T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 17 Jul 2026 01:55:22

Wakazi watumia teknolojia kuwakomboa punda 100 walioibwa

WAKAZI wa kijiji cha Kokuro, Kaunti ya Turkana, wameanza kutumia teknolojia ya kidijitali kukabiliana na wizi wa punda na magonjwa ya mifugo, hatua inayobadilisha maisha katika eneo la mpakani mwa Kenya na Ethiopia. Mabadiliko hayo yalidhihirika mwezi uliopita baada ya wavamizi wenye silaha kuiba zaidi ya punda 100. Badala ya kuanza msako wa siku nyingi, wakazi waliripoti tukio hilo kupitia Kituo cha Kidijitali cha Habari za Punda (Donkey Digital Information Hub). Taarifa zilifika haraka kwa maafisa wa usalama na punda hao wakapatikana. Katika eneo hilo, punda ni nguzo ya maisha ya kila siku. Hutumika kubeba maji, chakula, wagonjwa, watoto na mizigo wakati wa kuhama kutokana na ukame. Hapo awali, ukosefu wa mtandao na umbali wa vituo vya serikali ulifanya iwe vigumu kuripoti wizi au magonjwa kwa wakati. Kupitia programu ya Punda Wangu, kila punda husajiliwa kwa picha na alama zake maalumu kama rangi, makovu na michoro ya mwili. Mfumo huo wa kutumia Akili Unde hurahisisha kutambua punda aliyeibwa au kupatikana. Wafugaji wanaweza pia kuripoti wizi, magonjwa au ukatili dhidi ya wanyama kupitia kituo hicho au simu bila malipo, huku maafisa wa usalama na madaktari wa mifugo wakichukua hatua kwa haraka. Mwanafunzi, Nathan Ebei, anasema teknolojia hiyo pia imewasaidia vijana kupata huduma za intaneti na kuwapa wafugaji ushauri wa kitabibu kuhusu chanjo, matibabu na utunzaji wa punda bila kusafiri umbali mrefu. Kwa mujibu wa Takwimu za Kitaifa (KNBS), idadi ya punda nchini ilipungua kutoka milioni 1.8 mnamo 2009 hadi kati ya milioni 1 na 1.17 mnamo 2019. Kupungua huko kunahusishwa na biashara haramu ya ngozi za punda, uchinjaji na wizi unaochochewa na mahitaji ya ngozi hizo katika bara la Asia. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Kuhusu Ufugaji wa Kuhamahama (IPDR), Mariko Akileng, alisema mfumo huo unalenga kuunganisha wafugaji moja kwa moja na polisi husika ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa. Pia shirika hilo linaimarisha utekelezaji wa sheria kwa kuwapa mafunzo maafisa wa serikali na wadau kuhusu ulinzi wa wanyama na uendeshaji wa mashtaka dhidi ya wahalifu.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 17 Jul 2026 00:55:07

Mke mwenza aliyeuguza mume ashinda kesi ya urithi wa Sh200 milioni

MAHAKAMA Kuu ya Mombasa imeamua kwamba, katika hali za kipekee, talaka inaweza kuchukuliwa kuwa ilitokea pale ambapo ndoa imekoma, kwa kuzingatia vitendo vya wanandoa ambao wameendelea na maisha yao tofauti hata kama hakuna amri rasmi ya talaka. Mahakama ilisema ndoa inapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha ya wahusika na kwamba ndoa inaweza tu kuendelea kuwepo kwa muda ambao wanandoa wote wanakubali kuendelea nayo. Kulingana na mahakama, kushikilia vinginevyo kunaweza kuifanya ndoa ionekane kama aina ya kifungo gerezani na kukiuka haki ya kikatiba ya ridhaa ya hiari ya kuingia katika ndoa. Uamuzi huo ulitolewa katika mzozo wa urithi wa mali yenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni kufuatia kifo cha Prem Lal Ramnath mnamo Novemba 24, 2019. Mzozo uliwahusisha Bi R.B, aliyedai kuwa mjane wa marehemu, dhidi ya Bi A.G na watoto wake, V.L na Y.G. Bi R.B aliwasilisha cheti kilichoonyesha kuwa alifunga ndoa na marehemu mwaka 1999 Mombasa na baadaye akaomba barua za usimamizi wa mirathi. Alisema aliishi na marehemu kwa karibu miaka 20, akimsaidia katika biashara zake na kumhudumia wakati wa ugonjwa. Pia alitoa figo moja mwaka 2012 ili kuokoa maisha ya marehemu. Hata hivyo, Bi A.G na watoto wake walipinga mchakato huo, wakidai kwamba ndoa ya Kihindu kati ya Bi A.G na marehemu haikuwahi kuvunjwa, hivyo marehemu hangeweza kufunga ndoa nyingine kihalali. Pia walidai kuwa Bi R.B alificha taarifa muhimu na alihusika katika udanganyifu wa kupata usimamizi wa mali. Hata hivyo, ushahidi ulionyesha kuwa Bi A.G alihamia Canada mwaka wa 2001 na hakurejea Kenya hadi baada ya kifo cha marehemu mwaka 2019. Pia ilikubaliwa kuwa marehemu aliishi na Bi R.B wakati wa kifo chake. Mahakama ilibaini kuwa Bi A.G na marehemu walikuwa wameishi mbali kwa miaka mingi, huku Bi R.B akiwa ndiye aliyemhudumia marehemu wakati wa ugonjwa wake. Mahakama ilikataa kubatilisha ndoa ya Bi R.B na marehemu, ikisema alikuwa mke wake na alikuwa na haki ya kuomba urithi bila kuhitaji ridhaa ya watoto wa marehemu. Mahakama pia ilikataa madai kwamba Bi R.B alitoa figo kwa malipo, ikisema hakuna ushahidi wa malipo hayo na kwamba madai hayo yalilenga kuchafua sifa yake. Pia ilikosoa walalamishi kumtaja kwa dharau kutokana na kazi yake ya awali ya kusakata densi, ikisema mtazamo huo unaonyesha ubaguzi wa kitabaka. Kwa kuzingatia hali halisi ya uhusiano huo, mahakama ilisema si haki kwa mwenzi anayemwacha mwenzake kwa muda mrefu na kuishi maisha ya kujitegemea kurejea baadaye na kudai mali ambayo huenda mwenzi mwingine aliitafuta na kuijenga wakati wa kutokuwepo kwake.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Fri, 17 Jul 2026 00:21:49

Ol Kalou: DCP ya Gachagua yabwaga UDA ya Ruto

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imemtangaza Sammy Douglas Kamau Waweru Ngotho kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou baada ya kumshinda mpinzani wake mkuu kwa tofauti kubwa ya kura. Bw Ngotho alipata kura 35,440 huku mpinzani wake mkuu, Muchina Nyaga wa chama cha United Democratic  Alliance (UDA), akipata kura 5,460. Afisa Msimamizi wa Uchaguzi, Anthony Njiraini, alitangaza matokeo hayo saa kumi na mbili Ijumaa alfajiri baada ya zoezi la kujumlisha kura lililodumu usiku kucha katika Shule ya Sekondari ya Ol Kalou, mjini Ol Kalou. Ni mgombea huyo wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) na maajenti wake pekee waliohudhuria zoezi hilo. Akihutubu kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa mshindi, mbunge huyo mteule alilaani ghasia zilizodaiwa kusababishwa na wahuni wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi siku ya Alhamisi, hali iliyovuruga upigaji kura katika vituo vingi vya kupigia kura ndani ya mji wa Ol Kalou. "Inasikitisha kwamba tumepoteza maisha kutokana na vurugu hizi za uchaguzi. Mmoja wa waliojeruhiwa, ambaye nilimfahamu vyema na alikuwa mfuasi wangu mkubwa, alifariki kutokana na majeraha yake. Wahuni hao pia waliwashambulia wanahabari wasio na hatia ambao silaha zao pekee zilikuwa kamera, simu na vijitabu. Inauma kwa sababu uhuni huu ulipangwa na kufadhiliwa na baadhi ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya kwa usaidizi wa maafisa wakuu wa polisi," alisema Bw Ngotho. Alisema ushindi wake mkubwa ni ujumbe wazi kwa serikali kwamba imepoteza uungwaji mkono wa wananchi. "Kilichotokea hapa kinaonyesha yatakayojiri mwaka ujao. Ninaishukuru IEBC kwa kazi nzuri. Ikiwa uchaguzi wa mwaka ujao utaendeshwa kwa namna hii, sina shaka kuwa  Muungano wa Upinzani utashinda. Mmeonyesha sisi na Wakenya wote kuwa IEBC ni tume huru kweli," alisema. Pia, aliwapongeza maafisa wa polisi waliovalia sare rasmi, akisema walitekeleza wajibu wao kwa weledi. Kamishna wa IEBC Hassan Noor aliwahakikishia Wakenya kuwa tume hiyo itaendesha uchaguzi ulio bora zaidi mwaka ujao. "Zoezi hili limefanikiwa na tumepata mafunzo muhimu yatakayotusaidia kuboresha uchaguzi ujao. Ninawasihi wanasiasa waelekeze nguvu zao kwa wapigakura, si kwetu. Tuna IEBC moja pekee, na tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha uchaguzi wa mwaka ujao utakuwa huru na wa kuaminika," alisema kamishna huyo. Seneta wa Nyandarua John Methu, aliyeratibu kampeni za mgombeaji wa DCP, pia alilaani vurugu hizo akisisitiza kuwa waliowashambulia wananchi walikuwa maafisa wa polisi. "Ninamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi awakamate na kuwafikisha mahakamani wahuni hawa. Tuna sura zao, taarifa zao na video zinazowaonyesha wakitekeleza vitendo hivyo. Ukiwakamata utakuwa umeitumikia Kenya kwa uadilifu. Usipofanya hivyo, utakuwa umeacha nchi hii kuelekea pabaya," alisema Seneta Methu. Bi Jedidah Muchoki, mwanasiasa kutoka Ndia aliyefuatilia uchaguzi huo kwa niaba ya mgombeaji wa DCP, alisema polisi wanapaswa kuwadhibiti wahuni hao kabla hali haijawa mbaya zaidi. "Tunawashukuru wapigakura wa Ol Kalou kwa jinsi walivyoendesha uchaguzi kwa amani. Uchaguzi ulikuwa wa utulivu hadi wahuni walipoingilia kati. Ushindi mkubwa wa DCP unaonyesha wazi kuwa Wakenya wamechoshwa na serikali hii. Serikali hii haiwezi kujirekebisha na inapaswa kuhudumu kwa muhula mmoja tu," alisema Bi Muchoki, ambaye pia analenga kuwania kiti cha eneo bunge la Ndia.

read more