T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 16 Jul 2026 22:55:56

Mpango wa kutimua Sifuna ulivyosukwa usiku wa manane baada ya ziara Ikulu

KIKAO cha kundi la wabunge kilichojawa na vurugu usiku wa manane Jumatano kilisababisha pigo jingine kwa Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Baada ya kikao hicho, jana katibu huyo wa zamani wa ODM alitimuliwa katika wadhifa wake wa Kiranja wa Wachache huku migawanyiko ikichacha katika upinzani. Mkutano huo uliofanyika katika afisi ya Kiranja wa Wachache wa Bunge la Seneti, Ledama ole Kina ulifichua migawanyiko katika muungano wa Azimio na kuzidisha madai kwamba kundi la maseneta wa ODM lilitekeleza mpango uliodaiwa kupangwa awali mapema katika kikao na Rais William Ruto katika ikulu. Spika wa Seneti, Amason Kingi tayari ametekeleza mabadiliko. Seneta wa Migori Eddy Gicheru Oketch amechukua usukani wa afisi hiyo. Uamuzi huo ulijiri siku chache tu baada ya Bw Sifuna kupoteza wadhifa mwingine muhimu alipotemwa kutoka kwa kamati maarufu ya kawi ya seneti inayoongozwa na kinara wa ODM Oburu Oginga. Hatua hiyo vilevile ilifuatia kung'olewa kwake kama Katibu Mkuu wa ODM, uamuzi alioapa kupinga, kuashiria kampeni kali ya kambi hiyo inayounga mkono serikali ya muungano kudidimiza ushawishi wake. Mkutano wa Jumatano ulijawa na sarakasi tele huku ukigeuka upesi mapambano ya kimchakato yaliyoishia kuwa majibizano makali na makabiliano miongoni mwa maseneta kuhusu uhalali wa kikao hicho. Kundi la maseneta waliozungumza na Taifa Leo walidai waligutuka kupokea notisi kuhusu kikao hicho saa chache tu kabla ya kuanza. Notisi hiyo iliyotumwa na Kiongozi wa Wachace katika Seneti, Ole Kina mwendo wa saa kumi na mbili kasorobo iliwaalika maseneta kuhudhuria kikao cha kundi la wabunge mwendo saa moja unusu usiku afisini mwake. Mawasiliano hayo hayakueleza ajenda, jambo lililozua shaka miongoni mwa maseneta wanaoegemea upande wa Bw Sifuna na kundi la kujitenga la Linda Mwananchi, wengi wao waliosikia ripoti kuwa kundi la maseneta wa ODM walikuwa ikulu adhuhuri. Kulingana na waliohojiwa, wasiwasi uliongezeka kwa sababu mwaliko ulijiri saa chache baada ya wajumbe wa ODM wakiongozwa na Dkt Oginga kushiriki chamcha kilichoandaliwa na Rais Ruto katika ikulu. Seneta wa Kisumu, Tom Ojienda alithibitisha kuwa baadhi ya maseneta walihudhuria hafla hiyo. "Tulienda kushiriki chamcha na Rais, jambo ambalo ni la kawaida. Ni kawaida kwetu kushiriki maakuli ya mchana na Rais kwa hivyo haihusiani na hatua hii," akasema Seneta Ojienda. Alithibitisha vilevile kuwa yeye binafsi aliwasilisha hoja ya kumtimua Sifuna. "Ni mimi niliwasilisha hoja ya kumwondoa Sifuna," alisema. Wanachama waliuliza kwa nini kikao kiliandaliwa kupitia notisi fupi jinsi hiyo na kwa nini maseneta hawakufahamishwa mbeleni kwamba mabadiliko ya uongozi yalikuwa sehemu ya ajenda. Wengine walihoji kuwa uamuzi muhimu jinsi hiyo haungefanywa haraka bila kuwapa wanachama wote wa muungano muda wa kutosha kuhudhuria.

read more
T

taifaleo.nation.co.ke

@taifaleo Thu, 16 Jul 2026 21:55:02

Jinsi uchaguzi wa Ol Kalou ulitekwa na hongo, uhuni, vitisho na ghasia

UCHAGUZI mdogo wa Ol Kalou ulioandaliwa jana ulikumbwa na ghasia, hongo, vitisho na majeraha huku viongozi mbalimbali wakilaani matukio hayo. Tume Huru ya Uchaguzi Nchini (IEBC) ilitarajiwa kumtangaza mshindi baada ya shughuli ya kuhesabu wa kura kukamilika. Uchaguzi huo uliandaliwa kumsaka mrithi wa marehemu David Kiaraho ambaye aliaga dunia mnamo Machi mwaka huu. Kulikuwa na ushindani mkali kati ya wawaniaji wa UDA na DCP. Shughuli ya upigaji kura ilianza saa 12 asubuhi vituoni 144 katika eneobunge hilo lenye wapigakura 73,480 na wadi tano. Katika vituo mbalimbali ambavyo Taifa Leo ilitembelea, wapigakura wengi walikuwa wazee huku Gen Z wachache wakijitokeza. Kufikia saa sita mchana, IEBC walikuwa wametathmini kuwa waliojitokeza mjini walikuwa asilimia 70 huku mashambani ikiwa ni asilimia 30. Milolongo mirefu ilishuhudiwa katika Shule ya Msingi ya AC ambako mgombeaji wa DCP Kamau Ngotho alipiga kura yake na pia Shule ya Msingi ya Huruma ambapo mwenzake wa UDA Muchina Nyaga alitekeleza wajibu huo wa kidemokrasia. Kampeni zilinoga katika vituo hivyo vilivyoko umbali wa mita 300 kutoka mji wa Ol Kalou. Huruma iko katika wadi ya Kaimbaga nayo AC wadi ya Karai. Wawaniaji wengi walikuwa wamepiga kura zao kufikia saa sita mchana. Hata hivyo, dalili kuwa ghasia zingetokea zilianza saa 10 asubuhi wakati kundi la vijana lilizunguka kuwaamsha watu waende vituoni huku wengine wakihakikisha hakuna aliyeingia kituoni wakiwa ndani ya magari. Mbunge wa Mathira Erick Wamumbi alizuiwa kuingia katika kituo cha Huruma akitumia gari lake. [caption id="attachment_190188" align="alignnone" width="2547"] Wakzi wenye hasira wafukuza magari meusi yaliyokuwa yamebeba watu waliofunika nyuso zao ambao walikuwa wanafyatua risasi ovyo Ol Kalou. Picha|Boniface Mwangi[/caption] Mgombeaji wa UDA Muchina Nyaga ambaye alipiga kura yake katika kituo hicho alisema angekubali kushindwa lakini kwa haki. "Kuna vitisho na utoaji hongo ambao unaendelea katika vituo mbalimbali na tumewasilisha malalamishi kwa IEBC," akasema Bw Nyaga akilalamika kuwa gari lake liliteketezwa. Ghasia zilishuhudiwa katika kituo cha upigaji kura cha Shule ya Msingi ya St Joseph wakati wanaume waliofunika nyuso walirusha vitoza machozi na kusababisha waliokuwa wakisubiri kupiga kura kutimka mbio. Hali iliendelea kuwa mbaya baada ya magari mengi aina ya Toyota Prado kuingia eneo hilo kuwabeba watu waliokuwa wamejihami na kujificha nyuso. Fujo hizo hazikuwasaza wanahabari ambapo wanahabari wa NMG walivamiwa katika Shule ya Msingi ya AC na wanaume waliojifunika nyuso na kujihami vikali. Wakati wa ghasia hizo, Mpigapicha wa NTV George Kieru aliibiwa kamera naye ripota Fabiola Akinyi akapokonywa simu yake baada ya kuelekezewa bunduki. Kwa mujibu wa wanahabari hao, wanaume sita waliwasili kwenye magari ya kifahari kisha wakawavamia wanahabari. "Tulikuwa tumeenda hapo kufuatilia uhasama kati ya wakazi na maafisa wa polisi. Ghafla wanaume waliovalia mavazi ya kujificha nyuso walichomoa bunduki na kuanza kutuvamia. Nilifanikiwa kutoroka na kupata hifadhi kwenye duka la karibu," akasema Mhariri wa NMG Ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa Brygettes Ngana. Bi Ngana alisema wavamizi hao walimpiga Bw Kieru kisha wakaondoka na kamera yake. Pia walimuibia Bi Akinyi simu yake. "Walinipiga na kunilazimisha kufuta picha na video zote nilizokuwa nimechukua. Wameniumiza mgongo na mkononi," akasema Bw Kieru. "Mmoja kati ya wanaume hao alinielekezea bunduki tumboni na kunilazimisha nimpe simu yangu. Walinipokonya simu kisha wakatoka mbio wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado TX," akasema. Mwenyekiti wa NMG Joe Muganda alikashifu kuvamiwa kwa wanahabari wa NMG na kuwataka waliohusika waadhibiwe. "Uvamizi dhidi ya wanahabari ni uvamizi dhidi ya haki ya umma kupata habari. Nataka vyombo husika vichunguze tukio hili haraka kisha wahusika wachukuliwe hatua za kisheria. Pia wanahabari wanaoripoti kuhusu masuala ya umma wahakikishiwe usalama wao," akasema Bw Muganda. "Uchaguzi ni miongoni mwa nguzo muhimu za demokrasia katika jamii yoyote, na uwepo wa vyombo vya habari ni muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi kwa mchakato huo. Vurugu, vitisho au aina yoyote ya kuzuia wanahabari kutekeleza wajibu wao hazina nafasi katika jamii ya kidemokrasia." akaongeza. "Kwa zaidi ya miongo sita, NMG imeendelea kushikilia misingi ya uandishi wa habari unaowajibika, uhuru wa uhariri na viwango vya juu vya taaluma. Mwenendo huo hautatikiswa wala kudhoofishwa na vitendo vya vurugu au vitisho." Katibu Mkuu wa Chama cha Wanahabari Nchini (KUJ) Eric Oduor pia alikashifu kushambuliwa kwa wanahabari hao na kutaka wahakikishiwe usalama wao. "Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama vilinde wanahabari ili wafahamishe Wakenya kile kinachoendelea Ol Kalou," akasema Bw Oduor. Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alishutumu serikali akisema ilitumia wahuni kama mbinu ya kuishurutisha IEBC ifutilie mbali uchaguzi huo. Pia alidai kuwa wanaume waliokuwa wamejihami walikuwa wakilindwa na polisi waliingia kwenye hoteli moja baada ya kuvuruga upigaji kura. "Ghasia hizi zinaonyesha yatakayotokea 2027. Polisi ndiyo wanatumiwa," akasema Bw Gachagua. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen naye aliamrisha uchunguzi ufanyike kuhusu kisa ambacho polisi waliovalia kiraia waliwarushia raia vitoza machozi. "Inspekta Jenerali wa Polisi aliwatuma polisi wa kutosha Ol Kalou na wanaoshiriki ghasia wachunguzwe na kuadhibiwa," akasema. Alisisitiza kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi ya polisi yeyote ambaye alihusika na ghasia hizo.

read more