T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 07 Oct 2026 03:55:52

Winnie Odinga na Kakake Raila Junior washindana kurithi baba yao kisiasa

SUALA la nani atakayevishwa urithi wa kisiasa wa marehemu Raila Odinga limeingia sura mpya baada ya bintiye Winnie Odinga kutawazwa kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake. Winnie, ambaye ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), alitawazwa Jumamosi katika hafla iliyohudhuriwa na mama yake Ida Odinga pamoja na wazee na washirika wa familia. Hata hivyo, kutokuwepo kwa kaka yake, Raila Odinga Junior, kulifanya tukio hilo kuzua maswali kuhusu mwelekeo wa familia kuelekea uchaguzi wa 2027. Raila Junior alisema hakujua kuhusu hafla hiyo na akasisitiza kuwa tayari anaendelea kujenga safari yake ya kisiasa. Siku hiyo hiyo, Raila Junior na Jaoko Oburu, mwanawe kiongozi wa ODM Oburu Oginga, walimtembelea Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya nyumbani kwake Mabole, Kakamega. Katika ziara hiyo, Oparanya aliunga mkono azma ya Raila Junior kuwania ubunge  Kibra na Jaoko kuwania kiti cha Bondo. Matukio hayo mawili yaliyofanyika siku moja yameonyesha jinsi familia hiyo inavyokabili suala nyeti la urithi wa kisiasa baada ya kifo cha kiongozi huyo. Winnie amekuwa akishinikizwa na baadhi ya wafuasi wa marehemu baba yake kuchukua nafasi ya mbele katika siasa kuelekea 2027. Kiti cha useneta Nairobi kimetajwa kuwa mojawapo ya nafasi anazoweza kuwania. Wafuasi hao wanamtaja Winnie kama mtu aliyekuwa karibu na kampeni za baba yake kwa miaka mingi na aliyeshiriki katika kazi za ubunifu, mawasiliano na matumizi ya teknolojia katika kampeni zake. Baada ya kutawazwa, Winnie alisema alikuwa amejitenga na siasa kwa muda ili kuomboleza kifo cha baba yake. "Watu wengi walikuwa wakiuliza nilikoenda lakini niliamua kuchukua muda kumuomboleza Jakom. Niliona askari wa Raila walivunjika moyo alipofariki na hawakutaka tena kupigana. Ndiyo maana nilikaa kimya kwa mwaka mmoja kuomboleza, lakini sasa muda huo umeisha na ni wakati wa kusonga mbele," alisema. Winnie pia alizungumzia umuhimu wa wazee katika masuala ya urithi, akisema madaraka hayapaswi kunyakuliwa kwa nguvu. "Cheo au nafasi si kitu cha kuchukuliwa kwa nguvu. Wazee wana jukumu la kuhifadhi na kulinda jamii, kwa hivyo lazima tuamue njia inayotufaa," alisema. Kwa upande wake, Raila Junior alisema analenga kujijengea jina kisiasa badala ya kutegemea jina la baba yake. "Ninazingatia kujenga taaluma yangu ya kisiasa kama Raila Junior, Raila Kembo. Nina matumaini nitafanikiwa. Sitategemea tu jina la Baba wala kupigana kuidhinishwa na mtu," alisema. Alisema pia alikuwa na shughuli nyingine siku hiyo na hakujua kuhusu hafla ya kutawazwa kwa dada yake. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Luo, Odungi Randa, alisema hakuwa kwenye hafla hiyo na angezungumza na wazee waliohudhuria kabla ya kutoa msimamo. Hata hivyo, mzee Jotham Ajiki, ambaye ni katibu wa baraza hilo, alisema hakuwa na sababu ya kuomba msamaha kwa sababu alialikwa nyumbani kwa Ida bila kujua yaliyokuwa yamepangwa. "Niliitwa na Mama Ida kwa hafla hiyo na nikaelekezwa nilichopaswa kufanya. Siwezi kuomba msamaha kwa kilichotokea kwa sababu nilikuwa mgeni wa Mama," alisema. Wakati huo huo baadhi wamemtaka Ida Odinga kutoa mwelekeo kuhusu nafasi ya familia ndani ya ODM. Bw,Jaramogi Ogana, alisema wanataka familia ikubaliane kuhusu mtu mmoja wa kuwakilisha urithi huo ili kuepusha migongano. "Tunataka mkubaliane mtoe mtu mmoja kwa sababu hatutaki mgongano na tutamuunga mkono," alisema.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 07 Oct 2026 02:55:19

Ebola ilivyoingia Kenya licha ya tahadhari mipakani

BAADA ya kuchukua tahadhari kwa miezi kadhaa,  Wizara ya Afya jana ilithibitisha kisa cha kwanza cha Ebola aina ya Bundibugyo nchini Kenya. Wizara ilisema mgonjwa huyo aliyekuwa raia wa Kenya alifariki Jumatatu usiku na hatua zimechukuliwa kwa kuzingatia taratibu za kiafya. Waziri wa Afya Aden Duale alisema Jumanne kuwa mwanamume huyo alikuwa ameishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa miaka saba, ambako aliugua takriban mwezi mmoja uliopita na kutibiwa katika hospitali kadhaa. Mgonjwa huyo alisafiri kwa barabara kutoka DRC hadi Kampala, Uganda, kabla ya kupanda ndege ya Jambojet 8523 kuelekea Nairobi. Alifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa saba mchana Jumamosi, Oktoba 3, na kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa afya katika kituo cha afya cha uwanja huo kabla ya kupitia taratibu za uhamiaji. Jamaa na rafiki walimchukua JKIA kwa gari aina ya Toyota Fielder na kumpeleka katika hospitali moja jijini Nairobi, ambako alitengwa haraka katika chumba maalum katika kitengo cha dharura kabla ya kuhamishiwa kituo cha kutengwa wagonjwa cha East Wing. Alifika hospitalini akiwa na homa, baridi, uchovu mwingi, udhaifu, maumivu ya misuli, maumivu wakati wa kumeza, maumivu ya koo na kutokwa na damu chini ya ngozi katika maeneo aliyodungwa sindano. Madaktari walishuku alikuwa na homa ya virusi inayosababisha kutokwa na damu kutokana na dalili na historia yake ya safari nchini DRC. Sampuli zake zilipimwa katika Maabara ya Kitaifa ya Virusi na maabara ya Kenya Medical Research Institute (KEMRI), na zote zikathibitisha kuwa alikuwa na Ebola aina ya Bundibugyo. Mgonjwa huyo alipatiwa matibabu ya kumsaidia, lakini alifariki. Mazishi yake yalipangwa kufanyika Jumanne kwa kuzingatia taratibu salama na zenye heshima za mazishi ya waathiriwa wa Ebola. Wizara imetambua watu 28 waliowasiliana na marehemu, wakiwemo jamaa na wahudumu wa afya waliomhudumia. Duale alisema pia abiria 23 na wahudumu wanne waliokuwa katika ndege moja na marehemu wanafuatiliwa huku mipango ya kuwaweka walio katika hatari karantini ikiendelea. "Kenya imekuwa katika hali ya tahadhari ya juu tangu mlipuko huu ulipoanza Mei 2026," alisema Duale. Kufikia Jumanne, Wizara ilikuwa imewapima wasafiri 652,584 na kuchunguza sampuli 267 katika maabara tano. Aidha, wahudumu 4,971 wa afya katika ngazi ya kitaifa na kaunti wamefunzwa kuhusu kinga na udhibiti wa Ebola. "Ni kipimo kimoja pekee ambacho kimepatikana kuwa cha Ebola," taarifa ya Wizara ilisema. Duale aliwataka Wakenya kutokuwa na hofu, akisema mifumo yote ipo tayari kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Aliwashauri wananchi kunawa mikono mara kwa mara, kutumia dawa za kusafisha mikono na kuepuka mawasiliano ya karibu na wagonjwa wanaotoka katika nchi zilizo na maambukizi. Wananchi wenye dalili wanashauriwa kutafuta matibabu katika vituo vya afya vinavyotambuliwa na kutoa taarifa kuhusu wagonjwa wanaowajua. Wizara pia imewaagiza wahudumu wa afya kuzingatia viwango vya juu vya kuzuia na kudhibiti maambukizi. Wananchi wanaweza kupata taarifa kupitia majukwaa rasmi ya Wizara au kupiga simu ya bila malipo 719.

read more