T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 15 Oct 2026 10:50:58

Ushuru mpya wa chai wazua hofu kwa wakulima

KANUNI mpya za ushuru wa chai za mwaka 2026 zimezua mjadala katika sekta hiyo huku wakulima wadogo wakihoji iwapo gharama hizo zitapunguza mapato yao na kusababisha kutozwa ushuru mara mbili. Kanuni hizo zimewasilishwa upya Bungeni baada ya Mbunge wa Gatundu Kusini George Kagombe, aliyekuwa mdhamini wa mapendekezo ya awali, kulaumiwa kwa kulenga maslahi yake binafsi katika sekta ya chai. Kagombe pia alitajwa kuwa mkurugenzi wa eneo wa Shirika la Maendeleo ya Chai (KTDA). Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula alirejesha suala hilo kwa wabunge baada ya malalamishi yaliyowasilishwa na Dkt John Kennedy Omanga kuruhusiwa, na kubainika kuwa Kagombe hakutangaza maslahi yake kama inavyotakiwa na kanuni za Bunge. Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Chai nchini (TBK), Willy Mutai, hata hivyo, amehakikishia wakulima kuwa ushuru huo hautakatwa kutoka kwa malipo yao ya kila mwezi wala bonasi ya kila mwaka. Katika mahojiano na Taifa Leo, Mutai alisema ushuru huo utatozwa waagizaji na wanaosafirishaji chai nje ya nchi, wala si wakulima au viwanda vya chai. "Mapato ya wakulima kutokana na malipo ya kila mwezi na bonasi ya kila mwaka yataendelea kuwa kama yalivyoamuliwa na viwanda vyao," alisema. Chini ya kanuni hizo, wasafirishaji wa chai watalipa ushuru wa asilimia 0.8 ya thamani ya chai inayouzwa moja kwa moja au kupitia minada, huku waagizaji wakitozwa asilimia 100 ya thamani ya kila shehena ya chai inayoingizwa nchini. Mutai alisema ushuru huo unalenga kufadhili utafiti, kutangaza chai ya Kenya katika masoko ya kimataifa, kuboresha miundombinu na kuimarisha mapato ya wakulima. Asilimia 50 ya fedha hizo zitaelekezwa kwa hazina ya kuleta uthabiti wa bei ya chai, asilimia 20 kwa Taasisi ya Utafiti wa Chai iliyoko Kericho, asilimia 15 kwa serikali za kaunti zinazolima chai kwa ajili ya miundombinu na asilimia 15 kwa TBK. Alisema fedha hizo zitakaguliwa kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa fedha za umma, huku matokeo ya ukaguzi yakitarajiwa kuwekwa wazi. Mutai alitaja ushindani katika soko la kimataifa kama sababu nyingine ya kuanzishwa kwa ushuru huo. Kenya huuza chai katika masoko 100, lakini asilimia 85 ya mauzo yake yanategemea masoko 10, yakiwemo Pakistan, Iran, Uingereza, Urusi na Misri. Bodi hiyo inalenga kupanua soko hadi Amerika Kaskazini, Afrika Magharibi, China na maeneo mengine ya Asia. Wakati huo huo, wakulima wanaanza kupokea bonasi ya mwaka ya msimu wa 2025/2026, huku viwanda vya KTDA vikitarajiwa kulipa kati ya Sh12.50 na Sh50 kwa kila kilo ya majani, kutegemea masoko ya ndani na nje. Mutai alisema ushuru huo utasaidia kuboresha utafiti, huduma za ugani, uzalishaji na ubora wa chai, hatua zinazotarajiwa kuongeza ushindani na mapato ya wakulima. Hata hivyo, maswali kuhusu athari za ushuru huo kwa gharama za biashara na uwezekano wa gharama hizo kuhamishiwa kwa wadau wengine yanaendelea kusubiri majibu huku kanuni hizo zikisubiri hatua za Bunge.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 15 Oct 2026 11:02:56

Kukosa kutoka jasho ni ulemavu? Jamii yataka kutambuliwa rasmi

JAMII ya Ilimanyang katika Kaunti ya Turkana inataka itambuliwe rasmi kama watu wenye ulemavu kutokana na hali adimu ya kiafya inayowafanya washindwe kutoa jasho, jambo linalohatarisha maisha yao katika joto kali la eneo hilo. Jamii hiyo inayokadiriwa kuwa na watu 600, wengi wao wakiishi katika kijiji cha Kapua, Turkana ya Kati, hulazimika kunyunyiziwa maji  mara kwa mara ili kupunguza joto na kuzuia miili yao kupata joto kupita kiasi. Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa (NGEC), Rehema Jaldesa, amesema tume hiyo itashirikiana na wataalamu wa afya kufanya uchunguzi kubaini hali hiyo na hatua zinazofaa kuchukuliwa. Afisa mkuu wa huduma za afya Turkana, Gilchrist Lokoel, alisema dalili zilizoripotiwa zinafanana na ugonjwa adimu wa kurithi unaojulikana kama hypohidrotic ectodermal dysplasia (HED), unaoweza kuathiri tezi za jasho, nywele na meno. Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kina unahitajika kuthibitisha iwapo jamii hiyo ina ugonjwa huo. Nancy Ebolon, ambaye amekuwa akipigania haki za watu wa Ilimanyang, alisema waathiriwa hulazimika kula mara kwa mara na kunyunyiziwa maji ili kuendelea kuishi katika mazingira yenye joto kali. "Mtu hapa Ilimanyang huzimia asipokula ndani ya saa moja au asipopata maji ya kunyunyiziwa mwilini baada ya nusu saa. Hali ikizidi kuwa mbaya, hufariki," alisema. Alisema watoto wanaozaliwa na hali hiyo wako katika hatari kubwa zaidi, kwani huhitaji uangalizi wa karibu na kupozwa mara kwa mara ili kuzuia miili yao kupata joto kupita kiasi. Mbali na changamoto za kiafya, jamii hiyo inakabiliwa na unyanyapaa na imani potofu. Baadhi ya watoto wanaozaliwa na hali hiyo hukataliwa na baba zao, hali inayozidisha mateso ya familia zinazowalea. Elimu pia imeathirika kutokana na mazingira magumu wanayoishi. Jaldesa alisema baadhi ya wanafunzi hulazimika kusafiri kilomita 120 kwenda na kurudi ili kufanya mitihani ya kitaifa. "Mtoto anawezaje kusafiri kilomita 120 katika joto kali kwa siku moja ili kufanya mtihani?" aliuliza, akitaka mipango maalumu ya kuwasaidia wanafunzi hao. Jaldesa alisema NGEC itaratibu kambi ya matibabu na kushirikisha Baraza la Kitaifa la Watu Wenye Ulemavu ili kubaini uwezekano wa jamii hiyo kusajiliwa na kupata msaada wa serikali. Kutambuliwa kama walemavu kunaweza kuwawezesha watu wa jamii hiyo kupata huduma maalumu za afya, elimu na ulinzi wa kijamii. Hata hivyo, jamii hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa maji, umaskini na changamoto za kupata vitambulisho vya taifa na vyeti vya kuzaliwa, hali inayoweza kuwazuia kupata huduma muhimu. Wanatumai kuwa kutambuliwa rasmi kutasaidia kupunguza ubaguzi na kufungua njia ya kupata huduma zinazozingatia mahitaji yao ya kipekee.

read more