T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Wakazi Turkana wahofia vikosi vinalinda maeneo ya mafuta badala ya usalama wao

WAKAZI wa vijiji vya Lopii, Nakukulas, Lokwamosing, Lokori na Kahuruko katika Bonde la South Lokichar, Kaunti ya Turkana, wanasema sasa wanaishi kwa hofu ya vikosi vya usalama licha ya miaka mingi wakikabiliwa na mashambulizi ya majangili. Wakazi hao wanadai oparesheni kali iliyoanzishwa mwezi uliopita na kikosi maalumu cha polisi imegeuza eneo hilo kuwa kama kambi ya kijeshi. Wanasema magari ya kivita yanazunguka vijijini huku wakazi wakizuiwa kutembea  kwa uhuru, jambo linalozua hofu kuwa serikali inalenga kulinda maeneo ya mafuta badala ya wananchi. Serikali, hata hivyo, inasema oparesheni hiyo inalenga kukomesha wizi wa mifugo na mashambulizi ya majangili. Mfugaji Meshack Etiir wa kijiji cha Lopii alisema wakazi wamekuwa wakitegemea mtandao wa kutoa taarifa za kiusalama ili kubaini watu wanaoshukiwa kushirikiana na majangili. Alisema taarifa hizo zilisaidia kupanga mikakati na Polisi wa Akiba pamoja na maafisa wa utawala ili kukabiliana na mashambulizi. Kwa mujibu wake, familia nyingi zimeendelea kuwa maskini baada ya kupokonywa mifugo huku juhudi za serikali za kurejesha wanyama hao zikikosa kuzaa matunda. Mwakilishi wa Wadi ya Lokichar, Samwel Lomodo, alisema viongozi wamekuwa wakiripoti mashambulizi ya mara kwa mara katika vijiji vya Lopii, Lokwamosing na Nakukulas bila serikali kuchukua hatua za haraka. Alidai kuwa majangili bado wanaendelea kujificha katika maeneo ya Kailongol, Lokwatuba, Lochakula, Lotongot na Loritit licha ya oparesheni ya kuwasaka. Bw Lomodo alisema badala ya vikosi vya usalama kuwafuatilia majangili na kurejesha mifugo iliyoibwa, vinaelekeza nguvu kwa wakazi wasio na hatia. Naye mkazi wa Nakukulas, Mark Epurui, alisema wakazi hawawezi tena kupeleka mifugo karibu na maeneo ya mafuta wala kutafuta taarifa kuhusu nafasi za kazi zinazotarajiwa wakati uchimbaji wa mafuta utakapoanza tena. Kwa upande wake, Eunice Ateyo wa shirika la Friends of Lake Turkana alisema wanaharakati wa haki za binadamu wamebaini hofu kubwa miongoni mwa wakazi kutokana na uwepo wa magari ya kivita. Alidai baadhi ya wakazi wamefurushwa na nyumba kadhaa kuchomwa moto wakati wa oparesheni hiyo. Mwakilishi wa Wadi ya Lokori/Kochodin Willy Napuyo, alisema ikiwa serikali inapanga kutwaa ardhi kwa ajili ya miradi ya mafuta, wakazi wanapaswa kufahamishwa mapema kuhusu fidia na makazi mapya. Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Turkana, Julius Kavita, alitetea oparesheni hiyo akisema ilianzishwa baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi. Alisema serikali itaendelea na juhudi za kurejesha mifugo iliyoibwa na kuwakamata wahusika wa mashambulizi hayo.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

Mali ya kifahari ya Wa Iria kupigwa mnada kwa kushindwa kulipa mkopo

MALI inayohusishwa na aliyekuwa Gavana wa Murang'a, Mwangi wa Iria, inatarajiwa kuuzwa kwa mnada baadaye mwezi huu baada ya kudaiwa kushindwa kulipa mkopo ambao kiasi chake hakijafichuliwa, hali inayoongeza matatizo yake ya kisheria huku pia akikabiliwa na kesi ya ufisadi ya zaidi ya Sh542.6 milioni. Tangazo la kampuni ya Dalali Traders Auctioneers linaonyesha kuwa nyumba yake ya kifahari iliyoko Karen, Nairobi, pamoja na Edinburgh Mountain Hospital iliyoko Murang'a, zitauzwa kwa mnada mnamo Agosti 25. Hatua hiyo imejiri chini ya miaka miwili tangu Rais William Ruto amteue Bw Wa Iria kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA). Tangazo hilo linaonyesha kuwa hospitali hiyo iko kwenye shamba la ekari 2.96 katika eneo la Milimani, Kiharu, Murang'a, karibu na Chuo Kikuu cha Murang'a na Chuo cha Matibabu cha Edinburgh. Hospitali hiyo inamilikiwa kikamilifu na Bw Wa Iria kupitia kampuni ya Edinburgh Mountain Hospital Limited. Mali hiyo imestawishwa kwa jengo la hospitali la ghorofa tano pamoja na maeneo ya kupumzikia. Nyumba inayotarajiwa kuuzwa iko katika eneo la Karen, kwenye ploti ya ekari 0.48 katika Muiri Lane. Mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la Bw Wa Iria na ilitumika kama dhamana ya mkopo uliochukuliwa na Edinburgh College Ltd pamoja na Edinburgh Mountain Hospital Ltd. Nyumba hiyo ya ghorofa tatu ilikuwa karibu kukamilika na pia ina nyumba ya wageni, maegesho ya magari, pamoja na mipango ya kujenga bwawa la kuogelea, gazebo na nyumba za wafanyakazi. Bw Wa Iria na kampuni ya madalali hawakufichua jina la mkopeshaji wala kiwango cha mkopo unaodaiwa. Mbali na madai ya mkopo, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pia imewasilisha kesi ikitaka kurejesha Sh542.6 milioni, ikidai fedha hizo zilipatikana kupitia ufisadi na ukiukaji wa taratibu za ununuzi alipokuwa gavana wa Murang'a. Hata hivyo, Bw Wa Iria amekanusha madai hayo na kesi bado iko mahakamani. Bw Wa Iria ni miongoni mwa viongozi wa zamani ambao mali yao iko hatarini kupigwa minada au kurejeshwa kwa serikali. Wengine ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, ambaye pia amepoteza baadhi ya mali zake kutokana na migogoro ya mikopo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Oburu 'Youth Leader' naye ataka nafasi ya Naibu Rais

IDADI ya wanaomezea mate wadhifa wa Naibu Rais katika muungano wa kisiasa unaounga mkono Rais William Ruto imeendelea kuongezeka, viongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) pia wakitaka nafasi hiyo. Wiki mbili tu baada ya baadhi ya viongozi kumpendekeza Waziri wa Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati, Wycliffe Oparanya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, sasa kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, ametangaza hadharani kuwa anataka wadhifa huo. Akizungumza Jumanne katika Ikulu ya Nairobi wakati Rais Ruto alipokutana na wazee wa vijiji kutoka sehemu mbalimbali nchini, Dkt Oburu alisema ODM haitatoa mgombea urais mwaka 2027 bali itamuunga mkono Rais Ruto. "Wakati huu ODM haitakuwa na mgombeaji wa urais. Mgombea wetu ni Rais William Ruto. Lakini nafasi nyingine zote zinaweza kujadiliwa, hasa ya Naibu Rais. Hamuoni kwamba mimi ninafaa kuwa nambari mbili? Mimi pia nina sifa zinazohitajika," alisema Dkt Oburu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 82, alisema ODM itaunga mkono azma ya Rais Ruto kutetea urais kwa muhula wa pili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa chama hicho, kikiwa miongoni mwa vyama vikuu katika muungano unaotawala, kitajadiliana ili kipate unaibu rais. Dkt Oburu pia alimpongeza Rais Ruto kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini na kwa uamuzi wa serikali kutoa malipo ya kila mwezi kwa wazee wa vijiji. "Rais anajitahidi. Upinzani nao unapaswa kueleza wananchi sera zao. Je, wangekuwa madarakani, wangewalipa wazee wa vijiji? Sidhani," alisema. Seneta huyo wa Siaya alisema marehemu kaka yake, Raila Odinga, aliacha ODM ikiwa sehemu ya serikali jumuishi na kwamba chama hicho kitaendelea kushirikiana na Rais Ruto. "Marehemu Raila Odinga alituacha ndani ya serikali jumuishi. Hatutamezwa na Rais Ruto bali tutashirikiana kuunda serikali imara," alisema. Kauli zake zinajiri huku Rais Ruto akizidisha juhudi za kuimarisha uungwaji mkono katika maeneo ya Nyanza na Magharibi, kufuatia kuzorota kwa uhusiano wake wa kisiasa na eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimuunga mkono kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa 2022. Wakati huo huo, mjadala kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto umeendelea pia katika eneo la Mlima Kenya. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki tayari ametangaza kuwa ananuia kutetea nafasi yake mwaka 2027. Prof Kindiki amesema eneo la Mlima Kenya linaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto na halipaswi kuacha mradi walioanza pamoja kabla ya kukamilika. Jina la Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru pia limeendelea kutajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania unaibu rais chini ya muungano unaoongozwa na Rais Ruto.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Gachagua awasha moto kwa kutaka vyama vya Mlima Kenya vivunjwe

MVUTANO wa kisiasa unaendelea kutokota katika eneo la Mlima Kenya na kutishia juhudi za kuunganisha upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao. Chanzo cha mzozo huo ni matamshi ya aliyekuwa Naibu Rais na kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua kwamba vyama vingine vya Mlima Kenya vivunjwe na viongozi wake wahamie DCP. Kauli hiyo imekosolewa vikali na viongozi kutoka Mlima Kenya Mashariki, ambao wanamlaumu Gachagua kwa kutaka kujitangaza kinara wa eneo hilo. Wakizungumza Jumanne, viongozi wa Democratic Party (DP), Party of National Unity (PNU) na Devolution Empowerment Party (DEP) walimtaka Gachagua kuheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa. Kiongozi wa PNU Peter Munya alisema kila chama ni taasisi huru inayolindwa na Katiba. "Hakuna mwanasiasa mwenye mamlaka ya kuamuru chama kingine kivunjwe, kiunganishwe au kuamua mustakabali wake. Huko ni kudharau wanachama na viongozi waliokijenga," alisema Munya. Aliongeza kuwa Katiba inampa kila Mkenya haki ya kuunda au kujiunga na chama chochote cha kisiasa. "Gachagua hana mamlaka ya kisheria wala ya kimaadili ya kuamua hatima ya vyama vingine," alisema. Hata hivyo, viongozi hao walisisitiza kuwa bado wanaunga mkono juhudi za kuunganisha upinzani ili kumng'oa Rais William Ruto mwaka ujao. Walimuonya Gachagua dhidi ya matamshi yanayoweza kuzua migawanyiko. "Tunataka aache kauli za kugawanya watu na badala yake akubali mazungumzo ya kuheshimiana. Miungano ya kudumu hujengwa kwa usawa, imani na heshima," walisema. Viongozi hao pia walikataa madai kwamba Gachagua ndiye msemaji wa Mlima Kenya. "Hakuna aliyempa mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya watu wote wa Mlima Kenya au vyama vya eneo hili," walisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 6 hours ago

Kikosi cha maprofesa watano wanaomwandalia Ruto ruwaza ya Kenya 2060

RAIS William Ruto amewapa wasomi watano mashuhuri jukumu la kuandaa mpango mpya wa maendeleo utakaoongoza Kenya baada ya kumalizika kwa Ruwaza ya 2030, akisema kazi hiyo inahitaji utafiti wa kina badala ya siasa. Badala ya kuwateua wanasiasa au maafisa wa serikali kuandaa ruwaza hiyo, Rais Ruto aliwachagua maprofesa Hiroyuki Hino, Anyang' Nyong'o, Michael Chege, Karuti Kanyinga na Peter Wanyande kuongoza zoezi hilo. Akipokea ripoti yao mnamo Julai 21, Rais aliwashukuru kwa mchango wao katika kuandaa mkakati wa maendeleo wa muda mrefu. "Ninawashukuru tena Profesa Hiroyuki Hino, Profesa Anyang' Nyong'o, Profesa Michael Chege, Profesa Karuti Kanyinga, Profesa Peter Wanyande na wenzao wote walioshiriki katika kazi hii muhimu," alisema. Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, alisema uteuzi huo ulilenga kuwaleta pamoja wataalamu wa uchumi wa kisiasa, utawala, sera za umma na mipango ya maendeleo ili kutoa mapendekezo yatakayovuka mipaka ya siasa za uchaguzi. Alisema uzoefu wa wasomi hao unatokana na kazi zao katika serikali mbalimbali, taasisi za kimataifa na vyuo vikuu nchini na nje ya nchi. Profesa Hiroyuki Hino Profesa Hino ni raia wa Japan mwenye tajriba ya miongo kadhaa katika masuala ya fedha na maendeleo. Aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu mwaka 1975 na baadaye kuwa mkurugenzi wa ofisi yake ya Asia na Pacific. Pia aliwahi kuwa mshauri wa kiuchumi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakati wa Serikali ya Muungano. Kulingana na Ikulu, tajriba yake kuhusu mageuzi ya kiuchumi katika mataifa ya Asia kama Korea Kusini, Singapore, China na Vietnam itasaidia Kenya kuandaa mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda. Profesa Anyang' Nyong'o Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang' Nyong'o, analeta uzoefu mkubwa katika siasa, utawala na taaluma. Baada ya kupata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere, aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Chicago alikopata Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Sayansi ya Siasa. Aliwahi kuwa mhadhiri na baadaye profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi pamoja na kufundisha katika vyuo vikuu vya Mexico na Ethiopia. Katika serikali ya Rais Mwai Kibaki, alihudumu kama Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kitaifa na kushiriki katika mageuzi yaliyozaa Ruwaza ya 2030. Profesa Nyong'o anasema ruwaza mpya haikusudiwi kufuta ile ya 2030 bali kuendeleza msingi uliowekwa na mipango ya awali ya maendeleo. Profesa Michael Chege Profesa Michael Chege ni mtaalamu wa utawala bora, uchumi wa kisiasa na ujenzi wa taasisi za serikali. Kwa sasa anafundisha sera za umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuhudumu katika taasisi mbalimbali zikiwemo UNDP, Ford Foundation na Chuo Kikuu cha Florida nchini Amerika. Amefanya pia kazi za ushauri kwa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika na mashirika mengine ya kimataifa. Ikulu inaamini mchango wake utasaidia kuimarisha taasisi zinazoweza kuendeleza sera za maendeleo bila kutegemea mabadiliko ya serikali. Profesa Karuti Kanyinga Profesa Karuti Kanyinga ni mmoja wa wataalamu wakuu nchini kuhusu ugatuzi, utawala bora, Katiba na sera za umma. Kwa zaidi ya miaka 30 amefanya utafiti kuhusu haki za ardhi, demokrasia, uchaguzi, ushiriki wa wananchi na maendeleo. Akiwa katika Taasisi ya Tafiti za Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Nairobi, ameongoza tafiti nyingi zilizochangia mageuzi ya utawala nchini. Profesa Peter Wanyande Profesa Peter Wanyande anakamilisha timu hiyo. Yeye ni mtaalamu wa utawala wa umma, taasisi za kidemokrasia na usimamizi wa serikali. Mbali na kuwa mhadhiri wa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliwahi pia kuwa mshauri wa sera wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Kwa mujibu wa Ikulu, kila mmoja wa wasomi hao analeta utaalamu tofauti unaokamilishana. Kwa pamoja, wamekusanya mamia ya miaka ya uzoefu katika kufundisha, kufanya tafiti, kuhudumu serikalini na kutoa ushauri kuhusu sera za maendeleo. Serikali inaamini kuwa mchango wao utaisaidia Kenya kuandaa ruwaza mpya ya maendeleo itakayodumu kwa vizazi na kuendelea kutekelezwa bila kujali mabadiliko ya kisiasa baada ya uchaguzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Sifuna, washirika wamsukuma msajili akubali Linda Mwananchi kama chama cha kisiasa

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna na washirika wake Jumanne waliendeleza juhudi zake za kusajili Linda Mwananchi kama chama cha kisiasa watakachotumia kuwania urais mwaka 2027. Viongozi wa kundi hilo walikutana kwa faragha na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou, wakitaka maelezo kuhusu uamuzi wa kukataa kuhifadhi jina la chama hicho. Baada ya mkutano huo, msemaji wa Linda Mwananchi Caroli Omondi alisema msajili ameahidi kupitia upya uamuzi huo na kutoa msimamo wake kabla ya mwisho wa wiki. "Msajili ametuhakikishia kwamba atapitia upya uamuzi wake na kutupa majibu kabla ya wiki hii kuisha," alisema Omondi. Hapo awali, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) ilikataa ombi la kuhifadhi jina Linda Mwananchi Party of Kenya (LMPK) ikisema linafanana na majina au kaulimbiu nyingine zilizopo kama Linda Mkenya na Boresha Kenya, jambo linalokiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Mkutano huo ulihudhuriwa na Sifuna, Omondi, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Mbunge wa Mavoko Patrick Makau, Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo na aliyekuwa Rais wa LSK, Faith Odhiambo. Osotsi alisema waliamua kumuona msajili baada ya mawakili wao kuwasilisha ombi la kuhifadhi jina hilo lakini likakataliwa. "Tulienda kwa msajili kwa sababu tulikuwa tumewaagiza mawakili wetu kusajili jina hilo. Pia tulimtaka afanye uamuzi wake bila kushinikizwa na mtu yeyote," alisema Osotsi. Awali, mwanaharakati Charles Wanyonyi alikuwa ameomba kusajili jina hilo, hatua iliyopingwa na viongozi wa Linda Mwananchi kupitia kampuni ya mawakili ya Henia Anzala and Associates. Kundi hilo lilieleza kuwa kwa miezi kadhaa limekuwa likifanya mikutano na kampeni nchini kote kwa jina la Linda Mwananchi, hivyo jina hilo sasa linahusishwa moja kwa moja na harakati zake za kisiasa. Lilisema kulisajili jina hilo bila ushiriki wake kungechanganya umma kuhusu umiliki na mwelekeo wa vuguvugu hilo. Harakati za Linda Mwananchi zilianza kama kaulimbiu ya kisiasa kupinga kauli ya "Linda Ground" ya kiongozi wa ODM Oburu Oginga, lakini sasa zimekua na kuwa vuguvugu lenye viongozi, mtandao wa waratibu na ajenda ya kuwahamasisha Wakenya kudai uwajibikaji katika utumishi wa umma.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 7 hours ago

Mpango wa Uhuru kufufua Azimio wapingwa vikali na vyama vya Upinzani

MPANGO wa Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta wa kufufua muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 umepingwa vikali na baadhi ya vyama vya upinzani, hali inayotishia kuvuruga juhudi za kuunganisha mrengo huo dhidi ya Rais William Ruto. Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na kundi la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, vimesema havina mpango wa kujiunga na Azimio kwa sasa. Viongozi hao wa DCP na Linda Mwananchi wanasema kipaumbele chao ni kuimarisha vyama vyao kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu miungano. Katika chama cha Uhuru cha Jubilee, baadhi ya viongozi pia wanapinga mpango huo wakidai unalenga kumpa kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, nafasi ya moja kwa moja ya kuwania urais kwa tiketi ya upinzani. Chama cha People's Liberation Party (PLP) cha Martha Karua pia kimeibua wasiwasi kikidai kuna njama za kupuuza ripoti ya kamati ya kiufundi ya upinzani iliyoongozwa na Kipruto Kirwa, ambayo ilipendekeza jina jipya la muungano na mfumo wa kugawana nyadhifa za uongozi. Kiini hasa cha mvutano ni kipengele katika katiba ya Azimio kinachomtambua kiongozi wa muungano kuwa mgombea wa urais moja kwa moja. Mnamo Februari mwaka huu, Uhuru alimteua Kalonzo kuwa kiongozi mpya wa Azimio baada ya marehemu Raila Odinga, ambaye alikuwa mgombea wa urais wa muungano huo 2022. Mnamo Jumanne, Kalonzo alikutana na Gachagua pamoja na kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa, katika juhudi za kudhibiti migawanyiko inayozidi kujitokeza. Alisema mazungumzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kupanua Azimio na kuimarisha umoja wa upinzani. Hata hivyo, vinara wapya wa Azimio akiwemo Justin Muturi, Peter Munya na Lenny Kivuti, walimshutumu Gachagua kwa madai ya kuwashinikiza wavunje vyama vyao na kuhamia DCP. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema haelewi kwa nini kuna haraka ya kufufua Azimio, akidai baadhi ya viongozi wamekuwa wakitengwa kwa kumuunga mkono Fred Matiang'i badala ya Kalonzo. "Tunapaswa kuambiwa kwa nini Azimio inafufuliwa sasa. Kalonzo mwenyewe aliwahi kupendekeza ivunjwe. Ningependa kujua kwa nini ghafla kuna haraka ya kuifufua," alisema Kioni. Kwa upande mwingine, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kundi la Linda Mwananchi linaendelea kujenga umaarufu wa Edwin Sifuna kabla ya kujadili miungano. "Kwa sasa tunajikita katika kuvumisha Linda Mwananchi na kuhakikisha mgombea wetu anatangaza rasmi azma yake ya kuwania urais. Hatusemi kwamba hatuwezi kujiunga na muungano, lakini kwa sasa tunajenga chama chetu na mgombea wetu, " alisema. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema kundi hilo halijawahi kujadili suala la kujiunga na Azimio. Kwa upande wa DCP, Mbunge wa Gatanga Edward Muriu alisema chama hicho kitawazia kujiunga na Azimio iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika muundo na uongozi wa muungano huo. Alisema ODM bado ni mhimili mkuu wa Azimio, jambo linalohitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya mazungumzo yoyote. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru (Mejja Donk) alisema hakuna chama kitakachokubali "kumezwa" na muungano uliopo bila masharti ya usawa. Naye Gachagua aliwaambia wafuasi wake kuwa hakuna mgombea atakayeteuliwa kwa makubaliano ya viongozi pekee. "Hebu kila chama kitafute uungwaji mkono kivyake kwanza. Tusifikirie kuwa tutaketi mahali na kugawana vyeo," alisema. Katika mkutano ulioongozwa na Uhuru Jumatatu, viongozi walikubaliana kupatia Azimio sura mpya na kuwaleta pamoja viongozi wote wa upinzani kabla ya kumteua mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto mwaka ujao. Katika mabadiliko hayo, Fred Matiang'i, Munya na Kivuti walijumuishwa katika baraza la uongozi wa Azimio huku vyama vya Democratic Party (DP), People's Democratic Party (PDP) na Umoja na Maendeleo Party (UMP) vikijiunga na muungano huo. Muturi alisema mkataba wa Azimio unapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha vyama vyote vinashiriki kikamilifu katika maamuzi, hasa kipengele kinachompa kiongozi wa muungano tiketi ya moja kwa moja ya urais. Katibu Mkuu wa Azimio Caroli Omondi alisema mazungumzo yanaendelea kuwashawishi Gachagua na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kujiunga na muungano huo. Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha mazungumzo, muungano huo unaweza kubadilisha jina ili kuwavutia washirika wapya na vijana wa Gen Z, huku ukidumisha wafuasi wa Raila Odinga. Mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika Profesa David Monda, alisema kufufuliwa kwa Azimio kunaweza kumuinua Kalonzo kisiasa, lakini mafanikio yake yatategemea kama vyama vingine vya upinzani vitakubali kufanya kazi chini ya mwavuli huo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Idara ya Usalama, Bodi ya Utalii wazindua ligi ya 'Panga Boys' Lamu

IDARA ya Usalama kupitia Kitengo cha Polisi wa Watalii (TPU) kwa ushirikiano na Bodi ya Utalii Lamu (LTA), Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF), tawi la Lamu, na serikali ya kaunti wamezindua ligi maalum inayolenga kukabiliana na uhalifu wa mapanga na dawa za kulevya miongoni mwa vijana eneo hilo. Ligi hiyo ya mpira wa miguu iliyozinduliwa Jumatatu inajumuisha vijana wasiozidi umri wa miaka 18. Jumla ya timu kumi na sita (16) zimeshirikishwa kwenye ngarambe hiyo ya wiki tatu mfululizo. Vilabu hivyo ni Nyundo FC, Crocodile FC, AC Milan, Swafaa FC, Dragon Fly FC, Al Aman, Kashmir City, Real Madrid FC, Rising Stars, Gen 2, Mararani FC, Lamu Boys FC, Home Boys FC, Al Azhar, Riyadha FC na Ukhtein FC. Timu zote ni za kisiwa cha Lamu. Akizungumza kwenye hafla ya kuzindua kiny'anganyiro hicho kwenye uwanja wa Twaif kisiwani Lamu Jumatatu, katibu wa kamati andalizi, ambaye pia ni Mwakilishi wa Vijana katika FKF, Lamu, Bw Athman Farid, maarufu Pirezi, aliwataka vijana kupendana na kuepuka kujiingiza kwenye magenge ya uhalifu na mihadarati. "Ligi yenyewe imeanzishwa madhumuni yakiwa ni kumaliza uhalifu wa mapanga na kuweka amani. Na ndiyo sababu tukaipa jina 'Weka Panga Chini, Chukua Mpira-Jenga Amani na Mustakabali wa Vijana'. Tupendane na kudumisha amani tunapocheza," akasema Bw Farid. Kauli yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Lamu (LTA) Fridah Njeri, aliyesisitiza kuwa ili Lamu kuvutia wageni zaidi wa kitaifa na kimataifa, lazima amani na utulivu vidumishwe. "Lamu ni kivutio cha watalii na wageni hawawezi kuvutiwa kuja hapa iwapo usalama unadorora. Tutumie ligi hii kuhubiri amani ili Lamu yetu iwe eneo zuri la wageni kuja na uchumi wetu kuimarika," akasema Bi Njeri. Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Vijana wa Kaunti ya Lamu Peter Ndichu, alisema mbali na kukabiliana na mihadarati na 'Panga Boys,' kinyang'anyiro kilichozinduliwa pia kinalenga kutambua vipaji vya kandanda miongoni mwa vijana wanaoshiriki ili kuwatafutia nafasi ya kucheza nje ya Lamu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Korti yaagiza EABL kuweka kando Sh10m kabla kusikiza kesi ya zogo na mwanahabari Willis Raburu

MAHAKAMA ya Biashara iliyoko Milimani, Nairobi, imeamuru kampuni ya East African Breweries PLC (EABL) iweke Sh10 milioni katika akaunti ya pamoja inayosimamiwa na mawakili wa pande zote kusubiri kusikizwa kwa kesi ya kibiashara iliyowasilishwa na mwanahabari na mshawishi wa mitandao ya kijamii Willis Raburu. Hakimu Mkuu Mwandamizi A. Nyoike alitoa agizo hilo huku akitupilia mbali ombi la Raburu la kusimamisha au kufuta leseni ya EABL kutokana na madai ya kutolipwa ada za mkataba. Mahakama ilisema kuwa ombi hilo lilikuwa sawa na kuomba amri ya lazima, ambayo Raburu hakufikia kiwango cha kisheria kinachohitajika ili kutolewa. Kupitia kampuni yake ya Steizon Limited, Raburu alishtaki Game Changer Marketing Limited pamoja na EABL akidai aliajiriwa kutoa huduma za ushawishi wa kidijitali, kuvumisha chapa, kuratibu hafla na matangazo ya mitandaoni katika tamasha la Furaha City Festival lililofanyika Desemba 2024. Alidai kuwa pande hizo zilikubaliana malipo Sh10 milioni, lakini hadi sasa hajalipwa. Raburu alisema alitekeleza kikamilifu wajibu wake, ikiwa ni pamoja na kutengeneza zaidi ya video 60 fupi za mitandaoni, machapisho zaidi ya 100, kuratibu washawishi wa mitandao ya kijamii na kusimamia shughuli za hafla hiyo. Aliongeza kuwa aliwasilisha ripoti baada ya tamasha na mara kadhaa kudai malipo, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda. Kwa upande wake, Game Changer Marketing ilikana kumwajiri Raburu kwa shughuli za Furaha City Festival. Kampuni hiyo ilisema ushirikiano wake na Raburu ulihusu tu kampeni ya awali ya Chrome Wabebe Campus Caravan, ambayo ilisema tayari alilipwa baada ya EABL kuidhinisha gharama na kutoa agizo rasmi la ununuzi. Nayo EABL ilikana kuwajibika ikisema tamasha la Furaha City lilikuwa sehemu ya mwisho ya kampeni ya Wabebe na si mradi mpya uliostahili malipo mengine. Aidha, ilisema hakukuwa na agizo jipya la ununuzi wala mkataba uliotiwa saini unaounga mkono madai ya Raburu ya Sh10 milioni. Katika uamuzi wake, Hakimu Nyoike alisema Raburu ameibua masuala yanayostahili kusikilizwa wakati wa kesi kamili. Hata hivyo, alisema ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili unakinzana na hawezi kutolewa uamuzi wa mwisho kupitia ombi la awali. "Ushahidi unaokinzana lazima uchunguzwe wakati wa kusikiliza kesi," alisema hakimu. Aliongeza kuwa Raburu hakuthibitisha kuwepo kwa "haki iliyo wazi na isiyoweza kutiliwa shaka" inayohitajika ili apewe amri ya lazima aliyoomba. Mahakama pia ilikataa hoja ya EABL kwamba kesi hiyo ilizimwa kwa kuwa kulikuwa na kesi nyingine inayohusu suala hilo katika Mahakama Kuu. Hakimu alisema kampuni hiyo haikuthibitisha kuwa kesi hiyo ilikuwa bado inaendelea baada ya Raburu kuonyesha kwamba ilikuwa imeondolewa. Hata hivyo, licha ya kukataa kuamuru EABL imlipe Raburu mara moja Sh10 milioni zinazodaiwa, mahakama iliagiza kampuni hiyo kuweka kiasi hicho katika akaunti ya pamoja inayosimamiwa na mawakili wa pande zote kama dhamana hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 05:03:34

Wadau wa utalii wahofia bima ya afya ya Sh6.5 milioni kwa kila mtalii itaua biashara

SERIKALI sasa inakabiliwa na kesi mahakamani kupinga agizo jipya linalowataka wageni wote wanaoingia Kenya kuwa na bima ya afya ya usafiri. Agizo hilo limezua upinzani mkali kutoka kwa wadau wa sekta ya utalii wanaosema litaongeza gharama za kusafiri na kupunguza ushindani wa Kenya kama kivutio cha watalii. Chama cha Watumiaji Bidhaa Nchini (COFEK) limewasilisha kesi katika Mahakama Kuu likitaka utekelezaji wa agizo hilo usimamishwe, likidai serikali ililitangaza bila ushirikishaji wa umma na bila kuzingatia Katiba kuhusu uwazi na utawala bora. Agizo hilo lilichapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali la Julai 30, 2026 na kutiwa saini na Waziri wa Afya Aden Duale. Linawataka wageni wote wanaoingia nchini kuwa na bima ya afya yenye kiwango cha chini cha fidia cha dola 50,000 (Sh6.5 milioni). Serikali inasema bima hiyo itawawezesha wageni kupata matibabu ya dharura bila kutegemea hospitali za umma. Hata hivyo, COFEK inahoji kuwa haijabainishwa jinsi kampuni za bima zitakavyoidhinishwa, jinsi ada zitakavyotozwa wala usimamizi wa fedha utakavyofanywa. Katibu Mkuu wa COFEK Stephen Mutoro alisema shirika hilo halipingi bima ya afya kwa wageni, bali linapinga namna sera hiyo ilivyoanzishwa bila kufuata taratibu za kikatiba. Wakati huo huo, wadau wa utalii wameonya kuwa agizo hilo litafanya Kenya kuwa ghali zaidi kwa watalii ikilinganishwa na mataifa jirani kama Tanzania, Rwanda na Afrika Kusini. Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Hoteli na Wapishi (KAHC) Dkt Sam Ikwaye, alisema sekta hiyo inapinga hatua hiyo kwa sababu inawaongezea watalii gharama nyingine wakati serikali inapaswa kuhamasisha wageni wengi zaidi kutembelea nchi. Alisema serikali inapaswa kuboresha usafiri wa ndege za moja kwa moja, hasa kuelekea Pwani, badala ya kuongeza ada mpya. Mshauri wa masuala ya utalii Tony Kirimi alihoji kwa nini wageni walazimishwe kununua bima ya Kenya ilhali wengi tayari husafiri wakiwa na bima kutoka nchi zao. Wadau hao pia wanataka serikali ifafanue iwapo bima za kimataifa zitatambuliwa na ni kampuni zipi zitakazoruhusiwa kutoa huduma hiyo. Mzozo huo umeibuka wakati sekta ya utalii nchini inaonyesha dalili za kuimarika, huku Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) likiripoti zaidi ya ziara milioni 3.5 katika hifadhi za taifa mwaka huu. Wadau sasa wanaitaka serikali kusitisha utekelezaji wa agizo hilo hadi mashauriano ya kina yafanyike.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 02:55:08

Magenge ya ulanguzi wa bangi yazidisha ujanja kuificha kwa ndizi, biskuti kuhepa polisi

MISAKO mikali ya Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) dhidi ya dawa za kulevya katika kipindi cha miezi sita iliyopita imefichua mbinu mpya zinazotumiwa na walanguzi kusafirisha na kusambaza bangi nchini wakikwepa mtego wa polisi. Uchunguzi umebaini kuwa walanguzi wamebadili njia za usafirishaji, aina ya magari wanayotumia na hata mbinu za kuficha mzigo ili usigunduliwe. Baadhi yao sasa hupanda bangi katikati ya mashamba ya mahindi na mazao mengine ili kuficha mimea hiyo. Baada ya kuvunwa, huifunga kwa ustadi na wakati mwingine kuificha ndani ya bidhaa kama vile ndizi, biskuti au marobota ya nguo kabla ya kuisafirisha. Aidha, badala ya kutumia malori makubwa, sasa wanatumia magari madogo ya kibinafsi kama Toyota Probox na Toyota Wish, ambayo hayushukiwi kwa urahisi. Kutoka mpakani Sirare, bangi husafirishwa kwa pikipiki ikiwa imefichwa kama mizigo ya kawaida kabla ya kukabidhiwa kwa mawakala wanaoipakia upya kwenye magari yanayoelekea Nairobi na miji mingine. Mashambani Walanguzi pia hutumia barabara za mashambani zisizo na vizuizi vya polisi, hasa usiku, alfajiri au jioni, ili kukwepa ukaguzi. Wakati mwingine bangi husafirishwa kwa mabasi na matatu ikiwa imefichwa pamoja na mizigo halali katika hifadhi za mizigo. Katika visa vingine, maafisa wa DCI wamekuta bangi ikiwa imefichwa ndani ya magunia ya ndizi, marobota yaliyofungwa kwa karatasi maalumu na hata masanduku ya chuma. Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin alisema magenge ya kisasa ya dawa za kulevya sasa yanafanya kazi kama mitandao ya kimataifa inayotumia teknolojia na mbinu mpya za usafirishaji. "Ufanisi wa vita dhidi ya dawa za kulevya haupimwi kwa idadi ya waliokamatwa bali kwa ubora wa uchunguzi, kufanikiwa kwa mashtaka na kuvunjwa kabisa kwa mitandao ya uhalifu," akasema. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen naye alisema serikali itaendelea kuimarisha operesheni za kijasusi ili kuwafuatilia walanguzi na kuvunja mitandao yao. Katika miezi ya hivi karibuni, DCI imekamata shehena kadhaa za bangi zenye thamani ya mamilioni ya pesa katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hiyo haramu inayozidi kuhatarisha jamii, hasa vijana na wanafunzi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 01:55:57

Wakora sasa watawala kituo cha mabasi cha Green Park Terminus kilichogharimu Sh250 milioni

UCHUNGUZI umeibua madai kuwa Kituo cha mabasi cha Green Park jijini Nairobi, kilichojengwa kwa gharama ya Sh250 milioni ili kupunguza msongamano wa magari katikati mwa jiji, kinadhibitiwa na vijana wanaodaiwa kuwa na uhusiano na viongozi wakuu wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi. Duru kutoka City Hall zinadai kuwa vijana hao hukusanya ada za maegesho kutoka kwa mabasi na magari huku maafisa rasmi wa kaunti wakitengwa. [caption id="attachment_190791" align="alignnone" width="2000"] Uharibifu mkubwa waonekana Green Park Terminus baada ya kutelekezwa licha ya kugharimu mamilioni ya pesa kujenga. Picha|Dennis Onsongo[/caption] Inadaiwa kuwa fedha zinazokusanywa haziingii kwenye hazina ya kaunti. Ingawa hivyo, Afisa Mkuu wa Idara ya Mapato Tiras Njoroge, alikanusha madai hayo akisema kituo hicho kinaendelea kuingiza mapato, lakini hakutoa ushahidi. Uchunguzi pia ulibaini kuwa kituo hicho kiko katika hali mbaya, huku baadhi ya huduma zikiwa hazifanyi kazi. [caption id="attachment_190792" align="alignnone" width="2000"] Kituo cha Green Park Terminus kilichojengwa kwa gharama ya Sh250 milioni. Picha|Dennis Onsongo[/caption] Aidha, kaunti imeidhinisha ujenzi wa kituo cha mafuta na inapanga kukodisha sehemu ya eneo hilo kwa kampuni ya China kujenga kituo cha kupasha moto magari ya umeme. Awali, Green Park ilikusudiwa kuwa kituo cha kushusha na kuwachukua abiria wa mabasi ya masafa marefu na matatu, lakini haijatimiza lengo hilo tangu ilipokamilika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 02:55:02

Wadau wapinga hatua ya serikali ya kutaka watalii wanaoingia nchini kuwa na bima ya lazima

WADAU katika sekta ya utalii wamepinga vikali uamuzi wa serikali wa kutaka wageni wote wanaoingia nchi kuwa na bima ya lazima wakionya kuwa hatua hiyo itaathiri nchi kuvutia watalii wa kimataifa. Kulingana na tangazo lililochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la Julai 30, 2026 na kutiwa sahihi na Waziri wa Afya, Bw Aden Duale, wageni wote wanaoingia humu nchini watalazimika kuwa na bima ya afya yenye kiwango cha chini cha karibu Sh6.45 milioni. Bima hiyo itagharamia hadi Sh2.58 milioni za matibabu, Sh3.22 milioni za usafiri wa dharura wa mgonjwa, Sh38,700 za dawa zilizoagizwa na daktari, Sh129,000 za matibabu ya afya ya akili na Sh645,000 za kusafirisha mwili wa marehemu kurejeshwa nchini kwao. Kulingana na serikali, hatua hiyo inalenga kuhakikisha watalii wanapata huduma wanapokumbwa na dharura za kiafya. Hata hivyo, wadau wa utalii wamejitokeza na kupinga hatua hiyo wakisema itaongeza gharama za kuzuru Kenya. "Hatua hii itaongeza gharama kwa watalii. Kama sekta ya utalii tunapinga hatua hii. Huu si mwelekeo unaofaa, tunafaa kuweka mikakati ya kuvutia watalii si kuwazuia kuzuru nchi yetu," Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha wamiliki wa hoteli na wahudumu (KAHC), Dkt Sam Ikwaye, alisema. Wadau hao walisema bima hiyo ya lazima inaongezwa juu ya ada nyingine ambazo wageni tayari hulipa, ikiwemo ada ya Kibali cha Kielektroniki cha Kusafiri (ETA) na ada za kuingia katika hifadhi za taifa za wanyamapori iliyooongezwa hivi majuzi. Mtaalamu wa utalii, Bw Tony Kirimi alisema watalii wengi tayari huingia nchini wakiwa na bima kamili ya afya walizonunua nchi zao. "Hivyo basi hakuna sababu ya kuwalazimisha kununua nyingine nchini Kenya. Tulikubali ada ya ETA, ada za kuingia kwenye mbuga zilipandishwa na sasa tunaanzisha bima ya afya ya lazima ambayo ni ghali zaidi kuliko ilivyo katika baadhi ya mataifa ya Ulaya. Kulikuwa na maana gani ya kuondoa visa halafu tuanzishe gharama nyingine?" aliuliza. Aliongeza kuwa Kenya bado inapambana kuvutia watalii na kujenga jina lake kama kitovu kikuu cha utalii duniani na hivyo haipaswi kuweka sera zitakazozuia watalii kuchagua mataifa mengine. Wadau wa utalii pia wanaitaka serikali kufafanua ikiwa bima za afya ambazo watalii tayari wanazosafiri nazo kutoka mataifa yao zitatambuliwa, kiwango cha malipo kitakachotozwa na kampuni zitakazoruhusiwa kutoa huduma hiyo. Bw Mohammed Hersi ambaye ni mtaalamu wa utalii alisema sera hiyo itaongeza gharama kwa watalii. "Mtalii analipia bima akiwa kwao kabla ya kuja Kenya, halafu analazimishwa kununua nyingine hapa. Je, ingekuwaje kama kila nchi zingekuwa na sharti kama hilo? Swali si kama ni dola kumi au mia moja, ikiwa malipo hayo hayana msingi, basi ni mzigo usiofaa," alisema kwenye mjadala katika mtandao wa Facebook. Wadau hao sasa wanataka serikali kusitisha utekelezaji wa sera hiyo na kuanza kufanya mashauriano kati ya Wizara za Afya, Utalii, kampuni za bima na wadau wa sekta hiyo. Mjadala huo umeibuka wakati ambapo sekta ya utalii inaendelea kunoga. Hii ni baada ya Kenya kunakili idadi kubwa ya watalii wanaozuru mbuga za kitaifa za Wanyama porini. Kulingana na shirika la huduma ya Wanyamapori nchini (KWS), hifadhi za taifa zimepokea zaidi ya watalii milioni 3.5 huu mwaka ikilinganishwa na milioni mbili mwaka jana. Hata hivyo asilimia 60 ya wageni hao ni watalii wa humu nchini. Mkurugenzi Mkuu wa KWS, Prof Erustus Kanga, alisema mapato ya shirika hilo pia imeongezeka kutoka Sh2.9 bilioni mwaka 2022 alipochukua mamlaka hadi Sh10.5 bilioni mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii na uhamasisho. Hata hivyo, wadau wa sekta ya utalii wanaonya kuwa gharama hiyo mpya ya bima ya afya kwa wageni itaathiri utalii.

read more