T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:34:43

Viongozi watuzwa kwa uongozi bora

AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC) ni miongoni mwa viongozi wa kampuni na mashirika ya umma na ya kibinafsi waliotambuliwa kwa uongozi bora na mchango wao katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Dkt Rose Mkalama alituzwa Afisa Mkuu Mtendaji bora wa mwaka wakati wa makala ya pili ya East Africa Leadership Awards, kwa uongozi wake katika kupanua upatikanaji wa umeme nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity. Chini ya juhudi za kitaifa za kusambaza umeme, kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini Kenya kimeongezeka hadi zaidi ya asilimia 76, kutoka karibu asilimia 27 mwaka 2013. Kulingana na Dkt Mkalama, tuzo hiyo si mafanikio yake binafsi pekee, bali ni utambuzi wa kazi inayofanywa na REREC kuhakikisha umeme unawafikia maelfu ya Wakenya katika maeneo ya vijijini na mashambani. "Nina furaha kuwa REREC imeweza kufikia maelfu ya Wakenya katika karibu kila kijiji nchini kupitia Mpango wa Last Mile Connectivity," alisema. REREC ilipoanzishwa, kiwango cha kuunganishwa kwa umeme nchini kilikuwa takriban asilimia 8. Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa shirika hilo alisema ongezeko hilo limechangiwa na ufadhili wa serikali, ushirikiano na wabunge pamoja na utekelezaji endelevu wa miradi ya usambazaji umeme katika maeneobunge yote 290 nchini. [caption id="attachment_192455" align="aligncenter" width="300"] Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Maeneo ya Mashambani (REREC), Dkt Rose Mkalama akizungumza awali. Picha|Hisani[/caption] Anasema manufaa ya umeme yameendelea kuyapa maboma mwangaza, ikizingatiwa yamesaidia kufanikisha elimu, afya, kilimo na biashara, na hivyo kuwezesha jamii kushiriki zaidi katika maendeleo ya kiuchumi. "Kwa sasa, tunatekeleza miradi inayolenga kuunganisha taasisi za umma na jamii kwenye huduma za umeme, huku mipango ya usambazaji umeme kupitia gridi ikilenga kufikia mamia ya maelfu ya wateja," Dkt Mkalama akadokeza. Viongozi wengine waliotuzwa ni pamoja na Dkt Lilian Nyawada, Kamishna wa Forodha na Udhibiti wa Mipaka katika Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), na Dkt David Okeyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Nutrition and Dieticians Institute. Kabla ya kutawazwa viongozi bora, huduma za mashirika na kampuni zao zilipigwa msasa na jopo la majaji mashuhuri kutoka World Human Resource Congress, wasimamizi wa huduma za wafanyakazi kutoka India na viongozi tajika wa kijamii. Akizungumza wakati wa kuwatuza, Mkuu wa Kitengo cha Bionuwai, Ujumuishaji na Haki za Watu wenye Mahitaji Maalum (Head of the Office of Diversity, Inclusion and Disability Rights in the Executive Office of the President) katika Afisi ya Rais, Isaac Mwaura, aliwataka viongozi wa taasisi za umma na kibinafsi kuhamasisha wafanyakazi wao kujitahidi kutoa huduma bora. "Uongozi haupaswi kupimwa kwa cheo pekee, bali pia kwa urithi ambao viongozi wanaacha katika taasisi na jamii," Mwaura akasema. Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya Prof Bindu Madhavi, pia alitambuliwa kwa tuzo ya Profesa mwenye ushawishi mkubwa kutokana na mchango wake katika elimu, utafiti, kunoa wanafunzi makali na masuala ya dawa na sayansi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:55:51

Maoni mseto Rais akimpa mzee wa Waluo gari ya mamilioni kama zawadi

ZAWADI ya gari jipya aina ya Toyota Prado TX lililotolewa na Rais William Ruto kwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Luo, Ker Odungi Randa, imeibua mjadala mkali wa kisiasa katika eneo la Nyanza. Gari hilo la thamani ya mamilioni lilifikishwa nyumbani kwa Bw Randa katika eneo la Boya na maafisa kutoka afisi ya Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, siku chache baada ya kiongozi huyo wa kitamaduni kumuomba Rais msaada wa usafiri wakati wa ziara yake katika eneo hilo. Kwa mujibu wa taarifa, ombi hilo lilitolewa wakati wa mkutano uliofanyika Homa Bay, ambapo Rais aliahidi kulitekeleza. Afisa kutoka afisi ya Dkt Omollo, Bw Charles Osako, alisema Rais alitimiza ahadi yake kwa Baraza la Wazee wa Luo na kwamba gari hilo litasaidia shughuli na majukumu ya wazee hao. "Gari hili linaonyesha kutambuliwa kwa mchango muhimu wa wazee na viongozi wa kitamaduni katika kuhifadhi maadili, mila na utambulisho wetu," alisema Bw Osako. Mbunge wa Lang'ata, Phelix Jalango Odiwuor, ambaye alishuhudia mazungumzo hayo, alisema baada ya mkutano wa mwisho wa hadhara Migori, Dkt Omollo alimwalika kuhudhuria kikao kati ya Rais na viongozi wa Baraza la Wazee wa Luo. Alisema mwishoni mwa mkutano huo, Bw Randa alimuomba Rais amsaidie kupata gari la kurahisisha shughuli zake za kila siku. "Kwa utulivu, Rais alimwambia angepata gari Ijumaa. Leo asubuhi timu ya Dkt Omollo imekabidhi gari hilo jipya aina ya Toyota Prado," alisema Bw Odiwuor baada ya gari kuwasilishwa. Bw Randa alipokea funguo za gari hilo na kulijaribu kabla ya kurejea nyumbani kwake. "Nashukuru Rais Ruto kwa zawadi hii. Itanisaidia kusafiri na kukutana na Waluo walioko Nairobi, Mombasa, Uganda, Tanzania na maeneo mengine mengi," alisema. Hata hivyo, zawadi hiyo imezua maswali kuhusu uhuru wa Baraza la Wazee wa Luo, ambalo kwa kawaida halifai kuzingatia siasa za vyama na linatarajiwa kuwa sauti ya maridhiano katika jamii. Wakosoaji wanasema kupokea gari kutoka kwa Rais kunaweza kuathiri msimamo wa baraza hilo, hasa wakati ushindani wa kisiasa kati ya vyama vya UDA na ODM unaendelea kushika kasi Nyanza. Mkazi wa Kisumu, Bw Martin Oria, alihoji jinsi baraza hilo litakavyodumisha kutopendelea upande wowote wakati litakapohitajika kutatua mizozo ya kisiasa. Lakini wengine wametetea zawadi hiyo, wakisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakiwasaidia wazee wa jamii kwa miaka mingi. Kwa mujibu wa David Dimba Jakobuya, Bw Randa ni mmoja wa wazee wachache waliosalia ambao walishiriki katika harakati za ukombozi wa kwanza na wa pili nchini Kenya. Alisema amekuwa akikabiliwa na changamoto za usafiri tangu gari lake la awali lilipoibwa miaka kadhaa iliyopita. Akijibu ukosoaji huo, Bw Randa alisema wale wanaopinga zawadi hiyo hawakuwahi kujitokeza alipokuwa akikosa usafiri.  "Sikusikia mtu yeyote akilalamika kwa niaba yangu wakati sikuwa na gari. Sasa nimepewa gari, kila mtu ana maoni. Marais wengine pia wamekuwa wakitoa zawadi kwa watu wengi nchini," alisema. Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wamehoji iwapo gari hilo ni mali ya Bw Randa binafsi au ya Baraza la Wazee wa Luo. Hata hivyo, kiongozi huyo amesisitiza kuwa ni zawadi ya kibinafsi aliyopewa na Rais kufuatia ombi lake. Mjadala huo umechukua sura ya kisiasa zaidi baada ya Bw Randa kutoa wito kwa jamii ya Waluo kumuunga mkono Rais Ruto katika azma yake ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 08:57:46

Karua ashtaki Uganda kwa kumtimua asiwakilishe Besigye

Kiongozi wa Chama cha People's Liberation Party (PLP) na aliyekuwa Waziri wa Haki nchini Kenya, Martha Karua, amewasilisha kesi katika mahakama ya Uganda akitaka kubatilishwa kwa uamuzi wa kufurushwa kwake nchini humo na kuruhusiwa kurejea ili kumwakilisha kiongozi wa upinzani, Dkt Kizza Besigye, na mshtakiwa mwenzake. Besigye aliyekamatwa akiwa Nairobi Nairobi mwaka 2024 anakabiliwa na kesi ya uhaini. Bi Karua, kwa ushirikiano na Chama cha Wanasheria cha Uganda (Uganda Law Society), wanapinga uamuzi uliotolewa Juni 22 na Afisa Mkuu wa Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe wa kumzuia kuingia nchini Uganda na kutangaza kuwa  mtu asiyehitajika nchini humo. Wanasema uamuzi huo ulikuwa kinyume cha sheria na ulifanywa bila kumpa nafasi ya kujitetea au kusikilizwa. Kupitia Kitengo cha Malalamishi cha Mahakama Kuu mjini Kampala, Karua anataka mahakama ibatilishe uamuzi huo na kuzuia maafisa wa uhamiaji kuingilia haki yake ya kuingia Uganda ili kutekeleza majukumu yake ya kitaaluma kama wakili. Katika hati zake za kesi, Karua anaeleza kuwa alisafiri kwenda Uganda Juni 22 ili kuwakilisha Dkt Besigye na Hajj Obeid Lutale baada ya kupata Cheti Maalum cha Uwakili kilichomruhusu kufanya kazi katika mahakama za Uganda. Anasema maafisa wa uhamiaji walimzuia kuingia nchini humo, wakachukua simu zake na baadaye wakampatia notisi ya kumtaka arejee Kenya. Dkt Besigye na Bw Lutale walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini na makosa mawili ya kuficha taarifa kuhusu uhaini. Upande wa mashtaka unadai walihusika katika njama za kupindua serikali ya Uganda. Mashtaka hayo yalitokana na kukamatwa kwa wawili hao jijini Nairobi mnamo Novemba 2024. Awali walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kijeshi ya Uganda kabla ya kuhamishiwa mahakama za kiraia kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu uliosema kuwa raia hawawezi kushtakiwa katika mahakama za kijeshi. Baadaye walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu ya Nakawa mnamo Februari 21, 2025. Hatua ya Karua kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Uganda kutokana na vitendo vya maafisa wa uhamiaji imefuatia ombi la awali lililowasilishwa na Dkt Besigye na Bw Lutale kuhusu suala hilo hilo. Mahakama Kuu ilikataa kuamua iwapo uamuzi wa uhamiaji ulikuwa halali, ikisema kuwa changamoto hiyo ilipaswa kuwasilishwa kupitia mchakato wa mapitio ya mahakama, na hivyo ikatupilia mbali ombi hilo. Karua na Chama cha Wanasheria cha Uganda wanataka mahakama itangaze kuwa uamuzi huo ulikuwa haramu, wa kiholela, usio na sababu za msingi na uliofanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa kisheria. Pia wanataka mahakama iubatilishe, kuagiza mamlaka za uhamiaji kutathmini upya suala hilo, na kutoa amri ya kudumu ya kutomzuia kuingia Uganda kwa madhumuni ya kitaaluma. "Uamuzi huo ni haramu, hauna mantiki na ulifanywa kinyume cha taratibu zinazotakiwa na sheria," walisema. Katika kiapo chake cha kuunga mkono kesi hiyo, makamu wa rais wa Chama cha Wanasheria cha Uganda, Anthony Asiimwe, alisema Karua ni Wakili Mkuu na anamiliki Cheti Maalum cha Uwakili kilichotolewa chini ya Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mawakili. Alisema cheti hicho kilimruhusu kuongoza timu ya utetezi katika kesi  inayowahusu Besigye na Lutale. Asiimwe alieleza kuwa alisafiri hadi Entebbe kumpokea Karua baada ya kuwasili kutoka Kenya, lakini akakuta maafisa wa uhamiaji tayari wamemzuia kuingia nchini. Walalamishi hao wanasisitiza kwamba Karua hakupatiwa nafasi ya kusikilizwa wala sababu zinazokidhi kanuni za haki za asili kabla ya uamuzi huo kufanywa. Wanasema hatua hiyo ilikiuka Katiba ya Uganda, Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na misingi inayolinda uhuru wa taaluma ya sheria. Kwa mujibu wao, Karua amepata hasara kitaaluma na kifedha kwa sababu hawezi kurejea Uganda kutekeleza majukumu yake. "Mlalamishi wa pili ameendelea kupata madhara makubwa ya kitaaluma na jina lake kuharibiwa baada ya kutangazwa hadharani kuwa ' mtu asiyetakiwa' bila msingi wowote wa kisheria," alisema Asiimwe. Kabla ya kuwasilisha kesi hiyo, Chama cha Wanasheria cha Uganda kilijaribu kutafuta suluhu kupitia njia za kiutawala. Barua zilizoambatishwa katika kesi zinaonyesha kuwa chama hicho kiliwaomba maafisa wa Uganda kufuta uamuzi huo na kumruhusu Karua kuingia nchini. Hadi sasa, Mwanasheria Mkuu wa Uganda hajawasilisha majibu kuhusu madai yaliyomo katika kesi hiyo mpya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 25 Sep 2026 07:55:37

Shughuli zakwama Mombasa mihadarati ya thamani ya Sh8.2 bilioni ikiteketezwa

SHUGHULI za kawaida zilisitishwa kwa muda Mombasa Alhamisi asubuhi wakati msafara wenye ulinzi mkali ulipokuwa ukielekea katika kiwanda cha simiti cha Bamburi kutoka kambi ya jeshi la wanamaji iliyo Mtongwe. Msafara huo uliojumuisha walinzi wa usalama wenye silaha ulikuwa ukienda kwa shughuli ya kuteketeza dawa za kulevya aina ya methamphetamine zilizokadiriwa kuwa za Sh8.2 bilioni. Operesheni hiyo ilihusisha maafisa kutoka Jeshi la Wanamaji, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Idara ya Huduma ya Polisi, Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Tanuri za Bamburi Cement zimeidhinishwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) kwa ajili ya uharibifu salama na uchakataji wa taka hatari na zisizo hatari. Kupitia Geocycle Kenya, kiwanda hicho pia hutumia taka zinazochomwa kama chanzo mbadala cha nishati ya joto katika uzalishaji wa simiti. Dawa hizo haramu kwanza zilipimwa uzani na kuthibitishwa kuwa zile halisi zilizokamatwa, kabla ya mahakama kutoa amri ya mwisho kuruhusu mchakato uliofuata.  Hakimu Mkuu Anthony Mwicigi alisimamia shughuli hiyo na kuamrisha kwamba dawa hizo ziharibiwe, baada ya mahakama kuridhika kwamba zilikuwa zile zile ambazo zilipatikana kwa washukiwa. Washukiwa hao ambao ni raia wa Iran ni Jaseem Darzadeh Nia, Nadeem Jadgal, Hassan Baloch, Raheem Baksh, Imran Baloch na Imtiyaz Daryay. Wanadaiwa kusafirisha kilo 1,036.044 za methamphetamine zenye thamani ya takriban Sh8.2 bilioni, na kesi yao bado inaendelea katika Mahakama ya Shanzu. Upande wa mashtaka unadai kuwa dawa hizo zilisafirishwa ndani ya meli MV Mashaallah, ambayo inadaiwa haikusajiliwa na haikuwa na uraia wa nchi yoyote. Meli hiyo ilikamatwa katika bahari kuu, huku kosa linalodaiwa kutendeka kati ya Oktoba 17 na 20, 2025. Washukiwa hao sasa wataanza kuwasilisha utetezi wao mmoja baada ya mwingine huku kesi hiyo ikiendelea. Tanuri ya Bamburi Cement imewahi kutumiwa kwa shughuli kama hiyo awali. Katika mwaka wa 2025, mihadarati aina ya heroin na kokeni za Sh400 milioni ziliharibiwa hapo baada ya washukiwa kupatikana na hatia au kupoteza maisha kwa njia zisizoeleweka. Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alisema shughuli hiyo ya Alhamisi ilithibitisha nia ya serikali kukatiza mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya kimataifa.  "Leo tunatuma ujumbe sio tu kwa watumizi bali pia walanguzi wakubwa wa mihadarati. Tumeweka wazi kwamba serikali itatwaa mali za walanguzi wote na kuzitumia kurekebisha tabia za waraibu na shughuli nyingine za kukabiliana na biashara hiyo haramu," akasema. Shughuli nzima ilifanywa kwa utaratibu na kushirikisha pande zote husika za kesi, ili kuepusha changamoto kama zile zilizoibuka baada ya serikali kulipua meli iliyodaiwa kuwa na mihadarati baharini mwaka wa 2014 chini ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta. Hatua hiyo ilizua utata na kutatiza kesi iliyokua ikiendelea, hadi baadhi ya washukiwa wakaachiliwa huru mwaka wa 2025 wakati mahakama ilipoamua kulikuwa na udhaifu wa kisheria, ikiwemo uharibifu wa meli husika kabla ushahidi muhimu kukusanywa.

read more