T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 15 Jul 2026 23:55:05

Ajabu bunduki ya jaji Muchelule kuhusishwa na ujambazi Nairobi, Kiambu na Kilifi

BUNDUKI iliyoibwa kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule mnamo 2025 imehusishwa na uvamizi dhidi ya wateja wa mkahawa mmoja eneo la Westlands wiki iliyopita. Silaha hiyo pia imehusisha na visa vya uhalifu katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Kilifi. Jumanne jioni, Jaji Muchelule aliwaambia polisi kwamba aligundua bunduki yake aina ya Beretta 92 ilikuwa imeibwa baada ya maafisa wa upelelezi kumpigia simu na kumfahamisha kuwa silaha hiyo imepatikana eneo la Joska, Kaunti ya Machakos. Bunduki hiyo ilipatikana nyumbani kwa mshukiwa wa ujambazi ambaye polisi wanaamini alikuwa miongoni mwa watu walionaswa na kamera za CCTV wakiwapora wateja wa mkahawa wa Chaii Wali Café Westlands. Aliwapora simu, fedha na vitu vingine vya thamani. Mshukiwa huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi Jumatatu baada ya kufyatuliana risasi na maafisa katika nyumba ya mpenzi wake huko Joska. Kamanda wa Polisi wa Joska Peter Gichohi alisema mshukiwa alikuwa amejificha eneo hilo tangu kisa cha Chaii Wali Café, huku polisi wakiendelea kuwatafuta washukiwa wengine watatu waliotoroka. Maafisa wa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) kutoka makao makuu na kituo cha polisi cha Matungulu walimkabili mshukiwa huyo, ambaye inadaiwa alianza kuwafyatulia risasi badala ya kujisalimisha. DCI ilisema walipata bunduki hiyo, risasi nne za milimita tisa na simu tatu za mkononi. Baada ya kuchunguza nambari ya usajili wa bunduki hiyo, ilibainika kuwa ilitolewa kwa Jaji Muchelule mnamo 2018. Jaji huyo aliwaambia maafisa wa DCI kuwa baada ya kupokea simu kuhusu kupatikana kwa bunduki hiyo, alikimbia nyumbani kwake kuangalia kama bado ilikuwa salama, lakini hakuiona. Katika taarifa yake kwa polisi, alisema alipokabidhiwa bunduki hiyo mnamo 2018 alikuwa amepewa risasi 15. Hii inaonyesha kuwa angalau risasi 11 tayari zimetumika. Uchunguzi unaonyesha bunduki hiyo pia ilitumika katika tukio la ujambazi wa kutumia nguvu huko Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, Februari mwaka huu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 15 Jul 2026 21:55:32

Leo ni leo Ol Kalou uchaguzi ukitarajiwa kutambulisha 'mwenye Mlima' kati ya Ruto na Rigathi

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou leo yatatoa mwelekeo wa kisiasa katika eneo lenye idadi kubwa ya wapigakura la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ni katika eneo hili ambapo chama cha UDA cha Rais William Ruto kilipata ushindi wake wa kwanza wa kisiasa baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa wadi ya Rurii dhidi ya Jubilee mnamo 2021. Wakati huo, Dkt Ruto alikuwa na uhasama wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya uchaguzi wa 2022. Yamkini historia inajirudia huku uchaguzi wa Ol Kalou ukigeuka pambano la kisiasa kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Wawili hao wamekuwa na tofauti kali ya kisiasa tangu Bw Gachagua abanduliwe madarakani mnamo Oktoba 2024. Baada ya ushindi wa Rurii, UDA iliendelea kushinda chaguzi ndogo mbalimbali katika Mlima Kenya na pia ikafagia viti vingi 2022 huku Jubilee ikipoteza ushawishi wake eneo hilo. Wandani wa Bw Gachagua wamesema uchaguzi wa Ol Kalou ni nafasi ya kuizika UDA Mlima Kenya na kuizindua rasmi DCP kama chama chenye umaarufu eneo hilo kuelekea 2027. Kwa upande wake, UDA inasema uchaguzi huo ni pambano kati ya siasa za maneno matupu na maendeleo. Chama hicho pia kinasema hata kama DCP itashinda kwa tofauti ndogo ya kura, huo utakuwa ushindi usio na maana kwa kuwa Bw Gachagua amekuwa akidai chama chake kitashinda kwa mwanya mkubwa. Ingawa hivyo, pande zote mbili zimeonyesha imani kuwa zitapata ushindi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) iliidhinisha wagombea tisa kuwania kiti hicho. Wao ni Sammy Ngotho (DCP), Abdullahi Hussein (Federal Party of Kenya), Kariuki Kamau (People's Renaissance Party), Samuel Muchina (UDA), Edward Mathenge (Kenya Moja Movement) na Rachael Njoroge (People's Democratic Party). Wengine ni Wilson Kigwa (Jubilee), Stephen Wanyoike (National Liberal Party) na Edward Muchiri (Party of National Unity). Mbunge katiika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, ambaye amekuwa akimpigia debe mgombea wa DCP, alisema ushindi wa chama hicho utathibitisha mwisho wa UDA Mlima Kenya. "Tunasema kifo cha UDA kitathibitishwa Ol Kalou Alhamisi. Hapa ndipo UDA ilizaliwa 2021, na hapa ndipo itazikwa. Siku hiyo hiyo tutakuwa tukisherehekea kuzaliwa kwa DCP Mlima Kenya," akasema. Aliongeza kuwa ushindani ni mkali kwa sababu UDA inataka kuonyesha bado ina ushawishi katika Mlima Kenya. "Ndiyo maana wametumia mamilioni ya fedha na kuzindua miradi ya mabilioni ya shilingi," akaongeza. Matokeo ya uchaguzi huo yanachukuliwa kuwa ya umuhimu mkubwa kwa Rais Ruto na Bw Gachagua kwa kuwa yanatoa taswira jinsi 2027 itakavyokuwa. Iwapo UDA itashinda, Rais ataonekana kama bado ana ushawishi mlimani. Pia utawapa viongozi wa Kenya Kwanza imani kuwa wananchi wanatambua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Aidha, ushindi huo utapunguza dhana kwamba Mlima Kenya umejitenga na Rais Ruto tangu Bw Gachagua aondolewe madarakani. Isitoshe ushindi unaweza kuvuruga mipango ya upinzani kwa kuonyesha kuwa kutoungana kwao kunarahisishia UDA kazi 2027. Kwa upande mwingine, iwapo UDA itapoteza, matokeo hayo yatafasiriwa kuwa wananchi wa Mlima Kenya wameikataa serikali ya Rais Ruto. Hii ni licha ya kumpa karibu kura milioni tatu katika uchaguzi wa 2022. Kushindwa huko kunaweza pia kuwashawishi viongozi zaidi kuhamia DCP ili kuokoa nafasi wanazoshikilia kisiasa. Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alisema uchaguzi huo utathibitisha madai ya DCP kuwa imeiteka Mlima Kenya ni uongo. "Matokeo haya yataondoa uongo unaoenezwa kuhusu umaarufu wa DCP. Wamekuwa wakidai UDA imepoteza Mlima Kenya kabisa," akasema. "Hawawezi kudai wanaidhibiti Mlima Kenya hata kiwa watashinda kwa idadi ndogo ya kura. Kwa vyovyote vile sisi tutashinda na mlima si ngome yao," akaongeza. Aliyekuwa Waziri Moses Kuria alisema uchaguzi huo ni mtihani kati ya siasa za matamshi na maendeleo ya kiuchumi. "Nataka kuona kama wananchi wataacha maendeleo na kufuata siasa za maneno. Je, watachagua maendeleo au porojo?" akauliza. UDA iliwatuma wabunge 25 kufanya kampeni huku pia ikipewa usaidizi na sekretarieti ya kampeni iliyoongozwa na Mtaalamu masuala ya kidijitali Dennis Itumbi. Kura ya maoni ya Infotrak iliyotolewa Jumatatu inaonyesha kuwa UDA inaungwa mkono na asilimia tisa pekee katika Mlima Kenya, tofauti kubwa na ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa 2022. Kwa sasa DCP ndiyo chama kinachoongoza kwa asilimia 33 huku asilimia 36 ya wapigakura wakisema bado hawajaamua. Kwa Gachagua, uchaguzi huo ni nafasi ya pili ya kupambana ana kwa ana na UDA baada ya uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, ambapo UDA ilishinda. UDA pamoja na mshirika wake ODM wamekuwa wakishinda chaguzi ndogo za hivi karibuni katika maeneo ya Mbeere North, Ugunja, Kasipul, Magarini, Malaba na pia kiti cha Seneta wa Baringo. Iwapo Bw Gachagua atashinda Ol Kalou, ushindi huo utathibitisha kuwa bado ana ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kuhalalisha madai yake kuwa DCP ndicho chama kikuu katika eneo hilo. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema uchaguzi huo ni suala la "maisha au kifo" kwa DCP. "DCP inataka kuonyesha inaweza kushindana na UDA bila msaada wa chama kingine, " akasema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 15 Jul 2026 21:55:36

Mkutano mkubwa wa Sifuna Bungoma wachemsha Magharibi Didmus naye akidaiwa kupanga wake

UMAARUFU unaozidi kuongezeka wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna umeibua ushindani mkali wa kisiasa katika eneo la Magharibi, huku viongozi wanaounga mkono serikali wakizidisha juhudi za kupunguza ushawishi wake. Bw Sifuna anatarajiwa kuongoza mkutano mkubwa wa kisiasa katika uwanja wa Posta, Bungoma mnamo Julai 26. Inatarajiwa kuwa baadhi ya wazee wa jamii ya Waluhya watamtawaza Bw Sifuna kuwa kinara mpya wa kisiasa wa eneo hilo na kumpa baraka za kuwania urais mnamo 2027. Kabla ya mkutano huo, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anatarajiwa kuwa mwenyeji wa Bw Sifuna na viongozi wenzake wa Linda Mwananchi mjini Kitale Julai 16. Kaunti za Bungoma na Trans Nzoia ni nyumbani kwa jamii ya Bukusu, ambako Sifuna anatoka. Jamii hiyo pia imewahi kuwatoa viongozi mashuhuri kama aliyekuwa Makamu wa Rais Wamalwa Kijana na mwanasiasa marehemu Masinde Muliro ambaye alipigania mfumo wa vyama vingi. Duru zinaarifu kuwa Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa anapanga kufanya mkutano sambamba mjini Bungoma siku hiyo hiyo Bw Sifuna anatarajiwa mjini humo. Bw Barasa, ambaye ametangaza kuwa atagombea ugavana wa Bungoma kwa tiketi ya UDA mnamo 2027, hakujibu simu wala ujumbe alipotafutwa kuthibitisha taarifa hizo. Mabw Barasa na Sifuna wamekuwa wakirushiana cheche katika mikutano ya hadhara na mazishi, hali inayozua hofu kwamba mikutano yao kufanyika siku moja kunaweza kuzua ghasia. Aliyekuwa Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi amelaani kile alichokitaja kuwa kampeni ya kupinga Sifuna inayoendeshwa na baadhi ya viongozi wa Mulembe. "Ninawasihi watu wetu wajitokeze kwa wingi kumpokea mwana wetu Sifuna. Katika ziara za upinzani zilizopita kulikuwa na njama za kuvuruga mikutano yetu, na sasa tuna taarifa kuwa kuna mipango kama hiyo dhidi ya ziara ya Linda Mwananchi ila wananchi tayari wameamua," alisema. Uhasama kati ya Bw Sifuna na Barasa umejitokeza mara kadhaa katika hafla za umma. Katika mazishi ya Patrick Wangamati, babake aliyekuwa Gavana wa Bungoma Wafula Wangamati, Bw Barasa aliondoka na umati mkubwa baada ya kuhutubia waombolezaji huku Bw Sifuna akimshutumu kwa kuwahonga wananchi. "Anapoona ninasimama kuhutubu, huondoka na kuwapanga watu kwenye foleni kuwapa Sh200. Bungeni hupigia kura nyongeza ya ushuru ili wananchi waumie, halafu anarudi kuwagawia pesa," akasema Bw Sifuna. Bw Barasa baadaye alijibu kwa mzaha akidai marehemu Wangamati alimjia kwenye ndoto na kumshukuru kwa kuwapa waombolezaji fedha. Katika mazishi ya nduguye Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka Julai 5, Bw Sifuna alisisitiza Barasa azungumze mwisho ili asiondoke na waombolezaji. Hata hivyo, Bw Barasa alitumia nafasi hiyo kuwashutumu viongozi wa Linda Mwananchi na kuwaita wachoyo. Baadaye kulitokea mzozo kati yake na Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, kabla ya Bw Barasa kufupisha hotuba yake na kuondoka akiwa ameandamana na umati mkubwa. Iwapo mikutano yote miwili itafanyika Julai 26, huenda hali ya kisiasa Bungoma ikawa na taharuki zaidi, hasa wakati ambapo kumekuwa na visa vya makundi ya wahuni kuvuruga mikutano ya kisiasa. Licha ya Bw Sifuna kuwa mzaliwa wa Bungoma, viongozi wanaomuunga mkono kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang'ula wanaendelea kusisitiza kuwa bado hajakomaa kuwania urais. Kati ya viongozi waliochaguliwa Bungoma, ni Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka na mwenzake wa Kabuchai Majimbo Kalasinga pekee waliotangaza wazi kumuunga mkono katibu huyo wa zamani wa ODM. Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, ambaye anaratibu kampeni za Rais William Ruto Magharibi, amesema eneo hilo linafaa kulenga kutoa rais mnamo 2032 badala ya 2027. "Wakenya wanaweza kukushawishi ugombee urais, lakini siku ya kura wakakuacha peke yako," alisema. Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula ameongeza mikutano ya mashinani na programu za uwezeshaji katika Magharibi, hatua inayotafsiriwa kama juhudi za kukabiliana na ushawishi unaoongezeka wa Sifuna.

read more