T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 1 hours ago

Ushirikiano wa mama na mwanawe ulivyotia nguvu mradi wao wa ufugaji sungura

TANGU akiwa kijana mdogo Francis Karanja alivutiwa na shughuli ya kufuga sungura. Alipokuwa darasa la tano alimpa mamake, Rachel Chebet, ombi moja: amnunulie sungura kadha afuge ili aboreshe somo lake la kilimo katika mtaala mpya wa elimu ya umilisi na utendaji (CBE). Mamake akaahidi kumnunulia baadaye kwani mahali walipoishi wakati huo hapakuwa na nafasi kubwa ya kufanya ufugaji wowote. Mwaka 2024 Chebet alinunua mabati, mbao, nyaya za kuweka ua, misumari na vifaa vingine akajenga vyumba vidogo tisa vya sungura kwa gharama ya Sh10,000. Pia alinunua sungura wanne - ndume wawili na jike wawili kwa Sh500 kila moja. Karanja, 15, ambaye sasa yuko darasa la nane katika shule ya Michinda mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru, asema ilikuwa furaha tele mama alipomtimizia ombi lake. "Sungura walinunuliwa wakati wa likizo na hilo lilinipa fursa nzuri ya kuwatunza," aeleza. [caption id="attachment_190590" align="alignnone" width="2560"] Francis Karanja, 15, mwanafunzi wa Gredi ya Nane katika shule ya Michinda, Elburgon ambaye ni mfugaji sungura. Picha|John Njoroge[/caption] Baada ya miezi mitatu sungura mmoja alizaa wana watano na mwingine saba. Karanja anapokuwa shuleni mamake ndiye huchukua jukumu la kutunza sungura hao. Pia wanakusanya mkojo na kinyesi cha mifugo hao kutengeneza mbolea asili ili kutumia katika shamba lao dogo la nyumbani. Mkojo wanakusanya takriban lita 10 hadi 20 kila wiki. Bidhaa hii ina nitrojeni nyingi na ni kiungo bomba katika kuunda mbolea asilia, na huuzwa kama andazi moto. Hivyo, baada ya kumimina kiwango wanachohitaji kuunda mbolea asili yao, mkojo ambao husalia wanawauzia wakulima wa eneo hilo Sh70 kila lita. Kipindi cha ujauzito cha sungura huwa kati ya siku 28 na 35. Hata hivyo, Chebet na mwanawe wameweka ratiba ili kwamba sungura wa kike anajamiiana na ndume baada ya miezi mitatu, ili kuzuia wana wengi kuzaliwa kila mara hasa wakati wa kiangazi ambapo ni vigumu kupata lishe yao ya kutosha. Mbali na kuuza mkojo, Karanja anasema wao pia huchinja sungura hao kupata nyama. "Baada ya muda fulani sungura wakiongezeka kuwa wengi sana hasa wakati wa kiangazi malisho yakididimia, mama huchinja kadha tunatumia kutengeneza mchuzi nyumbani. Mchuzi wa nyama ya sungura ni mtamu sana," aeleza kwa itabasamu. Kwa mujibu wa afisa wa mifugo eneo la Kuresoi Kaskazini, Nicholas Rono, ufugaji sungura ni tija tosha. Mfugaji anahitaji tu kuhakikisha amejenga vyumba vizuri vya malazi, vinasafishwa kila wakati na kuzuia unyevunyevu kwani huleta magonjwa kama vile nimonia ambayo husababishwa na baridi. "Sungura pia huvamiwa na utiriri kwenye kichwa, mapua na masikio, tatizo ambalo hufanya wajikune sana kwenye ngozi na kuwaletea mwasho mkali. Kuna dawa ya unga ambayo wafugaji wanahitaji kupaka sehemu hizo ili kuzuia tatizo hilo," aeleza Rono. Anaongeza kuwa lishe ya sungura inafaa kuwa bora yenye virutubisho kamili na kiwango cha kutosha, hasa kwa vijike waliojifungua kwani baadhi hugeuka kula wanawao wakilemewa na njaa. Karanja huuza sungura wake kwa ajili ya ufugaji au nyama. Sungura aliyekomaa huwa kati ya Sh500 na Sh700 kulingana na saizi, na Sh300 kwa mwana wa sungura. "Ninatumia pesa hizo kuongeza lishe, na senti zinazosalia ninanunua vifaa vyangu vya shule. Kielimu mradi huu umefanya somo la kilimo kuwa kati ya zile ninazopenda zaidi shuleni," asema. [caption id="attachment_190591" align="alignnone" width="2560"] Kijana Francis na mamake Rachel Chebet wakikusanya mkojo wa sungura ulio na soko bomba ambapo lita moja huuzwa Sh70 sokoni. Picha|John Njoroge[/caption] Sungura hawana misimu pevu au kavu hivyo mfugaji hupata mauzo wakati wowote kulingana na hitaji la soko. Katika hatua ya kukuza ujuzi wa usimamizi wa biashara, anadokeza kwamba kwa usaidizi wa mamake wanaweka kila siku kumbukumbu za taarifa za ufugaji wa sungura wao kila siku. Ili kusawazisha kazi ya shule na mradi wake wa sungura, Karanja ana ratiba ya kibinafsi ili kufanya mambo kwa mpangilio na urahisi. Kwa sasa ana zaidi ya sungura 100 huku lengo likiwa kufikisha zaidi ya sungura 600 ifikapo Desemba. "Tamanio langu ni kufuga sungura zaidi ili kuvuna mkojo ya kuunda mbolea asili ya kutosha kukidhi mahitaji ya wakulima msimu wa upanzi, hasa katika kilimo cha viazi na mboga," asema. Mamake asema sio tu manufaa ya kifedha wanapata kutoka kwa mradi. "Ufugaji pia umemfunza maadili ya nidhamu, uwajibikaji na kumzuia kutangamana na vijana watundu kwani huwa ana shughuli nyingi za kufanya anaporejea jioni kutoka shule au wakati wa likizo," aeleza Chebet.

read more

Other Headlines


T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 55 minutes ago

Mashine hii mahuluti inafanya shughuli kibao shambani kuwa rahisi

KILIMO cha usahihi [Precision Agriculture kwa Kimombo] kinaendelea kupata nguvu barani Afrika huku teknolojia zake za utekelezaji zikinuia kuwasaidia wakulima wadogo kuongeza kiwango cha uzalishaji mazao kwa kutumia mashine nyepesi na rahisi ila zenye uwezo mkubwa wa utendaji. Moja ya teknolojia bunifu zilizovutia wakati wa makala ya 12 ya Maonyesho ya Teknolojia za Kilimo Afrika (Agritec Africa) wiki jana ni mashine inayoweza kufanya kazi anuwai za shambani. Mashine hiyo Multipurpose Power Tiller imebuniwa na mjasiriamali barobaro kutoka India, Shubham Patel, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Alphachem yenye makao yake Gujarat. "Mashine hii inampa mkulima uwezo wa kuendesha shughuli mbalimbali kwa kutumia kifaa kimoja badala ya kununua vingi tofauti," Patel, 22, aliambia Akili Mali wakati wa maonyesho hayo yaliyofanyika Juni 17 hadi 19 katika jumba la mikutano la kimataifa la Kenyatta (KICC), Nairobi. Mashine hiyo inaweza kutayarisha shamba, kulima, kupanda mbegu kwa kuzingatia nafasi na kina sahihi, kunyunyiza dawa ya kuua wadudu na magonjwa, kukatakata mimea ya malisho na hata kupiga maji kwa ajili ya unyunyizi. Hali kadhalika, mtambo huu unaweza kuunganishwa kwa vifaa vya upanzi wa mimea kama mahindi, mtama, vitunguu, njugu na vitunguu. Patel aeleza kuwa alitumia zaidi ya miaka mitatu na nusu kufanya utafiti na kuboresha mashine yake kabla kuizindua rasmi sokoni mwaka jana. Anasema madhumuni yake yalikuwa kutengeneza mashine inayowezesha wakulima kufanya kazi kwa wakati unaofaa, jambo ambalo ni msingi wa kilimo cha usahihi. "Wakulima wengi wadogo hawawezi kumudu gharama ya kununua au kukodi trekta na mashine kwa kila kazi. Mashine hii inawawezesha kufanya shughuli nyingi kwa kutumia kifaa kimoja na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji," asema. Alihoji kwamba visa vya ucheleweshwaji wa shughuli za kilimo kama kulima, kupanda au kupalili hutokana pakubwa na wakulima kusubiri mashine za kukodi. Power Tiller hii hutumia injini ya dizeli na inaweza kuchapa kazi katika ekari 10 hadi 15 kwa siku kutegemea shughuli inayotekelezwa. "Pia imeundwa kwa vipuri vinavyopatikana kwa urahisi na mchakato wake wa utengenezaji ni wa kawaida tu," alieleza Patel. Kwa sasa Alphachem huunda karibu mashine 100 kila mwezi. Wakati wa maonyesho ya Agritec Africa 2026 mashine hiyo ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya Sh420,000 ikiwa na vifaa vyake vyote. Mkurugenzi huyo alisema licha ya bei hiyo kuonekana kubwa ni nafuu kuliko kununua mashine tofauti za kulima, kupanda, kunyunyizia dawa, kukata mimea ya malisho na kupiga maji. Alidokeza kuwa wazo la kubuni mashine hiyyo lilitokana na ziara alizofanya katika nchi mbalimbali za Afrika. Alibaini kuwa mashamba mengi yanaendelea kugawanywa kuwa madogo kutokana na urithi wa kifamilia, hali ambayo imefanya matumizi ya matrekta makubwa kutofaa kwa wakulima wengi wa mashamba madogo. "Kilimo cha usahihi kinahitaji mashine zinazoendana na saizi ya shamba na zinazoweza kutekeleza kazi kwa urahisi na ufanisi pasipo kuongezea mkulima gharama," akaongeza. Waziri wa Kilimo na Mifugo Mutahi Kagwe, ambaye alifungua rasmi maonyesho hayo, alihimiza wakulima kukumbatia teknolojia na mashine za kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao na mapato, jambo ambalo pia litavutia vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo kama biashara. "Mashine za bei nafuu zinaweza kununuliwa au kukodishwa na vyama vya ushirika au makundi ya wakulima, na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisasa za kilimo," Kagwe alisema. Mbali na mashine hiyo Alphachem pia huuza pampu za kupiga maji, mashine za kukatakata malisho na vifaa vya kupanda mbegu katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania, Zambia, Ghana, Angola, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 2 hours ago

Kisa cha afisa wa DCI kudungwa kisu chaibua hofu ya ujasiri wa wahalifu

ONGEZEKO la mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi katika Kaunti ya Lamu limezua wasiwasi kuhusu iwapo makundi ya wahalifu yanazidi kupata ujasiri licha ya juhudi za miaka mingi zilizolenga kurejesha amani katika kaunti hiyo. Ndani ya kipindi cha miezi miwili pekee, angalau maafisa watatu wa usalama wameshambuliwa. Tukio la hivi majuzi zaidi lilimhusu afisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ambaye alishambuliwa na kujeruhiwa na mwanamume alipokuwa akitembea katika eneo la Langoni, kisiwani Lamu, mwendo wa saa nne asubuhi Ijumaa iliyopita. Mashahidi walisema afisa huyo alichomwa kisu tumboni, shingoni na mbavuni kabla ya mshambuliaji kutoroka. Afisa huyo bado amelazwa hospitalini akiendelea kupokea matibabu. Kwa mujibu wa mashahidi, alikuwa akitembea pamoja na mwenzake, wote wakiwa wamevalia nguo za kiraia. Ghafla, mwanamume aliwagonga kwa nguvu. Mmoja wa maafisa hao alirudi nyuma kwa tahadhari, akamshika mkono mwanamume huyo na kumuuliza kwa ukali kwa nini alikuwa na fujo. Badala ya kuomba radhi, mwanamume huyo alionyesha uhasama, akapaza sauti na kumsukuma afisa huyo. Bw Abdi Osman, mchuuzi, alisema walianza kupigana ghafla kwa karibu dakika nne. Afisa wa pili aliingilia kati ili kumvuta mshambuliaji huyo. "Hata kabla ya maafisa hao wawili kutoa bunduki zao ili kudhibiti hali, mshambuliaji alitoa kwa kasi kisu alichokuwa amekificha kiunoni na kumchoma mmoja wa maafisa. Kisu kilimdunga tumboni, mbavuni na shingoni," alisema Bw Osman. Bw Simon Kadenge, shahidi mwingine, alisema mara tu afisa wa pili alipoona mshukiwa ametoa kisu na kumchoma mwenzake, alikimbia kutoka eneo la tukio. "Eneo hilo liliendelea kuvutia wananchi wengi. Walifika na kumsaidia afisa aliyejeruhiwa. Kufikia wakati huo, mshukiwa alikuwa tayari ametoweka," alisema. Duru za polisi zilisema maafisa hao wawili wa DCI walikuwa wamehamishiwa eneo hilo karibu wiki moja kabla ya tukio hilo. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu Shadrack Ruto, alikashifu tabia za wananchi ambao wamekuwa wakiwalenga maafisa wa usalama na kuwadhuru akionya kuwa chuma chao kiko motoni. Alisema katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, maafisa watatu wa usalama wamevamiwa na kujeruhiwa na raia katika maeneo ya kisiwa cha Lamu na Hindi. "Mbali na shambulio la Ijumaa mjini Lamu, mwezi mmoja uliopita kuna askari wetu wawili wa akiba (NPR) waliolazimika kumpiga risasi na kumuua mwanamume raia aliyejaribu kuwavamia mjini Hindi akiwa amebeba mkuki na panga. Lazima watu waepuke kushambulia polisi kwani hatutawavumilia kamwe," akasema Bw Ruto. Wanaharakati na wakazi pia walikashifu vitendo hivyo. Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki la Vocal Africa, Bw Hussein Khalid, alisema mashambulio hayo ni ishara ya ongezeko la ukosefu wa usalama unaotendwa na vijana wa eneo hilo kwa muda sasa. "Miaka ya zamani tumewahi kuona hata machifu wakiuawa, vijana wakikatwa miguu na sasa maafisa wa usalama wameanza kudungwa visu. Wizara ya usalama wa Ndani lazima ishuke Lamu kukabiliana na kumaliza tatizo hilo," akasema Bw Khalid. Bi Zeinab Ahmed, mkazi, alitoa wito kwa wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuwakomesha kuingilia makundi ya uhalifu. Naye Afisa wa Haki Africa Mathias Shipeta alisema tatizo la utovu wa usalama linahitaji nyanja zote, zikiwemo zile za siasa kuhusika.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 3 hours ago

NCIC yasema itaendelea kufuatilia matamshi ya Duale, Gachagua na wengine sita

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imesema itaendelea na uchunguzi dhidi ya Waziri wa Afya Aden Duale na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu matamshi ya chuki na uchochezi wa kikabila, licha ya wawili hao kutangaza hadharani kwamba hawataitikia wito wa tume hiyo. Mwenyekiti wa NCIC Askofu Kepha Nyamweya, alisema tume hiyo haitaruhusu wanasiasa kuamua namna uchunguzi wake unavyofanywa na kwamba itaendelea kutekeleza wajibu wake bila uoga, upendeleo wala msukumo wa kisiasa. "Kuna wakati wa siasa na kuna wakati wa kazi na hatuwezi kuruhusu mchezo wa aina hiyo. Mtu hawezi kusema atafika mbele ya tume baada ya mwingine kufika. Tutafanya kazi yetu kwa mujibu wa sheria," akasema Bw Nyamweya. Kauli hiyo ilijiri baada ya Bw Duale kusema hatafika mbele ya NCIC hadi pale Bw Gachagua atakapoitwa kwanza kujibu matamshi yake yaliyofasiriwa kuwa ya uchochezi. "Kama hakuna Gachagua, hakuna Duale," alisema waziri huyo, akisisitiza kuwa sheria inapaswa kutumika kwa usawa kwa wote. Hata hivyo, Bw Nyamweya alisema watu wanaochunguzwa hawawezi kuielekeza tume yake jinsi ya kutekeleza majukumu yake. "Tunatoa wito kwa wanaohitajika kufika mbele yetu. Wakikosa kufika, sheria imeweka utaratibu wa kushughulikia hali hiyo. Tutachukua hatua bila mapendeleo," akaongeza. Kwa upande wake, Bw Gachagua ameendelea kutetea matamshi yake aliyosema "watamuua nyoka pamoja na mayai yake," akidai yalikuwa ya kimethali, yakimaanisha kuwashinda kisiasa Rais William Ruto na washirika wake kupitia kura, wala si kutumia vurugu. Alisema iwapo NCIC inahitaji maelezo yake, imuandikie rasmi naye atajibu. Mbali na viongozi hao wawili, NCIC pia imeanzisha uchunguzi dhidi ya Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Gavana wa Busia Paul Otuoma, Naibu Gavana wa Mandera Ali Maalim Mohamud, Mbunge wa Sirisia John Waluke pamoja na Tipape Naini Musa na Dkt Dennis Adison Ouma kwa madai ya matamshi ya chuki na uchochezi. Tume imesisitiza kuwa wote wanaochunguzwa wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi uchunguzi utakapokamilika. Nyamweya alionya kuwa matamshi ya kisiasa nchini yanazidi kuwa makali huku baadhi ya viongozi wakitumia lugha inayowagawa wananchi kwa misingi ya kikabila badala ya kushindana kwa sera. "Lugha inatumiwa kuwafanya wapinzani waonekane maadui badala ya majirani wenye mitazamo tofauti. Hali hii inaweza kuhatarisha umoja wa taifa," alisema. Alieleza kuwa NCIC imepewa mamlaka chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano ya kuchunguza matamshi ya chuki, kuwaita mashahidi, kukusanya ushahidi na kuwasilisha faili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa hatua zaidi. Bw Nyamweya alikanusha madai kwamba tume hiyo inaweza kushinikizwa kisiasa, akisema itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa haki huku ikishirikiana na Baraza la Kidini Kenya kuimarisha juhudi za kuzuia matamshi ya chuki na kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unafanyika kwa amani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 4 hours ago

Dalili Nyayo za Kijana Wamalwa na Raila zinamwongoza Sifuna

SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna anaendelea kutamba katika ulingo wa siasa. Nyota yake Sifuna inaendelea kung'aa kwenye ramani ya humu nchini kwa mwendokasi wa ajabu. Sifuna ni mwanafunzi mmakinifu wa siasa za watangulizi wake Raila Amollo Odinga na kigogo wa siasa Michael Kijana Wamalwa ambao walionyesha umahiri hata katika wimbi kali la upinzani. Baada ya kubanduliwa katika wadhifa wa katibu mkuu wa chama cha ODM, Seneta Sifuna hajafa moyo. Ufuasi wake Unaendelea kushamiri huku akifanikiwa kupata kibali katika kila eneo analozuru nchini. Hili linashuhudiwa kupitia umati wa watu wanaojitolea kuhudhuria mikutano anayoandaa pamoja na wenzake katika mrengo wa Linda Mwananchi. Safari yake Sifuna katika siasa ni sura ya siasa ya aliyekuwa waziri mkuu na kinara wa ODM Raila Odinga. Raila ndiye mwanasiasa wa pekee aliyelipinga wimbi la chama kikuu cha upinzani cha FORD katika mwaka wa 1994 na baadaye kujiuzulu. Raila alithamini demokrasia na nguvu za wananchi zaidi ya nguvu za dola. Sifuna amehitimu katika chuo cha mwamba aliyegundua kuanza mapema akiwa na nguvu na mvuto kwa wananchi. Hulka yake seneta huyo inachukuliana na yake Kijana Wamalwa ambaye alipendwa na wengi wa wapigakura katika ukanda wa magharibi. Ni wazi kuwa Sifuna ni mmoja wa viongozi walioweza kuwavutia wananchi wengi zaidi kisiasa katika eneo la Magharibi. Siasa yake inatikisa ngome za wanasiasa wakongwe wakiwemo Musalia Mudavadi, Moses Wetang'ula, Wycliffe Oparanya na wengine. Mvutano kati ya Raila na Wamalwa ulichangia FORD Kenya kusambaratika baada ya Jaramogi Oginga kufariki dunia. Raila alionekana kama aliyetaka kurithi chama naye Wamalwa akitaka kuwa kiongozi wa chama hicho. Hatimaye Ford Kenya iligawanyika mara tatu. Hii ndiyo njia ya chama cha ODM baada ya Raila kuondoka. Sharti Sifuna ajichongee kao lake la siasa kwa nyakati zijazo akifahamu kuwa ufuasi na ushabiki humwandama mtu jasiri anayejijengea chama chake. Raila aliviunda vyama kadhaa kama silaha yake dhidi ya serikali. Ni bayana kuwa Sifuna yuko njiani kukiunda chama chake. Tukielekea katika uchaguzi mkuu wa 2027, Sifuna ana nafasi murua ya kujinadi kupewa fursa ya kugombea kiti cha urais au kumpiga pambaja mgombea mwingine kuwania kiti hicho. Kibarua kikubwa ni kuwa kuna wanasiasa wa upinzani ambao huenda hawatampa nafasi hiyo kwa madai ya kukosa tajriba ya kisiasa. Kinachobakia ni kujijenga kisiasa wala si kutafuta ushindi wa kiti cha urais. Kadi yake Sifuna kama mgombea wa urais ni bora hasa kwa ushawishi alio nao kwa vijana na wananchi wanaotaka mabadiliko. Hata hivyo, haijadhihirika iwapo viongozi katika upinzani watakubali kumuunga mkono ama ukosefu wa umoja katika upinzani utalemaza uwezo wake. Sifuna hana la kupoteza upinzani ukishinda au ukikosa kushinda urais. Atakuwa ameuboresha msingi wake wa kisiasa kwa siku za usoni.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 5 hours ago

Kindiki kona mbaya tishio kutoka pande tatu zikimuandama

NAIBU wa Rais Prof Kithure Kindiki anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku mjadala kuhusu iwapo atasalia mgombeaji mwenza wa Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 ukizidi kushika kasi na kuzua maoni mseto. Japo amehudumu kwa chini ya miaka miwili tangu achukue nafasi hiyo, Prof Kindiki sasa ana kibarua cha kupambana na changamoto kutoka pande tatu zinazotishia mustakabali wake kisiasa. Mtihani wa kwanza unatokana na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameanzisha kampeni kali katika ukanda wa Mlima Kenya Mashariki, ngome ya kisiasa ya Profesa Kindiki. Baada ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Bw Gachagua ameahidi kufuatilia kila ziara ya Rais Ruto katika eneo hilo kwa mikutano ya kisiasa akinuia kupunguza ushawishi wa serikali kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao. Tangu ateuliwe naibu rais (DP), Prof Kindiki amekuwa akiongoza hafla za kufungua miradi ya maendeleo katika eneo hilo ikiwemo uzinduzi wa barabara, nyumba za gharama nafuu na hata miradi ya kilimo. Baadhi ya wafuasi wake wanasema ziara hizo zimedumisha imani ya wakazi kwamba eneo la Mlima Kenya bado lina sauti serikalini, ila Bw Gachagua anataka kuhakikisha imani hiyo haigeuki kuwa kura kwa Kenya Kwanza 2027. Kibarua cha pili kinatokana na siasa ambazo zinaendelea ndani ya Kenya Kwanza baada ya ushirikiano mpya na ODM. Hii ni kwa sababu viongozi wa ODM wameweka wazi kuwa wanataka nafasi ya naibu rais ikiwa ushirikiano wao na UDA utaendelea kabla na baada ya uchaguzi wa 2027. Baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwemo Naibu Kiongozi Simba Arati na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, wamesema nafasi hiyo inapaswa kutolewa kwa ODM. Chama hicho kimewataja Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Waziri wa Madini Hassan Joho na Wycliffe Oparanya kama wanaotosha kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema msukumo wa ODM unamweka Profesa Kindiki katika hali ngumu kwa sababu Rais Ruto anaweza kulazimika kutathmini kusalia naye au kumwondoa na kutumia nafasi hiyo kuimarisha ushirikiano na ODM. Prof Kindiki amejipata katika hali ngumu zaidi baada ya taarifa kudai kuwa baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakihusishwa na afisi ya naibu rais yamehamishiwa kwa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi. Hata hivyo, Prof Kindiki amekanusha madai hayo na kuyataja kuwa habari za uongo. Mkuu wa Uchumi wa Ubunifu na Miradi Maalum katika Afisi ya Rais Dennis Itumbi naye alisisitiza kuwa majukumu ya kila afisi yamebainishwa kwenye Katiba na sheria, na hakuna mamlaka yaliyoondolewa kutoka kwa Naibu Rais. Licha ya magumu yanayomkabili Profesa Kindiki, wadadisi kadhaa wa kisiasa wanaamini bado ndiye chaguo bora zaidi kwa Rais Ruto. Wanasema ameonyesha uaminifu, utulivu, uwezo na amekuwa akiepuka migogoro ya hadharani na rais, tofauti na waliomtangulia. Mdadisi wa masuala ya kisiasa Steve Ngari anasema Profesa Kindiki ameonyesha sifa zinazotarajiwa kwa afisi yake na anafaa kuendelea kusalia katika kambi ya Rais. Aidha, kura za maoni za Infotrak zimemweka Prof Kindiki kileleni mwa wanaopendelewa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto kwa asilimia 34, akifuatiwa na Gladys Wanga kwa asilimia 11 na Oburu Oginga kwa asilimia tano. Kwa mujibu wa Bw Ngari, kumwondoa Prof Kindiki kunaweza kuwakera wapigakura wa Mlima Kenya Mashariki ambao wanaona nafasi ya naibu rais kama ishara ya ushawishi wao serikalini. "Kazi ya Naibu Rais ni kuhudumu kama msaidizi wa karibu wa Rais. Kindiki ameonyesha sifa ambazo zinamwezesha kuendelea kuhudumu kwa wadhifa," akasema Bw Ngari. Pia, kunaweza kuibua taswira kwamba uaminifu na utendakazi hauthaminiwi ndani ya Kenya Kwanza. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku naye ameendelea kumtetea Prof Kindiki, akisisitiza kuwa hakuna nafasi iliyo wazi ya naibu rais na kwamba, Rais Ruto tayari ameamua mgombea wake mwenza.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 16 hours ago

Chelsea yahemea saini za wakongwe

CHELSEA inaonekana kubadili mbinu yake ya usajili wa wachezaji baada ya kuelekeza macho kwa wachezaji wazoefu wenye umri uliokomaa. Hii ni baada ya klabu hiyo ya Stamford Bridge kutupia ndoano difenda wa Crystal Palace Maxence Lacroix, straika wa Brighton Danny Welbeck na kiungo wa kati wa Brentford Jordan Henderson. Hatua hiyo ni tofauti na mwelekeo waliochukua miaka minne iliyopita wa kusajili wachezaji chipukizi kwa mikataba mirefu. Baada ya klabu hiyo kununuliwa na BlueCo mwaka 2022, Chelsea ilitumia fedha nyingi kusajili nyota waliokuwa tayari wamejijengea majina makubwa. Raheem Sterling aliwasili kutoka Manchester City akiwa na miaka 27, Kalidou Koulibaly (31) alitua kutoka Napoli ya Italia huku Pierre-Emerick Aubameyang (33) akiingia kutokea Barcelona ya Uhispania. Lakini ukosefu wa mataji ulimgarimu kocha Thomas Tuchel kazi yake. Wakati wa kipindi kirefu cha uhamisho 2022 wamiliki wa BlueCo walipiga abautani kugeukia chipukizi. Aliyefungua ukurasa huo ni Enzo Fernandez kisha wakafuata mastaa wengine ikiwemo Moises Caicedo na Cole Palmer ambao wameonyesha ukwasi wao kwa kiwango fulani. Hata hivyo, kulikuwepo pia mastaa walioishia kuwa moto wa karatasi - Mykhailo Mudryk, Joao Feli na Wesley Fofana. Sasa baada ya miaka minne ya kukamata nafasi ya 12, sita, nne na 10 msimu jana pamoja na mataji 'madogo ya Conference League na Kombe la Klabu Bingwa Duniani, wamiliki wamegeukia tena mastaa wakongwe wenye uzoefu. Lacroix 26, ndiye mwenye umri mdogo kati ya watatu hao kwani Welbeck ana umri wa miaka 35 naye Henderson miaka 36. Chelsea inasemekana kuwa tayari kutoa Pauni milioni 52 (Sh9.2 billioni) kumsajili Lacroix. Naye Welbeck anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na miamba hao kwani amebakisha mwaka mmoja pekee katika mkataba wake Brighton. Iwapo Welbeck atatua Chelsea huenda akachukua nafasi ya Liam Delap, 23, ambaye alisajiliwa kutoka Ipswich Town mwaka jana akiwa mmoja wa washambuliaji waliopigiwa upatu mkubwa kung'ara. Kocha mpya Xabi Alonso, ambaye amewasili kutoka Bayer Leverkusen ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), anasemekana kupendelea kikosi chenye mseto wa chipukizi na wazoefu. Sajili hizi kongwe zikifua dafu mashabiki wa Blues watasubiriwa kuona iwapo watawapaisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (EPL).

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 20 hours ago

Ndovu 14 wafa kwa njia ya kutatanisha mbugani Amboseli

SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) limeanzisha uchunguzi kuhusu vifo vya kutatanisha vya ndovu 14 katika Mbuga ya Wanyama ya Amboseli mwezi uliopita. Viongozi wa Kaunti ya Kajiado nao wanataka ripoti ya haraka kubaini kilichosababisha vifo vya ndovu hao. Mizoga ya wanyama hao, waliokuwa wa umri na jinsia tofauti, ilipatikana katika maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo ndani ya kipindi cha wiki mbili. Madaktari wa mifugo wa KWS walichukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara ili kubaini chanzo cha vifo hivyo. Afisa mmoja wa KWS, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema ndovu hao walikuwa wakifuatiliwa na madaktari baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa kabla ya kufariki. "Madaktari walijaribu kuwapa matibabu lakini hawakupata nafuu. Mwanzoni ilidhaniwa walikuwa na uchovu wa misuli, lakini matibabu hayakufaulu. Baada ya uchunguzi wa mizoga na ukusanyaji wa sampuli, ilizikwa ndani ya hifadhi," akasema. "Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya tembo kufa kwa muda mfupi katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli," akaongeza. Mkuu wa Mawasiliano wa KWS, Duncan Juma, alisema sampuli zilifikishwa kwa maabara ya Serikali na uchunguzi unaendelea. Vifo hivyo vimewatia wasiwasi viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, ambao wametaka KWS ichapishe mara moja ripoti ya uchunguzi. "Jamii zimeishi na ndovu hao kwa miaka kadhaa. Hatujawahi kushuhudia idadi kubwa namna hii ikifa kwa muda mfupi," akasema Bw Lenku. Seneta wa Kajiado Samuel Seki pia aliikosoa KWS, akiishutumu kwa kutumia kesi mahakamani kuchelewesha uhamishaji wa usimamizi wa mbuga ya Amboseli kwa Serikali ya Kaunti ya Kajiado pamoja na mapato yake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo 22 hours ago

Iran yasema ingali inadhibiti Hormuz licha ya kunyeshewa mabomu na Amerika wiki 2 mfululizo

DUBAI, UAE: IRAN imesema ingali inadhibiti Mkondo-Bahari wa Hormuz wala haikusudiii kurejelea mazungumzo ya amani na Amerika baada ya Rais Donald Trump kusitisha kampeni ya mabomu ya wiki mbili ambayo wandani wake walimweleza imetimiza azma yake. Kufuatia mashambulizi makali ya mabomu siku 13 mfululizo yaliyosababisha Tehran kulenga ngome za Amerika kulipiza kisasa, Trump alisimamisha kampeni hiyo wikendi. Iran ilisema itasitisha mashambulizi yake binafsi kwa kipindi ambacho Amerika itasimamisha. Mwisho wa kampeni ya mabomu ya Amerika ulisababisha bei za mafuta kuporomoka kwa matumaini kuwa michakato ya usambazaji bidhaa iliyotatizwa duniani itarejelea shughuli zake. Lakini kwa ishara kuwa Tehran huenda tayari inafanyia majaribio mkataba mpya wa kusitisha vita, Jordan iliripoti kuangusha droni mbili na duru za usalama za Iraqi zikasema droni hizo zililenga wapiganaji wa Wakurdi wa Iran eneo la Iraq Kaskazini. Majeruhi hawakuripotiwa katika visa hivyo. Uamuzi wa Trump kusitisha kampeni unaashiria ushauri kutoka kwa jeshi lake kwamba mabomu, yaliyonuiwa kuvunja udhibiti wa Irani kwenye mkondo, yamefikia upeo ambao yangeweza kufanikisha, kulingana na afisa wa Amerika na ripoti kadhaa za vyomvo vya habari. Afisa wa Amerika alisema kwamba makamanda wa jeshi walimshauri rais kwamba wameishiwa na vituo vya kushambulia. Mwenyekiti wa Wakuu wa Wahudumu, Jenerali Dan Caine, alielezea wasiwasi kuhusu kumalizika kwa silaha za kujikinga angani, alisema afisa. Balozi wa Amerika kwa Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alisema Jumapili kuwa Trump alisitisha kampeni kuruhusu majadiliano. Trump, Waziri wa Masuala ya Kigeni Marco Rubiona maafisa wengine wa Amerika wameelezea Iran kama "inayosihgi kuwepo mkataba." Lakini msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Iran, Esmail Baghaei, alisema katika kikao cha vyombo vya habari jana kwamba Iran haijaomba kurejelea mazungumzo ya amani na Amerika. Jumbe bado zilitumwa kati ya pande husika kupitia wapatanishi na Iran haikutelekeza diplomasia, lakini "ripoti kuhusu Iran kuomba majadiliano na Amerika ni za uongo," alisema Baghaei. "Hii haimo katika DNA yetu." Tehran vilevile iliashiria ingali inadhibiti mkondo muhimu zaidi wa maji na masoko ya nishati duniani.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 28 Jul 2026 02:55:19

Walimu wapata matumaini baada ya TSC kutangaza nafasi 34,000 za kuwapandisha vyeo

TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) imetangaza nafasi 34,016 za kupandisha walimu vyeo katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya mafunzo ya walimu. Waliopandishwa wapo katika madaraja 30, kuanzia Mwalimu Mkuu Mwandamizi II (Senior Teacher II) hadi Mkuu wa Shule (Chief Principal). Walimu wametakiwa watume maombi ya kazi hizo kupitia mtandao wa TSC kabla ya Agosti 10, 2026, huku TSC ikisisitiza kuwa maombi yanayowasilishwa moja kwa moja kupitia kwa mwalimu kufika na stakabadhi katika afisi za tume hayatakubaliwa. "Walimu wenye sifa zinazohitajika wanapaswa kutuma maombi yao kupitia tovuti ya TSC www.teachersonline.go.ke kabla ya Jumatatu, Agosti 10, 2026. Hakuna kuwasilisha stakabadhi katika afisi za TSC," ilisema TSC katika tangazo lake. Hatua hiyo inawapa matumaini walimu wengi ambao wamekwama katika madaraja yale yale kwa miaka mingi licha ya kutimiza masharti ya kupandishwa vyeo. Serikali imetenga Sh2 bilioni katika bajeti ya sasa kufanikisha shughuli hiyo. Hivi majuzi, TSC iliambia Bunge kuwa walimu 178,871 wa shule za msingi na upili wameendelea kubaki katika madaraja yao kutokana na uhaba wa fedha kwa muda mrefu. Walimu wengi waliokwama wako katika daraja la C3 kwa sekondari na C1 kwa shule za msingi. Kati ya nafasi zilizotangazwa, nyingi zinalenga madaraja ya kati ya taaluma. Kuna nafasi 13,490 za Senior Teacher II, nafasi 5,956 za Senior Master IV, na nafasi 4,210 za Senior Teacher I, ambazo zinatarajiwa kuwapa maelfu ya walimu nafasi ya kupanda vyeo. Tangazo hilo limekuja wakati Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) ukiendelea kushinikiza TSC kutangaza nafasi za kupandisha walimu 135,000 ambao wamekwama kwa muda mrefu katika madaraja yao ya kazi. Katibu Mkuu wa Kuppet, Akello Misori, alisema walimu wengi wamekuwa wakisubiri kupandishwa vyeo kwa miaka mingi licha ya kustahili. Kwa upande mwingine, wakuu wa shule kupitia chama cha KESSHA pia wameitaka TSC kuharakisha mchakato huo, wakisema walimu wakuu wengi hasa walio katika daraja la D3 wamevunjika moyo kwa kukosa nafasi za maendeleo ya kazi. Mwenyekiti wa TSC, Dkt Jamleck Muturi, alisema serikali imewapandisha vyeo walimu 274,285 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, lakini akakiri kuwa wengi bado wamekwama katika madaraja yao. TSC pia ilisema waliofaulu katika mahojiano watatakiwa kuwasilisha hati halali za zinazozingatia masharti ya Sura ya Sita ya Katiba kabla ya kuteuliwa rasmi, na watapangiwa shule ambako nafasi hizo zinapatikana.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 28 Jul 2026 01:55:00

Raia wa kigeni apigania mali baada ya ndoa yake na mkewe Mkenya kuvunjika

RAIA wa Ireland aliyekuwa amehamia Kenya kwa matumaini ya kuanza maisha mapya na mwanamke aliyefahamiana naye kupitia mtandao sasa amejikuta akihusika katika kesi tatu mahakamani zinazohusu mamilioni ya pesa, mali na kuvunjika kwa ndoa yao. Bw Joel Patrick Fitzpatrick anasema aliuza mali aliyorithi kutoka kwa marehemu mama yake nchini Ireland na kuhamia Watamu, Kaunti ya Kilifi, akiwa na hamu ya kuanzisha biashara na kujenga makazi pamoja na Bi Martha Wanjiru Muhoro, ambaye baadaye alifunga naye ndoa ya serikali mnamo Julai 23, 2025. Hata hivyo, chini ya mwaka mmoja tangu ahamie Kenya, mwanajeshi huyo mstaafu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani sasa anakabiliwa na kesi kadhaa, zikiwemo za madai kuhusu matumizi yasiyo halali ya urithi wake. Katika kesi ya hivi punde iliyo mbele ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Malindi, Bw Fitzpatrick anataka Mahakama imzuie Bi Muhoro kuuza, kuhamisha umiliki, kukodisha au kufanya shughuli yoyote kwa ardhi ya Gede/Dabaso, akidai ilinunuliwa kwa Sh25 milioni alizomtumia ili anunue kwa niaba yake. Jumanne iliyopita, Mahakama ilimpa Bi Muhoro wiki mbili kuwasilisha majibu yake baada ya wakili wake kuomba muda zaidi. Mahakama pia iliongeza amri ya kudumisha hali ilivyo na kuagiza pande zote mbili kubadilishana stakabadhi za kesi kabla ya kesi hiyo kutajwa Oktoba 12 kwa maelekezo zaidi. Kulingana na stakabadhi za Mahakama, Fitzpatrick ni mshauri wa masuala ya biashara, siasa na mazingira. Katika kesi nyingine ya madai, anaitaka Mahakama iamuru arejeshewe zaidi ya Sh35.8 milioni ambazo anadai alituma kwenye akaunti ya Benki ya Family inayomilikiwa na Bi Muhoro, huku akiomba akaunti hiyo izuiwe ili fedha zilizomo zisitolewe hadi kesi itakapoamuliwa. Stakabadhi za Mahakama zinaonyesha kuwa wawili hao walifahamiana kupitia tovuti ya kutafuta wapenzi mwaka 2023. Bw Fitzpatrick anasema alirithi asilimia 75 ya mali za marehemu mama yake, ikiwemo nyumba katika Kaunti ya Dublin nchini Ireland, na akamkabidhi Bi Muhoro jukumu la kuandaa uhamisho wake kwenda Kenya kwa kutafuta ardhi, kufuatilia taratibu za uhamiaji na kusimamia mipango ya kifedha. Anadai alimtumia fedha nyingi, zikiwemo euro 250,000 (takriban Sh36.9 milioni) mwezi Aprili 2025 kwa ajili ya kununua ardhi na gari, pamoja na uhamisho mwingine wa euro 10,000 (takriban Sh1.5 milioni) mara nne, euro 15,000 (takriban Sh2.2 milioni) mwezi Septemba na euro 226,860 (takriban Sh33.4 milioni) mwezi Oktoba, ambazo anasema zilikuwa sehemu ya mwisho ya urithi wake. Anadai Bi Muhoro alimshawishi fedha zote zipitie kwenye akaunti yake hadi atakapohamia Kenya, lakini baadaye hakumjumuisha katika umiliki wa ardhi na gari licha ya kuwa ndiye aliyefadhili ununuzi wake. Bw Fitzpatrick anasema amebaki hana mali na ana hofu kuwa fedha zilizobaki zinaweza kutolewa kwenye akaunti hiyo kabla ya kesi kusikilizwa. Kwa upande wake, Bi Muhoro anakiri kupokea fedha hizo lakini anakanusha kuzitumia vibaya. Anasema matumizi yote yalifanywa kwa uwazi na kwa makubaliano ya pamoja walipokuwa wakijiandaa kuanza maisha yao ya ndoa. Pia anasema aliacha kazi yake ya ualimu nchini Qatar kwa ombi la Fitzpatrick na kurejea Kenya kujiandaa kwa harusi yao. Anaeleza kuwa mali hizo zilisajiliwa kwa jina lake kwa sababu wakati huo Fitzpatrick, akiwa raia wa kigeni, hakuwa na stakabadhi zilizohitajika kusajili mali hizo kwa jina lake. Bi Muhoro anasema baadaye uhusiano wao ulivurugika na kumshutumu Bw Fitzpatrick kwa ukatili na unyanyasaji, akiiomba Mahakama itupilie mbali kesi hiyo.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Tue, 28 Jul 2026 00:55:43

Omtatah apinga kinga ya IMF na Benki ya Dunia inayowazuia kushtakiwa nchini

SENETA wa Busia Okiya Omtatah akishirikiana na wanaharakati Bernard Muchiri na Naomi Misati, wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakitaka sheria inayoyapa mashirika ya kifedha ya IMF na Benki ya Dunia, kinga dhidi ya mashtaka, ushuru na kufichua taarifa kuwa kinyume cha Katiba. Walalamishi wanapinga Kifungu cha Sheria ya Bretton Woods ya 1963, wakisema kimepitwa na wakati wala hakiendani na Katiba ya 2010. Kwa mujibu wa kesi hiyo, sheria hiyo inaipa serikali mamlaka makubwa ya kuingia mikataba ya kimataifa ya kifedha, kukopa fedha na kutumia hazina ya umma bila usimamizi wa kutosha wa Bunge. Aidha, sheria hiyo inalinda IMF na Benki ya Dunia dhidi ya kuwajibishwa katika mahakama za Kenya. Wanadai kuwa Kifungu cha tano cha sheria hiyo kinazipa taasisi hizo kinga dhidi ya kushauri mahakama, ushuru, ukaguzi, kutwaliwa kwa mali, jambo ambalo linawanyima Wakenya haki ya kupata haki, kusikilizwa kwa usawa na kupata taarifa. Aidha, wanasema sheria hiyo inaruhusu serikali kutekeleza mikataba ya kimataifa bila idhini ya Bunge na kutoa fedha kutoka Hazina Kuu ya Fedha moja kwa moja kwa IMF na Benki ya Dunia bila kuidhinishwa kila mwaka na wabunge. Bw Omtatah na wenzake wanaeleza kuwa hali hiyo inadhoofisha mamlaka ya Bunge na Mahakama katika kusimamia matumizi ya fedha za umma. Pia inakiuka masharti mbalimbali ya Katiba, pamoja na sura inayohusu usimamizi wa fedha za umma. Mahakama Kuu imewaagiza washtakiwa na wahusika wengine kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 14. Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 29, 2026, kwa mwelekeo zaidi.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Mon, 27 Jul 2026 22:55:30

Serikali yasema imepata shamba la kuzipa makao familia 21,000 zilizofurushwa Mau

SERIKALI inakaribia kutatua moja ya migogoro ya muda mrefu katika Bonde la Ufa baada ya kuthibitisha kuwa imepata mashamba makubwa katika Kaunti ya Narok ili kuzipa makazi mapya familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau pamoja na watu wengine wasio na ardhi. Hatua hiyo inalenga kumaliza mateso ya zaidi ya familia 21,000 zilizofurushwa katika oparesheni mbalimbali za serikali ndani ya kipindi cha miaka 21 iliyopita. Tangazo hilo linajiri huku Rais William Ruto akitarajiwa kuzuru Kusini mwa Bonde la Ufa mwezi ujao. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kuwafidia waathiriwa wa Mau na kuwapa makazi mapya waliokosa ardhi katika Kaunti ya Narok. Akizungumza Kapkwen, Kaunti ya Bomet, alisema Wizara ya Ardhi inakamilisha taratibu za mwisho na kwamba orodha ya walionufaika itatangazwa hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh, pia alisema maagizo ya Rais Ruto ya kuwahamisha waathiriwa hao tayari yanatekelezwa. "Serikali imefanikiwa kupata ardhi ya kuhamishia familia zilizofurushwa kutoka Msitu wa Mau katika maeneo ya Narok Kusini na Narok Magharibi pamoja na watu wasio na ardhi Angata Barikoi, eneobunge la Kilgoris," akasema. Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, alisema serikali tayari imelipia baadhi ya mashamba hayo na hatimiliki zimekabidhiwa Wizara ya Ardhi. Pia alisema serikali iko katika hatua za mwisho za kununua zaidi ya ekari 5,000 zinazomilikiwa na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Isaiah Cheluget, katika eneo la Tendwet, Narok Magharibi. Kwa mujibu wa Seneta huyo, uhakiki wa majina ya waathiriwa umekamilika na serikali sasa inakamilisha utaratibu wa kugawa fidia na ardhi. Suala la kufurushwa kwa wakazi wa Mau limekuwa ajenda ya kisiasa kwa zaidi ya miongo miwili. Tangu 2005, marais na wagombea mbalimbali wameahidi kuwafidia na kuwapa makazi mapya walioathiriwa, lakini ahadi hizo zimekuwa zikicheleweshwa. Katika muhula wa pili wa Rais Uhuru Kenyatta, maelfu ya familia zilifurushwa tena kutoka maeneo yanayopakana na msitu, huku nyumba, mashamba na mali nyingine zikiharibiwa katika operesheni iliyoongozwa na aliyekuwa Kamishina Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya. Rais Ruto amesema serikali yake tayari imelipa familia 2,000 fidia ya Sh300,000 kila moja na imeahidi kuwahamisha jumla ya familia 12,000 ili ziishi maisha ya kibinadamu. Hata hivyo, baadhi ya viongozi na wakazi wanasema kiwango hicho cha fedha hakitoshi kununua ardhi wala kujenga nyumba. "Kiasi cha Sh300,000 hakitoshi hata kununua kiwanja, sembuse kujenga nyumba. Watu walipoteza mashamba, mifugo, mazao na mali nyingine. Wanastahili fidia ya haki," alisema kiongozi wa eneo hilo Johnstone Kiptanui. Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, ambaye hapo awali aliunga mkono kufurushwa kwa wakazi hao ili kulinda msitu, sasa anasema wakati umefika serikali iwape makazi mapya na fidia kwa kuwa lengo la kuhifadhi Msitu wa Mau. Hatua ya serikali ya kuharakisha mpango huo inachukuliwa kuwa jaribio la kumaliza mgogoro ambao umeathiri maelfu ya familia na umekuwa ukitumiwa kama ajenda ya kisiasa katika kila uchaguzi mkuu tangu 2007.

read more