T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 17 Jul 2026 23:55:34

EBOLA: Kenya imewahifadhi raia wa Amerika licha ya migomo

WAFANYAKAZI saba wa shirika la kutoa misaada kutoka Amerika waliokuwa wakisaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wametengwa kwa siku 21 katika kituo kipya cha uangalizi nchini Kenya, kufuatia masharti mapya ya usafiri yaliyowekwa na serikali ya Amerika. Franklin Graham, rais na mtendaji mkuu wa shirika la misaada la Kikristo la Samaritan's Purse, aliambia Reuters kuwa wafanyakazi hao hawana dalili zozote za Ebola, lakini wanazingatia utaratibu wa kutengwa kama tahadhari. "Wafanyakazi wetu saba wa kundi la Kukabiliana na Majanga wako huko. Hawana dalili zozote, lakini wanatengwa kwa siku 21 chini ya usimamizi wa serikali ya Kenya," alisema Graham. Kwa mujibu wa sera mpya ya Amerika, raia wake wanaorejea kutoka DRC, ambako kuna mlipuko wa Ebola, lazima wakae kwa wiki tatu katika nchi ya tatu kabla ya kuruhusiwa kuingia Amerika. Serikali ya Amerika inajenga kituo chenye uwezo wa vitanda 50 katika kambi ya jeshi la anga katikati mwa Kenya kwa ajili ya kuwafuatilia raia wake ambao huenda waliathiriwa na virusi vya Ebola nchini DRC au Uganda lakini hawajaonyesha dalili za ugonjwa. Ujenzi wa kituo hicho umekumbana na upinzani mkubwa nchini Kenya. Wakenya wengi wanahisi kuwa Amerika inahamishia hatari ya kiafya nchini humo. Mwezi uliopita, Waziri wa Afya alitangaza kusitishwa mara moja kwa ujenzi huo baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau mahakama kwa kutotekeleza amri ya kusimamisha shughuli hizo hadi kesi iamuliwe. Afisa wa Wizara ya Masuala ya Kigenu ya Amerika alisema kundi hilo la wahudumu lilihamishiwa kwa hiari katika kituo hicho kwa uangalizi na kutengwa kama tahadhari. Alisema maafisa wa Kenya wameruhusu hatua hiyo chini ya usimamizi wa madaktari wa Huduma ya Afya ya Umma ya Amerika. Chanzo kilichofahamu suala hilo kilisema kundi hilo liliwasili katika kituo hicho Jumatatu. Baadhi yao walikuwa wamewahudumia wagonjwa wa Ebola nchini Congo huku wengine wakifanya kazi za ujenzi bila kukutangamana moja kwa moja na wagonjwa. Kilisema kuna mtu mmoja anayeshukiwa kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi, lakini afya ya wote inaendelea kufuatiliwa. Pia maafisa wa Kenya hawajawaruhusu kutoka katika kituo hicho hadi kipindi cha uangalizi kitakapokamilika. Ebola huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu au mnyama aliyeambukizwa. Shirika la Samaritan's Purse ni miongoni mwa mashirika makubwa yanayosaidia kukabiliana na Ebola nchini DRC kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO). Aina ya virusi vya Bundibugyo, ambayo haina chanjo wala tiba iliyothibitishwa, imeua angalau watu 828 tangu katikati ya Mei. WHO inasema maambukizi bado yanaendelea kusambaa bila kutambuliwa kwa kiwango kikubwa. Graham alisema baada ya kutembelea kituo hicho wiki hii ameridhishwa na vifaa vilivyopo. "Ni kituo cha kisasa kabisa. Iwapo mtu angeugua, hapo ndipo mahali pazuri pa kumpatia matibabu," alisema.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Besigye azirai akiwa kortini, atwaliwa na ambulansi na kuondolewa

KIGOGO wa Upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alizirai Jumatano wakati akihudhuria kusikizwa kwa kesi yake jijini Kampala. Besigye, 70, amekuwa akikabiliwa na mashtaka ya uhaini tangu kunyakwa na maafisa wa Uganda akiwa ziarani Kenya karibu miaka miwili iliyopita. Alitiwa nguvuni pamoja na msaidizi wake Obeid Lutale Novemba 2024 jijini Nairobi. Walikanusha mashtaka na mawakili wao wametaja mashtaka hayo kuwa yaliyochochewa kisiasa. Majaribio kadhaa ya kuwaachilia yamezimwa na utawala wa Rais Yoweri Museveni na mwanawe mkuu wa jeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba. "Besigye alizirai…alikuwa amesimama halafu ghafla akaanguka. Baada ya muda, ambulansi ilikuja ikamchukua na kumpeleka tusikojua," Harold Kaija, afisa wa ngazi za juu katika chama cha Besigye cha PFF aliambia Reuters. SOMA PIA: Karua anyakwa na kuzuiliwa Uganda alikoenda kumwakilisha mwandani wa Besigye kortini Msemaji wa Magereza Frank Baine hakupokea simu alipopigiwa kutafuta maoni yake huku Msemaji wa Mahakama Ereemye Mawanda alisema hakuwa na uwezo wa kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakuwa na habari kuhusu kisa hicho. Kuzuiliwa kwa Besigye kumekuwa kukiibua hasira za wanaharakati nchini humo na kimataifa huku Jumuiya ya Madola ikitaka aachiliwe huru. Mkenya mwanasiasa na wakili wa haiba ya juu Martha Karua alikuwa miongoni mwa utetezi wake kabla ya serikali kumzuilia katika uwanja wa ndege wa Entebbe na kumbadika kuwa 'mgeni asiyetakikana' Wakosoaji wa Museveni, 81, wanasema kuendelea kuzuiliwa kwa Besigye bila dhamana ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na uwindaji wa wakosoaji nchini humo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Dakika za mwisho za afisa polisi aliyejiangamiza kwa risasi kituoni

KIFO cha ghafla cha afisa wa polisi Marjori Bosibori kimewaacha wenzake na jamaa wakiwa na maswali mengi huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichotokea katika saa zake za mwisho. Bosibori, mwenye umri wa miaka 42 na aliyekuwa afisa wa mawasiliano katika Kituo cha Polisi cha Kisii Central, alifariki kutokana na jeraha la risasi kifuani ndani ya chumba cha mawasiliano cha kituo hicho. Afisa huyo alirejea kazini Jumanne baada ya mapumziko mafupi nyumbani kwao, Kisii. Aliripoti kazini kama kawaida, akafanya shughuli zake katika duka moja kubwa mjini Kisii, akazungumza na wenzake na hata kushiriki nao chakula cha mchana. Kwa waliokuwa wakifanya kazi naye, alionekana mtulivu, mwenye bashasha na tayari kuendelea na majukumu yake. Hata hivyo, chini ya saa 24 baadaye, alipatikana amefariki ndani ya chumba cha mawasiliano akiwa na jeraha moja la risasi kifuani huku bunduki aina ya AK-47 ikiwa imelala karibu naye. Kifo chake kimewashtua maafisa wenzake na familia yake. "Aliripoti kazini kama kawaida yake. Hatukushuku chochote. Bado siamini kilichotokea," alisema mmoja wa maafisa aliyekula naye chakula cha mchana siku hiyo. Afisa mwingine alisema Bosibori alikuwa mtu mtulivu na aliyependa kuweka siri maisha yake ya kibinafsi, hali iliyofanya iwe vigumu kubaini alipokuwa akikabiliwa na changamoto. Marafiki zake pia wanamkumbuka kama shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United. Polisi wanachunguza uwezekano kuwa alijitoa uhai, ingawa wanasema bado hawajabaini kilichotokea katika saa zake za mwisho. Kamanda wa Polisi wa Kisii Central, Musa Imamai, alisema Bosibori alimaliza shughuli zake katika duka hilo kabla ya kurejea kituoni muda mfupi baada ya saa sita usiku akiwa na mwenzake. Walipofika kituoni, alimwambia mwenzake kuwa anaelekea chooni. Mwenzake hakushuku chochote. Badala yake, wachunguzi wanaamini aliingia katika chumba cha mawasiliano, ofisi yenye ulinzi mkali ambayo haitumiki sana wakati huo wa usiku, akajifungia kutoka ndani na hakutoka tena. Ilikuwa hadi Jumanne asubuhi afisa mwingine aliporipoti kazini ndipo iligundulika kuwa mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa kwa muda mrefu. Baada ya juhudi za kuufungua kugonga mwamba, maafisa walivunja mlango. Ndani walimkuta Bosibori ameketi kwenye kiti bila uhai akiwa na jeraha la risasi kifuani huku bunduki ya AK-47 ikiwa sakafuni karibu naye. "Tulimkuta akiwa ameketi na damu ikitoka kwenye jeraha la risasi. Uchunguzi wa awali unaonyesha alipigwa risasi moja kifuani na risasi hiyo ikatokea mgongoni," alisema Bw Imamai. Tukio hilo liliwaacha hata maafisa wenye uzoefu mkubwa wakiwa na mshtuko. Polisi walipata bunduki hiyo, ganda moja la risasi, magazini yenye risasi 29, ufunguo wa ofisi, simu tatu za mkononi na dawa mbalimbali. Bosibori alikuwa bado amevaa sare zake za polisi. Bw Imamai alisema alikuwa miongoni mwa maafisa wachache walioaminiwa kufanya kazi katika chumba cha mawasiliano kutokana na nidhamu na uadilifu wake. "Hii ni ofisi muhimu na ni maafisa wachache pekee wanaoruhusiwa kufanya kazi humo. Bosibori alikuwa mmoja wao," alisema. Aliongeza kuwa wachunguzi wanachunguza kila upande wa maisha yake, ikiwemo iwapo kulikuwa na matatizo ya kifamilia au ya kibinafsi ambayo huenda yalichangia mkasa huo. "Kufikia sasa hatuna fununu zozote kuhusu kilichosababisha kile kinachoshukiwa kuwa kujiua kwake," alisema. Mwili wake ulihamishwa hadi mochari ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii ambako unatarajiwa kufanyiwa uchunguzi kubaini chanzo kamili cha kifo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 9 hours ago

Serem arejesha nyota ya Kenya Michezo ya Madola

KENYA imepata sababu mpya ya kuamini kuwa inaweza kurejesha ubabe wake katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi kwa wanaume baada ya ushindi wa kuvutia kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Glasgow, Scotland. Edmund Serem, mwenye umri wa miaka 18 na mshindi wa medali ya shaba katika Riadha za Dunia 2025, aliiongoza Kenya kutwaa nafasi zote tatu za juu mbele ya bingwa wa dunia Geordie Beamish wa New Zealand. Serem alishinda kwa muda wa dakika 8:18.23, Simon Koech alimaliza wa pili huku Leonard Bett akifunga ushindi wa Kenya kwa nafasi ya tatu baada ya kurejea kutoka wakati mgumu wa majeraha. Kwa Serem, ushindi huo ulikuwa zaidi ya medali ya dhahabu. Alisema alifurahia kuletea familia yake na Wakenya wote fahari. Alifichua kuwa baba yake, Joseph Serem, ambaye pia ni kocha wake wa kwanza, alimpa motisha kubwa kupitia simu nyingi na ujumbe wa kumtia moyo kabla ya mbio. Ujumbe wa mwisho wa baba yake ulikuwa: "Nenda mwanangu, endelea. Nakupenda." Maneno hayo yalimbeba hadi ushindi. Hii ni mara ya sita kwa Kenya kutwaa nafasi zote tatu katika mbio hizi kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola. Tangu Ben Jipcho alipoanza historia hiyo mwaka 1974, Kenya imeendelea kutawala mbio za kuruka viunzi, ikishinda taji hilo mara 11 kupitia wanariadha mashuhuri kama Henry Rono, Ezekiel Kemboi, Richard Mateelong na Abraham Kibiwot. Ingawa Ethiopia na Morocco hazikushiriki mashindano haya, ushindi wa Serem una uzito mkubwa kwani alimpiku bingwa wa dunia Beamish kwa tofauti kubwa ya sekunde saba. Kenya bado ndilo taifa lililofanikiwa zaidi katika mbio hizi kwenye Mashindano ya Dunia ikiwa na medali 13 za dhahabu, lakini imekuwa katika kipindi cha ukame tangu Conseslus Kipruto alipotwaa taji lake la pili mwaka 2019. Mwaka 2025, Beamish aliandika historia kwa kutwaa ubingwa wa dunia mbele ya Soufianne El Bakkali. Hata hivyo, Serem alitoa dalili za mafanikio kwa kushinda medali ya shaba katika mashindano hayo akiwa na miaka 17 pekee, akionyesha uwezo wa kushindana na wanariadha bora duniani. Maendeleo yake yamekuwa ya haraka. Mwaka 2024 alitwaa dhahabu ya Dunia kwa wanariadha chini ya miaka 20. Mwaka 2025 akashinda shaba ya Dunia katika msimu wake wa kwanza wa wakubwa, na sasa mwaka 2026 ametwaa ubingwa wa Jumuiya ya Madola baada ya kumshinda bingwa wa dunia anayetawala. Safari ya Serem inaonyesha Kenya inaweza kuwa imepata mrithi wa nyota waliotangulia katika mbio za kuruka viunzi. Ikiwa ataendelea kuwa na afya njema, uthabiti na maendeleo haya, anaweza kuiongoza Kenya kurejesha ubingwa wa dunia mwaka 2027 na kufufua matumaini ya taifa katika moja ya mbio ambazo kwa muda mrefu zimekuwa alama ya mafanikio ya riadha za Kenya.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

MAONI: Bila kuwa na 'mwanajeshi mtiifu' Kindiki, Ruto atapoteza pakubwa uchaguzini

MATAMSHI ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuwa hawezi kutoka kwa serikali ni jambo zito sana. Kwanza ni sauti inayotoka kwa mwanajeshi mtiifu kwa Rais William Ruto. Alikuwa kimbilio na chaguo lake la kwanza baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua. Gachagua mwenyewe amechafua anga ya Rais Ruto mlima Kenya sehemu iliyochangia pakubwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa 2022. Ila sasa habari zimemfikia kuwa waziri Wycliffe Oparanya huenda ndiye atakayekuwa mgombea mwenza wa Ruto. Hesabu hii ya Rais ikiwa itatekelezwa inaweza kumpa majeraha makubwa kuliko angesalia na Kindiki. Ni wazi kuwa Gachagua amekimbia na idadi kubwa ya wapiga kura. Swali ni je, Oparanya ataweza kumletea Rais Ruto kura zaidi? Jibu la wazi ni kuwa huenda matokeo yakawa mabaya zaidi kutokana na msisimko wa seneta Edwin Sifuna. Oparanya anakabiliwa na upinzani mkubwa kwanza kutoka kwa gavana wake Farnandes Barasa ambaye anadhania kuwa hamtakii mema kwa kuungana na wapinzani wake katika kinyang'anyiro cha ugavana mwaka 2027. Sasa Rais Ruto atakuwa na kazi ya kuwapatanisha awali ndipo waanze kuzunguka naye nchini. Ilivyo ni kuwa Oparanya hana misuli ya kusukuma kampeni za kitaifa jinsi alivyo Kindiki. Ikiwa Kindiki na Ruto wataachana basi pacha waliovumiliana katika mateso watakuwa wametengana. Ikumbukwe Kindiki alikuwa naibu spika wa bunge la seneti na akaondolewa mamlakani na upande wa Rais Uhuru Kenyatta kwa sababu ya ushirika wake na Ruto. Wote wamekuwa na misiba tofauti ya kisiasa lakini kilio ni kimoja. Katika kampeni za mwaka 2022 Profesa Kindiki ndiye aliyekuwa wakala mkuu wa Ruto kule Bomas. Alikubali wadhifa huo licha ya kunyimwa nafasi kuwa mgombea mwenza wa Ruto licha ya wanachama kumdhania kuwa angekuwa chaguo bora. Hii inatoa sifa ya mtu mvumulivu ila wakati mwingine anajulikana kama 'fireman". Wapo wanaosema kuwa matokeo ya Ol Kalou yamemfanya Rais kumdhania Kindiki kuwa mtu asiyesukuma ajenda ya mlima kwa dhati ya moyo wake. Jambo lisilo na mjadala ni kuwa ikiwa Ruto atabadilisha mgombea mwenza kutoka kwa Kindiki basi hata asili mia 30 itakuwa vigumu kupata kutoka mlima Kenya. DCP itamega sehemu kubwa ya UDA Rais akose uwakilishi wa kitaifa. Kwa waziri Oparanya ngoma hiyo ni kubwa kumzidi. Ana kibarua kwanza cha kuzima wimbi la Sifuna na gavana Natembeya ambalo limewameza Spika Moses Wetangula na Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi. Kwa ufupi ni heri Kindiki kuliko Oparanya. Paul Nabiswa ni mhariri, NTV

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 11 hours ago

Mahakama yakataa ombi la mwanaharakati kuahirisha kura za 2027

MAHAKAMA Kuu jijini Nairobi imekataa ombi la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa 2027 hadi Katiba ya 2010 ifanyiwe marekebisho makubwa, ikiwemo kutathmini mihula ya viongozi na kuundwa kwa afisi ya Kiongozi wa Upinzani yenye mamlaka ya kutathmini utendakazi wa serikali. Jaji Patricia Nyaundi aliamua kuwa mabadiliko ya Katiba hayawezi kufanikishwa kupitia mahakama bali lazima yafuate taratibu zilizowekwa na Katiba. Alisema mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu mlalamishi hakufuata njia halali za marekebisho ya Katiba. Kesi hiyo iliwasilishwa na Bernard Mwanzia dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Mwanasheria Mkuu, Spika wa Bunge la Kitaifa na Spika wa Seneti. Bw Mwanzia alitaka maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yasimamishwe akidai Katiba ya sasa ina mapungufu yanayodidimiza umoja wa kitaifa, utawala bora na uthabiti wa uchumi. Alidai kuwa masuala kama mpangilio wa uchaguzi, mihula ya viongozi kuhudumu, matumizi ya lugha za mama katika mabunge ya kaunti, uwakilishi wa viongozi waliochaguliwa, kuhifadhi utamaduni wa Kenya na haki ya maandamano yanahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika. Iwapo ombi hilo lingefaulu, maandalizi yote ya uchaguzi mkuu yangesimamishwa hadi kukamilika kwa mchakato wa marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, IEBC ilipinga kesi hiyo ikisema Katiba tayari imeweka utaratibu wa kuifanyia marekebisho kupitia Bunge au mpango wa kuwashirikisha wananchi. Jaji Nyaundi alikubaliana na hoja hiyo akisema mlalamishi alikimbilia mahakamani kabla ya kutumia njia zinazotambuliwa kikatiba. "Katiba imeweka njia ya wazi, ya kipekee na inayojitekeleza ya kuifanyia marekebisho, na utaratibu huo lazima uheshimiwe," akasema. Bw Mwanzia pia alikuwa akipendekeza kuanzishwa kwa afisi ya Kiongozi wa Upinzani iliyo na mamlaka ya kutathmini utendakazi wa serikali, kupitia upya mfumo wa ugatuzi na uwakilishi bungeni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 12 hours ago

Mashine hii mahuluti inafanya shughuli kibao shambani kuwa rahisi

KILIMO cha usahihi [Precision Agriculture kwa Kimombo] kinaendelea kupata nguvu barani Afrika huku teknolojia zake za utekelezaji zikinuia kuwasaidia wakulima wadogo kuongeza kiwango cha uzalishaji mazao kwa kutumia mashine nyepesi na rahisi ila zenye uwezo mkubwa wa utendaji. Moja ya teknolojia bunifu zilizovutia wakati wa makala ya 12 ya Maonyesho ya Teknolojia za Kilimo Afrika (Agritec Africa) wiki jana ni mashine inayoweza kufanya kazi anuwai za shambani. Mashine hiyo Multipurpose Power Tiller imebuniwa na mjasiriamali barobaro kutoka India, Shubham Patel, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Alphachem yenye makao yake Gujarat. "Mashine hii inampa mkulima uwezo wa kuendesha shughuli mbalimbali kwa kutumia kifaa kimoja badala ya kununua vingi tofauti," Patel, 22, aliambia Akili Mali wakati wa maonyesho hayo yaliyofanyika Juni 17 hadi 19 katika jumba la mikutano la kimataifa la Kenyatta (KICC), Nairobi. Mashine hiyo inaweza kutayarisha shamba, kulima, kupanda mbegu kwa kuzingatia nafasi na kina sahihi, kunyunyiza dawa ya kuua wadudu na magonjwa, kukatakata mimea ya malisho na hata kupiga maji kwa ajili ya unyunyizi. Hali kadhalika, mtambo huu unaweza kuunganishwa kwa vifaa vya upanzi wa mimea kama mahindi, mtama, vitunguu, njugu na vitunguu. Patel aeleza kuwa alitumia zaidi ya miaka mitatu na nusu kufanya utafiti na kuboresha mashine yake kabla kuizindua rasmi sokoni mwaka jana. Anasema madhumuni yake yalikuwa kutengeneza mashine inayowezesha wakulima kufanya kazi kwa wakati unaofaa, jambo ambalo ni msingi wa kilimo cha usahihi. "Wakulima wengi wadogo hawawezi kumudu gharama ya kununua au kukodi trekta na mashine kwa kila kazi. Mashine hii inawawezesha kufanya shughuli nyingi kwa kutumia kifaa kimoja na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji," asema. Alihoji kwamba visa vya ucheleweshwaji wa shughuli za kilimo kama kulima, kupanda au kupalili hutokana pakubwa na wakulima kusubiri mashine za kukodi. Power Tiller hii hutumia injini ya dizeli na inaweza kuchapa kazi katika ekari 10 hadi 15 kwa siku kutegemea shughuli inayotekelezwa. "Pia imeundwa kwa vipuri vinavyopatikana kwa urahisi na mchakato wake wa utengenezaji ni wa kawaida tu," alieleza Patel. Kwa sasa Alphachem huunda karibu mashine 100 kila mwezi. Wakati wa maonyesho ya Agritec Africa 2026 mashine hiyo ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya Sh420,000 ikiwa na vifaa vyake vyote. Mkurugenzi huyo alisema licha ya bei hiyo kuonekana kubwa ni nafuu kuliko kununua mashine tofauti za kulima, kupanda, kunyunyizia dawa, kukata mimea ya malisho na kupiga maji. Alidokeza kuwa wazo la kubuni mashine hiyyo lilitokana na ziara alizofanya katika nchi mbalimbali za Afrika. Alibaini kuwa mashamba mengi yanaendelea kugawanywa kuwa madogo kutokana na urithi wa kifamilia, hali ambayo imefanya matumizi ya matrekta makubwa kutofaa kwa wakulima wengi wa mashamba madogo. "Kilimo cha usahihi kinahitaji mashine zinazoendana na saizi ya shamba na zinazoweza kutekeleza kazi kwa urahisi na ufanisi pasipo kuongezea mkulima gharama," akaongeza. Waziri wa Kilimo na Mifugo Mutahi Kagwe, ambaye alifungua rasmi maonyesho hayo, alihimiza wakulima kukumbatia teknolojia na mashine za kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao na mapato, jambo ambalo pia litavutia vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo kama biashara. "Mashine za bei nafuu zinaweza kununuliwa au kukodishwa na vyama vya ushirika au makundi ya wakulima, na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisasa za kilimo," Kagwe alisema. Mbali na mashine hiyo Alphachem pia huuza pampu za kupiga maji, mashine za kukatakata malisho na vifaa vya kupanda mbegu katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania, Zambia, Ghana, Angola, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 13 hours ago

Ushirikiano wa mama na mwanawe ulivyotia nguvu mradi wao wa ufugaji sungura

TANGU akiwa kijana mdogo Francis Karanja alivutiwa na shughuli ya kufuga sungura. Alipokuwa darasa la tano alimpa mamake, Rachel Chebet, ombi moja: amnunulie sungura kadha afuge ili aboreshe somo lake la kilimo katika mtaala mpya wa elimu ya umilisi na utendaji (CBE). Mamake akaahidi kumnunulia baadaye kwani mahali walipoishi wakati huo hapakuwa na nafasi kubwa ya kufanya ufugaji wowote. Mwaka 2024 Chebet alinunua mabati, mbao, nyaya za kuweka ua, misumari na vifaa vingine akajenga vyumba vidogo tisa vya sungura kwa gharama ya Sh10,000. Pia alinunua sungura wanne - ndume wawili na jike wawili kwa Sh500 kila moja. Karanja, 15, ambaye sasa yuko darasa la nane katika shule ya Michinda mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru, asema ilikuwa furaha tele mama alipomtimizia ombi lake. "Sungura walinunuliwa wakati wa likizo na hilo lilinipa fursa nzuri ya kuwatunza," aeleza. [caption id="attachment_190590" align="alignnone" width="2560"] Francis Karanja, 15, mwanafunzi wa Gredi ya Nane katika shule ya Michinda, Elburgon ambaye ni mfugaji sungura. Picha|John Njoroge[/caption] Baada ya miezi mitatu sungura mmoja alizaa wana watano na mwingine saba. Karanja anapokuwa shuleni mamake ndiye huchukua jukumu la kutunza sungura hao. Pia wanakusanya mkojo na kinyesi cha mifugo hao kutengeneza mbolea asili ili kutumia katika shamba lao dogo la nyumbani. Mkojo wanakusanya takriban lita 10 hadi 20 kila wiki. Bidhaa hii ina nitrojeni nyingi na ni kiungo bomba katika kuunda mbolea asilia, na huuzwa kama andazi moto. Hivyo, baada ya kumimina kiwango wanachohitaji kuunda mbolea asili yao, mkojo ambao husalia wanawauzia wakulima wa eneo hilo Sh70 kila lita. Kipindi cha ujauzito cha sungura huwa kati ya siku 28 na 35. Hata hivyo, Chebet na mwanawe wameweka ratiba ili kwamba sungura wa kike anajamiiana na ndume baada ya miezi mitatu, ili kuzuia wana wengi kuzaliwa kila mara hasa wakati wa kiangazi ambapo ni vigumu kupata lishe yao ya kutosha. Mbali na kuuza mkojo, Karanja anasema wao pia huchinja sungura hao kupata nyama. "Baada ya muda fulani sungura wakiongezeka kuwa wengi sana hasa wakati wa kiangazi malisho yakididimia, mama huchinja kadha tunatumia kutengeneza mchuzi nyumbani. Mchuzi wa nyama ya sungura ni mtamu sana," aeleza kwa itabasamu. Kwa mujibu wa afisa wa mifugo eneo la Kuresoi Kaskazini, Nicholas Rono, ufugaji sungura ni tija tosha. Mfugaji anahitaji tu kuhakikisha amejenga vyumba vizuri vya malazi, vinasafishwa kila wakati na kuzuia unyevunyevu kwani huleta magonjwa kama vile nimonia ambayo husababishwa na baridi. "Sungura pia huvamiwa na utiriri kwenye kichwa, mapua na masikio, tatizo ambalo hufanya wajikune sana kwenye ngozi na kuwaletea mwasho mkali. Kuna dawa ya unga ambayo wafugaji wanahitaji kupaka sehemu hizo ili kuzuia tatizo hilo," aeleza Rono. Anaongeza kuwa lishe ya sungura inafaa kuwa bora yenye virutubisho kamili na kiwango cha kutosha, hasa kwa vijike waliojifungua kwani baadhi hugeuka kula wanawao wakilemewa na njaa. Karanja huuza sungura wake kwa ajili ya ufugaji au nyama. Sungura aliyekomaa huwa kati ya Sh500 na Sh700 kulingana na saizi, na Sh300 kwa mwana wa sungura. "Ninatumia pesa hizo kuongeza lishe, na senti zinazosalia ninanunua vifaa vyangu vya shule. Kielimu mradi huu umefanya somo la kilimo kuwa kati ya zile ninazopenda zaidi shuleni," asema. [caption id="attachment_190591" align="alignnone" width="2560"] Kijana Francis na mamake Rachel Chebet wakikusanya mkojo wa sungura ulio na soko bomba ambapo lita moja huuzwa Sh70 sokoni. Picha|John Njoroge[/caption] Sungura hawana misimu pevu au kavu hivyo mfugaji hupata mauzo wakati wowote kulingana na hitaji la soko. Katika hatua ya kukuza ujuzi wa usimamizi wa biashara, anadokeza kwamba kwa usaidizi wa mamake wanaweka kila siku kumbukumbu za taarifa za ufugaji wa sungura wao kila siku. Ili kusawazisha kazi ya shule na mradi wake wa sungura, Karanja ana ratiba ya kibinafsi ili kufanya mambo kwa mpangilio na urahisi. Kwa sasa ana zaidi ya sungura 100 huku lengo likiwa kufikisha zaidi ya sungura 600 ifikapo Desemba. "Tamanio langu ni kufuga sungura zaidi ili kuvuna mkojo ya kuunda mbolea asili ya kutosha kukidhi mahitaji ya wakulima msimu wa upanzi, hasa katika kilimo cha viazi na mboga," asema. Mamake asema sio tu manufaa ya kifedha wanapata kutoka kwa mradi. "Ufugaji pia umemfunza maadili ya nidhamu, uwajibikaji na kumzuia kutangamana na vijana watundu kwani huwa ana shughuli nyingi za kufanya anaporejea jioni kutoka shule au wakati wa likizo," aeleza Chebet.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 14 hours ago

Kisa cha afisa wa DCI kudungwa kisu chaibua hofu ya ujasiri wa wahalifu

ONGEZEKO la mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi katika Kaunti ya Lamu limezua wasiwasi kuhusu iwapo makundi ya wahalifu yanazidi kupata ujasiri licha ya juhudi za miaka mingi zilizolenga kurejesha amani katika kaunti hiyo. Ndani ya kipindi cha miezi miwili pekee, angalau maafisa watatu wa usalama wameshambuliwa. Tukio la hivi majuzi zaidi lilimhusu afisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ambaye alishambuliwa na kujeruhiwa na mwanamume alipokuwa akitembea katika eneo la Langoni, kisiwani Lamu, mwendo wa saa nne asubuhi Ijumaa iliyopita. Mashahidi walisema afisa huyo alichomwa kisu tumboni, shingoni na mbavuni kabla ya mshambuliaji kutoroka. Afisa huyo bado amelazwa hospitalini akiendelea kupokea matibabu. Kwa mujibu wa mashahidi, alikuwa akitembea pamoja na mwenzake, wote wakiwa wamevalia nguo za kiraia. Ghafla, mwanamume aliwagonga kwa nguvu. Mmoja wa maafisa hao alirudi nyuma kwa tahadhari, akamshika mkono mwanamume huyo na kumuuliza kwa ukali kwa nini alikuwa na fujo. Badala ya kuomba radhi, mwanamume huyo alionyesha uhasama, akapaza sauti na kumsukuma afisa huyo. Bw Abdi Osman, mchuuzi, alisema walianza kupigana ghafla kwa karibu dakika nne. Afisa wa pili aliingilia kati ili kumvuta mshambuliaji huyo. "Hata kabla ya maafisa hao wawili kutoa bunduki zao ili kudhibiti hali, mshambuliaji alitoa kwa kasi kisu alichokuwa amekificha kiunoni na kumchoma mmoja wa maafisa. Kisu kilimdunga tumboni, mbavuni na shingoni," alisema Bw Osman. Bw Simon Kadenge, shahidi mwingine, alisema mara tu afisa wa pili alipoona mshukiwa ametoa kisu na kumchoma mwenzake, alikimbia kutoka eneo la tukio. "Eneo hilo liliendelea kuvutia wananchi wengi. Walifika na kumsaidia afisa aliyejeruhiwa. Kufikia wakati huo, mshukiwa alikuwa tayari ametoweka," alisema. Duru za polisi zilisema maafisa hao wawili wa DCI walikuwa wamehamishiwa eneo hilo karibu wiki moja kabla ya tukio hilo. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu Shadrack Ruto, alikashifu tabia za wananchi ambao wamekuwa wakiwalenga maafisa wa usalama na kuwadhuru akionya kuwa chuma chao kiko motoni. Alisema katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, maafisa watatu wa usalama wamevamiwa na kujeruhiwa na raia katika maeneo ya kisiwa cha Lamu na Hindi. "Mbali na shambulio la Ijumaa mjini Lamu, mwezi mmoja uliopita kuna askari wetu wawili wa akiba (NPR) waliolazimika kumpiga risasi na kumuua mwanamume raia aliyejaribu kuwavamia mjini Hindi akiwa amebeba mkuki na panga. Lazima watu waepuke kushambulia polisi kwani hatutawavumilia kamwe," akasema Bw Ruto. Wanaharakati na wakazi pia walikashifu vitendo hivyo. Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki la Vocal Africa, Bw Hussein Khalid, alisema mashambulio hayo ni ishara ya ongezeko la ukosefu wa usalama unaotendwa na vijana wa eneo hilo kwa muda sasa. "Miaka ya zamani tumewahi kuona hata machifu wakiuawa, vijana wakikatwa miguu na sasa maafisa wa usalama wameanza kudungwa visu. Wizara ya usalama wa Ndani lazima ishuke Lamu kukabiliana na kumaliza tatizo hilo," akasema Bw Khalid. Bi Zeinab Ahmed, mkazi, alitoa wito kwa wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuwakomesha kuingilia makundi ya uhalifu. Naye Afisa wa Haki Africa Mathias Shipeta alisema tatizo la utovu wa usalama linahitaji nyanja zote, zikiwemo zile za siasa kuhusika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 15 hours ago

NCIC yasema itaendelea kufuatilia matamshi ya Duale, Gachagua na wengine sita

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imesema itaendelea na uchunguzi dhidi ya Waziri wa Afya Aden Duale na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu matamshi ya chuki na uchochezi wa kikabila, licha ya wawili hao kutangaza hadharani kwamba hawataitikia wito wa tume hiyo. Mwenyekiti wa NCIC Askofu Kepha Nyamweya, alisema tume hiyo haitaruhusu wanasiasa kuamua namna uchunguzi wake unavyofanywa na kwamba itaendelea kutekeleza wajibu wake bila uoga, upendeleo wala msukumo wa kisiasa. "Kuna wakati wa siasa na kuna wakati wa kazi na hatuwezi kuruhusu mchezo wa aina hiyo. Mtu hawezi kusema atafika mbele ya tume baada ya mwingine kufika. Tutafanya kazi yetu kwa mujibu wa sheria," akasema Bw Nyamweya. Kauli hiyo ilijiri baada ya Bw Duale kusema hatafika mbele ya NCIC hadi pale Bw Gachagua atakapoitwa kwanza kujibu matamshi yake yaliyofasiriwa kuwa ya uchochezi. "Kama hakuna Gachagua, hakuna Duale," alisema waziri huyo, akisisitiza kuwa sheria inapaswa kutumika kwa usawa kwa wote. Hata hivyo, Bw Nyamweya alisema watu wanaochunguzwa hawawezi kuielekeza tume yake jinsi ya kutekeleza majukumu yake. "Tunatoa wito kwa wanaohitajika kufika mbele yetu. Wakikosa kufika, sheria imeweka utaratibu wa kushughulikia hali hiyo. Tutachukua hatua bila mapendeleo," akaongeza. Kwa upande wake, Bw Gachagua ameendelea kutetea matamshi yake aliyosema "watamuua nyoka pamoja na mayai yake," akidai yalikuwa ya kimethali, yakimaanisha kuwashinda kisiasa Rais William Ruto na washirika wake kupitia kura, wala si kutumia vurugu. Alisema iwapo NCIC inahitaji maelezo yake, imuandikie rasmi naye atajibu. Mbali na viongozi hao wawili, NCIC pia imeanzisha uchunguzi dhidi ya Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Gavana wa Busia Paul Otuoma, Naibu Gavana wa Mandera Ali Maalim Mohamud, Mbunge wa Sirisia John Waluke pamoja na Tipape Naini Musa na Dkt Dennis Adison Ouma kwa madai ya matamshi ya chuki na uchochezi. Tume imesisitiza kuwa wote wanaochunguzwa wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi uchunguzi utakapokamilika. Nyamweya alionya kuwa matamshi ya kisiasa nchini yanazidi kuwa makali huku baadhi ya viongozi wakitumia lugha inayowagawa wananchi kwa misingi ya kikabila badala ya kushindana kwa sera. "Lugha inatumiwa kuwafanya wapinzani waonekane maadui badala ya majirani wenye mitazamo tofauti. Hali hii inaweza kuhatarisha umoja wa taifa," alisema. Alieleza kuwa NCIC imepewa mamlaka chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano ya kuchunguza matamshi ya chuki, kuwaita mashahidi, kukusanya ushahidi na kuwasilisha faili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa hatua zaidi. Bw Nyamweya alikanusha madai kwamba tume hiyo inaweza kushinikizwa kisiasa, akisema itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa haki huku ikishirikiana na Baraza la Kidini Kenya kuimarisha juhudi za kuzuia matamshi ya chuki na kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unafanyika kwa amani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Dalili Nyayo za Kijana Wamalwa na Raila zinamwongoza Sifuna

SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna anaendelea kutamba katika ulingo wa siasa. Nyota yake Sifuna inaendelea kung'aa kwenye ramani ya humu nchini kwa mwendokasi wa ajabu. Sifuna ni mwanafunzi mmakinifu wa siasa za watangulizi wake Raila Amollo Odinga na kigogo wa siasa Michael Kijana Wamalwa ambao walionyesha umahiri hata katika wimbi kali la upinzani. Baada ya kubanduliwa katika wadhifa wa katibu mkuu wa chama cha ODM, Seneta Sifuna hajafa moyo. Ufuasi wake Unaendelea kushamiri huku akifanikiwa kupata kibali katika kila eneo analozuru nchini. Hili linashuhudiwa kupitia umati wa watu wanaojitolea kuhudhuria mikutano anayoandaa pamoja na wenzake katika mrengo wa Linda Mwananchi. Safari yake Sifuna katika siasa ni sura ya siasa ya aliyekuwa waziri mkuu na kinara wa ODM Raila Odinga. Raila ndiye mwanasiasa wa pekee aliyelipinga wimbi la chama kikuu cha upinzani cha FORD katika mwaka wa 1994 na baadaye kujiuzulu. Raila alithamini demokrasia na nguvu za wananchi zaidi ya nguvu za dola. Sifuna amehitimu katika chuo cha mwamba aliyegundua kuanza mapema akiwa na nguvu na mvuto kwa wananchi. Hulka yake seneta huyo inachukuliana na yake Kijana Wamalwa ambaye alipendwa na wengi wa wapigakura katika ukanda wa magharibi. Ni wazi kuwa Sifuna ni mmoja wa viongozi walioweza kuwavutia wananchi wengi zaidi kisiasa katika eneo la Magharibi. Siasa yake inatikisa ngome za wanasiasa wakongwe wakiwemo Musalia Mudavadi, Moses Wetang'ula, Wycliffe Oparanya na wengine. Mvutano kati ya Raila na Wamalwa ulichangia FORD Kenya kusambaratika baada ya Jaramogi Oginga kufariki dunia. Raila alionekana kama aliyetaka kurithi chama naye Wamalwa akitaka kuwa kiongozi wa chama hicho. Hatimaye Ford Kenya iligawanyika mara tatu. Hii ndiyo njia ya chama cha ODM baada ya Raila kuondoka. Sharti Sifuna ajichongee kao lake la siasa kwa nyakati zijazo akifahamu kuwa ufuasi na ushabiki humwandama mtu jasiri anayejijengea chama chake. Raila aliviunda vyama kadhaa kama silaha yake dhidi ya serikali. Ni bayana kuwa Sifuna yuko njiani kukiunda chama chake. Tukielekea katika uchaguzi mkuu wa 2027, Sifuna ana nafasi murua ya kujinadi kupewa fursa ya kugombea kiti cha urais au kumpiga pambaja mgombea mwingine kuwania kiti hicho. Kibarua kikubwa ni kuwa kuna wanasiasa wa upinzani ambao huenda hawatampa nafasi hiyo kwa madai ya kukosa tajriba ya kisiasa. Kinachobakia ni kujijenga kisiasa wala si kutafuta ushindi wa kiti cha urais. Kadi yake Sifuna kama mgombea wa urais ni bora hasa kwa ushawishi alio nao kwa vijana na wananchi wanaotaka mabadiliko. Hata hivyo, haijadhihirika iwapo viongozi katika upinzani watakubali kumuunga mkono ama ukosefu wa umoja katika upinzani utalemaza uwezo wake. Sifuna hana la kupoteza upinzani ukishinda au ukikosa kushinda urais. Atakuwa ameuboresha msingi wake wa kisiasa kwa siku za usoni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 17 hours ago

Kindiki kona mbaya tishio kutoka pande tatu zikimuandama

NAIBU wa Rais Prof Kithure Kindiki anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku mjadala kuhusu iwapo atasalia mgombeaji mwenza wa Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 ukizidi kushika kasi na kuzua maoni mseto. Japo amehudumu kwa chini ya miaka miwili tangu achukue nafasi hiyo, Prof Kindiki sasa ana kibarua cha kupambana na changamoto kutoka pande tatu zinazotishia mustakabali wake kisiasa. Mtihani wa kwanza unatokana na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameanzisha kampeni kali katika ukanda wa Mlima Kenya Mashariki, ngome ya kisiasa ya Profesa Kindiki. Baada ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Bw Gachagua ameahidi kufuatilia kila ziara ya Rais Ruto katika eneo hilo kwa mikutano ya kisiasa akinuia kupunguza ushawishi wa serikali kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao. Tangu ateuliwe naibu rais (DP), Prof Kindiki amekuwa akiongoza hafla za kufungua miradi ya maendeleo katika eneo hilo ikiwemo uzinduzi wa barabara, nyumba za gharama nafuu na hata miradi ya kilimo. Baadhi ya wafuasi wake wanasema ziara hizo zimedumisha imani ya wakazi kwamba eneo la Mlima Kenya bado lina sauti serikalini, ila Bw Gachagua anataka kuhakikisha imani hiyo haigeuki kuwa kura kwa Kenya Kwanza 2027. Kibarua cha pili kinatokana na siasa ambazo zinaendelea ndani ya Kenya Kwanza baada ya ushirikiano mpya na ODM. Hii ni kwa sababu viongozi wa ODM wameweka wazi kuwa wanataka nafasi ya naibu rais ikiwa ushirikiano wao na UDA utaendelea kabla na baada ya uchaguzi wa 2027. Baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwemo Naibu Kiongozi Simba Arati na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, wamesema nafasi hiyo inapaswa kutolewa kwa ODM. Chama hicho kimewataja Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Waziri wa Madini Hassan Joho na Wycliffe Oparanya kama wanaotosha kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema msukumo wa ODM unamweka Profesa Kindiki katika hali ngumu kwa sababu Rais Ruto anaweza kulazimika kutathmini kusalia naye au kumwondoa na kutumia nafasi hiyo kuimarisha ushirikiano na ODM. Prof Kindiki amejipata katika hali ngumu zaidi baada ya taarifa kudai kuwa baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakihusishwa na afisi ya naibu rais yamehamishiwa kwa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi. Hata hivyo, Prof Kindiki amekanusha madai hayo na kuyataja kuwa habari za uongo. Mkuu wa Uchumi wa Ubunifu na Miradi Maalum katika Afisi ya Rais Dennis Itumbi naye alisisitiza kuwa majukumu ya kila afisi yamebainishwa kwenye Katiba na sheria, na hakuna mamlaka yaliyoondolewa kutoka kwa Naibu Rais. Licha ya magumu yanayomkabili Profesa Kindiki, wadadisi kadhaa wa kisiasa wanaamini bado ndiye chaguo bora zaidi kwa Rais Ruto. Wanasema ameonyesha uaminifu, utulivu, uwezo na amekuwa akiepuka migogoro ya hadharani na rais, tofauti na waliomtangulia. Mdadisi wa masuala ya kisiasa Steve Ngari anasema Profesa Kindiki ameonyesha sifa zinazotarajiwa kwa afisi yake na anafaa kuendelea kusalia katika kambi ya Rais. Aidha, kura za maoni za Infotrak zimemweka Prof Kindiki kileleni mwa wanaopendelewa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto kwa asilimia 34, akifuatiwa na Gladys Wanga kwa asilimia 11 na Oburu Oginga kwa asilimia tano. Kwa mujibu wa Bw Ngari, kumwondoa Prof Kindiki kunaweza kuwakera wapigakura wa Mlima Kenya Mashariki ambao wanaona nafasi ya naibu rais kama ishara ya ushawishi wao serikalini. "Kazi ya Naibu Rais ni kuhudumu kama msaidizi wa karibu wa Rais. Kindiki ameonyesha sifa ambazo zinamwezesha kuendelea kuhudumu kwa wadhifa," akasema Bw Ngari. Pia, kunaweza kuibua taswira kwamba uaminifu na utendakazi hauthaminiwi ndani ya Kenya Kwanza. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku naye ameendelea kumtetea Prof Kindiki, akisisitiza kuwa hakuna nafasi iliyo wazi ya naibu rais na kwamba, Rais Ruto tayari ameamua mgombea wake mwenza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 28 Jul 2026 11:04:36

Chelsea yahemea saini za wakongwe

CHELSEA inaonekana kubadili mbinu yake ya usajili wa wachezaji baada ya kuelekeza macho kwa wachezaji wazoefu wenye umri uliokomaa. Hii ni baada ya klabu hiyo ya Stamford Bridge kutupia ndoano difenda wa Crystal Palace Maxence Lacroix, straika wa Brighton Danny Welbeck na kiungo wa kati wa Brentford Jordan Henderson. Hatua hiyo ni tofauti na mwelekeo waliochukua miaka minne iliyopita wa kusajili wachezaji chipukizi kwa mikataba mirefu. Baada ya klabu hiyo kununuliwa na BlueCo mwaka 2022, Chelsea ilitumia fedha nyingi kusajili nyota waliokuwa tayari wamejijengea majina makubwa. Raheem Sterling aliwasili kutoka Manchester City akiwa na miaka 27, Kalidou Koulibaly (31) alitua kutoka Napoli ya Italia huku Pierre-Emerick Aubameyang (33) akiingia kutokea Barcelona ya Uhispania. Lakini ukosefu wa mataji ulimgarimu kocha Thomas Tuchel kazi yake. Wakati wa kipindi kirefu cha uhamisho 2022 wamiliki wa BlueCo walipiga abautani kugeukia chipukizi. Aliyefungua ukurasa huo ni Enzo Fernandez kisha wakafuata mastaa wengine ikiwemo Moises Caicedo na Cole Palmer ambao wameonyesha ukwasi wao kwa kiwango fulani. Hata hivyo, kulikuwepo pia mastaa walioishia kuwa moto wa karatasi - Mykhailo Mudryk, Joao Feli na Wesley Fofana. Sasa baada ya miaka minne ya kukamata nafasi ya 12, sita, nne na 10 msimu jana pamoja na mataji 'madogo ya Conference League na Kombe la Klabu Bingwa Duniani, wamiliki wamegeukia tena mastaa wakongwe wenye uzoefu. Lacroix 26, ndiye mwenye umri mdogo kati ya watatu hao kwani Welbeck ana umri wa miaka 35 naye Henderson miaka 36. Chelsea inasemekana kuwa tayari kutoa Pauni milioni 52 (Sh9.2 billioni) kumsajili Lacroix. Naye Welbeck anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na miamba hao kwani amebakisha mwaka mmoja pekee katika mkataba wake Brighton. Iwapo Welbeck atatua Chelsea huenda akachukua nafasi ya Liam Delap, 23, ambaye alisajiliwa kutoka Ipswich Town mwaka jana akiwa mmoja wa washambuliaji waliopigiwa upatu mkubwa kung'ara. Kocha mpya Xabi Alonso, ambaye amewasili kutoka Bayer Leverkusen ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), anasemekana kupendelea kikosi chenye mseto wa chipukizi na wazoefu. Sajili hizi kongwe zikifua dafu mashabiki wa Blues watasubiriwa kuona iwapo watawapaisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (EPL).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 28 Jul 2026 07:05:08

Ndovu 14 wafa kwa njia ya kutatanisha mbugani Amboseli

SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) limeanzisha uchunguzi kuhusu vifo vya kutatanisha vya ndovu 14 katika Mbuga ya Wanyama ya Amboseli mwezi uliopita. Viongozi wa Kaunti ya Kajiado nao wanataka ripoti ya haraka kubaini kilichosababisha vifo vya ndovu hao. Mizoga ya wanyama hao, waliokuwa wa umri na jinsia tofauti, ilipatikana katika maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo ndani ya kipindi cha wiki mbili. Madaktari wa mifugo wa KWS walichukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara ili kubaini chanzo cha vifo hivyo. Afisa mmoja wa KWS, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema ndovu hao walikuwa wakifuatiliwa na madaktari baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa kabla ya kufariki. "Madaktari walijaribu kuwapa matibabu lakini hawakupata nafuu. Mwanzoni ilidhaniwa walikuwa na uchovu wa misuli, lakini matibabu hayakufaulu. Baada ya uchunguzi wa mizoga na ukusanyaji wa sampuli, ilizikwa ndani ya hifadhi," akasema. "Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya tembo kufa kwa muda mfupi katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli," akaongeza. Mkuu wa Mawasiliano wa KWS, Duncan Juma, alisema sampuli zilifikishwa kwa maabara ya Serikali na uchunguzi unaendelea. Vifo hivyo vimewatia wasiwasi viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, ambao wametaka KWS ichapishe mara moja ripoti ya uchunguzi. "Jamii zimeishi na ndovu hao kwa miaka kadhaa. Hatujawahi kushuhudia idadi kubwa namna hii ikifa kwa muda mfupi," akasema Bw Lenku. Seneta wa Kajiado Samuel Seki pia aliikosoa KWS, akiishutumu kwa kutumia kesi mahakamani kuchelewesha uhamishaji wa usimamizi wa mbuga ya Amboseli kwa Serikali ya Kaunti ya Kajiado pamoja na mapato yake.

read more