T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 03:55:01

Chaguzi ndogo nchini zinavyotabiri jinsi mambo yatakuwa 2027

CHAGUZI ndogo zimekuwa zikitumika kama kipimo cha hali ya kisiasa nchini, zikitoa ishara kuhusu mabadiliko ya msimamo wa wapigakura na nguvu za vyama kabla ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou uliofanyika Alhamisi haukuwa tofauti na zingine wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na ule wa sasa wa Rais William Ruto. Ingawa chaguzi hizo huathiriwa na masuala ya eneo husika, mara nyingi huonyesha mabadiliko ya nguvu za kisiasa, maoni ya wananchi na miungano inayoibuka. Kwa miaka mingi, chaguzi ndogo zimegubikwa na mvutano wa kisiasa, madai ya matumizi ya idara za serikali, kuhonga wapiga kura na fujo kutokana na uzito wa matokeo yake. Uchambuzi wa chaguzi ndogo tangu mwaka 2017 unaonyesha kuwa mara nyingi zimekuwa zikitabiri mwelekeo wa uchaguzi mkuu kwa kupima umaarufu wa vyama, hisia za wapigakura na mabadiliko ya miungano ya kisiasa. Katika uchaguzi wa Ol Kalou, mgombea wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Sammy Kamau Ngotho, alishinda kwa kura 35,440. Mgombea wa United Democratic Alliance (UDA), Samuel Muchina Nyaga, alipata kura 5,450. Baada ya ushindi huo, DCP ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ilisema matokeo hayo yanathibitisha kuwa chama hicho sasa ndicho chenye nguvu zaidi katika eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Kabla ya uchaguzi wa 2022, UDA ilitumia ushindi katika chaguzi ndogo kujijenga kisiasa katika Mlima Kenya baada ya uhusiano kati ya Dkt Ruto na aliyekuwa Rais Kenyatta kuzorota. Chama hicho kilipata ushindi wake wa kwanza katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Rurii, iliyoko ndani ya eneo la Ol Kalou. Katika uchaguzi wa Mei 18, 2021, Francis Muraya wa UDA alipata kura 4,178 dhidi ya Peter Thinji wa Jubilee aliyepata 3,051. UDA pia ilishinda uchaguzi mdogo wa Kiambaa uliofanyika Julai 15, 2021, ambapo Njuguna Wanjiku alimshinda Kariri Njama wa Jubilee. Katika Juja, Dkt Ruto alimuunga mkono George Koimburi aliyegombea kwa tiketi ya People's Empowerment Party. Koimburi alipata kura 12,159, huku mgombea wa Jubilee Susan Njeri akipata 5,764. Baadaye, uchaguzi mkuu wa 2022 ulithibitisha mwelekeo huo baada ya UDA kutwaa viti vingi katika Mlima Kenya. Dkt Ruto alipata karibu kura milioni tatu kutoka eneo hilo na kushinda urais dhidi ya Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na Uhuru Kenyatta. Uchaguzi mdogo wa Bonchari pia ulitoa picha ya mwelekeo wa kisiasa katika eneo la Gusii. Licha ya ushirikiano wa kisiasa kati ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga baada ya "Handshake" ya mwaka 2018, Jubilee na ODM zilipambana vikali. Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kufariki kwa Mbunge John Oroo Oyioka. Katika uchaguzi huo, Pavel Oimeke wa ODM alipata kura 8,049, huku Zebedeo Opore wa Jubilee akipata 7,279. ODM ilidai polisi na serikali walitumiwa kushawishi matokeo. "Uchaguzi ni nafasi ya wananchi kueleza mapenzi yao kupitia kura, si jukwaa la kutimiza maslahi mafupi ya kisiasa," alisema Raila Odinga wakati huo. Aliongeza kuwa yaliyoshuhudiwa Bonchari na Juja yalikuwa matumizi mabaya ya polisi na kuonyesha kiburi cha baadhi ya maafisa wa serikali. Baadaye ODM iliendelea kuwa chama chenye nguvu zaidi katika eneo la Gusii. Chaguzi ndogo za Kabuchai, Matungu na Msambweni pia zilitoa ishara muhimu kabla ya uchaguzi wa 2022. Katika Kabuchai na Matungu, kulikuwa na madai ya rushwa, fujo na matumizi makubwa ya polisi. Kabuchai ilionekana kama pambano kati ya Ford Kenya ya Moses Wetang'ula na UDA ya Dkt Ruto. Mwisho wa uchaguzi, Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya alipata kura 19,274, huku Evans Kakai wa UDA akipata 6,445. Katika Matungu, chama cha ANC kilishinda kupitia Oscar Nabulindo. Msambweni, mgombea huru Feisal Badar aliyekuwa akiungwa mkono na Dkt Ruto alimshinda Omar Boga wa ODM katika uchaguzi wa Desemba 2020. Wachambuzi wengi wanatafsiri kushindwa kwa UDA Ol Kalou kama ishara kwamba Mlima Kenya umekataa serikali ya Rais Ruto. Matokeo hayo pia yanaweza kuwashawishi viongozi wengi waliochaguliwa kuhama UDA na kujiunga na DCP ili kulinda mustakabali wao wa kisiasa. Kwa DCP, ushindi huo unaimarisha hoja ya Gachagua kuwa chama chake sasa ndicho chenye ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alisema chama hicho hakijakata tamaa. "Tutashiriki uchaguzi kila mahali. Rais hatakata tamaa. Tulikuwa tunauza maendeleo huku wengine wakiuza hisia. Tuliwekeza pakubwa kwa sababu hii ni ngome yetu," alisema. Lakini mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika, Profesa David Monda, alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa Mlima Kenya umeondoka UDA. Alisema chama hicho kinapaswa kuelekeza rasilimali zake katika maeneo ambako bado kina nafasi ya kushinda badala ya kutumia nguvu nyingi katika Mlima Kenya. "UDA inapaswa kutarajia wimbi la viongozi kuhama hasa kutoka Mlima Kenya uchaguzi unapokaribia. Chama hicho hakina tena msingi imara katika eneo hilo," alisema. Aliongeza kuwa matokeo ya Ol Kalou yanaonyesha kuwa matumizi ya fedha, magenge ya wahuni na rasilimali za serikali si lazima yabadili uamuzi wa wapigakura. Licha ya kushindwa Ol Kalou, UDA pamoja na mshirika wake wa serikali, ODM, vimeshinda chaguzi ndogo nyingine zikiwemo Mbeere North, Ugunja, Banisa, Kasipul, Magarini, Malaba na kiti cha Seneti cha Baringo. UDA pia ilishinda uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr. Hata hivyo, utafiti wa Infotrak uliotolewa Jumatatu unaonyesha kuwa UDA imepoteza uungwaji mkono katika baadhi ya ngome zake, hasa Mlima Kenya. Kwa mujibu wa utafiti huo, UDA inaungwa mkono na asilimia 9 pekee ya wakazi wa Mlima Kenya, huku DCP ikiongoza kwa asilimia 33. Asilimia 36 ya wananchi katika eneo hilo bado hawajaamua chama watakachounga mkono. Ngome kubwa za UDA sasa ni Kaskazini Mashariki (asilimia 45), Bonde la Ufa (39) na Pwani (29). Kwa upande mwingine, umaarufu wa ODM umeshuka kutoka asilimia 38 mwezi Septemba 2024 hadi asilimia 21 sasa, hali inayohusishwa na ushirikiano wake na serikali ya Rais Ruto. Hata hivyo, ODM bado ndiyo chama kinachoongoza Nyanza (asilimia 50), ikifuatiwa na Pwani (46) na Magharibi (32).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sun, 19 Jul 2026 02:55:43

Aliyekuwa mfungwa Mwendwa, 35 hatimaye ajiunga na chuo kikuu

MFUNGWA wa zamani ambaye juma lililopita aliwashangaza wengi alipomtafuta hakimu aliyemhukumu kifungo cha miaka minne gerezani ili kumshukuru sasa amejiunga na chuo kikuu. Mwendwa Kilatya Nthenge,35, Ijumaa alijiunga na chuo kikuu cha Africa Nazarene kilichoko eneo la Ongata-Rongai, kaunti ya Kajiado. Jaji aliyemhukumu, Bw Eugene Pascal Nabwana ndiye aliyemsafirisha kwa gari lake la kibinafsi kutoka eneo la Syokimau, kaunti ya Machakos hadi Africa Nazarene University kujiunga rasmi na chuo hicho. Bw Nabwana pia alikuwa wa kwanza kumsaidia kwa kumlipia sehemu ya karo yake ya muhula wa kwanza chuoni anakosomea cheti cha masuala ya Biashara na Usimamizi. Akizungumza na Taifa Leo, Bw Nabwana alimtaja Bw Kilatya kuwa mtu aliyebadilika na kwamba furaha yake ni kumuona ametimiza ndoto yake ya masomo, kupata kazi nzuri na kujiendeleza maishani. "Kwanza kabisa nashukuru shirika la habari la Nation Media Group kwa kuangazia taarifa ya Kilatya. Nimeonelea vyema nimfikishe hapa angalau asajiliwe rasmi chuoni. Nimelipa sehemu ya karo ila deni bado ni kubwa. Ningeomba sana wahisani zaidi wajitokeze ili kuchangia Bw Kilatya asome chuoni bila kutatizwa," akasema Bw Nabwana. Taifa Leo pia iliona barua ya usajili ya Bw Kilatya ya chuo cha Africa Nazarene ambapo nambari yake ya usajili ni CBM2027/083. Ili kufanikisha masomo yake, nambari maalum ya kumchangishia karo ilitolewa kama Paybill Number 7291071 ilhali akaunti yake ikiwa ni CBM2027/083. Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Kilatya hakuficha furaha yake kujiunga na chuo cha Africa Nazarene ambacho kimekuwa ndoto yake ya muda mrefu. "Nimefurahi. Nashukuru Nation Media Group. Zaidi ninamshukuru jaji Nabwana. Amedhihirisha moyo wa upendo. Yeye ni zaidi ya mzazi wangu sasa. Mungu ambariki kwa msaada wake," akasema Bw Kilatya. Aliahidi kutia bidii masomoni. "Nitasoma kwa bidii na punde nikikamilisha na kuhitimu cheti, nitajikaza nifanye Diploma kabla ya kusomea Digrii. Wote waliochangia na watakaochangia kufaulu kwangu wabarikiwe," akasema Bw Kilatya. Naibu Chansela anayehusika na masuala ya wanafunzi na masomo katika chuo kikuu cha Africa Nazarene, Prof Simon Obwatho, alimtaja Bw Kilatya kuwa mtu aliyebadilika kikweli kutoka kwa 'mui hadi kuwa mwema." Prof Obwatho pia alimshukuru Bw Kilatya kwa kuchagua taasisi ya Africa Nazarene alikosajiliwa kuanza muhula wake wa 2026. "Tutashirikiana naye kwa karibu. Twataka awe kielelezo cha wengine ambao wanapitia changamoto kama zake kwamba bado unaweza kufungwa jela lakini ukabadilika, kuwakielelezo na kioo cha jamii," akasema Bw Obwatho. Julai 2,2026, Bw Kilatya alimtembelea Bw Nabwana ofisini mwake katika jumba la mahakama ya Wamunyu, kaunti ya Machakos wiki kmfafanulia kuwa baada ya kumfunga miaka minne gerezani kwa kosa la wizi wa mifugo, alitumia muda huo kusoma, kujisajili katika mtihani wa kidato cha nne (KCSE) alioufanya 2025. Alipata alama ya D. Punde alipokamilisha kifungo cha mwaka huu, alionelea amtafute Bw Nabwana kumshukuru na pia kumuomba kabisa msaada wa kuendeleza masomo yake. "Nilitii ushauri wako. Nikasoma kwa bidii nikiwa jela na kupata alama ya D nikiwa gerezani. Bado nina hamu kubwa ya kuendeleza masomo yangu ila sina namna.Nisaidie nipate ufadhili nisome," akasema Bw Kilatya. Hivyo Ijumaa Bw Kilatya alionekana kuwa mwingi wa furaha alipokubaliwa na kusajiliwa chuoni Africa Nazarene kuanza rasmi masomo yake ya juu.

read more