T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 23:55:10

2027: Siasa za ubabe zatikisa mrengo wa Linda Mwananchi na ule wa upinzani

HUKU upinzani ukiendelea kuonyesha wana umoja hadharani, mvutano mkali unaendelea kushuhudiwa kati ya mrengo wa Linda Mwananchi na Umoja wa Upinzani, kila upande ukipambana kudhibiti kampeni za kumng'oa madarakani Rais William Ruto. Migawanyiko hiyo ilijitokeza wazi Ijumaa baada ya aliyekuwa Naibu Rais ,Rigathi Gachagua, kumshambulia Gavana wa Murang'a, Irungu Kang'ata, kuhusu uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. "Nimesikia Kang'ata akisema anataka kuja Ol Kalou akiwa na Linda Mwananchi. Hatukuhitaji hapa. Kama unataka kupigia debe UDA, Jubilee au chama kingine chochote, uko huru kufanya hivyo, lakini kampeni za DCP ni suala la wenyeji," akasema Bw Gachagua. Kauli hiyo iliwafanya viongozi wa Linda Mwananchi kuhamisha mikutano yao Nyahururu na kusitisha mipango ya kumpigia kampeni mgombea wa DCP. Bw Kang'ata alijiunga na Linda Mwananchi mwezi uliopita wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika Thika. Matamshi ya Bw Gachagua dhidi ya Bw Kang'ata yamefichua mapambano makubwa zaidi ya kupigania ushawishi ndani ya upinzani. Duru kutoka upinzani zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wana hofu kwamba ajenda yao ya kisiasa inaweza kudhoofishwa na kundi la Linda Mwananchi ilhali wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali tangu 2022. Magharibi mwa Kenya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemkosoa Bw Sifuna akisema hana ushawishi wowote wa kisiasa. "Nataka kusema Sifuna hana kura Kakamega na Bungoma Didmus Barasa amemshinda kwa umaarufu. Eugene Wamalwa ndiye mwanasiasa maarufu zaidi ambaye ataleta kura kwa upinzani bila kujali atashikilia wadhifa gani," akasema Bw Salasya. "Wamejaa kiburi na wanataka kuleta mkanganyiko. Wania urais tuone utakakofika na jinsi itakavyomalizika," akaongeza Bw Salasya. Si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kupuuza ushawishi wa kisiasa wa Bw Sifuna na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya katika eneo hilo. Mrengo wa Sifuna na Natembeya umeitikisa kambi ya DAP-Kenya. Wawili hao sasa wanapanga mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma Julai 25 na 26. Bw Natembeya tayari ametangaza kuwa atatetea kiti chake kupitia chama kipya cha kisiasa badala ya DAP-Kenya kinachoongozwa na Bw Wamalwa. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Natembeya na Bw Wamalwa walitofautiana kuhusu uongozi wa DAP-Kenya, hali iliyomfanya gavana huyo kuanzisha vuguvu la Tawe. Wakati wa ziara ya upinzani Magharibi mwa Kenya mwezi uliopita, Bw Gachagua alimtangaza Bw Natembeya kuwa mratibu wa kampeni zake Magharibi. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, naye amewashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kujaribu kuelekeza shughuli za Linda Mwananchi huku wakimtumia Bw Sifuna kuendeleza maslahi yao binafsi. Alimtaja Bw Kang'ata kuwa mmoja wa viongozi wanaochochea migawanyiko ndani ya upinzani. "Linda Mwananchi haitatekwa nyara nikiwa macho. Hatutakuruhusu wewe (Kang'ata) kumtumia vibaya mwana wetu Edwin Sifuna," akasema Bw Amisi, ambaye amekuwa akiongoza kampeni za chama chake cha People Renaissance Movement (PRM) katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Seneta wa Kisii, Richard Onyonka ,anaamini kuwa hatimaye makundi hayo mawili yataungana chini ya muungano mmoja, akisema migawanyiko ya sasa inadhoofisha upinzani. Bw Onyoka amesisitiza kuwa pande zote mbili zinapaswa kuweka kando kiburi na kushirikiana. "Lazima tushirikiane kwa sababu ajenda ya Upinzani na Linda Mwananchi ni kuhakikisha utawala wa sasa unaondolewa madarakani mwaka ujao," akasema Bw Onyonka, ambaye yuko ndani ya Linda Mwananchi lakini anaunga mkono azma ya urais ya Dkt Matiang'i.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 22:55:41

Mbunge aliyehusishwa na uvamizi wa msafara wa Linda Mwananchi ajitokeza hadharani, adai hatatishwa

MBUNGE wa Nyaribari Chache, Zaheer Jhanda, Jumamosi alijitokeza hadharini wiki moja baada ya kuhusishwa na uvamizi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi eneo la Keumbu, Kaunti ya Kisii. Bw Jhanda jana alisema hakuna mtu ambaye atamtishia licha ya kuamrishwa afike mbele ya Idara ya Upelelezi Nchini (DCI). Uvamizi dhidi ya kambi ya Linda Mwananchi ulisababisha mauti ya mtu mmoja na kuwajeruhi wengine. Jumamosi, mbunge huyo alihutubia mamia ya wafuasi wake katika eneo la Keumbu. Alikuwa ameamrishwa afike mbele ya DCI kutokana na tukio hilo la Julai 3 ambapo kando na maafa ya mtu mmoja, wengine 20 walijeruhiwa. "Hapa inaitwa nini?" akauliza ambapo umati ulijibu "Keumbu" Umati aliouhutubia ulijumuisha vijana na akina mama huku akiongea kwa lugha ya Ekegusii. "Nchi lazima ijue kuwa kuna mbunge wa Nyaribari Chache ambaye yupo Keumbu, nyumbani na haogopi" Kujitokeza kwake kunajiri wakati ambapo kuna uchunguzi unaoendelea kutokana na uvamizi wa msafara wa Linda Mwananchi ambao uliongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Aliyekuwa Jaji Mkuu, David Maraga, ambaye alikuwa kwenye msafara wa Linda Mwananchi alinusurika bila kujeruhiwa ingawa gari lake liliharibiwa vibaya. Vincent Osiemo maarufu kama Mapinduzi aliaga dunia baada ya kupigwa na mawe na kuanguka kwenye mojawapo ya magari kisha akapigwa na umati. Upasuaji wa maiti ambao ulifanywa na Mwanapatholojia wa serikali, Dkt Peter Morebu, ulibaini kuwa marehemu aliaga dunia kutokana na majeraha ya kichwa ambayo yalisababishwa na kupigwa kwa kifaa butu. Maandalizi ya mazishi yamekuwa yakiendelea nyumbani kwao Gionseri, eneobunge la Bobasi huku akitarajia kuzikwa mnamo Julai 17. Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imetangaza kuwa imewanyaka washukiwa saba kuhusiana na ghasia hizo za Keumbu. Hata hivyo, washukiwa hao waliachiliwa huru baada ya kufikishwa kortini bila afisa wa uchunguzi au kiongozi wa mashtaka. Ingawa hivyo, polisi nao wanasisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na wote waliohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 12 Jul 2026 21:55:43

Uhuni na vurugu zatawala kampeni licha ya onyo la IEBC

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imewaonya wawaniaji dhidi ya kufadhili au kupanga ghasia kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. IEBC imesema kuwa wawaniaji wanaoshiriki tabia hizo watapigwa faini na pia uchaguzi utafutiliwa mbali kwenye maeneo yenye ghasia. Kwenye mahojiano na Taifa Leo Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume hiyo itahakikisha mwongozo wa uchaguzi unafuatwa kuhakikisha kuna uwazi na uwajibikaji.  "Hatuwezi kumruhusu mtu mmoja kuvuruga uchaguzi ambao unafadhiliwa na walipaushuru ili awe mbunge. Kama tume, tuna mamlaka ya kumpiga marufuku, kumtoza faini au hata kumzima mwaniaji ambaye amevunja sheria kushiriki uchaguzi," akasema Bw Ethekon.  Alisema IEBC haitakuvumilia uhuni wa kisiasa na haitajali mrengo ambao mwanasiasa anaegemea. Alisisitiza IEBC itachukua hatua kali kwa kutegemea ushahidi ambao utawasilishwa. "Kama tuna ushahidi kuwa kuna mtu anawatumia wahuni, kuwalipa au kuwafadhili, basi mtu huyo anahujumu uchaguzi wa amani na atatozwa faini au kuzuiwa kuwania," akasema. Bw Ethekon alisema pia IEBC haitakuwa na budi ila kufutilia mbali uchaguzi katika maeneo ambako kuna utovu wa usalama. Mwenyekiti huyo aliwataka wapigakura pia wanakili visa vya ghasia na aina yoyote ya uvunjaji wa sheria kisha wawasilishe ushahidi huo kwa IEBC. "Umma haufai kushutumu tume kuwa haina meno ya kungáta bali pia wanakili uhalifu na matukio mengine kisha wawasilishe malalamishi kwetu. Ni kwa kutegemea ushahidi huu ndipo tutachukua hatua," akasema. Alisisitiza kuwa kuandaliwa kwa uchaguzi huru kunahitaji ushirikiano kutoka kwa washikadau wote. Kauli, Bw Ethekon imekuja wakati ambapo kumekuwa na ghasia za kisiasa ikiwemo ya jana jijini Kisumu na hivi majuzi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi katika Kaunti ya Kisii. Jana ghasia ziliibuka jijini Kisumu wakati ambapo wahuni walijaribu kuwauzuia Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuhudhuria ibada katika Kanisa la St Stephen Cathdral. Wahuni hao walizuia wanasiasa hao wawili kuondoka na kuwalazimu polisi kutumia vitoza machozi kuwatimua. Ghasia hizo zilichipuka baada ya Bw Orengo kuwahutubia waumini. Ilibidi Mabw Orengo na Sifuna waondolewe kupitia mlango wa nyuma. Jana ilikuwa mara ya kwanza ambapo Bw Sifuna alijitokeza hadharani baada ya kubanduliwa kama katibu mkuu wa ODM. "Nawashukuru sana wale ambao wamesimama nami tangu wakati nikihudumu kama katibu mkuu wa ODM," akasema Bw Sifuna. Suala hilo pia linatarajiwa litachipuka sana wakati ambapo Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen atafika mbele ya Kamati ya Bunge baadaye mwezi huu. Akizungumza katika kikao cha faragha na wabunge mnamo Februari, Bw Murkomen alidai kuwa baadhi ya wanasiasa wanayafadhili makundi ya wahalifu wakijiandaa kwa uchaguzi. "Suala la magenge ya wahalifu limekuwa gumu kwa polisi kwa sababu wanaoyafadhili wameketi katika Bunge hili, wanashikilia nyadhifa za juu serikalini na wana ushawishi mkubwa ndani ya vyama vya kisiasa. Kila wanapokamatwa, viongozi wa kisiasa huwatisha maafisa wa polisi wanaoshughulikia kesi hizo," akasema Mbali na hayo, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja naye ameonya kuwa wahuni wa kisiasa na magenge ya uhalifu watakabiliwa vikali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Alisisitiza Huduma ya Kitaifa ya Polisi haitaruhusu ghasia kuvuruga kampeni wala kuhatarisha usalama wa wananchi. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) za Kaunti-ndogo ya Sotik katika Kaunti ya Bomet, Bw Kanja alisema watu wanaojihusisha na uhuni wa kisiasa, uhalifu uliopangwa na makosa mengine watafuatiliwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria. "Ninatoa onyo kwa wahuni na magenge ya uhalifu kote nchini kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na hawatapata nafasi ya kuendelea na shughuli zao," akasema Bw Kanja. Aliongeza kuwa kila mtu atawajibika binafsi kwa uhalifu wake na kuwaonya wanaojihusisha na ghasia za kisiasa kwamba watakabiliwa kibinafsi na matokeo ya vitendo vyao. Inspekta Jenerali huyo alisema maafisa polisi 10,000 walioajiriwa mwezi Machi mwaka jana kwa sasa wanapitia mafunzo katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo na watapelekwa katika maeneo mbalimbali nchini mara tu watakapohitimu ili kuimarisha juhudi za kuzuia uhalifu.

read more