T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 23 Oct 2026 11:45:22

Waititu apata pigo tena akipoteza kesi

ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kukataa kufuta sheria inayowazuia waliopatikana na hatia ya ufisadi kushikilia nyadhifa za umma kwa miaka 10. Jaji Enock Chacha Mwita alisema Waititu na walalamishi wengine walishindwa kuthibitisha kwa nini Kifungu cha 64 cha Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi kinapaswa kutangazwa kuwa kinyume cha Katiba. Sheria hiyo inawazuia waliopatikana na hatia ya ufisadi au uhalifu wa kiuchumi kuchaguliwa au kuteuliwa katika nyadhifa za umma kwa miaka 10 baada ya kuhukumiwa. Waititu anatumikia kifungo cha miaka 12 kuhusiana na sakata ya ufisadi ya Sh588 milioni iliyohusisha utoaji wa zabuni ya ujenzi wa barabara Kiambu kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited. Alitozwa faini ya Sh53.5 milioni au kifungo cha miaka 12 gerezani. Aliyekuwa afisa mkuu wa barabara Kiambu Luka Mwangi Wahinya alitozwa Sh21 milioni au kifungo cha miaka saba, huku mkurugenzi wa kampuni hiyo Charles Chege Mbuthia akitozwa Sh295 milioni au kifungo cha miaka tisa. Walalamishi walipinga vifungo hivyo, wakisema vilizidi viwango vilivyowekwa na Sheria ya Kanuni za Adhabu. Hata hivyo, Jaji Mwita alisema mahakama ya rufaa ndiyo iliyofaa kushughulikia masuala hayo. "Mamlaka ya mahakama hii si mbadala wa mamlaka ya mahakama ya rufaa," alisema. Rufaa zao dhidi ya hukumu na adhabu zilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu inayoshughulikia kesi za ufisadi. Waititu, mkewe Susan Wangari na washirika wao wanatarajiwa kufika mahakamani Oktoba 27, 2026, kwa hatua ya kupunguziwa adhabu na kuhukumiwa kuhusu makosa ya kufua fedha na kupokea mapato ya uhalifu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 23 Oct 2026 11:15:56

Maelfu wakimbilia Moyale mapigano yakichacha Ethiopia

Hali ya wasiwasi imetanda mjini Moyale, kaunti ya Marsabit, huku maelfu ya wanawake na watoto wakikimbilia Kenya kutafuta usalama kufuatia mapigano makali kati ya vikosi vya Somali na Oromia nchini Ethiopia. Mapigano kati ya vikosi vya maeneo ya Nne na Tano nchini humo pamoja na maafisa wa usalama yameingia siku ya nne, huku milio ya risasi ikisikika karibu na mpaka. Wakazi walisema mapigano yaliripotiwa Ijumaa asubuhi katika maeneo ya Moyale na Hudhat nchini Ethiopia. Maelfu ya waliokimbia makazi yao wameingia Kenya, baadhi wakitafuta hifadhi kwa jamaa zao huku wengine wakilala mitaani na katika maeneo ya umma. Mamia wamepata hifadhi katika madrasa ya Manyatta, wadi ya Heillu Manyatta. Ali Abdullahi, mkazi wa Moyale, alisema mapigano yalikuwa yakiendelea takriban kilomita tano kutoka upande wa Kenya. "Mnamo Alhamisi, risasi  ziliwapata baadhi ya watu na majengo upande wa Kenya. Wakenya kadhaa walijeruhiwa na tuna hofu kuwa mapigano haya yanaweza kuendelea," alisema. Mfanyabiashara Ali Mumin alisema biashara kadhaa, zikiwemo benki, zimefungwa kutokana na hali ya usalama. "Biashara zimeathirika pakubwa kwa sababu tunategemea sana biashara kutoka Ethiopia. Kufikia sasa, maelfu ya wakimbizi wamekimbilia maeneo mbalimbali mjini Moyale," alisema. Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, alisema maafisa wa usalama wanafuatilia hali hiyo kuzuia mapigano yasivuke mpaka. Aliwataka wakazi kuwa macho na kuripoti shughuli zozote zinazotiliwa shaka, huku akiomba mashirika ya kibinadamu kusaidia wakimbizi. Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, Ahmed Idris, alisema shirika hilo limeanza kusaidia familia zilizoingia nchini, likilenga awali 1,000. Alisema wengi waliwasili bila mali nyingi na wanahitaji haraka makazi, chakula, maji na huduma za afya. Wahudumu wa shirika hilo, kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Marsabit na maafisa wa serikali ya kitaifa, walitoa mahema, blanketi, mikeka, mitungi ya maji na vifaa vya jikoni. Pia wanatoa huduma ya kwanza na chakula maalumu chenye virutubisho kwa watoto wadogo na kina mama wajawazito na wanaonyonyesha. Shirika hilo pia linasaidia familia zilizotenganishwa na mapigano kuwasiliana tena. "Kipaumbele chetu ni kuhakikisha kila familia inayowasili Moyale iko salama, ina makazi na inatendewa utu," alisema Dkt Idris.

read more