T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 23 Jul 2026 04:55:13

EACC kuandama wanaomwaga mamilioni kwenye hafla za uwezeshaji

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imesema inawafuatilia wanasiasa wanaotumia mamilioni ya pesa katika hafla za uwezeshaji wa wananchi, ikionya kuwa mali waliyotangaza inaweza kufichua iwapo fedha hizo zinatokana na vyanzo halali. Tume hiyo ilisema kutoa fedha taslimu katika mikutano ya kisiasa kumeibua maswali kuhusu iwapo baadhi ya viongozi wanaishi zaidi ya kipato chao kinachojulikana. Katika miezi ya hivi majuzi, viongozi wa upinzani, viongozi wa kidini na wanaharakati wamekuwa wakitaka serikali ichunguze chanzo cha fedha zinazotolewa katika hafla hizo. Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alisema maafisa wa umma hulazimika kutangaza mali, mapato na madeni yao kila baada ya miaka miwili, jambo litakalowezesha tume kulinganisha mali waliyotangaza na kiasi cha fedha wanachogawa hadharani. "Maafisa wa umma wanatakiwa kutangaza mali yao kila baada ya miaka miwili. Tukigundua kuwa kuna mali ambayo hawawezi kueleza ilivyopatikana, tunafanya uchunguzi na kuwasilisha suala hilo mahakamani ili iamue iwapo ilipatikana kinyume cha sheria," alisema Bw Mohamud. Alizungumza Kisumu Jumanne wakati EACC ilipotangaza kuanza mchakato wa kurejesha ardhi ya Huduma ya Magereza ya Kenya yenye thamani ya Sh4.3 bilioni inayodaiwa kutwaliwa isivyo halali. Bw Mohamud alisema tume ilitoa notisi mnamo Novemba 12, 2025 ikiwataka maafisa wa umma kutangaza mapato, mali na madeni chini ya Sheria ya Migongano ya Maslahi ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa notisi hiyo,  tangazo hili lilipaswa kuwasilishwa kati ya Novemba 1 na Desemba 31, 2025. EACC pia inatarajiwa kuwataka baadhi ya wanasiasa kueleza chanzo cha fedha wanazotumia katika shughuli hizo na kubaini iwapo ni misaada ya kawaida, kampeni za kisiasa au matumizi mabaya ya nyadhifa za umma. Hata hivyo, Bw Mohamud alisema kubeba fedha taslimu si kosa la jinai. "Kuwa na pesa si kosa. Swali ni, fedha hizo zimetoka wapi? Je, ni matokeo ya uhalifu au zinanuiwa kutoa hongo? Ni lazima fedha zihusishwe na uhalifu kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa," alisema. Katika miezi ya hivi majuzi, viongozi wengi hasa wanaounga mkono serikali jumuishi wamekuwa wakifanya hafla za uwezeshaji katika maeneo mbalimbali wakitoa mamilioni ya fedha. Mfano mmoja ni hafla iliyofanyika Suna Mashariki, ambapo Mbunge Junet Mohamed alitoa Sh10 milioni akiwa amebeba kwenye mkoba mgongoni, huku Rais William Ruto naye akichangia Sh10 milioni. Kwa mujibu wa taarifa za mishahara ya viongozi wa umma, mbunge hupokea mshahara na marupurupu yanayofikia takriban Sh1.45 milioni kwa mwezi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 23 Jul 2026 03:55:30

Gachagua aiga mbinu za siasa za Raila za kupambana na serikali

KWA takriban miongo mitatu, aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga alijijengea jina kama kinara wa siasa za upinzani nchini. Alitumia mbinu mbalimbali kama kususia bidhaa, kuhamasisha wananchi kupitia mikutano ya kisiasa, kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa na kuunda miungano ya kisiasa ili kuongeza presha kwa serikali zilizokuwa mamlakani. Sasa, chini ya miaka miwili tangu atofautiane na Rais William Ruto, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaonekana kufuata mkondo huo huo aliokuwa akiukosoa vikali alipokuwa serikalini. Kauli yake ya kuwashauri watalii na wawekezaji wa kigeni wasubiri hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kabla ya kuja Kenya inachukuliwa na wachambuzi kama ishara kwamba sasa amekumbatia mbinu za jadi za upinzani. Kama alivyofanya Raila kwa miaka mingi, Bw Gachagua sasa anatumia shinikizo za kiuchumi, ujumbe kwa jamii ya kimataifa na siasa za miungano kujaribu kushinikiza serikali bila kuwa mamlakani. Mfanano mkubwa zaidi kati ya viongozi hao wawili ni matumizi ya uchumi kama silaha ya kisiasa. Mwaka 2017 na baadaye 2023, Raila aliwataka Wakenya kususia bidhaa na huduma za kampuni alizodai zinaunga mkono serikali. Wakati huo, Bw Gachagua akiwa Naibu Rais alimshutumu Raila kwa kuharibu biashara na kuhatarisha ajira. Lakini sasa, Bw Gachagua ameenda hatua zaidi kwa kuwashauri watalii na wawekezaji wa kigeni waahirishe safari na uwekezaji wao nchini akidai hali ya usalama imezorota. Kauli hiyo imeibua ukosoaji mkubwa, si kutoka kwa serikali pekee bali pia ndani ya muungano wa upinzani. Msemaji wa Muungano wa Upinzani Dkt Mukhisa Kituyi alisema hakubaliani na wito wowote unaoweza kudhoofisha sekta muhimu ya utalii, akisema kuna njia nyingine za kukosoa serikali bila kuathiri uchumi. Mbinu nyingine ambayo Raila alitumia kwa miaka mingi ilikuwa kupeleka malalamishi ya kisiasa ya Kenya katika jukwaa la kimataifa. Baada ya uchaguzi tata na wakati wa misukosuko ya kisiasa, Raila mara kwa mara alikutana na mabalozi na jamii ya kimataifa kueleza changamoto za utawala na demokrasia. Bw Gachagua naye sasa anaonekana kufuata njia hiyo kwa kutumia majukwaa ya kimataifa kueleza madai ya ukosefu wa usalama, ukiukaji wa haki za kisiasa na matumizi mabaya ya mamlaka. Aidha, kama Raila, Bw Gachagua amejikita katika kujenga muungano mpana wa kisiasa. Mbali na viongozi wa Muungano wa Upinzani kama Kalonzo Musyoka, Dkt Fred Matiang'i, Martha Karua, Justin Muturi na Eugene Wamalwa, amekuwa akifanya mikutano na kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi nyumbani kwake Wamunyoro. Lengo ni kuunganisha viongozi kutoka maeneo mbalimbali ili kutoa changamoto kubwa kwa serikali ya Kenya Kwanza. Kama Raila alivyoanza kwa kuimarisha ngome yake ya Nyanza kabla ya kupanua ushawishi wake, Bw Gachagua naye ameanza kwa kuimarisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya kabla ya kuelekea Ukambani, Magharibi na Pwani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 23 Jul 2026 02:55:50

Ilikuwa uongo? Helb yasema haina pesa kufadhili wanafunzi siku moja baada ahadi ya Ruto

MAELFU ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu na taasisi za mafunzo ya kiufundi (TVET) Septemba mwaka huu wako hatarini kukosa ufadhili wa serikali baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kutangaza kuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha. Kulingana na ripoti iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, HELB inahitaji Sh114.36 bilioni kufadhili wanafunzi milioni 1.2 katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027, lakini kwa sasa ina Sh56.71 bilioni pekee. Hii inaacha pengo la Sh57.65 bilioni. Bodi hiyo ilisema imekuwa ikikumbwa na uhaba wa fedha kwa miaka minne iliyopita huku idadi ya wanafunzi wanaohitaji msaada ikiendelea kuongezeka. "Changamoto kubwa inayoathiri jukumu la HELB ni pengo linalozidi kupanuka kati ya fedha zinazohitajika na bajeti inayotolewa," ilisema katika taarifa kwa wabunge. HELB imeomba Wizara ya Fedha kuongeza fedha ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji wanaendelea kupata mikopo na ufadhili. Bodi hiyo ilieleza kuwa kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili wa wanafunzi mwaka 2023 kuliongeza idadi ya wanaofaidika kutoka 576,338 hadi 823,691 mwaka uliopita, hali iliyoongeza mzigo wa kifedha. Katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026, HELB ilipokea Sh45.66 bilioni kutoka kwa serikali na mapato yake mengine, lakini ilitumia Sh48.6 bilioni kufadhili wanafunzi. Jumla ya wanafunzi 823,691 walipokea mikopo, huku 23,333 wakinufaika na basari na wengine 364,279 wanaosomea kozi za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati, Ubunifu, Uvuvi na Kilimo wakipata ufadhili. Haya yanajiri siku moja baada ya Rais William Ruto kutangaza kuwa wanafunzi wote watakaofuzu kujiunga na vyuo vikuu watafadhiliwa kikamilifu na serikali, hatua inayoashiria kuwa serikali inaweza kubadilisha mfumo wa ufadhili ulioanzishwa mwaka 2023 ambao umekuwa ukikosolewa na wanafunzi.

read more