T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Wed, 08 Jul 2026 00:55:03

Zamzam, Masito kibarua kura za 2027 watangulizi wao wote wakiwa wantam

MBUNGE Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohamed na mwenzake wa Kwale Bi Fatuma Masito, wanakabiliwa na ushindani mkubwa kuelekea 2027 wakijaribu kuvunja mtindo wa jinsi wote waliowatangulia walivyohudumu kwa muhula mmoja pekee. Tangu uchaguzi wa kwanza wa mwaka 2013 chini ya Katiba iliyoleta ugatuzi, wapigakura wamekuwa wakichagua viongozi wapya kila baada ya miaka mitano. Katika kaunti ya Mombasa, Bi Asha Hussein ambaye alikuwa wa kwanza kushinda nafasi hiyo mwaka wa 2013 kupitia chama cha ODM, amekuwa akijitahidi kurudi mamlakani bila mafanikio. Alitumikia muhula mmoja kabla ya kushindwa na Bi Mishi Mboko mwaka wa 2017. Kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Bi Mboko aliamua kuwania ubunge Likoni na kufanikiwa. Hatua hii ilimpa nafasi Bi Mohamed kurithi kiti hicho. Katika Kaunti ya Kwale, marehemu Zainab Chidzuga alikuwa wa kwanza kushinda wadhifa huo 2013 lakini akashindwa na Bi Zuleikha Hassan mwaka 2017. Naye Bi Hassan alipoteza kiti hicho kwa Bi Masito wa ODM katika uchaguzi wa 2022. Bi Mohamed na mwenzake wa Kwale, Bi Masito, ambao wote ni wanachama wa ODM wameanza kuweka mikakati ya kubadili desturi katika kaunti zao. Bi Mohamed asema hana wasiwasi kuhusu uchaguzi ujao, akisisitiza kuwa kazi aliyoifanya ndiyo itakayomrudisha mamlakani. Alisema ataendelea kuwahudumia wakazi wa Mombasa na kwamba yuko tayari kugombea akiwa ndani au nje ya ODM, akidai kwamba kuna njama ya kumnyima tikiti ya chama. Aidha, ametangaza nia ya kuwania ugavana wa Mombasa baada ya kukamilisha kipindi cha miaka 10 kama Mbunge Mwakilishi wa Kike. Anakabiliwa na ushindani kutoka kwa kwa diwani wa wadi ya Kadzandani, Bi Fatma Kushe, mwanasiasa wa UDA, Bi Fatma Barayan, na mwanasiasa Amina Abdalla, huku wagombea wengine wakitarajiwa kujitokeza ifikapo hapo mwakani. Kwa upande mwingine, Bi Masito, ambaye amekuwa akiendeleza ziara za kiamendeleo mashinani, anatarajia pia kurejea mamlakani kwa msingi wa utendakazi wake. "Mimi watu wa Kwale nimewatembelea sana. Tushakubaliana na viongozi kwamba siasa hapa kwetu Kwale ni ODM," akasema, katika mkutano wa kuchangisha fedha za kuwezesha kina mama eneo la Matuga hivi majuzi. Wachanganuzi wa siasa wanasema mtindo wa wabunge wawakilishi wa kike kuhudumu kwa muhula mmoja pekee ni mzuri na unafaa kuigwa nchini, kwani wadhifa huo ulinuiwa kuwapa wanawake uzoefu wa kisiasa. "Hii nafasi ilitengewa wanawake ili waweze kuingia siasani, kupata tajriba au uzoefu, umaarufu, marafiki na fedha za kuwasaidia kugombea viti vingine vya kisiasa. Mwanamke hafai kusalia katika mamlaka hayo kwa zaidi ya miaka mitano. "Maliza miaka mitano upishe wanawake wengine ili tuweze kuhakikisha kuna wanawake wengi kwenye siasa," asema Bi Grace Oloo, mchanganuzi wa siasa. Bi Oloo pia aliwasihi wanawake kuwashikilia wenzao mikono ili kuwawezesha kisiasa.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 07 Jul 2026 23:55:33

Mapambano bado, wasema mashujaa wa Saba Saba

MIAKA 36 baada ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba ya Julai 7, 1990, baadhi ya viongozi walioongoza mapambano ya kurejesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa wanasema safari ya kupigania utawala bora bado haijakamilika. Viongozi hao walikumbuka jinsi walivyokabiliana na ukandamizaji wa utawala wa aliyekuwa Rais Daniel arap Moi, huku wakisema hali iliyoshuhudiwa Jumanne ya kufungwa kwa barabara na kumwagwa kwa polisi wengi mijini iliwakumbusha matukio ya miaka hiyo. Katika Saba Saba ya kwanza, serikali ya Moi ilizuia mkutano uliokuwa umeitishwa katika Uwanja wa Kamukunji, Nairobi na viongozi Kenneth Matiba na Charles Rubia. Kabla ya mkutano huo, Matiba, Rubia na Raila Odinga walikamatwa na kuzuiliwa, lakini wanaharakati waliendelea na maandamano licha ya msako mkali wa vitengo vya usalama. Shinikizo lililotokana na maandamano hayo lilichangia kufutwa kwa Kifungu cha 2A cha Katiba mwaka wa 1991 na kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano haya walikuwa Odinga, James Orengo, Paul Muite, Gitobu Imanyara, Kiraitu Murungi, Njeru Kathangu, Mukhisa Kituyi, Martin Shikuku na Masinde Muliro, pamoja na viongozi wa kidini akiwemo Askofu Ndingi Mwana a'Nzeki, Mchungaji Timothy Njoya, Askofu David Gitari, Henry Okullu na Alexander Muge. Gavana wa Siaya, Orengo, ambaye alijiunga na maadhimisho ya Saba Saba jijini Nairobi jana, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa taifa hili bado halijatenga siku rasmi ya kuwaenzi mashujaa wa mapambano ya ukombozi wa pili. "Kama ningekuwa rais chini ya Katiba hii mpya, ningetangaza Saba Saba kuwa siku ya kitaifa ya kuwaenzi watu kama Kenneth Matiba, Charles Rubia na Raila Odinga," alisema. Aliyekuwa mbunge wa Runyenjes, Kathangu, alisema kurejeshwa kwa vyama vingi hakukuleta mageuzi yote yaliyotarajiwa kwa sababu wengi wa wanaharakati walikuwa gerezani wakati vyama vipya viliposajiliwa. "Tulitarajia Wakenya wapate viongozi wapya, lakini wengi wetu tulikuwa kizuizini. Vijana wa Gen Z wanapaswa kuendelea kupigania utawala bora kama tulivyofanya mwaka wa 1990," alisema. Kwa upande wake, wakili Muite alisema mapambano ya Saba Saba yalizaa matunda makubwa, ikiwemo Katiba ya mwaka wa 2010 ambayo imeimarisha haki na uhuru wa wananchi. Alisema Wakenya, hasa vijana wa Gen-Z, wameonyesha ujasiri mkubwa wa kuwawajibisha viongozi na kusisitiza kuwa ukiukaji wa haki za binadamu lazima uwajibishwe watu. Hata hivyo, kiongozi wa ODM, Oburu Oginga alisema Saba Saba haipaswi kuwa siku ya maandamano ya barabarani bali ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Naye Seneta wa Kitui, Enoch Wambua alisema Saba Saba inaendelea kuwa ukumbusho wa mapambano ya demokrasia na utawala bora, akiongeza kuwa vijana wa sasa wamechukua nafasi ya kizazi kilichopigania mageuzi miaka ya 1990 katika kudai uongozi wajibifu.

read more