amewahi kuonyesha nia ya kutaka wadhifa huo na kusisitiza kuwa kiongozi achaguliwe kupitia mifumo ya chama. Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu pia ametaka suala hilo liamuliwe na wajumbe wa chama katika NDC. Mbali na masuala ya uongozi wa Jubilee, Bw Kenyatta alirejelea uchaguzi wa urais wa 2022 na kutetea uamuzi wake wa kumuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga. Alipinga madai kwamba, alishindwa kisiasa na Rais William Ruto katika uchaguzi huo. "Wanaposema walinishinda, ni mimi nilikuwa kwenye kura au Raila Odinga? Walinishandaje ilhali nilikuwa tu nikimuunga mkono Raila?" alihoji. Uhuru aliendelea kudai kuwa Raila ndiye aliyeshinda uchaguzi huo licha ya matokeo rasmi yaliyomtangaza Dkt Ruto mshindi. Tume ya IEBC ilimtangaza Dkt Ruto mshindi kwa kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,942,930 za Bw Odinga, matokeo yaliyothibitishwa na Mahakama ya Juu. Kauli hizo zilipingwa na viongozi wa UDA. Katibu Mkuu wa chama hicho Hassan Omar alisema matamshi ya Uhuru yanaonyesha bado hajakubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2022. Wakati huo huo, Bw Kenyatta alipuuzilia mbali madai kwamba analenga kurejea kuwania urais, akisema Katiba inaruhusu mihula miwili pekee na kwamba tayari alihudumu kwa vipindi hivyo viwili. Badala yake, alisema Jubilee inapaswa kujipanga kuandaa wagombea wa nyadhifa mbalimbali kuanzia uwakilishi wa wadi, ubunge, ugavana hadi Seneti, huku ikitafuta mshirika atakayeongoza muungano wa upinzani kwenye kinyang'anyiro cha urais mnamo 2027. Katika mpangilio huo mpya, Uhuru anabaki kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Jubilee akiwa mshauri mkuu, huku Dkt Matiang'i akipewa jukumu la kuendesha shughuli za kila siku za chama na kuongoza kampeni zake za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Mwanablogu kulipwa Sh5 milioni kwa kuvamiwa na polisi

MAHAKAMA Kuu imempa mwanablogu na mtumiaji wa mitandao ya kijamii, Ndiang'ui Kinyagia, fidia ya Sh5 milioni baada ya kubaini kwamba maafisa wa polisi walikiuka haki zake walipovamia nyumba yake, kuipekua, kutwaa mali yake na kumzuia kusafiri kwa uhuru. Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Patricia Nyaundi wa Kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu jijini Nairobi, mahakama ilisema polisi waliingia nyumbani kwa Kinyagia mnamo Juni 21, 2025, bila kibali cha mahakama na bila kuthibitisha kuwa walitimiza masharti ya kufanya upekuzi bila kibali hicho. Jaji Nyaundi alisema maafisa hao walishindwa kuwasilisha sababu zilizoonyesha kwamba kupata kibali cha mahakama kungeathiri au kuchelewesha uchunguzi wao. "Sehemu ya 60 ya Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi si tu tamko la kawaida. Ni kinga ya kikatiba iliyowekwa kisheria ili kulinda haki za wananchi," alisema jaji huyo. Kinyagia, ambaye ni mjasiriamali wa teknolojia na mchangiaji wa masuala ya umma mtandaoni, alipata umaarufu mnamo Juni 2025 baada ya kujificha alipogundua kwamba maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walikuwa wakimtafuta kufuatia chapisho la mtandaoni lililohusishwa na maandamano yaliyokuwa yakipangwa dhidi ya serikali. Polisi walikuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu ujumbe uliowekwa katika mtandao wa X waliodai ulikuwa wa uchochezi na wenye maudhui ya uasi. Baada ya kufuatilia akaunti hiyo hadi kwa Kinyagia na kupata usaidizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Kenya, maafisa walielekea nyumbani kwake. Mahakama ilielezwa kwamba polisi walipiga kambi katika makazi hayo kwa muda mrefu kabla ya kuvunja mlango na kuingia ndani waliposhindwa kumpata. Walipekua nyumba hiyo na kuondoka na vifaa mbalimbali huku wakiacha orodha ya vitu vilivyochukuliwa kwa msimamizi wa eneo hilo. Jaji Nyaundi aliamua kuwa hatua hiyo ilikiuka haki za Kinyagia za faragha, mali, utu, usalama wa kibinafsi na uhuru wa kutembea. Mahakama pia ilizuia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) pamoja na polisi kuendelea kumshtaki Kinyagia kuhusiana na uchunguzi huo, ikisema mchakato mzima ulianza kwa vitendo visivyozingatia Katiba.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

Vyombo vya habari Amerika vyamgomea Trump

WASHINGTON, Amerika: TELEVISHENI Amerika Jumatatu zilisitisha kwa pamoja kurusha matangazo ya shughuli za Rais Donald Trump kutoka Ikulu ya White House, baada ya CNN, Politico na MS NOW kuzuiwa kuingia katika jengo hilo. Trump alitangaza marufuku hiyo Ijumaa, akishutumu mashirika hayo kwa 'kuandika habari za kutunga na uongo' kuhusu utawala wake. Vyombo hivyo vilisema waandishi wao walizuiwa kuingia White House mnamo Jumamosi. CNN, Politico na MS NOW baadaye zilitangaza kuwa zitawasilisha kesi dhidi ya utawala wa Trump ili kutetea kanuni kwamba serikali haiwezi kuamua kile ambacho vyombo vya habari vinaripoti. Kufuatia hatua hiyo, White House ilianzisha kituo chake cha matangazo mtandaoni, Trump TV, kinachorusha sehemu za video ya rais saa 24 kwa siku. Vyombo vingine vya habari pia vilisema havitashiriki katika mfumo wa pamoja wa kuripoti shughuli za rais. New York Times na Washington Post, kwa mfano, zilisema hazitachapisha picha za matukio ya Trump. Hatua hiyo ilisababisha kukosekana kwa picha za televisheni za Trump akipanda ndege ya Air Force One au akiwasili New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Trump pia alishiriki katika hafla ya kuzindua uwanja mpya wa helikopta ya Marine One katika bustani ya White House. Hafla hiyo ilikuwa mbashara kwenye tovuti ya White House, ingawa sauti ya hotuba yake haikusikika. Baadaye rais alionekana kwenye televisheni baada ya kukutana na Meya wa New York Zohran Mamdani. Mamdani alimweleza kuwa waandishi wote wa habari watakaribishwa katika mkutano na wanahabari. Trump alisema hakushtushwa na hatua hiyo, akisema vyombo vya habari vilivyodai vitamsusia havijawahi kufanya hivyo. Mfumo wa ushirikiano wa vyombo vya habari huyawezesha mashirika ya habari kushirikiana ili kupunguza gharama na matumizi ya nafasi wakati wa kuripoti shughuli za rais. Bryan Boughton, mkuu wa afisi ya Fox News Washington, alisema katika barua pepe kuwa mfumo huo hautaendelea kuripoti shughuli za Trump zinazowashirikisha vyombo vyote vya habari. Alisema hatua hiyo ilifuatia White House kuzuia CNN kutekeleza jukumu lake katika ziara ya Trump New York. Siku hiyo hiyo, CNN, Politico na MS NOW ziliwasilisha kesi Mahakamani jijini Washington, zikisema White House ilifuta vibali vya waandishi wao bila kuwapa taarifa wala nafasi ya kujitetea. Vyombo hivyo vilisema hatua hiyo inatishia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya umma kupata habari huru bila kuingiliwa na serikali.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Wakazi wajenga ua kuzunguka  ardhi ya chuo baada ya agizo la Ruto

Wanajamii wa eneo la Oloitikosh katika Kaunti ya Kajiado wameanza kuweka ua kuzunguka ekari 60 za ardhi inayomilikiwa na Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Kajiado East (TVET), wiki mbili baada ya Rais William Ruto kuagiza ardhi hiyo ilindwe kwa ajili ya upanuzi wa taasisi hiyo. Shughuli ya kuweka ua Jumatatu iliongozwa na Naibu Chifu wa Oloitikosh, Moses Karaine, kwa ushirikiano na wakazi wa eneo hilo. Hatua hiyo imefuatia madai kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya awali ya chuo hicho yenye ukubwa wa ekari 76 ilinyakuliwa na kugawanywa na watu binafsi kwa ushirikiano wa mabroka na baadhi ya wanasiasa. Inadaiwa kuwa chuo kilibaki na ekari saba pekee ambako majengo yake yamejengwa. Wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo hilo wiki mbili zilizopita, Rais Ruto aliamuru ekari 60 zilizokuwa zikizozaniwa ziwekwe ua mara moja ili kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye ya chuo hicho. "Ardhi hii lazima ilindwe na kuwekwa ua. Nitarudi mwenyewe kukagua maendeleo. Baadaye TVET hii inaweza kukua na kuwa chuo kikuu," alisema Rais wakati wa uzinduzi wa mabweni ya wanafunzi chini ya mpango wa Boma Yangu. Chuo hicho, ambacho kina umri wa miaka 10, kwa sasa kina takriban wanafunzi 800 wanaosomea kozi mbalimbali za kiufundi. Pia ndicho taasisi pekee ya serikali katika Kaunti ya Kajiado iliyo na kituo cha kidijitali cha Jitume Digital Hub. Mkuu wa chuo hicho, Watiri Kiragu, alisifu hatua ya rais akisema kurejeshwa kwa ardhi hiyo kutatoa nafasi muhimu kwa upanuzi wa taasisi hiyo siku zijazo. "Msingi wa upanuzi wa taasisi yoyote ni upatikanaji wa ardhi. Uamuzi huu ni wa manufaa makubwa kwa maendeleo ya chuo," alisema. Mzee Daniel Lepatei, ambaye alipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa ua huo, alisema jamii imejitolea kulinda ardhi hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Kwa mujibu wake, mabroka wa ardhi walianza kugawa sehemu ya ardhi hiyo miaka mitano iliyopita na kupata barua za ugavi kwa njia isiyo halali. "Amri ya rais imeokoa mustakabali wa vijana wetu. Fedha za kujenga ua zimepatikana na taratibu za kurejesha ardhi zimekamilika," alisema. Nao viongozi wa jamii walidai kuwa baadhi ya maafisa wa utawala, wanasiasa na maafisa wa ardhi walihusishwa na unyakuzi wa ardhi hiyo. Hata hivyo, Waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Kajiado, Hamilton Parseina, alisema barua zote za ugavi zilizokuwa zimetolewa kwa watu binafsi tayari zimefutwa. "Ardhi hii ni mali ya chuo cha TVET. Barua zilizokuwa zimetolewa hapo awali zimebatilishwa ili kuruhusu upanuzi wa taasisi hiyo," alisema. Hatua ya kuzungusha ua ardhi hiyo imepokelewa kwa furaha na wakazi, ambao wanasema italinda rasilimali ya umma wakati ambapo maeneo mengi ya Kitengela yanaendelea kukabiliwa na ongezeko la visa vya unyakuzi wa ardhi ya taasisi za umma.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Murkomen sasa atangaza vita dhidi ya pombe Baringo

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewaamuru maafisa wa usalama katika Kaunti ya Baringo kuimarisha msako dhidi ya pombe haramu na kuwawajibisha wanaohusika na biashara hiyo. Bw Murkomen alisema amepokea ripoti kwamba utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu, ikiwemo ile inayodaiwa kuwa na kemikali ya ethanol, umeongezeka Kabarnet na maeneo ya jirani. Akizungumza wikendi wakati wa ibada ya madhehebu mbalimbali katika Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Kabarnet, Bw Murkomen aliwataka maafisa wa usalama kumtafuta mwanamke anayejulikana kwa jina la Targok, ambaye anadaiwa kujihusisha na biashara hiyo. "Nimeambiwa wakuu wa maeneo wamejaribu kukomesha pombe haramu, lakini kuna baadhi ambayo ni mbaya sana, kama yenye kemikali ya ethanol. Nimesikia kuna mwanamke anayeitwa Targok, ambaye ni mtengenezaji na muuzaji wa pombe haramu na mara nyingi hukamatwa na kuachiliwa mahakamani," akasema. Bw Murkomen alimtaka Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Baringo Macharia Wanjau kuhakikisha Targok anakamatwa na kufikishwa mahakamani. Alimweleza Kamishina wa Kaunti ya Baringo Wesley Koech kuwa nafasi yake itakuwa hatarini iwapo maafisa wa usalama watashindwa kukabiliana na biashara hiyo. "Ni jukumu lako kuchagua kati ya Targok maarufu na kazi yako. Chagua kumwokoa yeye au kazi yako," akasema. Wiki moja iliyopita, polisi walivamia boma moja katika kijiji cha Kaprogonya, nje kidogo ya Kabarnet, wakipata kile walichokieleza kuwa chumba cha siri kilichojengwa chini ya sakafu ya bafu. Polisi walikuwa wakimtafuta Targok baada ya kupata taarifa za kijasusi kwamba pombe haramu na kemikali zilikuwa zimefichwa katika boma hilo. Hata hivyo, alikuwa tayari ametoroka walipofika. Baada ya kupekua eneo hilo kwa karibu saa mbili, maafisa waligundua shimo chini ya vigae vya bafu. Ngazi iliwaongoza hadi kwenye chumba cha chini kilichojengwa kama tangi la majitaka. Ndani walipata zaidi ya mitungi 40, kila mmoja ukiwa na kemikali iliyoshukiwa ya ethanol kwa jumla ikiwa zaidi ya lita 1,000. Naibu Kamishina wa Kaunti ya Baringo ya Kati Joseph Ng'eny alisema boma hilo lilionekana kutengenezwa kwa njia maalumu ili kuficha biashara hiyo. "Kwa mtazamo wa kwanza unaweza kudhani hii ni nyumba ya kawaida, lakini tulipoingia tuligundua ilikuwa kiwanda cha kutengeneza pombe haramu," akasema. Mbali na pombe haramu, Bw Murkomen aliwataka machifu na wazee wa vijiji kuacha kushughulikia kesi za ubakaji na kulawiti watoto, akisema washukiwa wanapaswa kukamatwa na kufikishwa kortini. Alisema baadhi ya wahalifu wa unyanyasaji wa kimapenzi ni watu wanaoaminika na familia, wakiwemo jamaa, walimu, wachungaji na watu wengine wenye mamlaka.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Mnafaa kuheshimu wazee walionitawaza, Kindiki aambia wakosoaji

NAIBU Rais Kithure Kindiki amewataka viongozi wa Mlima Kenya kuwaheshimu wazee na kusikiza wito wao wa umoja, akisema tofauti za kisiasa hazifai kuruhusiwa kuvunja jamii ambayo imeshirikiana kwa miaka mingi. Profesa Kindiki alisema amezingatia kwa uzito wito wa wazee wa kuongoza juhudi za maridhiano na umoja katika eneo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Alisema ataheshimu mwongozo wa wazee anapozifikia jamii za Mlima Kenya Mashariki na Magharibi katika juhudi za kujenga umoja wa kisiasa. Naibu Rais alisema hayo siku chache baada ya wazee wa Mlima Kenya kukutana katika Uwanja wa Kirigiti, Kaunti ya Kiambu, na kumtawaza kama kigogo wa siasa za eneo hilo. Wazee hao walitoa wito wa umoja miongoni mwa jamii za Agikuyu, Embu, Ameru na Mbeere na kuwataka wakazi wa eneo hilo kubaki na umoja wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Pia walionyesha kuunga mkono utawala wa Rais William Ruto, hivyo kumpa Profesa Kindiki jukwaa jipya la kuhakikisha eneo hilo linamuunga mkono Rais. Profesa Kindiki alisema viongozi wanapaswa kuheshimu tofauti za kisiasa lakini wasizigeuze kuwa migawanyiko inayolemaza eneo hilo kimaendeleo. Amekuwa akipinga juhudi za kugawanya Mlima Kenya kwa misingi ya Mashariki na Magharibi, akisema jamii hizo zina uhusiano mkubwa wa kihistoria, kitamaduni na kiuchumi kuliko tofauti zao za kisiasa. Wito huo unakuja wakati siasa zikizidi kushika kasi katika eneo hilo, huku makundi hasimu yakitafuta kushawishi mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo kuelekea 2027. Profesa Kindiki alisisitiza atatekeleza maagizo ya wazee kwa kupitia ziara za maendeleo katika Mlima Kenya Mashariki na Magharibi. Baada ya mkutano wa Kirigiti, alikagua ujenzi wa Barabara ya Mukothima-Gaciongo-Gatunga katika eneobunge la Tharaka, Kaunti ya Tharaka Nithi, kabla ya kuhutubia wakazi katika Soko la Gaciongo wakati wa mkutano wa umma. Naibu Rais ameweka barabara, miundombinu na utekelezaji wa mipango ya Serikali kuwa nguzo kuu za ziara zake, akisema uongozi wa kisiasa unapaswa kulenga kuboresha maisha ya wananchi. Wazee wa Kirigiti waliwataka jamii za Mlima Kenya kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu masuala yanayoligusa eneo hilo na kukataa juhudi za kuunda makundi tofauti ya kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Makanisa 2 yapigana mahakamani kuhusu umiliki wa jina 'Gospel of God Church'

MAKANISA mawili yameingia katika mzozo wa kisheria kuhusu haki ya kutumia jina "Gospel of God Church", huku rekodi zinazokinzana za usajili zikiwa kiini cha mgogoro wa zaidi ya miongo minne kuhusu utambulisho na mali ya kanisa. Mzozo huo unahusu ni upande upi una haki kisheria kutumia jina hilo na kudai mali zilizopatikana kwa jina hilo. Hii ni baada ya usajili wa mnamo 1968 kufutwa 1985, kisha usajili mpya wa 2004 kabla ya kurejeshewa jina la awali mnamo 2009. Upande mmoja umesajiliwa kama Gospel of God Church (SOC 7670), awali ikijulikana kama African Gospel Church, iliyotambuliwa kisheria mnamo 1968. Upande mwingine ni Gospel of God Church International (SOC 45700), awali ikijulikana kama Glorious Gospel of God Church, iliyosajiliwa mnamo 2004. Mzozo huo umepitia Afisi ya Msajili wa Mashirika, mahakama zinazoshughulikia ardhi na Mahakama Kuu, huku kila upande ukiwasilisha maelezo tofauti kuhusu taasisi ambayo kisheria iliendelea kuwepo baada ya mabadiliko hayo. Mzozo huo pia unahusu ardhi, majengo ya makanisa, magari na mali nyingine zilizopatikana kwa miongo kadhaa. Wiki iliyopita, Jaji Roseline Aburili alitupilia mbali ombi la kikatiba la Gospel of God Church International (SOC 45700), bila kuamua ni upande upi unaomiliki jina hilo au mali zinazobishaniwa. Mahakama ilisema waliowasilisha kesi walipuuza utaratibu wa kisheria wa kukata rufaa baada ya Msajili wa Mashirika kutoa maamuzi Agosti na Oktoba 2024, akiamuru SOC 45700 irejee kwa jina lake la awali, Glorious Gospel of God Church, ndani ya siku 30 au ifutiwe usajili. Chini ya Sheria ya Mashirika, taasisi isiyoridhishwa na uamuzi wa Msajili inapaswa kwanza kukata rufaa kwa Serikali kabla ya kuelekea Mahakama Kuu. "Kwa hivyo, ninapata kwamba ombi hili liliwasilishwa mapema na kupuuza kabisa masharti ya Sheria ya Mashirika," alisema Jaji Aburili. Rekodi za mahakama zinaonyesha Gospel of God Church, SOC 7670, ilianzishwa Kenya 1968 na kupewa msamaha wa usajili Agosti 26 mwaka huo. Mnamo 1985, baada ya serikali kuingilia kati na viongozi wa kigeni kuondoka, wanachama wa Kenya walichagua viongozi wao. Naibu Msajili baadaye alifuta msamaha huo kupitia notisi ya gazeti rasmi. Waliowasilisha kesi walidai hatua hiyo ilimaliza uwepo wa kisheria wa kanisa hilo, na viongozi wa eneo hilo wakasajili Glorious Gospel of God Church of Kenya mnamo 2004. Msajili aliidhinisha mabadiliko ya jina kuwa Gospel of God Church International Machi 22, 2005. Hata hivyo, kundi la awali la Gospel of God Church, SOC 7670, lilirejeshwa katika usajili Novemba 11, 2009. Kundi hilo lilisema ndilo kanisa linalotambuliwa kisheria na lenye haki ya kumiliki mali yenye thamani ya mabilioni ya pesa. Jaji Aburili pia aligundua kuwa makanisa hayo hayakuwa na uwezo wa kufungua kesi kwa majina yao bila kutaja viongozi waliosajiliwa na kutoa idhini ya maandishi. Mahakama hivyo ilitupilia mbali ombi hilo na kuwaelekeza wahusika kufuata kwanza utaratibu wa rufaa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 23 hours ago

Shahbal njiapanda kuhusu ugavana, akumbushwa 'ana dili nyingi za kibiashara na serikali'

MWEKEZAJI na mwanasiasa Suleiman Shahbal anakabiliwa na changamoto ya kutenganisha mikataba yake ya mabilioni ya pesa katika miradi ya serikali na azma yake ya ugavana Mombasa, huku shinikizo ikizidi kwake ajiondoe kwenye kinyang'anyiro cha 2027. Shinikizo hizo zimezidi kujitokeza wiki chache baada ya kutia saini mkataba wa kuanzisha Eneo Maalum la Kiuchumi (SEZ) jijini Mombasa na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji bandarini ya DP World katika Ikulu ya Nairobi. Rais William Ruto awali alikuwa amemshauri Bw Shahbal kuachana na siasa, lakini mfanyabiashara huyo akakataa. Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Omar Hassan, ambaye pia analenga kumng'oa Gavana Abdulswamad Nassir kitini, sasa amesema kuna hatari ya kutokea mgongano wa maslahi iwapo Bw Shahbal atakuwa gavana wa Mombasa huku akiendelea kuwa mshirika mkubwa katika sekta ya biashara ya kaunti hiyo. Mkataba huo wa Sh12 bilioni kati ya kampuni yake ya GulfCap Group na DP World unalenga kujenga Eneo Maalum la Kiuchumi (SEZ) lenye ukubwa wa ekari 535 Jomvu. Ardhi hiyo inamilikiwa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa na hapo awali ilikodishwa kwa shirika la Kenya Meat Commission. Mbali na mradi wa SEZ, GulfCap pia inahusika katika ujenzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti mtaani Buxton. Mradi huo wa Sh6 bilioni ulianzishwa wakati wa utawala wa zamani wa kaunti chini ya gavana wa zamani Hassan Joho, ambaye sasa ni Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, baada ya kubomolewa kwa nyumba za zamani za kaunti. Vilevile, GulfCap ina mradi mwingine kama huo jijini Nairobi. "Ukiwa mfanyabiashara, shikilia biashara na uwaachie wasimamizi wa serikali jukumu la kuweka mifumo na taratibu zinazostahili, kwa sababu una mgongano wa maslahi," Bw Omar alisema. Huku akijipigia debe, Bw Omar alitaja uzoefu wake kama mwanaharakati wa haki za binadamu, seneta wa zamani wa Mombasa na Katibu Mkuu wa UDA kama sehemu ya sifa zake katika kinyang'anyiro cha ugavana. Alisema azma yake ya kisiasa imechochewa na hitaji la kuboresha utawala na kurejesha heshima, hadhi na uzingatiaji wa Katiba Mombasa. Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, pia alimkosoa Bw Shahbal kwa kumpinga Gavana Nassir katika uchaguzi wa 2027, licha ya serikali ya kaunti kumuunga mkono katika mpango wake wa kuendeleza SEZ. "Wale wanaomiliki SEZ wameanza kumpiga vita gavana hata kabla mradi haujaanza. Lakini leo tunawaambia kwamba gavana ataweka siasa kando. Huu sasa ni wakati wa maendeleo. Mtu mnayempiga vita ndiye huyo huyo atakayewanyooshea mkono na kuunga mkono mradi ili maendeleo yaje na watu wapate ajira," alisema. Wakati wa kusainiwa kwa mkataba wa SEZ Septemba 8, Rais Ruto alisema Kenya inahitaji wawekezaji wakubwa, wawekezaji na wajasiriamali makini wenye uwezo wa kutekeleza miradi itakayochangia ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, Bw Shahbal alikataa wito wa kuachana na siasa na ameendelea kusisitiza kuwa atawania kiti cha ugavana wa Mombasa mwaka 2027. Hivi majuzi, mbunge huyo wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) alieleza wasiwasi kwamba siasa za ugavana zinaweza kuathiri mradi wake na kuwataka wapinzani wake kuweka tofauti zao kando ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa. Bw Shahbal, ambaye ametangaza kuwa hatatafuta tiketi ya ODM kugombea mwaka wa 2027, alimuonya Rais Ruto dhidi ya mipango ya kisiasa ya kugawana maeneo kati ya ODM na UDA, almaarufu kama 'zoning'. "Upuuzi huu wote wa kugawana maeneo umeandaliwa na watu wanaoogopa kuenda mashinani kukutana na watu. Ikiwa una imani na uongozi wako, nenda kwa wananchi uwaambie ulichofanya nao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 16:37:32

Vyeti feki vyanoga miongoni mwa wanaoajiriwa serikalini

WAKENYA wanaotumia vyeti ghushi vya masomo kupata ajira, vyeo na mishahara mikubwa sasa wanaandamwa huku hukumu za hivi majuzi zikifichua jinsi barua hizo zimekuwa zikitumiwa kuingia na kupanda ngazi katika utumishi wa umma. Mnamo Jumatatu, mahakama moja jijini Nairobi ilimpiga faini ya Sh80,000 aliyekuwa afisa msaidizi wa uchaguzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), George Kipyatich Kibor, baada ya kupatikana na hatia ya kuwasilisha cheti ghushi cha shahada. Bw Kibor aliwasilisha cheti ghushi cha Shahada ya Usimamizi wa Biashara (Fedha na Benki) alichodai kilitolewa na Chuo Kikuu cha Moi. Hukumu yake ilitolewa siku chache baada ya aliyekuwa afisa wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme nchini (KenGen), David Mogire Nyabuti, kuhukumiwa kifungo cha miaka 11 kwa kutumia barua ghushi za masomo kupata ajira na kujipatia karibu Sh15 milioni. Bw Nyabuti alitumia cheti ghushi cha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne(KCSE) na hati ya matokeo kupata nafasi ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo cha Kampuni ya Umeme Nchini (KPC) kabla ya kupata ajira KenGen. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilibaini kuwa aliwasilisha barua hizo kama vyeti halali vilivyotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC). Kati ya Agosti 2003 na Septemba 2018, alipokea Sh14.94 milioni kama mishahara na marupurupu kutokana na udanganyifu huo. Mahakama ilimpata na hatia ya kujipatia mali ya umma kwa njia ya udanganyifu na kumuamuru kurejesha fedha hizo au kutumikia kifungo cha miaka mitano. Pia alipigwa faini ya Sh900,000, huku akikabiliwa na kifungo cha miaka miwili iwapo angeshindwa kulipa. Kesi hizo ni sehemu ya tatizo kubwa la vyeti ghushi katika taasisi za umma. EACC inasema imefikisha mahakamani kesi 90 zinazohusu vyeti ghushi vya masomo. Kati ya hizo, 43 zimeishia wahusika kuhukumiwa, 39 bado zinasubiri kuamuliwa, washukiwa saba waliachiliwa huru na kesi moja iliondolewa. Katika mwaka wa kifedha wa 2025/26 pekee, EACC ilirejesha Sh18.5 milioni zilizolipwa kwa njia ya udanganyifu kwa maafisa wa umma kupitia mishahara iliyotokana na vyeti ghushi na ajira mbili. Miongoni mwa waliopatikana na hatia ni Martin Maigua Maina, aliyedanganya kwa kutumia cheti cha Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa ili kupata cheo IEBC. Jecinter Hezron Adoyo alishtakiwa kwa kughushi barua za masomo kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ili kupata ajira katika Tume ya Ugavi wa Mapato kama mdadisi mkuu na msaidizi wa kibinafsi wa mwenyekiti. Katika Kampuni ya Maji ya Nairobi, Stacy Mwikali alitumia cheti ghushi cha Shahada ya Teknolojia ya Habari alichodai kimetolewa na Chuo Kikuu cha JKUAT kupata cheo cha kaimu meneja kampuni hiyo. Aliyekuwa mfanyakazi wa Kaunti ya Nairobi Gabriel Bukachi Chapia alihukumiwa mwaka jana kifungo cha miaka miwili na nusu, huku akipewa chaguo la kulipa faini ya Sh150,000, baada ya kukiri kughushi vyeti vya masomo. Pia aliamriwa kurejesha Sh3.9 milioni alizopata alipokuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 07:55:25

Kituo kikuu cha kujumuisha kura chazidi kuleta utata kuelekea uchaguzi 2027

ZIKIWA zimesalia miezi 11 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027, vita vya kisheria kuhusu kuwepo kwa Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura za Urais (NTC) vimeanza kushika kasi, huku macho yakielekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa kikatiba wa NTC Septemba 22, 2026, kufuatia kesi zilizowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah pamoja na viongozi wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DCP Rigathi Gachagua. Walalamishi wanataka mahakama itangaze kuwa kuanzishwa na kuendesha NTC kwa ajili ya kuthibitisha tena matokeo ya urais ni kinyume cha Katiba, na hivyo kubatilishwe. Wanadai kuwa katiba inaweka eneobunge kuwa kituo cha msingi na cha mwisho cha kuhesabu, kuthibitisha na kutangaza matokeo ya urais. Wanaopinga NTC pia wanataka IEBC izuiwe kuhesabu tena au kubadilisha matokeo yaliyotangazwa na maafisa wasimamizi wa uchaguzi wa maeneobunge. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ameunga mkono wito wa kuondolewa kwa NTC. "Katiba haitoi nafasi kwa kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura. Jukumu la IEBC ni kutangaza matokeo, wala si kuhesabu kura tena," akasema Maraga. Hata hivyo, msimamo huo unatofautiana na uamuzi wa Mahakama ya Juu katika kesi ya uchaguzi wa urais wa 2017. Mahakama hiyo ilisema IEBC ina jukumu la kujumuisha na kuthibitisha kura kabla ya kutangaza mshindi, huku mchakato huo ukiendelea kutoka kituo cha kupigia kura hadi eneobunge na hatimaye NTC. Katika kesi ya 2022, Mahakama ya Juu ilifafanua kuwa jukumu la kuhesabu na kuthibitisha matokeo katika NTC ni la IEBC kama taasisi, huku mamlaka ya kutangaza mshindi yakiwa ya mwenyekiti wa tume. Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na aliyekuwa rais wa Chama cha Mawakili (LSK) Nelson Havi pia wameunga mkono kuondolewa kwa NTC, wakisema matokeo yaliyohesabiwa na kutangazwa katika maeneobunge 290 yanapaswa kuwa ya mwisho. Kwa upande mwingine, aliyekuwa kamishIna wa IEBC Paul Kurgat anasema Katiba haijaweka jengo maalumu kuwa kituo cha kuhesabia kura, bali inasimamia mchakato. Anasema Kanuni za Uchaguzi zinahitaji kuhesabiwa kwa kura kikamilike katika kituo kilichotangazwa rasmi na IEBC. Mzozo huo sasa unahusu zaidi ya eneo la Bomas, kwani kesi hizo zinahoji iwapo IEBC ina mamlaka ya kikatiba na kisheria kuthibitisha matokeo ya urais katika ngazi ya kitaifa baada ya kutangazwa katika maeneo bunge. Kwa kuzingatia uwezekano wa suala hilo kufikishwa Mahakama ya Juu, uamuzi wa Mahakama Kuu unaweza kuwa hatua ya kwanza katika vita virefu vya kisheria kuhusu mfumo wa kuhesabu na kuthibitisha matokeo ya urais kuelekea uchaguzi wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 21 Sep 2026 06:55:28

Ruto kupigia uwekezaji nchini Kenya debe katika kongamano la UNGA

RAIS William Ruto aliondoka Nairobi kuelekea New York, Amerika, Jumamosi usiku ambako anatarajiwa kutumia Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) kutangaza Kenya kama kitovu cha uwekezaji, teknolojia na fedha Afrika. Ziara yake ya siku tano itajikita katika kuvutia uwekezaji katika sekta za kawi, miundomsingi, kilimo, viwanda, afya, teknolojia na Akili-Unde (AI). Mradi unaotarajiwa kupewa uzito ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Sh2.2 trilioni ($17 bilioni) mjini Lamu. Serikali inasema kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku kinaweza kuunda zaidi ya nafasi 60,000 za ajira na kusababisha Kenya na mataifa ya karibu kujitosheleza kwa kawi. Kulingana na Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, Rais Ruto atashirikiana na mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote kuongoza mikutano ya uwekezaji iliyoandaliwa na kampuni za Africa Finance Corporation na Global Africa Business Initiative. Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuanza Septemba 30. Katika hotuba yake UNGA, Rais Ruto pia anatarajiwa kutetea mpango wa Afrika kujifadhili, maarufu kama "Africa-financing-Africa", unaolenga kutumia zaidi akiba na mitaji ya Waafrika kufadhili maendeleo ya bara. Rais atatoa wito wa mageuzi na dhamana za kimataifa zitakazowezesha mtaji huu kutumika katika miundomsingi, biashara na vipaumbele vingine vya maendeleo," alisema Bw Mohamed. Rais pia atatangaza Hazina ya Kitaifa ya Miundomsingi inayolenga kukusanya hadi $40 bilioni (Sh5.7 trilioni) kupitia wawekezaji binafsi na taasisi bila kuongeza deni la serikali. Teknolojia na Akiliunde pia zitakuwa sehemu muhimu ya ziara hiyo. Rais Ruto na Rais wa Finland Alexander Stubb wataongoza AI Middle Powers Initiative, inayolenga kuunganisha rasilimali za kompyuta, data na wataalamu ili mataifa yaendeleze uwezo wao wa AI.

read more