T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

MAONI: Watanzania wasiogope 'vita' vya kuitafuta katiba mpya

HUKU Kenya ikitathmini hatua ilizokwisha kupiga katika utekelezaji wa Katiba yake'mpya' tangu ilipoidhinishwa 2010, Tanzania nayo inashuhudia mwamko mpya wa kuisaka katiba mpya. Kenya na Tanzania zilipata uhuru kwa ukaribu mno kiwakati. Huku Tanzania ikitupilia mbali nira ya ukoloni mkongwe wa Wajerumani na Waingereza, Desemba 9,1961 na kuwa Jamuhuri mnamo Aprili 26, 1964 (kufuatia muungano wa Tanganyika na Zanzibar), Kenya ilijikomboa kutoka kwa Waingereza Desemba 12, 1963, na kuwa Jamuhuri 1964. Wakenya na Watanzania ni 'watu wamoja' waliotenganishwa na mipaka ya wakoloni. Inatia moyo kwamba, baada ya miaka 16 tangu Kenya ijipatie Katiba 'mpya', tumeanza kuona vuguvugu nchini Tanzania kuisaka katiba mpya. Tangu uhuru nchini Tanzania, kuna mabadiliko mengi yaliyojiri kijamii, kiuchumi na kisiasa - kiasi kwamba, upo uwezekano mkubwa kuwa, Katiba ya Uhuru haiwezi tena kukidhi matakwa na matamanio ya Watanzania. Tanzania ima mengi ya kujifunza kutokana na safari na mchakato na mapambano yaliyojiri Kenya katika kuitafuta Katiba mpya. Kwanza, safari hiyo ya takriban miongo miwili haikuwa rahisi. Ilikumbwa na vikwazo na upinzani mkubwa wa kisiasa na hata kusababisha maafa. Lakini Wakenya hawakukata tamaa. Misukumo iliyochochea utashi wa katiba mpya nchini Kenya katika miaka ya 1990 ilisababishwa na mabadiliko mengi kwenye katiba ya uhuru yaliyomlimbikizia mamlaka rais na kumfanya awe mtawala wa kiimla. Dalili hizo zinaonekana Tanzania. Kwa sababu hiyo, wanaharakati na asasi za kidini zilijifungata masombo kuicheza ngoma ya mabadiliko ya katiba. Harakati hizo zilizaa matunda pale Kifungu cha 2A cha Katiba kiliporekebishwa kuirejesha Kenya kwenye mkondo wa demokrasia ya siasa za vyama vingi. Jambo hilo haikubadilisha hali ya rais mwenye mamlaka au nguvu nyingi. Mapambano hayo yalikwama baina ya 2000 -2005. Mnamo 2000, mwanasheria, Prof Yash Pal Ghai wa Tume ya Marekebisho ya Katiba (CKRC) alianza kukusanya maoni kutoka kwa umma, na kuandaa Mswada wa Bomas (Bomas Draft). Wasomi teule wa Kisiasa waliubadilisha mswada huo kuwa Wako Draft - ambao Wakenya waliuangusha katika kura ya maoni ya mwaka 2005. Mkosi wa ghasia za baada ya uchaguzi mnamo 2007/2008 ulitia chachu kwa wanasiasa na wasomi teule kutambua kwamba, ilikuwa ni hatari kwa usalama wa nchi yenye asasi zilizopendelea upande mmoja. Machafuko hayo nusura yaisambaratishe Kenya. Kamati ya Wataalamu ilipitia miswada tangulizi ya katiba. Mnamo Agosti 2010 asilimia 67 ya Wakenya waliipitisha Katiba hiyo kwenye kura ya maoni, na kuzindua serikali za ugatuzi. Bitugi Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 21 hours ago

Ruto sasa atumia maafisa wa umma 'kubembeleza' Mlima

RAIS William Ruto sasa anawategemea makatibu wa Baraza la Mawaziri na maafisa wengine wa serikali kupeleka ujumbe wa serikali mashinani katika juhudi za kurejesha uungwaji mkono wa Mlima Kenya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Mikakati hiyo inalenga kueleza wakazi mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza na kupunguza malalamishi kwamba eneo hilo limetengwa tangu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuondolewa mamlakani Oktoba 2024. Rais Ruto amekiri kuwa serikali imekuwa na tatizo la kuwasilisha mafanikio yake kwa wananchi, hali ambayo amedai imeacha nafasi kwa taarifa potovu na kuchochea kutoridhika. Maafisa wa serikali sasa wanafanya mikutano ya hadhara katika eneo la Mlima Kenya kueleza mipango ya serikali na kushughulikia malalamishi ya wananchi. Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alifanya baraza la wananchi Nyeri kupitia mpango wa Jamii Imara Mashinani, ambako alijibu maswali kuhusu afya, kilimo na miundombinu. Bi Muthoni alisema serikali imegundua pengo la mawasiliano kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), akieleza kuwa wananchi wengi hawajui wanaweza kulipa michango yao kwa awamu kupitia mpango wa Lipa SHA Polepole. Maafisa wengine waliohusika katika mikutano hiyo ni Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na Katibu Mkuu wa Kawi Alex Wachira. Katika upande wa miundombinu, Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KeNHA), Winfrida Ngumi, alisema miradi ya barabara yenye thamani ya zaidi ya Sh46 bilioni imekamilika au inaendelea Nyeri. Alisema pia barabara za Mau Mau, ambazo zilikuwa zimesimama, zimeanza tena baada ya wakandarasi kulipwa zaidi ya Sh5.5 bilioni.

read more