T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 02:55:21

Afisa asema mazishi yaliyofanywa katika eneo la Kwa Bi Nzaro yalikiuka tamaduni za Wagiriama

AFISA wa serikali ameieleza Mahakama ya Mombasa kuwa namna waathiriwa wa vifo vya Kwa Bi Nzaro walivyozikwa bila nguo, bila majeneza na katika makaburi ya kina kifupi ilikuwa kinyume na mila na desturi za jamii ya Wagiriama. Akitoa ushahidi mahakamani, Chifu wa eneo la Chakama, Bw Raymond Charo, alisema mazishi aliyoshuhudia wakati miili ya waathiriwa walikuwa wakifukuliwa yalifanana kwa kiasi kikubwa na yale yaliyobainika katika uchunguzi wa mkasa wa Shakahola. Bw Charo aliiambia mahakama kuwa miili kadhaa ilipatikana ikiwa imezikwa kwenye makaburi ya kina kifupi bila nguo wala majeneza, jambo ambalo alisema halikubaliki kabisa kwa mujibu wa mila za Wagiriama. "Napenda pia kueleza kuwa kwa mujibu wa utamaduni wa Wagiriama, mazishi hufanyika mchana yakifuatana na maombi kulingana na jinsia ya marehemu, na mwili huwekwa ndani ya jeneza. Aidha, kaburi halipaswi kuwa na kina kisichopungua futi sita," alisema Bw Charo. Alieleza kuwa wakazi wa eneo la Kwa Bi Nzaro wengi wao ni Wagiriama, lakini namna waathiriwa hao walivyozikwa haikufuata utaratibu wowote unaotambulika katika mila na desturi za jamii hiyo. Bw Charo alifafanua kuwa yeye si mpelelezi wala mtaalamu wa uchunguzi wa maiti na kwamba ushahidi wake ulitokana na yale aliyojionea wakati wa shughuli ya ufukuzi wa miili. Pia, aliiambia mahakama kuwa anafahamu polisi walipata mabaki mengine ya miili ya binadamu pamoja na viungo vya miili katika eneo hilo kabla ya kuanza shughuli kubwa ya ufukuzi wa miili, ingawa hakuweza kuthibitisha idadi kamili ya mabaki yaliyopatikana. Bw Charo alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambayo mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia kuhusiana na vifo vya waumini katika eneo la Kwa Bi Nzaro, waliokuwa washirika wa kanisa lake lililopigwa marufuku la Good News International. Mackenzie ameshtakiwa pamoja na Shallyne Temba Anindo, Kahindi Kazungu Garama, Tom Mkonwe, Julius Luwali na Johnson Richard. Upande wa mashtaka unadai kuwa kwa pamoja waliwaua watu 29 kwa kutekeleza makubaliano ya kujiua yaliyolenga kusababisha vifo vyao na vya watu wengine ambao hawako mahakamani. Shtaka la kwanza linahusu kifo cha Samuel Owino Owuoyo, mwanaume, huku mashtaka mengine yakihusu waathiriwa wengine 28 ambao wengi wao hawakufahamika majina yao, jinsia wala umri wao, na walitambuliwa kupitia ushahidi wa kitaalamu na vielelezo vilivyokusanywa eneo la tukio. Wanadaiwa kutekeleza makosa hayo katika eneo la Kwa Bi Nzaro, Chakama, Kaunti Ndogo ya Magarini, Kaunti ya Kilifi, mwaka 2025. Konstebo wa Polisi Isaiah Barasa kutoka Kituo cha Polisi cha Langobaya pia alitoa ushahidi akisema maafisa wa polisi walifika katika boma la Bi Anindo baada ya kupokea taarifa kwamba baadhi ya wafuasi waliokuwa wakiishi hapo walikuwa wameathiriwa na mafundisho yenye misimamo mikali yaliyowashawishi kujinyima chakula hadi kufa. Shahidi mwingine wa upande wa mashtaka, Allan Luwali, aliiambia mahakama kuwa Mei 18, 2024 alimuuzia Bw Garama pikipiki kwa Sh18,000 katika karakana yake. Alisema baadaye alitoa taarifa kwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai baada ya kupigiwa simu na mmoja wa maafisa hao aliyekuwa akihitaji taarifa kuhusiana na vifo vya watu wengi katika eneo la Kwa Bi Nzaro. Mahakama imeambiwa kuwa piki piki hii ndio iliotumika kusafirisha wafuasi was kanisa hilo kutoka mji wa Malindi hadi msitu wa Kwa Bi Nzaro. Mke wa Bw Garama, Salama Masha aliambia Mahakama katika ushahidi wake kuwa yeye ndio alimchukulia mumewe pesa ya kununua piki piki hiyo kutoka kwa chama chao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 01:55:09

Hatima ya mikopo ya Sh7 trilioni ya UhuRuto kubainika

MWANASHERIA mkuu na Waziri wa Fedha, John Mbadi wameitaka Mahakama Kuu kusimamisha kusikizwa kwa kesi muhimu inayohusu uhalali wa deni la umma la Sh7 trilioni inayosubiri rufaa. Wanahoji kuwa korti iliruhusu kwa njia isiyofaa kesi hiyo kusonga mbele licha ya uchunguzi maalum unaoendelea, wakisema kesi hiyo ipo chini ya jukumu la mkaguzi mkuu wa fedha za serikali kikatiba kabla ya korti kuingilia kati. Ombi hilo limetokana na uamuzi uliotolewa Juni 25, 2026 na majaji Justices Francis Gikonyo, Roselyne Aburili na Moses Ado, waliotupilia mbali hoja ya mwanasheria mkuu kwamba kesi hiyo, ambayo vilevile inaitisha ufichuzi wa deni la umma, ilikaidi kanuni za kukamilisha njia zote, ukomavu na kutenganisha mamlaka. Mwanasheria mkuu Dorcas Oduor na Bw Mbadi wanaazimia kusimamisha kikao cha kusikiza kesi hiyo kilichopangiwa kufanyika Oktoba, wakionya kwamba michakato ya kesi itahujumu rufaa inayodhamiriwa na kuvuruga mchakato wa uangalizi kikatiba. Mwanasheria Mkuu hajaridhishwa na uamuzi wa mahakama uliopuuzilia mbali jaribio lake la kusimamisha kesi ili kuruhusu uchunguzi maalum unaofanywa na mkaguzi mkuu, hivyo kusababisha rufaa hiyo inayopangiwa kuwasilishwa. "Baada ya kukosa kuridhishwa na uamuzi mwanasheria mkuu aliwasilisha notisi ya kukata rufaa Juni 30, 2026 akieleza nia ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wote. Iwapo kesi kuhusu suala hili haitasimamishwa, rufaa inayokusudiwa itaishia kuwa kazi bure," anahoji wakili wa serikali Samwel Kaumba, akimwakilisha mwanasheria mkuu katika nakala za korti. Kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah na walalamishi wengine wanane, inapinga ufaafu kikatiba wa takriban Sh6.95 trilioni za ukopaji wa umma zilizolundikana kati ya miaka ya fedha 2014/15 na 2023/24 ikiwemo mikopo ya Eurobond. Aidha, inaitisha kutangazwa kwa uhalali kuhusu mchakato wa ukopaji, uwajibikaji wa maafisa wa umma na uhalali kikatiba wa visehemu vya Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma. Walalamishi vilevile wanataka uamuzi kuhusu iwapo maafisa wa umma wa zamani na wa sasa, ikiwemo wanaoshikilia afisi za Hazina Kuu, Mdhibiti Bajeti na Mkaguzi Mkuu wanapaswa kuwajibika binafsi chini ya Kifungu 226(5) cha Katiba kuhusu madai ya kuelekeza, kuidhinisha au kuruhusu vitendo vinavyodaiwa kuwa haramu vya ukopaji, utowaji fedha, matumizi ya malipo ya fedha za umma kinyume cha sheria. Katika kesi mpya iliyowasilishwa, mwanasheria mkuu anasema korti inapaswa kusimamisha kesi zote hadi Korti ya Rufaa itakapotoa uamuzi kuhusu rufaa inayonuiwa kuwasilishwa.

read more