T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 13 Jul 2026 00:55:19

Oburu: Huku Luo Nyanza wimbo ni tutam

VIONGOZI wa ODM Luo Nyanza wameapa kuwa 'watakufa' na Rais William Ruto hadi 2027 kutokana na uimarishaji wa miundomsingi eneo hilo. Wakiongozwa na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, walisema ODM haina nia ya kuwa na mgombeaji wa urais 2027 na ni Rais Ruto ndiye atapigiwa kura mwakani. Kulingana naye, wagombeaji wengine kama Rigathi Gachagua, Martha Karua, Justin Muturi na wengine hawana nafasi ya kushinda urais. "Wanapambana na kujipiga kifua na hata hawajaamua nani ni mgombeaji wao wa urais. Sisi tunajua nani atakuwa mgombeaji wetu na tutawashinda," akasema. Dkt Oginga alisema Luo Nyanza ilitengwa na tawala za nyuma kutokana na msimamo wake wa kisiasa lakini ushirikiano kati ya UDA-ODM umebadilisha eneo hilo kimaendeleo. "Hatubaguliwi tena, tuko serikalini na tunajua mahali tunaelekea. Tuliingia kupitia dirishani lakini sasa tunajua mahali tunaenda," akasema Dkt Oginga. Aliwataka wakazi wa Nyanza kuwachagua viongozi wa ODM pekee ili chama hicho kiendelee kuwa na umaarufu mkubwa wa kisiasa. "Nikiketi na Rais Ruto baada ya uchaguzi wa mwaka ujao, atauliza nina watu wangapi. Kwa hivyo, wapigie wawaniaji wa ODM viti vingine lakini urais tunampa Ruto," akasema. Alikuwa akiongea katika ibada ya kanisa Kaunti ya Homa Bay. Aliandamana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo, Katibu wa Afya Ouma Oluga, Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang na Mbunge wa Homa Bay mjini Opondo Kaluma. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alisema eneo la Ziwa limepata maendeleo makubwa kupitia miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea imebadilisha kwa kiasi kikubwa sura ya eneo hilo. "Tunaposema tunaiunga mkono serikali, si bure. Ni kwa sababu ya umoja wa Wakenya.. Hilo ndilo jambo ambalo serikali jumuishi imefanikiwa kulitekeleza," alisema Bi Wanga. Pia alitetea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) dhidi ya mashambulizi ya kisiasa wakati tume hiyo ikijiandaa kuendesha uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Kwa upande wake, Seneta Moses Kajwang' alisema kuwa kwa muda mrefu wapigakura wa eneo la Ziwa waliamini kuwa maendeleo yangewezekana tu iwapo mmoja wao angekuwa kiongozi wa taifa. Hata hivyo, alisema Kenya haihitaji kiongozi wa kieneo bali mwenye mtazamo wa kitaifa. "Tutaendelea kuiunga mkono serikali. Ukweli kwamba tunataka kushika mamlaka haumaanishi hatutashirikiana na serikali," akasema seneta huyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 23:55:10

2027: Siasa za ubabe zatikisa mrengo wa Linda Mwananchi na ule wa upinzani

HUKU upinzani ukiendelea kuonyesha wana umoja hadharani, mvutano mkali unaendelea kushuhudiwa kati ya mrengo wa Linda Mwananchi na Umoja wa Upinzani, kila upande ukipambana kudhibiti kampeni za kumng'oa madarakani Rais William Ruto. Migawanyiko hiyo ilijitokeza wazi Ijumaa baada ya aliyekuwa Naibu Rais ,Rigathi Gachagua, kumshambulia Gavana wa Murang'a, Irungu Kang'ata, kuhusu uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. "Nimesikia Kang'ata akisema anataka kuja Ol Kalou akiwa na Linda Mwananchi. Hatukuhitaji hapa. Kama unataka kupigia debe UDA, Jubilee au chama kingine chochote, uko huru kufanya hivyo, lakini kampeni za DCP ni suala la wenyeji," akasema Bw Gachagua. Kauli hiyo iliwafanya viongozi wa Linda Mwananchi kuhamisha mikutano yao Nyahururu na kusitisha mipango ya kumpigia kampeni mgombea wa DCP. Bw Kang'ata alijiunga na Linda Mwananchi mwezi uliopita wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika Thika. Matamshi ya Bw Gachagua dhidi ya Bw Kang'ata yamefichua mapambano makubwa zaidi ya kupigania ushawishi ndani ya upinzani. Duru kutoka upinzani zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wana hofu kwamba ajenda yao ya kisiasa inaweza kudhoofishwa na kundi la Linda Mwananchi ilhali wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali tangu 2022. Magharibi mwa Kenya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemkosoa Bw Sifuna akisema hana ushawishi wowote wa kisiasa. "Nataka kusema Sifuna hana kura Kakamega na Bungoma Didmus Barasa amemshinda kwa umaarufu. Eugene Wamalwa ndiye mwanasiasa maarufu zaidi ambaye ataleta kura kwa upinzani bila kujali atashikilia wadhifa gani," akasema Bw Salasya. "Wamejaa kiburi na wanataka kuleta mkanganyiko. Wania urais tuone utakakofika na jinsi itakavyomalizika," akaongeza Bw Salasya. Si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kupuuza ushawishi wa kisiasa wa Bw Sifuna na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya katika eneo hilo. Mrengo wa Sifuna na Natembeya umeitikisa kambi ya DAP-Kenya. Wawili hao sasa wanapanga mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma Julai 25 na 26. Bw Natembeya tayari ametangaza kuwa atatetea kiti chake kupitia chama kipya cha kisiasa badala ya DAP-Kenya kinachoongozwa na Bw Wamalwa. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Natembeya na Bw Wamalwa walitofautiana kuhusu uongozi wa DAP-Kenya, hali iliyomfanya gavana huyo kuanzisha vuguvu la Tawe. Wakati wa ziara ya upinzani Magharibi mwa Kenya mwezi uliopita, Bw Gachagua alimtangaza Bw Natembeya kuwa mratibu wa kampeni zake Magharibi. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, naye amewashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kujaribu kuelekeza shughuli za Linda Mwananchi huku wakimtumia Bw Sifuna kuendeleza maslahi yao binafsi. Alimtaja Bw Kang'ata kuwa mmoja wa viongozi wanaochochea migawanyiko ndani ya upinzani. "Linda Mwananchi haitatekwa nyara nikiwa macho. Hatutakuruhusu wewe (Kang'ata) kumtumia vibaya mwana wetu Edwin Sifuna," akasema Bw Amisi, ambaye amekuwa akiongoza kampeni za chama chake cha People Renaissance Movement (PRM) katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Seneta wa Kisii, Richard Onyonka ,anaamini kuwa hatimaye makundi hayo mawili yataungana chini ya muungano mmoja, akisema migawanyiko ya sasa inadhoofisha upinzani. Bw Onyoka amesisitiza kuwa pande zote mbili zinapaswa kuweka kando kiburi na kushirikiana. "Lazima tushirikiane kwa sababu ajenda ya Upinzani na Linda Mwananchi ni kuhakikisha utawala wa sasa unaondolewa madarakani mwaka ujao," akasema Bw Onyonka, ambaye yuko ndani ya Linda Mwananchi lakini anaunga mkono azma ya urais ya Dkt Matiang'i.

read more