T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 16 Oct 2026 03:55:31

Vurugu katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha Raila

HAFLA ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga ilikumbwa na vurugu katika Kituo cha Utamaduni cha Migwena, Bondo, Kaunti ya Siaya, huku makundi hasimu ya kisiasa yakizozania urithi wake na mwelekeo wa chama hicho. Vijana waliojihusisha na wanasiasa tofauti walifurika kwenye hema la wageni mashuhuri, wakitatiza shughuli na kufanya iwe vigumu kwa viongozi kufuatilia ratiba ya hafla hiyo. Maombi yaliyoongozwa na Kanisa la Kianglikana nchini yalianza mwendo wa saa tano asubuhi, yakifuatiwa na hotuba za wanafamilia na burudani za muziki. Hata hivyo, juhudi za msimamizi wa hafla kuwatawanya vijana hao hazikufaulu, hali iliyolazimu mjane wa Raila, Mama Ida Odinga, pamoja na watoto wao Raila Junior, Rosemary na Winnie, kuhamia hema nyingine. Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya baadhi ya vijana kuanza kurusha mawe kuelekea hema la wageni mashuhuri. Maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda viongozi walitumia viti vya plastiki kuwakinga huku waliohudhuria wakitafuta mahali pa kujisitiri. Baadhi ya watu waliripotiwa kujeruhiwa. Vurugu hizo zilitokea huku kukiwa na mvutano kati ya wanasiasa wanaounga mkono mrengo wa Linda Mwananchi na wale wanaounga mkono ushirikiano wa ODM na serikali ya Rais William Ruto. Licha ya hali hiyo, hafla iliendelea huku familia ikitoa heshima kwa Raila, aliyefariki mwaka mmoja uliopita. Mama Ida aliwaomba vijana kuwa watulivu na kueleza kuwa mwaka uliopita ulikuwa mgumu kwa familia, ambayo pia ilimpoteza dada yake Raila ndani ya siku 40 baada ya kifo chake. Alisema bado wanaomboleza na akawashukuru wakazi wa Bondo, Kisumu na Wakenya wengine kwa kuendelea kuwafariji. Mama Ida pia alikumbuka jinsi alivyokabidhi mumewe wananchi aendelee na safari yake ya kisiasa, akisema alitamani angerudi nyumbani akiwa hai. Aliwataka viongozi na wazee kuwaelekeza vijana kwa upendo na subira, huku akiwahimiza vijana kuwaheshimu wazee. Vurugu hizo ziliangazia mgawanyiko unaozidi kujitokeza ndani ya ODM kuhusu jinsi ya kuendeleza siasa za Raila na msimamo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 16 Oct 2026 02:55:00

Vigogo wasusia hafla ya kumbukumbu ya Raila

KUMBUKUMBU ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga ilikumbwa na suintofahamu Alhamisi baada ya baadhi ya vigogo wa chama hicho na Rais William Ruto kukosa kuhudhuria hafla iliyofanyika Migwena, Bondo, kaunti ya Siaya. Kutohudhuria kwa viongozi hao kulizua maswali kuhusu mgawanyiko ndani ya ODM na uhusiano wake na serikali jumuishi ya Rais Ruto, huku mirengo pinzani ikizozana kuhusu urithi wa kisiasa wa Raila na mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, naibu kiongozi wa chama Abdulsamad Nassir na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed walikuwa miongoni mwa viongozi wakuu waliokosekana katika hafla hiyo. Vyanzo vya ndani ya chama vilisema baadhi ya maafisa hawakufurahishwa na mpangilio wa sherehe, ambao waliamini uliwapa nafasi kubwa viongozi wa upinzani, wakiwemo wale wanaohusishwa na kundi la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Rais Ruto naye hakuhudhuria hafla hiyo, licha ya serikali yake kusaidia mazishi ya kitaifa ya Raila na ujenzi wa kaburi lake Kang'o Ka Jaramogi. Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pia hakuhudhuria hafla hiyo. Vyanzo vya serikali vilisema Rais alijiondoa baada ya kubainika kuwa viongozi wa upinzani wangekuwa na nafasi kubwa katika sherehe hizo. Kutokuwepo kwa vigogo hao kulijiri huku mjane wa Raila, Mama Ida Odinga, akiwakaribisha viongozi wa upinzani katika shamba la familia la Opoda kabla ya kuelekea Migwena. Linda Mwananchi ilipokelewa Opoda, hatua iliyozidisha mjadala kuhusu iwapo kumbukumbu ya Raila ilipaswa kuwa hafla ya ODM pekee au jukwaa la kuwakutanisha viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa. "Siasa ni ushawishi, si udikteta kama tunavyoshuhudia hapa. Raila alitufundisha kuweka maisha ya wananchi mbele tunapofanya maamuzi," alisema Sifuna. Bw Orengo alisema upinzani utaungana nyuma ya mgombea mmoja ili kumshinda Rais Ruto, akitaja ukosefu wa ajira kuwa mojawapo ya changamoto zinazowakabili Wakenya Mama Ida alitetea uamuzi wa kuwapokea viongozi kutoka mirengo yote, akisema Raila alikuwa wa Wakenya wote na urithi wake haupaswi kufungwa ndani ya chama kimoja. Mvutano huo ulijitokeza wazi uwanjani, ambapo wafuasi wa mirengo tofauti walizozana na baadhi ya vijana kujaa katika hema la wageni waalikwa. Hali hiyo ilivuruga baadhi ya shughuli za hafla. Huku viongozi wanaounga mkono ushirikiano na serikali wakitetea mwelekeo huo, wanasiasa wa upinzani walisisitiza kuwa njia bora ya kumuenzi Raila ni kuunganisha nguvu na kumwondoa Rais Ruto madarakani mwaka 2027. Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati aliwaambia wanaofikiria kuondoka chama hicho kuwa wako huru kufanya hivyo, akisisitiza kuwa ODM bado ina nguvu katika Nyanza. Huku baadhi ya viongozi wakisisitiza kuwa urithi wa Raila unapaswa kulindwa ndani ya ODM na kwa kushirikiana na serikali, wengine walisema njia bora ya kumuenzi ni kuunganisha upinzani na kumuondoa Rais Ruto madarakani mwaka ujao. Mvutano huo ulijitokeza wiki kadhaa kabla ya sherehe hizo, huku familia ikiunda kamati ya kitaifa ya kuratibu kumbukumbu za Raila, iliyoongozwa na Profesa Adams Oloo na kusaidiwa na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, ODM ilianzisha sherehe za mwezi mzima za Mwezi wa Baba. Miongoni mwa viongozi wa upinzani waliohudhuria ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Seneta Godfrey Osotsi na kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi. Kutokuwepo kwa baadhi ya vigogo na mvutano uliojitokeza vilifanya kumbukumbu hiyo kuwa zaidi ya hafla ya maombolezo, huku maswali kuhusu umoja wa ODM na urithi wa Raila yakitawala mazungumzo kuelekea uchaguzi wa 2027.

read more