T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 05 Oct 2026 05:55:23

Mafuko wanaotishia umoja wa viongozi wa upinzani

SIASA za vibaraka wanaodaiwa kupenyezwa na serikali zimezua hofu na kutoaminiana katika upinzani na kutishia umoja wao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Viongozi wa upinzani sasa wana hofu kuwa serikali inaweza kupenyeza watu wake ndani ya vyama vya upinzani ili kuvuja mikakati, kuchochea migawanyiko na kuunga mkono wagombeaji wengi wa urais, kwa lengo la kumsaidia Rais William Ruto kushinda muhula wa pili. Kiongozi wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua tayari amedai mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani yuko mbioni kujiunga na Rais Ruto. "Ninataka kutoa unabii leo, si kwa sababu mimi ni nabii bali kutokana na uzoefu, kuona mbali na kuelewa siasa za Kenya. Mgombeaji mmoja wa urais atatangazwa; mtu mmoja ataondoka. Mtu huyo ataondoka mwenyewe," akasema Bw Gachagua. Akiwahutubia viongozi wa kidini jijini Boston, Amerika, aliyekuwa Naibu Rais pia alidai kuwa kuna mpango wa kupenyeza fuko katika upinzani ili kuzuia juhudi za kuunda muungano mmoja. Ingawa hakumtaja yeyote, chama cha Wiper Patriotic Front cha Kalonzo Musyoka kililazimika kukanusha madai ya mazungumzo ya siri na serikali ya Kenya Kwanza. Bw Musyoka aliripotiwa kukutana kwa siri na mwanasiasa mkongwe Johnson Muthama, mshirika wa karibu wa Rais Ruto. Mwenyekiti wa kitaifa wa Wiper Jamlek Kamau alithibitisha mkutano huo lakini akasema haukuwa wa kumshawishi Bw Musyoka kujiunga na serikali. "Ndiye nilianzisha mazungumzo na Johnstone Muthama. Hakuna wakati amekutana na kiongozi wetu wa chama kumshawishi kujiunga na serikali," akasema Bw Kamau. Baadaye Bw Musyoka aliwaonya wanasiasa wa upinzani dhidi ya kuwa fuko wa Rais Ruto. "Ikiwa mmoja wetu atakuwa fuko wa Kasongo, atapata madhara kama ya Loti wa Biblia," akasema. Tuhuma kama hizo pia zimekumba vuguvugu la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale wamekuwa na vyama vyao, huku Gavana wa Siaya James Orengo akisema anapanga kusajili chama kipya. Bw Natembeya na Bw Amisi wamekuwa wakivamiana kuhusu kuvuruga azma ya Bw Sifuna ya kuwania urais. Bw Amisi, kiongozi wa People's Renaissance Movement, amesema chama chake kiliundwa kuimarisha Linda Mwananchi lakini baadaye kikaitwa fuko. "Huwa na wasiwasi kwamba baadhi ya walio karibu naye wanataka jina lake zaidi kuliko wanavyomtakia mema. Tazama vyama vya kisiasa vilivyoibuka tangu wakati huo," akasema. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema kushukiwa huko kunatumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa maslahi ya binafsi. "Ni wale walio katika upinzani wanaoitana fuko. Hii haisaidii kuendeleza ajenda ya upinzani bali maslahi binafsi kwa kumchafua mwengine," akasema. Mbunge wa Gatanga Edward Muriu, hata hivyo, alidai serikali ya Rais Ruto inatumia mbinu hizi kudhoofisha upinzani baada ya kupoteza uungwaji mkono katika Mlima Kenya. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa David Monda alisema kutoaminiana katika upinzani kutaongezeka kadri uchaguzi unavyokaribia. "Kwa hakika upinzani iko mbali kuwa na umoja. Ni ndoa ya manufaa kati ya wanasiasa wanaopinga serikali lakini wamefungwa na kutoaminiana na sintofahamu," akasema. Aliongeza kuwa uwezo wa Rais Ruto kama kiongozi aliye mamlakani unampa nafasi nzuri ya kutumia migawanyiko ya upinzani kwa manufaa yake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 05 Oct 2026 04:55:51

Mwanabodaboda asimulia jinsi alivyotumia katika mauaji ya Mbobu bila kujua

MWENDESHAJI wa bodaboda ambaye jina lake limefichwa, Paul*, amewaambia wachunguzi wa mauaji jinsi alivyohusika bila kujua katika tukio la kuuawa kwa wakili Kyalo Mbobu mnamo Septemba 9, 2025. Paul (Si jina lake kamili) amerekodi taarifa tatu kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), akisema alikuwa rafiki wa afisa polisi Julius Cheruiyot ambaye alimwajiri kumpeleka sehemu mbalimbali kwa malipo ya Sh3,000. Kulingana na taarifa yake, Cheruiyot alipanga mkutano na Paul na polisi mwengine katika mkahawa wa Pangani, Nairobi, asubuhi ya Septemba 10, 2025. Polisi huyo aliyetajwa kama "Afande Sang" anaaminika kuwa Inspekta Kenneth Kipkemoi Sang, ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya Mbobu na mtafiti Victoria Mutiso. Paul alisema baadaye alimchukua Cheruiyot na kuelekea Langata Road kabla ya kusimama karibu na Galleria Mall. Baada ya saa 11.30 jioni, Cheruiyot alidaiwa kumwelekeza aingie Magadi Road. Takriban mita 50 kutoka eneo ambako Mbobu alipigwa risasi, Cheruiyot alidaiwa kumwambia asimame huku injini ya pikipiki ikiendelea kuwaka. Paul alisema hakumwona Mbobu akipigwa risasi lakini alisikia milio ya risasi kadhaa. Cheruiyot alikimbia hadi kwa pikipiki akihema na kumwamuru aondoke kwa kasi. Walirejea Pangani baada ya saa 12 jioni, ambapo Cheruiyot alidaiwa kumpa Paul salio la Sh2,000 na kumwonya asizungumzie yaliyotokea. Paul alisema alihofia kukamatwa na akabadilisha laini ya simu na kuhamia South B. Cheruiyot na Paul walikamatwa jijini Nairobi Septemba 24. Pikipiki iliyodaiwa kutumiwa katika tukio hilo pia ilipatikana. Wachunguzi wanamtuhumu Sang kuhusika katika mauaji hayo pamoja na ya Mutiso. Anaaminika kukimbilia Tanzania. Wachunguzi pia wanadai mauaji hayo yalihusishwa na mzozo wa shamba la ekari 21 Mlolongo, Kaunti ya Machakos

read more