T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 14 Oct 2026 06:55:39

Mwanamke aliyefariki Nanyuki hakuwa na Ebola, vipimo vyathibitisha

HOFU ya uwezekano wa mlipuko wa Ebola mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, imepungua baada ya vipimo kuthibitisha kuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 35 aliyefariki hospitalini hakuwa na virusi hivyo. Mwanamke huyo, aliyekuwa akifanya kazi katika duka la kuuza pombe mjini Nanyuki, alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nanyuki (NTRH). Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, Dkt Sammy Kilonzo, alisema mgonjwa huyo alifikishwa katika idara ya dharura saa 11 alfajiri Jumatatu akiwa na dalili za udhaifu wa mwili, homa na kikohozi kikavu kilichokuwa kikijitokeza mara kwa mara. Dkt Kilonzo alisema mwanamke huyo hakuwa na historia ya kusafiri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Uganda, wala kuwasiliana na mtu aliyekuwa na dalili kama zake. Hata hivyo, katika saa 24 kabla ya kufikishwa hospitalini, alianza kupata shida ya kupumua na kuvuja damu kupitia sehemu za mwili na maeneo yaliyokuwa yamedungwa sindano, hali iliyozua wasiwasi miongoni mwa wahudumu wa afya. Akizungumza na Taifa Leo, Dkt Kilonzo alisema sampuli za mgonjwa zilipelekwa katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini (Kemri) Jumatatu jioni kwa uchunguzi. Mwili wake ulihifadhiwa hospitalini huku wodi aliyokuwa amelazwa ikifungwa kwa muda wahudumu wakisubiri matokeo ya vipimo. Mhudumu mmoja wa afya katika hospitali hiyo, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa mwanamke huyo huenda alifariki kutokana na upungufu mkubwa wa damu. Dkt Kilonzo alisema hospitali iliruhusu mwili wake kuhamishwa hadi mochari baada ya kupokea matokeo yaliyothibitisha kuwa hakuwa na Ebola. Alisema hospitali ilichukua tahadhari zote muhimu kulinda wahudumu wa afya na kituo hicho wakati wa kumhudumia mgonjwa huyo. Baada ya taarifa hizo kusambaa, shirika la kijamii la Sheria Mashinani liliwataka wakazi wa Nanyuki na maeneo mengine ya Laikipia kutulia na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa. Mwangi Wangai, anayetaka kuwania ubunge wa Laikipia Mashariki, alisema taarifa hizo ziliwatia hofu wakazi, huku baadhi yao wakihoji kilichotokea. Aliitaka serikali kutoa taarifa sahihi na kwa wakati wakati wa dharura za kiafya ili kujenga imani ya wananchi na kuondoa mkanganyiko.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 14 Oct 2026 07:55:00

Ruto azindua kauli mbiu mpya, aponda upinzani

RAIS William Ruto amegeuza ziara yake ya siku 10 katika eneo la North Rift kuwa jukwaa la kushambulia wapinzani wake kisiasa huku akiwataka kueleza mipango yao ya maendeleo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Akiwa katika kaunti za Nandi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Baringo, Rais amekuwa akitetea rekodi ya serikali yake katika maendeleo huku akidai kuwa wapinzani hawana sera wala ajenda ya kuongoza nchi. Pia amezindua kaulimbiu mpya ya kisiasa, "Usawa ni Sawa", anayoitumia kueleza msimamo wake kuhusu usambazaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Akizungumza akiwa Kinyach, Baringo Kaskazini, Jumanne, Dkt Ruto alionya kuwa kuungana kwa wapinzani dhidi yake hakutawapa ushindi iwapo hawatakuwa na mipango madhubuti ya maendeleo. "Wameanza kuungana kwa jina la umoja, lakini hata wakiungana bila kuwa na ajenda, hesabu ya kikabila haitawasaidia. Wanapaswa kuwa na mpango ambao Wakenya watajiona ndani yake," alisema. Alisema uchaguzi wa 2027 unapaswa kuamuliwa kwa sera na ahadi za maendeleo badala ya ukabila, chuki, wivu na ubaguzi. Rais alidai kuwa serikali yake ina mpango wa kutekeleza miradi huku wapinzani wake wakikosa sera na manifesto wanayoweza kuwaeleza wananchi. Kaulimbiu ya "Usawa ni Sawa" ilipigiwa debe katika mikutano ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) mjini Kapyego na Chebara, Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Dkt Ruto aliwaongoza wafuasi wake katika wimbo wa kuitikiana akisema: "Nikisema UDA, nyinyi mjibu 'Usawa ni Sawa'. Nikisema 'Usawa ni Sawa', nyinyi mjibu 'Mbele Pamoja'." Kaulimbiu hiyo inajiri huku Rais akitetea miradi yake ya barabara, umeme, nyumba za bei nafuu, elimu na afya, akisema uwekezaji huo unalenga kubadilisha maisha ya wananchi. Pia alieleza wazi nia yake ya kuwania muhula wa pili, akiwataka wakazi wa North Rift kumpa kura kwa wingi. "Nahitaji kura zaidi milioni moja katika eneo hili. Urais hupatikana kupitia kura na ninahitaji uungwaji mkono wenu ili nipate muhula mwingine wa kuwatumikia," alisema. Aliwataka vijana waliotimu umri wa miaka 18 kupata vitambulisho vya kitaifa na kujisajili kama wapigakura. Rais pia alitetea mpango wa nyumba za bei nafuu dhidi ya wanaopinga ushuru wa nyumba, akisema mpango huo unazalisha ajira na kuwawezesha Wakenya kupata makazi bora. Alidai mpango huo umeunda ajira milioni moja. Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, alisema Sh15 bilioni zimetengwa kwa nyumba na miradi inayohusiana na mpango huo, ikiwemo zaidi ya nyumba 3,000 na mabweni wanafunzi. Alisema Sh18 bilioni zimetengwa kwa kilomita 270 za barabara na Sh1.6 bilioni kuunganisha zaidi ya nyumba 10,000 na umeme. Akiwa Baringo, alisema Sh22 bilioni zimetengwa kwa kilomita 350 za barabara, huku Sh2 bilioni zikilenga kuunganisha nyumba 25,000 na umeme. Pia alitaja barabara ya Kipsaraman-Kinyach yenye urefu wa kilomita 55 na gharama ya Sh4.5 bilioni, akisema itarahisisha biashara na kuimarisha usalama katika Bonde la Kerio. Katika sekta ya afya, Dkt Ruto alisema watu 365,000 wamejisajili katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) Elgeyo Marakwet, huku vituo vya afya vikipewa Sh1.2 bilioni. Kitaifa, alidai zaidi ya watu 33  milioni wamejisajili katika SHA na vituo vya afya vimepokea zaidi ya Sh200 bilioni.

read more