T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Sat, 18 Jul 2026 00:55:12

Ushindi wa Gachagua Ol Kalou wazua mjadala kuhusu mgawanyiko Mlimani

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, amesema matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou hayana athari kwa siasa za Mlima Kenya Mashariki, akisisitiza kuwa eneo hilo limeamua kuendelea kumuunga mkono Rais William Ruto. Kauli hiyo ilitolewa Alhamisi ilipobainika kuwa mgombea wa chama cha DCP alikuwa akielekea kupata ushindi mkubwa dhidi ya mgombea wa UDA. "Sisi wa Mlima Kenya Mashariki hatujali kinachotokea Mlima Kenya Magharibi," alisema Bw Ruku. Kwa miezi sita iliyopita, Bw Ruku amekuwa akihimiza kaunti za Kirinyaga, Embu, Tharaka Nithi na Meru kujitenga kisiasa na eneo la Mlima Kenya Magharibi. Hatua hiyo inaonekana kuwa mkakati wa kuimarisha ushawishi wa Rais Ruto katika eneo hilo huku ikizuia juhudi za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuunganisha Mlima Kenya chini ya DCP. Bw Ruku anaamini kuwa eneo la Mlima Kenya Mashariki linaweza kutoa zaidi ya kura milioni mbili na hivyo kuwa na nguvu kisiasa. Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Profesa Gitile Naituli amesema siasa za Kenya haziamuliwi na jiografia pekee. "Wazo kwamba Mlima Kenya Mashariki una umuhimu tu unapomuunga mkono Mkikuyu kutoka Magharibi ni rahisi mno. Historia ya Kenya inaonyesha kuwa ushindani wa kisiasa, maafikiano ya viongozi na miungano ndiyo huamua matokeo," alisema. Aliongeza kuwa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ni kipimo cha hali ya kisiasa nchini na unaweza kuashiria mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa 2027. Baada ya matokeo hayo, Naibu Rais Kithure Kindiki aliandika kwenye Facebook kuwa ni wakati wa "kurudi kujipanga upya ." Wiki iliyopita Prof Kindiki aliwahimiza wakazi wa Meru kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto, akisema kura kwa rais ni kura kwake pia. "Hapa Meru hatuna chaguo lingine isipokuwa kumpigia kura Rais Ruto mwaka 2027. Kumpigia kura William Ruto ni kunipigia kura mimi," alisema. Mnamo Jumatatu, Bw Ruku alikutana na zaidi ya vijana 300 kutoka Embu, Meru, Isiolo na Tharaka Nithi kuhimiza kampeni ya kujitegemea kisiasa kwa Mlima Kenya Mashariki. Alisema watahakikisha upinzani haupati nafasi katika eneo hilo. "Tutaweka mpaka kati ya Mlima Kenya Mashariki na Magharibi. Hatutampa Gachagua nafasi ya kujitanua huku mashariki," alisema. Aidha, madiwani 61 wa Bunge la Kaunti ya Meru walitangaza kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto na Prof Kindiki, wakisema kaunti hiyo imenufaika na miradi ya maendeleo. Lakini ushindi wa DCP Ol Kalou unaonekana kumpa Bw Gachagua nguvu mpya. Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Ngunjiri Wambugu alisema ushindi huo unaweza kumfanya Bw Gachagua kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya. "Huo ushindi unaweza kumfanya Gachagua kuwa na nguvu kubwa kisiasa. Wale ambao hatuwezi kufanya kazi naye lazima tukae chini na kupanga upya mikakati yetu," alisema. Kwa upande wake, Bw Gachagua ameendelea kusisitiza kuwa hataruhusu juhudi zozote za kugawa kisiasa eneo la Mlima Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 17 Jul 2026 23:55:34

EBOLA: Kenya imewahifadhi raia wa Amerika licha ya migomo

WAFANYAKAZI saba wa shirika la kutoa misaada kutoka Amerika waliokuwa wakisaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wametengwa kwa siku 21 katika kituo kipya cha uangalizi nchini Kenya, kufuatia masharti mapya ya usafiri yaliyowekwa na serikali ya Amerika. Franklin Graham, rais na mtendaji mkuu wa shirika la misaada la Kikristo la Samaritan's Purse, aliambia Reuters kuwa wafanyakazi hao hawana dalili zozote za Ebola, lakini wanazingatia utaratibu wa kutengwa kama tahadhari. "Wafanyakazi wetu saba wa kundi la Kukabiliana na Majanga wako huko. Hawana dalili zozote, lakini wanatengwa kwa siku 21 chini ya usimamizi wa serikali ya Kenya," alisema Graham. Kwa mujibu wa sera mpya ya Amerika, raia wake wanaorejea kutoka DRC, ambako kuna mlipuko wa Ebola, lazima wakae kwa wiki tatu katika nchi ya tatu kabla ya kuruhusiwa kuingia Amerika. Serikali ya Amerika inajenga kituo chenye uwezo wa vitanda 50 katika kambi ya jeshi la anga katikati mwa Kenya kwa ajili ya kuwafuatilia raia wake ambao huenda waliathiriwa na virusi vya Ebola nchini DRC au Uganda lakini hawajaonyesha dalili za ugonjwa. Ujenzi wa kituo hicho umekumbana na upinzani mkubwa nchini Kenya. Wakenya wengi wanahisi kuwa Amerika inahamishia hatari ya kiafya nchini humo. Mwezi uliopita, Waziri wa Afya alitangaza kusitishwa mara moja kwa ujenzi huo baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau mahakama kwa kutotekeleza amri ya kusimamisha shughuli hizo hadi kesi iamuliwe. Afisa wa Wizara ya Masuala ya Kigenu ya Amerika alisema kundi hilo la wahudumu lilihamishiwa kwa hiari katika kituo hicho kwa uangalizi na kutengwa kama tahadhari. Alisema maafisa wa Kenya wameruhusu hatua hiyo chini ya usimamizi wa madaktari wa Huduma ya Afya ya Umma ya Amerika. Chanzo kilichofahamu suala hilo kilisema kundi hilo liliwasili katika kituo hicho Jumatatu. Baadhi yao walikuwa wamewahudumia wagonjwa wa Ebola nchini Congo huku wengine wakifanya kazi za ujenzi bila kukutangamana moja kwa moja na wagonjwa. Kilisema kuna mtu mmoja anayeshukiwa kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi, lakini afya ya wote inaendelea kufuatiliwa. Pia maafisa wa Kenya hawajawaruhusu kutoka katika kituo hicho hadi kipindi cha uangalizi kitakapokamilika. Ebola huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu au mnyama aliyeambukizwa. Shirika la Samaritan's Purse ni miongoni mwa mashirika makubwa yanayosaidia kukabiliana na Ebola nchini DRC kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO). Aina ya virusi vya Bundibugyo, ambayo haina chanjo wala tiba iliyothibitishwa, imeua angalau watu 828 tangu katikati ya Mei. WHO inasema maambukizi bado yanaendelea kusambaa bila kutambuliwa kwa kiwango kikubwa. Graham alisema baada ya kutembelea kituo hicho wiki hii ameridhishwa na vifaa vilivyopo. "Ni kituo cha kisasa kabisa. Iwapo mtu angeugua, hapo ndipo mahali pazuri pa kumpatia matibabu," alisema.

read more