taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Uganda sasa yatangaza kutokomeza kabisa Ebola nchini mwao
KAMPALA, Uganda: WAZIRI wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, ametangaza rasmi kuwa nchi hiyo haina maambukizi ya Ebola baada ya kudhibiti mlipuko wa hivi karibuni uliowaambukiza watu 20 na kusababisha vifo vya watu wawili. Mkurupuko huo uliotangazwa katikati ya Mei ulihusisha pia watu 15 waliopata maambukizi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo ndiyo kitovu cha ugonjwa huo. DR Congo imeendelea kusajili zaidi ya visa 3,000 vilivyothibitishwa vya Ebola. Baryomunsi alisema Wizara ya Afya ilifuatilia ugonjwa huo kote nchini tangu mkurupuko ulipoanza na ikashawishiwa kuwa sasa maradhi hayo hayapo. "Katika kipindi chote hicho, wizara iliendelea na kutathmini hali nchini kote na hakuna kisa kipya cha Ebola kilichogunduliwa," akasema. Tangazo hilo ni afueni kwa Uganda baada ya juhudi za muda mrefu za kudhibiti maambukizi na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari katika eneo la Afrika Mashariki.
read moreOther Headlines
taifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 58 minutes ago
Chelsea yahemea saini za wakongwe
CHELSEA inaonekana kubadili mbinu yake ya usajili wa wachezaji baada ya kuelekeza macho kwa wachezaji wazoefu wenye umri uliokomaa. Hii ni baada ya klabu hiyo ya Stamford Bridge kutupia ndoano difenda wa Crystal Palace Maxence Lacroix, straika wa Brighton Danny Welbeck na kiungo wa kati wa Brentford Jordan Henderson. Hatua hiyo ni tofauti na mwelekeo waliochukua miaka minne iliyopita wa kusajili wachezaji chipukizi kwa mikataba mirefu. Baada ya klabu hiyo kununuliwa na BlueCo mwaka 2022, Chelsea ilitumia fedha nyingi kusajili nyota waliokuwa tayari wamejijengea majina makubwa. Raheem Sterling aliwasili kutoka Manchester City akiwa na miaka 27, Kalidou Koulibaly (31) alitua kutoka Napoli ya Italia huku Pierre-Emerick Aubameyang (33) akiingia kutokea Barcelona ya Uhispania. Lakini ukosefu wa mataji ulimgarimu kocha Thomas Tuchel kazi yake. Wakati wa kipindi kirefu cha uhamisho 2022 wamiliki wa BlueCo walipiga abautani kugeukia chipukizi. Aliyefungua ukurasa huo ni Enzo Fernandez kisha wakafuata mastaa wengine ikiwemo Moises Caicedo na Cole Palmer ambao wameonyesha ukwasi wao kwa kiwango fulani. Hata hivyo, kulikuwepo pia mastaa walioishia kuwa moto wa karatasi - Mykhailo Mudryk, Joao Feli na Wesley Fofana. Sasa baada ya miaka minne ya kukamata nafasi ya 12, sita, nne na 10 msimu jana pamoja na mataji 'madogo ya Conference League na Kombe la Klabu Bingwa Duniani, wamiliki wamegeukia tena mastaa wakongwe wenye uzoefu. Lacroix 26, ndiye mwenye umri mdogo kati ya watatu hao kwani Welbeck ana umri wa miaka 35 naye Henderson miaka 36. Chelsea inasemekana kuwa tayari kutoa Pauni milioni 52 (Sh9.2 billioni) kumsajili Lacroix. Naye Welbeck anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na miamba hao kwani amebakisha mwaka mmoja pekee katika mkataba wake Brighton. Iwapo Welbeck atatua Chelsea huenda akachukua nafasi ya Liam Delap, 23, ambaye alisajiliwa kutoka Ipswich Town mwaka jana akiwa mmoja wa washambuliaji waliopigiwa upatu mkubwa kung'ara. Kocha mpya Xabi Alonso, ambaye amewasili kutoka Bayer Leverkusen ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), anasemekana kupendelea kikosi chenye mseto wa chipukizi na wazoefu. Sajili hizi kongwe zikifua dafu mashabiki wa Blues watasubiriwa kuona iwapo watawapaisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (EPL).
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 3 hours ago
Shughuli za Nation Media Group Uganda kurejelewa kufuatia idhinisho la Rais Museveni
SHUGHULI za Nation Media Group nchini Uganda sasa zitarejelewa baada ya idhinisho kutoka kwa Rais Museveni, kampuni ya Taarifa Group imetangaza. Akitoa tangazo hilo, mwenyekiti Rostam Azizi alieleza kwamba shirika hilo limejitolea kuendeleza uanahabari ambao unagusa maisha ya wananchi. Maelezo zaidi yanafuata...
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 4 hours ago
Ndovu 14 wafa kwa njia ya kutatanisha mbugani Amboseli
SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) limeanzisha uchunguzi kuhusu vifo vya kutatanisha vya ndovu 14 katika Mbuga ya Wanyama ya Amboseli mwezi uliopita. Viongozi wa Kaunti ya Kajiado nao wanataka ripoti ya haraka kubaini kilichosababisha vifo vya ndovu hao. Mizoga ya wanyama hao, waliokuwa wa umri na jinsia tofauti, ilipatikana katika maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo ndani ya kipindi cha wiki mbili. Madaktari wa mifugo wa KWS walichukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara ili kubaini chanzo cha vifo hivyo. Afisa mmoja wa KWS, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema ndovu hao walikuwa wakifuatiliwa na madaktari baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa kabla ya kufariki. "Madaktari walijaribu kuwapa matibabu lakini hawakupata nafuu. Mwanzoni ilidhaniwa walikuwa na uchovu wa misuli, lakini matibabu hayakufaulu. Baada ya uchunguzi wa mizoga na ukusanyaji wa sampuli, ilizikwa ndani ya hifadhi," akasema. "Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya tembo kufa kwa muda mfupi katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli," akaongeza. Mkuu wa Mawasiliano wa KWS, Duncan Juma, alisema sampuli zilifikishwa kwa maabara ya Serikali na uchunguzi unaendelea. Vifo hivyo vimewatia wasiwasi viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, ambao wametaka KWS ichapishe mara moja ripoti ya uchunguzi. "Jamii zimeishi na ndovu hao kwa miaka kadhaa. Hatujawahi kushuhudia idadi kubwa namna hii ikifa kwa muda mfupi," akasema Bw Lenku. Seneta wa Kajiado Samuel Seki pia aliikosoa KWS, akiishutumu kwa kutumia kesi mahakamani kuchelewesha uhamishaji wa usimamizi wa mbuga ya Amboseli kwa Serikali ya Kaunti ya Kajiado pamoja na mapato yake.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 6 hours ago
Iran yasema ingali inadhibiti Hormuz licha ya kunyeshewa mabomu na Amerika wiki 2 mfululizo
DUBAI, UAE: IRAN imesema ingali inadhibiti Mkondo-Bahari wa Hormuz wala haikusudiii kurejelea mazungumzo ya amani na Amerika baada ya Rais Donald Trump kusitisha kampeni ya mabomu ya wiki mbili ambayo wandani wake walimweleza imetimiza azma yake. Kufuatia mashambulizi makali ya mabomu siku 13 mfululizo yaliyosababisha Tehran kulenga ngome za Amerika kulipiza kisasa, Trump alisimamisha kampeni hiyo wikendi. Iran ilisema itasitisha mashambulizi yake binafsi kwa kipindi ambacho Amerika itasimamisha. Mwisho wa kampeni ya mabomu ya Amerika ulisababisha bei za mafuta kuporomoka kwa matumaini kuwa michakato ya usambazaji bidhaa iliyotatizwa duniani itarejelea shughuli zake. Lakini kwa ishara kuwa Tehran huenda tayari inafanyia majaribio mkataba mpya wa kusitisha vita, Jordan iliripoti kuangusha droni mbili na duru za usalama za Iraqi zikasema droni hizo zililenga wapiganaji wa Wakurdi wa Iran eneo la Iraq Kaskazini. Majeruhi hawakuripotiwa katika visa hivyo. Uamuzi wa Trump kusitisha kampeni unaashiria ushauri kutoka kwa jeshi lake kwamba mabomu, yaliyonuiwa kuvunja udhibiti wa Irani kwenye mkondo, yamefikia upeo ambao yangeweza kufanikisha, kulingana na afisa wa Amerika na ripoti kadhaa za vyomvo vya habari. Afisa wa Amerika alisema kwamba makamanda wa jeshi walimshauri rais kwamba wameishiwa na vituo vya kushambulia. Mwenyekiti wa Wakuu wa Wahudumu, Jenerali Dan Caine, alielezea wasiwasi kuhusu kumalizika kwa silaha za kujikinga angani, alisema afisa. Balozi wa Amerika kwa Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alisema Jumapili kuwa Trump alisitisha kampeni kuruhusu majadiliano. Trump, Waziri wa Masuala ya Kigeni Marco Rubiona maafisa wengine wa Amerika wameelezea Iran kama "inayosihgi kuwepo mkataba." Lakini msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Iran, Esmail Baghaei, alisema katika kikao cha vyombo vya habari jana kwamba Iran haijaomba kurejelea mazungumzo ya amani na Amerika. Jumbe bado zilitumwa kati ya pande husika kupitia wapatanishi na Iran haikutelekeza diplomasia, lakini "ripoti kuhusu Iran kuomba majadiliano na Amerika ni za uongo," alisema Baghaei. "Hii haimo katika DNA yetu." Tehran vilevile iliashiria ingali inadhibiti mkondo muhimu zaidi wa maji na masoko ya nishati duniani.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 9 hours ago
Walimu wapata matumaini baada ya TSC kutangaza nafasi 34,000 za kuwapandisha vyeo
TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) imetangaza nafasi 34,016 za kupandisha walimu vyeo katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya mafunzo ya walimu. Waliopandishwa wapo katika madaraja 30, kuanzia Mwalimu Mkuu Mwandamizi II (Senior Teacher II) hadi Mkuu wa Shule (Chief Principal). Walimu wametakiwa watume maombi ya kazi hizo kupitia mtandao wa TSC kabla ya Agosti 10, 2026, huku TSC ikisisitiza kuwa maombi yanayowasilishwa moja kwa moja kupitia kwa mwalimu kufika na stakabadhi katika afisi za tume hayatakubaliwa. "Walimu wenye sifa zinazohitajika wanapaswa kutuma maombi yao kupitia tovuti ya TSC www.teachersonline.go.ke kabla ya Jumatatu, Agosti 10, 2026. Hakuna kuwasilisha stakabadhi katika afisi za TSC," ilisema TSC katika tangazo lake. Hatua hiyo inawapa matumaini walimu wengi ambao wamekwama katika madaraja yale yale kwa miaka mingi licha ya kutimiza masharti ya kupandishwa vyeo. Serikali imetenga Sh2 bilioni katika bajeti ya sasa kufanikisha shughuli hiyo. Hivi majuzi, TSC iliambia Bunge kuwa walimu 178,871 wa shule za msingi na upili wameendelea kubaki katika madaraja yao kutokana na uhaba wa fedha kwa muda mrefu. Walimu wengi waliokwama wako katika daraja la C3 kwa sekondari na C1 kwa shule za msingi. Kati ya nafasi zilizotangazwa, nyingi zinalenga madaraja ya kati ya taaluma. Kuna nafasi 13,490 za Senior Teacher II, nafasi 5,956 za Senior Master IV, na nafasi 4,210 za Senior Teacher I, ambazo zinatarajiwa kuwapa maelfu ya walimu nafasi ya kupanda vyeo. Tangazo hilo limekuja wakati Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) ukiendelea kushinikiza TSC kutangaza nafasi za kupandisha walimu 135,000 ambao wamekwama kwa muda mrefu katika madaraja yao ya kazi. Katibu Mkuu wa Kuppet, Akello Misori, alisema walimu wengi wamekuwa wakisubiri kupandishwa vyeo kwa miaka mingi licha ya kustahili. Kwa upande mwingine, wakuu wa shule kupitia chama cha KESSHA pia wameitaka TSC kuharakisha mchakato huo, wakisema walimu wakuu wengi hasa walio katika daraja la D3 wamevunjika moyo kwa kukosa nafasi za maendeleo ya kazi. Mwenyekiti wa TSC, Dkt Jamleck Muturi, alisema serikali imewapandisha vyeo walimu 274,285 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, lakini akakiri kuwa wengi bado wamekwama katika madaraja yao. TSC pia ilisema waliofaulu katika mahojiano watatakiwa kuwasilisha hati halali za zinazozingatia masharti ya Sura ya Sita ya Katiba kabla ya kuteuliwa rasmi, na watapangiwa shule ambako nafasi hizo zinapatikana.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 10 hours ago
Raia wa kigeni apigania mali baada ya ndoa yake na mkewe Mkenya kuvunjika
RAIA wa Ireland aliyekuwa amehamia Kenya kwa matumaini ya kuanza maisha mapya na mwanamke aliyefahamiana naye kupitia mtandao sasa amejikuta akihusika katika kesi tatu mahakamani zinazohusu mamilioni ya pesa, mali na kuvunjika kwa ndoa yao. Bw Joel Patrick Fitzpatrick anasema aliuza mali aliyorithi kutoka kwa marehemu mama yake nchini Ireland na kuhamia Watamu, Kaunti ya Kilifi, akiwa na hamu ya kuanzisha biashara na kujenga makazi pamoja na Bi Martha Wanjiru Muhoro, ambaye baadaye alifunga naye ndoa ya serikali mnamo Julai 23, 2025. Hata hivyo, chini ya mwaka mmoja tangu ahamie Kenya, mwanajeshi huyo mstaafu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani sasa anakabiliwa na kesi kadhaa, zikiwemo za madai kuhusu matumizi yasiyo halali ya urithi wake. Katika kesi ya hivi punde iliyo mbele ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Malindi, Bw Fitzpatrick anataka Mahakama imzuie Bi Muhoro kuuza, kuhamisha umiliki, kukodisha au kufanya shughuli yoyote kwa ardhi ya Gede/Dabaso, akidai ilinunuliwa kwa Sh25 milioni alizomtumia ili anunue kwa niaba yake. Jumanne iliyopita, Mahakama ilimpa Bi Muhoro wiki mbili kuwasilisha majibu yake baada ya wakili wake kuomba muda zaidi. Mahakama pia iliongeza amri ya kudumisha hali ilivyo na kuagiza pande zote mbili kubadilishana stakabadhi za kesi kabla ya kesi hiyo kutajwa Oktoba 12 kwa maelekezo zaidi. Kulingana na stakabadhi za Mahakama, Fitzpatrick ni mshauri wa masuala ya biashara, siasa na mazingira. Katika kesi nyingine ya madai, anaitaka Mahakama iamuru arejeshewe zaidi ya Sh35.8 milioni ambazo anadai alituma kwenye akaunti ya Benki ya Family inayomilikiwa na Bi Muhoro, huku akiomba akaunti hiyo izuiwe ili fedha zilizomo zisitolewe hadi kesi itakapoamuliwa. Stakabadhi za Mahakama zinaonyesha kuwa wawili hao walifahamiana kupitia tovuti ya kutafuta wapenzi mwaka 2023. Bw Fitzpatrick anasema alirithi asilimia 75 ya mali za marehemu mama yake, ikiwemo nyumba katika Kaunti ya Dublin nchini Ireland, na akamkabidhi Bi Muhoro jukumu la kuandaa uhamisho wake kwenda Kenya kwa kutafuta ardhi, kufuatilia taratibu za uhamiaji na kusimamia mipango ya kifedha. Anadai alimtumia fedha nyingi, zikiwemo euro 250,000 (takriban Sh36.9 milioni) mwezi Aprili 2025 kwa ajili ya kununua ardhi na gari, pamoja na uhamisho mwingine wa euro 10,000 (takriban Sh1.5 milioni) mara nne, euro 15,000 (takriban Sh2.2 milioni) mwezi Septemba na euro 226,860 (takriban Sh33.4 milioni) mwezi Oktoba, ambazo anasema zilikuwa sehemu ya mwisho ya urithi wake. Anadai Bi Muhoro alimshawishi fedha zote zipitie kwenye akaunti yake hadi atakapohamia Kenya, lakini baadaye hakumjumuisha katika umiliki wa ardhi na gari licha ya kuwa ndiye aliyefadhili ununuzi wake. Bw Fitzpatrick anasema amebaki hana mali na ana hofu kuwa fedha zilizobaki zinaweza kutolewa kwenye akaunti hiyo kabla ya kesi kusikilizwa. Kwa upande wake, Bi Muhoro anakiri kupokea fedha hizo lakini anakanusha kuzitumia vibaya. Anasema matumizi yote yalifanywa kwa uwazi na kwa makubaliano ya pamoja walipokuwa wakijiandaa kuanza maisha yao ya ndoa. Pia anasema aliacha kazi yake ya ualimu nchini Qatar kwa ombi la Fitzpatrick na kurejea Kenya kujiandaa kwa harusi yao. Anaeleza kuwa mali hizo zilisajiliwa kwa jina lake kwa sababu wakati huo Fitzpatrick, akiwa raia wa kigeni, hakuwa na stakabadhi zilizohitajika kusajili mali hizo kwa jina lake. Bi Muhoro anasema baadaye uhusiano wao ulivurugika na kumshutumu Bw Fitzpatrick kwa ukatili na unyanyasaji, akiiomba Mahakama itupilie mbali kesi hiyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 11 hours ago
Omtatah apinga kinga ya IMF na Benki ya Dunia inayowazuia kushtakiwa nchini
SENETA wa Busia Okiya Omtatah akishirikiana na wanaharakati Bernard Muchiri na Naomi Misati, wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka sheria inayoyapa mashirika ya kifedha ya IMF na Benki ya Dunia, kinga dhidi ya mashtaka, ushuru na kufichua taarifa kuwa kinyume cha Katiba. Walalamishi wanapinga Kifungu cha Sheria ya Bretton Woods ya 1963, wakisema kimepitwa na wakati wala hakiendani na Katiba ya 2010. Kwa mujibu wa kesi hiyo, sheria hiyo inaipa serikali mamlaka makubwa ya kuingia mikataba ya kimataifa ya kifedha, kukopa fedha na kutumia hazina ya umma bila usimamizi wa kutosha wa Bunge. Aidha, sheria hiyo inalinda IMF na Benki ya Dunia dhidi ya kuwajibishwa katika mahakama za Kenya. Wanadai kuwa Kifungu cha tano cha sheria hiyo kinazipa taasisi hizo kinga dhidi ya kushauri mahakama, ushuru, ukaguzi, kutwaliwa kwa mali, jambo ambalo linawanyima Wakenya haki ya kupata haki, kusikilizwa kwa usawa na kupata taarifa. Aidha, wanasema sheria hiyo inaruhusu serikali kutekeleza mikataba ya kimataifa bila idhini ya Bunge na kutoa fedha kutoka Hazina Kuu ya Fedha moja kwa moja kwa IMF na Benki ya Dunia bila kuidhinishwa kila mwaka na wabunge. Bw Omtatah na wenzake wanaeleza kuwa hali hiyo inadhoofisha mamlaka ya Bunge na Mahakama katika kusimamia matumizi ya fedha za umma. Pia inakiuka masharti mbalimbali ya Katiba, pamoja na sura inayohusu usimamizi wa fedha za umma. Mahakama Kuu imewaagiza washtakiwa na wahusika wengine kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14. Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 29, 2026, kwa mwelekeo zaidi.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 12 hours ago
Cherargei amshtaki Gachagua NCIC kwa 'uchochezi'
SENETA wa Nandi Samson Cherargei ameandikia Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) barua ya malalamishi akiitaka imchunguze Kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, kwa madai ya kutoa matamshi yanayoweza kuchochea vurugu za kikabila. Katika barua ya Julai 27, 2026, iliyonakiliwa kwa Mwenyekiti wa NCIC, Bw Cherargei alisema matamshi ya Bw Gachagua kuhusu jamii ya Wakalenjin yanastahili kuchunguzwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa. Bw Cherargei anadai kuwa kauli hizo, zilizotolewa katika mikutano ya kisiasa na mahojiano ya vyombo vya habari, zimeibua hofu kuhusu athari zake kwa umoja wa kitaifa. Kulingana na malalamishi hayo, Bw Gachagua anadaiwa kuhusisha baadhi ya wanajamii wa Wakalenjin na uhalifu, ukosefu wa usalama na ghasia zilizopangwa mbali na kutamka matamshi ya chuki. Seneta huyo alisema aliambatanisha ushahidi baadhi yazo ikiwa ni video na nakala ya hotuba ya Bw Gachagua kufuatia madai ya kutekwa nyara kwa mbunge mmoja. Anadai kuwa Bw Gachagua alidai baadhi ya maafisa wa serikali kutoka jamii ya Wakalenjin waliunda kikosi maalumu cha polisi cha kuwafuatilia viongozi wa upinzani, madai ambayo hayajathibitishwa na NCIC wala mahakama.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 13 hours ago
Serikali yasema imepata shamba la kuzipa makao familia 21,000 zilizofurushwa Mau
SERIKALI inakaribia kutatua moja ya migogoro ya muda mrefu katika Bonde la Ufa baada ya kuthibitisha kuwa imepata mashamba makubwa katika Kaunti ya Narok ili kuzipa makazi mapya familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau pamoja na watu wengine wasio na ardhi. Hatua hiyo inalenga kumaliza mateso ya zaidi ya familia 21,000 zilizofurushwa katika oparesheni mbalimbali za serikali ndani ya kipindi cha miaka 21 iliyopita. Tangazo hilo linajiri huku Rais William Ruto akitarajiwa kuzuru Kusini mwa Bonde la Ufa mwezi ujao. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kuwafidia waathiriwa wa Mau na kuwapa makazi mapya waliokosa ardhi katika Kaunti ya Narok. Akizungumza Kapkwen, Kaunti ya Bomet, alisema Wizara ya Ardhi inakamilisha taratibu za mwisho na kwamba orodha ya walionufaika itatangazwa hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh, pia alisema maagizo ya Rais Ruto ya kuwahamisha waathiriwa hao tayari yanatekelezwa. "Serikali imefanikiwa kupata ardhi ya kuhamishia familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau katika maeneo ya Narok Kusini na Narok Magharibi pamoja na watu wasio na ardhi Angata Barikoi, eneobunge la Kilgoris," akasema. Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, alisema serikali tayari imelipia baadhi ya mashamba hayo na hatimiliki zimekabidhiwa Wizara ya Ardhi. Pia alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kununua zaidi ya ekari 5,000 zinazomilikiwa na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Isaiah Cheluget, katika eneo la Tendwet, Narok Magharibi. Kwa mujibu wa Seneta huyo, uhakiki wa majina ya waathiriwa umekamilika na serikali sasa inakamilisha utaratibu wa kugawa fidia na ardhi. Suala la kufurushwa kwa wakazi wa Mau limekuwa ajenda ya kisiasa kwa zaidi ya miongo miwili. Tangu 2005, marais na wagombea mbalimbali wameahidi kuwafidia na kuwapa makazi mapya walioathiriwa, lakini ahadi hizo zimekuwa zikicheleweshwa. Katika muhula wa pili wa Rais Uhuru Kenyatta, maelfu ya familia zilifurushwa tena kutoka maeneo yanayopakana na msitu, huku nyumba, mashamba na mali nyingine zikiharibiwa katika operesheni iliyoongozwa na aliyekuwa Kamishina Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya. Rais Ruto amesema serikali yake tayari imelipa familia 2,000 fidia ya Sh300,000 kila moja na imeahidi kuwahamisha jumla ya familia 12,000 ili ziishi maisha ya kibinadamu. Hata hivyo, baadhi ya viongozi na wakazi wanasema kiwango hicho cha fedha hakitoshi kununua ardhi wala kujenga nyumba. "Kiasi cha Sh300,000 hakitoshi hata kununua kiwanja, sembuse kujenga nyumba. Watu walipoteza mashamba, mifugo, mazao na mali nyingine. Wanastahili fidia ya haki," alisema kiongozi wa eneo hilo Johnstone Kiptanui. Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, ambaye hapo awali aliunga mkono kufurushwa kwa wakazi hao ili kulinda msitu, sasa anasema wakati umefika serikali iwape makazi mapya na fidia kwa kuwa lengo la kuhifadhi Msitu wa Mau. Hatua ya serikali ya kuharakisha mpango huo inachukuliwa kuwa jaribio la kumaliza mgogoro ambao umeathiri maelfu ya familia na umekuwa ukitumiwa kama ajenda ya kisiasa katika kila uchaguzi mkuu tangu 2007.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo 14 hours ago
Mawaziri wa Ruto wazozana Wahome akimponda Duale, Kindiki naye akimkemea Ruku
UHASAMA mkali unaendelea kulikumba Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto huku mawaziri wake wakijibizana hadharani na kuibua maswali kuhusu uwezekano wa kutekeleza mabadiliko kuelekea kura ya 2027. Licha ya Rais Ruto kusema akiwa kituo cha kibiashara cha Amagoro, Teso, Busia kuwa hajaanza siasa, mawaziri wake wanaendelea kuzozana huku malumbano yao yakichukua mkondo wa siasa za kikabila. Uhasama wa ndani kwa ndani umeibua maswali kuhusu uwezo wa baraza hilo la mawaziri kuwajibikia Wakenya ipasavyo, miezi 12 kabla ya kura kuwadia. Tukio la hivi punde ni majibizano makali kati ya Waziri wa Afya Aden Duale na Waziri wa Ardhi Alice Wahome kuhusu matamshi ambayo Bw Duale anadaiwa kutoa dhidi ya jamii ya Mlima Kenya. Aidha, Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki ametofautiana vikali na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kutengana na Magharibi na kujiamulia kivyake mustakabali wake wa kisiasa. Kwenye video ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, Bw Duale akiongea kwa lugha ya mama, anadaiwa kulinganisha jamii ya Agikuyu na ya Wasomali kwa kutumia idadi yao nchini huku akidai jamii yake ya Wasomali imekuwa ikibaguliwa na tawala zilizopita za marais Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta wote huku nyingine zikinufaika. Akiongea katika Kaunti ya Mandera, Bw Duale alilinganisha jamii ya Agikuyu na fisi ambaye hutaka kula kila kitu isitake jamii nyingine zinufaike kwa miradi ya serikali. Katika video hiyo, Bw Duale alimshukuru Rais Ruto kwa kumaliza kile alichosema ni uongozi ambao umekuwa ukipendelea jamii moja na kubagua jamii nyingine. Waziri wa Ardhi, Alice Wahome ni kati ya viongozi kutoka Ukanda wa Mlima Kenya ambao sasa wanataka Bw Duale aombe msamaha kwa kauli yake. Waziri huyo tayari amesema hawezi kuomba msamaha kwa sababu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahi kuyatoa matamshi yanayoweza kufasiriwa kama ya kikabila lakini hajawahi kuchukuliwa hatua zozote. Vilevile Bw Duale amesema kuwa hatafika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) iwapo Bw Gachagua hatafanya hivyo kwanza. "Makosa mawili hayafanyi jambo liwe sawa na ni mpumbavu tu ndiye asiyebadilisha fikra zake," akaandika Bi Wahome kwenye mtandao wa X. Bi Wahome ambaye alihudumu kama mbunge wa Kandara kabla ya kuteuliwa waziri, ni wa kwanza kwenye baraza la mawaziri kumshambulia Bw Duale na kumtaka aombe msamaha. Mbali na waziri huyo baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya akiwemo Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba wamemshambulia Bw Duale kutokana na matamshi yake hayo. Waziri huyo naye amejitetea kuwa matamshi yake, 'Waraabe la-tagis bartay, ka-ridis waa ku dhib', ni methali ya Kisomali wala haikulenga jamii fulani. "Ujumbe wangu ulilenga kuhakikisha kuna umoja jinsi ambavyo serikali imekuwa ikifanya bila kujali dini au kabila," akasema Bw Duale. "Nilenga kuonyesha ugumu wa kumalizwa kwa mtindo ambao upande mmoja umekuwa ukinufaika kwa kipindi kirefu. Sikulenga jamii yoyote au kumdunisha yeyote. Kuna jaribio la kufasiri matamshi yangu visivyo," akasema. Uhasama mwingine ulioonekana wazi katika baraza la mawaziri ni ule kati ya Prof Kindiki na Bw Ruku kuhusu Mlima Kenya Mashariki kuwa na mwelekeo wa kisiasa 2027. Mlima Kenya Mashariki una kaunti za Embu, Tharaka-Nithi, Meru na sehemu ya kaunti za Kirinyaga na inakadiriwa itakuwa na karibu kura milioni mbili mnamo 2027. Eneo hili limekuwa likipiga kura kwenye kapu moja na wenzao wa Nyandarua, Murangá, Nyeri, Kiambu, Laikipia na Nakuru. Bw Ruku anasema mtindo huu umefanya wabaguliwe na hata sasa wanaonewa gere kwa kushikilia wadhifa wa Naibu Rais. "Mimi siwachukii Wakikuyu lakini lazima tufurahie utambulisho wetu. Tulikuwa na majenerali waliopigania uhuru wa nchi kutoka Mlima Kenya Mashariki ndiyo maana tuliwaunga Jomo Kenyatta, Kibaki na Uhuru," akasema mnamo Juni 30 katika ibada ya Kanisa Kaunti ya Kiambu. "Haiwezekani kuwa mwana wa kiume kutoka Mlima Kenya Mashariki akifanya kazi na Rais Ruto basi viongozi wa Mlima Kenya Magharibi wanatuambia serikali ni mbaya na tunafaa kutoka. Hatutatoka," akaongeza Bw Ruku. Hata hivyo, Naibu wa Rais alionekana kumkemea siku chache baadaye akisema eneo hilo limeungana kwa kipindi kirefu na linastahili kuendelea kufanya hivyo. "Sitaki watu wazungumze lugha tofauti kwa sababu tumefanya mambo mengi pamoja, tuna historia pevu na hakuna kitu ambacho kitatutenganisha," akasema Prof Kindiki mnamo Julai 19 wakati wa ibada katika Kaunti ya Embu. Aidha, Prof Kindiki alikiri kuwa anajikuna kichwa kuhusu unaibu rais ambao unamezewa mate na viongozi wengine kama Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya lakini akasisitiza hawabanduki serikalini. "Najua tumeongezeka akina Oparanya wamekuja lakini hatuondoki, tutang'ang'ana hapa ndani," akasema Kindiki. Wikendi iliyopita, Prof Kindiki aliwachemkia viongozi ambao wanamezea mate wadhifa wake na kumsawiri kama asiyefaa kushikilia wadhifa huo. "Serikali haiwezi kuwa mzuri wakati naibu rais akitoka upande wao na ni mbaya akitoka hapa. Wakati Uhuru alikuwa rais tulimuunga mkono na hatuwezi kubali jamii ya eneo hilo liongee lugha tofauti," akasema Profesa Kindiki. "Ni haki yao kuenda mahali wameenda lakini upande wao wamepangana na namba zote zimeenda na tuko namba 20. Rais Ruto akimaliza muhula wake urais utakuja pande hii," akasema. Wikendi viongozi wa ODM kutoka Nyanza na Magharibi walisisitiza kuwa UDA ikiwahi urais naye mgombeaji mwenza anastahili kutoka chama hicho cha chungwa. "Watu wakuje pole pole na wajue kwamba huwezi kuruka laini. UDA ikipata urais, sisi lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya," akasema Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed wikendi akiwa Kakamega. Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Profesa Lumala Masibo ni wazi kuwa baraza la mawaziri lina vita vya ndani kwa ndani hasa baada ya Profesa Kindiki kuonekana kuanza kuridhiana na Bw Gachagua. "Baadhi sasa wanamwona kama anayejipanga kivyake na hata alivyoongea wikendi, anaonekana kama mtu ambaye si mtiifu sana kwa Rais tena. Anaweza aje kudai unaibu rais utasalia kwake ilhali si anayeteua mshikilizi wa nafasi hiyo," akasema Profesa Masibo. Kauli yake inatokana na hatua ya Bw Gachagua kuwaamrisha viongozi wanaoumuunga mkono wasimshambulie Profesa Kindiki bali wamlenge Rais Ruto moja kwa moja. "Baada ya Ol Kalou ni dhahiri kuwa Rais amepoteza Mlima Kenya na shida sasa ni kupambania nafasi ya mgombeaji mwenza. Pia baadhi ya mawaziri kutoka Mlima Kenya sasa wanajificha nyuma ya kauli ya Bw Duale kumridhisha Gachagua kwa sababu ya umaarufu wake mlimani," akaongeza.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 10:23:43
Prof Okumu ateuliwa mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha Kenyatta
BARAZA la Chuo Kikuu cha Kenyatta jana lilimteua Profesa John Okumu kuwa Naibu Chansela wa chuo hicho baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa kuajiri ulioendeshwa na Tume ya Utumishi kwa Umma (PSC). Uteuzi huo ulitangazwa Jumatatu kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Profesa Clara S. Momanyi, ambaye alisema uamuzi huo ulifanywa kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu na kwa idhini ya Waziri wa Elimu. Profesa Okumu anafahamu vyema Chuo Kikuu cha Kenyatta kutokana na kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa miaka mingi. Aliwahi kuwa Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Kitaaluma kwa miaka 10, pamoja na kushikilia nyadhifa nyingine za juu za usimamizi. Baraza lilimsifu kama msomi na msimamizi mwenye tajriba kubwa katika uongozi wa elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya taasisi. Prof Momanyi alisema ana imani kuwa tajriba na uwezo wa Profesa Okumu katika kupanga mikakati, kusimamia taasisi na kushirikiana na wadau utasaidia kuimarisha maendeleo ya chuo hicho. "Tunamkaribisha Profesa Okumu katika nafasi hii muhimu na tunatoa wito kwa wanajamii wote wa chuo na wadau kumpa ushirikiano anaohitaji ili atekeleze wajibu wake na afanikiwe," akasema. Profesa Okumu alikuwa akishikilia wadhifa huo kwa muda tangu mwishoni mwa Januari 2026 baada ya kumrithi Profesa Paul Wainaina, aliyestaafu baada ya kuhudumu kwa miaka minane. Katika mahojiano yaliyofanywa na PSC, Profesa Okumu alipata alama 84.5, akiwashinda Profesa Stephen Odebero na Profesa Godfrey Mse. Hata hivyo, uteuzi huo ulikumbwa na changamoto za kisheria baada ya Profesa Waceke Wanjohi, Naibu Chansela wa Masuala ya Kitaaluma na mmoja wa waliowania wadhifa huo, kufikisha kesi Mahakama Kuu akidai ndiye aliyepata alama za juu zaidi na kwamba aliondolewa isivyo haki. Mnamo Aprili, Jaji Njoki Mwangi alitoa amri za muda zilizokizuia chuo kujaza nafasi hiyo hadi kesi hiyo isikizwe, huku pia akiamuru mkataba wa Profesa Wanjohi uongezwe. Mvutano huo uliibua sintofahamu kuhusu hatima ya nafasi hiyo kwa miezi kadhaa kabla ya Baraza la Chuo kuthibitisha rasmi uteuzi wa Profesa Okumu. Uteuzi huo unatarajiwa kuleta utulivu katika uongozi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 09:10:23
Demu anataka nimnunulie simu kabla nionje asali, inafaa hivyo kweli? Nishauri
Kuna msichana tunayependana na anataka nimnunulie simu ya bei ghali kisha anionjeshe asali. Nifanyeje? Mapenzi hayafunguliwi kwa simu bali kwa moyo. Ukianza kununua ili upendwe, utamalizia kuwa na madeni. Kaa mbali na penzi la biashara. Nilimsaidia rafiki yangu wa kike baada ya mume wake kufariki. Nilianza kumlipia ada mtoto wake kwa miaka kadhaa na nikawa karibu naye kiasi kwamba mtoto huyo alianza kuniita "Baba". Sasa mama yake ameolewa tena na mume wake mpya amekataa mtoto huyo kuendelea kuwasiliana nami. Anasema mimi si baba yake na anataka niondoke kabisa katika maisha yao. Mtoto huyo hunipigia simu kwa siri na kuniuliza kwa nini nimemtelekeza. Mimi sijawahi kutaka kuchukua nafasi ya baba yake, lakini nimekuwa sehemu ya maisha yake kwa miaka mingi. Je, nina haki ya kuendelea kumsaidia au ni lazima nikubali kuondoka? Ulifanya jambo nzuri kwa kumsaidia mtoto, lakini msaada wa muda mrefu unaweza kujenga uhusiano wa kihisia ambao hauwezi kufutwa kwa siku moja. Hata hivyo, unapaswa kuheshimu mipaka ya familia hiyo mpya. Usimlazimishe mtoto kukutana nawe kwa siri kwa sababu hilo linaweza kumweka katika mgogoro na mama yake na baba wa kambo. Jaribu kuzungumza na mama yake kwa utulivu na kumweleza kuwa lengo lako si kuingilia ndoa yake, bali kuhakikisha mtoto huyo anaendelea vizuri. Kama mawasiliano yataendelea, yawe ya wazi na yenye heshima. Kijana wa 'Gym' sasa animezea mate Nimependa mhudumu wa gym ninakofanya mazoezi. Kila siku ananisifu na kweli naona tamaa machoni mwake. Hata ananiambia nikuje mafunzo ya kipekee. Nimechanganyikiwa. Baadhi yao hufanya kazi ya kusifu wateja ili warudi kesho. Usichukue maneno yake kama ishara ya mapenzi. Kaa macho. Ataka nimlipe kodi sababu nyumba ni yake Shangazi, niliolewa miaka mitano iliyopita. Kabla ya ndoa, mume wangu alikuwa amenunua nyumba kwa mkopo. Sasa hivi kila tunapogombana, huniambia nyumba ni yake na ninapaswa kumshukuru kwa kuniruhusu kuishi humo. Mimi pia hufanya kazi na huchangia chakula, ada za watoto na bili zote za nyumbani. Juzi aliniambia kama sitaki kuitwa mpangaji, nianze kumlipa kodi kila mwezi. Maneno hayo yameniumiza sana. Nipe ushauri. Umiliki wa mali na heshima ndani ya ndoa ni mambo mawili tofauti. Inawezekana nyumba iko kwa jina la mume wako, lakini hilo halimpi haki ya kukudhalilisha au kutumia makazi kama silaha wakati wa ugomvi. Mnapaswa kuzungumza kuhusu michango ya kila mmoja na namna mnavyotaka kusimamia mali na fedha zenu. Usijenge maisha yako kwa kutegemea maneno ya "hii ni yangu" kila mnapokosana. Pia, usikubali kutishwa bila kuelewa haki na wajibu wako.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 09:40:56
Makosa yaliyozoeleka katika kutumia 'vivumishi safi', 'hodari' na 'nadhifu'
KIVUMISHI ni neno linalotoa habari zaidi kuhusu nomino inayozungumziwa. Kuna aina mbalimbali kama vile: vivumishi vya pekee, vivumishi vya sifa, vivumishi viashiria, vivumishi vimilikishi, vivumishi vya idadi na vivumishi viulizi. Maneno safi, hodari na nadhifu ni vivumishi vya sifa ambavyo ni kapa au tasa. Vivumishi hivyo vinapotumiwa katika sentensi huwa havichukui viambishi vya nomino au vya ngeli yoyote. Kwa hivyo havibadiliki katika kuzungumzia nomino yoyote katika umoja au wingi. Ingawa vivumishi safi, hodari na nadhifu havifai kubadilika katika wingi au kuchukua viambishi vyovyote vya nomino, kuna mazoea ya wanafunzi kutunga sentensi kama vile: *Mwanafunzi mhodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. *Wakulima wahodari walipata mavuno mengi. Sentensi hizi si sahihi. Isitoshe, katika matumizi ya neno safi utakumbana na sentensi kama vile: *Vikombe visafi vimetumiwa kunywea chai. *Mwanafunzi msafi anavutia. Vilevile, kivumishi nadhifu hutumiwa isivyofaa kwa kutunga sentensi kama vile: *Wanafunzi wanadhifu walisifiwa na mwalimu.Mifano hii ya sentensi ina kosa la kuvipa vivumishi kapa safi, hodari na nadhifu viambishi. Ili kuzisahihisha tunafaa kusema: Mwanafunzi hodari katika somo la Kiswahili alituzwa jana. Wakulima hodari walipata mavuno mengi. Vikombe safi vimetumiwa kunywea chai. Mwanafunzi safi anavutia. Wanafunzi nadhifu walisifiwa na mwalimu. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kutumia vivumishi safi, hodari na nadhifu kwa usahihi katika sentensi, anafaa kufanya mazoezi ya kutunga sentensi mbalimbali akitumia viumishi hivyo.
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 08:38:26
KAULI YA MATUNDURA: Ni kwa nini imani ya wananchi kwa Rais inadorora kila uchao?
JUZI, Naibu Rais Kithure Kindiki aliwakosoa viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi wanazotoa kwa raia. Kindiki alisema, mienendo ya kuwadanganya wananchi, na baadaye kurudi kwao (kuwaomba kura?) lazima ikomeshwe mara moja. Alisisitiza kuwa viongozi watoapo ahadi, ni sharti wahakikishe zimetimizwa kwa vitendo. Kauli ya Kindiki inasadifiana matamshi ya Rais Ruto kuhusu ufadhili wa elimu nchini. "Kuanzia sasa, mwanafunzi yeyote, mradi tu amefaulu mtihani na kuteuliwa kujiunga na taasisi au chuo kikuu, atafadhiliwa kuafikia elimu ya juu […] sasa tuna mfumo utakaomlipia kila mwanafunzi," akasema Dkt Ruto. Mpaka sasa, Wakenya wengi wanatilia shaka kauli hii ya rais kwa misingi kwamba, ahadi nyingi alizowahi kutoa mbeleni hazijawahi kutimizwa mpaka sasa. Hali hii imesababisha kupungua kwa imani ya wananchi katika serikali. Data kutokana na asasi za Utafiti ya TIFA inadokeza kwamba, Wakenya wengi hawamwamini Rais Ruto. Kwa nini? Kwanza, tathmini inaonesha katika mamia ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni kutangulia uchaguzi mkuu 2022, ni chache tu zilizokwisha kutimizwa. Hali hii imewatamausha wananchi. Pili, serikali inawatoza wananchi kiasi kikubwa cha ushuru. Hatua hii inakera kwa sababu Rais alipokuwa akisaka urais, alijisawiri kama mtetezi wa wanyonge na watu wa kipato cha chini. Alijinasibisha sana na mahasla, na kushabikiwa sana kwa mfumo wa kiuchumi wa Bottom – Up. Alivunja ahadi hii pindi alipotwaa mamlaka. Rais anatoa ahadi za kufadhili kikamilifu wanafunzi wa vyuo vikuu katika kipindi ambapo Taasisi ya Utoaji wa Mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu (HELB) ina nakisi ya takriban Sh57.65 bilioni. Kosa jingine ambalo yamkini analifanya Rais Ruto ni kujinaki kwamba kwa vyovyote vile, atashinda kwenye uchaguzi mkuu wa 2027. Huenda hajagundua, umaarufu aliokuwa nao 2022 unapungua kila uchao kwa sababu anasema sana kuliko anavyotenda. Katika kughairi misimamo yake mikali kuhusu sera zilizowaumiza wananchi zikiwemo kukubali kubadilisha mfumo wa ufadhili wa wanafunzi katika vyuo vikuu, yaelekea Rais Ruto anatumia mbinu ya Saikolojia kinyume (Reverse psychology). Hii ni mbinu ya kiushawishi ambapo mtu hutetea jambo lililo kinyume kabisa na kile anachokitaka, akitarajia mtu au watu wengine kupinga pendekezo lake, na badala yake kufanya jambo unalolitaka hasa. Kwa mfano: Ni kweli kwamba serikali haijui magenge au wahuni wanashirikiana na polisi kuhangaisha wananchi? Itakuwa hatari kwa Rais Ruto kuendelea kutoa ahadi hewa kwenye kampeni kutangualia 2027. Utekelezaji utafaa zaidi. Bitugi Matundura ni mhadhiri
read moretaifaleo.nation.co.ke
@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 06:39:43
Mume amlaghai mkewe mwanatenisi mabilioni ya pesa
ALIYEKUWA nyota wa tenisi nchini Uhispania, Arantxa Sanchez Vicario, amemlaumu mume wake wa zamani baada ya kupoteza utajiri wake wa Sh5.4 bilioni. Bingwa huyo mara nne wa Grand Slam mwenye umri wa miaka 54, aliolewa na mjasiriamali Josep Santacana kati ya 2008 na 2019. Arantxa na Santacana walikuwa na mtoto wa kiume na wa kike pamoja. Kupitia kipindi cha televisheni cha Universo Callejo nchini Uhispania, Arantxa alisema hivi kuhusu mumewe wa zamani: "Nilimwamini kwa sababu alikuwa baba wa watoto wangu. Nilimpenda kipofu na sikudhania ni mtu mbaya sampuli hiyo. Kumbe alikuwa laghai, mdanganyifu na tapeli." Arantxa na Santacana walifikishwa mahakamani mwaka wa 2023 wakituhumiwa kuficha mali ili kuepuka kulipa deni wanalodaiwa na Benki ya Luxembourg. Mwanatenisi huyo mstaafu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kulipa deni la thamani ya Sh957 milioni. Alipoulizwa kuhusu jinsi alivyopoteza mapato yake ya kazi, ya takriban Sh5.4 bilioni, Arantxa aliongeza: "Ni kweli, hicho ndicho kiasi kilichoonekana na vyombo vya habari. Nilizingatia sana kucheza tenisi na sikuwahi kushughulikia masuala yangu ya kifedha kwa sababu nilimwamini sana mume wangu. Ndiye aliyetoweka na mabilioni yangu yote huku nikiachwa na mzigo mkubwa." Kuhusu namna alivyofaulu kuepuka kifungo, aliongeza: "Sikuenda jela kwa sababu ninalipa asilimia 50 ya mapato yangu kama sehemu ya mkopo wa benki. Kumbe nilikuwa na mume laghai. Ilinibidi kwenda kwenye matibabu kwa sababu sikuamini alichonifanyia. Kwa wakati fulani niliona tukio hilo likiwa kama ndoto." Arantxa alishinda mataji matatu ya French Open na ndiye mchezaji wa kwanza kuwahi kufanya hivyo akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Mhispania huyo pia alishinda US Open mnamo 1994, pamoja na kufika fainali nyingi za Australian Open na Wimbledon. Aliorodheshwa nambari moja duniani mnamo 1995, na pia aliwakilisha nchi yake kwenye makala matano ya Olimpiki. Nyota huyo mzaliwa wa Barcelona alistaafu mnamo 2002. Sanchez Vicario pia alijaribu mkono wake katika ukocha na aliwahi kumnoa mwanatenisi Caroline Wozniacki aliyewahi kushikilia nambari ya kwanza duniani mnamo 2015.
read moreRight Column Content