T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 14 Jul 2026 22:55:43

Upinzani na serikali waanza kuhofia umaarufu wa Linda Mwananchi

MWANZONI, wengi walichukulia vuguvugu la Linda Mwananchi kama kundi jingine ambalo lingemezwa na miungano ya kisiasa inayobadilika kila mara nchini. Hata hivyo, hali imebadilika. Leo hii, serikali ya Rais William Ruto pamoja na muungano wa upinzani unaoongozwa na Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua wanalitazama kama nguvu mpya inayoweza kuathiri matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2027. Matokeo ya hivi punde ya utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na Infotrak yanaonyesha kuwa vuguvugu hilo limeongeza ushawishi wake kisiasa. Kulingana na utafiti huo, kiongozi wa Wiper Musyoka angepata asilimia 13 ya kura ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, huku kinara wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna akiwa sawa na Fred Matiang'i wa Jubilee kwa asilimia 12. Kwa mwanasiasa ambaye ameibuka hivi majuzi kama sura ya vuguvugu hilo, kiwango hicho cha uungwaji mkono kimebadili hesabu za kisiasa nchini. Wachambuzi wanasema Sifuna sasa anaungwa mkono kwa kiwango ambacho hakiwezi kupuuzwa na Rais Ruto wala upinzani hauwezi kudhani kwamba kura zake zitahamia moja kwa moja kwa mgombea wao wa urais. Hali hiyo imefanya Linda Mwananchi kujikuta ikikosolewa na pande zote mbili za kisiasa. Akizungumza katika Ikulu Jumatatu, Rais Ruto aliwataka Wakenya kukataa upinzani na kumpa muhula wa pili. "Wao ni hatari kubwa kwa nchi yetu. Hawana ajenda ya kuipeleka Kenya mbele, wanataka kuturudisha nyuma," alisema. Rais aliwashutumu wapinzani kwa kukosa mawazo mapya na kuendelea kurejelea sera ambazo tayari zilishindwa. Ingawa hakulitaja moja kwa moja vuguvugu la Linda Mwananchi, kauli yake ilijiri wakati ambapo linaendelea kupata umaarufu kote nchini. Kwa upande wake, Sifuna amesema serikali imeingiwa na hofu kutokana na ushawishi unaoongezeka wa vuguvugu hilo. "Kila Mkenya anaweza kuona kwamba Linda Mwananchi imewashtua watu walio madarakani. Wanaamini njia pekee ya kutukabili ni kutumia vurugu, lakini hatutatishwa. Lazima nchi hii iokolewe," alisema baada ya shughuli za vuguvugu hilo kuvurugwa Kisumu na Nyahururu. Mchambuzi wa siasa Arnold Maliba anasema wengi walikosea kuchukulia Linda Mwananchi kama mshirika mwingine wa kisiasa. Anasema kundi hilo limekuwa likiweka shinikizo kwa serikali na pia kwa upinzani kwa wakati mmoja. Kulingana naye, nguvu yake kubwa si siasa za ukabila bali ajenda ya utawala bora, uwajibikaji, kuheshimu Katiba na ushiriki wa wananchi katika maamuzi. "Lengo lake si kubadili tu aliye madarakani, bali kubadili namna siasa zinavyofanywa nchini," anasema. Anasema pia vuguvugu hilo limevuka mipaka ya vijana pekee. Mbali na Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, sasa limevutia wanafunzi, wataalamu, wafanyakazi, wastaafu na hata viongozi wa zamani wa mapambano ya demokrasia akiwemo Gavana wa Siaya James Orengo. Aidha, limeanza kujijenga katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yalikuwa ngome za vyama vikuu vya kisiasa, ikiwemo Nyanza, Nairobi, sehemu za Magharibi na Pwani. Ukuaji huo umeanza kuwatia wasiwasi viongozi wa muungano wa upinzani. Wiki iliyopita, Bw Gachagua alimuonya Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata dhidi ya kuwaalika viongozi wa Linda Mwananchi kufanya kampeni Ol Kalou kabla ya uchaguzi mdogo. "Nimesikia Irungu Kang'ata akisema ataleta Linda Mwananchi Ol Kalou. Asilete kiherehere huko, si lazima," alisema. Kwa miezi kadhaa, upinzani umekuwa ukijaribu kupata mgombea mmoja wa urais kati ya Kalonzo Musyoka na Fred Matiang'i. Hapo awali kulikuwa na mazungumzo kwamba Sifuna angeweza kuwa mgombea mwenza. Lakini matokeo ya Infotrak yamebadili hali hiyo. Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya anasema Sifuna sasa ni mwanasiasa ambaye hawezi kupuuzwa. "Sifuna ni nguvu kivyake. Uchaguzi ni mchezo wa nambari. Hakuna anayeweza kumpuuza," alisema. Kwa mujibu wa Gakuya, Sifuna bado ana uwezo wa kuvutia kura Nyanza, Magharibi, Pwani na Nairobi, jambo linalompa nguvu katika mazungumzo ya kisiasa. Hata hivyo, Seneta wa Nandi Samson Cherargei anaamini bado hana miundo na fedha za kutosha kuwania urais. "Kama ni kijana mwenye hekima, abaki kuwa Seneta wa Nairobi na ajenge nguvu zake polepole. Hana rasilimali wala chama cha kisiasa cha kutosha kuendesha kampeni za urais," alisema. Mchambuzi John Anditi anakubaliana naye akisema ushindi wa urais unahitaji fedha nyingi, maajenti wa uchaguzi, chama chenye mizizi kote nchini na muungano mpana wa kisiasa. Lakini Geoffrey Mboya anaonya kuwa si lazima vuguvugu lishinde uchaguzi ili libadilishe siasa za nchi. Anasema linaweza kubadili mjadala wa kitaifa, kuathiri mazungumzo ya miungano na kuvutia wapigakura ambao hawakuwa wakishiriki siasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 14 Jul 2026 22:25:48

Kizaazaa kortini mwanaharakati akivua nguo DCI waliposema Kiamaiko 3 hawako kwa polisi

KIZAAZAA kilizuka katika mahakama kuu ya Milimani Jumanne mwanaharakati Julius Kamau alipovua shati akabaki nusu uchi baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kudai wanaume watatu waliokamatwa Kiamaiko eneo la Mathare mnamo Juni 19, 2026 hawako mikononi mwa polisi. Baada ya wakili Paul Nyamondi anayemwakilisha IG Kanja kusema hayo, Jaji Alexander Muteti aliwaamuru mkuu huyu wa polisi na mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai Mohamed Amin kufika kortini Julai 20, 2026 (Jumatatu ijayo) kueleza kule waliko - Michael Oloo, Evans Otieno na MacMillan Mugo. Hata kabla ya Bw Nyamondi kukamilisha sentensi hiyo kuhusu hatma ya wahasiriwa, Bw Kamau alifyatuka mahala alipokuwa ameketi akatoa shati huku akipiga duru akisema "Kenya imeisha. Tumenyanyaswa vya kutosha sasa, tunauawa, tunaibiwa, tumeteswa vya kutosha. Kama nikufa nife leo." Akiwa nusu uchi, alisongea karibu na Jaji Alexander Muteti akilalama vikali huku wazazi na jamaa wa wahanga hao pamoja na wanaharakati waliozidi 15 wakijifunika bendera ya Kenya wakipasua vilio na kila mmoja kuongea lugha yake. Walivuruga shughuli mahakamani kwa kupiga duru wooooi.. huku wakilia na kupiga mayowe na kelele za kila aina wakisema "serikali inateka nyara na kuua watoto wasio na hatia." Mama na jamaa za wahasiriwa - Michael Oloo, Evans Otieno na MacMillan Mugo - walipasua vilio huku wakidondokwa na machozi wakisema "sasa ni siku 26 na hatujui watoto wako wapi." Wakaendelea: "Ni aibu kwa Inspekta Jenerali Douglas Kanja kusema hajui watoto wetu wako wapi na ndiye kinara wa usalama wetu sote." Kina mama wengine yamkini jamaa wa karibu wa wahasiriwa walianguka na kugaagaa sakafuni wakilia wakiuliza "kweli tutatoa watoto wengine wapi. Hata mtu akizaa atalea saa gapi na uchumi ndio huu umezorota, hatuna pesa na nchi inaenda segemnege." Baba wa mmoja wahasiriwa hao alisimama na kuchomoka nje mbio akipiga duru na kurudi tena kortini akisema "Kenya imegauka kuwa Haiti. Sasa tuko Haiti. Rais William Ruto anasukuma nchi hii kutumbukia pabaya. Hatuna tofauti na Haiti sisi Kenya." Huku akitetemeka, baba huyo alisaidiwa na polisi alipoanguka na kuzirai. Hali kortini iligeuka ikawa ni kama mnara wa Babeli kila mmoja akiongea lugha yake huku mawakili Abner Mango, Ian Mutiso na John Ndegwa wakishindwa kuwatuliza wanaharakati na wazazi wa wahasiriwa. Wakati huu wote Jaji Alexander Muteti aliendelea kuandika uamuzi huku hali ikitokota. Mwanaharakati Julius Kamau aliyevua shati alikamatwa na kupelekwa seli huku wenzake wakichacha kwa kupiga duru. Ilikuwa hali ya mshike mshike. Mawakili wa wahasiriwa waliomba mahakama iamuru IG na DCI wafike kortini wenyewe kueleza waliko wahasiriwa. Jaji Muteti aliombwa aamuru IG na DCI wawasilishe majibu katika muda wa siku tatu kueleza walikowapeleka wanaume hao watatu. Bw Mutiso alieleza korti kwamba aliyekuwa rubani Mwenda Mbijiwe alitoweka hivyo yapata miaka minne sasa na polisi walidai hawakumshika. Mbijiwe bado hajulikani aliko. "Naomba hii mahakama iamuru IG na DCI wafike kortini kueleza waliko wateja wetu," Bw Mutiso alimrai Jaji Muteti. Akitoa uamuzi, Jaji Muteti aliwaamuru Kanja na Amin wafike kortini kueleza waliko wahasiriwa. "Suala hili la kutoweka kwa watu halieleweki kabisa. Ikiwa polisi hawajui kule waliko wahasiriwa nani atajua," Jaji Muteti alimuuliza wakili wa serikali. Oloo alikamatwa Juni 19, 2026 alipoenda kinyozi. "Oloo alichukuliwa kutoka kwa kinyozi na hajulikani alipelekwa wapi alipokamatwa na kuingizwa ndani ya Subaru," Jaji Muteti alifahamishwa. Jaji huyo hatimaye alizishauri familia za wahasiriwa ziwe na subira korti iwachukulie hatua wahusika. Kesi iliahirishwa hadi Julai 20, 2026 kwa maagizo zaidi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 14 Jul 2026 21:55:18

Hali si shwari 2027, ripoti ya wakfu wa Kofi Annan yatoa tahadhari

MWAKA mmoja kabla ya Wakenya kupiga kura, ripoti mpya imeonya kuwa nchi iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa 2027 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. Ripoti hiyo ya Kofi Annan Foundation inakadiria kuwa kuna uwezekano wa asilimia 81.6 wa kutokea kwa ghasia za uchaguzi. Ingawa inasema Kenya imepiga hatua kubwa tangu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008, inaonya kuwa mizizi ya migogoro hiyo bado haijang'olewa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna sababu moja pekee itakayochochea fujo. Badala yake, ni mkusanyiko wa sababu mbalimbali kama vile ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa, siasa za ukabila, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, kupungua kwa imani kwa taasisi za umma na kuongezeka kwa makundi ya wahuni wanaotumiwa na wanasiasa. Ripoti inapatia Kenya alama ya 43.9 katika Kielezo cha Hatari ya Uchaguzi, kiwango kilicho chini ya wastani wa cha Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara cha 51.1. Hii inaonyesha kuwa Kenya ina taasisi imara zaidi kuliko mataifa mengi yaliyo katika hatari kubwa ya migogoro ya uchaguzi. Hata hivyo, taasisi hizo zinaendelea kupoteza uaminifu wa wananchi kutokana na migawanyiko ya kisiasa, malalamishi ambayo hayajatatuliwa na wasiwasi kuhusu kutopendelea upande wowote kwa baadhi ya taasisi za serikali. Ripoti inaeleza kuwa tangu uchaguzi wa 2022, mazingira ya kisiasa yamekuwa yakitawaliwa na ugumu wa maisha, maandamano dhidi ya ushuru, hasira kuhusu ufisadi na mwenendo wa polisi pamoja na maandamano ya vijana yaliyotokea nje ya miundo ya kawaida ya vyama vya kisiasa. Kwa msingi huo, uchaguzi wa 2027 unaweza kuwa si ushindani wa urais pekee bali pia jukwaa la wananchi kudai uwajibikaji wa viongozi. Wataalamu wa taasisi hiyo wanashauri polisi wapewe mafunzo zaidi kuhusu namna ya kudhibiti umati bila kutumia nguvu kupita kiasi na kuhakikisha wanabaki huru kisiasa. Aidha, wanaitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuchapisha mapema ratiba ya shughuli zake, utaratibu wa usajili wa wapigakura, ununuzi wa teknolojia ya uchaguzi na namna matokeo yatakavyosimamiwa ili kuondoa hofu na uvumi. Ripoti hiyo imechapishwa wakati joto la kisiasa nchini linaendelea kupanda. Katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa upinzani wamekuwa wakilalamikia mashambulizi katika mikutano yao wakidai serikali imelegeza kamba kwa makundi ya wahuni wanaofadhiliwa kisiasa. Miongoni mwa waliodai kushambuliwa ni kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua na kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa walipokuwa wakielekea mkutano wa kisiasa Kikuyu. Kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua pia amedai kutishwa aliposhambuliwa akisimamia utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu katika Shule ya Msingi ya Gatoto, Mukuru kwa Reuben, Nairobi. Kwa mujibu wa viongozi wa upinzani, matukio hayo si ya kawaida bali ni ishara kwamba mazingira ya kisiasa yanaendelea kuzorota kuelekea uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Jana, viongozi wa muungano wa upinzani walisema ripoti hiyo inapaswa kuwa onyo kwa serikali na IEBC kuchukua hatua mapema. Bw Musyoka alisema uwezekano wa asilimia 81.6 wa vurugu unapaswa kuwatia wasiwasi Wakenya wote kwa sababu athari zake zitagusa uchumi na uwekezaji. Kukataa siasa za vurugu Alisema wawekezaji wa ndani na wa nje hufuata kwa karibu tathmini kama hizo na kwamba, hali ya kutokuwa na utulivu inaweza kuathiri maisha ya wananchi wengi. Bi Karua alihimiza Wakenya kukataa siasa za vurugu na kuwataka polisi kutii Katiba badala ya maagizo yasiyo halali. Alikumbusha viongozi walioko mamlakani kuwa madaraka si ya kudumu na kwamba ushindani wa kisiasa unapaswa kukubaliwa bila vitisho. Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema kurejea kwa makundi ya wahuni wa kisiasa kunahatarisha si demokrasia pekee bali pia uchumi na taswira ya Kenya kimataifa. Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana na kupanda kwa gharama ya maisha sasa ni sababu kuu zinazowasukuma vijana kujiunga na makundi ya kisiasa yanayotumiwa kuzua fujo. Tofauti na chaguzi zilizopita ambapo vurugu zilichochewa zaidi na ukabila, sasa matatizo ya kiuchumi yanatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha maandamano na migogoro. Ripoti inasema matukio ya hivi karibuni ya vijana wenye silaha kuvamia mikutano ya kisiasa katika maeneo kama Kisumu, Kisii, Nyahururu na Nyeri yanaonyesha kuwa matumizi ya wahuni wa kisiasa yanaanza kuwa jambo la kawaida. Pia, imeonya kuwa hali ya kisiasa imebadilika kwa kasi. Kulingana na utafiti wa Infotrak, iwapo uchaguzi ungefanyika sasa hakuna mgombea wa urais ambaye angepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika kushinda katika duru ya kwanza. Rais William Ruto anatajwa kupata takriban asilimia 32 pekee, jambo linaloongeza uwezekano wa duru ya pili yenye ushindani mkali. Ripoti pia inaeleza kuwa kifo cha aliyekuwa kinara wa upinzani Raila Odinga kimeacha pengo kubwa katika siasa za upinzani. Kutokuwepo kwake kumeibua mashindano ya uongozi, mazungumzo ya miungano mipya na kupanga upya mirengo ya kisiasa, hali ambayo inaweza kuongeza mvutano katika ngazi ya kitaifa na kaunti. Katika kaunti, uchaguzi wa ugavana unaendelea kutajwa kuwa chanzo kikuu cha migogoro kutokana na ushindani wa kudhibiti rasilimali na nafasi za ajira. Ripoti inasema iwapo taasisi kama IEBC, polisi na mahakama zitafanya kazi kwa uwazi, haki na usawa, Kenya inaweza kuepuka vurugu. Lakini iwapo kutazuka mashaka kuhusu usajili wa wapigakura, ununuzi wa teknolojia ya uchaguzi au upeperushaji wa matokeo, hali hiyo inaweza kuchochea propaganda, taarifa za uongo na migogoro. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema tume imejifunza kutokana na makosa ya chaguzi zilizopita na itasimamia uchaguzi kwa uwazi huku maajenti wa vyama wakiruhusiwa kushuhudia kila hatua ya kuhesabu kura. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pia amesema polisi wameanza maandalizi mapema na hawataruhusu wahuni wala wanasiasa kuvuruga uchaguzi. Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin ameahidi kuwa wahusika wote wa vurugu za kisiasa watachunguzwa na kufikishwa mahakamani bila kujali misimamo yao ya kisiasa. Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) nayo imeonya kuhusu ongezeko la matamshi ya uchochezi na ubaguzi wa kikabila, huku Mwenyekiti Kepha Nyamweya Omae akiwataka viongozi kutumia lugha ya kuunganisha badala ya kugawanya wananchi.

read more