taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 23:55:10
2027: Siasa za ubabe zatikisa mrengo wa Linda Mwananchi na ule wa upinzani
HUKU upinzani ukiendelea kuonyesha wana umoja hadharani, mvutano mkali unaendelea kushuhudiwa kati ya mrengo wa Linda Mwananchi na Umoja wa Upinzani, kila upande ukipambana kudhibiti kampeni za kumng'oa madarakani Rais William Ruto. Migawanyiko hiyo ilijitokeza wazi Ijumaa baada ya aliyekuwa Naibu Rais ,Rigathi Gachagua, kumshambulia Gavana wa Murang'a, Irungu Kang'ata, kuhusu uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. "Nimesikia Kang'ata akisema anataka kuja Ol Kalou akiwa na Linda Mwananchi. Hatukuhitaji hapa. Kama unataka kupigia debe UDA, Jubilee au chama kingine chochote, uko huru kufanya hivyo, lakini kampeni za DCP ni suala la wenyeji," akasema Bw Gachagua. Kauli hiyo iliwafanya viongozi wa Linda Mwananchi kuhamisha mikutano yao Nyahururu na kusitisha mipango ya kumpigia kampeni mgombea wa DCP. Bw Kang'ata alijiunga na Linda Mwananchi mwezi uliopita wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika Thika. Matamshi ya Bw Gachagua dhidi ya Bw Kang'ata yamefichua mapambano makubwa zaidi ya kupigania ushawishi ndani ya upinzani. Duru kutoka upinzani zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wana hofu kwamba ajenda yao ya kisiasa inaweza kudhoofishwa na kundi la Linda Mwananchi ilhali wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali tangu 2022. Magharibi mwa Kenya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemkosoa Bw Sifuna akisema hana ushawishi wowote wa kisiasa. "Nataka kusema Sifuna hana kura Kakamega na Bungoma Didmus Barasa amemshinda kwa umaarufu. Eugene Wamalwa ndiye mwanasiasa maarufu zaidi ambaye ataleta kura kwa upinzani bila kujali atashikilia wadhifa gani," akasema Bw Salasya. "Wamejaa kiburi na wanataka kuleta mkanganyiko. Wania urais tuone utakakofika na jinsi itakavyomalizika," akaongeza Bw Salasya. Si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kupuuza ushawishi wa kisiasa wa Bw Sifuna na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya katika eneo hilo. Mrengo wa Sifuna na Natembeya umeitikisa kambi ya DAP-Kenya. Wawili hao sasa wanapanga mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma Julai 25 na 26. Bw Natembeya tayari ametangaza kuwa atatetea kiti chake kupitia chama kipya cha kisiasa badala ya DAP-Kenya kinachoongozwa na Bw Wamalwa. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Natembeya na Bw Wamalwa walitofautiana kuhusu uongozi wa DAP-Kenya, hali iliyomfanya gavana huyo kuanzisha vuguvu la Tawe. Wakati wa ziara ya upinzani Magharibi mwa Kenya mwezi uliopita, Bw Gachagua alimtangaza Bw Natembeya kuwa mratibu wa kampeni zake Magharibi. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, naye amewashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kujaribu kuelekeza shughuli za Linda Mwananchi huku wakimtumia Bw Sifuna kuendeleza maslahi yao binafsi. Alimtaja Bw Kang'ata kuwa mmoja wa viongozi wanaochochea migawanyiko ndani ya upinzani. "Linda Mwananchi haitatekwa nyara nikiwa macho. Hatutakuruhusu wewe (Kang'ata) kumtumia vibaya mwana wetu Edwin Sifuna," akasema Bw Amisi, ambaye amekuwa akiongoza kampeni za chama chake cha People Renaissance Movement (PRM) katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Seneta wa Kisii, Richard Onyonka ,anaamini kuwa hatimaye makundi hayo mawili yataungana chini ya muungano mmoja, akisema migawanyiko ya sasa inadhoofisha upinzani. Bw Onyoka amesisitiza kuwa pande zote mbili zinapaswa kuweka kando kiburi na kushirikiana. "Lazima tushirikiane kwa sababu ajenda ya Upinzani na Linda Mwananchi ni kuhakikisha utawala wa sasa unaondolewa madarakani mwaka ujao," akasema Bw Onyonka, ambaye yuko ndani ya Linda Mwananchi lakini anaunga mkono azma ya urais ya Dkt Matiang'i.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Mvutano wazuka kuhusu usajili wa Linda Mwananchi
MVUTANO kuhusu usajili wa chama kipya cha kisiasa cha Linda Mwananchi Party umechukua mwelekeo mpya baada ya mawakili wa Charles Wanyonyi, aliyekuwa wa kwanza kujaribu kukisajili kushtumu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kwa kutaka kupitia upya uamuzi wa awali bila kumshirikisha muombaji wa kwanza. Hatua hiyo imejiri siku moja baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na viongozi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi kukutana kwa faragha na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou. Baada ya mkutano huo, viongozi hao walitangaza kuwa msajili alikubali kupitia upya uamuzi wa kukataa kuhifadhi jina la chama hicho. Hata hivyo, mawakili wa Bw Wanyonyi wanasema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba na haki ya kila mtu kusikilizwa iwapo mteja wao hatahusishwa katika mchakato huo. Katika barua iliyowasilishwa kwa msajili Agosti 5, mawakili wa kampuni ya Wanzau, Odhiambo and Associates walisema Bw Wanyonyi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuomba kuhifadhi jina la "Linda Mwananchi Party of Kenya" mnamo Februari 24, 2026. Kwa mujibu wa mawakili hao, maombi ya kuhifadhi majina ya vyama yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata utaratibu wa aliyewasilisha kwanza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Unganisheni Wakenya badala ya kujitokeza tu wakati wa uchaguzi, Wetang'ula ahimiza NCIC
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula, amehimiza Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kurejesha imani ya Wakenya na kuwa mstari wa mbele kuimarisha umoja wa taifa wakati wote, badala ya kujitokeza tu kipindi cha uchaguzi. Wetang'ula alisema tume hiyo ilianzishwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ili kuponya migawanyiko ya kisiasa, lakini imeendelea kukumbwa na changamoto ya kutokuaminiwa na wananchi. "NCIC ina tatizo kubwa la kuaminiwa. Haipaswi kuonekana kama taasisi inayofanya kazi wakati wa uchaguzi pekee," alisema alipokutana na viongozi wa tume hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake, Askofu Kepha Omae, katika majengo ya Bunge. Alisisitiza kuwa elimu endelevu kwa wananchi ndiyo njia bora ya kubadili mitazamo na kujenga mshikamano wa kudumu. "Hakuna tatizo mtu kuwa wa jamii fulani. Tatizo ni pale utambulisho huo unapotumiwa kuwabagua au kuwanyanyasa wengine," alisema. Wetang'ula pia aliitaka NCIC kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu ili kukuza utamaduni wa umoja miongoni mwa wanafunzi na vijana. Aidha, alihimiza tume hiyo kuimarisha ushirikiano na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili kuongeza ufanisi wake. "Mnayo mamlaka ya kuchunguza, lakini mashtaka yanaendeshwa na DPP. NCIC inapaswa kujijengea heshima kwa kufanya kazi kwa weledi. Bunge litaendelea kuunga mkono kwa mujibu wa sheria," alisema. Spika huyo aliongeza kuwa uchaguzi ni mchakato unaoendelea na si tukio la siku moja, hivyo NCIC ina jukumu muhimu la kukabiliana na matamshi ya chuki na viongozi wanaochochea migawanyiko. Kwa upande wake, Askofu Kepha Omae alisema tume tayari imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kupitia mpango unaolenga kuzuia migogoro, kuimarisha ushirikiano na kushirikisha wadau mbalimbali. "Tumeandaa ramani ya utekelezaji. Tunataka kushirikiana na taasisi nyingine na viongozi wa kisiasa ili kupunguza ubaguzi na ukabila," alisema. Aliongeza kuwa NCIC itafanya kazi kwa karibu na wazee wa jamii, viongozi wa dini, shule na taasisi nyingine za elimu ili kuhamasisha siasa za amani na kuwataka viongozi kupunguza matamshi ya uchochezi. Kamishna wa NCIC Jerusha Mwaathime alitaka Bunge kupatia tume mamlaka makubwa zaidi ya uchunguzi ili iweze kushughulikia kwa ufanisi visa vinavyochochea chuki na migawanyiko nchini.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 7 hours ago
Biya afanya mabadiliko ya kijeshi bila kuonekana
DOUALA, Cameroon: RAIS wa Cameroon Paul Biya Jumanne alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu kutokuwepo kwake hadharani kwa muda wa miezi miwili. Kupitia amri tatu za rais zilizotiwa saini Jumatatu na kutangazwa kupitia redio ya taifa, Biya alipandisha cheo mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Rais kutoka kanali hadi brigedia jenerali. Pia aliwateua makamanda wapya katika maeneo manne kati ya matano ya kijeshi nchini humo na kufanya mabadiliko mengine katika uongozi wa vikosi vya jeshi. Mabadiliko hayo pia yalihusisha kuteuliwa kwa kamanda mpya wa Rapid Intervention Brigade (BIR), kikosi maalum kinachohusika na operesheni za kukabiliana na ugaidi na makundi yenye silaha. Aidha, Meja Jenerali Ebaka Hippolyte alipandishwa kuwa afisa mwandamizi katika Makao Makuu ya Jeshi, huku makanali kadhaa wakipandishwa cheo kuwa mabrigedia jenerali. Hatua hiyo imejiri wakati Biya hajaonekana hadharani tangu Juni 7, alipoondoka Cameroon kuelekea Ulaya kwa kile serikali ilichokitaja kuwa "ziara fupi ya kibinafsi". Hata hivyo, hajarejea nchini, jambo lililozua wasiwasi na uvumi kuhusu afya yake na uwezo wake wa kuendelea kuongoza taifa hilo. Msemaji wa serikali, Rene Emmanuel Sadi, alisema Biya yuko hai na anatarajiwa kurejea nchini humo hivi karibuni, lakini hakutoa tarehe rasmi ya kurejea kwake. Kutokuwepo kwa Biya kulisababisha chama tawala cha Cameroon People's Democratic Movement (CPDM) kuitisha kikao kisicho cha kawaida mwezi uliopita ili kujadili hali ya kisiasa nchini humo. Kikao hicho kilifanyika huku shinikizo likiongezeka kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na sehemu ya umma wanaotaka ufafanuzi kuhusu uongozi wa nchi. Biya, 93, ndiye kiongozi mzee zaidi duniani anayehudumu madarakani. Ameiongoza Cameroon tangu 1982 baada ya kumrithi Ahmadou Ahidjo. Katika kipindi hicho, alishinda chaguzi kadhaa ambazo mara nyingi zilikosolewa na wapinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa kwa madai ya kukosa uwazi na usawa. Kwa miaka mingi, Cameroon imekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo uasi wa waasi wa Boko Haram kaskazini, mzozo wa kujitenga katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi, pamoja na malalamishi ya ukosefu wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Biya amekuwa akitumia muda mrefu nje ya ya nchi, hasa Uswisi, kwa mapumziko au ziara binafsi. Hata hivyo, safari yake ya sasa ndiyo ndefu zaidi kuwahi kushuhudiwa, hali ambayo imeongeza mijadala kuhusu mrithi wake na mustakabali wa uongozi wa Cameroon kuelekea uchaguzi ujao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Hivi ni sahihi kutumia neno 'nyanja' kwa maana ya umoja na wingi?
JUMA hili nimesisimshwa na Makala yaliyoandikwa na mweledi mashuhuri wa lugha ya Kiswahili Ustadh Abdilatif Abdalla. Japo yeye daima hunyenyekea kwamba si msomi wa Kiswahili, mimi humuona kama mmoja kati ya wabobezi wachache wa Kiswahili, Uswahili na fasihi yake. Daima mimi huchukizwa na matumizi ya *nyimbo hii (na ninafikiri niliona Prof. F. E. M. K. Senkoro pia akitaja hilo) na kwa sababu hiyo maelezo ya Ustadh yalinichangamsha mno! Kwa kuwa Ustadh aliyaandika maelezo yake katika kumbi za umma kwa kusudi la kuelimisha, naomba niyanukuu neno kwa neno. "… neno nyanja ni wingi wa uwanja. Kwa hivyo, kwa maoni yangu mimi mzungumzaji wa Kiswahili wa kawaida tu (ambaye si mtaalamu wala si msomi), si sawa, wala si Kiswahili fasaha, wala si Kiswahili Sanifu, kulitumia neno nyanja kama kwamba umoja wake na wingi wake ni huo huo.Kuna na maneno mengine (ambayo nitayaorodhesha hapa chini) yaliyotiwa katika mkumbo huo wa matumizi ya makosa, kama hilo nyanja, kiasi cha kwamba wale wasioujua usuli wa maneno hayo haiwapitikii kamwe kuwa wafanyayo ni makosa! Na baadhi yayo yamekuwa yakitumiwa kwa makosa kwa muda mrefu (hata na wale wanaoshughulika na kukisanifu Kiswahili!) mpaka leo imekuwa ukimtanabahisha mtu kuwa hayo ni makosa, wewe mtanabahishaji ndiye utakayeonekana kuwa unakosea. Nimewahi kuambiwa na baadhi ya wataalamu wetu wa Sarufi na Isimu kwamba makosa yafanyikayo katika/kwenye lugha, na yakazowewa na baadhi ya watu na yakaendelea kufanywa kwa muda mrefu, makosa hayo huweza kukubaliwa kuwa sahihi. Kama nilivyotangulia kueleza, mimi si mtaalamu wala si msomi wa lolote. Kwa hivyo, napata tabu kuikubali hoja (huja) hii. Mtaniwia radhi wataalamu na wasomi. Huenda nisingekuwa na shida hiyo kama nami ningekuwa nimejaaliwa kuwamo katika/kwenye matengo hayo. Na linipalo tabu zaidi ni kuona jinsi baadhi yetu tulivyojipa leseni ya kuyafanya makosa kama haya kwa wepesi mno na (pengine) bila kujali, na kwa sababu hiyo niliyoieleza. Lakini huwa twalifanya hilo humu Kiswahilini tu. Hatuthubutu kulifanya hilo kwenye lugha za kigeni tujifunzazo. Huko huwa tuna hadhari sana, na hufanya juhudi kubwa, tusionekane tumefanya makosa. Na mtu huwa haachiliwi kuendelea kuyafanya makosa, hata kama makosa hayo yamekuwa yakitumiwa na baadhi ya watu kwa muda mrefu. Kwa nini, basi, makosa kama hayo yawe yanakubalika katika/kwenye hiki tukiitacho Kiswahili Sanifu? Naelewa, na ninakubali, kwamba nje ya Kiswahili fasaha na sanifu watu watakitumia Kiswahili vile watakavyo wao wenyewe, maadamu watakuwa wanaelewana wenyewe kwa wenyewe. Lakini tushughulikapo na Kiswahili fasaha na sanifu, yatubidi tuweke mipaka. Tusikifanye Kiswahili kama kwamba ni ng'ombe asiyekuwa na mchunga. Haya yafuatayo ni baadhi tu ya maneno ambayo wengine wetu tumekuwa tukitumia wingi wake kuwa ni umoja. Maneno yaliyoko kushoto yamo katika hali ya umoja, na yaliyo kulia ni wingi wayo:Wenzo (huu) - nyenzo (hizi) Usimulizi (huu) - simulizi (hizi) Utanzu (huu) - tanzu (hizi) Utungo (huu) - tungo (hizi) Ubeti (huu) - beti (hizi) Uga (huu) - nyuga (hizi) Uchango (huu) - chango (hizi) Waraka (huu) - nyaraka (hizi) Utumbuizo (huu) - tumbuizo (hizi) Wimbo (huu) - nyimbo (hizi)Juma lijalo nitaendeleza makala haya kwa kutoa hoja zilizotolewa na Prof Kineene wa Mutiso wakati akitoa jibu kuhusu makala haya.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Mali ya Champions: Bruno Guimaraes aacha unahodha Newcastle kuja kuwa kiungo wa Arsenal
MABINGWA wa Ligi Kuu Uingereza (EPL) Arsenal, wamekubaliana na Newcastle United kuhusu uhamisho wa nahodha wao Bruno Guimaraes kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza zilizochapishwa Jumatano. Kwa mujibu wa Sky Sports, ofa ya kwanza ya Arsenal kwa kiungo huyo wa Brazil ilikataliwa mapema wiki hii. Hata hivyo, klabu hiyo ya London ilirejea na ofa iliyoboreshwa na kufikia makubaliano na Newcastle. Guimaraes sasa ameuzwa kwa Arsenal kwa ada ya pauni milioni 75 (Sh13.2 bilioni). Ripoti zinasema Guimaraes, 28, alikuwa ameiambia Newcastle kwamba angependa kujiunga na Arsenal iwapo ofa inayofaa ingewasilishwa. Newcastle ilikuwa ikitaka kusalia na nahodha huyo, ambaye bado ana miaka miwili katika mkataba wake, pamoja na mwanya wa kuongeza mwaka mmoja zaidi. Guimaraes alijiunga na Newcastle akitokea Olympique Lyon ya Ufaransa mnamo Januari 2022 na tangu wakati huo amekuwa nguzo muhimu ya klabu hiyo. Amecheza mechi 195 katika mashindano yote, akifunga mabao 31, na aliiongoza Newcastle kutwaa League Cup (Carabao 2025) taji lao la kwanza baada ya kipindi kirefu. Iwapo uhamisho huo utakamilika, Guimaraes ataongeza ubora na uzoefu katika safu ya kati ya kocha Mikel Arteta huku Arsenal ikisaka kutetea ubingwa wa EPL na pia kutamba katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Guimaraes pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil katika Kombe la Dunia 2026. Kuondoka kwake kutakuwa pigo jingine kwa Newcastle, ambayo tayari imewapoteza Anthony Gordon, Sandro Tonali na kocha Eddie Howe. Wakati huo huo, Kocha Mfaransa Herve Renard naye amerejea kuinoa Ivory Coast, miaka 11 baada ya kuiongoza kutwaa Kombe la Afrika 2015. Shirikisho la Soka la Ivory Coast lilitangaza Jumanne kuwa Renard, 57, atamrithi Emerse Fae, ambaye mkataba wake haukuongezwa baada ya Kombe la Dunia 2026. Fae alifikisha Ivory Coast hatua ya mchujo kwa mara ya kwanza katika kombe la dunia ambao walishiriki kwa mara ya nne. Renard aliinoa Tunisia kwa muda katika Kombe la Dunia baada ya kuanza vibaya kwa kipigo cha 5-1 dhidi ya Uswidi. Alishindwa kubadili mambo huku wakipoteza pia dhidi ya Japan na Uholanzi. Kocha huyo pia amewahi kuzinoa Angola, Morocco, Saudi Arabia na Zambia, aliyoiongoza kutwaa taji la AFCON 2012. Sasa atalenga kutwaa ubingwa wake wa tatu wa AFCON mwaka ujao katika mashindano yatakayoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Utafiti: Waamerika hawaamini Rais Trump ataimarisha uchumi
WASHINGTON, Amerika: UTAFITI mpya wa Reuters/Ipsos unaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza katika karibu mwongo mmoja, raia wengi wa Amerika wanaamini Democrat ina uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia uchumi kuliko Republican. Utafiti huo pia umebaini kuwa utendakazi wa Rais Donald Trump umeshuka hadi asilimia 35 na raia wengi wanaelekea kukosa imani naye kutokana na uchumi mgumu. Asilimia 37 ya wapigakura waliosajiliwa walisema Democrats wana sera bora za uchumi ikilinganishwa na asilimia 36 waliounga mkono Republicans, huku asilimia 27 wakisema hawakuwa na msimamo kuhusu Trump na utawala wake. Matokeo hayo yanakuja huku raia wa Amerika wakikabiliwa na kupanda kwa gharama ya maisha, wengi wakilalamikia pia mapato kidogo. La mno zaidi kwa raia wa Amerika ni kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na vita kati ya Iran na Israel vinavyoungwa mkono na Amerika. Tangu vita hivyo vianze, bei ya petroli imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 25, jambo limeathiri pakubwa bajeti za familia nyingi na sekta za utengenezaji bidhaa. Kwa mujibu wa kura hiyo, asilimia 42 ya wapigakura wangewaunga wagombea wa Democratic iwapo uchaguzi wa Bunge ungefanyika sasa. Kwa upande mwingine asilimia 37 walisema wangewapigia kura Republicans. Wapigakura huru pia walionyesha kuwapendelea Democrats kwa tofauti ya asilimia 12 kuliko Republicans. Mwelekeo huo unaonyesha kuwa chama cha Republican kinachotarajia kutetea wingi wa wakilishi wake katika Bunge la Congress kwenye uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika Novemba, kina kibarua kudumisha umaarufu wake. Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wameonya kuwa matokeo ya kura za maoni za kitaifa hayawezi kutabiri moja kwa moja matokeo ya uchaguzi kwa sababu ushindani mkali unatarajiwa katika idadi ndogo ya maeneo ya uchaguzi na si taifa lote. Rais Trump naye amepuuzilia mbali matokeo ya tafiti hizo, akidai kupitia mtandao wake wa Truth Social umaarufu wake upo juu zaidi kuwahi kushuhudiwa, na kwamba tafiti zinazochapishwa na vyombo vya habari hazionyeshi hali halisi. Amedai kuwa raia wengi wanachangamkia utawala wake na wana matarajio mengi kuwa serikali yake itaipaza Amerika kimaendeleo. Uungwaji mkono wa Republican kuhusu usimamizi wa uchumi umeendelea kupungua katika muhula wa sasa wa Rais Donald Trump, hasa baada ya bei ya mafuta kupanda kufuatia mashambulizi ya Amerika na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari na vita vinavyoendelea.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Buda azusha kupewa ngombe waliokonda kama mahari ya bintiye na kuagiza warudishwe
KULISHUHUDIWA kioja cha mwaka kijijini hapa baba wa msichana alipodinda kupokea ng'ombe wawili kama mahari, akidai ni dharau kwa bintiye. Badala yake baba huyo aliamuru ng'ombe hao warudishwe walikotolewa mara moja. Waliofika kikao hicho cha mahari walijaribu kumbembeleza akubali mifugo hao kama sehemu ya mahari, bila mafanikio kwani baba alikaa ngumu. "Yaani wewe unanichukuliaje? Mimi nimemtunza binti yangu vyema kiasi kwamba kijana wako amependezwa naye na yuko tayari kumuoa, halafu waniletea ng'ombe mifupa mitupu? alifoka buda huyo. "Utarudi nao. Sitachukua kamwe ng'ombe waliokonda!" akasisitiza. Ilibidi kikao hicho cha mahari kisitishwe watu wakafumkana huku aliyeleta ng'ombe akilazimika kurudi nao.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 14 hours ago
Mali ya kifahari ya Wa Iria kupigwa mnada kwa kushindwa kulipa mkopo
MALI inayohusishwa na aliyekuwa Gavana wa Murang'a, Mwangi wa Iria, inatarajiwa kuuzwa kwa mnada baadaye mwezi huu baada ya kudaiwa kushindwa kulipa mkopo ambao kiasi chake hakijafichuliwa, hali inayoongeza matatizo yake ya kisheria huku pia akikabiliwa na kesi ya ufisadi ya zaidi ya Sh542.6 milioni. Tangazo la kampuni ya Dalali Traders Auctioneers linaonyesha kuwa nyumba yake ya kifahari iliyoko Karen, Nairobi, pamoja na Edinburgh Mountain Hospital iliyoko Murang'a, zitauzwa kwa mnada mnamo Agosti 25. Hatua hiyo imejiri chini ya miaka miwili tangu Rais William Ruto amteue Bw Wa Iria kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA). Tangazo hilo linaonyesha kuwa hospitali hiyo iko kwenye shamba la ekari 2.96 katika eneo la Milimani, Kiharu, Murang'a, karibu na Chuo Kikuu cha Murang'a na Chuo cha Matibabu cha Edinburgh. Hospitali hiyo inamilikiwa kikamilifu na Bw Wa Iria kupitia kampuni ya Edinburgh Mountain Hospital Limited. Mali hiyo imestawishwa kwa jengo la hospitali la ghorofa tano pamoja na maeneo ya kupumzikia. Nyumba inayotarajiwa kuuzwa iko katika eneo la Karen, kwenye ploti ya ekari 0.48 katika Muiri Lane. Mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la Bw Wa Iria na ilitumika kama dhamana ya mkopo uliochukuliwa na Edinburgh College Ltd pamoja na Edinburgh Mountain Hospital Ltd. Nyumba hiyo ya ghorofa tatu ilikuwa karibu kukamilika na pia ina nyumba ya wageni, maegesho ya magari, pamoja na mipango ya kujenga bwawa la kuogelea, gazebo na nyumba za wafanyakazi. Bw Wa Iria na kampuni ya madalali hawakufichua jina la mkopeshaji wala kiwango cha mkopo unaodaiwa. Mbali na madai ya mkopo, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pia imewasilisha kesi ikitaka kurejesha Sh542.6 milioni, ikidai fedha hizo zilipatikana kupitia ufisadi na ukiukaji wa taratibu za ununuzi alipokuwa gavana wa Murang'a. Hata hivyo, Bw Wa Iria amekanusha madai hayo na kesi bado iko mahakamani. Bw Wa Iria ni miongoni mwa viongozi wa zamani ambao mali yao iko hatarini kupigwa minada au kurejeshwa kwa serikali. Wengine ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, ambaye pia amepoteza baadhi ya mali zake kutokana na migogoro ya mikopo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 14 hours ago
Wakazi Turkana wahofia vikosi vinalinda maeneo ya mafuta badala ya usalama wao
WAKAZI wa vijiji vya Lopii, Nakukulas, Lokwamosing, Lokori na Kahuruko katika Bonde la South Lokichar, Kaunti ya Turkana, wanasema sasa wanaishi kwa hofu ya vikosi vya usalama licha ya miaka mingi wakikabiliwa na mashambulizi ya majangili. Wakazi hao wanadai oparesheni kali iliyoanzishwa mwezi uliopita na kikosi maalumu cha polisi imegeuza eneo hilo kuwa kama kambi ya kijeshi. Wanasema magari ya kivita yanazunguka vijijini huku wakazi wakizuiwa kutembea kwa uhuru, jambo linalozua hofu kuwa serikali inalenga kulinda maeneo ya mafuta badala ya wananchi. Serikali, hata hivyo, inasema oparesheni hiyo inalenga kukomesha wizi wa mifugo na mashambulizi ya majangili. Mfugaji Meshack Etiir wa kijiji cha Lopii alisema wakazi wamekuwa wakitegemea mtandao wa kutoa taarifa za kiusalama ili kubaini watu wanaoshukiwa kushirikiana na majangili. Alisema taarifa hizo zilisaidia kupanga mikakati na Polisi wa Akiba pamoja na maafisa wa utawala ili kukabiliana na mashambulizi. Kwa mujibu wake, familia nyingi zimeendelea kuwa maskini baada ya kupokonywa mifugo huku juhudi za serikali za kurejesha wanyama hao zikikosa kuzaa matunda. Mwakilishi wa Wadi ya Lokichar, Samwel Lomodo, alisema viongozi wamekuwa wakiripoti mashambulizi ya mara kwa mara katika vijiji vya Lopii, Lokwamosing na Nakukulas bila serikali kuchukua hatua za haraka. Alidai kuwa majangili bado wanaendelea kujificha katika maeneo ya Kailongol, Lokwatuba, Lochakula, Lotongot na Loritit licha ya oparesheni ya kuwasaka. Bw Lomodo alisema badala ya vikosi vya usalama kuwafuatilia majangili na kurejesha mifugo iliyoibwa, vinaelekeza nguvu kwa wakazi wasio na hatia. Naye mkazi wa Nakukulas, Mark Epurui, alisema wakazi hawawezi tena kupeleka mifugo karibu na maeneo ya mafuta wala kutafuta taarifa kuhusu nafasi za kazi zinazotarajiwa wakati uchimbaji wa mafuta utakapoanza tena. Kwa upande wake, Eunice Ateyo wa shirika la Friends of Lake Turkana alisema wanaharakati wa haki za binadamu wamebaini hofu kubwa miongoni mwa wakazi kutokana na uwepo wa magari ya kivita. Alidai baadhi ya wakazi wamefurushwa na nyumba kadhaa kuchomwa moto wakati wa oparesheni hiyo. Mwakilishi wa Wadi ya Lokori/Kochodin Willy Napuyo, alisema ikiwa serikali inapanga kutwaa ardhi kwa ajili ya miradi ya mafuta, wakazi wanapaswa kufahamishwa mapema kuhusu fidia na makazi mapya. Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Turkana, Julius Kavita, alitetea oparesheni hiyo akisema ilianzishwa baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi. Alisema serikali itaendelea na juhudi za kurejesha mifugo iliyoibwa na kuwakamata wahusika wa mashambulizi hayo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 15 hours ago
Oburu 'Youth Leader' naye ataka nafasi ya Naibu Rais
IDADI ya wanaomezea mate wadhifa wa Naibu Rais katika muungano wa kisiasa unaounga mkono Rais William Ruto imeendelea kuongezeka, viongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) pia wakitaka nafasi hiyo. Wiki mbili tu baada ya baadhi ya viongozi kumpendekeza Waziri wa Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati, Wycliffe Oparanya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, sasa kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, ametangaza hadharani kuwa anataka wadhifa huo. Akizungumza Jumanne katika Ikulu ya Nairobi wakati Rais Ruto alipokutana na wazee wa vijiji kutoka sehemu mbalimbali nchini, Dkt Oburu alisema ODM haitatoa mgombea urais mwaka 2027 bali itamuunga mkono Rais Ruto. "Wakati huu ODM haitakuwa na mgombeaji wa urais. Mgombea wetu ni Rais William Ruto. Lakini nafasi nyingine zote zinaweza kujadiliwa, hasa ya Naibu Rais. Hamuoni kwamba mimi ninafaa kuwa nambari mbili? Mimi pia nina sifa zinazohitajika," alisema Dkt Oburu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 82, alisema ODM itaunga mkono azma ya Rais Ruto kutetea urais kwa muhula wa pili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa chama hicho, kikiwa miongoni mwa vyama vikuu katika muungano unaotawala, kitajadiliana ili kipate unaibu rais. Dkt Oburu pia alimpongeza Rais Ruto kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini na kwa uamuzi wa serikali kutoa malipo ya kila mwezi kwa wazee wa vijiji. "Rais anajitahidi. Upinzani nao unapaswa kueleza wananchi sera zao. Je, wangekuwa madarakani, wangewalipa wazee wa vijiji? Sidhani," alisema. Seneta huyo wa Siaya alisema marehemu kaka yake, Raila Odinga, aliacha ODM ikiwa sehemu ya serikali jumuishi na kwamba chama hicho kitaendelea kushirikiana na Rais Ruto. "Marehemu Raila Odinga alituacha ndani ya serikali jumuishi. Hatutamezwa na Rais Ruto bali tutashirikiana kuunda serikali imara," alisema. Kauli zake zinajiri huku Rais Ruto akizidisha juhudi za kuimarisha uungwaji mkono katika maeneo ya Nyanza na Magharibi, kufuatia kuzorota kwa uhusiano wake wa kisiasa na eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimuunga mkono kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa 2022. Wakati huo huo, mjadala kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto umeendelea pia katika eneo la Mlima Kenya. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki tayari ametangaza kuwa ananuia kutetea nafasi yake mwaka 2027. Prof Kindiki amesema eneo la Mlima Kenya linaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto na halipaswi kuacha mradi walioanza pamoja kabla ya kukamilika. Jina la Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru pia limeendelea kutajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania unaibu rais chini ya muungano unaoongozwa na Rais Ruto.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 16 hours ago
Gachagua awasha moto kwa kutaka vyama vya Mlima Kenya vivunjwe
MVUTANO wa kisiasa unaendelea kutokota katika eneo la Mlima Kenya na kutishia juhudi za kuunganisha upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao. Chanzo cha mzozo huo ni matamshi ya aliyekuwa Naibu Rais na kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua kwamba vyama vingine vya Mlima Kenya vivunjwe na viongozi wake wahamie DCP. Kauli hiyo imekosolewa vikali na viongozi kutoka Mlima Kenya Mashariki, ambao wanamlaumu Gachagua kwa kutaka kujitangaza kinara wa eneo hilo. Wakizungumza Jumanne, viongozi wa Democratic Party (DP), Party of National Unity (PNU) na Devolution Empowerment Party (DEP) walimtaka Gachagua kuheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa. Kiongozi wa PNU Peter Munya alisema kila chama ni taasisi huru inayolindwa na Katiba. "Hakuna mwanasiasa mwenye mamlaka ya kuamuru chama kingine kivunjwe, kiunganishwe au kuamua mustakabali wake. Huko ni kudharau wanachama na viongozi waliokijenga," alisema Munya. Aliongeza kuwa Katiba inampa kila Mkenya haki ya kuunda au kujiunga na chama chochote cha kisiasa. "Gachagua hana mamlaka ya kisheria wala ya kimaadili ya kuamua hatima ya vyama vingine," alisema. Hata hivyo, viongozi hao walisisitiza kuwa bado wanaunga mkono juhudi za kuunganisha upinzani ili kumng'oa Rais William Ruto mwaka ujao. Walimuonya Gachagua dhidi ya matamshi yanayoweza kuzua migawanyiko. "Tunataka aache kauli za kugawanya watu na badala yake akubali mazungumzo ya kuheshimiana. Miungano ya kudumu hujengwa kwa usawa, imani na heshima," walisema. Viongozi hao pia walikataa madai kwamba Gachagua ndiye msemaji wa Mlima Kenya. "Hakuna aliyempa mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya watu wote wa Mlima Kenya au vyama vya eneo hili," walisema.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 17 hours ago
Kikosi cha maprofesa watano wanaomwandalia Ruto ruwaza ya Kenya 2060
RAIS William Ruto amewapa wasomi watano mashuhuri jukumu la kuandaa mpango mpya wa maendeleo utakaoongoza Kenya baada ya kumalizika kwa Ruwaza ya 2030, akisema kazi hiyo inahitaji utafiti wa kina badala ya siasa. Badala ya kuwateua wanasiasa au maafisa wa serikali kuandaa ruwaza hiyo, Rais Ruto aliwachagua maprofesa Hiroyuki Hino, Anyang' Nyong'o, Michael Chege, Karuti Kanyinga na Peter Wanyande kuongoza zoezi hilo. Akipokea ripoti yao mnamo Julai 21, Rais aliwashukuru kwa mchango wao katika kuandaa mkakati wa maendeleo wa muda mrefu. "Ninawashukuru tena Profesa Hiroyuki Hino, Profesa Anyang' Nyong'o, Profesa Michael Chege, Profesa Karuti Kanyinga, Profesa Peter Wanyande na wenzao wote walioshiriki katika kazi hii muhimu," alisema. Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, alisema uteuzi huo ulilenga kuwaleta pamoja wataalamu wa uchumi wa kisiasa, utawala, sera za umma na mipango ya maendeleo ili kutoa mapendekezo yatakayovuka mipaka ya siasa za uchaguzi. Alisema uzoefu wa wasomi hao unatokana na kazi zao katika serikali mbalimbali, taasisi za kimataifa na vyuo vikuu nchini na nje ya nchi. Profesa Hiroyuki Hino Profesa Hino ni raia wa Japan mwenye tajriba ya miongo kadhaa katika masuala ya fedha na maendeleo. Aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu mwaka 1975 na baadaye kuwa mkurugenzi wa ofisi yake ya Asia na Pacific. Pia aliwahi kuwa mshauri wa kiuchumi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakati wa Serikali ya Muungano. Kulingana na Ikulu, tajriba yake kuhusu mageuzi ya kiuchumi katika mataifa ya Asia kama Korea Kusini, Singapore, China na Vietnam itasaidia Kenya kuandaa mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda. Profesa Anyang' Nyong'o Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang' Nyong'o, analeta uzoefu mkubwa katika siasa, utawala na taaluma. Baada ya kupata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere, aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Chicago alikopata Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Sayansi ya Siasa. Aliwahi kuwa mhadhiri na baadaye profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi pamoja na kufundisha katika vyuo vikuu vya Mexico na Ethiopia. Katika serikali ya Rais Mwai Kibaki, alihudumu kama Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kitaifa na kushiriki katika mageuzi yaliyozaa Ruwaza ya 2030. Profesa Nyong'o anasema ruwaza mpya haikusudiwi kufuta ile ya 2030 bali kuendeleza msingi uliowekwa na mipango ya awali ya maendeleo. Profesa Michael Chege Profesa Michael Chege ni mtaalamu wa utawala bora, uchumi wa kisiasa na ujenzi wa taasisi za serikali. Kwa sasa anafundisha sera za umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuhudumu katika taasisi mbalimbali zikiwemo UNDP, Ford Foundation na Chuo Kikuu cha Florida nchini Amerika. Amefanya pia kazi za ushauri kwa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika na mashirika mengine ya kimataifa. Ikulu inaamini mchango wake utasaidia kuimarisha taasisi zinazoweza kuendeleza sera za maendeleo bila kutegemea mabadiliko ya serikali. Profesa Karuti Kanyinga Profesa Karuti Kanyinga ni mmoja wa wataalamu wakuu nchini kuhusu ugatuzi, utawala bora, Katiba na sera za umma. Kwa zaidi ya miaka 30 amefanya utafiti kuhusu haki za ardhi, demokrasia, uchaguzi, ushiriki wa wananchi na maendeleo. Akiwa katika Taasisi ya Tafiti za Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Nairobi, ameongoza tafiti nyingi zilizochangia mageuzi ya utawala nchini. Profesa Peter Wanyande Profesa Peter Wanyande anakamilisha timu hiyo. Yeye ni mtaalamu wa utawala wa umma, taasisi za kidemokrasia na usimamizi wa serikali. Mbali na kuwa mhadhiri wa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliwahi pia kuwa mshauri wa sera wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Kwa mujibu wa Ikulu, kila mmoja wa wasomi hao analeta utaalamu tofauti unaokamilishana. Kwa pamoja, wamekusanya mamia ya miaka ya uzoefu katika kufundisha, kufanya tafiti, kuhudumu serikalini na kutoa ushauri kuhusu sera za maendeleo. Serikali inaamini kuwa mchango wao utaisaidia Kenya kuandaa ruwaza mpya ya maendeleo itakayodumu kwa vizazi na kuendelea kutekelezwa bila kujali mabadiliko ya kisiasa baada ya uchaguzi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 18 hours ago
Sifuna, washirika wamsukuma msajili akubali Linda Mwananchi kama chama cha kisiasa
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna na washirika wake Jumanne waliendeleza juhudi zake za kusajili Linda Mwananchi kama chama cha kisiasa watakachotumia kuwania urais mwaka 2027. Viongozi wa kundi hilo walikutana kwa faragha na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou, wakitaka maelezo kuhusu uamuzi wa kukataa kuhifadhi jina la chama hicho. Baada ya mkutano huo, msemaji wa Linda Mwananchi Caroli Omondi alisema msajili ameahidi kupitia upya uamuzi huo na kutoa msimamo wake kabla ya mwisho wa wiki. "Msajili ametuhakikishia kwamba atapitia upya uamuzi wake na kutupa majibu kabla ya wiki hii kuisha," alisema Omondi. Hapo awali, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) ilikataa ombi la kuhifadhi jina Linda Mwananchi Party of Kenya (LMPK) ikisema linafanana na majina au kaulimbiu nyingine zilizopo kama Linda Mkenya na Boresha Kenya, jambo linalokiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Mkutano huo ulihudhuriwa na Sifuna, Omondi, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Mbunge wa Mavoko Patrick Makau, Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo na aliyekuwa Rais wa LSK, Faith Odhiambo. Osotsi alisema waliamua kumuona msajili baada ya mawakili wao kuwasilisha ombi la kuhifadhi jina hilo lakini likakataliwa. "Tulienda kwa msajili kwa sababu tulikuwa tumewaagiza mawakili wetu kusajili jina hilo. Pia tulimtaka afanye uamuzi wake bila kushinikizwa na mtu yeyote," alisema Osotsi. Awali, mwanaharakati Charles Wanyonyi alikuwa ameomba kusajili jina hilo, hatua iliyopingwa na viongozi wa Linda Mwananchi kupitia kampuni ya mawakili ya Henia Anzala and Associates. Kundi hilo lilieleza kuwa kwa miezi kadhaa limekuwa likifanya mikutano na kampeni nchini kote kwa jina la Linda Mwananchi, hivyo jina hilo sasa linahusishwa moja kwa moja na harakati zake za kisiasa. Lilisema kulisajili jina hilo bila ushiriki wake kungechanganya umma kuhusu umiliki na mwelekeo wa vuguvugu hilo. Harakati za Linda Mwananchi zilianza kama kaulimbiu ya kisiasa kupinga kauli ya "Linda Ground" ya kiongozi wa ODM Oburu Oginga, lakini sasa zimekua na kuwa vuguvugu lenye viongozi, mtandao wa waratibu na ajenda ya kuwahamasisha Wakenya kudai uwajibikaji katika utumishi wa umma.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 19 hours ago
Mpango wa Uhuru kufufua Azimio wapingwa vikali na vyama vya Upinzani
MPANGO wa Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta wa kufufua muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 umepingwa vikali na baadhi ya vyama vya upinzani, hali inayotishia kuvuruga juhudi za kuunganisha mrengo huo dhidi ya Rais William Ruto. Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na kundi la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, vimesema havina mpango wa kujiunga na Azimio kwa sasa. Viongozi hao wa DCP na Linda Mwananchi wanasema kipaumbele chao ni kuimarisha vyama vyao kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu miungano. Katika chama cha Uhuru cha Jubilee, baadhi ya viongozi pia wanapinga mpango huo wakidai unalenga kumpa kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, nafasi ya moja kwa moja ya kuwania urais kwa tiketi ya upinzani. Chama cha People's Liberation Party (PLP) cha Martha Karua pia kimeibua wasiwasi kikidai kuna njama za kupuuza ripoti ya kamati ya kiufundi ya upinzani iliyoongozwa na Kipruto Kirwa, ambayo ilipendekeza jina jipya la muungano na mfumo wa kugawana nyadhifa za uongozi. Kiini hasa cha mvutano ni kipengele katika katiba ya Azimio kinachomtambua kiongozi wa muungano kuwa mgombea wa urais moja kwa moja. Mnamo Februari mwaka huu, Uhuru alimteua Kalonzo kuwa kiongozi mpya wa Azimio baada ya marehemu Raila Odinga, ambaye alikuwa mgombea wa urais wa muungano huo 2022. Mnamo Jumanne, Kalonzo alikutana na Gachagua pamoja na kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa, katika juhudi za kudhibiti migawanyiko inayozidi kujitokeza. Alisema mazungumzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kupanua Azimio na kuimarisha umoja wa upinzani. Hata hivyo, vinara wapya wa Azimio akiwemo Justin Muturi, Peter Munya na Lenny Kivuti, walimshutumu Gachagua kwa madai ya kuwashinikiza wavunje vyama vyao na kuhamia DCP. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema haelewi kwa nini kuna haraka ya kufufua Azimio, akidai baadhi ya viongozi wamekuwa wakitengwa kwa kumuunga mkono Fred Matiang'i badala ya Kalonzo. "Tunapaswa kuambiwa kwa nini Azimio inafufuliwa sasa. Kalonzo mwenyewe aliwahi kupendekeza ivunjwe. Ningependa kujua kwa nini ghafla kuna haraka ya kuifufua," alisema Kioni. Kwa upande mwingine, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kundi la Linda Mwananchi linaendelea kujenga umaarufu wa Edwin Sifuna kabla ya kujadili miungano. "Kwa sasa tunajikita katika kuvumisha Linda Mwananchi na kuhakikisha mgombea wetu anatangaza rasmi azma yake ya kuwania urais. Hatusemi kwamba hatuwezi kujiunga na muungano, lakini kwa sasa tunajenga chama chetu na mgombea wetu, " alisema. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema kundi hilo halijawahi kujadili suala la kujiunga na Azimio. Kwa upande wa DCP, Mbunge wa Gatanga Edward Muriu alisema chama hicho kitawazia kujiunga na Azimio iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika muundo na uongozi wa muungano huo. Alisema ODM bado ni mhimili mkuu wa Azimio, jambo linalohitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya mazungumzo yoyote. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru (Mejja Donk) alisema hakuna chama kitakachokubali "kumezwa" na muungano uliopo bila masharti ya usawa. Naye Gachagua aliwaambia wafuasi wake kuwa hakuna mgombea atakayeteuliwa kwa makubaliano ya viongozi pekee. "Hebu kila chama kitafute uungwaji mkono kivyake kwanza. Tusifikirie kuwa tutaketi mahali na kugawana vyeo," alisema. Katika mkutano ulioongozwa na Uhuru Jumatatu, viongozi walikubaliana kupatia Azimio sura mpya na kuwaleta pamoja viongozi wote wa upinzani kabla ya kumteua mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto mwaka ujao. Katika mabadiliko hayo, Fred Matiang'i, Munya na Kivuti walijumuishwa katika baraza la uongozi wa Azimio huku vyama vya Democratic Party (DP), People's Democratic Party (PDP) na Umoja na Maendeleo Party (UMP) vikijiunga na muungano huo. Muturi alisema mkataba wa Azimio unapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha vyama vyote vinashiriki kikamilifu katika maamuzi, hasa kipengele kinachompa kiongozi wa muungano tiketi ya moja kwa moja ya urais. Katibu Mkuu wa Azimio Caroli Omondi alisema mazungumzo yanaendelea kuwashawishi Gachagua na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kujiunga na muungano huo. Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha mazungumzo, muungano huo unaweza kubadilisha jina ili kuwavutia washirika wapya na vijana wa Gen Z, huku ukidumisha wafuasi wa Raila Odinga. Mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika Profesa David Monda, alisema kufufuliwa kwa Azimio kunaweza kumuinua Kalonzo kisiasa, lakini mafanikio yake yatategemea kama vyama vingine vya upinzani vitakubali kufanya kazi chini ya mwavuli huo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 10:25:19
Serikali itapunguza bei ya mbolea na mbegu mwaka ujao, Rais aahidi
RAIS William Ruto ameahidi kwamba serikali itapunguza bei ya mbolea na mbegu mwaka ujao ili kutoa afueni kwa wakulima waliopata hasara mwaka huu baada ya mimea yao kunyauka kutokana na uhaba wa mvua. Walioathirika zaidi ni wakulima wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, linalotegemewa pakubwa kwa uzalishaji wa chakula cha kukidhi hitaji la kitaifa. "Serikali itaingilia kati kwa kupunguza bei ya mbolea na mbegu kuanzia msimu ujao wa upanzi ili kuhakikisha kuwa wakulima wanaongeza uzalishaji kufidia hasara ya mwaka huu," akasema mnamo Jumapili alipohudhuria ibada katika kanisa la Kianglikana, Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu. Hata hivyo, Rais hakubainisha ni kwa kiwango kipi bei ya pembejeo hizo zitapunguzwa. Wakati huu mbolea ya upanzi inauzwa kwa Sh2,500 kwa gunia la kilo 50, chini ya mpango wa serikali wa utoaji mbolea kwa bei nafuu. Nayo Kampuni ya Mbegu Nchini (KSC) inauza mbegu za mahindi kwa Sh260 kwa kilo huku ikiuza gunia la kilo 25 kwa Sh6,560.
read moreRight Column Content