T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 07:55:02

Wadau wapinga hatua ya serikali ya kutaka watalii wanaoingia nchini kuwa na bima ya lazima

WADAU katika sekta ya utalii wamepinga vikali uamuzi wa serikali wa kutaka wageni wote wanaoingia nchi kuwa na bima ya lazima wakionya kuwa hatua hiyo itaathiri nchi kuvutia watalii wa kimataifa. Kulingana na tangazo lililochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la Julai 30, 2026 na kutiwa sahihi na Waziri wa Afya, Bw Aden Duale, wageni wote wanaoingia humu nchini watalazimika kuwa na bima ya afya yenye kiwango cha chini cha karibu Sh6.45 milioni. Bima hiyo itagharamia hadi Sh2.58 milioni za matibabu, Sh3.22 milioni za usafiri wa dharura wa mgonjwa, Sh38,700 za dawa zilizoagizwa na daktari, Sh129,000 za matibabu ya afya ya akili na Sh645,000 za kusafirisha mwili wa marehemu kurejeshwa nchini kwao. Kulingana na serikali, hatua hiyo inalenga kuhakikisha watalii wanapata huduma wanapokumbwa na dharura za kiafya. Hata hivyo, wadau wa utalii wamejitokeza na kupinga hatua hiyo wakisema itaongeza gharama za kuzuru Kenya. "Hatua hii itaongeza gharama kwa watalii. Kama sekta ya utalii tunapinga hatua hii. Huu si mwelekeo unaofaa, tunafaa kuweka mikakati ya kuvutia watalii si kuwazuia kuzuru nchi yetu," Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha wamiliki wa hoteli na wahudumu (KAHC), Dkt Sam Ikwaye, alisema. Wadau hao walisema bima hiyo ya lazima inaongezwa juu ya ada nyingine ambazo wageni tayari hulipa, ikiwemo ada ya Kibali cha Kielektroniki cha Kusafiri (ETA) na ada za kuingia katika hifadhi za taifa za wanyamapori iliyooongezwa hivi majuzi. Mtaalamu wa utalii, Bw Tony Kirimi alisema watalii wengi tayari huingia nchini wakiwa na bima kamili ya afya walizonunua nchi zao. "Hivyo basi hakuna sababu ya kuwalazimisha kununua nyingine nchini Kenya. Tulikubali ada ya ETA, ada za kuingia kwenye mbuga zilipandishwa na sasa tunaanzisha bima ya afya ya lazima ambayo ni ghali zaidi kuliko ilivyo katika baadhi ya mataifa ya Ulaya. Kulikuwa na maana gani ya kuondoa visa halafu tuanzishe gharama nyingine?" aliuliza. Aliongeza kuwa Kenya bado inapambana kuvutia watalii na kujenga jina lake kama kitovu kikuu cha utalii duniani na hivyo haipaswi kuweka sera zitakazozuia watalii kuchagua mataifa mengine. Wadau wa utalii pia wanaitaka serikali kufafanua ikiwa bima za afya ambazo watalii tayari wanazosafiri nazo kutoka mataifa yao zitatambuliwa, kiwango cha malipo kitakachotozwa na kampuni zitakazoruhusiwa kutoa huduma hiyo. Bw Mohammed Hersi ambaye ni mtaalamu wa utalii alisema sera hiyo itaongeza gharama kwa watalii. "Mtalii analipia bima akiwa kwao kabla ya kuja Kenya, halafu analazimishwa kununua nyingine hapa. Je, ingekuwaje kama kila nchi zingekuwa na sharti kama hilo? Swali si kama ni dola kumi au mia moja, ikiwa malipo hayo hayana msingi, basi ni mzigo usiofaa," alisema kwenye mjadala katika mtandao wa Facebook. Wadau hao sasa wanataka serikali kusitisha utekelezaji wa sera hiyo na kuanza kufanya mashauriano kati ya Wizara za Afya, Utalii, kampuni za bima na wadau wa sekta hiyo. Mjadala huo umeibuka wakati ambapo sekta ya utalii inaendelea kunoga. Hii ni baada ya Kenya kunakili idadi kubwa ya watalii wanaozuru mbuga za kitaifa za Wanyama porini. Kulingana na shirika la huduma ya Wanyamapori nchini (KWS), hifadhi za taifa zimepokea zaidi ya watalii milioni 3.5 huu mwaka ikilinganishwa na milioni mbili mwaka jana. Hata hivyo asilimia 60 ya wageni hao ni watalii wa humu nchini. Mkurugenzi Mkuu wa KWS, Prof Erustus Kanga, alisema mapato ya shirika hilo pia imeongezeka kutoka Sh2.9 bilioni mwaka 2022 alipochukua mamlaka hadi Sh10.5 bilioni mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii na uhamasisho. Hata hivyo, wadau wa sekta ya utalii wanaonya kuwa gharama hiyo mpya ya bima ya afya kwa wageni itaathiri utalii.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 12:17:53

Iran yanyonga raia wake wawili waliotoa habari za kijasusi kwa Amerika na Israel

TEHRAN, Iran: NCHI ya Iran imewanyonga raia wake wawili baada ya kupatikana na hatia ya ujasusi na kushirikiana na Israel, vyombo vya habari vya serikali viliripoti hapa Jumatatu. Haya yanafanyika huku taifa hilo likiongeza utekelezaji wa hukumu za kifo kwa makosa yanayohusishwa na usalama wa Iran. Walionyongwa ni Omid Behzad na Pouria Safvat, ambao walishtakiwa kwa kuipatia Israel taarifa za kijasusi. Wawili hao wanadaiwa walituma picha na taarifa za siri wakati wa vita vya mwaka jana na katika mzozo unaoendelea sasa kati ya Amerika-Israel na Iran. Taarifa hiyo ilichapishwa na chombo cha habari mahakamani, Mizan. Hukumu hizo zimetekelezwa wakati Iran inaendelea kukabiliwa na hali ya taharuki kutokana na mivutano ya ndani na nje ya nchi. Mapema mwaka huu, serikali ilikabili maandamano makubwa yaliyotikisa taifa hilo na kuyadhibiti kwa nguvu. Baadaye, Amerika na Israel zilianzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran mnamo Februari 28, na kuongeza mvutano katika eneo hilo. Duru ziliarifu kuwa wawili hao walipatia Israel taarifa za kijasusi na kuchangia majeshi yake yalenge vituo vya ukaguzi vilivyokuwa vikilindwa na kikosi cha Iran. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema Julai 24 kwamba Iran imewaua kwa kunyongwa watu wasiopungua 50 katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Kunyongwa huko kunatokana na madai ya makosa ya usalama wa taifa. Kundi hilo lilisema baadhi ya waliouawa walikuwa vijana wenye umri wa miaka 18 na 19, huku likikosoa ukosefu wa uwazi katika kesi hizo. Ujumbe wa kudumu wa Iran jijini Geneva haukujibu ombi la Reuters la kutoa maoni kuhusu taarifa hiyo. Hata hivyo, Tehran imekuwa ikikanusha mara kwa mara madai ya ukiukaji wa haki za wafungwa. Wakati huo huo, Rais wa Amerika Donald Trump alisema mazungumzo kati ya nchi yake na Iran yangefanyika Jumatatu. Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Masuala ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema hakuna mazungumzo yanayoendelea kwa sasa kati ya mataifa hayo mawili. Vita vya siku 12 vya mwaka jana vilianza katikati ya Juni baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya anga yaliyokuja kuungwa mkono na Amerikan kabla ya kusitishwa baada ya maelewano. Mzozo wa sasa ulianza mwishoni mwa Februari kufuatia mashambulizi ya Amerika na Israel yaliyohusishwa na shinikizo dhidi ya mpango wa nuklia wa Iran, makombora ya masafa marefu na jinsi serikali ilivyoshughulikia maandamano ya Januari. Ingawa pande zote zilikubaliana kusitisha mapigano mnamo Juni, mvutano umeendelea, huku juhudi za mazungumzo zikishindwa kufikia makubaliano ya kudumu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 12:35:55

MAONI: Ruto si mwanasiasa mliyezoea pale kijijini, Upinzani wasipotumia akili watapigwa chobo!

KATI ya sasa na mwezi Agosti mwaka ujao, Mkenya hana budi ila kutumia akili sawasawa, na vilevile kumlazimisha mwanasiasa kutumia akili, lau sivyo atemwe kama kikohozi. Umesalia takriban mwaka mmoja ndipo Uchaguzi Mkuu ufanyike, na huu ndio mwaka ambao wanasiasa huingia mashinani kuwakoroga watu akili kana kwamba wana ukiritimba wa hoja. Kwa mfano, fununu za ajabu zimeanza kusambaa kote nchini kwamba kiongozi wa chama cha Wiper (WPF) Kalonzo Musyoka, anaelekea kwenye kambi ya serikali, yaani muungano wa Kenya Kwanza (KK) unaoongozwa na Rais William Ruto. Amekanusha lakini… Sawa na nguruwe ambaye hujikaanga kwa mafuta yake, Kalonzo akithubutu kufanya hivyo atajimaliza mwenyewe kisiasa na hatawahi kupata nafuu tena wala kutamba katika uga wa siasa za nchi hii. Serikali ya KK imewaumiza Wakenya mno hivi kwamba mwanasiasa yeyote aliye katika mrengo wa upinzani akithubutu kuingia serikalini atafanya hivyo peke yake, labda na wajinga wachache wanaomzingira kwa kuwa kila soko lina mwendawazimu wake. Nimesema ni lazima tutumie akili, na tuwashinikize wanasiasa kutumia akili, kwa kuwa enzi ya siasa za tumbo ambapo mwanasiasa kigogo akihongwa na kubadili msimamo wake, na bado kuendelea kuwa maarufu, zimepitwa na wakati. Nimeandika mara si haba katika kurasa hizi kwamba, hata kigogo wa siasa za janibu za Mlima Kenya, Rigathi Gachagua, akiamua kurejea serikalini iliyomtimua kama paka shume atafanya hivyo peke yake. Mlima umeasi na kushupaa shingo; haujali wala kubali itakatika ua la. Sote, wanasiasa na wafuasi wao, tuna lazima ya kutumia akili kwa kuwa mtu tunayejaribu kuondoa mamlakani ana akili tele kichwani. Rais Ruto si mwanasiasa uliyezoea pale kijijini kwenu na ndio sababu anasema atauvuruga muungano wa upinzani na kuutawanya kwa raha zake. Hebu angalia, Ruto, mwanasiasa ambaye anapaswa kuwa akitapatapa kwa kuhofia kuzama kisiasa, ameanzisha gumzo la kusisimua na kuuudhi pia – kwamba Kalonzo anaelekea serikalini. Ruto wa sasa anapaswa kuwa na wasiwasi mwingi kwa kuwa vigogo wa upinzani kutoka kila pembe ya nchi wameungana ili kumwondoa mamlakani, akaibuka na kijana bora nchini, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, akaapa kuwa hata useneta ukimtoka, na Ruto ang'olewe mamlakani, ni sawa tu. Naamini msomaji ungekuwa katika nafasi ya Ruto ungeanza kutetemeka, lakini mwenyewe haonekani kuogopa chochote, amejibadili ngozi kama nyoka, akajifanya maridadi wa kujadiliwa na labda kupiganiwa na wanasiasa wanaotaka kuwa wagombea wenzi wake. Mara... Ruto anaweza kumtema Naibu Rais Kithure Kindiki wakati wowote; mara... anamtaka Kalonzo; mara… anamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi; mara… ODM imempa Gavan awa Homabay Gladys Wanga; mara… Magharibi imempa Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya; mara… kipenzi chake ni Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari Hassan Joho. Nchi nzima, badala ya kumcheka Ruto kwa kuwa yupo katika nafasi hatari ya kupoteza urais, inazungumzia jinsi alivyo na watu wengi waliotunga foleni kujaribisha bahati ya kuwa manaibu wake. Ghafla weusi umekuwa weupe! Uvundo umekuwa manukato! Ajabu! Kwa kubuni mazingira yanayoonyesha kwamba nafasi ya naibu rais inaweza kuwa wazi wakati wowote, Ruto ametukoroga akili nusra tusahau kwamba ana madhaifu yake, wanaisasa walafi nao wakaaza kuimezea mate nafasi ile, wanaotamani kumng'oa wakasahau kufanya kampeni dhidi yake, wakaanza kujiona kama washirika wake. Kalonzo, aliyeonekana kama mpinzani wake mzito, ambaye alikuwa na nafasi ya kumshinda mwakani, ameshushwa thamani na kuwa mmoja wa hao wanaotaka kuwa watu wa mkono wa Ruto. Unahitaji akili nyingi ili kuwavuruga na kuwapanga watu hivyo. Na ndio maana nasisitiza: tusipotumia akili, Ruto atatupanga sote, kufumba na kufumbua tumpate ikulu akihudumu kwa muhula wa pili. Ikiwa humtaki Ruto, hakikisha unatumia akili zako saa zote ili asikupige chobo.Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika (mutua_muema@yahoo.com)

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 13:17:29

MAONI: Mbona Rais Ruto hutukumbusha mara kwa mara kuwa 'yeye si mwendawazimu'?

KAULI ya Rais William Ruto: I am not a mad man (Mimi si wazimu) inaibua miangwi ya tamthilia za mwandishi wa Nigeria, Ola Rotimi. Kazi hizo ni: Our Husband Has Gone Mad Again (OUP, 1977), na The Gods Are Not to Blame (OUP, 1971). Our Husband Has Gone Mad Again (Mume Wetu ni Mwendawazimu) ni kazi ya kitashtiti, inayoangazia maudhui ya ubarakala wa kisiasa, migongano kati ya ukale na usasa, na mafarakano ya ndoa na ya kijinsia. Kuhusiana na ubarakala wa kisiasa, mhusika mkuu, Major (Mstaafu) Lejoka-Bwown anaona siasa kuwa ulingo wa kujitajirisha, badala ya wenzo wa kuhudumia umma. Rotimi anawakejeli watawala wa mataifa ya Afrika baada ya uhuru wasiozingatia misingi ya demokrasia. Mbona Rais Ruto anatukumbusha mara kwa mara kuwa 'yeye si mwendawazimu'? Halikadhalika, Rais amesisitiza mara nyingi kuwa 'yeye si mlevi' wala 'mpumbavu', hasa anapotetea hatua zake za utekelezaji wa sera tata – ambazo aghalabu hupingwa na wananchi. Baadhi ya sera hizo ni pamoja na mpango wa Bima ya Matibabu (SHA), ujenzi wa nyumba za bei nafuu na mpango wa ufadhili wa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu. Tathmini inaonesha kwamba, anapolinganishwa na marais waliomtangulia – Mzee Jomo Kenyatta, Daniel arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, Ruto ndiye rais wa pekee aliyetekeleza kijasiri sera zilizovuruga (disruptive policies) maisha ya Wakenya jinsi tunavyoyafahamu. Hata pale anapofahamishwa na wataalamu kuhusu athari hasi ya sera hizo, Rais Ruto hupuuzilia mbali ushauri huo – kushadidia kuwa anajua analolifanya. Je, mbona sasa amekiri, baada ya miaka mitatu – kwamba mfumo wa ufadhili wa elimu ya juu hautekelezeki kamwe? Aidha, mnamo Juni 25, 2024, kulizuka mageuzi ya vijana (Gen-Z) yaliyochochewa na Mswada wa Fedha wa Mwaka 2024, uliopendekeza nyongeza ya ushuru. Baada ya vijana wengi kuuawa, Rais Ruto aliamua kutoutia saini mswada huo. Kulikuwa na mantiki gani kuchukua hatua hiyo baada ya maafa kutokea? Je, huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukikaribia kwa kasi, kuna uwezekano kwamba rais 'atalegeza misimamo yake mikali' kuhusiana na mipango, na sera ambazo wananchi wanahisi kwamba zinawakandamiza? Kuna mafunzo yotote kutokana na mikabala ya utawala wa Rais Ruto? Ndio. Kwanza, utekelezaji wa sera za kimajaribio zinazodhulumu na kuwakandamiza wananchi ni hatari. Pili, uongozi wa nchi unapaswa kuwa wa kikoa. Rais Mwai Kibaki aliwateua wataalamu (technocrats), akawapa uhuru wa kulielekeza dau la uongozi. Kazi yake ikawa unahodha, huku wataalamu wakipiga makasia. Bitugi Matundura ni mhadhiri (mwagechure@gmail.com)

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 03 Aug 2026 15:53:55

T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 02:55:00

Uhuru aagiza Azimio ifanyiwe mabadiliko, iwatafute Sifuna na Gachagua

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya umeanza mchakato wa kujijenga upya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 kwa kuvikaribisha vyama vipya na kuanzisha mazungumzo na makundi ya kisiasa yanayoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Katika mkutano wa Baraza la Azimio ulioongozwa kwa njia ya mtandao na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, viongozi hao walikubaliana kuufanyia muungano huo mabadiliko makubwa. Muungano huo sasa utapewa jina jipya na mawanda yake kutanuliwa ili kuunganisha vyama vyote vya upinzani kabla ya kumteua mgombea mmoja wa urais atakayemenyana na Rais William Ruto. Katika mabadiliko hayo, vinara Fred Matiang'i wa Jubilee, Peter Munya wa PNU na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti walijumuishwa katika Baraza la Muungano, asasi cha juu zaidi inayofanya maamuzi ndani ya Azimio. Aidha, vyama vya DP yake aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, PDP na UMP yake aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza vilikubaliwa rasmi kujiunga na Azimio. Muungano huo pia uliikaribisha tena DAP-K inayoongozwa na Eugene Wamalwa, baada ya chama hicho kusitisha mchakato wa kujiondoa Azimio. Hata hivyo, Narc-Kenya cha Martha Karua, ambacho sasa kinajulikana kama People's Liberation Party (PLP), kilijiondoa rasmi mnamo 2024. Katibu Mkuu wa Azimio Caroli Omondi alisema viongozi wameamua kuanzisha mazungumzo rasmi na chama cha DCP cha Rigathi Gachagua, pamoja na vuguvugu la Linda Mwananchi la Seneta Edwin Sifuna, kwa lengo la kuunda muungano mkubwa zaidi wa upinzani. Alisema pia Azimio inaendelea kufanya mazungumzo na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, ambaye ni Kiongozi wa UGM huku Linda Mwananchi ikitarajiwa kujiunga rasmi mara kitakapokamilisha usajili wake kama chama cha kisiasa. Kwa mujibu wa Bw Omondi, Linda Mwananchi ndiyo itachukua nafasi ya ODM ndani ya Azimio, kufuatia mgawanyiko ulioikumba chama hicho. "Tumeamua kupanga upya muungano na kuanza mchakato wa kubadilisha sura na jina la Azimio ili liwe jukwaa linalowakutanisha washirika wote wa upinzani," akasema Bw Omondi. Alisisitiza kuwa jukumu la Bw Kenyatta ni kutekeleza wajibu wake kama mwenyekiti wa muungano, akikanusha madai kuwa rais huyo mstaafu ndiye anayepanga mikakati ya kisiasa ya upinzani. Miongoni mwa sababu za kubadilisha Azimio ni kuhakikisha unaendelea kuwavutia wafuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga, huku pia ukivutia vijana wa kizazi cha Gen Z na washirika wapya wa kisiasa. Inaelezwa kuwa Bw Kenyatta anasukuma ajenda ya upinzani kuwa na mgombea mmoja wa urais ili kuepusha mgawanyiko ulioshuhudiwa mnamo 1992, ambapo wagombea wengi wa upinzani waligawana kura na kumwezesha Rais wa wakati huo Daniel arap Moi kushinda. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anayeishi Amerika, Profesa David Monda, alisema mafanikio ya mpango huo yatategemea kujiandaa kwa viongozi wengine wa upinzani kufanya kazi chini ya muungano wa Azimio. Alisema kufufuliwa kwa Azimio kunaweza kuwa mikakati ya kumweka mbele kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kama mgombea wa urais, huku ukiwalazimu viongozi wengine wa upinzani kuamua ikiwa wataendelea kushirikiana ndani ya muungano huo au watafuata mkondo tofauti. Kwa mujibu wa Profesa Monda, upinzani ukiendelea kugawanyika utampa Rais Ruto nafasi kubwa zaidi ya kutetea kiti chake 2027, ilhali muungano mmoja wenye mgombea mmoja unaweza kuongeza ushindani dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza. "Ni wazi Wakenya wanamjua yule mgombeaji ambaye hawatampigia kura lakini bado hawajui watamchagua nani. Hii ndiyo maana lazima upinzani uweke juhudi za kuhakikisha wanaungana," akasema Profesa Monda.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 03:55:27

Kindiki: Kalonzo hana ajenda, na hawezi kumshinda Ruto 2027

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki wikendi alimshambulia vikali Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, akisema hana ajenda mpya ya kuwaongoza Wakenya baada ya kuhudumu serikalini kwa zaidi ya miaka 40. Akizungumza katika ziara ya maendeleo Kaunti ya Tharaka Nithi, Profesa Kindiki aliwataka viongozi wa upinzani kuwasilisha sera mbadala badala ya kutegemea siasa za chuki, migawanyiko na ukabila. "Wale wasioamini maono yetu ya Kenya mpya walete maono yao. Hawawezi kushindana nasi kwa sababu muda wao mwingi wameutumia kuhubiri chuki, migawanyiko na ukabila," akasema. Kauli hiyo inajiri huku Bw Musyoka akijitokeza kama mmoja wa vinara wa upinzani wanaolenga kumng'oa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027. Profesa Kindiki alisema Bw Musyoka ameshindwa kuonyesha mafanikio makubwa licha ya kushikilia nyadhifa mbalimbali serikalini kwa miongo kadhaa. "Huyo Kalonzo mnayetaka kutuuzia, mlete hapa. Tunamfahamu vizuri kwa sababu alisoma hapa shule ya upili ya Meru. Kama baada ya miaka 40 ya uongozi hajafanya chochote, hana jipya la kutoa sasa," akasema Profesa Kindiki. "Aende nyumbani apumzike. Tutamjengea barabara na atuombee kwa sababu huu ni wakati wetu," akaongeza. Aidha, Naibu Rais aliwashutumu viongozi wa upinzani kwa kutumia vijana kuzua vurugu badala ya kuwatafutia ajira au kuunga mkono miradi ya serikali ya kuwafaa. "Kazi ya kiongozi ni kuwasaidia vijana wapate ajira, si kuwalipa Sh200 warushe mawe na kuharibu biashara za wenzao," akasema. Profesa Kindiki pia alitoa wito wa amani na umoja, hasa katika eneo la Mlima Kenya, akisema siasa hazipaswi kugawa jamii. Aliongeza kuwa Kenya Kwanza itatafuta kura kwa kuonyesha rekodi yake ya maendeleo ikiwemo barabara, umeme, maji na miradi mingine badala ya matusi na siasa za migawanyiko.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 04:55:07

Baya afichua kilichofanya Aisha Jumwa atimke kutoka UDA

NAIBU kiongozi wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Owen Baya, amefichua kile alichodai kilimsukuma aliyekuwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa, kujiondoa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA). Kulingana na Baya, Jumwa alihama baada ya kukosa hakikisho la tikiti ya kuwania ugavana wa Kilifi mwaka 2027. Kwa mujibu wa Bw Baya, Bi Jumwa alimtafuta Rais William Ruto kupitia ujumbe mfupi wa simu akiomba wakutane ili kujadili hatma yake ya kisiasa na matarajio yake ya kuwania ugavana wa Kilifi. "Tunangojea atuambie ataenda chama gani, lakini hatutakubali kutumia uongo, machozi na udanganyifu. Siku ya Jumapili, Bi Jumwa alimtumia Rais ujumbe mfupi akiomba kukutana naye. Rais akamwambia ataangalia ratiba yake, kwa sababu amekuwa akimtafuta kwa muda mrefu," alisema Bw Baya. Alisema Rais alikubali kukutana naye katika Ikulu siku ya Jumanne, ambapo walifanya mazungumzo kuhusu mustakabali wa kisiasa wa kaunti ya Kilifi. Kwa mujibu wa Bw Baya, Bi Jumwa alimweleza Rais kuwa hajaridhishwa na jinsi ambavyo, amekuwa akifanya ziara Kilifi akiwa pamoja na Gavana Gideon Mung'aro na viongozi wengine bila kumhusisha, na akaomba ahakikishiwe tikiti ya UDA katika kuwania ugavana mwaka 2027. "Alimwambia Rais amhakikishie tikiti ya ugavana. Lakini Rais alimwambia kuwa bado ni mapema mno kufanya uamuzi huo na hivyo kuombwa awe na subra," alisema Bw Baya kwenye mkutano na wanachama wa UDA huko Kilifi. Baya anadai kuwa Rais alimweleza Bi Jumwa kuwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya UDA na ODM, suala la mgombea wa ugavana wa Kilifi lingeamuliwa kupitia mashauriano ya viongozi wa vyama hivyo. Mbunge huyo wa Kilifi Kaskazini alisema kuwa Rais alipendekeza kikao kitakachowahusisha viongozi mbalimbali, akiwemo Gavana Mung'aro na viongozi wa ODM akiwemo kinara wake Bw Oburu Odinga, ili kujadili namna ya kupata mgombea mmoja. Hata hivyo, Bw Baya adai kuwa Bi Jumwa alisisitiza kuwa anahitaji hakikisho la tikiti hiyo, na pia akataka Rais ampigie simu Bw Baya ili ashurutishwe kumuunga mkono. "Rais alimwambia avumilie kidogo kwa sababu muda wa kufanya maamuzi haujafika. Pia alimweleza kuwa mgombea wa UDA ataamuliwa kwa kuzingatia maoni kuhusu nani ana nafasi bora ya kushinda. Atakayeshindwa angepewa nafasi nyingine ya uongozi kama uwaziri au useneta," alifichua Bw Baya. Bw Baya alimshutumu Bi Jumwa kwa kumwekea Rais masharti. "Unawezaje kumpa Rais masharti? Rais alimwambia kama hawezi kusubiri kwa miezi michache iliyobaki, basi yuko huru kufanya uamuzi," alisema. Tangu alipotangaza kujiondoa UDA, viongozi wa vyama mbalimbali na miungano ya kisiasa wamekuwa wakimtembelea katika makazi yake ya Kakuyuni, Malindi, wakimshawishi ajiunge nao. Miongoni mwa waliomtembelea ni kinara wa vuguvugu la Linda Mwananchi, Bw James Orengo, pamoja na viongozi kutoka vyama vya Wiper na Jubilee. "Munajua nimeshahama chama cha UDA, na sasa nimefungua milango ya mashauriano na watu wa Kilifi, pwani na taifa zima. Kwa sasa sitaongea, nitapasua mbarika kadri tunavyoendelea lakini niko katika kipindi cha mazungumzo, nimepata fursa ya kuzungumza na kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka na atakuja Malindi na tutafanya mkutano mkubwa sana," alisema Bi Jumwa. Alisema wakazi wa Kilifi wanakandamizwa na kulazimishwa kuchagua gavana wa muungano wa UDA-ODM. Hata hivyo, Bi Jumwa amesisitiza kuwa bado anaendelea na mashauriano na wananchi pamoja na wadau wa kisiasa kabla ya kutangaza chama atakachotumia kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Kilifi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 04 Aug 2026 05:55:49

Tuju hapumui, sasa yu hatarini kupoteza mali nyingine kwenye mnada

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju yuko mbioni kupoteza mali nyingine ya thamani baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kutangaza mnada wa jumba lake la Entim Sidai Wellness Sanctuary lililoko Karen, Nairobi, ili kurejesha deni la Sh4.5 bilioni. Kwa mujibu wa tangazo la kampuni ya mnada ya Garam, mali hiyo itauzwa kwa mnada mnamo Agosti 25, 2026. Jumba hilo liko katika shamba la ekari 20 na lina nyumba ya kifahari ya mtindo wa kikoloni yenye vyumba tisa vya kulala, vyote vikiwa na mabafu ya ndani. Hatua hiyo inajiri miezi michache baada ya mali nyingine ya Bw Tuju kuuzwa kufuatia kushindwa kulipa mkopo aliouchukua kutoka EADB zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Mnamo Mei 21 mwaka huu, Mahakama Kuu ilisimamisha kwa muda mnada wa Entim Sidai kwa masharti kwamba Bw Tuju awe ameweka Sh50 milioni mahakamani kwa muda wa siku 30 na kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo ndani ya siku 60. Kushindwa kutimiza masharti hayo kungeruhusu mnada kuendelea. Hata hivyo, mahakama ilikubali uuzaji wa mali yake nyingine, Tamarind Karen na Dari Business Park, ikisema uhamisho wa umiliki ulikuwa tayari umekamilika mnamo 2024. Mali hiyo ilinunuliwa kwa Sh450 milioni na kampuni ya Ultra Eureka Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara Jackson Kiplimo Chebett, mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Stabex International. Baadaye kampuni hiyo ilitumia hati ya umiliki wa ardhi hiyo kupata mkopo wa dola milioni 2.5 kutoka Benki ya KCB. Bw Tuju aliweka Entim Sidai na mali nyingine kama dhamana ya mkopo wa dola milioni 9.3 (Sh1.2 bilioni wakati huo) aliopata kupitia kampuni yake ya Dari Limited mnamo Aprili 2015. Kutokana na riba, adhabu na gharama nyingine, deni hilo sasa limefikia karibu Sh4.5 bilioni. Bw Tuju amekuwa akidai kuwa EADB ilikiuka makubaliano kwa kushindwa kutoa awamu ya pili ya mkopo wa Sh294 milioni iliyokuwa imekusudiwa kufadhili ujenzi wa nyumba za kifahari za wastaafu mtaani Karen. Kwa upande wake, EADB imesema haikutoa fedha hizo kwa sababu Bw Tuju hakutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha uthibitisho wa maendeleo ya ujenzi na kutoa dhamana ya ziada. Mzozo huo wa kisheria umeendelea kwa miaka kadhaa huku Bw Tuju akijaribu kuzuia kuporomoka kwa himaya ya biashara aliyojenga kwa miongo mingi.

read more